Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joseph Zacharius Kamonga (36 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, lakini pia nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa neema na rehema zote, niwashukuru pia wananchi wa Jimbo la Ludewa na chama changu Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nimshukuru pia Mheshimiwa Rais na Serikali yake yote kwa kazi nzuri ambazo zimekuwa zikifanyika na sisi kule Ludewa tumekuwa tukiziona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Ludewa kwa kuniamini na kunituma nije niseme hapa Bungeni kwa niaba yao na vilevile sisi Wanaludewa tumezisoma vizuri hotuba zote za Mheshimiwa Rais na tukajitahidi kuzitafsiri ziendane na mazingira yetu ya Jimbo la Ludewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza na eneo la uwekezaji kwenye miradi mikubwa ambayo inaweza ikaongeza mapato ya Taifa letu. Mwaka 1996 Baraza la Mawaziri kupitia Waraka wa Baraza la Mawaziri Na. 06/96 wa mwaka 1996 waliridhia miradi ya Mchuchuma na Liganga iweze kuanzishwa na viwanda vikubwa vijengwe kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2011, NDC kwa maelekezo ya Serikali na Baraza la Mawaziri waliunda Kampuni ya ubia Tanzania-China International Mineral Resources Limited. Kampuni hii ilikwenda Ludewa na kufanya uthamini kwa nia ya kuwekeza kwenye huu mradi wa Mchuchuma na Liganga, baada ya kufanya upembuzi yakinifu na kujiridhisha eneo lile lina mali za kutosha.

Upande wa Liganga kuna chuma ambapo kampuni hii ingeweza kuzalisha zaidi ya tani milioni 2.9 kwa mwaka na kwa makaa ya mawe wangeweza kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka na ajira za moja kwa moja milioni sita na laki nne na ajira zisizo za moja kwa moja milioni 33. Lakini cha kushangaza ni kwamba mradi huu umekwama.

Mheshimiwa Spika, Wabunge watangulizi wangu wamejitahidi kupambana miradi ianze, lakini hatujaweza kufanikiwa. Wananchi wa Ludewa wana imani na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na wanamwalika sana aweze kwenda kutembelea miradi hii mapema iwezekanavyo kwani Wabunge wengi hapa wamekuwa wakilalamika fedha TARURA. Mimi nikuhakikishie Serikali ikiamua kuwekeza kwenye miradi ile tutapata fedha nyingi ambayo itatatua changamoto ya fedha na changamoto ya ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile upo mradi wa Chuo cha VETA ambao ulianzishwa pale Shaurimoyo ambao nao umekwama kwa muda mrefu sana. Tulikwenda kufanya ziara Desemba na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na ninamshukuru Rais kwa kutuletea Mkuu wa Mkoa mahiri, Engioneer Marwa Rubirya, tulikwenda naye, watu wa VETA waliahidi Januari wangeweza kuanza kujenga chuo kile, lakini cha kushangaza bado hakijafanikiwa. Kwa hiyo, tunaomba chuo kile kijengwe ili miradi hii inavyoanza na sisi wananchi wa Ludewa na Wananjombe tuweze kupata ajira kwenye miradi ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye Sekta ya Maji; namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji, nilipata nafasi nikateta naye, akanihakikishia kwamba mambo yatakwenda vizuri. Pale Ludewa kuna mradi ulitengewa shilingi bilioni saba, lakini kwa miaka mitatu zimeletwa milioni 180 tu, kwa hiyo pana mkwamo mkubwa. Tarafa ya Masasi ina changamoto kubwa ya maji, pale Lupingu walitengeneza mradi wa maji ila umesombwa na maji kwa hiyo kuna changamoto.

Na vilevile pale Kiogo kuna wanafunzi huwa wanakwenda kuchota maji kwenye Mto Ruhuhu kwa hiyo wanaliwa sana na mamba. Manda Sekondari kuna changamoto kubwa ya maji na wataalam wamejitahidi kufanya upembuzi yakinifu Kata ya Mawengi na maeneo mengine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kamonga.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, ahsante. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa maoni yangu kwenye Mpango huu wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa wasilisho zuri la Mpango na hasa vipaumbele sita vya Taifa letu kwa ajili ya kuleta maendeleo. Wananchi wa Ludewa wanaipongeza sana Serikali ingawa wana mashaka bado sababu wakati wa awamu ya nne hii miradi ya Mchuchuma na Liganga walishaandaa hadi eneo kwa ajili ya uzinduzi. Mheshimiwa aliyekuwa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alishaandaliwa kwa ajili ya kwenda kuzindua Miradi ya Mchuchuma na Liganga lakini bahati mbaya mpaka sasa muda mrefu umepita.

Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya kuwa Serikali imeingiza miradi hiyo kwenye kipaumbele na imeweka mpango, lakini bado wananchi wana mashaka na hilo. Mimi kama kiongozi wao nimeendelea kuwapa moyo na kuwaaminisha kwamba Serikali ya sasa ni Serikali ya vitendo, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri tuwe pamoja kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo wananchi ambao wameathirika na Mradi wa Mchuchuma na Liganga nao wamesubiria fidia kwa muda mrefu sana takribani bilioni 11 ni pesa chache sana kwa Serikali iwapo dhamira ya kuwafuta machozi wananchi hawa ili waweze kuondoka kwenye maeneo haya wakafanye shughuli zao katika maeneo mengine. Toka miaka ya sabini wamezuiwa kabisa kuendeleza maeneo haya na fidia hawalipwi, kwa hiyo wananchi wanaona kama Serikali imekuwa katili kwao, hawa ni wananchi wa Nkomang’ombe na wananchi wa Mundindi na Amani ambao wanalinda mali hizi kwa muda mrefu sana. Kwa hiyo naomba hili la fidia litekelezwe, kwa sababu tunavyozidi kuchelewa thamani ya ardhi inazidi kupanda, tutaingia mgogoro mkubwa sana na wananchi iwapo hatutachukua hatua mapema. Kwa hiyo, hil ni muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa kuwa Wilaya hii ina miradi mikubwa miundombinu yake bado ni changamoto kubwa. Barabara inayoanzia Itoni kwa Mheshimiwa Deo Mwanyika, Lusitu mpaka Ludewa na kwenda Manda takribani kilometa 211.44. Tunashukuru Serikali imetutengenezea lami kwa kiwango cha zege, lazima tuwe waungwana tukubali na tushukuru, kilometa hamsini ambapo thelathini zimekwisha kukamilika. Kwa hiyo tunaomba barabara hii ikamilike yote kwa sababu Serikali hii imetuletea meli kule Ziwa Nyasa ambazo zinatoa mchango mkubwa sana kuinua uchumi wa mwambao, lakini bahati mbaya meli zile zinakosa mzigo wa kutosha kwa sababu barabara hizi hazijaunganishwa. Kwa hiyo uchumi huu na miundombinu yake lazima viwe na mawasiliano kwa sababu sekta moja ya uchumi inaweza kutoa mchango kwenye sekta nyingine. Sambamba na hilo wananchi wa mwambao wanaomba kuwe na kituo cha meli kwenye Kata ya Makonde ili iweze kusaidia hali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Wabunge wengi hapa wamechangia kwamba wananchi wengi Watanzania ni maskini sana na wanaishi vijijini zaidi ya asilimia 75. Kwa hiyo tukijitahidi kutafuta masoko ya mazao kwa maeneo ya vijijini, tunavyosema uchumi jumuishi, uchumi shirikishi tutawagusa wananchi ambao wanaajiriwa kwenye sekta ya kilimo. Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wanatoka maeneo vijijini kama mimi ambako kuna wakulima wengi, wamezungumzia mazao yanakosa masoko. Kwa mfano wilaya yangu wanaongoza kwa kulima mahindi, nitatoa takwimu chache, kwa mwaka 2019/2020 tani zilizozalishwa zilikuwa 110,800 lakini ambazo kwa makisio zinatosha kwa matumizi ya chakula ni tani 46,852, tani za ziada ni 63,239 na ambazo mnunuzi mkuu wa mahindi kwa kule ni hawa wanaitwa NFRA.

Mheshimiwa Naibu Spika, NFRA walikwenda wakanunua tani 709 tu. Kwa hiyo unakuta tani zaidi ya 62,000, mahindi ya wananchi yalioza kwa kukosa soko, kwa hiyo ni muhimu Serikali ikaona haja sasa ya kutafuta wawekezaji waweze kufungua viwanda kwa ajili ya kuzalisha vyakula vya mifugo, viwanda kwa ajili ya kusaga nafaka na kwenda kuuza katika maeneo mbalimbali ili kuweza kuongeza soko kwa wakulima.

Mhehimiwa Naibu Spika, wananchi wengi wa Jimbo la Ludewa na maeneo mengine wanalalamikia sana changamoto ya vijana kuhitimu vyuo vikuu na kukosa ajira. Kwa hiyo, tunavyozungumzia katika Ilani ya Uchaguzi kuzalisha ajira 8,000,000 wanaona kama ni chache sana, kwa hiyo wanaamini sekta mbalimbali hizi kama zitaanzishwa za viwanda na mikopo ya vijana kama ambavyo Mheshimiwa Nyamoga amezungumzia, tunaweza tukafungua soko la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kwenye utumishi wa umma kuna pengo kubwa sana katika ile Seniority, kwa hiyo unakuta wako Principal Officer lakini wale Juniors hakuna, kwa hiyo kuna kupindi fulani tutazalisha tatizo kwenye utumishi wa umma na tutalazimika wakati mwingine kutengua baadhi ya kanuni za utumishi wa umma na sheria. Kwa mfano inakwambia ili mtu awe Mkuu wa Idara lazima awe amefanya kazi miaka saba, sasa itafika kipindi tutawakosa hawa watu, kwa hiyo lazima tuangalie na athari ambazo zinaweza kutoka hapo mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili watumishi wa umma muda mrefu kidogo hawajapandishiwa mishahara yao. Bahati nzuri aliyekuwa Rais wetu Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli apumzike kwa amani huko aliko, wakati akiomba kura aliahidi kwamba awamu hii anakwenda kutatua tatizo la ajira. Kwa hiyo ili kumuenzi, tumsaidie mama yetu mama Samia Suluhu Hassan kuweza kuajiri vijana ambao wengi hawana kazi. Hapa kwa kwakweli tutakuwa tumeongeza tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile na hii hoja ya kupandisha mishahara, nayo Mheshimiwa Rais wetu alikuwa ameshaahidi kwamba safari hii atapandisha mishahara na hili ni kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma, Sheria ya mwaka 2002 inasema mtumishi wa umma atapanda daraja kila baada ya miaka minne wengine, wengine miaka mitatu, kwa hiyo kupuuza sheria wakati ipo wakati mwingine sio hekima sana, ni heri kuifuta. Kwa hiyo tuangalie hiyo, tuweze kuangalia watumishi wa umma kama ambavyo alama za Chama Cha Mapinduzi ni jembe na nyundo; jembe ni wakulima na nyundo ni wafanyakazi. Kwa hiyo tuwaenzi kwa sababu hata kwenye alama ya Chama cha Mapinduzi watumishi wa umma wamo na hawa wafanyakazi wamo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hata wafanyabiashara kero zao bahati nzuri mama ameanza kuzishughulikia…

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, sijui ni kengele ya pili, au ya kwanza?

