Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Stella Simon Fiyao (23 total)

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri lakini naomba niulize maswali ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:-

Swali la kwanza; ni dhahiri kuwa Taifa letu linahitaji wawekezaji wengi kutoka Mataifa mengine, lakini naamini itakuwa ni ngumu kupata wawekezaji ikiwa hawa tu tulionao wanashindwa kuwekeza kutokana na mrundikano mkubwa wa kodi zilizoko ndani ya Taifa letu.

Sasa nataka kujua je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kulichukua jambo hili na kufanya marekebisho ya sheria za kodi ili wananchi wetu waweze kufanya biashara kwa uhuru? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa TRA wamekuwa na utaratibu wa kufanya makadirio ya kodi wanapofika kwenye biashara za watu; ni nini tamko la Serikali katika hili maana TRA wamekuwa wakiwakadiria watu kodi kubwa ambazo zinazidi mitaji yao na kusababisha watu wengi kufilisika na kufunga biashara. Ni nini tamko la Serikali kwa hiki kinachoendelea leo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Fiyao kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kutokana na mazingira mazuri na rafiki hakuna ukandamizaji wa kodi kwa wananchi/wafanyabiashara atakayekimbia kwa kufanya biashara kwa sababu ya kulipa kodi kubwa ambazo Serikali imeziweka kiurafiki na kulipa kodi kwa sheria na utaratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la pili la Mheshimiwa Stella Fiyao kuwa kama Mheshimiwa anaona kuna kodi kandamizi ambazo wafanyabiashara wanapatiwa basi tungemuomba atuletee changamoto hizo na Serikali itazifanyia kazi kwa mujibu wa sheria na mipango yote iliyowekwa katika Serikali. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri, naomba kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, hali ya barabara ni mbaya sana kwa wananchi wa Wilaya ya Songwe na hali hii imesababisha wananchi kupoteza maisha, ikiwa ni pamoja na kuzikosa huduma za muhimu na za msingi ambazo wanatakiwa kuzipata katika Ofisi ya Mkoa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kulichukulia jambo hili kwa dharura, ili wananchi waweze kuepukana na changamoto ambayo imekuwa ikiwakabili kila mwaka katika Wilaya ya Songwe? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara anayoisema mwaka huu ilikuwa imesimama kwasababu ya mvua nyingi ambayo inaendelea kunyesha. Na kuna daraja linalounganisha Kijiji cha Tanga na Mbala ambapo mto ulitoka kwenye njia yake ukakata barabara na ukawa umetengeneza bwawa.

