Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Suma Ikenda Fyandomo (30 total)

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante; kauli ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ni kumtua ndoo mama kichwani, lakini Tukuyu kuna shida sana ya maji, Serikali ilipanga kutoa fedha shilingi bilioni
4.5 kumaliza tatizo la maji Tukuyu mjini. Lakini mpaka sasa wamepeleka shilingi milioni 500 tu sasa akinamama wa Tukuyu hali ni mbaya sana kutafuta maji.

Sasa je, ni lini Serikali itapeleka hizo fedha kiasi cha shilingi bilioni nne ili kumaliza tatizo la maji Tukuyu mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Mbeya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli na hii si mara ya kwanza Mheshimiwa Suma Fyandomo kufuatilia na amekuwa akifuatilia kwa ushirikiano wa karibu kabisa na Mheshimiwa Mwantona na sisi Wizara ya Maji tumekaa jana, tumeshaweka kwenye mpango tunaongeza shilingi milioni 500 nyingine ili kazi ziweze kuendelea na mgao ujao tutaongeza tena shilingi milioni 500 hadi kuweza kukamilisha mradi huu muhimu kwa sababu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan lengo ni kuona maeneo yote maji yanapatikana bombani na Tukuyu ni moja ya eneo muhimu sana na Mheshimiwa Mbunge tutafanyakazi kwa pamoja, tutaleta maji kuhakikisha wakinamama wa Tukuyu pia tunawatua ndoo kichwani.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwetu kule Mkoa wa Mbeya Wilaya ya Rungwe kuna hospitali kubwa sana ambayo ilikuwa ikiwatibu watu wenye ugonjwa wa ukoma na watu kutoka nchi mbalimbali walikuwa wakitibiwa ikiwa ni pamoja na Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda na Malawi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali ile, ukoma ulifungwa rasmi mwaka 2002. Majengo yale ni hospitali kubwa ambayo ina wodi ya wanaume, wanawake na watoto, ina mochwari, bwalo, jiko kubwa, mpaka machine ya kuchomea takataka na Makanisa yapo pale, pia heka zaidi ya 100 ziko pale, lakini yamekaa bila kufanyiwa kazi yoyote: -

Je, Serikali ina mpango gani na majengo yale? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kujibu swali zuri la Mheshimiwa Mbunge, ameeleza kwamba kuna hospitali yenye facilities hizo. Sasa niweke tu vizuri kwamba suala la ukoma, bado tunaenda kuongeza nguvu kwa sababu tunataka mwaka 2030 ukoma uwe umeisha kabisa Tanzania. Ila wazo lake hilo ambalo anasema kuna facility hiyo ambayo inaweza kutumika kwa namna nyingine; baada ya Bunge tarehe 24, nitakuwepo Njombe, nitapitia Songwe kuangalia Hospitali ya Mkoa wa Songwe halafu tutaenda pamoja kutembelea hilo eneo na watalaam ili tuweze kuamua kwa kuangalia mazingira halisi na kuleta majibu ambayo yatakuwa sahihi kulingana na hali halisi ya kule. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ninaipongeza Serikali kwa kupata mkandarasi wa maji kwa ajili ya mradi wa Kiwira ambao utalisha wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya. Sasa je, ni lini Serikali itatoa fedha ili mkandarasi aanze kufanya kazi mara moja?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali muhimu la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mbeya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Suma kwa ufuatiliaji mzuri wa mradi huu muhimu ambao utakwenda kuleta manufaa kwa Mbeya Jiji na Wilaya jirani. Lini fedha inakwenda kupelekwa, tayari kazi zimeshaanza na Wizara tunafanya ununuzi na kupata Wakandarasi kwa sababu Mhandisi Mshauri ameshakamilisha kazi yake. Hadi kufikia Desemba mwaka huu mradi utaendelea na utekelezaji. Kwa hiyo, kwa kila hatua fedha inatolewa. Fedha ilishaanza kutolewa toka Februari na sasa hivi ipo katika maandalizi ya kumpata Mkandarasi.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, tumepata barabara ya mchepuo ya kilometa tatu ambapo mvua ikinyesha hali itakuwa mbaya zaidi. Je, Serikali ni lini itatujengea barabara ya lami kwa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mbeya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo barabara tuliyojenga ni kwa ajili ya dharura ili kuepusha ajali zilizokuwa zinatokea. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango wa Serikali sasa ni kuijenga barabara hiyo ya lami. Kwa hiyo, Serikali inatafuta fedha ili iijenge na liwe ni suluhisho la kudumu. Ahsante. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Mkoani Mbeya Wilayani Rungwe maarufu kama Tukuyu hakuna Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi yapata miaka minne sasa ambapo Halmashauri ya Busekelo inategemea hapo na tatizo hilo Mbarali kuna tatizo hakuna pia Mwenyekiti na Chunya, ukizingatia wananchi wa Chunya wanatoka mbali kabisa Kambi Katoto wanakwenda Mbeya Mjini ambapo ni karibu na Mkoa wa Tabora. (Makofi)