NAIBU SPIKA: Ya kwanza, malizia mchango wako.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi nimshukuru Mheshimiwa Waziri William Lukuvi na Mama Mabula, walezi wangu hawa, wamenilea vizuri na nawaheshimu sana, walitoa ufafanuzi kwa swali alilouliza jirani yangu Mbunge wa Nyasa, Mheshimiwa Stella Manyanya kuhusiana na ile capital gain tax.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri na wewe ni Mwalimu wangu pale Law School, sheria inayoanzisha kodi hii ni Sheria ya Kodi ya mwaka 2004, Sura 332 na kuna sheria nyingine ambazo zinasimamia ambayo ni Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Usajili wa Ardhi, Sura ya 334, rejeo la mwaka 2002.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ambazo zipo kwenye kodi hizi ni kwamba ili mwananchi aweze kuhamisha umiliki wa ardhi yake ambayo amenunua au amepewa kama zawadi, anakwenda Ofisi zaidi ya moja, Ofisi za Ardhi zinahusika katika kufanya uthamini, TRA wanakwenda kukadiria kodi. Kwa hiyo ile ya mwananchi nenda hapa, nenda hapa imekuwa kama usumbufu, kwa hiyo kama wangeachiwa Wizara ya Ardhi kwa sababu Serikali ni moja, hii kodi wangeweza kuisimamia vizuri, nina imani sana na Mheshimiwa Lukuvi na Mama Mabula.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Kamishna wa TRA amepewa mamlaka makubwa sana kwenye hii kodi, kwa hiyo hii nayo inachanganya sana wananchi. Pia ina mlolongo mrefu na kupoteza muda wa mlipakodi, ile nenda sijui kafanye valuation, kwa hiyo wananchi wengi wanabaki na nyaraka wanajenga bila kubadilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo hayajapimwa vile vile kodi hii haitozwi, kwa hiyo kuna maeneo mengine katika miji mikubwa ambayo hayajapimwa transaction kubwa zinafanyika, lakini watu hawalipi kodi. Kwa hiyo kuna maeneo ya kuangalia na hata asilimia yenyewe kumi ni asilimia kubwa sana. Mtu ameuza nyumba milioni 100, asilimia kubwa, akiambia asilimia 10 anaondoka anaenda nyumbani na nyaraka. Kwa hiyo hapa tunaweza tukaangalia kuna mambo ambayo yanaweza yakarekebishwa ikiwa ni pamoja na elimu kwa mlipa kodi na vilevile kuboresha namna ya ukusanyaji. Mwananchi asisumbuliwe kuambiwa nenda hapa, nenda hapa, nenda pale, kuwe na mtu mmoja anasimamia kama ni wa Wizara ya Ardhi, afanye uthamini yeye kwa sababu ana watalaam, akusanye yeye kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono pia Waheshimiwa Wabunge waliozungumzia ile kodi ya majengo (Proper tax) ile wangerejeshewa halmashauri ili kuweza kuongeza mapato. Kwa sababu wana wataalam wa GIS wanaweza wakaweka vizuri mifumo ya ukusanyaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho zuri na mpango mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo wananchi wa Jimbo la Ludewa wamenituma niombe mambo machache yaweze kufanyiwa kazi kwenye sekta ya barabara za vijijini na sekta ya afya. Kwa kuanzia na barabara za vijijini, mara zote tafiti zimekuwa zikituonyesha kwamba wananchi wengi wa Tanzania wanaishi maeneo ya vijijini na tatizo kubwa ni umaskini ambao unawasumbua. Kwa hiyo, ningependa kumwomba Waziri wa mwenye dhamana Ofisi ya Rais, TAMISEMI aweze kuwaongezea fedha watu wa TARURA ili zile barabara za vijijini ziweze kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina changamoto kubwa sana kule Jimboni kwangu Ludewa, kuna barabara inaanzia Lusitu inakwenda Madilu, Ilininda mpaka Mundindi; msimu huu wananchi wanatumia gharama kubwa sana kuweza kukodi bodaboda, barabara hazipitiki kabisa. Barabara hii hasa inayoanzia Madilu mpaka Ilininda halijapata matengenezo kwa miaka zaidi ya nane. Wananchi wa Ludewa wamekuwa wakijitolea sana kuchimba hizi barabara kwa majembe ya mkono, lakini wanakatishwa tamaa baada ya kuona Serikali haiwaungi mkono kwa kutenga fedha na kufanya ukarabati wa mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika, kuna eneo la Kigasi – Milo - Ludende mpaka Amani; barabara hii nayo ni muhimu sana, wananchi wa maeneo hayo ni wakulima, wana mazao mengi yanapaswa kupita kwenye barabara hii, lakini ina changamoto kubwa sana msimu wa mvua haiwezi kabisa kupitika. Mwaka huu nimelazimika mara kadhaa kwenda kushirikiana na wananchi kwa ajili ya kwenda kufanya matengenezo. Kwa hiyo, wananchi wanajihisi kama Serikali imewaacha, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri, naomba eneo hili liweze kuangaliwa na barabara hii ipewe fedha na kuweza kutengenezwa kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna ile Kijiji cha Masimavalafu, kuna Mto Ruhuhu ambapo panahitajika kivuko, ambako inakuwa ni rahisi sana wananchi kwenda Hospitali ya Peramiho kuweza kupata matibabu. Kwa hiyo katika eneo hili tungeomba hata kama kuna kivuko kimeachwa sehemu, tupewe sisi kitusaidie pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia na sekta ya afya; naomba sana hawa wananchi tunaowahamasisha waweze kuwa na hizi bima za afya, wanavyokwenda hospitali waweze kupata dawa na matibabu stahili yanayohitajika. Maana imekuwa ni changamoto kubwa sana, wataalam wanajitahidi kuwahamasisha wananchi wanakuwa na bima za afya lakini hawapati huduma kwa kiwango kile ambacho kinakubalika. Kwa hiyo, naamini sana Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake wote wawili wanaweza wakasimamia eneo hili tukaboresha ili wananchi waweze kuona kwamba Serikali inawathamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, napenda kushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara nyeti ambayo inawagusa wananchi moja kwa moja. Nianze kwa kumpongeza sana Waziri, Mheshimiwa William Lukuvi, kimsingi huyu ni mlezi wangu, kwa sababu miaka 10 ambayo nimefanya kazi kwenye sekta hii, amenitumia vizuri sana na nimejifunza mambo mengi sana. Kwa hiyo, namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile namshukuru Mheshimiwa Angeline Mabula, naye amekuwa kama mzazi na mlezi wa karibu, kwa kweli niwapongeze, mnafanya kazi nzuri sana. Nampongeza Katibu Mkuu, Mary Gasper Makondo, bosi wangu wa zamani, naye anafanya kazi nzuri sana. Naweza kusema ni Katibu Mkuu wa kwanza ambaye ame-practice kwenye sekta hii kwa muda mrefu. Kwa hiyo, anaisimamia vizuri na anaifahamu sana. Kamishna Mathew na Makamishna wenzangu wote, maana mimi niliachia hicho cheo cha Ukamishna Mkoa wa Dodoma. Kwa hiyo, nawashukuru sana, tupo pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi, naomba Serikali iangalie Wizara hii kwa jicho la karibu sana, kwa sababu ardhi ni rasilimali namba moja. Mheshimiwa Waziri wa Fedha anajua, ni mchumi mzuri kwamba number one resource ni ardhi. Migogoro mingi siyo wakati wote inatokana labda na matatizo yaliyomo kwa wataalam, wakati mwingine ni kutokana na ardhi yenyewe kuwa ni kitu cha thamani. Kitu cha thamani lazima kigombaniwe. Changamoto za wataalam zipo, lakini na ardhi yenyewe nayo ni tatizo kwa sababu ni kitu cha thamani, kwa hiyo, inahitaji umakini zaidi na bajeti ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukiangalia wakati huu; nampongeza Mheshimiwa Waziri na Serikali wameanzisha Ofisi za Mikoa, maana yake huduma zimesogea jirani na wananchi. Kwa hiyo, wananchi wanapata hati kwa gharama nafuu zaidi na gharama ya muda, gharama ya fedha tumeweza kumwondolea mwananchi wa hali ya chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naipongeza sana Serikali, lakini niombe sasa Serikali iweze kuongeza fedha kwenye hii Wizara kwasababu nayo itakuwa na fursa yakukusanya zaidi iwapo itapewa vitendea kazi. Nitatoa mfano mmoja, pale Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa, nina maana ya Ofisi ya Ardhi Mkoa, ina vitengo vinne ambavyo vinafanya kazi tofauti kabisa. Kuna watu wa Mipango Miji, kuna Kamishna wa Ardhi, kuna Wathamini na kuna wale Wapima. Sasa kila mmoja unakuta anahitaji aweze kusafiri kwenda kusimamia kazi, kuna miji mipya huko inakua, inatakiwa itangazwe kwenye magazeti ya Serikali ili ipangwe, lakini wanashindwa kutokana na vitendea kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Wizara hii iweze kuongezewa fedha ili ofisi zile za mikoa ziweze kuboreshwa na kuwa na vitendea kazi vya kutosha; kama vyombo vya usafiri na vifaa vya kupimia ardhi, maana sasa hivi teknolojia imekuwa kubwa. Vile vile wakiongezewa fedha za kutosha wataweza kuboresha hii mifumo ya ardhi; Kuna mfumo unaitwa ILMIS, kuna mfumo unaitwa Land Rent Management System na mifumo mingine ambayo inahitaji uwekezaji mkubwa wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo hii itawezesha Wizara kupunguza muda ambao mwananchi anapata huduma, kwa sababu kila kitu kikiwa kwenye computer ni mouse click mwananchi anahudumiwa. Kwa sababu kitu ambacho kinawakwaza sana wananchi kwenye hii sekta ni upotevu wa muda, kwa sababu sekta hii ina mambo mengi. Kuna mtu anaandaa michoro ya mipangomiji, kuna mtu mwingine anaenda kupima na kuweka beacon, kuna mtu anafanya uthamini kwa ajili ya fidia na mtu mwingine anamilikisha. Kwa hiyo, kuna milolongo mingi ambapo hakuna mlolongo ambao unaweza ukauacha kisheria na kila kitu kipo kwa nia njema. Kwa hiyo, wakiongezewa fedha, waweze kuboresha mifumo hii ya umilikishaji ardhi na utunzaji wa kumbukumbu tutaongeza sana tija kwenye sekta hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Wizara hii ina upungufu sana wa watumishi, kwa hiyo, naomba Serikali iweze kuangalia namna ya kutoa kibali ili watumishi waweze kuajiriwa. Kwa mfano, mahitaji ya watumishi kwenye sekta hii; nilikuwa nasoma hotuba ya bajeti, inaonekana ni 4,847 lakini watumishi waliopo ni 2,378. Upufungu ni watumishi 3,114, lakini wenzetu wa Utumishi wa Umma wametoa kibali cha kuajiri watumishi 36 tu. Kwa kweli hapa tutaendelea kulaumu Wizara hii kwa sababu hatuwawezeshi kuajiri watumishi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri tuna vyuo vikuu; tuna chuo kinafundisha pale Morogoro, ni chuo kizuri, kinatoa wataalam wa ngazi ya Cheti na Diploma ya Upimaji, kuna chuo Tabora nacho kinatoa mpaka ngazi ya Diploma, kuna Chuo Kikuu cha Ardhi, kuna Chuo Kikuu cha Dodoma, kuna Chuo cha Mipango na vyuo vingine, vinatoa wahitimu hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakumbuka pale Jiji la Dodoma tulikuwa na watoto wanakuja ku-volunteer wakati mwingine wanafika mpaka 50, 60 na wengine tumewafundisha kazi, ni wazuri. Kwa hiyo, kuendelea kuwatumia wakiwa wanajitolea ni risk sana kwa Serikali. Kwa hiyo, napenda kutoa ushauri kwa Serikali, iweze kuwaajiri hawa na wengine ambao wapo mtaani ili waweze kusaidia kuongeza kasi ya upangaji ardhi, upimaji na utoaji hati za umiliki wa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile napenda kuzungumzia kipengele cha upimaji, upimaji shirikishi na urasimishaji. Wabunge wengi wameonekana hawajaridhika sana na kipengele cha urasimishaji. Hii kurasimisha maana yake ni kufanya makazi ambayo hayakuwa rasmi yawe rasmi. Sasa mazoezi haya huwa yanakuwa na migogoro na malalamiko mengi sana kwa sababu wananchi tayari wameshaendeleza maeneo yao, namna ya kuwapanga kwa kweli ni lazima itokee migogoro mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ile ya upimaji shirikishi ni njia ambayo inasaidia sana kuepusha matatizo ambayo yanatokana na uhitaji mkubwa wa fedha kwa ajili ya fidia. Kwa hiyo, kama fedha hamna, maana yake wataalam watakubaliana na wananchi, wanawapimia viwanja, halafu wanagawana viwanja. Viwanja vingine vinakuwa vya wenye ardhi na vingine vinakuwa vya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kinachotakiwa tu, wale wananchi kwa sababu tunawapa viwanja vingi, tuweke tu utaratibu wa kuwasaidia kuuza ili wapate kipato ambacho kinaendana na bei ya soko. Vinginevyo wananchi hawa watakuwa na viwanja vingi na hawana cha kufanyia. Kwa hiyo, tungeweka utaratibu mzuri wa kuwasaidia kuuza ili wapate fedha halali ya haki ambayo inaendana na bei ya soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naipongeza Wizara kwa kuanzisha huu mfuko wa kukopesha fedha kwenye Halmashauri. Sasa Wizara iende mbali zaidi, iangalie pia na haya makampuni binafsi ambayo yanatambulika na Bodi za Mipango Miji na Upimaji. Kama nao wanaweza kuwakopesha hata kwa interest kidogo ili wabadilishe mfumo wa utendaji wao wa kazi, kwa sababu inaonekana hawana mitaji na ni Watanzania, wamesajiliwa na vyombo vinavyokubalika, kwa hiyo, wakipewa mikopo hii hata kwa riba kidogo, tutakuwa tunatengeneza ajira ndani ya nchi yetu na vile vile tunaongeza kasi ya upimaji na sasa hivi upimaji wao kwa kiasi kikubwa unategemea fedha za wananchi. Ndiyo maana utakuta takwimu zinaonesha makampuni binafsi yanawadai wananchi zaidi ya shilingi bilioni 70. Sasa kwenda kupima kutegemea hela ya wananchi ni changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naomba kule kwangu Ludewa, nami nina miji midogo mitano ambayo imetangazwa tokea mwaka 2001 ila bado haijapimwa; na wananchi wa Ludewa wanaamini kwamba Mbunge wao ni mtaalam mbobevu kwenye Sekta ya Ardhi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri na wataalam wako mniondoe aibu hapa ili tuweze kuwapimia wananchi. Kuna Kijiji cha Lugarawa, Mawengi, kuna Manda pale, kuna Beach Plots, kuna Kijiji cha Amani ambako miradi ya Mchuchuma na Liganga inakwenda, kuna Kijiji cha Mavanga na Mawengi. Kwa hiyo, maeneo haya bila kusahau Kata ya Mlangali pale, ni maeneo ambayo yameshaiva kimji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Nashukuru sana Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu aliwapokea Madiwani wangu, walikwenda pale Wizarani wakapata mafunzo. Kwa hiyo, wana ari ya kupokea hii huduma ya mipango miji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mipango hii ya maendeleo ambayo ni muhimu sana kwa Taifa letu. Niwashukuru pia wale wote ambao wameweza kutambua juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kueleza kwamba asilimia 75 mpaka 80 ya Watanzania wanaishi kijijini na ni maskini. Tushukuru Serikali kwa kutuingiza kwenye uchumi wa kati ila pia tuiombe iongeze fursa, kazi ya Serikali ni kuandaa mazingira mazuri ya biashara ili watu waweze kupata kipato na pato la Taifa liweze kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pia nimshukuru dada yangu, Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana, amezungumzia changamoto ya bei ya mbolea. Ni kweli; kwa mfano kule kwetu Ludewa mfuko mmoja wastani unauzwa kati ya 56,000 mpaka 65,000 na kwa ekari moja mkulima anatumia mifuko siyo chini ya minne ambapo mavuno yake anapata sanasana roba kumi. Sasa akija kuuza hizi roba kumi, roba moja shilingi 40,000, kwa hiyo anapata mapato ya shilingi 400,000 wakati amewekeza gharama zaidi ya shilingi 400,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuangalie namna sasa, nashukuru Mheshimiwa Waziri wa Kilimo amekaa na wataalam wa kilimo na kuweka mikakati. Hii ni ishara njema na nimwombe yale ambayo ameahidi aweze kuyatekeleza kwa sababu Wabunge wengi humu tunatokea maeneo ambapo wananchi wetu ni wakulima na wanategemea hasa jembe la mkono. Kwa hiyo naamini atawatoa jembe la mkono wakulima wale ambao asilimia kubwa wako vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na vituo vya utafiti, lakini vituo hivi vijengewe uwezo zaidi ili viweze kutoa taarifa nzuri na taarifa hizi zisibaki kwenye makabrasha, wawashirikishe wataalam wa kilimo kwenye halmashauri zetu, zinaweza kusaidia katika kuongeza tija. Vile vile kwenye ile mikoa yetu ambayo inajishughulisha na kilimo kungekuwa na vituo ambavyo vinafanya uchunguzi wa udongo, zile maabara. Kwa sababu mwananchi anaweza akawa anatumia mbolea ambayo saa nyingine haihitajiki kwenye udongo wa eneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyokuwa kwenye Mkutano wa RCC Njombe, watu wa madini waliwasilisha taarifa kwamba Wilaya ya Ludewa ina leseni 104 za madini ambazo hazitumiki zimekuwa zikihuishwa tu. Kwa hiyo waliomba kwamba kwa kuwa eneo hili linaweza kutoa ajira nyingi kwa Watanzania na Wanamkoa wa Njombe na kanda nzima ile ya nyanda za juu; leseni hizi ziweze kufutwa, maeneo haya yagawiwe kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuongeza kipato chao na kipato cha Taifa kiongezeke. Namshukuru Mheshimiwa Waziri, aliahidi kwamba atalishughulikia na atafanya ziara Ludewa; nimshukuru sana. Wananchi wa Ludewa wanamsubiri kwa hamu kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile wanaomba kwenye eneo la makaa ya mawe pale kuna leseni kubwa mbili ambazo zote zimeshikiliwa na Serikali. Sasa si halmashauri mapato pale ni hafifu sana, milioni 800 na sisi tulitamani Mheshimiwa Waziri wa Madini angetumegea kidogo halmashauri pale tuweze kuwekeza kwenye uchimbaji ili pato letu la halmashauri liinuke, tuweze kuhudumia wananchi. Tukihudumia vizuri wananchi maana yake watakuwa na kipato kizuri watafungua biashara na Serikali itapata mapato kupitia kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa Sheria ya Kodi ya Mapato, TRA. Kuna kodi moja inaitwa Capital Gain Tax; mwananchi anavyonunua au kuuza ardhi hii kodi inatozwa kwa mujibu wa Sheria ya Mapato ya Mwaka 2004. Kodi hii siyo rafiki, wananchi wengi ambao wananunua ardhi wanashindwa kuhamisha umiliki wa viwanja vyao. Kwa hiyo naomba iangaliwe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze wewe binafsi Mheshimiwa Waziri, Naibu wako pamoja na wasaidizi wenu wote kwa namna mnavyoisimamia vizuri Wizara hii nyeti iliyotoa ajira kwa Watanzania walio wengi (75%) na kuchangia 24% ya pato la Taifa. Kutokana na umuhimu huo, na mimi naomba kuchangia yafuatayo:-

Kwanza, Serikali iingie ubia na wawekezaji wa ndani na nje ili kuweza kujenga viwanda vikubwa vya mbolea hapa nchini ili isaidie kupunguza gharama kwa wakulima wetu. Mfano toka Ludewa DAP inauzwa shilingi 80,000 kwa mfuko 24/05/2021, CAN mfuko mmoja unauzwa shilingi 58,000 na UREA ni shilingi 55,000.

Pili, kodi za matumizi ya maji kwa watumiaji wa maji ziangaliwe vizuri ili kodi hizo zisiwe mzigo kwa wakulima na hivyo kudidimiza sekta ya kilimo. Wizara ya Kilimo ikutane na Wizara ya Maji na Mamlaka za Mabonde ili kujadili hilo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo; mazao yote ni mazao ya biashara hivyo mtizamo wa kuwa kuna mazao ya chakula na mazao ya biashara unatuchelewesha kuboresha kilimo cha mahindi, alizeti, karanga na ufuta kufanyika kibiashara na kumnufaisha mkulima. Mazao yote haya ni malighafi kwenye viwanda.

Mheshimiwa Spika, Wizara za Serikali zijenge utamaduni wa kukutana na kujadili masuala mtambuka, mfano barabara za vijijini zikiwa bora na zipitike msimu wote hakika zitachangia sana kuinua sekta ya kilimo na viwanda vya uongezaji thamani ya mazao. Wakulima walioko maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao wanakabiliwa na changamoto kubwa za ubovu wa barabara Ludewa. Mfano barabara ya Lusitu-Madilu-Ilininda-Mundindi kuna viazi, chai, kahawa, mahindi, maharage, njegere, mbao na parachichi. Pia barabara ya Kigasi-Milo-Ludende-Amani au Muhoro-Ludende-Mkongobaki-Lugarawa; barabara ya Ludewa- Ibumi-Masimavalafu au Nkomang’ombe-Iwela-Bandari ya Manda na Luilo-Lifua-Liugai na maeneo mengineo.

Mheshimiwa Spika, vyuo vikuu vya kilimo vishiriki kwa vitendo katika kufanya utafiti, ubunifu na kuelimisha wakulima ili kuongeza tija vyuo viendeshe mashamba ya mfano hasa mazao yatakayouzwa nje na kuingiza mapato ya kigeni.

Mheshimiwa Spika, vijana wanaomaliza mafunzo ya JKT wapewe mikopo chini ya uangalizi na waanzishe mashamba ya miwa, alizeti ili kuzalisha sukari na mafuta ya alizeti na karanga.

Mheshimiwa Spika, wahitimu mbalimbali wa vyuo vikuu nao wawezeshwe mitaji ili kujiajiri kwenye kilimo cha kibiashara na kukuza uchumi wa nchi na kujiongezea kipato chao.

Mheshimiwa Spika, Serikali iajiri wataalam wengi wa kilimo na kuwasambaza kwenye kata na vijiji vyetu nao wapewe malengo, wafuatiliwe ili watende kazi kama sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu. Nianze kwa kumpongeza sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan hasa kwa kauli yake aliyoitoa akiwa Mwanza kuhusu madini ya Mchuchuma na Liganga. Jana nilikwenda Ludewa Jimboni na kauli ile ilivyotoka nimepokea meseji nyingi sana kutoka kwa wananchi wa Ludewa kwamba sasa Mama yetu kweli ameikumbuka Ludewa kwa kuanzisha miradi hii na wanaomba sana viwanda vijengwe eneo lile lile la Ludewa, ili kuweza kufanya kitu ambacho wachumi wanaita diversification of economy na hizo decentration of industries.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii itasaidia sana kupunguza wale vijana wa Mkoa wa Njombe ambao wanahama sana kwenda maeneo ya mbali kutafuta ajira. Kwa hiyo kukiwa na viwanda kule tutapunguza msongamano wa watu kwenye Jiji la Dar es Salaam, Dodoma na Miji mingine mikubwa kama Mwanza na maeneo mengine. Vijana wengine wabaki kule ili na mimi niwe Mbunge ambaye nina nguvu kazi ya kutosha, sio vijana wakishakua wanakwenda kutafuta ajira maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile wameomba sana katika miradi hiyo kuwe na maandalizi ya wale wananchi waweze kupewa elimu waone namna ya kunufaika na hizo fursa; kwa sababu miradi hii inakwenda kunufaisha kwa kiasi kikubwa Taifa letu kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengine wameeleza. Vile vile tukiwaandaa wananchi na ile local content na ile community base inayozunguka mradi ikaweza kupata manufaa na wakati na Taifa nalo linapata manufaa kutokana na miradi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo wananchi wa Ludewa licha ya kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, wameomba vilevile wasaidizi wake waiangalie Ludewa kwa macho ya karibu. Kwa sababu imeonekana kuna miradi yake mingi ambayo inakwama; kuna daraja la Ruhuhu limekwama kwa takriban miaka sita. Jana nilikwenda kule Mwenyekiti wa Kijiji alinipeleka pale, wamelima sana mpunga bonde la Ruhuhu, soko lipo Ruvuma kwa sababu Kyela ni mbali, lakini wale wachuuzi wanashindwa kwenda kwa sababu kuna kivuko pale toka mwezi Septemba, 2020 hakifanyi kazi na daraja hilo ndio toka mwaka 2016 limekwama. Kwa hiyo haya yanaweza kusaidia kuleta tafsiri nzuri ya uchumi jumuishi, uchumi shindani iwapo na wananchi wote wanaweza kupata manufaa. Kwa hiyo naomba hilo liweze kuangaliwa kwa karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulisema hapa pia mradi mwingine ambao umekwama kwa muda mrefu ule wa VETA. Miaka karibu 10, ulichimbwa msingi, wamezungusha mabati, kwa hiyo wananchi wa Ludewa wanajiona wao ni losers wakati wote. Kwa hiyo hili la Mama kuweza kutaja jana kwamba Serikali sasa imepania kuanza kushughulikia Mradi wa Mchuchuma na Liganga limeleta faraja kubwa sana kwa wananchi wa Ludewa na wamekuwa na Imani kubwa sana na Serikali hii na kimsingi mimi sina sababu za kutounga mkono bajeti hii. Kwa hiyo naunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono kwa sababu nimeangalia vile vile kuna maeneo kama ya sekta ya afya, kuna changamoto ile ya watu kwenda kupata dawa. Mtu anakuwa na bima ya afya, anakwenda hospitali lakini walikuwa wanachelewa kupata dawa. Kwa hiyo sasa naona kwa bajeti hii inakwenda kumwangalia mwananchi wa chini ili aweze kupata matibabu ambayo ni ya uhakika. Ila tu niiombe Wizara ya Afya waangalie pia baadhi ya sheria ambazo wamezitoa kwenye Vituo vya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sheria inazuia Kituo cha Afya kumwandikia mgonjwa baadhi ya dawa. Sasa sisi ambao tupo maeneo ya pembezoni, kuna mwananchi anatakiwa kutembea kilometa 140 kutoka Mavanga mpaka Ludewa kwenda kufuata matibabu. Kwa hiyo kama kuna Kituo cha Afya pale Jirani, Daktari aliyopo Kituo cha Afya sasa hivi tunashukuru Serikali imetuletea qualified Doctors, kwa hiyo wangeruhusiwa, lazima tuangalie intension of ile legislation, ile dhamira ya kuweka ile sheria ya kuzuia. Miaka hiyo kulikuwa hakuna wataalam kwenye Vituo vya Afya, sasa hivi tunao. Kwa hiyo miongozo ya aina hiyo kwa kweli tuweze kui-review na kuweza kuruhusu Vituo vya Afya kuandika dawa kwa sababu kuna wataalam wa kutosha. (Makofi)

