Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Stella Simon Fiyao (15 total)

MHE. STELLA S. FIYAO Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuondoa kodi kandamizi kwa wafanyabiashara na kuweka kodi rafiki ili kuwasaidia kufanya biashara kwa uhuru na kulipa kodi kwa wakati na kuondokana na sintofahamu ya wafanyabiashara kukimbilia kufanya biashara nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitozi kodi kandamizi. Aidha, Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara ikiwa ni pamoja na kuongeza vivutio na fursa mbalimbali za uwekezaji kwa wazawa na wawekezaji kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kupitia na kuimarisha mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi kwa kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Ufanyaji wa Biashara nchini (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment) wenye lengo la kurahisisha mazingira ya kufanya biashara ambapo kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2019/2020 ilifuta tozo na ada zisizo rafiki 54 zilizokuwa zinatozwa na wakala, taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imekuwa ikifanya maboresho mbalimbali kwenye viwango vya kodi kupitia Sheria ya Fedha (Finance Act) kila mwaka kwa lengo la kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi na mapato mengine ya Serikali, kuchochea ukuaji wa biashara ndogo na za kati pamoja na kuhamasisha uzalishaji viwandani na kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani kutoka nje.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatengeneza kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mbalizi – Mkwajuni ili kuepusha adha wanayokutana nayo Wananchi hususani kipindi cha mvua?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Mbalizi – Chang’ombe – Mkwajuni – Patamela – Makongolosi yenye urefu wa kilometa 117 ni barabara ya Mkoa inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Songwe na inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu ya Mbalizi hadi Galula yenye urefu wa kilometa 56.

Aidha, taratibu za ununuzi kwa ajili ya kumpata Mhandisi Mshauri wa kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina zizonaendelea kwa sehemu ya Galula – Mkwajuni - Makongolosi kilometa 61 zinaendelea. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu ya Mbalizi hadi Galula chenye urefu wa kilometa 56 ambayo upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekamilika.

Mheshimiwa Spika, wakati ujenzi kwa kiwango cha lami ukisubiri upatikanaji wa fedha, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), inaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali kila mwaka barabara hii. Ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Asilimia 70 ya wakazi wa Mkoa wa Songwe wanategemea kilimo: -