Sasa je, Serikali ni lini itatupelekea Wenyeviti Baraza la Ardhi kwenye Wilaya hizo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi Wizara inaendelea na utaratibu, ni maeneo mengi hayana Mabaraza haya, kwa hiyo Wizara inaendelea kufanya matayarisho kwa ajili ya kuajiri Wenyeviti wa Mabaraza na moja ya watakaoajiriwa tuta-consider hilo eneo la Tukuyu, ahsante. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ninashukuru sana kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutujengea jengo kubwa sana la zaidi ya bilioni 11 pale Mkoani Mbeya hospitali ya Meta.

Mheshimiwa Rais alizindua jengo hilo pindi alipofika mkoa wa Mbeya, hali imekuwa mbaya sana wanawake bado wanatumia jengo la zamani kujifungulia. Ni lini Serikali italeta vifaa hata angalau vitanda 100 ili wakinamama wanusurike kulala wanne wanne kwenye wodi ya zamani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Rais wetu alikwenda akafungua jengo kubwa sana la akinamama pale Mbeya Meta, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mkoa wa Mbeya ni kati ya Mikoa yenye hali nzuri sana ya afya ukilinganisha na sehemu zingine. Kwa maana ya kwamba ukiangalia hospitali ya Mkoa kuna ujenzi mkubwa sana unafanyika wa zaidi ya bilioni 21 na unaujua, pia ukienda kwenye hospitali ya Rufaa pale umeona jengo lililojengwa. Rais wetu alipoondoka alielekeza kwamba shilingi bilioni 2.1 zielekezwe pale kwa ajili ya kuhakikisha jengo hilo linawekwa vifaa na tayari vifaa vimenunuliwa kwa hiyo ndani ya miezi miwili zitakuwa zimefikishwa pale na kufanyia kazi. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pia nashukuru kwa majibu ya Serikali kwamba imejiandaa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa bypass, hata hivyo nina maswali ya nyonge. La kwanza, je, ni lini wananchi ambao wanakaa Uyole mpaka Ifisi watalipwa fidia zao ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, naomba kwa uzito wake, kuanzia Uyole mpaka Mbeya Mjini mpaka kufika airport ile barabara haina hata service road kwa maana hiyo mabasi, bajaji, maguta, malori pamoja na ambulance ambazo zinapeleka wagonjwa wa rufaa Mbeya, lakini usiombe kama unakwenda airport unaweza ukapaki gari pembeni ukapanda bajaji ama bodaboda ili kuwahi kule inakuwa shughuli.

Je, ni lini Serikali itatafuta Mkandarasi kwa haraka ili kuweza kuepusha ajali zinazotokea mara kwa mara kwa ufinyu wa barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la fidia kabla ya kuanza ujenzi wa barabara hii, fidia italipwa kwa wananchi ambao watapisha ujenzi huu. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jiji la Mbeya kwamba Serikali italipa fidia kabla ya kuanza ujenzi wa barabara hii.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge lakini pia na Mheshimiwa Spika ambaye najua hili jiji ni jiji lako kwamba, ni kweli barabara hii ambayo Serikali imeamua kuchukua hatua za haraka sana kulingana na ukweli kwamba msongamano ni mkubwa.

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba hatuna barabara hizi za kupaki bajaji na pikipiki lakini pia tunatambua kwamba barabara hii ndio inayopitisha mizigo karibu asilimia zaidi ya 50 ya mizigo inayotoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda DRC, Zambia na Malawi na ndio maana Serikali imechukua jitihada na hatua za haraka kuhakikisha kwamba barabara hii inapanuliwa na wakati inafanya design ni pamoja na kutengeneza hayo maeneo ambayo yatakuwa ni ya kupaki malori, mabasi na bajaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii itafanyika na tayari tupo kwenye hatua za manunuzi ili tunavyoanza tu Julai kazi ianze ya ujenzi huu pamoja na hizo parking ambazo Mheshimiwa Mbunge amezisema. Kwa hiyo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge hivyo. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, siku ya Jumanne liliulizwa swali la nyongeza la kuhusu hii barabara na majibu yako yalisema, ujenzi unaanza mwaka huu wa fedha ambao ni 2021/2022, majibu ya msingi hapa yanaonesha kwamba katika mwaka wa fedha 2022/2023, Sasa kwa sababu hapa umenitaja nimeona uliweke vizuri hilo tuwe tunajua 2021/2022 au 2022/2023. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba niliweke vizuri suala hili. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, tutaanza ujenzi kwa maana ya kupeleka mkandarasi site mara tunapoanza mwezi Julai, utekelezaji wa bajeti.