Mheshiwa Naibu Spika, nipongeze pia agizo moja liliwahi kutolewa na Mheshimiwa Ardhi, Mheshimiwa William Lukuvi kwamba kwenye maeno ya hii miradi mikubwa ya mikakati kama kwenye SGR kufanyiwe mipango ya matumizi bora ya ardhi ili sasa mindset zetu ziweze kubadilika. Zibadilike kwa sababu watu wengi wanavyoona kwamba reli imetoka bandarini na kwenda maeneo mbalimbali, wanadhani iko maalum kwa ajili ya kusafirisha mizigo inayotoka viwandani peke yake au inayotoka nje ya nchi, kumbe maeneo yale ya ardhi ya pembezoni kufanyiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi kama ilivyoelekezwa katika Sheria ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi Na. 6 ya mwaka 2007, wananchi wanaweza kutenga maeneo kwa ajili ya kilimo, mifugo na vile vile kuzalisha mazao yakasafiri kupitia reli hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii itasaidia sana kuinua kipato cha wananchi na wanaoishi kandokando ya Reli. Wataweza kuzalisha mazao ya kutosha, kunaweza kukawa hakuna mwingiliano wa matumizi ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, matokeo yake hii reli itapata mzigo wa kutosha, kwa sababu kilimo nacho kinatoa mazao kwa ajili ya viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuangalia lile eneo la malipo ya mbele wakati mwananchi anamiliki ardhi premium. Eneo hili lilikuwa linawasababisha wananchi wengi sana wanashindwa kuchukua hati miliki za ardhi kwa kushindwa gharama. Kwa hiyo kitendo cha kupunguza ada hii ni ukombozi mkubwa sana kwa wananchi hasa wa hali ya chini. Kwangu kule Lugarawa wananchi wale wameanza kufanya mambo ya urasimishaji na Mlangali na maeneo mengine. Naamini nao watamudu kupata hati miliki bila kikwazo. Kwa kweli hii nipende kuipongeza sana Serikali na tuangalie pia maeneo mengine ambayo Waheshimiwa Wabunge wameendelea kuyalalamikia na kushauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi baadhi ya Wabunge wamezungumzia kwenye ile kodi ya Majengo. Ni vema sana tukaziangalia halmashauri zetu ambazo vyanzo vingi vya mapato vilichukuliwa. Kwa hiyo tujitahidi sana kuwaajiri wale vijana waliosoma GIS ile Geographical Information System. Wale wanaweza kukusanya taarifa za majengo yote wakayaweka kwenye mifumo ya kompyuta, ukiwa pale ofisini unaweza ukaona kila jengo na kuweza kujua kirahisi uweze kutoza kodi kiasi gani. Vijana hawa wanasoma katika Vyuo vya Ardhi, kuna Chuo cha Ardhi Tabora na Chuo cha Ardhi Morogoro na vyuo vingine ambavyo vinatoa mafunzo kama hayo wanaweza kusaidia sana kuboresha ukusanyaji wa kodi ya majengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile nilichokuwa namwomba Mheshimiwa Waziri waangalie hiyo asilimia 15 kupeleka kwenye halmashauri ni changamoto haitoshi, wangefikiria kuongeza ongeza kidogo, kwa sababu Wakurugenzi wengi ukiwaangalia ukiwakuta kama hana ugonjwa wa moyo, basi ana presha au ana kisukari au tatizo lingine. Inakuwa hivyo kwa sababu wana matatizo mengi sana lakini hawana fedha. Kwa hiyo eneo hili tungeliangalia, hata halmashauri zingeachiwa asilimia 50, ingesaidia hata kujenga madarasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetembelea baadhi ya madarasa kwenye jimbo langu, yana hali duni sana. Unakuta darasa ni la vumbi. Nilikwenda Shule ya Msingi Liunji, nashukuru Serikali ilipeleka fedha pale, lakini ndio maana naomba sasa halmashauri zifikiriwe kuongezewa mapato. Wakurugenzi wataweza kumudu changamoto ndogo ndogo za madarasa na vituo vya afya. Nitatoa mfano kwenye jimbo langu, kuna kata saba ambazo zimejenga vituo vya afya lakini wanashindwa kumalizia. Wakurugenzi wangekuwa na fedha mambo yangekuwa mepesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nirudie kumpongeza sana na kumshukuru Rais mpendwa kwa hoja yake ya jana ya Mchuchuma na Liganga. Wananchi wa Ludewa wanampenda, wanamwombea na wanamkaribisha sana Ludewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nashukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika bajeti hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Doto Biteko, Waziri kwa wasilisho zuri. (Makofi)

Vilevile nitumie nafasi hii kutoa pole sana kwa Mwenyekiti wa CCM wa Jimbo la Ludewa kwa kuondokewa na Diwani Viti Maalum mama yetu mpendwa Grace Mapunda.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nianze kwa kusema naamini kwamba rasilimali inafaa kuitwa rasilimali pale ambapo inatumika kikamilifu ili iweze kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa letu. Kama tuna rasilimali halafu tunaziangalia tu hapo inapaswa tutafute jina lingine, sio rasilimali tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hilo, Jimboni kwangu Ludewa kuna madini mengi ambayo watu wa GST wameweza kuyabaini na hivyo watafiti mbalimbali wamekuwa wakienda kule. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba anajitahidi kufanya vizuri sana, wale watafiti wa madini wanavyokwenda kwenye vijiji wanavamia mashamba ya wananchi bila kulipa fidia na mashamba mengine yanakuwa yako kwenye miliki za vijiji kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na.5 ya mwaka 1999.

Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Ibara ya 24 inazungumzia haki ya kila mwananchi kumiliki mali na mali yake ilindwe na Serikali na pale inavyotwaliwa anapaswa kulipwa fidia. Sasa watafiti wa madini wakienda kule wanavamia mashamba ya wananchi wanaanza kuchimba bila kulipa fidia.

Mheshimiwa Spika, zile fedha wangekuwa wanalipa kama ni kwenye vijiji au wananchi zingesaidia sana hasa kupunguza michango ambayo wananchi wanatozwa kila leo kwa ajili ya madawati, madarasa na vituo vya afya. Kwa hiyo, kama vijiji vingekuwa vinalipwa ile fedha kama fidia ya ardhi yao ambayo wanaichimbachimba kufanya utafiti kwa sababu wanaochukua leseni za utafiti wengine wanachimba madini, wakilipa zile fidia zitasaidia vijiji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nipongeze Bunge lako Tukufu hasa la Awamu ya Tano ambalo liliweza kupitisha sheria nyingi za kulinda rasilimali zetu. Naomba sasa elimu itolewe kwa wananchi na wapewe maandalizi hasa maeneo ambapo miradi mikubwa inakwenda kuhusu nini sheria hizi zinazungumzia kuhusiana na masuala haya. Kwa mfano, kule jimboni kwangu tunaenda sasa kutekeleza mradi wa Mchuchuma na Liganga lakini wananchi hawajaandaliwa.

Mheshimiwa Spika, wale Waheshimiwa Madiwani pia wanaweza kupewa mafunzo kuhusiana na hii CSR, kwa sababu unakwenda kujadiliana na mtu ambaye ni tajiri, bepari, mwenye uwezo kwa hiyo nao wawe wamejengewa uwezo wazijue vizuri hizi sheria ili waweze kutetea haki zao. Kwa sababu hii CSR ukisoma Sheria ya Kodi ya mwaka 2004, kifungu cha 16 kinatumika katika kufanya assessment ya kodi zingine. Wanaotoza kodi wanaangalia mchango wake alioutoa kwenye hizo CSR kwenye jamii. Kwa hiyo, sio hisani kama ambavyo tunadhani, wale wanasheria wa Halmashauri Waheshimiwa Madiwani na wakuu wa idara wajengewe uwezo ili waweze kujiamini. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba sana tumsikilize mchangiaji hata ninyi mkisikiliza kwa masikio yenu mtaona kuna haja ya kupunguza sauti.

Endelea Mheshimiwa Kamonga.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunilinda. Naomba hizi sheria nzuri ambazo zinalinda rasilimali zetu ziweze kutolewa elimu na wananchi wajengewe uwezo ili kuandaliwa na miradi mikubwa ambayo inakwenda kwenye maeneo yao waweze kujua haki na wajibu wao na waweze kutetea haki zao. Vinginevyo wananchi wataendelea kutembea kwenye ardhi tajiri lakini wao wataendelea kuwa maskini. Kwa hiyo, hivi ni vitu vya muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nimuombe Mheshimiwa Waziri atoe tamko juu ya wachimbaji wadogo ambao waliomba vitalu vya makaa ya mawe pale Ludewa kwa sababu soko ni kubwa, rasilimali hizi zipo tumeendelea kuziangalia tu kwa miaka mingi. Ndiyo hayo sasa tunasema kama rasilimali hazitunufaishi hizo sio rasilimali tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo wako tayari na masoko wanayo, kuna wachimbaji wengine wazalendo kama Kampuni ya Maganga Matitu na kuna vikundi kule niliwatembelea wengine nimeona wanachimba copper kwa kutumia nyundo na tindo. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie namna ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kukuza mitaji yao, ikiwezekana kuwapa vifaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa inaiomba sana Serikali kuzifungua kata nne ambazo hazifikiki kabisa kwa gari. Kata hizo ni Lifuma, Makonde, Kilondo na Lumbila ambazo zipo kandokando mwa Ziwa Nyasa ambako hata meli tuliyoitegemea kwa muda mrefu haifanyi kazi. Wilaya imeanzishwa mwaka 1975 na Wabunge tisa walionitangulia wameomba sana jambo hili pasipo mafanikio. Sasa wakati umefika Serikali iwahurumie wananchi wa maeneo haya na ipeleke fedha za kutosha ili barabara za maeneo hayo ziweze kupitika kwa magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tunaomba sana TARURA makao makuu itume wahandisi wake ili kujionea changamoto hii na kushauri njia nzuri ya kuondoa kero ya kukosekana kwa barabara kwenye kata hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Njombe kupitia Wilaya ya Ludewa wanategemea sana huduma za matibabu na kuokoa maisha yao Hospitali ya Peramiho. Ili kufika hospitali hii iliyoko Mkoa wa Ruvuma, wananchi wanaiomba sana Serikali kutoa fedha za kujenga daraja kwenye Mto Ruhuhu eneo la Igugu ili kuunganisha Kata ya Ibumi iliyoko Wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe na Kata ya Itumbandiosi iliyoko Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma. Hii itaongeza sana fursa za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Madilu, Ludewa, Lupingu, Lugarawa, Luana, Ludende, Mkongobaki zimekamilisha maboma ya jengo la utawala ya vituo vya afya hadi hatua ya uezekaji na upigaji ripu kwa kutumia nguvu za wananchi hivyo wanaiomba Ofisi ya Rais - TAMISEMI kutembelea maeneo haya ili kutoa msaada wa umaliziaji na kutoa maelekezo mahususi kwa Halmashauri kuelekeza mapato yake ya ndani kwa awamu kwa ajili ya umaliziaji wa vituo hivyo vya afya ili jasho la wananchi lisipotee bure na tusiwavunje moyo wa kushiriki katika kujitafutia maendeleo yao na ya nchi yao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali kwa kumalizia ujenzi wa kituo cha polisi na nyumba za askari pale Ludewa. Naomba sasa wapewe gari ili kuwaongezea ufanisi wa kazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, Ludewa kuna tatizo kubwa linalowavunja sana moyo wananchi waliojitolea nguvu zao kujenga vituo vya afya ambavyo havijamaliziwa na Serikali. Kata ya Lumbila, Kata ya Lupingu, Kata ya Ludewa, Kata ya Lupanga, Kata ya Luana, Kata ya Ludende, Kata ya Madope, Kata ya Lugarawa, Kata ya Madilu, Kata ya Mkongobaki na Kata ya Masasi walianzisha majengo ya utawala ya vituo vya afya ila Serikali haijavimalizia. Jambo hili linaua sana moyo wa wananchi kujitolea. Naomba sana Serikali iweze kuvimalizia kwa awamu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia bajeti hii muhimu ya Viwanda na Biashara, lakini vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, bajeti yake imekaa vizuri na inaleta matumaini na pia niipongeze Kamati ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Kihenzile kwa sababu walifanya ziara jimboni kwangu kuangalia miradi mikubwa ile ya Mchuchuma na Liganga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli bajeti inaleta matumaini, tunamuomba tu Mheshimwa Waziri aendelee kuisamimia ili iweze kutekelezwa. Na bahati nzuri nimekaa naye jana kwa muda mrefu kidogo akiwa na Naibu wake na wiki iliyopita baada ya kumuomba aweze kutembelea Jimboni Ludewa aliridhia kwamba atakwenda baada ya kuwasilisha bajeti hii ili aweze kuzungumza na wananchi. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana na wananchi wa Ludewa wanakusubiri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hali kadhalika siku chache zilizopita Waheshimiwa Madiwani wa Jimbo la Ludewa walikuwepo hapa Bungeni na waliweza kukutana na Mheshimiwa Biteko, nako walileta mawazo yao mbalimbali Mheshimiwa Waziri aliweza kufafanua vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niwashukuru pia Waheshimiwa Wabunge mbalimbali ambao nao wamekuwa wakiona kwamba miradi hii ya Mchuchuma na Liganga ni muhimu sana na ni kitovu kwa uchumi wa nchi yetu. Wabunge wengi sana wamechangia juu ya miradi hii, kwa hiyo, wanaonesha kwamba wanaona umuhimu wa miradi hii. Kwa hiyo naomba sana Serikali iweze kuwa sikivu iwasikilize Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia umuhimu wa miradi hii maana na sauti za Wabunge ni sauti za wananchi moja kwa moja.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Ludewa wanapoona miradi inazinduliwa maeneo mengine wanajisikia wanyonge sana, wanasononeka, wanafadhaika, lakini kwa mpango huu wanakuwa wana imani kwamba miradi hii sasa itakwenda kutekelezwa, hasa hasa suala la fidia kwa wananchi wa Mchuchuma pale vijiji vya Nkomang’ombe, Kipangala, Iwela wanadai fidia na wamesubiria kwa muda mrefu sana. Wananchi wa Kijiji cha Amani na Mundindi wamesubiria fidia hizi tokea mwaka 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini kwa fedha hizi zilizotengwa Mheshimiwa Waziri atakwenda kuwalipa fidia wananchi wale mapema iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mzee mmoja alikuwa anaitwa Mzee Machupa, mwaka 2017 aliwahi kuwaeleza wananchi wa NDC kwamba hizi fidia Serikali inashindwa kutulipa wanataka ije ijenge makaburi yetu, tutakufa tutaziacha hizi fedha, bahati mbaya mzee yule Mwenyezi Mungu amemchukua bila kulipwa zile fedha. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba sana utekelezaji wa jambo hili na kukumbusha ile ziara ya Ludewa kwenda kuzungumza na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na vilevile tutambue kwamba katika madini haya tunazungumzia tu makaa ya mawe na chuma, kwenye chuma cha Liganga ambacho kinaonekana kwamba kuna mashapo ya chuma ambayo ni tani milioni 126, kwa eneo la kilometa 10 tu ambao walijaribu kufanya uchunguzi. Lakini kwa eneo lote linakadiriwa na tani milioni 700 mpaka milioni 1,400 za chuma ambazo ndani yake kuna madini mengine ya titanium, ya vanadium na madini haya ni muhimu sana kwa sababu mengine yanatumika kutengeneza vitu vya thamani sana, kama laptop, computers na ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna madini mengine ambayo yanathamani kubwa, kwa hiyo, hii ni utajiri mkubwa kwa nchi yetu, ni Serikali haina sababu ya kutoanza miradi hii. (Makofi)

Vilevile miradi hii naomba Serikali izidi kuwasiliana, Wizara za Serikali, kwa sababu uwekezaji huu tunavyosema kwamba ni mradi kielelezo, miundombinu nayo inapaswa iendane na miradi hii. Bahati mbaya sana nilisoma bajeti ya Wizara ya Ujenzi nikaona uwanja wa ndege wa Njombe haumo kwenye mpango, wakati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri mama Samia Suluhu Hassan alivyokwenda kwenye...

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Neema Mgaya.

T A A R I F A

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nilikuwa napenda kumpa taarifa kaka yangu Joseph Kamonga, Mbunge wa Ludewa, nilikuwa napenda kumwambia kaka yangu Joseph kwamba Serikali pia itueleze imejiandaa vipi kwenye mradi huu wa Liganga na Mchuchuma kuwatayarisha wananchi wetu wa Ludewa kuupokea mradi ule, kuwapa elimu namna gani ambayo wananchi wataweza kwenda kunufaika na fursa mbalimbali zitakazotokana na mradi huu wa Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Joseph.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hii kwa sababu ananikumbusha NDC walianzisha mradi wa kuelimisha jamii unaitwa PAKA. Mradi ule haupo tena, nina imani Mheshimiwa Waziri atatoa taarifa na atasema bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kuwapa elimu wananchi wa Jimbo la Ludewa na maeneo jirani ili waweze kujiandaa na miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo uwanja wa ndege nayo ni sehemu ya uwekezaji, bahati mbaya Wizara ya Ujenzi nimeona wameondoa wakati ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi na wananchi wa Njombe kiasili ni wafanyabiashara kwa hiyo uwanja ule ni muhimu sana na unaendana na miradi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nami niweze kuchangia taarifa hizi za Kamati juu ya ripoti ya CAG.

Mheshimiwa Spika, nimeona Wabunge wengi wamezungumza kwa uzito ambao unastahili kabisa juu ya madhaifu yaliopo kwenye ripoti hii ya ukaguzi na hasa hatua kutochukuliwa.

Mheshimiwa Spika, Ningependa nizungumzie eneo la utaratibu mrefu wa manunuzi ya umma. Nitatoa mfano mmoja; kwenye miradi ya maji au miradi ya barabara, unakuta ule mlolongo wa kufanya taratibu za manunuzi unapishana na Mwaka wa Fedha wa Serikali. Tarehe moja mwezi wa saba, mpaka tarehe 30 mwezi June mwaka unaofuatia Serikali inakuwa imepanga mipango yake, lakini unakuta sheria ya manunuzi inakwamisha baadhi ya michakato. Kwa mfano, halmashauri inaweza ikawa imepewa mradi wa maji au mradi wa barabara. Ni na mfano mmoja kule kwangu Mawengi kuna mradi wa maji ambao mikataba imesainiwa mwezi wa pili, lakini mpaka leo tunakwenda Disemba msamaha wa kodi kwenye ununuzi wa mabomba haujatoka. Kwa hiyo sasa tuangalie hizi sheria pia zisiwe zinatukwamisha katika kukamilisha miradi mbalimbali ya utendaji kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunakwenda kule tunawaeleza wananchi kwamba Serikali imeleta mradi huu hapa Mawengi lakini utaratibu wa kupata ule msamaha, kwa sababu sheria inataka miradi ya maji vile vifaa vipewe msamaha wa kodi. Tangu mwezi Februari mkataba unaingia mpaka Novemba exemption hiyo haijatoka. Kwenye miradi ya barabara pia hizo exemption zinachelewa sana. Kwa hiyo ukija kuangalia kwa mikoa yetu ile mvua zinaanza mwezi Oktoba mpaka mwezi Mei mwaka unaofuatia; kwa hiyo unakuta mkandarasi anakuwa na miezi miwili tu ya kufanya kazi. Anakuwa na mwezi Juni, Julai halafu hapo mwaka mwingine wa fedha unaanza. Kwa hiyo unakuta kuna kuwa na miradi mingi haikamiliki kutokana na sheria zetu kuwa na urasimu.

Mheshimiwa Spika, ningependa kuishauri sana Serikali, ili kupunguza baadhi ya hoja tuangalie pia sheria yetu ya manunuzi na kuweza kuifanyia marekebisho. Hii inapelekea sasa miradi mingi; nitatoa hapa mfano mwingine; katika Kamati ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa tuliona kwamba kuna halmashauri 147 hazikupeleka fedha benki. Halmashauri 83 hazikuchangia bilioni saba kwenye vikundi vya wanawake, lakini kuna halmashauri 21 ambazo miradi yake ilikuwa imetelekezwa. Ukija kufuatilia sababu za kutelekeza hii miradi na hayo mengine yote niliyoyasema, Serikali imeweza kupoteza jumla ya shilingi bilioni 74.

