Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Florence George Samizi (24 total)

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, asante sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yako mazuri nichukue nafasi hii kwanza kabisa kuishukuru Serikali kwa kutupatia kituo hicho katika Kata ya Bunyambo ambayo ilikuwa hatuna kituo cha afya katika Tarafa hii ya Kibondo Mjini tangu tupate uhuru. Lakini hata hivyo Kata hii ya Murungu iko takribani kilometa 31 kutoka Kibondo Mjini ambapo kuna hospitali ya wilaya na ukizingatia kwamba sasa bado tuna kata 8 katika tarafa hii ambazo hazina kituo cha afya.

Mheshimiwa Spika, swali langu la msingi ni lini Serikali itatujengea kituo cha afya katika Kata hii ya Murungu kwa kuzingatia umbali huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi Mbunge wa Muhambwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninatambua na Serikali inatambua kwamba tunahitaji kupata kituo cha afya katika Kata ya Murungu na ni ahadi za viongozi wetu wa kitaifa.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Serikali inaendelea kutafuta fedha na mara fedha zikipatikana tutapeleka fedha pale kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, asante sana. (Makofi)
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nami nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga na kuboresha miundombinu ya maji katika Jimbo la Muhambwe, hususan Kata za Kibondo Mjini, Bunyambo na Kitahana ili kukabiliana na uhaba mkubwa wa maji ulioko katika jimbo hilo?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe, nadhani mwezi mmoja ama miwili iliyopita, Mheshimiwa Mbunge wa Mihambwe ameingia katika Bunge hili. Amekuja ofisini, na jana tumekwisha mpa pesa, zaidi ya milioni 100 ili kuhakikisha kwamba wananchi wake wanakwenda kupata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa jinsi ambavyo inaendelea kupambana kuwasaidia wananchi ili waweze kujikwamua kiuchumi: -

Mheshimiwa Spika, soko hili la ujirani mwema ni soko kati ya nchi ya Tanzania na Burundi. Kama nilivyouliza kwenye swali langu la msingi, mahali pale Serikali imeweka pesa kujenga yale mabanda kwa ajili ya biashara, lakini hakuna kituo cha polisi, hakuna TRA, wala hakuna uhamiaji, hivyo, kufanya utendaji wa soko lile kuwa hafifu kwa sababu ya hatarishi hii.