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye jibu la msingi tunasema taratibu za manunuzi zimeshaanza kwa maana ya kutafuta Mkandarasi, kusaini zabuni na kuanza kufanya tathmini. Kwa hiyo, ujenzi tunasema tayari tumeshaanza kwa sababu hizo hatua zimeanza na kwamba tutakapoanza tu mwaka mpya Mkandarasi anakuwa yupo site. Lakini taratibu za manunuzi zimeshaanza na tayari tumeshatangaza. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Napata shida sana mimi pamoja na wananchi wa Mkoa wa Mbeya, kwamba mradi wa zaidi karibu bilioni 300 sasa hivi unapewa shilingi 4,000,000,000, any way, ngoja niende kwenye maswali ya nyongeza.

Swali la kwanza; je, ni lini sasa Serikali itakamilisha mradi wa phase II ili kuhakikisha Wilaya ya Mbarali, Rungwe, Kyela na Chunya, Mbeya Mjini na Mbeya Vijijini ili waweze kupata maji?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Rais alivyokuja mwezi Agosti, 2022 alipita pale Wilayani Rungwe, alitoa agizo kwamba kufika mwezi Oktoba mradi wa maji unaoendelea pale Tukuyu uwe umekamilika, lakini sasa hivi Kata zote Bagamoyo, Msasani, Buliaga, Bitigi, Makandana, Kawetele maji ni shida kweli kweli. Sasa je, ni lini Serikali itakamilisha mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Suma Fyandomo amekuwa akifuatilia mradi huu muhimu, ni mradi wa kimkakati, phase II ambayo anaiulizia kupitia wilaya nyingine zote, itafanyika baada ya phase one kukamilika.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi tayari kupitia Mhandisi Mshauri ameshamaliza kuandaa nyaraka za zabuni kwa kufikia tarehe 26 Oktoba, kupitia Mamlaka ya Maji na tayari Mamlaka ya Maji imetoa nyaraka za zabuni za kandarasi za ujenzi katika mradi huu na tunategemea kwa namna ambavyo wakandarasi wameshapatiwa tarehe 8 Novemba, kandarasi nne zimeshafanikiwa kufika kwenye eneo la mradi, kuangalia hali ya mradi ili sasa ifikapo tarehe 7 Disemba tunatarajia vitabu vya zabuni viwe vimetoka, kwa hiyo wataenda kuvichukua. Ikifika mwisho wa mwezi Disemba sasa hapo ujengaji wa mradi phase one ndio unaanza. Kwa hiyo kwa maeneo hayo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge, yatafanyiwa kazi baada ya phase one kukamili.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na agizo la Mheshimiwa Rais, binafsi nilifika Tukuyu, nilikwenda kwenye chanzo, nilihakikisha tarehe ambayo tulimwahidi Mheshimiwa Rais, tuliweza kufikisha maji yale kutoka kwenye kile chanzo na tulishayaingiza kwenye existing line za Tukuyu Mjini na maji tayari yalishaanza kuingia kwenye maeneo yote. Kwa hiyo, kipindi hiki cha ukame, sio tu Tukuyu wala sio tu Mbeya, ni maeneo yote ya Tanzania tunapitia changamoto kwa sababu vyanzo vyetu vya maji kina kimeshuka.

Mheshimiwa Spika, kwa kupitia Bunge lako Tukufu, niombe sisi Wabunge wote tumwombe sana Mwenyezi Mungu mvua zinyeshe, hiyo ndio itakuwa suluhu na maeneo yote tutaendelea kupata maji kwa uzuri.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa maswali madogo mawili ya nyongeza.

Je, Serikali inampango gani kuajiri wanasheria ambao wanaweza kusaidia kuleta elimu ya mirathi katika ngazi ya kata?