Mheshimiwa Spika, vitu vingine tunaweza kuwalaumu watendaji lakini hata sheria zetu nazo; naona Mwanasheria Mkuu anasikiliza vizuri, hiyo imenipa moyo kidogo; kwa hiyo tuangalie sheria zetu za manunuzi yale maeneo ambayo yana urasimu, yanatuchelewesha kukamilisha kazi kwa wakati, yanatuchonganisha Serikali na wananchi, tutuyafanyie kazi ili wananchi waweze kuwa na miradi ambayo imekamilika.

Mheshimiwa Spika, vile vile kuna changamoto moja ya kutokuwa na watumishi wa kutosha kwenye halmashauri zetu. Kwa mfano, Serikali inaweza ikawa imepeleka fedha labda bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa jengo la halmashauri au majengo ya hospitali. Anayeandika makisio ya gharama za ujenzi unaweza kukuta sometimes hana sifa. Tumeona kwenye taarifa humu, mtu ni technician anaandaa BOQ ambayo inahitaji mtu mwenye weledi mkubwa kitaaluma. Nishukuru mwaka jana, tulishauri TAMISEMI waliweza kupata wahandisi, hata mimi pale Ludewa nililetewa Mhandisi angalau mambo yanaanza kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo utakuta ile BOQ mtu anakisia materials ambayo fedha nyingi inatumika kununua materials ambayo hatimaye yatabaki na mradi haukamiliki. Pia, tuangalie hizi fedha tunazopoteza; namuona Waziri wa Utumishi ananisikiliza; ile tuanita wage bill, tuangalie hizi fedha ambazo zinapotea huku. Tukija kuzijumlisha zote, hiyo ni mshaara wa watumishi wengi sana. Tutaweza kutatua tatizo la vijana wetu ambao wanalalamika ajira kila siku. Ukiweka QS pale, suala la kuandaa BOQ mtu anakaa darasani anafundishwa na anafanya mazoezi ya kutosha, sio kila mmoja anaweza akaandaa hiyo BOQ.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utakuta Serikali inapeleka fedha nyingi kwenye halmashauri zetu, kwenye taasisi mbali mbali za umma; lakini kutokana kuwepo na baadhi ya watumishi wasio na weledi wanaopewa kazi hizo za kuandaa hayo hesabu tunapoteza fedha nyingi ambayo ingeweza kusaidia Watanzania wengi, ambapo sasa hivi kuna crisis ya ajira.

Mheshimiwa Spika, tukienda hata kwenye zile ofisi za mikoa (RS) nazo tuziangalie vizuri. Ukiona kuna mtumishi halmashauri msumbufu, mkorofi ana changamoto nyingi ndiyo sasa tuanamuhamishia tunampeleka RS. Kumbe RS ndiyo zina wajibu mzito, zina wajibu muhimu wa kusimamia halmashauri au Mkurugenzi muda wake umefika wa mwisho ametenguliwa uteuzi wake tunampeleka pale. Halafu hatuna watumishi wa kutosha kwenye hizi RS. Kwa hiyo tutawalaumu ma-RAS na Wakuu wa Mikoa, lakini hawana watumishi wa kutosha na wenye weledi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ningeiomba sana Serikali, ili kuokoa hizi fedha, kutoa thamani kwenye fedha hizi ambazo tunapeleka kwenye halmashauri na taasisi mbalimbali tungepeleka pia wataalamu wa kutosha na wenye weledi. Tunaweza tukaziongezea uwezo hizi RS ili ziweze kusimamia vizuri miradi.

Mheshimiwa Spika, vile vile Ofisi ya CAG ina jukumu la udhibiti. Kuna Waheshimiwa Wabunge wamesema hili jukumu la uthibiti bado halijaonekana sawa sawa, zaidi wanakuwa kama polisi kama TAKUKURU, ambao wakati mambo yamesharibika ndipo wanakwenda. Kumbe wana jukumu lingine la kuthibiti, kuzuia matatizo yasiweze kutokea. Tunaweza tukapunguza hoja nyingi sana eneo hili. Kwa hiyo ningeomba sana wale wataalam Ofisi ya CAG wajengewe uwezo ili wasiendelee kuwa tu kama mapolisi kwenda kukamata mwishoni watu wakishaharibu mambo.

Mheshimiwa Spika, wanaweza wakafanya ule ukaguzi wakati miradi bado inaendela kujengwa. Umepeleka fedha, msingi umejengwa waende wakague pale, watoe taarifa wataokoa fedha nyingi sana au wale wakaguzi wa ndani kule tukiwajengea uwezo mradi tusisubiri mpaka uishe mambo yaharibike zaidi, ndipo tunakwenda kukagua. Wangekuwa wanafanya ile real time audit, mradi unapokwa unaendelea mara kwa mara wanafanya ukaguzi na kutoa ripoti. Sasa mradi umekamilika mwaka huu CAG anakwenda mwakani tunapoteza sana fedha.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ni muhimu kufanya ni kuwajengea uwezo Waheshimiwa Madiwani hasa Mameya na Wenyeviti wa halmashauri, nao wana nafasi kubwa ya kuweza kuzuia na kupunguza hizi hoja za ukaguzi, hasa kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, kila mwezi taarifa ya mapato na matumizi inapelekwa kwenye Kikako cha Kamati ya Fedha, uongozi na mipango. Kwa hiyo, laiti wangekuwa wajengewa uwezo kuweza kusoma zile taarifa vizuri, kuzichambua vizuri na ukaguzi wa miradi, Kamati ya Fedha inafanya mara kwa mara; wajengewe uwezo, kama hawajengewi uwezo maana yake watakuwa wanapelekwa kwenye miradi kwenda kutembea na ku- justify perdiem. Tukiwajengea uwezo wataweze kubaini kama dosari zipo eneo na kuweza kuchukua hatua kabla hata CAG hajaweza kwenda kuona hizo changamoto.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo unakuta tunapoteza fedha nyingi sana ambazo zingeweza kwenda kwenye maeneo mengine. Pia, nimeona baadhi ya Wabunge wamechangia kuhusiana na bilioni 68 ambazo zimelipwa kama penalty. Hii ni fedha nyingi sana ambazo tungeweza kuzuia zisilipwe kama penalty na zingekwenda kutengeneza hata kilometa 100 za lami. Sisi kule Ludewa tunahangaika sana kipande kile cha kutoka Mawengi mpaka kwenda Manda, Mlima Kimelembe tumekuwa tukihangaika na bilioni 6 tu. Fedha hizi wananchi wanavyosikia itawatia uchungu sana. Naungana na Wabunge wote ambao wamesema tuchukue hatua kuzuia haya mambo kabla hayajatokea.

Mheshimiwa Spika, pia hii tabia ya kuchelewa kulipa wakandarasi tuiangalie kwa umakini sana. Jana nilikuwa naongea na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, wale wakandarasi waliopewa jukumu la kusambaza mbolea yaani wanafanya kazi wengine wanachuki kwa sababu kuna malipo ambayo nao wanadai kwa muda mrefu. Sasa, unakuta wanapaki lori kwa wananchi, anawalazimisha wananchi wote siku hiyo ndiyo waende kuchukua mbolea. Wananchi wanafika pale asubuhi na mapema, lori linafika usiku, wanakaa na njaa. Hii imetokea jana pale Lugarao.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuangalie kwa makini sana. Hawa, kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri, walitakiwa wawe na maghala wameyafungua. Kwa sababu muda wa mwananchi kupata fedha haufanani; si kwamba wananchi wote watakuwa na fedha siku mmoja au wakati mmoja. Mwananchi akishahangaika akiuza ulanzi wake na komoni akipata fedha ya mfuko mmoja aweze kuipta pale, na si kusubiri mpaka lori lije lipaki pale, wananchi wanateseka sana. Nashukuru jana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo aliweza kuchukua hatua; nampongeza sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wale wandarasi wana kinyongo kwa kuwa baadhi ya madai yao hawajaweza kulipwa.

Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nichangie Mpango wa Maendeleo ya Taifa. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na wataalam wake ambao wameshirikiana katika kuainisha vipaumbele mbalimbali. Katika kipaumbele ambacho kimenivutia zaidi ni kuona kwamba sasa Mchuchuma na Liganga inapaswa ianze kufanya kazi. Hili sio kwamba limeandikwa huku, niwe shuhuda hapa, hata kule jimboni kwangu wananchi wanaendelewa kuhakikiwa kwa ajili ya kulipwa fidia na maeneo yaliyosalia nayo yanaendelea kufanyiwa uthamini kwa ajili ya ulipaji fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumashukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha hizo bilioni 11 kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wa Nkomang’ombe, Iwela, Kipangala, Mundindi, Amani na wengine ambao walikuwa na mashamba yao kwenye ile miradi. Kwa hiyo niishukuru sana Serikali na niombe sasa baada ya uhakiki tu, wananchi wale waweze kulipwa fedha zao na miradi ianze kama ambavyo Serikali imeweka kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napiga hesabu ndogo hapa, ule Mradi uliokwama wa makaa ya mawe, sasa hivi makaa ya mawe yamepanda sana bei duniani. Tani moja inafika mpaka USD 350 kwenye Soko la Dunia, lakini kwa ndani ni USD 50. Sasa ule mradi ulikuwa una mpango wa kuzalisha tani milioni tatu za makaa ya mawe ambazo ukizidisha tu kwa hizi USD 50 unaona kwa mwaka Serikali ingekuwa inapata karibu trilioni mbili kutokana na makaa ya mawe. Hizi ni fedha nyingi sana ambazo zingetusaidia sana kuepukana na zile kodi ambazo ni kero ambazo tunazianzisha na wananchi wanatulalamikia. Nadhani wazo sasa la kuona hii miradi ianze ni la msingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile upande wa Liganga, ule mradi ulikuwa umekusudia kuzalisha tani milioni 2.9 na kwenye Soko la Dunia kile chuma ghafi kwa tani moja ni USD 81.5. Kwa hiyo ukichukua hiyo, ukizidisha mara tani milioni 2.9 utaona kuna trilioni tatu na point ambazo Serikali ingelikuwa inazipata kutokana na uzalishaji wa chuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumechelewa sana kuanza hii miradi, uchumi wetu umechelewa, lakini kwa kitendo cha kuingiza kwenye Mpango sasa, naomba Bunge hili liweze kuunga mkono Mpango huu na tuisimamie Serikali kuhakikisha kwamba miradi hii inaanza ili tuweze kuingiza mapato mengi kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hizo fedha pia kuna fursa nyingine nyingi, sasa hivi kuna changamoto kubwa sana ya ajira, sasa miradi hii ina uwezo wa kuajiri Watanzania hata milioni kumi ajira zile za moja kwa moja na bado kuna wale watakaokuwa wanapata ajira za udereva, wale watakuwa wanajiajiri kwenye kuanzisha garage, watakaoanzisha vituo vya mafuta na nyumba za kulala wageni, kwa hiyo tutatengeneza ajira nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia takwimu za sensa ya watu na makazi ambazo Mheshimiwa Rais wetu amezisoma hivi karibuni, utaona Mkoa wa Njombe una idadi ndogo ya watu. Idadi ile siyo kwamba ndiyo watu wote walioko Njombe. Hii ni ishara kwamba Njombe watu wanazaliwa na kuhamia maeneo mengine. Kwa hiyo tunavyofanya decentralizations ya hizi projects, tunavyotawanya hii miradi tunasaidia vilevile ku-control ule mtawanyiko wa watu nchini, watu wasisongamane uelekeo mmoja. Kwa hiyo hawa watu milioni kumi wakipelekwa kule kwenye hizi ajira kwa kweli tutakuwa tumeinua sana uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na miradi hii, lazima ionekane pia kwenye miundombinu ya barabara, kuna ile barabara inayoanzia Itoni – Ludewa - Manda, nashukuru sana Serikali wameidhinisha bilioni 95 upande wa Itoni mpaka Lusitu na bilioni 179 kutoka Lusitu mpaka Mawendi, lakini barabara hii haijafika Makao Makuu ya Wilaya na haijafika kwenye Mgodi wa Makaa ya Mawe ambapo ni kilometa 68 na haijafika Manda ambako kuna bandari ambayo nayo ingeweza kuunganisha usafiri wa mizigo kwa sababu tuna meli ya mizigo ambayo haina mzigo pale Ziwa Nyasa. Kwa hiyo barabara hii ikikamilika hata meli hii itaweza kufanya kazi vizuri na itapata mzigo wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara pia inayounganisha Liganga na Mchuchuma, kwenye uwekezaji huu dhamira na Mheshimiwa Rais, ionekane pia katika kuandaa mazingira ya miundombinu ya barabara na Kiwanja cha Ndege cha pale Njombe. Vilevile kutoka Mkiu – Liganga - Madaba na ile Liganga na Mchuchuma ni kilometa 70. Kuunganishwa kwa barabara hizi ni ishara tosha kwamba miradi sasa itakuwa inaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pale Mlima Kimelembe sasa hivi kuna wachimbaji wengine wadogo ambao wanashindwa kusafirisha makaa ya mawe, tulikuwa tunahangaika bilioni sita ili ule mlima uweze kukatwa, lakini kwa mapato haya kama iwapo tutakata mlima, tani milioni tatu za makaa ya mawe zitasafiri, mapato yake ni trilioni mbili kwa nini tujiulize mara tatu kutoa bilioni sita kwa ajili ya kukata mlima? Kwa nini tujiulize kupata hiyo bilioni mia moja kwa ajili ya kukamilisha barabara? Kwa hiyo hoja ya msingi hapa ni dhamira, hivyo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili sasa niende kwenye kilimo. Ninaipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwenye mipango yake kwenye sekta ya kilimo ni jambo zuri, vilevile kilimo kinakwenda sambamba na kuongeza thamani kwa mazao, viwanda mbalimbali ili kuongeza ajira kutokana na crisis ya ajira. Kwa hiyo, tuone pia namna ya kuongeza thamani ya mazao vile viwanda ili kuongeza thamani ya mazao kwa ajili ya kuongeza ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imetoa fedha nyingi kwenye sekta ya kilimo lakini bado nako kuna upungufu wa watumishi. Nitatoa mfano, kule Jimboni kwangu ninavyo Vijiji 77 lakini ninao watumishi wapatao 48 tu, kwa hiyo ilikuwa ni muhimu sana hizi fedha tunazopeleka na hii miradi ambayo imepokelewa vizuri kule na wananchi tuongeze pia wataalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaipongeza Serikali kwa kutoa ruzuku kwenye mbolea. Najua mwanzo ni mgumu na niwashukuru wataalam, Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na wataalam wake kuna mtu anaitwa Ngairo, yule bwana anapokea simu saa 24, nampongeza sana, ila sasa ule udongo kule kwetu Ludewa unahitaji mifuko mitatu ya mbolea. Hivi asubuhi nimepata taarifa, nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, kuna ghala la pale Ludewa Kijijini kuna mbolea wananchi wanagawiwa, lakini foleni ni kubwa siyo tatizo, ila ombi lao ni kwamba, ekari moja inahitaji mifuko mitatu, mfuko mmoja wa dap wanapandia na mifuko miwili ya urea kwa ajili ya kukuzia. Kwa udongo ule ukiweka mbolea mifuko miwili huwezi kupata mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu kutokana na wao kusomea field wamekuwa wataalam saa nyingine kuliko hata wataalam wa kilimo, wanaweza kukabiliana na mazingira yao. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali tuweze kuwasikiliza hawa wananchi badala ya kuwapa mifuko miwili tuweze kuwapa mifuko mitatu ya mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, tumeanza sasa na changamoto na nimekiri kwamba Wizara inajitahidi, lakini tuongeze kasi ya kuwasimamia hawa mawakala ili waweke vituo maeneo yale ambayo ni catchment areas zenye wakulima wengi waweze kupata mbolea kwa wakati bila usumbufu ili tuweze kufidia hii changamoto ya mazao ya chakula ambayo imejitokeza kutokana na bei ya mbolea kupanda sana mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivi na tukaendelea kuboresha barabara za vijijini hakika tutakuwa tumemkomboa mkulima. Kwa sababu, ataweza kutoa