Mheshimiwa Spika, tunavyoongea na hasa kupitia Mbunge Mulugo wa Jimbo la Songwe tumekuwa mara nyingi tunawasiliananae na anafahamu fika kwamba, hadi sasa wakandarasi wako site. wameanza Alhamisi ya wiki iliyopita, tumapata fedha shilingi milioni 700 kwa ajili ya kukarabati batabata hiyo na kurejesha mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, lakini baada ya hiyo barabara kukatika kuna barabara nyingine ambayo walikuwa wanapitia sasa Chunya – Mbeya kwenda Songwe. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, suala hilo lipo na tayari wakandarasi wako site na milioni 700 ziko tayari kwa ajili ya kuendesha mawasiliano ya barabara. Ahsante.
MHE. STELLA S. FIAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kutokana na changamoto kubwa ya upungufu wa mafuta iliyopo katika nchi yetu, nataka kujua Serikali imejipanga vipi kuhakikisha inaleta mbegu bora ya alizeti kwa bei ndogo na ya chini ambayo kila mkulima ataweza kuimudu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kutokana na changamoto kubwa ya upatikanaji wa mbegu ya mahindi na mbolea katika Mkoa wa Songwe, je, Serikali iko tayari kuwaruhusu wananchi wa Mkoa wa Songwe kununua mbegu ya mahindi na mbolea katika Nchi jirani ya Zambia pasipo kuwabughudhi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Stella, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba wananchi wamekuwa wakinunua mbegu hasa waliopo mipakani katika maeneo ya Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Songwe kupitia mbegu zinazoingia kwa njia ambazo si halali. Vilevile tunajiridhisha na naweza nikamtolea mfano Mheshimiwa Hasunga akiwa mkulima katika Mkoa wa Rukwa aliwahi kununua mbegu za njia hizo na matokeo yake mahindi hayakuweza kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niahidi tu mbele ya Bunge lako kwamba hii changamoto tunaifanyia kazi na tutakaa na wadau wa maeneo hayo ili tutathmini njia nzuri ya kuingiza mbegu kihalali ambazo tuna upungufu nazo na kwa gharama nafuu kwa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la alizeti ni kweli kama nchi tuna upungufu wa karibu metric tons laki nne za mafuta ya kula. Hatua ambayo tunachukua mwaka huu, jana Waheshimiwa Wabunge wametupitishia bajeti, tumekaa na sekta binafsi na taasisi yetu ya ASA; mahitaji yetu ya mbegu ni kati ya metric tons 5,000 – 6,000 ambazo tutaenda kutumia kuzalisha kwenye eneo la hekari milioni 1.3 ambalo hili litatupatia zaidi ya tani milioni 1.2 za mbegu kwa ajili ya kwenda viwandani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua tunayoichukua uzalishaji wa ndani utazalisha tani 2,000, tunakaa na ASA na waagizaji kutoka nje tutaagiza deficit ya mbegu kwa mwaka huu na tutaipeleka kwa wakulima at subsidized rate kwa sababu tumetenga fedha katika bajeti ili kupunguza bei ya hybrid kutoka Sh.30,000 kwa kilo moja angalau ifike kati ya Sh.7,000 hadi Sh.10,000 na Wizara ita-subsidize mbegu hizo ili wakulima waweze kupata kwa bei rahisi. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza mradi wa kutoka Ileje Mto Songwe kuja Tunduma ulifanyiwa upembuzi yakinifu kutoka mwaka elfu 2013 na kampuni ya networkers kutoka Marekani. Mradi huu ulikuwa unagharimu kiasi cha Shilingi bilioni tatu. Sasa nataka kujua;