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa mpaka uko kilometa tano ndani ya nchi ya Tanzania kwa hiyo, hata pale ambapo uhamiaji wanafanya shughuli zao za kawaida inasababisha usumbufu sana kwa wananchi. Hivyo, napenda kujua ni lini Serikali itaweka vile vipaumbele vya One Stop Centre kama nilivyouliza kwenye swali langu la msingi, ikiwamo forodha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Florence kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwasemea wananchi wa Muhambwe, lakini nimhakikishie kwamba, hoja hizi zote ambazo amezileta Serikali imeanza kufanyia kazi, likiwemo suala hili la kupima maeneo ya viwanja 145 kuzunguka soko, ili tuweze kupata maeneo kwa ajili ya kujenga Vituo vya Polisi, Forodha, lakini pia nae neo la Uhamiaji. Kwa hiyo, mara baada ya ramani zile kukamilishwa ambazo tayari mchakato unatarajiwa kuanza wakati wowote, sasa tutaenda kuomba kwenye sekta husika waweze kujenga vituo hivi na kuwezesha soko kufanya kazi vizuri. Ahsante.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipatia nafasi.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kibondo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wa Mkoa wa Kigoma kwamba nyaraka za zabuni kwa sasa ziko kwa Mwanasheria Mkuu kwa ajili ya vetting ili kazi ya upanuzi wa uwanja huo zianze. Ahsante.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Kizazi ambacho kimejengwa kwa nguvu za wananchi katika Jimbo la Muhambwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Florence Samizi, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wananchi wa Kata aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge wametoa nguvu zao, wameanza ujenzi wa kituo cha Afya na Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia. Tumekubaliana kwamba tukipata fedha tutakwenda kuchangia nguvu za wananchi pale, kituo cha afya kikamilike tuanze kutoa huduma za afya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunakwenda kutafuta fedha kwa ajili ya kazi hiyo. Ahsante.(Makofi)
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, halmashauri hii makusanyo yake ya mwaka 2021 ilikuwa bilioni 5.3 kwa mwaka na Jimbo hili la Muhambwe liko mpakani ambapo tuna biashara za ujirani mwema kwenye Masoko ya Mkarazi na Kumshwabure. Je, Serikali haioni ni muda muafaka sasa kujenga TRA ya kudumu lakini pia na kujenda ushuru wa pamoja mpakani ili kudhibiti biashara holela za mpakani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, wananchi wa Muhambwe wanafuata huduma za leseni Mkoani Kigoma ambapo ni kilomita 240 kutoka Jimbo la Muhambwe. Je, ni lini Serikali itaanzisha huduma za leseni katika Jimbo la Muhambwe ili kuwaondolea adha wananchi hawa wa Muhambwe?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi, Mbunge wa Muhambwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza, Serikali imelichukua na tutalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba ikimpendeza Mheshimiwa Mbunge niambatane naye kwenda kuona hali halisi ya Wilaya ya Kibondo, tuone namna gani tunaweza tukatatua usumbufu huu ambao wanapata wananchi wetu wa Kibondo. Ahsante.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa skimu zilizojengwa katika Jimbo la Mhambwe, ikiwemo Nyendara, lumpungu, Kigina, Mgondogondo, Kahambwe, lili ziweze kuwasaidia wakulima wa jimbo hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika moja ya mikakati tuliyonayo katika mwaka huu wa fedha ni kuhakikisha tunakarabati na kukamilisha skimu ambazo tulizipitia na kuona zinahitaji marekebisho madogo ili wananchi waendelee kutumia kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika baadhi ya skimu katika Jimbo lake zitatekelezwa mwaka huu na nyingine katika mwaka ujao wa fedha. (Makofi)
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Ukosefu wa copper wire na mita ni moja ya sababu inayochelewesha uunganishwaji wa umeme katika Jimbo la Muhambwe, ikiwemo kata ya Busagara, Kitahara, Kumsenga na Mlungu;

Je, ni lini Serikali italeta vifaa hivi, ili kata hizi ziweze kunufaika na kuunganishiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Florence Samizi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa uzalishaji wa vifaa ulitokea katika maeneo mengi baadaya kupata matatizo ya UVIKO, na hivyo milango ilivyofunguliwa order zilikuwa nyingi na wahitaji walikuwa wengi, Kwa hiyo na sisi tunahakikisha tunatoa order za kutosha na kwa kadri zinavyozaliswha tunazipata. Nimuhakikishie tu Mheshimiwa Samizi kwamba, katika eneo lake na maeneo mengine vifaa vitapatikana na huduma kwa wananchi itaendelea kuunganishwa kwa sababu pesa tunayo na tunaendelea kufatilia kwa ajili ya upatikanaji wake.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Tunaendelea kuishukuru Serikali kwa jinsi ambavyo inaendelea kupambana kuongeza vituo vya afya na vifaa kama ilivyojielekeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo changamoto kubwa ya watumishi kutokukaa katika vituo vya afya ni ukosefu wa nyumba.

Je, nini mkakati wa Serikali kuwajengea watumishi wa afya nyumba ili waweze kukaa kwenye vituo hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dokta Florence Mbunge wa Muhambwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tuna upungufu wa nyumba za watumishi katika vituo vyetu na mpango wa Serikali sasa ni kuendelea kutenga fedha kupitia mapato ya ndani lakini pia kutoka Serikali Kuu kuhakikisha nyumba za watumishi zinajengwa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mpango huu tayari umeratibiwa.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ninaishukuru Serikali kwa kutuwekea mpango mzuri wa kutuletea minara katika Jimbo letu. Hata hivyo, Jimbo la Muhambwe lina mnara mmoja tu wa TTCL ambao umelemewa na badala yake inatumia kufanya roaming kwa minara ya kampuni nyingine.

Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuweka minara mingi ya TTCL ili tuweze kupata usikivu lakini pia mawasiliano ya bei nafuu?

(b) Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali pia kwa kutuletea kifaa hicho ambacho kitaenda kuboresha usikivu wa TBC Redio katika Jimbo letu, hata hivyo usikivu wa TBC Redio katika Jimbo letu ni hafifu sana inayopelekea wananchi wa Muhambwe kusikiliza zaidi Redio ya Burundi kuliko ya TBC Redio.

Je, nini mkakati wa Serikali kuboresha zaidi usikivu wa Radio katika Jimbo zima la Muhambwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi Mbunge wa Muhambwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, hivi leo nimejulishwa na Mheshimiwa Waziri amekuwa akiwasiliana nae kukumbushia kuhusu zile ahadi zake katika kipindi cha kampeni, Mheshimiwa Waziri ameshatoa maelekezo na ahadi hizo ambazo zinalenga katika Wizara yetu zitafanyiwa kazi zote. Vilevile suala la usikivu kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi ni kwamba kifaa hiki kitakaporejeshwa na kufanyiwa majaribio nina uhakika kabisa kwamba tatizo la usikivu katika Jimbo la Muhambwe litakuwa limemalizika kabisa. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Mkoa wa Kigoma umejaaliwa neema ya kuwa na Ziwa Tanganyika na Mto Malagarasi, lakini ni mkoa ambao bado unakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji. Je, nini mkakati wa Serikali kutumia maji ya Mto Malagarasi na Ziwa Tanganyika ili kumaliza uhaba wa maji katika Mkoa wa Kigoma hususan Jimbo la Muhambwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Florence, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya vyanzo vya maji vya Maziwa Makuu na mito mikubwa ni moja ya mikakati ya Wizara, hivyo Mto Malagarasi na Ziwa Tanganyika navyo pia viko kwenye mikakati ya Wizara kadiri tutakavyokuwa tunapata fedha za kutosha tutatoa kipaumbele kwenye vyanzo hivi vikubwa ili tuendelee kupata miradi endelevu.
MHE: DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali la nyongeza. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itaanzisha mchakato huo ili kuwasaidia kuchochea biashara ya ujirani mwema inayofanyika katika Kijiji hiki cha Kibuye katika Kata ya Kumsenga? (Makofi)

Mheshimiswa Spika, swali la pili; kwa kuwa Mto huo unatenganisha takribani vijiji sita vya Jimbo hili la Muhambwe na wananchi wanapita mipaka holela, je, Serikali haioni iko sababu ya kuharakisha mchakato huu wa daraja ili kuwe na mahali maalum pa kupita hili kudhibiti vitendo vya uhalifu katika Jimbo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi, Mbunge wa Muhambwe, kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, daraja hili halipo na linaunganisha nchi mbili, kwa hiyo ni daraja ambalo litahusisha wadau wengine si tu Burundi na Wizara ya Ujenzi, pia itahusisha Taasisi nyingine kama Ulinzi na Usalama, TAMISEMI, Ardhi, Wizara ya Fedha na Mambo ya Nje. Kwa hiyo, wadau wote hawa watakapokuwa wameona kuna haja thabiti ya kujenga na kuona inakidhi vigezo na sisi tukajiridhisha kama nchi, ndiyo tutaanza sasa kuwasiliana na wenzetu wa Burundi. Kwa hiyo sisi tumeshaanzisha huo mchakato kwa upande wetu kuona vigezo vyote vinakidhi, halafu tuweze kuwahusisha wenzetu wa Burundi, ahsante.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi. Shule ya Sekondari ya Kumkubwa ni shule ya kidato cha tano na sita inayotumia majengo chakavu yaliyokuwa kambi ya wakimbizi.

