Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Bahati Khamis Kombo (5 total)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza, nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia kutupa uhai na uzima na tukaweza kufika hapa tukiwa katika hali ya salama na amani kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru tena wewe kwa kunipa nafasi hii ikiwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge letu hili Tukufu. Nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kuwa ni Rais wetu na akiwa ni mwanamama. Niseme tu mwanamama huyu ni hodari mno na ni shujaa. Tunamuombea dua Mwenyezi Mungu amjalie azidi kuimarika zaidi. Mama yetu koleza majani ya chai na kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee moja kwa moja katika bajeti yetu. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wa Fedha kwa kutuletea bajeti hii ambayo imewagusa Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja katika upande wa TASAF, naipongeza Serikali yetu kwa kutenga tena bajeti ya kutuletea miradi hii ya TASAF. Kwa kweli miradi hii imesaidia sana kaya zetu maskini na tuna imani kwamba kwa bajeti hii itazidi kuimarika zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwa upande wa Zanzibar, ripoti imeonyesha kwamba Zanzibar imefanya vizuri. Naipongeza sana Serikali yangu ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufanya vizuri katika kusimamia miradi hii ya TASAF, lakini pia pongezi zaidi ziende kwa wasimamizi wakuu walioweza kuisimamia TASAF Zanzibar na tukaweza kufikia lengo kuu lililokusudiwa na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja katika mchango wangu wangu wa pili kwa upande wa Jeshi letu la Polisi. Mheshimiwa Waziri hapa amegusia changamoto ya Jeshi la Polisi. Nimwambie tu Mheshimiwa Waziri waende wakaitatue changamoto hii kwani Jeshi letu la Polisi linafanya kazi nyingi usiku na mchana bila kujali mvua au jua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha akae makini anisikilize katika jambo hili moja ambalo naomba kulichangia. Jeshi letu la Polisi, kuna fedha ambazo wanazikosa, hawa wenzetu baadhi yao natoa mfano; mwanajeshi huyu anapokea shilingi 565,000 anatakiwa apewe asilimia 15 ya mshahara wake ikiwa ni posho la pango. La kusikitisha mwanajeshi huyu anatakiwa apewe shilingi 84,750, lakini posho anayopewa ni shilingi 40,545. Mheshimiwa Waziri aende akakae na Waziri mwenzake ili waweze kuitatua changamoto hii Jeshi letu liweze kufanya kazi likiwa na ufanisi mzuri na hii haki yao ya posho waweze kuipata kwa mujibu wa utaratibu uliopangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu sina la ziada ila nampongeza tena mama yetu Mama Samia, niwaambie Waheshimiwa Wabunge tunapompongeza mama tunamsahau baba, tumpongeze na baba yetu kwani yeye ndiye anayempa maliwazo mazuri na akaweza kutuongoza vizuri. Nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Spika, mchango wangu umejielekeza katika ukurasa wa kumi na moja ambapo hotuba hii imejielekeza katika kuboresha usafiri wa abiria na mizigo katika maziwa makuu.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuipongeza Serikali kwa kuendelea kujenga miundombinu rafiki ya usafirishaji abiria na mzigo. Ujenzi wa meli mpya ijuilikanayo kwa jina la Hapa Kazi Tu unaoendelea Mwanza kwa sasa umefikia asilimia 65; ushauri wangu kwa Serikali wale vijana wetu wazawa ambao wameshiriki katika utengenezaji wa meli hiyo itakapomalizika kutengenezwa ni vema kupewa kipaumbele kwa kupatiwa ajira katika meli hiyo kwa sababu ninaimani kubwa pindi wakipatiwa ajira katika meli hiyo watakuwa na uzalendo mkubwa kwa kuitunza ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na pia naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia machache katika Kamati yetu ya Miundombinu.