Je, ni lini mradi huu utakamilika ili wananchi wa Tunduma waweze kunufaika na maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa wananchi wa Kata ya Mpemba na Kata ya Katete wamekuwa wakitegemea mradi wa maji kutoka katika Wilaya ya Mbozi maeneo ya Ukwile, lakini mradi huu umekuwa ukisumbua sana kutokana na miundombinu kuwa mibovu, miundombinu iliyopo ilitengenezwa kutoka mwaka 1971 sasa nataka kujua;

Je, ni lini Serikali itaweza kuboresha miundombinu hii ili wananchi wa Kata ya Katete na Kata ya Mpemba waweze kupata maji kwa ukamilifu kabisa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Fiyao kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu wa maji kutoka Ileje kwenye Mto Bupigu ni mradi mkubwa. Kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi mwaka ujao wa fedha 2021/2022 mhandisi anatarajiwa kuja kwa ajili ya usanifu wa kina, na tunaratajia mwaka ujao wa fedha usanifu wa kina utakamilika. Kwa hiyo, kadri tutakavyokuwa tukipata fedha mradi huu utatekelezwa kwa haraka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kutokana na maeneo ya Mpemba na Katete kupata maji kwa kusumbua sumbua. Binafsi nimeshafika pale kwenye mradi ule, nilikwenda nikiwa na Mbunge wa Jimbo na tulifanya kazi vizuri sana na niliacha maagizo ya kujitosheleza. Na yule meneja ambaye alikuwa pale ambaye kidogo alisuasua tulimbadilishia kazi, tulimwondoa pale na sasa hivi anakuja meneja mwingine mwenye maagizo kamili ili miradi hii yote iweze kutekelezwa kwa kina.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; baadhi ya wananchi waliovunjiwa nyumba hizi tayari walikuwa na hati ambazo zilikuwa zimetolewa na Serikali. Sasa je, Serikali haioni imefanya maonezi makubwa kwa kuwavunjia wananchi ambao tayari walikuwa na hati zilitolewa na Serikali yenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili nataka kujua sasa ni lini Serikali itatoa viwanja mbadala kwa wananchi hao ili kutokuwaumiza kama walivyofanya sasa? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la hati miliki pia kuhusiana na suala la pili la viwanja mbadala kwa kuwa jambo au shauri hili liko mahakamani, ningeomba tuwe na subira na tutakapopata mwongozo wa mahakama tutakuja kueleza hatua zinazofuatia.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba niwe na maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza: Kwa kuwa nyavu nyingi zinaagizwa kutoka nje ya nchi na kuingizwa ndani ya nchi, lakini mwisho wa siku, mvuvi ndio amekuwa mhanga mkubwa wa hizi nyavu: Je, Serikali imewahi kuwawajibisha watendaji wengine kama ilivyowataja kwenye swali la msingi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha wavuvi kupata vifaa vya kisasa ili waondokane na zana za uvuvi zilizopitwa na wakati?