Je, ni lini Serikali itajengea miundombinu ya madarasa katika Shule hii ya Sekondari ya Kumkubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lengo la Serikali kuboresha miundombinu ya shule zote, si tu za sekondari, kuanzia za msingi, sekondari na hizi za A-level. Hivyo basi tutaona ni namna gani ambavyo tunaweza tukaanza ukarabati wa shule hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mnamo mwaka 2021 Mheshimiwa Waziri Mkuu aliweka Jiwe la Msingi wa ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Kifura ambao wakati huo ulikuwa asilimia 43, mpaka leo mradi huo umetelekezwa na uko asilimia 43 hiyohiyo. Je, ni nini mpango wa Serikali kutenga fedha ili kukwamua mradi huu wa maji ili wananchi wa Kifura waweze kupata maji?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge, kubwa mradi huu wa Kifura ni mradi ambao ulikuwa unatekelezwa na kampuni ya Nangai pamoja na taasisi ambayo inaitwa ENABEL, tulikuwa na changamoto baina ya huyu Mkandarasi na hii taasisi, tumekwisha kaa nao na moja ya maelekezo ambayo tumempatia yule Mkandarasi, Tarehe 31 Agosti, akabidhi mradi huo ili wananchi wa Kifura waendelee kupata huduma ya maji safi na salama.(Makofi)
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi. Shule ya Sekondari ya Busagara na Shule ya Sekondari Kumgogo zilizoko katika Jimbo la Muhambwe zina miundombinu ya madarasa kwa ajili ya kuanzisha kidato cha tano na cha sita.

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kujenga hosteli ili tuweze kuanza huduma ya kidato cha tano na sita katika shule hizi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi Mbunge wa Jimbo la Mhambwe. Kama ambavyo nimeeleza hapo awali katika majibu mbalimbali ambayo nimeyatoa kwa waheshimiwa Wabunge, nimwondoe hofu kwamba sehemu ya timu ambayo itatumwa nafikiri itatumwa kupokea maoni yote ambayo Wabunge wote wameeleza; mapungufu katika shule ambazo tunaweza kuongeza aidha hosteli, bweni ama jengo la utawala na zikatumika kama kidato cha tano na sita zikiwemo za jimbo lako. Kwa hiyo waondoe hofu wananchi wa Muhambwe kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo kazi na itafanya kazi hiyo, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naishukuru sana Serikali kwa majibu hayo mazuri pamoja na majibu hayo mazuri bado nina maswali ya nyongeza. Wahanga waliozulumiwa pesa zao katika Jimbo la Muhambwe ni Lugongwe AMCOS, Chapakazi AMCOS, Amani AMCOS na Migwezi AMCOS ambao hawa waliingia mikataba na JESPAN baada ya kuwa wamejiridhisha kwamba Serikali imewapatia vibali hawa JESPAN.

Je, Serikali aioni iko ukunimu wa kulipa hizi pesa kwa sababu wao ndiyo waliyowadhamini hawa wakulima halafu wenyewe Serikali itaendelea na hizo kesi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa makampuni haya ya wazawa yanawazulumu hawa wakulima hii JESPAN ni mfano tu. Serikali imejipanga vipi kuyadhibiti haya makampuni ili wakulima wetu wasiendelee kudhulumiwa? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli makampuni haya tumeanza kuchukua hatua za kisheria, baadhi ya makampuni yanatoa huduma kwenye sekta ya tumbaku baadhi yao tumeishayakata fedha kupitia TCJE kama dola lakini nne ambazo walitoa huduma ili tuweze kuzirudisha kwa wakulima. lakini hatua ya pili ni kwamba Serikali inapompa leseni kwenda kufanya biashara anapokwenda kinyume kuna utaratibu wa kisheria na kwake yeye kupewa leseni ya kwenda kufanya biashara haina maana ile responsibility siku ya mwisho itahamia kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tabia ya wakulima kudhulumiwa na wafanyabiashara na hii haipo tu kwenye tumbaku, ipo kwenye pamba, ipo kwenye korosho, ipo kwenye maeneo mengi, na wizi mwingine hushirikisha vyama vya ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano kesi iliyoko Mkoa wa Katavi chama cha ushirika kimeshirikiana na Kampuni ya NEIL kuweza kuwaibia wakulima. Kwa hiyo, tunachukua hatua za kisheria niwaombe Waheshimiwa Wabunge wa Sikonge Wilaya ya Sikonge Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Tabora na Wilaya ya Chunya wa tumbaku waliyopata madhara mwaka 2019/2020 niwahakikishie kwamba Serikali inachukua hatua na tutamaliza haya matatizo na yamekuwa fundisho kwetu ndiyo maana tumewaondoa wanunuzi wa namna hii na tunakuja na sheria ya kilimo itakayoweza ku–criminalize wizi unaofanyika kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itajenga stendi ya mabasi katika Jimbo la Muhambwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Muhambwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawaelekeza Halmashauri ya Kibondo kufanya tathmini ya gharama zinazohitajika kwa ajili ya ujenzi na kuanza kutenga mapato ya ndani. Lakini kama uwezo hautatosha walete andiko hilo Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya kutafuta fedha za kujengea stendi hiyo.