mazao yake shambani kuyapeleka kwenye soko kwa ajili ya kujipatia kipato. Na hii itaendelea kuwapa hamasa wakulima kuweza kulima zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mifugo na lenyewe pia kwa kuwa Wilaya yangu kwa mfano, nitatoa mfano Jimbo langu la Ludewa tunakwenda sasa kupata miradi mikubwa kutakuwa na uhitaji mkubwa sana wa maziwa, nyama, mayai na vitu kama hivyo. Sasa niiombe Wizara ya Mifugo itusaidie kule kuna vyama vya ushirika vya wafugaji, lakini hawana madume bora kwa ajili ya kuboresha ile mbegu ya ng’ombe wa mawziwa waliyonayo. Kwa sababu Ludewa mpaka sasa kwa takwimu ambazo nilizipata inaonesha kuna ng’ombe wa nyama 33,000 kwa hiyo, hawawezi kutosheleza. Kwa hiyo, tungeweza kuanzisha ranches kule Ibumi na wataalam wa kilimo walishaomba maeneo ya mashamba zile block farming na hizi ranch kule eneo la Ibumi, Masimavalafu tunahitaji sana usaidizi wa Serikali ili kuweza kufikia malengo yetu ya kuongeza idadi ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele imegonga na mambo yangu sikumaliza. Niunge mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuonesha dhamira kubwa ya kukuza Sekta hii ya Madini hapa nchini. Vile vile namshukuru kwani alipokuja Njombe nilimwomba amtume Mheshimiwa Waziri wa Madini aje Ludewa aweze kuzungumza na Wachimbaji wadogo juu ya kuwagawia vitalu vya makaa ya mawe. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Doto Biteko na Naibu wake, kwani Naibu Waziri aliweza kufika Ludewa, nimshukuru sana. Vikao vile vimezaa matokeo mazuri. Kwa hiyo, naipongeza sana Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nashukuru sana kwa Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko kuikuza Wizari hii ya Nishati na Madini, kwa sababu namba zinamtetea. Tumeona sasa Sekta ya Madini inatoa mchango kwa asilimia 9.7 kwenye pato la Taifa. Jitihada ambazo amezifanya siyo ndogo, kwa hiyo, anastahili pongezi sana. Kwa hiyo, tunamtia moyo kwamba aendelee kuhakikisha kwamba sekta hii inaongeza zaidi pato la Taifa. Kwa sababu tukiangalia Sekta ya Kilimo ina asilimia 26, Sekta ya Utalii ina asilimia 17. Kwa hiyo, nikiangalia madini tuliyonayo, na mwendo huu ambao Mheshimiwa Dkt. Biteko anao, naamini atasogea na sekta hii itakuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye pato la Taifa, na vile vile kuzalisha ajira kwa wananchi. Ndiyo maana Wabunge wengi hapa wamechangia na kuona kwamba kuna haja sasa ya Serikali kuangalia sana wachimbaji wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na wananchi wote wa Ludewa kwa mapokezi mazuri ya Mwenge wa Uhuru. Nilikwenda huko, hamasa iliyokuwa mwaka huu siyo ya mfano. Kwa hiyo, nawapongeza sana wananchi na ninawashukuru. Naomba tunapowahamasisha awamu nyingine, wafanye kama mwaka huu. Kila mmoja aone jambo ni la kwake kama ilivyokuwa mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ziara ile ya Mwenge, tulipita Kijiji cha Mkomang’ombe, wananchi walikuwa wanalalamikia sana zile fidia zao za Mchuchuma na Liganga. Naishukuru sana Serikali, mnatambua kwamba exchequer ilishatoka ya Shilingi bilioni zote 15, lakini nilipofuatilia NDC kwa nini hawaendi kulipa fidia? Ilionekana hawajapewa fedha zile za kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nitumie fursa hii kumwomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, namwona hapo, atusaidie wananchi waweze kupewa zile fedha, kwani wamezisubiri kwa muda mrefu sana. Kimsingi wananchi wale kwa Mkomang’ombe, Iwela, Kitongoji cha Malamba, wananchi wa Idusi, wanasubiri fedha hizi kwa hamu kubwa sana. Wananchi wale wa Kijiji cha Amani, wananipigia simu kila siku. Kwa hiyo, naomba kwa sababu Mheshimiwa Rais ameshaidhinisha hizi fedha, wale NDC wapewe zile fedha za kufanyia kazi ili waende mara moja tukamalize mgogoro na wananchi wa Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naomba sana, kuna hoja hii ya wachimbaji wadogo. Nilikuwa nasoma ukurasa wa saba kwenye ule Mpango aliowasilisha Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nikaona watu wa GST wamenunuliwa vifaa, mitambo kwa ajili ya kufanyia utafiti. Pia Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti yake ule nadhani ni ukurasa wa 84 ameonesha kwamba hawa GST kwa mwaka huu wa fedha watakwenda kufanya utafiti wa madini Mkoa wa Njombe. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, naishukuru sana Serikali, kwani Wilaya ile ina madini mengi na hakuna tafiti ambazo zimefanyika ukiacha zile zilizofanywa na Wawekezaji wa Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kule Lupanga, kuna chuma unakiona kabisa na unajua ule mkondo wa madini umefika mpaka kule; maeneo ya Utilili, unakwenda mpaka Makete kule kwa Mheshimiwa Festo Sanga. Kwa hiyo, wakienda kufanya utafiti, tunaweza tukajua potential ambayo nchi hii tunayo, na tunaweza tukaweka mipango kwa ajili ya kuendeleza. Vile vile wananchi kule wanachimba dhahabu, ruby, sapphire na madini mbalimbali, hadi hizo earth minerals pale Mawengi zipo, lakini hakuna tafiti ambazo zimeweza kufanyika na kujua tuna madini kiasi gani, na je, yanafaa kwa uwekezaji wa kiwango kipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa kwenda kufanya utafiti maeneo hayo. Hii itasaidia sana kuongeza ajira kwa wananchi, kwa sababu sasa hivi tuna vijana wengi ambao wamesoma na wengine walipelekwa nje ya nchi kwenda kusomea eneo hili la mafuta na gesi, wengine madini mbalimbali lakini waliporudi nchini hawajaweza kupewa ajira. Baadhi ya wananchi wamekuwa wakitusumbua sisi Wabunge. Kwa hiyo, tunavyokuza Sekta hii ya Madini hasa wachimbaji wadogo, tunazalisha ajira nyingi zaidi, licha ya kuwa tunaongeza pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni kwamba kule Ludewa wale wanaochimba makaa ya mawe, Serikali; namwona Mheshimiwa Jafo yupo, tuangalie sasa mpango wa kusimamia mazingira. Kwa sababu makaa ya mawe wote tunatambua kwamba yana sumu. Kwa hiyo, yanaweza kuleta hatari ya maji yake kwenda kwenye mito na mfumo mzima wa maji, hata haya maji ya chini ya ardhi. Tuweze kuwalinda wananchi kwa kushirikiana na wale watu wa OSHA na watu wengine kwa sababu unaweza kupita sehemu nyingine unakuta wananchi wanachambua makaa ya mawe kwa mikono. Hii ni hatari sana. Kwa hiyo, tuweke mpango mzuri wa kusimamia mazingira, kuangalia mfumo mzima wa maji ili kuweza kuwalinda wananchi wasiweze kupata maradhi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile hata kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo; twende tukatoe elimu ili waweze kuujua vizuri huu mnyororo mzima wa thamani kwenye Sekta ya Madini. Waweze kujua, wawe na taarifa, tuanzishe information centers, waweze kupata taarifa ni namna gani wanaweza wakapata mitaji. Nina mfano mmoja wa mchimbaji yuko Kijiji cha Amani pale Ludewa, anaitwa Berege. Amehangaika, amemtafuta geologist, kamwandikia mradi mkubwa. Sasa anahangaika ili aweze kupata mtaji. Kwa hiyo, naomba Wizara hii iweze kuwaita hawa wachimbaji wadogo, iwape taarifa, wafanye nini ili waweze kupata hiyo mitaji kwa ajili ya uchimbaji? Kwa sababu wataajiri Watanzania wengine na fedha hii pia wanaiwekeza hapa hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, napenda sana kuishauri Serikali kama ambavyo Wabunge wengi wameshauri. Bajeti ambayo wanatengewa Wizara ya Madini hasa watu wa GST ni ndogo sana. Hakuna nchi ambayo imeendelea bila tafiti hapa duniani. Kwa hiyo, ilikuwa ni vyema sana, hata kama ni kurekebisha sheria, weka pale sharti kwamba haya mapato yanayotokana na Sekta hii ya Madini; tunaweza tukasema, Bunge likapitisha sheria asilimia tatu hadi tano ziende kwenye utafiti zaidi wa madini, kwa sababu hii itatusaidia kufanya Sekta hii ya Madini iweze kutimiza malengo ya kuongeza pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bila kuwepo kwa sheria ambayo itatubana, itatulazimisha kuongeza fedha kwenye eneo la utafiti wa kisayansi wa madini, nina hofu kama safari yetu inaweza ikawa na changamoto nyingi. Kwa sababu nchi hii ina mambo mengi, na fedha inahitajika maeneo mengi. Kwa hiyo, kama hamna sheria ambayo inatubana, inaibana Serikali kutenga fedha kwa ajili ya utafiti wa kisayansi, tunaweza tukakutana na changamoto kidogo. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Mheshimiwa Waziri atuletee hiyo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali waangalie eneo hilo. Kuwepo sheria kabisa ambayo inatubana. Hizi tafiti zitatusaidia sana kuweza kuongeza mapato na ajira kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia, linahusiana na eneo la madini ya dhahabu. Kule kwetu Ludewa kuna wananchi ambao wanachimba hizi alluvial gold, na vile vile zile za kwenye miamba. Hoja hii ya utafiti, ndiyo maana nairudia zaidi, ni vizuri wananchi wale wanaweza, na Mheshimiwa Waziri hata siku moja ukipata nafasi, nikakukusanyia wale wananchi, wakakutana na wewe ukawasikiliza changamoto zao, itapendeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto mojawapo nashindwa kuisema sana kwako kwa sababu inagusa pia Wizara ya Viwanda na Biashara. Wale watu wa NDC, vile vitalu walivyovigawa vya makaa ya mawe, wangeweka na mpango mahususi kwa ajili ya wale wachimbaji wadogo, kwa sababu Mheshimiwa Waziri wanakunukuu kabisa, kwamba ulikwenda kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na waliomba vitalu kwa ajili ya migodi yao ya shaba ambayo imechanganyika na dhahabu. Kwa hiyo, ukiwasikiliza, utaona namna ya kuweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema hivyo kwa sababu masharti yale yanayowekwa na NDC…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kamonga.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Kalemani na Naibu wake, Mheshimiwa Stephen Byabato. Bahati nzuri Waheshimiwa Madiwani kutoka Ludewa walikuja, Mheshimiwa Kalemani aliwapokea, alizungumza nao, alisikiliza changamoto za Ludewa, kwa hiyo, nampongeza na namshukuru sana. Halikadhalika Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Byabato, naye nampongeza anatupa heshima sana wanafunzi tuliomaliza Chuo Kikuu cha Tumaini pale Iringa. Hongera sana Mheshimiwa Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niipongeze sana Serikali kwa bajeti nzuri ya Wizara ya Nishati kwa sababu umeme siyo anasa ni maendeleo. Nadhani kila mtu anaelewa, kwa hiyo, ni vema sana kuhakikisha kwamba hii mipango ambayo inatekelezwa inapewa fedha za kutosha ili wananchi waweze kupata umeme wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika niishukuru sana Serikali tulipata mkandarasi, kule Jimboni kwangu Ludewa kuna kata zile za mwambao ambazo zina mazingira yenye changamoto sana kutokana na uwepo wa Ziwa Nyasa na milima mikali sana. Hata hivyo, nashukuru kwenye Kata za Lupingu, Lifuma na Makonde tayari mkandarasi ameshapeleka nguzo za umeme, kwa hiyo, wananchi wanamuomba tu aongeze kasi zile nguzo wameziona vya kutosha sasa wanatamani kuona umeme. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba utusaidie hapo. Halikadhalika tumempata mkandarasi mwingine kwa ajili ya kata zilizosalia; Kata za Ibumi, Lumbila na Kilondo, tunashukuru sana Serikali kwa hilo.

Mheshimiwa Spika, sambamba na pongezi naomba Mheshimiwa Waziri afahamu kwamba kuna kata tano za kule Ludewa zina changamoto sana ya umeme; Kata hizo ni Milo na Mawengi. Kata hizi mbili zina mradi ambao ulikuwa unasimamiwa na mzalishaji binafsi ambaye alikuwa chini ya Kanisa Katoliki. Tumshukuru sana Baba Askofu Alfred Maruma huko aliko apumzike kwa amani, alitusaidia sana kupata umeme kwenye Kata za Milo na Mawengi kabla maeneo mengi nchini hayajapata umeme. Kwa bahati mbaya ule umeme sasa hivi unasumbua sana. Kwa hiyo, naomba Serikali iingilie kati ili wananchi wa Kata za Milo na Mawengi waweze kupata umeme wa uhakika kwa sababu kata hizi mbili zina wakazi wasiopungua 21,000, hospitali kubwa ya Milo ambayo iko chini ya Kanisa la Anglican, shule za sekondari na zahanati ambazo zinahitaji umeme.

Mheshimiwa Spika, pia kuna umeme ule wa Lugarawa ambao unahudumia vijiji 20 kwenye Kata za Lupanga, Madilu, Lugarawa, Mlangali, Lubonde na Madope. Nako huku kuna wakazi wasiopungua 51,000 na umeme huu pia ulikuwa chini ya mzalishaji binafsi unakuwa wa mgao zaidi ya saa 12 vilevile mzalishaji anashindwa kuuza umeme kwa maelekezo ya Serikali kwa sababu gharama zake za uzalishaji ziko juu. Kwa hiyo, wananchi 51,000 katika vijiji 20 kupata umeme wa mgao wa saa zaidi ya 12 na wakati mwingine mitambo ile inazima kwa muda mrefu inakuwa siyo sawa. Mheshimiwa Waziri niombe kwanza tuwashukuru wale wazalishaji binafsi kwa sababu walitusaidia sana lakini Serikali iweze kuingilia kati kwa sababu tayari TANESCO wameshaingia mkataba mdogo kununua umeme kwa kampuni ile ya Madope basi inunue umeme wote ili shughuli ya kusambaza na changamoto nyingine ziweze kufanywa na Serikali. Wananchi hawa wa vijiji 20 ndiyo waliokichagua Chama cha Mapinduzi, kwenye kata hizi zote wamechagua madiwani wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwanye Wizara hii ya Fedha. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa bajeti nzuri na pia Naibu wake na wataalam wote.

Mheshimiwa Spika, nilikwenda pale Hazina kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa walikuwa hawakupata zile fedha, nilivyowaona tu wasaidizi wa Mheshimiwa Waziri waliweza kutoa fedha zile kwa asilimia 100. Kwa hiyo, naomba niwe muungwana, nianze kwa kuwashukuru watumishi wa Hazina na naomba sana na awamu ijayo kwa sababu Ludewa na Njombe kuna muda mrefu sana wa mvua muda wa kufanya kazi unakuwa mchache sana, huu mwezi wa tano mpaka wa kumi ndio muda wa kufanya kazi. Ndiyo maana juzi nilimuona hapa Waziri wa Ujenzi baada ya kuona zile barabara zimesimama kwa sababu kule Hazina walikuwa hawajafanya malipo kwa mkandarasi muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, naomba sasa nijikite kwenye hoja ambazo nilikuwa nimejipanga kuzisema kwenye Wizara hii. Niliwahi pia kuzungumzia ile kodi inayoitwa Capital Gain Tax, kodi ambayo inalipwa kwa mwananchi ambaye ameuza ardhi. Kodi hii Serikali inakosa mapato mengi sana kwa namna tu ambavyo sheria zimekaa na namna ambavyo inakusanywa. Kwa hiyo, nina mapendekezo machache ya kuboresha. Moja, naomba sana Wizara ya Fedha ikutane na wataalamu wa Wizara ya Ardhi watafute namna kodi hii iwe inakusanywa na ofisi moja, sanasana Wizara ya Ardhi. Kwa sababu mwananchi akishauza ardhi yake anakwenda kwa Afisa Ardhi anaambiwa aende TRA, wakati uthamini wa kodi wanafanya watu wa Ardhi, kwa hiyo, kunakuwa na mizunguko mwananchi nenda pale nenda pale. Kwa kweli tunampotezea muda sana mwananchi na ili wananchi waone raha kulipa kodi ni muhimu sana ikawa ina mazingira rafiki ya kuweza kuikusanya. Kwa hiyo, tuangalie namna mamlaka moja ikusanye kodi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nachoweza kusema ni kwamba ile asilimia 10 ya kodi hii inayokusanywa mwananchi akishafanyiwa uthamini kwa ajili ya kulipa ile kodi ya kuhamisha umiliki wa ardhi, kama umeuza kiwanja milioni 70 akiambiwa asilimia 10 milioni 7, mwananchi anachukua nyaraka zake anaondoka haji tena. Kwa hiyo, hata tukifanya sampling tukasema wananchi ambao wamenunua ardhi hawajaweza kubadilisha wafike tutagundua kwamba kodi nyingi sana hapa iko nje ambayo Serikali ingeichukua tungeweza kuipeleka kwenye miradi na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile hata namna hii ya kuwa na makisio ya kodi kwa mtu kuonana na mteja moja kwa moja tungeangalia namna ya kupunguza mifumo hii. Kwa sababu tuna wataalamu wanamaliza vyuo vikuu wanaweza kututengenezea mifumo ya computer ambayo tukitengeneza mwongozo mzuri wanaingiza tu data kwenye mifumo hii kodi inakadiriwa, lakini tukimpa mtu binafsi madaraka ya kukadiria kodi, saa nyingine mtu anaweza akakadiria kodi kubwa ili kutengeneza mazingira ya majadiliano kidogo na mwisho wake mazingira ya rushwa lakini ikiwa mtu akifanya mouse click kodi imekuja, kidogo inajenga trust kwa mwananchi. Kwa hiyo, tuondoke kwenye ule mfumo wa manual twende kwenye mifumo ya computer. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nizungumzie maeneo ambayo hayajapimwa. Ukisoma Sheria ya Usajili wa Ardhi, Sura ya 334, inasema kodi hii inapaswa itozwe kwenye ardhi iliyopimwa tu, lakini kuna maeneo mengi ambayo hayajapimwa, kuna miamala mingi na mikubwa ambako tungeweza kupata kodi nyingi sana. Kwa hiyo, tuangalie maeneo haya ikiwezekana turekebishe sheria ili ituruhusu tukishirikiana na Wenyeviti wa Mitaa, tukawapa hata posho kidogo Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, watatusaidia kupata mapato mengi sana ambayo yatalisadia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Kibaigwa na sehemu nyingine unakuta mji mkubwa watu wanauziana petrol stations, majengo na ardhi kwa fedha nyingi. Kwa hiyo, unakuta kodi hii maeneo mengine Wenyeviti wa Mtaa wanakusanya na hawatoi risiti. Kwa hiyo, nafikiri ni eneo ambalo tunatakiwa tuliangalie.

Mheshimiwa Spika, maeneo ya vijijini kuna vikundi vinaanzishwa ambavyo vinachukua hadi tenda labda ya kufyeka barabara au kujenga mifereji, vikundi vya akina mama na vijana. Sasa vikundi hivi wanavyotaka kwenda kulipwa malipo yao wanaambiwa wawe na mashine za EFD, halafu wanatambuliwa kama wakandarasi. Mimi nafikiri hili eneo tungeangalia kwa sababu wale wanajikimu tu kwa zile kazi za kufyeka na kutengeneza mitaro miwili/mitatu. Kwa hiyo, kuwaambia wale wawe na EFD machine ambayo inauzwa Sh.590,000 na kuwawekea kama ni sharti la muhimu, nafikiri tungeangalia kwa sababu wale akina mama na vijana wanajikimu tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, vilevile tuendelee kutoa elimu hasa kwa wale wajasiriamali wa vijijini kwa sababu kuna malalamiko kwamba wanakadiriwa kodi kubwa sana. Kwa hiyo, nipongeze sana juhudi za Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kuonesha kwamba eneo hilo sasa anakwenda kuliangalia kwa karibu. Vilevile Mheshimiwa Waziri nimemsikia mara kadhaa ameonesha naye ana dhamira ya kusimamia suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siku moja nilikaa na wananchi pale Jimboni kwangu Ludewa, kundi la wafanyabiashara, wakaniambia kwamba suala la ulipaji kodi kiserikali mwananchi anapaswa awe mzalendo na anatambua umuhimu wake. Hata kwenye Imani, ukisoma Marko 12:17 wale Mafarisayo walimuuliza Yesu, je, ni halali kwa wananchi hawa kwenda kupeleka mapato kwa Kaisari? Kwa hiyo, aliwajibu pale, mpeni Kaisari yaliyo yake Kaisari. Kwa hiyo, hata misingi ya kiimani inatambua umuhimu wa kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia wale maaskari waliambiwa watosheke na mishahara yao, wasichukue zaidi na wasimsingizie mtu mashtaka. Kwa hiyo, haya mazingira ya Afisa wa TRA kukadiria kodi yeye binafsi na siyo mfumo yanajenga mazingira, hasa maeneo ya vijijini kwa mwananchi kukadiriwa kodi kubwa ili kuwe na negotiation na kuwe na malipo ya pembeni. Kwa hiyo, kukiwa na mfumo kwa kweli wananchi wanapenda sana kulipa kodi kwa sababu kwa sasa hivi wanaziona kodi zao zinakoenda; wanaona miradi ya maendeleo inafanyika kwa hiyo, wanapenda kulipa kodi. Kwa hiyo, tukitengeneza mazingira rafiki wananchi watalipa kodi bila shida yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kusisitiza kwamba wale wafanyabiashara wa vijijini huwa wanaambiwa wanunue zile mashine za EFD. Sasa ile mashine Sh.590,000/= wanaambiwa watarejeshewa lakini unakuta inachukua miaka mitatu mpaka minne kumrejeshea. Mtaji wa mwananchi wa kijijini unaweza ukakuta Sh.1,000,000, sasa ukimwambia mashine Sh.590,000/= kidogo tungetafuta namna nyingine ama Serikali ingekuwa inaziagiza nje na kuhakikisha zinapatikana kwenye ofisi za TRA ili bei ipungue kuliko kuacha wananchi waendelee kununua mashine kwa gharama kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, nashukuru sana ila nimuombe tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha pale Hazina akipitapita yale malipo ya Barabara ya Lusitu – Mawengi yafanyike. Ile barabara imejengwa kwa miaka sita haiishi na chanzo kikubwa ni kucheleweshwa malipo kwa mkandarasi, hivi sasa amendoka site.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, Jimbo la Ilemela asilimia 87 ni maji, nchi kavu ni asilimia 13 tu, hivyo uchumi wa Ilemela kwa kiasi kikubwa wanategemea rasilimali za majini hususani Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, maombi; akina mama wengi wanaofanya bidhaa ya dagaa wanahitaji vifaa vya kukaushia dagaa tofauti na sasa wanakausha dagaa katika mazingira yasiyoridhisha.