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana na inatia huzuni wanawake wajane baadhi yao wamejikunja hawajui hatima yao kwasababu wanadhurumiwa haki zao za mirathi, hivyohivyo wanakuwa wanateseka kwa namna hata ya kusomesha Watoto wao;

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaleta sheria ambayo itasaidia kuleta mpango mkakati kwa ajili ya kunusuru ndoa na mirathi ili kuepusha changamoto za mirathi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa kuajiri wanasheria katika ngazi ya kata, kimsingi kule tuna Mahakama ambapo shughuli zote za kimahakama zinafanywa katika maeneo yale, na wale mahakimu ni watalamu ambao wamehakikiwa. Tunakwenda kubadili Sheria ile ya Wazee wa Baraza na badaye kuruhusu wanasheria binafsi vilevile kwenda kusimama kwenye mahakama hizo ili kuwasaidia wananchi wengi ambao wangehitaji msaada wa kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo suala la ule mkandamizaji napenda nitumie nafasi hii kuanza kuwafahamisha wananchi wote; kumekuwa na mkanganyiko tu wa akili za wananchi wachache wenye tamaa, unapopewa nafasi ya kuwa msimamizi wa mirathi huko ndiko kunako anzia tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msimamizi wa mirathi si mrithi. Msimamizi wa mirathi kazi uliyopewa ni kukusanya mali za marehemu na kusimamia warithi kupata kwa kuzingatia haki zao na mrithi namba moja kwenye haki za mirathi ni mke wa marehemu, watoto wa marehemu ndilo kundi la pili na kundi la mwisho ni wazazi wa marehemu, kama wapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kinachotokea sasahivi ni kwamba mtu akipewa tu nafasi ya kusimamia mirathi, anaanza kujirithisha yeye mwenyewe. Huyu ni mwizi na anastahili kushtakiwa kama mwizi wa kuaminiwa. Hili ndiyo jambo ambalo kimsingi linakera sana kwenye jamii zetu. Akina mama wengi wananyanyasika katika mazingira kwamba shemeji aliye aminiwa na ile familia kusimamia na kukusanya mali za marehemu yeye mwenyewe ndiye anabaki katika mazingira ya kurithi na kuila ile mali ya wale walengwa ambao kimsingi wanakuwa ni familia ile ya marehemu iliyoachwa baada ya kifo cha wazazi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili ni jambo tu la uelewa, hakuna mtu mwingine yeyote mwenye haki ya kurithi mali iliyoachwa na marehemu nje ya hao niliowataja. Kuna mila nyingine ni potofu sana; kwa mfano kuna mila ambazo zinamfanya mtu anaitwa mrithi awe na sauti asilimia mia kwenye mali zile. Ile si urithi wa kisheria. Urithi wa kisheria unaotambuliwa ni mke, watoto na mzazi wa marehemu; na katika mgao mzazi wa marehemu anapata kiasi kidogo sana kuliko watoto na mke wa marehemu kwasababu mke wa marehemu anakuwa bado anaendelea kuilea ile familia ambayo imeachwa na yule marehemu, ahsante.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, naomba kuiuliza Wizara, wananchi wa Mkoa wa Mbeya wanataka kujua ni lini barabara ya njia nne itaanza kujengwa ambayo ilisaidiwa kwamba kuanzia Uyole mpaka Mbalizi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, natambua umuhimu wa barabara hii ya Mbeya mpaka Tunduma na tayari Serikali ilikwishaitangaza na mkandarasi amepatikana na tunachosubiri na hata kwa maelekezo yako ni kwamba hivi karibuni hususan ndani ya mwezi huu wa pili tutasaini mkataba ili barabara hii ianze kujengwa kwa njia nne kama ambavyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alivyoahidi alivyotembelea Mkoa wa Mbeya, ahsante.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba tu kwa hekima, Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan amatusaidia sana kutupa fedha kiasi cha shilingi bilioni 7.2 pale Inyala binadamu wengi wamepoteza uhai.

Swali langu naomba kuuliza, je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara ya bypass kuanzia pale Mlima Nyoka mpaka Mbalizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kipande hicho kiko kwenye sehemu ya Igawa kwenda Tunduma na sasa hivi tupo kwenye evaluation, ahsante. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pale kwenye hospitali ya Wilaya ya Makandana tunaishukuru sana Serikali imepeleka vyombo muhimu sana kwa maana ya X-Ray na Ultrasound, lakini pale kuna Mtaalam mmoja kiasi kwamba akiugua au akipata dharura huduma hiyo inasitishwa kwa muda pale.