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika ahsante kwa kunipa nafasi.

Je, ni lini Serikali itajenga bweni katika shule ya sekondari ya Busagara ili tuweze kutoa huduma ya Kidato cha Tano na cha Sita kama tulivyoomba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali itajenga mabweni katika shule hii ya Busagara kadri ya upatikanaji wa fedha. Mkurugenzi wa Halmashauri aanze kutenga fedha kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa mabweni haya na kisha kuleta maombi Serikali Kuu kwa ajili ya kumalizia mabweni haya ambayo yataanza kwa jitihada za halmashauri yenyewe.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Je, lini Serikali itatekeleza ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano ya kujenga Kituo cha Afya katika Kata ya Mulungu Jimboni Muhambwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Daktari Samizi la lini Serikali itatekeleza ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kujenga kituo cha afya. Tutaangalia ahadi hii na nitakaa na Mheshimiwa Samizi kuona ni namna gani tunaweza tukakaa na wataalam wetu kuona tunapataje fedha za kutekeleza ahadi hii katika mwaka wa fedha wa 2023/2024. (Makofi)
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza kabisa naishukuru Serikali kwa majibu mazuri ambayo yameonesha matumaini kwa kuwa wameshafanya tathmini, lakini, je, Serikali haioni kwamba iko sababu ya kuharakisha ukarabati wa nyumba hizi ili kuboresha ufanisi wa askari angalau kwa kuanza na pesa kidogo mwaka huu, then mwaka kesho tumalizie? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, haja ya kufanya haraka ya kuharakisha upatikanaji wa hizi huduma ni jambo la msingi na sisi kama Wizara tutahakikisha kwamba tunakwenda kutafuta fedha kokote ziliko ilimradi tuhakikishe kwamba Vituo vya Polisi nchini kote ikiwemo Jimbo la Mheshimiwa Mbunge la Muhambwe vituo hivi vifike.

Mheshimiwa Spika, hii ni kwa sababu ya azma njema ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba kwanza wananchi wote wanapata huduma za ulinzi na usalama, lakini pia kuhakikisha kwamba tunaboresha mazingira yawe mazuri zaidi kwa upande wa vyombo hasa Jeshi la Polisi ikiwemo magari na Vituo vya Polisi na nyumba za makazi, nakushukuru.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi; je, ni lini Serikali itaunganisha Mkoa wa Kigoma na Gridi ya Taifa?