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Eng. Stella Simon Fiyao, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali kuhusu je, wapo ambao wamewahi kuwajibishwa kutokana na kwamba nyavu hizi huwa zinaagizwa kutoka nje au zinazalishwa na watu, wapo? Zipo kesi kadhaa ambazo zimewahusisha waagizaji na zilizowahusisha watengenezaji na kesi hizi zote tulipokwenda Mahakamani Serikali ilifaulu kwa kushinda kesi zile. Zipo kesi nyingine ambazo hata sasa bado zinaendelea. Wako watendaji ambao walichukuliwa hatua mbalimbali na wengine kesi zao bado ziko Mahakamani.

Mheshimiwa Spika, swali la pili alitaka kujua juu ya uwezeshaji wa makundi ya wavuvi kwa kupata vifaa vya kisasa. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Serikali yetu ya Awamu ya Sita. Tunayo program kubwa ambayo inaendelea hivi sasa ya kuhakikisha kwamba tunakwenda kukopesha boti za kisasa takribani 150 hadi 160 kwa wavuvi wote nchini, wale watakaokidhi vigezo. Boti hizi zitakuwa na vifaa kama vile fish finder kwa maana ya kile kifaa cha kujua Samaki walipo, vilevile eneo la kuhifadhia samaki takribani tani moja hadi tani moja na nusu, GPS na zitakuwa zimeunganishwa katika Satelite ili mvuvi kabla hajatoka kwenda katika uvuvi awe tayari na picha ya kujua mahali walipo samaki. Ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka kujua ni lini mradi mkubwa wa maji kutoka Wilaya ya Ileje, Mto Songwe kwenda Jimbo la Tunduma utaanza kutekelezwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mradi huu ni mradi mkubwa na tayari umeshaanza utekelezaji kwa hatua za awali na tunatarajia maji Tunduma yatafika kwa sababu ni mradi ambao unajengwa kwa awamu.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango gani wa kupanua barabara ya kutoka Mpemba mpaka Transfoma Tunduma ili kuepusha changamoto ya mrundikano wa magari ambayo wananchi wamekuwa wakikabiliano nayo ambayo inasababisha ajali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara ya Mpemba kwenda Tunduma ni sehemu ya barabara ya Igawa - Songwe - Tunduma na ipo kwenye evaluation hivi tunavyoongea, ahsante. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Nataka kujua ni lini Serikali itaanza upanuzi wa barabara kutoka Mpemba mpaka Tunduma – Transfoma ili kuepusha changamoto ambayo wananchi wamekuwa wakiipata kutokana mlundikano na msongamano mkubwa wa magari makubwa ambayo yamekuwa yakivuka mpaka wa Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFRY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stella Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja imeshafanyiwa usanifu na ni sehemu ya barabara ya kuanzia Igawa – Mbeya hadi Tunduma. Na barabara hii kipande cha Mpemba hadi Tunduma kitapanuliwa kuwa njia nne. Kwa hiyo iko kwenye mpango na tunategemea mwaka ujao wa fedha tutaanza kupanua hii barabara kuwa njia nne ili kupunguza msongamano ambao upo katika mji wa Tunduma. Ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imetambua uwepo na umuhimu wa Bandari Kavu ndani ya Mji wa Tunduma na tayari Halmashauri ya Mji wa Tunduma imetenga zaidi ya ekari 2,000 kwa ajili ya uwekezaji wa bandari kavu. Sasa nataka kujua je, ni sekta ngapi binafsi ambazo zimefikiwa mpaka sasa ili kuja kuwekeza bandari kavu ndani ya Mji wa Tunduma?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Taifa sasa lipo katika ushindani wa kibiashara; je hatuoni kuchelewachelewa tunaweza tukaleta matokeo hasi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalumu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Halmashauri ya Tunduma ina eneo la kuweza kujenga bandari hii kavu na sekta ambazo ziko tayari kwa ajili ya uwekezaji katika eneo hili la bandari kavu, kuna Sekta ya Kilimo, Sekta ya Viwanda na Sekta ya Mifugo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali lake la pili, suala la kuchelewachelewa. Kimsingi Serikali imechukua hatua za kuongea na watu binafsi na ndio maana hadi sasa tupo kwenye majadiliano ya mwisho ili eneo la Mpemba ambalo litakuwa linaunganisha upande wa Malawi pamoja na Zambia na DRC liweze kujengwa Bandari hii kavu, ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi; nataka kujua ni lini scheme ya umwagiliaji itajengwa Makwale Wilayani Kyera?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, scheme ya Makwale Wilayani Kyera ni moja kati ya scheme muhimu sana kwa wakulima wa Wilaya ya Kyera. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba tarehe 25/4/2023 tunakwenda kusaini mkataba na mkandarasi na kazi itaanza mapema kwa ajili ya ujenzi wa scheme hiyo.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naoma kujua ni lini Serikali itaona umuhimu wa kujenga barabara ya kutoka Chapwa halmashauri ya Mji wa Tunduma kuelekea Chindi mpaka Chitete ili kurahisisha mawasiliano ndani ya Wilaya ya Momba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kwa sasa inahudumiwa na wenzetu wa TARURA, ambayo inaunganisha Makoa Makuu ya Wilaya ya Momba Chitete kuja Tunduma. Hata hivyo nitaichukua ili kama Serikali tuone namna tukavyofanya kuijenga kwa kiwango cha lami ili kuiunganisha Tunduma na Makao Makuu ya Wilaya ya Momba Chitete, ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Mkoa wa Songwe una halmashauri tano na magari yako katika halmashauri mbili ambayo ni halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na Halmashauri ya Mji wa Tunduma, lakini kuna halmashauri ya Ileje, Momba na Songwe mpaka sasa hayana magari ya zimamoto.

Je, mnatumia njia gani kukabiliana na majanga ya moto yanapotokea katika Wilaya hizi?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa magari yaliyopo katika Wilaya ya Halmashauri ya Mbozi na Halmashauri ya Mji wa Tunduma ni magari madogo hayana uwezo mkubwa wa kukabiliana na majanga makubwa ya moto.