Mheshimiwa Spika, vijana wanahitaji mashine za boti kwa ajili ya uvuvi katika maji yenye kina kirefu na vizimba kwa ajili ya ufugaji samaki wa vizimba.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia mpango huu. Nianze moja kwa moja kwa kuishukuru sana Serikali, kuanzia Rais wetu, Mheshimiwa Waziri Mkuu na viongozi wote kwa miradi mingi ambayo imeelekezwa kwenye Jimbo la Ludewa. Wananchi wa Ludewa walikuwa wanaliwa sana na mamba Mto Ruhuhu, hawakuwa na daraja, wamelilia kwa miaka sita, nashukuru sana, sasa daraja lile limekamilika na wananchi wanaweza kufanya shughuli zao na hawaliwi tena na mamba. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali, ni jambo ambalo limewafurahisha sana wananchi wa Ludewa na wameahidi kuiunga mkono Serikali kwa nguvu zao zote na uwezo wao wote aliowajaalia Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa daraja lile limekamilika, kwa hiyo, wanaomba pia ile meli ambayo inapita Ziwa Nyasa kuanzia Itungi kwenda Nyasa nayo iweze kuanza safari zake. Kwa sababu kwa muda wa miezi mitano sasa, toka mwezi Mei, ilikuwa matengenezo na wananchi wanatumia usafiri wa mitumbwi na maboti; hivyo, wengi wanazama kwenye maji na kupoteza mali zao. Kwa hiyo, wanaiomba sana Serikali, huu uchumi ambao tumesema umekua kwa asilimia 4.8 na robo hii 4.7 nao wanatamani kufanya shughuli ili uchumi wao uweze kukua. Kwa hiyo wanaiomba sana Serikali meli ile ianze safari zake mara moja, maana katika Ziwa Nyasa, Wilaya ya Ludewa ina kata nane; kuna kata ya Kilondo, Lumbila, Lifuma, Makonde, Lupingu, Iwela, Manda na Ruhuhu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kata zote hizi nane zinategemea sana usafiri wa maji kwa sababu maeneo haya yana changamoto sana za barabara. Kwa hiyo, jambo hili linarudisha nyuma jitihada za wananchi katika kujishughulisha na uchumi ili nao waweze kuongeza kipato chao na kulipa kodi ili uchumi wa nchi yetu uweze kukua zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, upande wa sekta ya kilimo kuna changamoto moja kwamba hizi sheria zetu nyingine zimekuwa kama zinadidimiza wananchi. Kuna Sheria ya Matumizi ya Rasilimali za Maji; Sheria Na. 11 ya Mwaka 2009. Sheria hii imeanzisha utaratibu kuwa, mtu yeyote anayetaka kutumia maji, anatakiwa apate kibali ambalo siyo tatizo; lakini sambamba na kibali hicho, kuna tozo ambazo zimeanzishwa. Sasa wananchi wa Mkoa wa Njombe na hasa Ludewa Kata ile ya Madilu na Madope wanalima sana viazi vya umwagiliaji. Sasa sheria hii inawarudisha wananchi kwenye kilimo cha kutegemea mvua, kwa sababu mwananchi ananunua ma-roll yale ya mabomba, anatafuta maji, anachimba mtaro, anaingia gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii inamwanzishia kodi ya shilingi 250,000 na gunia moja la viazi unakuta linauzwa shilingi 12,000. Kwa hiyo, ili upate hizo 250,000 unahitaji siyo chini ya gunia 23. Kwa hiyo, tozo hii naiomba sana Serikali, kwani inakuwa inawarudisha wakulima kwenye kutegemea kilimo cha mvua. Hii iko sana maeneo ambayo yana miradi ile ya umeme wa maji. Hizi jumuiya na haya mabonde yanakwenda kutoa elimu, yanaanzisha jumuiya za watumia maji. Kule kwangu wananchi wanalia sana na hii tozo ya shilingi 250,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kwenye sekta hiyo hiyo ya kilimo, Wabunge wengi wamezungumzia changamoto ya mbolea. Nitatoa mfano wa bei chache ambazo ziko kwa Njombe. Mbolea aina ya DAP ilikuwa inauzwa shilingi 55,000 mwaka 2020, lakini sasa hivi inakwenda kwa shilingi 97,000 mpaka shilingi 106,000; na hii mbolea ni muhimu sana kutokana na virutubisho ambavyo vinahitajika kwenye udongo. Kwa hiyo, kuna mbolea nyingine ambayo ni muhimu ya UREA, nayo imetoka kwenye shilingi 55,000 mpaka shilingi 80,000 au shilingi 90,000. Kwa hiyo, imepanda karibia mara mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mbolea nyingine ambayo inahitajika zaidi aina ya CAN, nayo kwa sasa inauzwa kati ya shilingi 60,000 mpaka shilingi 72,000 kwa Mkoa wa Njombe. Kwa hiyo, kwa hali hii, niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba Serikali ina kila sababu ya kutoa ruzuku kwenye mbolea ili bei iweze kushuka irejee kwenye hali yake ya mwaka 2020 au pungufu zaidi ili wakulima waweze kulima mazao yao kama kawaida, kwa sababu imekuwa ni kilio kikubwa sana. Kwa hiyo, naomba Serikali ichukulie katika uzito wa pekee ili tuweze kumnusuru huyu mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwenye sekta hii ya kilimo, naishukuru sana Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mahindi. Bahati mbaya sana mfumo uliotumika mwaka huu wa kutumia vikundi vya ushirika umewaumiza sana wale wakulima wenye gunia tano, sita saba au 15, wengi hawajauza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda Kijiji kimoja cha Mkongobaki kufanya mkutano, nikajaribu kuuliza pale wakulima mmoja mmoja ambao waliweza kuuza mahindi. Kwa kweli katika Kata ile ya Mkongobaki nilipata mwananchi mmoja tu. Kwa hiyo, zile tani nyingi hazieleweki zilikwenda wapi? Wakulima wanalia mahindi yanaoza, sasa hivi watoto wanaripoti Vyuo Vikuu, masomo ya mahindi hakuna. Kwa hiyo naomba hapa napo paangaliwe mfumo ule, ama tungeweza kuwaandaa wananchi kwa kuwapa elimu ya kutosha au tungetumia mfumo wa soko la miaka yote, tusingepitia kwenye hivi vikundi. Kwa Ludewa, wananchi; mkulima mmoja mmoja wameumia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niishukuru Serikali kwenye miradi ya umeme. Miradi ya umeme kwa kweli vijana wa kileo wanasema Serikali imeupiga mwingi sana. Kule kwangu Ludewa kuna vijiji ambavyo havina umeme kabisa ambavyo ni vitatu. Naomba Serikali iweze kuviingiza kwa wakandarasi hawa REA. Kuna Kijiji cha Ndoa, Kijiji cha Kimata na Kijiji cha Kitewele. Vijiji hivi havijaingia kwenye Mpango ili wananchi hawa nao waweze kuona wananufaika na uchumi huu ambao uko chini ya Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ambaye ameelekeza fedha nyingi kwenye Mpango huu kwa ajili ya miradi ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, kuna hii miradi ambayo ya umeme ya wazalishaji binafsi. Kuna Kampuni ya Madope, inazalisha umeme kwa ajili ya vijiji 20. Kwa hiyo, umeme huu umekuwa na changamoto ya mgao wa masaa zaidi ya 12 kwa muda wa miaka miwili sasa. Naishukuru Serikali na Waziri wa Nishati, Bodi ya REA imekwenda kule na wameona changamoto hizi.

Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba ile tathmini waliyoifanya ya kutatua hizi changamoto ziende haraka ili Kata ya Mlangali, Lubonde, Madilu, Madope, Lupanga na Lugarawa waweze kupata umeme wa uhakika na wa bei nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye kipengele cha uchumi shindani na hii miradi vielelezo, kuna huu mradi wa Mchuchuma na Liganga, nashukuru sana Mheshimiwa Rais alishatolea maelekezo kwamba miradi hii ianze, amechoka sana kuisikia; na ninafikiri ametambua kwamba miradi hii itatoa ajira nyingi sana. Ajira za moja kwa moja zaidi ya milioni nane pale zitapatikana. Wale wote watalipa kodi Serikalini, Serikali itaongeza mapato nao watapata kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hoja unayoizungumza ya mabilionea, sisi pale tuna makaa ya mawe ambapo leseni zake zote zimeshikiliwa na NDC halafu uchimbaji haufanyiki. Kwa hiyo, wangepewa wachimbaji wadogo, nina imani (namwona Mheshimiwa Biteko ananisikiliza vizuri) na sisi Ludewa tungezalisha mabilionea. Naomba wananchi wale waweze kulipwa fidia wakati Serikali inaendelea na majadiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye taarifa hizi za Kamati na niungane na Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kwa kuanza kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita iliyo chini ya Mama Samia Suluhu Hassan, maana hata kule Jimboni kwangu Ludewa kila kona ambako wananchi wapo, kuna miradi ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, naye nimkumbushe kwamba ana ahadi na wananchi wa Ludewa na wanamsubiri sana kule. Ziara yake ameshaiahirisha mara nne, kwa hiyo, wananchi wameniomba sana niweze kumkumbusha, wana hamu naye sana, wanataka aende akashuhudie kazi nzuri ambazo Rais wetu amefanya ikiwemo daraja la Ruhuhu, barabara ya zege na mambo mengine lukuki. Nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika nakupongeza kwa kuchaguliwa. Nami binafsi nikiri kwamba nakufahamu tokea Law School ukiwa mwalimu wangu Cohort ya 12. Kwa kweli Mwenyezi Mungu amekupa karama nyingi, naamini hata Bunge hili litaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache nirudi sasa kwenye hoja mahususi ambapo ningependa kuanza kuchangia kwenye Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Nimemsikiliza RC wangu wa zamani wa Mkoa wa Njombe, Mheshimiwa Ole-Sendeka, amezungumzia hoja ya Ngorongoro ambayo vilevile imekuwa ikijadiliwa sana kwenye vyombo mbalimbali vya Habari. Wako ambao wanasema kwamba wananchi waendelee kuwepo vilevile kwa sababu ni aina ya pekee ya utalii; watu, mifugo na wanyama wa asili, lakini wapo ambao wanaona kwamba ongezeko la mifugo kama ng’ombe, kondoo, mbuzi na wanadamu inaharibu ekolojia ya eneo lile na wanyama wale walikwenda pale kwa sababu za kiasili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata tukisoma maandiko matakatifu tutaona kwamba Mwenyezi Mungu baada ya kuumba mbingu, ardhi, wanyama, ndege ndiyo akamuumba mwanadamu. Kwa hiyo, tuna jukumu vile vile la kutunza hizi maliasili. Ila hoja ya mahususi na ya msingi ni kwamba tunavyoshughulikia mambo haya kama alivyoongea Mheshimiwa Ole-Sendeka, tuweze kuzingatia haki za binadamu, kwamba Serikali inavyotekeleza wajibu wake wa kulinda hifadhi ile ambayo iko kwenye urithi wa dunia, Hifadhi ya Ngorongoro, ni sharti na ni muhimu sana kuheshimu haki za binadamu. Tunapowahamisha wale watu, lazima tuangalie sheria zinasemaje kuhusu haki za binadamu? Zikoje? Vile vile kuwe na ushirikishwaji wa hali ya juu.

Nimemuona Mheshimiwa amesisitiza zaidi ushirikishwaji kwa hiyo hoja zote ni za msingi lakini ile Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ina sheria yake, Sura ya 284 na Kifungu cha 6 kama alivyokinukuu, kinaelezea majukumu ya ile mamlaka ya uhifadhi wa Ngorongoro. Kwa hiyo, mamlaka ile ilikuwa na majukumu ambayo imepewa na sheria na ilikuwa na wajibu wa kuyasimamia. Kwa hiyo, watu walikuwa wanaongezeka tunaangalia, lakini sasa tunavyotaka kuilinda ile Hifadhi tuzingatie haki za binadamu, lakini hoja ya ile hifadhi kuendelea kuwepo ni muhimu sana ikapewa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika kwenye Kamati yetu tuliona kwamba Serikali imewekeza fedha nyingi sana kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere na takribani shilingi trilioni
6.5 zimewekezwa pale na asilimia siyo chini ya 60 ya maji yanatokana na bonde la Mto Kilombero. Kwa hiyo, na kwenyewe ni muhimu sana Serikali ikachukua hatua za haraka pasipo kuathiri haki za binadamu. Wale wananchi wote ambao wanafanya shughuli zinazoathiri ustawi wa bonde hili la Mto Kilombero na kuathiri uwepo wa maji ya kutosha yatakayoenda kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, kwa kweli ni vizuri Serikali ikachukua hatua za haraka bila kuathiri haki za binadamu. Ninavyosema haki za binadamu, nafikiri ni neno ambalo ni pana kidogo.

Mheshimiwa Spika, halikadhalika tukija kwenye masuala ya utalii, huku Nyanda za Juu Kusini kuna vivutio vingi sana vya utalii, kule Jimboni kwangu Ludewa, Ziwa Nyasa kuna samaki wa mapambo, kuna milima ya Livingstone, ingawa bahati mbaya kuna Kata nne pale hazifikiki kwa gari; Kata ya Lumbila, Kata ya Kilondo, Kata ya Makonde na Kata ya Lifuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika zile safu za milima ya Livingstone kuna nyani wale wakubwa, wazuri, ni kivutio kizuri cha utalii. Pia kuna miamba ile ya Ziwa Nyasa na Kitulo kule kwa Mheshimiwa Festo Sanga, Makete. Kwa hiyo, vivutio ilikuwa ni vizuri vikatambulika na Wizara hii ya Maliasili na kuweza kukuza utalii wa Nyanda za Juu Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika kuna ngoma za asili. Mheshimiwa Naibu Waziri tulimpelekea ngoma moja ya Mganda ya Boma la Mtumbati, kulikuwa na tukio la watu wa Makete. Alivutiwa sana na ile ngoma, mavazi yao wanavaa kaptura nyeupe na shati jeupe. Ngoma ile kwa kweli ni kivutio kizuri sana na muhimu cha utalii. Pia kuna ngoma nyingine kama Ngwaya, Matuli; hata vyakula vya asili. Kwa hiyo, ni vizuri Wizara hii ikatambua vitu vile na kuviingia kwenye mradi wa regrow, itasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikirejea kwenye Wizara ya Ardhi, Wizara hii inafanya kazi kubwa sana na sasa hivi wamewekeza sana kwenye mifumo ya kielektroniki; Teknolojia Habari na Mawasiliano kuna mfumo unaitwa Landrent Management System, kuna mfumo unaitwa Molis na mifumo mingine mingi. Mifumo hii kwa kweli inasaidia sana katika kuongeza ufanisi. Isipokuwa Wizara hii inakabiliwa na upungufu mkubwa sana wa wafanyakazi. Takribani wafanyakazi 2,000 wanahitajika waongezeke. Kwa hiyo, Wizara hii iangaliwe kwa jicho la karibu ili isaidie kupunguza migogoro.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, tunaishukuru sana Serikali kwa mradi wa umwagiliaji Ruhuhu. Tunaomba utumike kutatua changamoto ya mafuriko Kata ya Ruhuhu hasa Vijiji vya Kipingu, Ilela na Ngelenge ambapo mpunga, mihogo na mahindi ya wakulima kuzama.