Je, ni lini Serikali italeta pembejeo za kilimo kwa bei nafuu ambayo wakulima wengi wataweza kumudu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tumeanza kuboresha mifumo ya upatikanaji wa pembejeo kwa maana ya mbegu, mbolea na viuwatilifu, kuratibu mahitaji ya pembejeo kutoka katika mikoa na kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya makampuni kupeleka na kuuza. Majukumu hayo yanatekelezwa kwa kutumia mfumo wa bulk purchase hasa katika eneo la mbolea.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwa mfumo huu wa ununuzi bei za ununuzi kwa maana ya Free on Board zimepungua. Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni gharama za usafiri na bima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza upatikanaji wa pembejeo kwa kuvutia wawekezaji wa kampuni binafsi hasa katika eneo la mbegu, mikataba maalum kwa ajili ya kupunguza gharama.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati mingine ni kuanzisha mifumo ya ugharamiaji wa sekta ikiwemo uanzishwaji wa Mfuko wa Pembejeo (Credit Guarantee Scheme) pia kupunguza au kufuta baadhi ya tozo na ada. Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali imepitia na kufuta tozo 12 katika mbegu na tozo nne za mbolea ili kupunguza bei na gharama za pembejeo hizo.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Mradi mkubwa wa maji katika Mji wa Tunduma ili kutatua changamoto wanayoipata wakazi wa mji huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Tunduma unapata maji kutoka kwenye visima virefu tisa vilivyoko maeneo ya Ikulu, Sogea, Mamboleo, Tazara, Maporomoko, Mahakamani, Majengo, Msongwa na Makambini. Visima hivyo vinazalisha maji lita 2,072,000 kwa siku wakati mahitaji ya maji kwa Mji huo ni lita 4,413,000 kwa siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha huduma ya maji safi na salama katika Mji wa Tunduma, Serikali inatekeleza mipango ya muda mfupi na muda mrefu, ambapo katika mpango wa muda mfupi mwaka 2020/21, Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), imechimba visima virefu sita vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita 600,000 kwa siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji ya visima hivyo utafanyika kuanzia mwezi Julai, 2021, na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Septemba, 2021. Vilevile, Serikali itafanya upanuzi wa mtandao wa maji katika maeneo mengine ya Mji wa Tunduma ikiwemo maeneo ya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa muda mrefu wa kuboresha huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza katika Mji wa Tunduma, Serikali imepanga kujenga mradi kupitia chanzo cha maji cha Mto Bupigu uliopo Wilaya ya Ileje wenye uwezo wa kuzalisha maji kiasi cha lita milioni 73 kwa siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina (detailed design) wa mradi huo anatarajiwa kupatikana katika robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2021/2022. Aidha, Serikali itaendelea kufanya utafiti wa vyanzo vya maji juu na chini ya ardhi ili kupata maji yenye kutosheleza katika Mji wa Tunduma na miji mengine hapa nchini.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani kwa wananchi wa Kata ya Majengo Tunduma waliovunjiwa nyumba zao?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 133 lililoulizwa na Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba kabla sijajibu swali nitoe maelezo machache ya utangulizi. Kikao cha Makatibu Wakuu wa Nchi za Tanzania na Zambia kilichofanyika mwezi Oktoba, 2013, pamoja na mambo mengine kiliazimia kwamba alama za katikati ya mpaka (Intermediate Boundary Pillars) kwa sehemu ya mpaka yenye urefu wa kilomita 50 ziongezwe ili kuzuia ongezeko la shughuli za kibinadamu na pia eneo la hifadhi ya mpaka lipunguzwe kutoka mita 100 kila upande zilizokuwa zinatambulika hapo awali hadi mita 50 kila upande. Hata hivyo, pamoja na maazimio hayo kutekelezwa, baadhi ya wananchi waliendelea kuvamia eneo la hifadhi ya mipaka kwa kujenga makazi.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017, Serikali ilitoa tamko la kuvunja nyumba zote zilizojengwa katika eneo la hifadhi ya mpaka suala ambalo lilipingwa na wananchi 134 kwa kufungua Shauri Na. 195/2017 katika Mahakama Kuu, Mbeya. Shauri hilo lilifutwa mwaka 2019 na hatimaye jumla ya nyumba 193 zilizokuwa ndani ya eneo la mita 50 za hifadhi ya mpaka zilibomolewa.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua hiyo, wananchi 35 walifungua tena shauri Na. 12/2019 katika Mahakama Kuu Mbeya kudai fidia kutokana na kubomolewa kwa nyumba zao. Baada ya mazungumzo nje ya Mahakama (mediation) yenye lengo la kuwapatia viwanja mbadala, wananchi hao kushindikana, shauri hilo limepangwa kuendelea kusikilizwa tarehe 5 Oktoba, 2022.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua shauri hilo na kauli yetu ni kwamba tusubiri mwongozo au maamuzi ya mahakama ili tujue hatua zinazofuatia.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuzuia nyavu haramu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara imeandaa Mkakati wa Kusimamia Rasilimali za Uvuvi ambao unajumuisha mbinu mbalimbali za kudhibiti utengenezaji, uagizaji, matumizi na biashara ya nyavu haramu za uvuvi. Utekelezaji wa mkakati huo unahusisha wadau mbalimbali ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, sheria, watendaji wa taasisi zilizopo mipakani, bandarini na viwanja vya ndege; Viongozi wa Mikoa na Wilaya, wavuvi pamoja na watendaji wa Wizara kupitia vituo vya ulinzi wa rasilimali za uvuvi. Aidha, elimu kwa wadau kuhusu matumizi ya nyavu sahihi, uvuvi endelevu na wenye tija inaendelea kutolewa. Ahsante.
MHE. KUNTI Y. MAJALA K.n.y. MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Ivuna hadi Chole ili kurahisisha mawasiliano kati ya Wilaya ya Momba na Songwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Ivuna hadi Chole yenye urefu wa kilomita 18.5 ni barabara muhimu iliyopo Wilaya ya Momba ambayo inaungainisha barabara ya Muheza hadi Isanzu yenye urefu wa kilomita 12 katika Wilaya ya Songwe. Ili kuunganisha Wilaya hizi mbili jumla ya kilometa 30.50 zinatakiwa kufanyiwa matengenezo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/ 2023, Serikali itatenga jumla ya Shilingi Milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 200 katika barabara ya Ivuna – Chole Wilaya ya Momba na kwa upande wa Wilaya ya Songwe Shilingi Milioni 100 kwa ajili ya kufanya matengenezo yenye urefu wa kilomita 3 katika barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara katika barabara hii yenye urefu wa kilometa 30.5 kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Bandari kavu katika Mji wa Tunduma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekamilisha zoezi la kufanya upembuzi yakinifu wa kuendeleza bandari kavu zote nchini ikiwemo ya Bandari Kavu ya Tunduma.

Mheshimiwa Spika, Kiuchumi na kibiashara, Bandari Kavu ya Tunduma ni muhimu sana kwa sababu ndilo langu kuu la kupitisha bidhaa za nchi za Zambia, DRC na nchi nyingine kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Bandari hiyo ina mvuto zaidi wa kibishara, mpango wa Serikali ni kushirikisha sekta binafsi ikiwa pamoja na halmashauri kwenye maeneo husika. TPA inaendelea na vikao vya wadau ili kushawishi uwekezaji huo.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kununua Gari la Zimamoto katika Mkoa wa Songwe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Songwe lina magari mawili ya kuzima moto. Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe Wilaya ya Mbozi Mji Mdogo wa Vwawa kuna gari moja aina ya Fuso yenye namba za usajili ZT 0014. Gari hilo linaujazo wa lita 1,500 za maji na lita 500 za foam. Katika Wilaya ya Tunduma kuna gari moja aina ya Mitsubish Canter yenye namba za usajili STL 4914 na lina ujazo wa lita 1,200 za maji.