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Florence Samizi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kigoma ni mmoja wapo kati ya mikoa michache iliyokuwa imebakia bila kuunganishwa na Gridi ya Taifa, na nimpe taarifa na habari njema ya Serikali ya Awamu ya Sita kwamba kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu Gridi ya Taifa itakuwa imeanza kufika Kigoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, na tutapeleka Gridi ya Taifa Mkoa wa Kigoma kwa njia nyingi, naomba uniruhusu nizitaje kwa haraka haraka; tunaanza na njia ya msongo wa Kv33 kutoka katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Nyakanazi kwenda Kakonko – Kibondo – Kasulu mpaka Kigoma Mjini, na hiyo itakamilika mwezi Agosti. Kuna njia ya msongo wa Kv 400 ambayo inajengwa kutoka Nyakanazi kwenda mpaka Kigoma, mkandarasi wa TATA yuko site; lakini kuna njia ya msongo wa kv 400 inayotoka Sumbawanga kuja kuingia mpaka Kigoma, na yenyewe itapeleka pia umeme wa Gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema zaidi ni kwamba tunajenga mradi wa kuzalisha umeme katika Mto Malagarasi (megawati 49.5), kufikia mwaka 2025 utakuwa na wenyewe umefikisha umeme.

Mheshimiwa Naibu Sapika, nashukuru.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Je, ni lini Serikali itapeleka Shilingi Milioni 200 katika Kituo cha Afya cha Nyalioba, ikiwa ni ni utekelezaji wa ahadi ya Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Florence Samizi, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samizi anawasemea sana wananchi wa Jimbo la Muhambwe, nakumbuka katika ziara ya Mheshimiwa Makamu wa Rais tulikuwa pamoja tuliahidi Milioni 200 Mheshimiwa Makamu wa Rais aliahidi. Ninakuhakikishia kwamba Ofisi ya Rais – TAMISEMI tayari imetenga fedha hizo na wakati wowote zitaingia kwenye Kituo cha Afya cha Nyalioba, ahsante.

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi. Ujenzi wa barabara ya kutoka Kabingo hadi Kibaoni kilometa 25 kwa kiwango cha lami unasuasua sana.

Je, ni lini Serikali itakwamua ujenzi wa barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara hii inayoisema ni Kibondo link, barabara ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami. Nimeitembelea hiyo barabara kuangalia changamoto zilizopo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeshaona changamoto zilizokuwepo za kiutendaji kwa Mkandarasi na tuna hakika baada ya kukaa nae barabara hii sasa itaanza kwenda kasi ili tukamilishe zile kilometa 25. Ahsante.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kituo cha Afya cha Kifura ambacho Serikali imekiri kwamba ni chakavu sana kinapokea wagonjwa wa nje 110 hadi 150 kwa siku lakini kinazalisha kinamama 120 mpaka 150 kwa mwezi. Je, kutokana na mzigo wa wagonjwa wengi ulioko katika Kituo hiki chakavu, Serikali haioni sasa iko sababu ya kuharakisha mchakato wa kuleta pesa za ukarabati wa Kituo hiki cha Afya cha Kifura? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Serikali iliahidi kumalizia ujenzi wa Kituo cha Afya cha Nyaruyoba kupitia ziara ya Mheshimiwa Makamu wa Rais mwaka 2021. Kituo hiki cha Afya cha Nyaruyoba kinahudumia takribani kata tatu ikiwemo Mkabule, Rusohoko na Kigaga iliyoko Kata ya Rugongwe. Je, Serikali haioni iko sababu ya kuharakisha kuleta pesa za kumalizia Kituo hiki cha Afya ambacho kinahudumia takribani kata nne katika Jimbo la Muhambwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba nianze tu kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo amefuatilia ahadi hizi za Serikali kuhakikisha kwamba zinakarabati Kituo cha Afya cha Kifura na ni kweli kituo hiki ni chakavu, kina upungufu wa miundombinu na kinahudumia wananchi wengi. Nimhakikishie kwamba katika mpango wa Benki ya Dunia hivi karibuni, hiki ni miongoni mwa vituo ambavyo vimeingizwa na tunaamini fedha zitakwenda kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Nyaruyoba ni ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais nimhakikishie kwamba tayari Serikali inaendelea kutafuta fedha na mapema iwezekanavyo fedha ikipatikana itapelekwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kituo hiki cha Afya, ahsante. (Makofi)