Je, ni lini mpango wa Serikali kuhakikisha wanaleta magari makubwa na ya kisasa kwa akili ya kukabiliana na majanga ya moto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, ni kweli tunatambua uwepo wa Halmashauri tatu za Wilaya ambazo hazina magari, na ndiyo maana kwenye jibu la msingi nimesema tunaendelea kuliwezesha Jeshi la Zimamoto hatua kwa hatua kutegemea upatikanaji wa fedha. Hata hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wabunge wa majimbo, akiweno Mwenisongole amewasiliana na Wizara kwa kaaribu na Mkuu wa Fire nchini na tumewaahidi kuwapa gari moja hata kabla ya magari ambayo tuna plan kununua hatujanunua.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu uwezo mdogo wa magari tunatambua, ndiyo maana kwenye bajeti ijayo ambayo tutaleta tuombe Bunge lako lituhidhinishie ipo bajeti ya kununua magari makubwa na kadri yatakavyokuwa yananunuliwa tutakuwa tunapeleka kwenye Wilaya zenye changamoto zikiwemo hizo Wilaya za Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Spika, niwashukuru watu wa Songwe, kwenye wilaya tatu alizozitaja hakuna matukio ya mara kwa mara ya majanga ya moto yanayohitaji uokoaji. Tunashukuru kwamba elimu ya zimamoto na wokozi wanaizingatia wananchi wa Mkoa huo. Ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Wananchi wa Mkoa wa Songwe wana changamoto wanapokwenda kuhitaji huduma kutoka mkoani imewalazimu kwenda kupitia Mkoa wa Mbeya na kuanza usafiri kuelekea Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Barabara kutoka Mloo – Isasa – Magamba mpaka Mkwajuni ili kurahisha huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Songwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyotamka Mheshimiwa Mbunge iko katika mpango wa Serikali wa kujenga na sasa tunatafuta fedha ili tuanze ujenzi wa barabara hii, ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Naibu Waziri, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, ninataka nijue barabara hizo unganishi ambazo zimejengwa kwa kiwango cha lami ni zipi.

Swali langu la pili, barabara hii ya Mlowo – Kamsamba imekuwa na changamoto kubwa sana kwa wananchi wetu, lakini changamoto hizi zinatukosesha fursa muhimu za kiuchumi. Nataka kujua Serikali ina mkakati gani wa maksudi kuhakikisha inajenga barabara hizi kwa wakati na muda muafaka ili kuondoa changamoto ambazo wanakutana nazo wananchi wa Mkoa wa Songwe, Momba na maeneo mengine kwa ujumla. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nimemuelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa nasema tumeanza kuijenga, tuna Daraja la Mto Momba ambalo liko katika hiyo barabara, katika hilo daraja tumejenga approach roads ambazo zinaunganisha lile daraja ukitokea Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Rukwa. Kwa hiyo, kwa pande zile mbili tayari kuna lami upande huu na huu, zile ndiyo barabara unganishi na lile daraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maksudi, kwamba je, tuna mkakati gani kuhakikisha kwamba tunajenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami. Bajeti inaendelea, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imetenga fedha, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, kwamba tutaanza kuijenga hiyo barabara ili kukuza uchumi pia kurahisisha usafiri kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe wa Mlowo, Igamba, Utambalila, Kamsamba lakini pia Utambalila kwenda Makao Makuu ya Mji wa Momba ambayo ni Makao Makuu ya Wilaya. Ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niwe na maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Swali langu la kwanza, Taasisi nyingi za Umma zimejikita katika kutoa huduma na hazifanyi biashara: Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka kuondoa kodi ya ardhi ili kuziwezesha taasisi nyingi kuweza kupata hati? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, nataka kujua: Ni lini Serikali itakamilisha kutoa hati katika maeneo 787 yaliyosalia katika Halmashauri za Mkoa wa Songwe ili yaweze kupatiwa hati na kuepusha migogoro ya ardhi isiyokuwa na ulazima baina ya wananchi na Serikali? Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu hizi Taasisi za Umma kuziondolea kodi, hili tumelichukua na tutakwenda kulichakata na kuona namna nzuri ya kufanya. Mara nyingi sana taasisi zinazoomba kumilikishwa maeneo haya zinakuwa na makusudio maalum pamoja na miradi maalum. Kwa hiyo, kwao inakuwa ni rahisi sana kutumia vyanzo vyao vidogo kwa ajili ya kumilikishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la lini maeneo yaliyobaki katika Mkoa wa Songwe yatakwenda kukamilishiwa umilikishwaji wake? Niwaombe hizo taasisi kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, waanze mchakato wa kuomba namna ya umilikishwaji. Hatua zote ziko wazi na taasisi hizo zote zinaelewa utaratibu ambao tumejiwekea katika uratibumzima wa kumilikisha ardhi hapa nchini.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kuna changamoto kubwa sana ya mlundikano wa malori ndani ya Mji wa Tunduma ambao unasinyaza na kufubaza uchumi wa Wana-Tunduma. Serikali mna mpango gani wa kujenga njia ya dharura ili kunusuru hali iliyopo kwenye Mji wa Tunduma? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna msongamano mkubwa sana katika Mji wa Tunduma ambao ndipo tunapotoka pale kwenda Zambia. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Tunduma kwamba tunakwenda siyo tu kufanya mpango wa dharura, lakini mpango kamili wa kujenga barabara ya njia nne katika Mji wa Tunduma ambapo tutakwenda kujenga kwa mpango wa EPC+F.