Je, ni lini Serikali itatuongezea Mtaalam mwingine kwa ajili ya Ultrasound na X-Ray?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Suma Fyandomo Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Hospitali ya Halmashauri ya Rungwe maarufu Makandana ni muhimu sana inaendelea kutoa huduma za jamii kwa wananchi wa Rungwe, Serikali imetambua uhitaji wa vifaatiba kama X-Ray na Ultrasound imepeleka inafanya kazi. Ni kweli kwamba tuna mtumishi mmoja lakini mpango wa Serikali ni kuhakikisha tunaendelea kuajiri watumishi hao na hivi sasa tumeweka mpango mkakati wa kuwasomesha wataalamu wa usingizi na Radiology ili wawe wa kutosha katika halmashauri zetu. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatafuta watumishi ili kuongeza watumishi katika hospitali ile.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Tukuyu una changamoto kubwa sana ya maji ikiwa ni Kata za Bulyaga, Msasani, Bagamoyo, Makandana, Ibigi, Kawetele; na Serikali iliahidi kupeleka shilingi bilioni 4.5 lakini mpaka sasa wamepeleka shilingi milioni 700 tu. Wananchi wa kule hasa akina mama wanaacha kufanya kazi kubwa za kutafuta riziki kwa ajili ya watoto wanashinda kutafuta maji.

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha hizo ili kumalizia mradi huo wa maji? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua maji hayana mbadala, maji ni uhai na Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan kila mwezi tunapokea zaidi ya shilingi bilioni 14, 15 katika Mfuko wetu wa Maji.