Mheshimiwa Spika, Aidha, Serikali itaendelea kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuliongezea wataalam na vitendea kazi ikiwemo magari ya kuzima moto na uokoaji kwa Mkoa wa Songwe kwa madhumuni ya kuzifikia wilaya zote kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mlowo – Kamsamba kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Mlowo – Kamsamba yenye urefu wa kilometa 130.1 kwa awamu kwa kuanza na ujenzi wa Daraja la Momba lenye urefu wa mita 80 pamoja na barabara zake unganishi zenye urefu wa mita 950 na kazi ya ujenzi imekamilika. Aidha, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii. Katika mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa Hati kwa maeneo yote ya Umma katika Halmashauri za Mkoa wa Songwe?

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri tano za Mkoa wa Songwe, jumla ya maeneo ya umma 1,679 yanatumika kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama vile Shule, Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali, Vyuo, Ofisi, Vituo vya Polisi, Mahakama, Maeneo ya Majeshi, Hifadhi za Misitu na Wanyama na Maeneo ya Makumbusho yanayotumiwa na Serikali au Taasisi. Aidha, maeneo 892 yameshapimwa ambapo kati ya hayo, maeneo 637 yameshakamilishwa na kutolewa Hatimilki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuongeza kasi ya umilikishaji wa maeneo ya matumizi ya umma, Serikali imefanya jitihada madhubuti ikiwemo kuondoa au kupunguza baadhi ya gharama za umilikishaji wa maeneo hayo. Hata hivyo, baadhi ya Taasisi za Serikali zikiwemo Halmashauri zetu zimeshindwa kutenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya umilikishwaji wa maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa viongozi wa Serikali na Wakuu wa Taasisi nchini wakiwemo viongozi wa Halmashauri za Mkoa wa Songwe kuhakikisha wanatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kugharamia upimaji na umilikishwaji wa maeneo yao, ahsante.
MHE. TUNZA I. MALAPO K.n.y MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha Vijiji vyote vya Mkoa wa Songwe vinapatiwa umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Songwe una jumla ya vijiji 307 ambapo hadi kufikia tarehe 31 Mei 2023, vijiji 240 vilikua tayari vimepatiwa umeme, Vijiji 67 vilivyosalia viko kwenye mkataba wa Mkandarasi M/s Derm Electrics Ltd anayetekeleza mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu III Mzunguko wa II katika Mkoa wa Songwe. Kazi za ujenzi wa miundombinu na kuunganisha wateja katika vijiji hivyo inaendelea na mradi unatarajiwa kukamilika Desemba, 2023, nakushukuru.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA K.n.y. MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutafuta masoko ya mazao ya kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2023/2024, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itaendelea kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi kwa kujenga masoko ya kimkakati mipakani, ujenzi wa vituo vya masoko na kuboresha miundombinu ya maabara za TPHPA ili ziweze kupata ithibati itakayowezesha kufanya uchunguzi na kutoa vyeti vya ubora vinavyokubalika Kimataifa, kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali inaendelea na majadiliano na nchi mbalimbali na kufungua masoko ya mazao katika nchi hizo. Hadi sasa tumefanikiwa kufungua soko la korosho nchini Marekani, soko la parachichi China, India na Afrika Kusini na tunaendelea kuhudumia masoko ya nafaka katika nchi mbalimbali za Afrika.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango wa kuhakikisha vijiji vyote vya Mkoa wa Songwe vinapata umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Songwe una jumla ya vijiji 307; vijiji 180 vina umeme na vijiji 127 havijafikiwa na miundombinu ya umeme. Vijiji hivyo 127 ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme vinanufaika kupitia mradi wa REA III mzunguko wa pili unaoendelea. Utekelezaji wa mradi unaendelea na Mkandarasi Derm Electrics ndiye anayetekeleza mradi kwa kipindi cha miezi kumi na nane kwa gharama ya shilingi bilioni 11.23. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2022.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA Mkoa wa Songwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa sasa inatekeleza azma ya kujenga Chuo cha Ufundi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali ilitenga shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kujenga vyuo vya ufundi stadi katika Wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi ikiwamo Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe. Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe kimetengewa fedha shilingi bilioni 6.53 kwa ajili ya ujenzi wa jumla ya majengo 25 ikijumuisha jengo la utawala, karakana, madarasa, maktaba, bwalo la chakula, vyoo, stoo pamoja na nyumba za watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshapeleka shilingi bilioni 1.14 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe ambapo kwa sasa ujenzi umefikia hatua ya kukamilika kwenye baadhi ya majengo na kazi ya ujenzi wa kuta inaendelea. Ahsante.