Mheshimiwa Spika, tunaomba Bonde la Masimavalafu lenye ekari 5,000 nalo lipate mradi wa kilimo cha umwagiliaji. Bonde hili lipo Kata ya Ibumi, Kijiji cha Masimavalafu, Wilaya ya Ludewa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, naomba tu bandari ya Manda pale Ludewa ijengwe. Aidha, barabara kuanzia Mawengi hadi Manda na Mkiu – Liganga - Madaba zijengwe kwa kiwango cha lami.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niungane na Wabunge wenzangu wote waliompongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa kipaumbele kwenye sekta hii ya ardhi. Hali kadhalika nimpongeze sana Mheshimiwa Angeline Mabula, Waziri wa Ardhi na mlezi wangu, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri na wataalamu wote wa sekta hii ya ardhi. Nitakuwa pia mchoyo wa fadhila nisipo mpongeza Mthamini Mkuu, mthamini amesimamia zoezi la uthamini wa fidia vizuri kule Ludewa; aliitwa kwenda kuhakiki akaenda na wataalamu wake, na hivi sasa ninavyozungumza wananchi wanalipwa fidia ya bilioni 15.4. Kwa hiyo niipongeze sana Wizara kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi niombe pia waweze kushirikiana na watu wa NDC na Wizara ya Viwanda na Biashara. Upimaji ule uliofanyika kule Liganga na Mchuchuma kulikuwa na haki mbili. Kulikuwa na mineral right yaani zile leseni za madini na kulikuwa na land right, hati za umiliki wa ardhi. Sasa, mwekezaji alimiliki eneo kubwa la ardhi lakini ulipaji wa fidia alipunguza eneo lake atakalofanya uwekezaji, na lile eneo jingine ambalo halijalipiwa fidia tulitaka tulipange tutoe hati kwa wananchi ili nao waweze kunufaika na mradi. Kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Waziri ili kuepusha mgongano na wananchi wataalam wawahi mapema sana, nina imani sana wanaweza wakafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua mpira mtu anaweza akaucheza vizuri akiwa nje ya uwanja, ukiwa nje unaweza kuwa na mawazo mazuri zaidi kuliko wachezaji walioko ndani; lakini na wewe ukipewa nafasi uende kucheza utaona pale unakuwa kituko. Sekta ya ardhi ni tofauti sana na tunavyo ichukulia. Sekta hii ina sheria nyingi sana, na zote za muhimu. Lakini mpaka hati ije kutengenezwa kuna hatua nyingi za kupitia na kuna wataalamu wengi wanahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashukuru nimebahatika kufanya kazi kwenye sekta hii ya ardhi kwenye Wizara ya Ardhi kwa muda usiopungua miaka kumi. Katika kipindi hicho nimesimamiwa na kufundishwa kazi na wengi na mimi nimesimamia na kufundisha kazi wengi; kwa hiyo nina ufahamu mkubwa wa sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kazi zile za kuandaa mpango kabambe (master plan) ikishaandaliwa ile waje wale watu wa mipango miji. Na master plan ile inakuwa ni shirikishi, inahusisha watu wengi zaidi. Wanakuja watu wa mipango miji, anachokifanya Afisa Mipango Miji, mpima ardhi hawezi kukifahamu na hawezi kufanya. Ni taalum mbili tofauti wote wanakaa darasani miaka miwili mitatu minne wanafundishwa, na anachokifanya Afisa Ardhi ni kazi tofauti. Ndiyo maana kuanzia ukurasa wa 30 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, nilikuwa naisoma, ameainisha pale eneo la uandaaji wa mpango kabambe (master plan), uandaaji wa mipango kina, upimaji wa ardhi, umilikishaji, na mambo ya utatuzi wa migogoro. Kwa hiyo kuna vipengele vingi ambavyo ni muhimu sana ningeomba ikiwezekana wizara iweze kutoa mafunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuna kitu pia nimekibaini, tunachanganya sana upimaji wa vijiji na upimaji wa mashamba ya wananchi na utoaji wa hati milki za kimila. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge tunachukulia kwamba upimaji wa vijiji ndio huohuo upimaji wa mashamba ya wananchi na utoaji wa hati miliki za kimila. Kwa hiyo haya maeneo ningeomba Wizara iweze kukutupa semina za kutosha ili tuweze kuwa na uelewa ili tunavyoishauri tuweze kutoa ushauri ambao uko sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano. Kwenye upimaji wa mipaka ya vijiji hili linanyika sana wakati ule inavyokuja sensa labda ya watu na makazi au uchaguzi, wanapotaka kuzaliwa vijiji vipya; au wakati wowote Ofisi ya Rais TAMISEMI wanavyo kuwa wanaongeza vijiji. Sasa, inatakiwa wananchi wakae wakubaliane mipaka ndipo wataalamu waweze kwenda kuweka mipaka hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na eneo hili ningeiomba Wizara ipunguze kutumia mipaka ile ya asili kama mito na milima, kwa sababu mazingira ya kijiografia yanabadilika. Kuna mito inakauka, kuna mito inahama. Kwa hiyo ni vizuri wakaweka zile bicorn kubwa kama ambavyo mmeweka kwenye mipaka ile ya kule kwenye hifadhi, na kule kwenye mipaka ya nchi. Zile nguzo ni kubwa zimefyatuliwa pale, mwananchi yeyote anaweza kuona, kwa sababu tukitegemea mto kuna wakati mwingine mto unahama. Kwa hiyo ni muhimu sana tukafyatua nguzo kubwa za bicorn ili wananchi wasije wakaingia kwenye migogoro. Kila mwananchi akiona anajua kwamba hapa ni mpaka wa kijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mipango ya matumizi bora ya ardhi niipongeze sana wizara imejitahidi kadri ya uwezo wake, imejitahidi sana; na Tume ya Mipango ya Matumizi Mora ya Ardhi nayo imejitahidi kufanya kazi vizuri. Niishukuru Serikali, mwaka jana wakati wa bajeti mara ya kwanza tuliweka ile bilioni 205 lakini zikaongezwa zaidi ya hizo ili angalau waweze kupima vijiji vingi zaidi. Kwa hiyo naomba sasa wataalamu wetu waweze kwenda kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji ambavyo vimepangwa kutekelezewa mradi huo, wapime mashamba ya wananchi na kutoa hati miliki ya kimila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile sijui tutatumia njia gani, bado baadhi ya maeneo hati miliki ya kimila haina uzito sana, mwananchi akienda benki kuomba mkopo wa trekta bado haitambuliki sana. Sasa sijui tutatumia njia gani kuweza kuelimisha taasisi zinazotoa mikopo kwa wananchi waweze kuitambua vyema hati ya haki miliki ya kimila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunavyopima maeneo mengi zaidi kwenye nchi yetu na kutunza kumbukumbu za wamiliki vizuri tunapunguza muda wa kutatua migogoro wa ardhi. Mwananchi akija kama kumbukumbu ziko vizuri za mwananchi ni rahisi kumpa majibu. Kwa hiyo ni muhimu sana, Waheshimiwa Wabunge wanavyoshauri maeneo mengi katika nchi hii yaweze kupimwa na kutolewa hati miliki ni ushauri ambao ni mzuri sana ambao wizara haina budi kuufuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Serikali iongeze zaidi fedha na itoe kibali kwa Wizara hii kuweza kuajiri watumishi wa kutosha, kwa sababu wizara hii ina upungufu mkubwa sana wa watumishi, haijaajiri muda mrefu. Kwa hiyo ni muhimu sana Serikali Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma wakawapa kibali waweze kuajiri; kwa sababu vyuo vipo vijana wako mtaani hawana ajira na wana uwezo na wana utayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia takwimu, inaonesha watumishi waliopo hawazidi asilimia 30, kwa hiyo upungufu ambao upo kwenye Wizara hii ni zaidi ya asilimia 70, kwa hiyo ni pengo kubwa sana, hivyo tusitarajie miujiza kwa idadi hii ya upungufu wa watumishi. Kwa hiyo naomba Serikali iweze kuajiri watumishi wa kutosha. Na kwa eneo la Dodoma nimeona Mheshimiwa Waziri amejaribu kuelezea pale kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa hapa Dodoma. Dodoma inabidi ichukuliwe kwa namna nyingine tofauto, kwa sababu moja, tangu mwaka 1973 kulikuwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu CBA. CBA walikuwa na sheria tofauti walikuwa hawatumii Sheria ya Ardhi Namba Nne. Walikuwa hawafuari sana Sera ya Taifa ya Ardhi, walikuwa na taratibu zao ziko tofauti. Kwa hiyo baada ya kuvunjwa ndipo sasa tuka-switch, na mimi ndiye niliyekuwa Afisa Ardhi wa kwanza kuja kubadilli mfumo. Changamoto kubwa niliyokuwa nakutana nayo moja ni kutofautiana kwa sheria. Kwa hiyo tuangalie namna ya kuziba gap katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile Dodoma baada ya Makao Makuu kuja ardhi ilipanda sana thamani. Mahitaji ya ardhi yakawa mengi, na upimaji wataalam wamejitahidi wana viwanja, najua saa hivi wanakwenda kwenye milioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Wizara ikaaangalia uwezekano wa kuongeza Kamishna mwingine wa ardhi hapa Dodoma. Kamishna mmoja mtamuua kabla ya siku zake, atazeeka kabla ya wakati wake. Kwa hiyo ateuliwe Kamishna mwingine wa ardhi ili aweze kusaidiana majukumu na Kamishna aliyepo namna ya kugawa majukumu Kamishna wa hapa atajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kulipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu mwaka huu limepitisha sheria ambayo imerejesha Tume ya Mipango. Halikadhalika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha sheria ile na kuitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaye Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo amekaa hapo na ametuandalia taarifa nzuri sana. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Profesa ns Waziri wa Fedha, taarifa zenu nimeanza kuzisikiliza, kwani mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, tumezichambua na ushauri wetu ni kama ambavyo umewasilishwa na Mwenyekiti wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, nianze kwa kuangalia eneo la umuhimu wa utafiti katika kuandaa mipango ya maendeleo ya nchi kwa sababu kuna mjumbe mmoja Mheshimiwa Zaytun Swai nilimsikiliza, alitoa tafsiri ya Mpango. Alisema; “kupanga ni kuchagua.” Maana yake unakuwa na vitu vingi, unachagua lipi lianze na lipi lifuatie kutegemeana na umuhimu wake na vipaumbele vyake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naona kwamba eneo la utafiti ni nyenzo muhimu sana katika kupata mipango mizuri. Sasa tukiangalia kwenye Mfuko wa Utafiti wa Maendeleo (COSTECH) naona kwa mwaka 2024/2025 kwenye hii taarifa ya Mpango inaonesha kwamba mwaka 2022/2023 fedha ambazo zilitengwa kwa ajili ya utafiti ni shilingi bilioni 4.9 ambayo ni sawa na 0.003% ya pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kinyume kabisa na lengo la nchi yetu ambapo tumejiwekea malengo ya kila mwaka kwenye pato la Taifa angalau 1% iende kwenye eneo la utafiti. Hii 1% hatujaweza kuifikia. Kwa hiyo, naishauri Serikali vipindi vinavyokuja iongeze bajeti kwenye eneo la utafiti. Katika lile pato la Taifa angalau tuweze kutimiza hii 1% ya pato la Taifa. Kwa sababu tafiti na ripoti mbalimbali zinaonesha kwamba nchi nyingi ambazo zimepata maendeleo, utafiti umesaidia sana katika kuweka mipango ambayo ni madhubuti na endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa utafiti unasaidia sana watunga sera katika kufanya maamuzi ambayo ni sahihi. Kwa mfano, tukiangalia Benki ya Dunia, taarifa yake ya mwaka 2023 inaonesha kwamba Taifa la China limefanikiwa kupata maendeleo makubwa sana kwenye nyanja za afya, elimu, teknolojia na ubunifu kutokana na kuwekeza kwa kiwango kikubwa kwenye eneo la utafiti. Halikadhalika, hata nchi kama vile Rwanda na Korea Kusini zinaonesha kwamba wameweza kuzisaidia nchi zao katika kujenga, kuimarisha na kuendeleza uwezo wake wa ndani. Kwa hiyo, naishauri Serikali yangu iweze kutimiza angalau hili lengo la 1% ya pato la Taifa kwenye eneo la utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyo vyuo mbalimbali hapa nchini; tuna Chuo Kikuu cha Sokoine SUA, vinaweza vikatumika katika kufanya tafiti kwenye maeneo mbalimbali. Kwenye eneo la kilimo nampongeza sana Waziri wa Kilimo amekuja na mikakati na mipango mizuri kwenye eneo la kukuza kilimo nchini. Ameungwa mkono na Serikali kwa kuongeza bajeti kwenye eneo la kilimo, lakini kwa kiwango gani tunavitumia vyuo vikuu vyetu kwenye eneo la utafiti ili viweze kuboresha mipango na mikakati ile? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, eneo la tafiti naona ni eneo ambalo ni nyeti sana. Litatusaidia katika kuendeleza eneo la kilimo na masoko ya bidhaa mbalimbali hapa nchini. Kwa mfano, eneo la kilimo, tuna hawa watu wa NFRA, ukiwaangalia wao jukumu lao la msingi kisheria ni kuhifandhi tu chakula ili kukitokea tatizo waweze kusaidia maeneo yale yenye upungufu wa chakula. Tuna chombo gani ambacho kinasaidia haya mazao ya chakula kutafuta masoko kwa mfano mahindi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri asubuhi amejibu vizuri swali la wakulima kucheleweshewa malipo yao ya mahindi. Alitoa ufafanuzi mzuri na nina imani kwamba Serikali itawalipa, kwa sababu sasa hivi mvua zimeshaanza, wanaanza kilimo, wanazitegemea kwa ajili ya shughuli. Kwa hiyo, tumewaambia watulie, wasubiri maelekezo aliyoyatoa asubuhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tafiti katika maeneo haya ya masoko, kuongeza thamani ya mazao na vitu vingine yatasaidia sana kupata mipango madhubuti ambayo itachangia kwa kiwango kikubwa kuleta maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niongelee eneo la ardhi, mipango miji na maendeleo ya makazi. Tukiangalia eneo hili tunaona linakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinasababisha washindwe kufikia malengo. Tukiangalia kwa mfano eneo la makusanyo ya kodi za ardhi, kuanzia Julai, 2022 mpaka Mei, 2023 malengo yalikuwa ni shilingi bilioni 250.1 lakini ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 132 ambayo ni 53.2% ya malengo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia changamoto ambazo zinaisababishia Wizara ya Ardhi ishindwe kufikia malengo: moja; uhaba mkubwa wa watumishi. Tuna vyuo vikuu vinatoa wahitimu kila mwaka, lakini ajira zake hazijatoka muda mrefu. Kwa hiyo, Wizara hii ingeweza kuongezewa wapima ardhi, maafisa mipango miji kwa sababu kuna ripoti ambayo inaonesha kwamba kasi ya ukuaji wa makazi holela ni 67%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, makazi holela yanakua kwa kasi na kasi ya upimaji wa ardhi haiendani na kasi ya ongezeko la idadi ya watu. Vilevile, tunatambua kwamba ardhi ikipimwa, kodi itaongezeka kwenye Serikali lakini wananchi watakuwa na usalama wa milki zao, vilevile watakuwa na dhamana ambayo itawawezesha kupata mikopo kwenye taasisi za fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili eneo nadhani tungeliangalia kwa kuongezea vifaa, lakini hata kupitia vile viwango ambavyo tunatoza kodi kulingana na eneo husika na matumizi ya ardhi. Je, ni rafiki? Zinalipika? Ule mfumo ambao tunautumia kudai kodi tungeutumia kama wa watu wa maji, muda ukifika unatumiwa message kwenye simu yako na control number kwamba unadaiwa kiasi hiki. Huo mfumo ukiwa rafiki, tutaweza kuongeza mapato eneo hili la kodi ya pango la ardhi. Kwa hiyo, napenda kusisitiza kwamba viwango vile viangaliwe lakini mifumo iboreshwe iwe rafiki inamvutia mlipaji kuweza kulipa kodi ya pango la ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile watumishi waliopo natambua kwamba ni chini ya 15% ya mahitaji yote yaliyopo nchini. Bajeti wanayopewa wangeweza kuongezewa ili wapime kwa kasi kubwa sana. Katika hili nampongeza sana Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Jerry Silaa, watu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, wamefanya kazi nzuri sana Makete na Ludewa. Kwa hiyo, naomba waendelee kuongezewa fedha ili wafanye kazi nzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile eneo ambalo napenda kuliangazia ni eneo la matumizi ya makaa ya mawe. Tunatambua kwamba kuna makubaliano huko ya Kimataifa ambayo yanakwenda kuondoa kabisa matumi ya makaa ya mawe ifikapo 2030. Sisi tuna zaidi ya tani bilioni tano ambazo hatujazichimba. Walau Kiwira na Ngaka kidogo tumeanza ambapo Ngaka wanatoa tani 250,000 na Kiwira tani 150,000. Lini tutazifikia hizi tani bilioni tano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiangalia logistics, namna ya kutoa mkaa kule unakopatikana mpaka kupeleka kwenye bandari miundombinu nayo bado ni changamoto. Kulikuwa na mpango ule wa kujenga reli inayoanzia Mtwara mpaka Mbamba Bay, Tawi, Mchuchuma na Liganga. Sasa mradi huu wabia ambao wanatarajiwa, wanaanza kuangalia sasa Serikali inafanya nini kwenye kuanza kwa mradi wa Liganga na Mchuchuma? Kwa sababu bila kupata uhakika wa mzigo wa kusafirisha tunaweza tukachelewa sana kupata mbia wa kujenga ile reli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali yangu iharakishe majadiliano na mwekezaji ili kuwe na uhakika wa mzigo wa kutosha wa chuma na makaa ya mawe kwenda Bandari ya Mtwara. Vilevile, naishauri Serikali yangu iangalie uwezekano wa kupitia hizi sheria hii Reli ya Tazara ambayo inahusisha pia nchi ya Zambia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama inawezekama kufanya majadiliano, kungekuwa na tawi pale, litoke Makambako liende pale Liganga ili nayo iweze kusaidia kusafirisha mzigo, kwa sababu siyo mzigo wote utasafiri kupitia Bandari ya Mtwara. Mzigo mwingine unaweza kuhitaji bandari nyingine. Kama itawezekana, itakua njema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, majadiliano yale yafikie kikomo na tuangalie multiply effects kwa sababu kuna ajira nyingi pale zimelala na sasa hivi kuna uhaba wa dola, lakini madini yale yamechanganyika na madini ya Titanium na Vanadium ambayo ni madini yenye thamani zaidi ya mara tano ya chuma chenyewe. Kwa hiyo, ule uhaba wa dola, mradi ule ukianza kwa kiasi kikubwa itakuwa ni mwarobaini. Tunaweza tukapata fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia miradi hii itaongeza pato kubwa sana kwenye Taifa letu na hasa uhaba wa dola kama nilivyoeleza. Kwa hiyo, nashauri kwenye Mpango huu, yale majadiliano yafikie mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona muda umenitupa mkono. Baada ya kusema hayo machache, nitamke kwamba naunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Ludewa walinizuia kabisa leo kumpongeza Mheshimiwa Bashungwa kwa sababu wana changamoto hasa wale wananchi wa Mwambao, lakini kwa namna Mheshimiwa Bashungwa alivyo muungwana, ukimpigia simu anapokea na juzi nimewasilisha changamoto zangu mbalimbali za Jimboni ikiwemo kile kituo cha afya cha Mundindi wamekamilisha ujenzi, lakini wanakosa vifaa tiba ili waweze kuanza kutao huduma. Nilimpigia Mheshimiwa Waziri usiku alipokea simu na alinisikiliza vizuri. Kwa hiyo, kwa namna hiyo na kwa jinsi Mheshimiwa Waziri alivyo mnyenyekevu na Manaibu wake, nitakuwa sio muugwana nisipompongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kutoa pongezi kwa Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Jimboni Ludewa kuna changamoto ambazo ningependa Mheshimiwa Waziri azitilie maanani. Kuna Tarafa ya Mwambao ambayo ipo kando kando ya Ziwa Nyasa. Tarafa hii kwa miaka mingi walikuwa wanategemea usafiri wa meli, bahati mbaya ile meli imekuwa na changamoto na muda mwingi haifanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarafa hii ina Kata nne ambazo hazijaunganishwa kabisa kwa barabara. Kuna Kata ya Lifuma haifikiki kwa gari na wananchi hawajawahi kuwa na gari maisha yao yote, kuna Kata na Makonde haifikiki kwa gari na wananchi hawajawahi kuona gari maisha yao yote, kuna Kata ya Kilondo na Kata ya Lumbila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo jitihada za Serikali kupitia TARURA, nilikwenda kwa CEO wa TARURA nikiwa na Madiwani wangu, waliweza kuwasikiliza vizuri, lakini changamoto kubwa, bajeti ambayo wanapewa kwa ajili ya hizi barabara ni finyu sana. Kwa hiyo, naomba Serikali iweze kuwaongezea fedha hawa watu wa TARURA na ikiwezekana wahandisi kutoka TARURA Makao Makuu waende wakasaidiane na wale walioko Mkoani na Jimboni, wafanye tathmini maana wananchi wa huku wanaona kama Serikali imewasahau na wanaona mimi Mbunge wao kama siwasemei. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba ulipe uzito. Kimsingi kuna barabara nyingine kupitia TARURA nazo wamekuwa wakifanya kazi nzuri, lakini changamoto ni bajeti wanayopewa, haitoshelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilikwenda kuwapa pole wananchi wa Kiogo; kutoka pale Masasi kwenda Kiogo, barabara ni changamoto kubwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, siku ile nilimwona Mheshimiwa Bashe wakati anazungumzia mapinduzi ya Kilimo; Kilimo Biashara, alikupa nafasi ulizungumza pale. Kwa hiyo, mimi ni miongoni mwa Wabunge ambao tunaamini maendeleo na mapinduzi ya kilimo yanaenda sambamba na kuboreshwa kwa barabara za vijijini. Kwa sababu kama Wizara ya Kilimo watakuwa wamepewa bajeti kubwa, halafu TAMISEMI kupitia TARURA wananchi wanalima mazao halafu hawawezi kuyatoa shambani kuyafikisha kwa walaji, kwa kweli hata ufanisi wa kilimo biashara utakuwa mdogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana barabara za vijijini; na ninamshukuru pia Mheshimiwa Waziri siku ile aliona clip ya gari iliyokuwa inapata shida kwenye Kijiji cha Ilininda, wananchi wanahangaika sana kwenye matope. Mheshimiwa Waziri alinitafuta na kuniambia kwamba anataka kwenda kule. Nakushukuru alitoa maelekezo kupitia TARURA, wameanza kujenga zile concrete strips. Kwa hiyo, ninaamini ule ni ufumbuzi wa kudumu. Kwa hiyo, nakuomba ahadi yake ya kutembelea Jimbo la Ludewa ibakie pale pale kwa sababu kumekuwa kuna malalamiko ya wananchi kwamba Waheshimiwa Mawaziri wengi wanarudia pale Njombe, hawaendi Ludewa kule kusikiliza changamoto na nimaamini sasa tutaendelea kupata Mawaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ambayo inalikabili Jimbo la Ludewa ni uhaba wa watumishi. Unakuta shule ya msingi ina walimu watatu; mmoja yupo masomoni, mwingine yupo maternity leave, shule imebaki na mwalimu mmoja, labda na walimu wawili au watatu wa kujitolea. Hawa walimu wa kujitolea nafasi zinavyotangazwa Serikalini nao hawapewi kipaumbele cha kupata ajira. Changamoto ya kule walimu wengi wakipelekwa wanahama. Kwa hiyo, naomba wale wanaojitolea kule Mheshimiwa Waziri nipo tayari kukuletea orodha ili wapewe kipaumbele cha kupata ajira kwenye sekta ya elimu na afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ludewa tuna upungufu wa watumishi 986, wengi ni kwenye sekta ya elimu na afya. Kwa hiyo, naomba kwenye ajira hizi Ludewa tuweze kupata kipaumbele ili tuwaondolee wazazi usumbufu wa kuchangishwa fedha ili kulipa walimu wanaojitolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Ludewa wamejitolea sana kujenga vituo vya afya kata saba, lakini havijakamilika muda mrefu. Kwa hiyo, hili nalo naomba Mheshimiwa Waziri alichukue kwa sababu tulishazungumza ili wananchi jasho lao lisipotee bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya haya machache. naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambazo zinaendelea na kule Jimboni kwangu Ludewa wananchi wanazishuhudia zinaonekana kwa macho. Ila leo naomba nijikite zaidi kwenye maeneo ya miundombinu ya barabara Jimboni kwangu Ludewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya yote, nianze kwa kutoa pole nyingi sana kwa wananchi wa Kijiji cha Liugayi kilichopo Kata ya Luilo, Kijiji cha Lifuma na Kitongoji cha Liumba kwa mafuriko makubwa ambayo wazee wenye umri mkubwa wanasema mara ya mwisho yalionekana mwaka 1963/1964. Mto Ketewaka kutokana na mvua nyingi ambazo zilinyesha upande wa Ruvuma kwa maana ya Mbinga na upande wa Ludewa na Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Ketewaka ambao unaenda kuungana na Mto Ruhuhu ulifurika sana na kuweza kuathiri wananchi wa Kijiji cha Liugayi kama nilivyoeleza ambapo nyumba zao zimebomoka, mazao yao yamesombwa na maji, kwa hiyo, hawana chakula, hali kadhalika, mifugo yao imesombwa na maji. Kwa hiyo, kuna wananchi kama wa kaya 20 wanaishi kwenye Kanisa hivi sasa. Hali kadhalika, Kijiji cha Kiyogo, Kijiji cha Kipingu, Ngerenge na baadhi ya mashamba ya wananchi wa kandokando ya Mto Mchuchuma, Kijiji cha Igalu na Kijiji cha Mbongo. Kwa hiyo, nitoe pole nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa huko, nilikwenda kuwafariji wananchi, kimsingi naomba Serikali iweze kutoa msaada wa haraka. Hatuwezi kumkufuru Mwenyezi Mungu kwa kuleta mvua nyingi kwa sababu mvua tunaihitaji, tunaiombea wakati wote tuweze kuipata na kule Ludewa imetusaidia, mwaka huu tuna mahindi mengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri wa Kilimo aanze kututafutia masoko, ni mvua hiyo hiyo ndio imewezesha kutokana na Mheshimiwa Rais kuleta ruzuku ya mbolea, wananchi wamelima zaidi na mazao wamepata zaidi, lakini mvua kutokana na kuzidi imesababisha maafa kama ambavyo nimesema. Kwa hiyo nitoe pole nyingi kwa wananchi na niwasihi waendelee kuwa na subira kwa sababu Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na wasaidizi wake wanaendelea kuliratibu vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa miundombinu ya barabara, natambua kwamba Wizara hii inashughulika na mambo mengi ya wananchi na jana nimetoka Ludewa, wananchi wanatarajia kusikia nikisemea changamoto mbalimbali ambazo zinazikabili barabara mbalimbali za Ludewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na barabara ambazo ziko chini ya TANROADS, niishukuru Serikali awamu ya kwanza ilitoa shilingi bilioni 179 kwa ajili ya kutujengea barabara kwa kiwango cha zege, kilometa 50 kutoka Lusitu hadi Mawengi. Barabara imekamilika na inatumika vizuri na ni barabara bora sana kutokana na kiwango kile cha zege. Changamoto ni kuwa, jiografia yetu ina milima mikali sana kwa hiyo kifusi kimekuwa kikiporomoka, milima inaporomoka inafunga barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi mimi mwenyewe nimepata vikwazo sehemu mbili, kwenye hii Barabara ya Itoni – Ludewa – Manda, pale Mlima Kimelembe kuna kazi inaendelea ya kukata mlima mita 20 ambao ulikuwa unagharimu maisha ya watu na mali zao, Serikali ilitoa fedha bilioni tano kwa ajili ya kuukata mlima. Sasa bahati mbaya mvua ziliwahi kufika kabla mkandarasi hajafika mwisho wa kazi, lakini nadhani hata ule upana wa barabara nao ulikuwa mdogo, kwa sababu ule udongo ni udongo ambao uko kwa asilimia mia moja. Kwa hiyo mvua inaponyesha unayeyuka kama biskuti unaporomoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa Manda kuwafariji wale wananchi wa Bonde la Ruhuhu nilikuwa siwezi kupita Ruvuma kwa sababu Mto Ruhuhu ulifurika. Kuna Mto Kipingu nao ulijaa maji, gari haiwezi kupita na kwa upande wa Nyasa maji yalikuwa yamejaa, hakuna gari linapita, lakini Mlima Kimelembe ulikuwa umeporomoka umefunga barabara. Kwa hiyo ningeugua kule, nisingeweza kufikishwa hata hospitali ya wilaya labda ningepewa milungulungu na wale wananchi ambazo ni tiba mbadala ambazo wao wamekuwa wakitumia muda wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwamba tukio hili lilinikuta mimi, sasa wananchi wanakuwa katika hali gani pale ambao barabara zinafunga, wanakuwa hawawezi kupelekwa sehemu yoyote. Kwa hiyo naomba juhudi za haraka sana na za makusudi ziweze kufanywa na Serikali kuongeza wataalam ili kwenda kutathmini na kuweza kuona ni namna gani tunaweza tukapata suluhisho la kudumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Mlima Kimelembe kwa bahati mbaya sana uligharimu maisha ya kijana mmoja wa bodaboda ambaye hata miaka 30 hajafikisha. Kifusi kilishuka na kwa bahati mbaya alikuwa pale, akafunikwa akafariki. Tunaiombea roho yake ipumzike kwa amani huko aliko. Kwa hiyo naomba sasa Serikali iweze kutuma wataalam waungane na wale wa TANROADS waliopo Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Meneja wa TANROADS pale Njombe, ni msikivu na mwepesi sana, ukimpigia simu yuko tayari kuacha shughuli zake kwenda kusaidia. Siku ile nimefungiwa nilimpigia simu, alitoka mwenyewe na wataalam wakaenda kufungua barabara. Sasa kwa bahati mbaya sana ilifunga maeneo mawili na huku kwenye hii ya Lusitu - Mawengi na yenyewe ilikuwa imefunga hata kupeleka mitambo ilikuwa haiwezekani. Kwa hiyo zinahitajika juhudi za makusudi na za haraka sana ziweze kuchukuliwa ili kuondoa vikwazo hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika kuna barabara nyingine ambayo ni ya TANROADS ambayo inaitwa Mkiu - Liganga kwenda Madaba, barabara hii ndio inayoenda kwenye Mgodi wa Liganga, ambako kuna utajiri mkubwa, tani milioni 126 za chuma ambazo ndani yake ina titanium na vanadium. Madini ambayo yana thamani zaidi ya mara 20 ya chuma chenyewe. Kwa hiyo ni barabara muhimu na ni barabara ya kiuchumi na inaunganisha na Mkoa wa Ruvuma kwa jirani yangu Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama. Sasa pale kuna lile eneo la Ndolela na kwenyewe kuna daraja pale limeondolewa na maji. Kwa hiyo, naomba sana, tunashirikiana vizuri na Mheshimiwa Mhagama kufuatilia kwa sababu wananchi wangu nayo ni alternative route na hilo eneo la Ndolela lina mashamba makubwa ya kiuchumi ambayo nayo ni barabara ya kimkakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ule mpango wa kuijenga Barabara hii ya Mkiu – Liganga - Madaba ungeanza haraka, kwa sababu Mheshimiwa Rais anavyozungumzia uwekezaji wa Mchuchuma na Liganga amechoka kusikia ngonjera hizi za muda mrefu. Hii inatakiwa iwe reflected kwenye barabara. Namwona Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi anaandika, namshukuru sana Mheshimiwa kwa usikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Rais anavyozungumzia barabara ya kiuchumi, ya kimkakati, ya uwekezaji, haya yawe reflected kule kwenye barabara hata wananchi wakiona ujenzi umeanza kwa kiwango cha lami watajua ni yale ambayo Mheshimiwa Rais anayazungumza. Kwa hiyo niombe sana Serikali iweze kuchukua hatua za haraka kwa sababu hata kutoka Mkiu kwenda Lugarao mwaka huu wananchi wamehangaika sana. Kuna daraja pale, unapotoka Lugarao kwenda Shaurimoyo kwenye Chuo cha VETA napo pana hali ngumu kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya yote hayo, nimpongeze sana yule Meneja wa TANROADS Mkoa wa Njombe yule mama, kwa kweli anafanya kazi nzuri, anajituma sana. Namwomba Waziri wa Ujenzi wasituhamishie labda kama watampandisha cheo, hilo sitakuwa na uwezo wa kuzuia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara vilevile inaanzia Mlangali – Lupanga kwenda Ikonda, Ikonda ni hospitali kubwa sana ambapo wananchi wengi wanategemea kwa ajili ya matibabu. Namshukuru Mheshimiwa Bashungwa, mwezi uliopita alikuja Ludewa, alifanya mkutano mkubwa pale Mlangali na alitoa ahadi nzuri sana kuhusu hii barabara. Kwa hiyo naomba nisiizungumzie sana ila tu ule mpango wa kuendeleza lot three kutoka pale Mawengi mpaka Nkomang’ombe. Naomba sana Serikali iendelee na iweze kujengwa kwa kiwango cha zege kwa sababu sasa hivi malori ya makaa ya mawe zaidi ya 40 yanakwama mle barabarani. Ukiwauliza kwa nini msisubiri mvua ziiishe ndio mje? Wanasema haiwezekani Wakurugenzi wa Makampuni wamekuja wana order kubwa nzuri zenye faida, kwa hiyo malori lazima yaendelee kwenda. Kwa hiyo ni ishara kwamba tusipojenga kipande hiki kilometa 68 kutoka Mawengi mpaka Nkomang’ombe, tunafunga uchumi wa nchi na tunazuia pato la Taifa kuongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu Ruvuma walipoanza kuchimba makaa ya mawe waka-shoot kwenye makusanyo ya TRA kutoka kusikojulikana mpaka kuwa namba tatu, kwa hiyo kuna uchumi, kuna kodi nyingi pale. Barabara kama hizi ambazo zinakuza pato la Taifa, zinaleta uchumi, zingepewa kipaumbele kwa sababu zinaweza kuongeza fedha ambazo zitakwenda kujenga barabara maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ambazo ziko chini za TARURA, Kata ya Ibumi nayo iko kisiwani, mwananchi akiugua pale hawezi kupelekwa hospitali ya wilaya, hawezi kupelekwa popote kwa sababu vifusi vimedondoka na vimefunga barabara. Daraja la Mto Ketewaka na lenyewe limekuwa changamoto. Halikadhalika kuna barabara hii inayoanzia Kigasi inakwenda Milo - Ludende mpaka Amani inaunganisha kata nne na barabara nyingine inayokwenda Madilu eneo la…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kamonga pole na msiba, muda wako umekwisha.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi, lakini vilevile niishukuru Serikali kwa kutusikiliza sisi Wabunge kwa sababu tunayoyasema ndio ambayo wananchi wetu wametutuma.