Nataka nimhakikishie tutawapa kipaumbele Wanatukuyu ili kuhakikisha miradi yake nayo inapata fedha ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati wananchi wapate huduma ya maji.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Sambamba na Bima kwa Walemavu umezuka ugonjwa kwa wanawake wanaojifungua watoto ambao wana mgongo wazi, hasa kule Mkoa wa Mbeya kwenye Hospitali ya Rufaa pale wanachaji fedha kuanzia 500,000 mpaka 1,000,000. Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia kuwapunguzia mzigo wa kulipa gharama hizo wanawake wanaojifungua watoto wa mgongo wazi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa wa Waziri wa Afya alishaelekeza na ameshasema mara nyingi kwamba akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano wanatakiwa wapate huduma bure, hilo ni la kwanza. Lakini ninyi ni mashahidi Waheshimiwa Wabunge jinsi ambavyo Serikali imeendelea kuboresha infrastructure kwa miaka sasa mingi sasa hivi tunaenda ndani ya miezi miwili hakutakuwepo na hospitali ya Mkoa haina na CT scan na vile vifaa ambavyo vitatusaidia kufanya operation zile ambazo zinahitaji utaalam wa juu kama hizo. Kwa hiyo kikubwa ni kwamba tutaboresha hiyo, ili iwe inaenda sambamba na suala la watoto njiti. Kwa hiyo watoto njiti na hao wanaozaliwa na malformation mbalimbali imewekwa utaratibu na ma-specialist wanapelekwa kwenye maeneo kwa ajili ya kuhakikisha hilo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge mkikutana na matatizo specific kwa sababu binaadam ndiyo wale wale mnatuambia mimi na Waziri na hata information kutoka popote zinafanyiwa kazi kwa wakati wake. Ahsante. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kuna mradi wa Kiwira ambao naweza kusema ni mradi mama kwa sababu utawatua ndoo kichwani wanawake wengi wa Mkoa wa Mbeya. Mkandarasi alishasaini mkataba, lakini mpaka sasa hivi hajaanza kazi ya ujenzi wa mradi huo. Sasa je, ni lini mkandarasi huyo ataanza kazi rasmi ya ujenzi huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Tunaishukuru sana Serikali kwamba ilitoa ahadi ya kuleta fedha zaidi ya Shilingi bilioni nane kwenye mradi wa Kyela Kasumulu, mradi huo ambao utawasaidia wananchi wa Kata ya Nkuyu, Ndandalo, Mbugani, Kajunjumele, Bondeni, Serengeti, Kyela Mjini, Ikolosheni, Itungi na Ipyana: Je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili mradi huo uanze kujengwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Suma Fyandomo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mradi wa Kiwira, tayari umeanza kushughulikiwa. Kuhusu mkandarasi kutoonekana site, lakini kuna kazi za awali tayari zimeshaanza na suala la kupeleka hela kwenye mradi wa Kyela Kasumulu, huu mradi tumeshaupelekea hela mara nyingi na tutaendelea kuupelekea kadiri tunavyopata fedha.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mbeya ni jiji lakini hatuna stendi kubwa ya kutosha, stendi ile ni ndogo lakini hata taa haina. Je, ni lini Serikali itajenga stendi kubwa ya kutosha kwenye Mkoa wetu wa Mbeya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu tulichukue kama Serikali na tutashirikiana na wenzetu wa TAMISEMI ambao hasa kwa kweli ndio wanaohusika na kujenga stendi hizi kwenye miji na majiji na kama TANROADS tutahitaji kusaidia, basi tutafanya hivyo ili Mkoa wa Mbeya hasa Jiji la Mbeya liweze kupata stendi kama alivyoomba Mheshimiwa Mbunge, ahsante.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tukuyu Mjini kuna barabara ya lami inayojengwa kule njia ya kwenda Masoko, tunashukuru. Barabara ile mkandarasi ameweka kifusi kikubwa maeneo ya Ranbos kuelekea Mpindo; sasa, je, ni lini mkandarasi yule atasawazisha kifusi hicho ili wananchi wa Mpindo wapite vizuri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, haya ni maelekezo tu kumuelekeza; namuelekeza Meneja wa Mkoa wa Mbeya wa TANROADS kuhakikisha kwamba anamsimamia mkandarasi huyo kuondoa kifusi na kukisawazisha haraka inavyowezekana. Ahsante.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Halmashauri ya Busekelo wananchi wamejenga maboma kwa ajili ya vituo vya afya, maboma manne. Ikiwa ni Kata ya Lufilyo, Kisegese, Mpombo na Kambasegela. Je, ni lini Serikali itaunga juhudi za wananchi hao kukamilisha maboma hayo ya vituo vya afya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Suma Fyandomo, Mbunge wa viti maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze wananchi wa Jimbo la Busekelo kwa kutoa nguvu zao kuanzisha ujenzi wa maboma ya vituo vya afya, lakini niwahakikishie tu kwamba, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha vituo vya afya kwenye kata za kimkakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda kufanya tathimini kuona kati ya hayo maboma lipi ni lakimkakati ili Serikali itafute fedha kwa ajili ya kuwaunga mkono kukamilisha maboma hayo, ahsante. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa mpango wa malezi na makuzi kwa mtoto ulishazinduliwa: Je, ni lini utekelezaji huu utaanza? Ahsante (Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Suma, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu wa malezi na makuzi ya awali ya mtoto tulishauzindua tangu mwaka 2021, unakwenda mpaka 2026. Mojawapo ya afua zilizopo mle ni hizi za kujenga vituo hivi vya malezi na makuzi. Tayari vituo 200 vimeshajengwa kwenye maeneo mbalimbali ya jamii na sasa tunatafuta rasilimali na kuhamasisha jamii na wadau tuendelee kujenga kwenye maeneo ambayo yana hali mbaya zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mpango huu unatekelezwa na tayari kuna watoto wapo humo wanapata hizi huduma na jamii imethibitisha kwamba kweli sasa hivi wazazi wanapata amani ya kwenda kutafuta maendeleo huku watoto wao wakiwa salama. Tutaongeza kasi hii na tutaleta taarifa kupitia Kamati zetu tunavyoendelea. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mbeya ni Jiji, lakini hauna stendi yenye hadhi ya jiji. Sasa je, ni lini Serikali itajenga stendi Mkoa wa Mbeya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mkoa wa Mbeya ni Jiji na jiji lile kwa bahati nzuri Mbunge wake ni Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson ambaye ni Spika wa Mbunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali inatambua na imeweka kipaumbele kuhakikisha kwamba tunajenga stendi ya kisasa inayoendana na Jiji la Mbeya, ahsante. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mji mdogo wa Mbalizi una kilomita 33 za vumbi. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hizo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Suma Fyandomo juu ya barabara hizi za Mbalizi zenye urefu wa kilomita 33. Tutatuma timu ya kuweza kufanya tathmini kutoka Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini (TATURA) ili kuona ni kiasi gani kinahitajika ili kujenga barabara hizi kwa kiwango cha lami. Baada ya kufanya tathmini hiyo tutaona ni kwa namna gani Serikali inaweza ikatafuta fedha kadri ya upatikanaji wake kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hizi.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, Wilayani Rungwe, Kata ya Kiwira ina Mahakama ya Mwanzo. Mahakama hiyo ni ya muda mrefu sana haijafanyiwa ukarabati, ukizingatia Mahakama hiyo inategemewa na Kata ya Ndanto, Isongole, Kinyala, Swaya, Kyimo na Kiwira yenyewe.