Mheshimiwa Spika, mimi nitajikita katika sekta ya ujenzi; kwa kweli wenzetu wa TANROADS wanafanya kazi kubwa na ni watu ambao huwa ni wa kupigiwa mfano, sote Wabunge tunaitegemea TANROADS. Sasa hivi Barabara nyingi ziko katika hali nzuri na ambazo bado hazijatengenezwa lakini tayari ule uelekeo upo. Kwa kweli tuwapongeze sana wenzetu wa TANROADS kwa jinsi ambavyo wanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile niiombe Serikali kuwaongezea bajeti wenzetu hawa wa TANROADS. Bila ya kuwa na bajeti kubwa hawatoweza kumaliza kazi ambazo tumezitegemea, lakini vilevile TANROADS wana ukosefu wa wafanyakazi. Niiombe Serikali iwaongezee wafanyakazi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja katika TBA; kwa kweli ni wa kupigiwa mfano. Tumewatembelea na tumeona kazi zao ambazo wanazifanya ni kazi nzuri sana, lakini wana changamoto ya kudai fedha nyingi katika Serikali. Niiombe Serikali kusimama wima ili waweze kurejeshewa fedha hizi na waendelee kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije moja kwa moja katika TEMESA, vilevile wana ukosefu wa wafanyakazi, niiombe Serikali kuwapatia wafanyakazi ili waweze kuimarisha kazi zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie mchango wangu mdogo kwa upande wa High Court. Kuna changamoto kubwa ya bajeti yao ambayo haikidhi haja, niiombe Serikali kwamba waongezewe bajeti ili na wao waweze kufanya kazi vizuri, lakini pia wana changamoto ya wafanyakazi. Wafanyakazi ni kidogo mno naomba sana waongezewe wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nimalizie kwa kukupongeza wewe kwa kuonesha juhudi zako nzuri kutuletea Bonanza la Wabunge kuona kwamba Wabunge wote miili yao iweze kuimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono kwa asilimia 100. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Spika, mchango wangu zaidi utagusa sekta ya bandari.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali kufanya utaratibu kuongeza vifaa vya kushushia makontena. Pia kuna vijana ambao walishiriki ujenzi wa meli MV Mwanza, vijana wale nakuomba Mheshimiwa Waziri kuwaangalia kwa jicho la huruma pindi ikimalizika kama kutakuwa na ajira basi uwape kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, tumejenga barabara nyingi, naomba sana tusisubiri mpaka zikaharibika, tukiona ishara tu ya dosari basi tufanye matengenezo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaali kunipa uzima na kuweza kusimama mbele ya Bunge letu kuweza kuchangia bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, niendelee kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha kwamba analeta maendeleo katika nchi yetu. Nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha pamoja na timu yao yote kwa kutuletea bajeti hii ambayo imemgusa kila Mtanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja katika Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi. Pia niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Nitakwenda katika meli yetu ya MV Mwanza Hapa Kazi tu. Meli hii pamoja na changamoto zilizopo, tuwapongeze sana vijana wetu wazawa ambao wameshiriki katika ujenzi wa meli hii. Kwa kweli vijana hawa wamefanya kazi kubwa na ni vijana wa mfano. Naomba tu Serikali itakapomaliza meli hii, basi nao waweze kupatiwa ajira kwa wale ambao wanaweza kufanya kazi katika meli ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niende moja kwa moja katika Sekta ya Kilimo. Naomba nisome kidogo maelezo ya Mheshimiwa Waziri, ameeleza kwamba, Tanzania ni aibu kulia kwa shida ya ngano au mafuta ya kula, kwani tunayo fursa ya kulisha Afrika, Ulaya, Asia katika baadhi ya mazao. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuliona hili. Kama Tanzania kweli tunaweza, na tunaweza kwa kila upande. Hata kule Zanzibar kwa upande wa Pemba sasa hivi tunapata tender kubwa sana kwa ndizi zetu za mkono wa tembo au kwa jina jingine mkono mmoja. Hili ni soko kubwa na tunaiomba Serikali wale wakulima waweze kupatiwa mikopo ya uhakika. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni soko kubwa na tunaiomba Serikali wale wakulima waweze kupatiwa mikopo ya uhakika. Vilevile nije katika zao letu la alizeti, niiombe Serikali kupitia Mfuko wa TASAF kule Zanzibar, wananchi waweze kuelekezwa juu ya kilimo hiki cha alizeti, bado Zanzibar hatujawa na utaalam wa kulima alizeti. Kipindi ambacho Waziri wa Kilimo wa Tanzania Bara na Waziri wa Kilimo wa Zanzibar watapeana ushauri wa kusaidiana, basi naamini kwamba tatizo hili la mafuta litaondoka Tanzania nzima. Nije moja kwa moja katika sekta ya elimu, tunavyo vyuo vikuu vingi hapa Tanzania Bara, lakini kule Zanzibar tunakosa matawi yake. Tunaiomba Serikali vile vyuo ambavyo kule Zanzibar hatuna matawi yake basi tuweze kupatiwa matawi, ili wale wanafunzi ambao wanahitaji kuomba nafasi zile za kusoma wasipate ule usumbufu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naamini kwamba sekta ya elimu ya vyuo vikuu ni sekta ya Muungano, niiombe tu Serikali kwa upande wa Pemba, tuweze kujengewa chuo kimoja kikuu ili iwe urahisi kwa wananchi ambao wako kule kupata ile elimu. Pia, tutapata fursa nzuri ya watoto wetu ambao wako Mwanza, wako Kigoma kuja kusoma kule Pemba. Hii pia itasaidia na wao kuijua nchi yao lakini pia wataiona kwamba Pemba kweli inanukia marashi ya karafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)