Mheshimiwa Spika, moja ya maeneo ambayo tunategemea kuanza ni pamoja na miji ya Tunduma ili kukwamua na kuondoa changamoto ambayo ipo inayosababisha msongamano mkubwa katika Mji wa Tunduma. Kwa hiyo, mkataba huo tunategemea utasainiwa Juni mwaka huu wa fedha, ahsante. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma Kata ya Chiwezi bado haijafikiwa na umeme. Serikali mna mkakati gani wa kuhakikisha wananchi wa Chiwezi wanapata huduma ya umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Chiwezi watapata umeme kabla ya mwezi Desemba mwaka 2023.

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini naomba niwe na swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara imekuwa na utaratibu wa kufikisha huduma katika makao makuu ya vijiji na kusababisha watu wa vitongoji kukosa huduma.

Je, ni lini Wizara hii itaanza kufikisha huduma hii kwenye vitongoji ili wananchi wengi waweze kufikiwa na huduma hii ya Umeme? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba hatua ya kupeleka miundombinu ya umeme kwenye maeneo yote ya vijiji imekuwa ikienda awamu kwa awamu, ni kwamba tulianza na vijiji kidogo kulingana na uwezo wa Serikali uliokuwepo, lakini baadaye Serikali ikajihimu na kuhakikisha vijiji vyote vinafikishiwa miundombinu ya umeme angalau kwa kuanza na makao makuu ya vijiji. Lakini ipo mipango ya Serikali madhubuti kabisa ya kuhakikisha kwamba kila eneo linafikiwa na umeme na njia hizo ni kwa kuanza na miradi yetu ya ujazilizi inayoitwa densification ambapo tuna ya kwanza, ya pili na ya tatu zinaendelea, na zitaendelea kufanyika kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, lakini Serikali imeona ni vema kutafuta fedha nyingi kwa wakati mmoja na kumaliza vitongoji vyote ambavyo havijafikiwa na umeme na kama ambavyo tumeshasema mara kadhaa hapa Bungeni tumeona kwamba tunahitaji takribani shilingi trilioni sita na bilioni kama mita tano ili kumaliza maeneo yote ya vitongoji na Serikali ipo katika harakati za kuhakikisha kwamba inapata fedha hii kufikisha umeme katika maeneo hayo, lakini katika kipindi hiki cha kuanzia fedha inapopatikana Serikali inazidi kusogeza miundombinu ya umeme katika vitongoji kwenye maeneo yetu. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. Maeneo mengi ya Wilaya ya Ileje, kuna changamoto kubwa ya mawasiliano ni upi mpango wa Serikali kupeleka miundombinu ya mawasiliano ya kutosha ili kurahishisha huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Ileje?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge, ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu na kwa bahati nzuri amekuwa mshauri mzuri sana katika Wizara yetu kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto za mawasiliano. Jambo jema kabisa ni kwamba katika minara ile 758, kati ya Majimbo ambayo yamebahatika sana ni Jimbo la Ileje ambalo limepata minara mitano. Kwa hiyo, ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, hivyo, tumuombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kutupatia ushirikiano kuhakikisha kwamba wananchi wanatoa maeneo bila kuwa na masharti magumu ili tuhakikishe kwamba miradi hii inaanza kwa wakati na kukamilika kwa wakati, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, pamoja na majibu ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, fedha iliyokuwa imetengwa ni shilingi bilioni 6.53 lakini mpaka sasa fedha iliyotolewa ni shilingi bilioni 1.14 hasa ukizingatia sasa hivi tuko mwezi wa Nane wa mwaka wa kibajeti bado miezi minne tu ili tuweze kumaliza mwaka wa fedha. Nataka kujua ni mpango upi wa Serikali kuhakikisha mnapeleka fedha zote kwa wakati ndani ya mwaka huu wa bajeti ili chuo hiki kiweze kujengwa kwa wakati?