Je, ni lini Serikali itakwenda kufanya ukarabati wa Mahakama hiyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Suma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, awali nilisema kwamba tuna mpango wa kukarabati majengo ya Mahakama kote nchini. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwamba ameridhia wenzetu wa World Bank wametupa zaidi ya dola milioni 90, zaidi ya bilioni 200 kuhakikisha tunaboresha miundombinu ya Mahakama kote nchini. Nikuhaidi Mheshimiwa Mbunge baada ya tafiti yetu kufanyika kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama akishirikiana na Watendaji wa Mikoa kuona maeneo ambapo pamechakaa zaidi tutakuja na mpango huu ili tuingize na hayo maeneo ambayo yamechakaa tuyaboreshe, ahsante. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Mbalizi – Shigamba, ile barabara ni muhimu sana, ambayo inaunganisha na Mkoa wa Songwe;

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hiyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; hili swali linajirudiarudia lakini halijapata majibu sahihi ya Serikali; barabara ya kutoka Katumba – Suma – Mwakaleli – Luangwa – Mbambo na Tukuyu Mjini, hii ni ahadi ya tangu awamu ya nne;

Je, ni lini Serikali itaanza kuijenga barabara hiyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Mbalizi – Shigamba tayari tulishapata maelekezo na tunaifanyia kazi. Hivi sasa tunakamilisha usanifu wa kina na mhandisi mshauri yupo kazini. Akishakamilisha barabara hii ambayo ni ya Mbalizi – Shigamba na inaunganisha Itumba na Malawi, sasa Serikali itaanza kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, na barabara ya pili aliyoitaja, kimsingi tumeshaitengea fedha kwa kipande kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa na mii swali la nyongeza. Je, Serikali imefikia wapi kwenye ujenzi wa Skimu za Umwagiliaji Wilayani Mbarali? Ahsante.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumekuwa na miradi ya umwagiliaji katika Wilaya ya Mbarali na ninavyozungumza hivi sasa Wakandarasi wapo site katika mradi wa Msesule, Isenyela, Matebete, Hemanichosi na Gwanakubagogolo kote huko tayari wakandarasi wako site na kazi inaendea. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba kazi inaendelea na wananchi watanufaika na kilimo cha umwagiliaji.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha ambazo zilikwenda kukamilisha ujenzi ule na usimamizi wa Engineer Masige pamoja na Mkuu wa Mkoa barabara ile hatimaye ikakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru pia kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; je, Serikali ni lini itaanza ujenzi wa barabara kutoka Katumba – Kapugi - Ushirika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kutoka Kiwira – Isangati kutokea Mbalizi ambao huo ni mpango ulio kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nikianza na barabara ya kwanza bahati nzuri hizi barabara zote nazifahamu mimi binafsi, lakini Barabara ya kwanza ya Katumba – Kapugi hadi Ushirika hii barabara bado ilikuwa haijafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na Meneja wa Mkoa hii ni pamoja na Kiwira na Isangati ameshaanza kuzitembelea hizo barabara ili aweze kubaini gharama za kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara yote ya Katumba – Kapugi - Ushirika lakini pia Ushirika – Isangati - Mbalizi.

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo sasa ndiyo Serikali itaanza kufikiria kuijenga kwa kiwango cha lami baada ya kukamilisha usanifu wa kina, ahsante. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kule kwetu Mkoani Mbeya askari wanafanya kazi nzuri sana ya kulinda rai ana mali zao, lakini askari hawa nyumba zao ni chakavu kweli kweli ukizingatia ni Wilaya zote hakuna nyumba za askari ambazo zinaridhisha.

Sasa je, ni lini Serikali itafanya mpango wa kufanya ukarabati kwenye nyumba hizo za askari wetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Mbeya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nitambue kwamba, maeneo mengi ya vituo vya polisi, makazi ya askari katika maeneo hayo ni chakavu sana na ni kwa msingi huo ndio maana tumeanza ukarabati katika maeneo hayo. Na kwa kweli Mbeya kama Mkoa mkubwa ukanda wa Nyanda za Juu Kusini, kipaumbele kimewekwa kule katika mwaka ujao tutatia kipaumbele ukarabati wa nyumba za askari katika Jiji la Mbeya. Nashukuru sana.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ninaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba ni sikivu sana, kwa sababu niliuliza hili swali la imelitekeleza. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuyaelimisha Mabaraza ya Kata ili yasitoe hukumu kwenye mashauri ya ardhi?
Swali langu la pili, katika Wilaya ya Chunya hakuna kabisa Baraza la Ardhi, ukizingatia wananchi wa Chunya wanatoka Kambikatoto, Kipambawe, Mafieko, Bintimanyanga, Matwiga, Luhanga, Ifumbo na Shoga wanakwenda kushtaki mashauri yao kwenye Jiji la Mbeya.

Je, ni lini Serikali itawaepushia shida hiyo wananchi wa Wilaya ya Chunya?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, Mabaraza ya Ardhi ya Kata yameanzishwa chini ya Sheria Sura ya 206 na kupitia Bunge lako Tukufu kwenye Marekebisho ya Sheria Namba 3 ya Mwaka 2021 Mabaraza haya yalipunguziwa nguvu ya kimaamuzi na yanapaswa kufanya usuluhishi ndani ya siku 30 baada ya shauri kufikishwa.

Mheshimiwa Spika, tuliongea na Waandishi wa Habari lakini naomba kutumia Bunge lako Tukufu kuwatangazia wananchi wote kwamba Mabaraza ya Ardhi ya Kata nguvu yake ya kisheria ni kufanya usuluhishi ndani ya siku 30 tokea shauri lifikishwe mbele yake. Baada ya hapo kama usuluhishi utashindwa kufanyika mashauri yawasilishwe kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya. Ninaomba tena kupitia Bunge lako, Wakurugenzi wa Halmashauri maana Mabaraza ya Ardhi ya Kata yanasimamiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wakurugenzi wa Halmashauri wanasimamia kwa niaba yake, Waendelee kusimamia mabaraza haya ili wananchi waendelee kupata haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kweli kati ya Mabaraza ya Wilaya zote 139 ni Mabaraza 94 tu ndiyo yenye Wenyeviti wa Baraza la Wilaya. Tayari ofisi yangu imeendelea kufanya mawasiliano ya kuomba vibali vya ajiri kwa ajili ya kupata ajira ya kuajiri Wenyeviti wengine 45, lakini kwenye maeneo yote ikiwemo Wilaya ya Chunya kwenye maeneo aliyotaja Mheshimiwa Mbunge ikiwemo Maeneo ya Bintimanyanga na maeneo ya Shoga tunaendelea kutoa maelezo kwa Msajaili wa Baraza la Ardhi la Wilaya kutumia Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya ya jirani kwenda kwenye mabaraza haya kwenda kusikilza mashauri mpaka pale Serikali itakapokamilisha Wenyeviti kwenye Mabaraza ya Wilaya zote, ninakushukuru. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Busokelo ukizingatia mpaka sasa ni miaka 10 imepita? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya utawala katika halmashauri zetu. Nawapongeza Halmashauri ya Busokelo kwa kupokea fedha za Serikali Kuu, lakini jengo halijakamilika kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema. Naomba nilichukue hilo nilifanyie kazi tuweze kuona kiasi gani cha fedha hakijapelekwa kwa ajili ya ukamilishaji na tuweze kuweka mpango kazi kuhakikisha kwamba sasa fedha hiyo inapatikana lakini jengo hilo linakamilishwa kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa Busokelo, ahsante.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Eneo la Ikuti Wilayani Rungwe kijiografia lipo mbali sana na Makao Makuu ya Wilaya ya Rungwe.

Sasa je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi maeneo ya Ikuti, ili kuwaepushia shida wanayoipata kwa sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, eneo la Ikuti ambalo ametuambia Mheshimiwa Mbunge lipo mbali sana na eneo Makao Makuu ya Wilaya ya Rungwe, anapendekeza tujenge jengo la Polisi pale na ndiyo dhamira ya Serikali. Kama utakuwa umefatilia hotuba ya Waziri wa Fedha mwaka huu, tumesema tunataka kujenga vituo vya Polisi karibu kila Kata. Tayari Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imezungumza na TAMISEMI kuhusu mikakati ya kujenga vituo hivyo imeanza kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, ni matarajio yetu kwamba, eneo hili la Ikuti - Rungwe ni moja ya maeneo yatakayonufaika na mpango huu, ahsante. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Wilayani Rungwe kuna tatizo kubwa la maji hasa Kata ya Bulyaga, Makandana, Bagamoyo, Kawatere, Msasani na Ibigi. Sasa je, ni lini ujenzi wa tenki ambalo linatakiwa kuhudumu Kata hizo utakamilika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Suma Ikenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Suma Fyandomo kwa kufuatilia Mradi wa Maji Tukuyu lakini ushirikiano mkubwa sana wa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo, Mheshimiwa Mwantona amefuatilia pia kwa karibu Mradi wa Maji Tukuyu Mjini na hili tenki ujenzi unaendelea na fedha milioni mia tano tunarajia kupeleka tena mgao wa mwezi huu. Kwa hiyo, nikutoe hofu Mheshimiwa Mbunge na mradi huu unakwenda kukamilika na wananchi wa Tukuyu wanaenda kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)