Swali langu namba mbili, nataka kujua, je, Serikali mna mkakati gani sasa wa kuhakikisha mnapata wakufunzi wa kutosha na wanafunzi ili chuo hiki kitakapoanza kiweze kufunguliwa kwa muda na kuanza kwa wakati, nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Stella Fiyao, kama alivyouliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ni kweli kwamba kulikuwa na ucheleweshaji kidogo wa upelekaji wa fedha katika fedha ambayo ilikuwa imetengwa ya shilingi bilioni 6.53 lakini mpaka hatua hii ninavyosema shilingi bilioni 1.14 imekwenda na katika mwaka huu wa fedha katika hatua hii ya mwisho tayari kuna fedha zingine ambazo tunatarajia kuzitoa kwenye disbursements nyingine. Changamoto tu ilikuwa ni ya upatikanaji wa fedha lakini azma ya Serikali na dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassani ya kujenga imeendelea kuwepo na siyo tu kwa Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge atakumbuka kuwa tunajenga eneo la Mbozi katika Halmashauri ile lakini pia kwenye Mikoa mingine ujenzi unaendelea. Kwa hiyo, usiwe na wasiwasi nafurahia kwamba ana dhamira ya dhati kuona kwamba chuo kile kinaanza kufanya kazi. Kwa hiyo, fedha zitapelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza kama tunao mpango gani kuhusiana na kupeleka wakufunzi pamoja na wanafunzi wa kujifunza pale. Dhamira ya Serikali ya kujenga vyuo hivi katika andiko lake kuu ni pamoja na uwepo wa vitendeakazi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanakuwepo lakini pia vifaa vya kijifunzia na mashine za wanafunzi hawa kujifunza, yote haya yako katika mpango wa bajeti na kwamba tutaenda kukamilisha mara pale chuo kitakapokamilika ili wanafunzi hawa wa Kitanzania waweze kupata fursa hiyo ya kujifunza na kuchangia katika ujenzi wa Taifa, ahsante. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kujua mradi mkubwa wa maji kutoka Momba kwenda Tunduma mpaka Mbozi umefikia hatua gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stella Fiyao, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi mkubwa anaouongelea ni mradi wetu wa kimkakati kama Wizara, tukitambua changamoto kubwa ya maji katika Mji wa Tunduma vilevile Mji wa Momba. Mradi huu tayari utekelezaji unaendelea na tutahakikisha unakwisha kwa wakati.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kata ya Mlowo ni Kata ambayo iko katikati ya Mji ndani ya Wilaya Mbozi, lakini kuna baadhi ya maeneo kumekuwa na changamoto kubwa ya mawaliano ikiwepo eneo la Saganoti na maeneo mengine ya Forest. Serikali ina mkakati gani wa kurekebisha mawasiliano katika maeneo haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti ni dhamira ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kupitia utekelekezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma ya mawasiliano. Kwa sababu hiyo, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunajiridhisha kila sehemu ambayo ina changamoto ya mawasiliano, basi tunafika na kuchukua hatua stahiki ili Watanzania wote waweze kupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Stella, baada ya Bunge hili tuweze kuwasiliana ili tuweze kuchukua taarifa kamili kuhusiana na maeneo husika ili sasa tutume watalamu wetu wakajiridhishe ni nini kikafanyike katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya mawasiliano, ahsante.