Ningependa nianze kwa kuchangia Wizara hii kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda amewasilisha bajeti nzuri sana. Nilikuwa naisoma hapa naifuatilia naona bajeti iko vizuri, ila nimuombe tu Mheshimiwa Waziri, Wizara yake iongeze kasi katika kusimamia bei ya bidhaa, mfumuko wa bei. Nimeona una mikakati mizuri, naomba sana uweze kusimamia ili wananchi waweze kupungukiwa na hizi changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano jana nilikuwa nazungumza na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbongo kilichopo Kata ya Manda, Wilaya ya Ludewa, alinipa bei ya vitu vichache sana na alisema atafurahi sana akiona nimekutajia. Alitaja bei ya sukari, mwaka jana ilikuwa shilingi 2,500 kwa kilo sasa ni shilingi 3,500; sabuni ilikuwa shilingi 2,000 leo ni shilingi 4,000 kwa mche mmoja; chumvi ilikuwa shilingi 500 sasa shilingi 700; mafuta ya kula yalikuwa shilingi 7,000 kwa lita sasa ni shilingi 16,000; petroli ilikuwa shilingi 2,500 sasa shilingi 4,000; nondo ilikuwa milimita kumi na mbili shilingi 22,000 leo shilingi 28,000 na mabati hizi ni bidhaa ambazo wananchi walikuwa wananitajia, pamoja na mbolea ambayo ilitoka shilingi 50,000 mpaka shilingi 150,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Serikali iongeze kasi ya kufuatilia hizi sababu ambazo Mheshimiwa Waziri ameziainisha kwenye bajeti yake. Sababu nyingi tunazozitoa zimekaa kitaalamu sana, zimekaa kisomi sana, wale wananchi kule Ligumbiro wanapata taabu sana kutuelewa. Unavyomueleza chumvi imepanda bei kwa sababu ya vita anashindwa kuelewa, unavyomueleza sabuni imepanda bei, wananchi hawatuelewi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisali misa ya Pasaka pale Ludewa wananchi walilalamika sana. Nimejaribu kujieleza mpaka nalia na machozi hawanielewi kabisa.

Kwa hiyo, naomba Wizara hii ijitahidi sana kufanyia kazi pamoja na mapendekezo ya Wabunge wengine ili wananchi waweze bkufurahia maisha kwenye nchi yao, lakini nina imani kubwa Mheshimiwa Waziri kwa wepesi wako, kwa umahiri wako hili linawezekana kwako, kwa hiyo, natarajia kuona mabadiliko na wananchi watafurahi. Na kwa kweli nikuhakikishie wananchi wa Ludewa hawana shida wakiona mambo yanakwenda vizuri wataendelea kuiunga mkono Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ningependa nizungumzie huu Mradi wa Mchuchuma na Liganga. Nimesoma kwenye ripoti mwaka jana ilikuwa kwamba majadiliano yanaendelea na sasahivi majadiliano yanaendelea. Pamoja na hii niipongeze Kamati ya Viwanda na Biashara ambayo iko chini ya Mheshimiwa Kihenzile, niliweza kushiriki kikao chao walivyojadili huu mradi, niliona kwa kweli Serikali ina mkakati mzuri, sasa naomba kwa kweli hili jambo limezungumzwa mno, kwa hiyo, hata wananchi tunavyowaeleza wanajua tunawapiga kamba tu, tunawadanganya. Kwa hiyo, naomba kwa kweli mambo yaanze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano huu mradi ulipitishwa na Waraka wa Baraza la Mawaziri mwaka 1996 kwa Waraka Namba 06/96 kwamba mradi uanze. Ilivyofika mwaka mwaka 2011 mkataba ulisainiwa ubia kati ya NDC na Kampuni ya Tanzania China International Mineral Resources Limited. Kwa hiyo, toka mwaka 2011 uthamini ukaja kufanyika mwaka 2015 kwa nia ya kulipa fidia eneo la wananchi wale wa makaa ya mawe pale Nkomang’ombe, lakini na huku kwenye chuma cha Liganga huku Mundindi. Sasa toka mwaka 2015 mpaka sasa ni miaka saba/nane imepita, kwa kweli wananchi wamepoteza matumaini ila nimesoma kwenye bajeti yako kwamba umetenga fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ila ningependa sana kuishauri Serikali lile wazo la kwenda kurudia kufanya uthamini, Serikali isilipe kipaumbele sana kwa sababu gani; mwananchi akishapewa ile fomu namba 69 kwamba sasa eneo lako tunalifanyia uthamini, hupaswi kubadili chochote, hupaswi kuondoa chochote.

Kwa hiyo, wananchi w akule walitii Serikali, ukisema uende leo ukafanye uthamini upya ile itawaumiza sana wananchi, pale jambo la kwenda kuangalia ni thamani ya ardhi inaweza kuwa imeongezeka kidogo, lakini mambo mengine wananchi kule walitii sheria walivyozuiwa kufanya chochote wale wananchi wa Nkomang’ombe na Mundindi hawakufanya chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hata hii sheria ambayo inasema kwamba maisha ya jedwali la uthamini ni miaka miwili ni Sheria ya Uthamini na Usajili wa Thamini Namba 7 ya mwaka 2016. Sasa hawa wananchi walitumia ile Sheria ya Ardhi ya Vijiji ndio iliyotumika kuwafanyia uthamini ya mwaka 1999 sasa hii imekuja baadaye na ni msingi wa haki na sheria duniani kote kwamba sheria inayotungwa leo haiwezi kunyang’anya haki zilizotolewa jana. Kwa hiyo, wale wananchi walielezwa kwamba watalipwa fidia pamoja na riba kwa kila muda unaochelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ningeshauri Serikali iweze kwenda kuwasikiliza wananchi wale na kuwalipa....

(Hapa kengele ililia kushiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa ruhusa nami niwe mchangiaji wa mwisho siku hii ambayo na wewe umekaa kwenye Kiti hicho kwa mara ya kwanza, kama Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Bajeti ninakupongeza sana kwa nafasi hiyo, nina imani kubwa na wewe kwamba utafanya vizuri na tunakutakia kila la kheri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo niende moja kwa moja kwenye mchango wangu. Mosi, nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri sana anazozifanya kwenye taifa letu ikiwemo Jimbo langu la Ludewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku Mheshimiwa Rais anapokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alitaja mashirika ambyo yanamkera likiwemo Shirika la NDC. Wakati ametaja Shirika hili la NDC wananchi wa Ludewa walifurahi sana na walishangilia sana na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa sababu NDC wamechukua vitalu Ludewa miaka mingi sana vya makaa ya mawe, chuma lakini hakuna ambacho kinafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua huyu Mkurugenzi wa sasa kwa kweli anajitihada kubwa sana, naamini akimpa muda Dkt. Nicholaus atafanya mambo yale yaende kwenye vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliambiwa na watu wa NDC kwamba mwezi Oktoba wananchi wale wa Mchuchuma na Liganga wangeweza kulipwa fidia yao ya shilingi bilioni 15. Tunawashukuru walikwenda walihakiki wananchi wote, lakini Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alikwenda pale, Mheshimiwa Antony Mtaka nami nikiwepo akawahakikishia wananchi kwamba fidia zinalipwa mwezi Oktoba, bahati mbaya uhakiki umekamilika bado mpaka leo tunaenda Aprili ile fidia ilikuwa bado haijalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi wananchi walikusanyika vikundi vikundi na kuanza kuhangaika kutaka kutafuta Waandishi wa Habari waweze kufikisha hisia zao kwa Mheshimiwa Rais kuonesha kwamba agizo lake halijatekelezwa la kuwalipa fidia wale wananchi wa Liganga na Mchuchuma. Katika ile taharuki bahati nzuri waliponipigia simu nami nilikwenda Wizara ya Fedha kufuatilia, nikabaini kwamba kibali cha kulipa ile fidia kilishatoka. Mheshimiwa Rais alitoa kibali kilitoka mwezi ule ambapo Mkuu wa Mkoa alikwenda kutoa ile ahadi kwa wananchi, bahati mbaya tu hapa katikati kuna vitu vingine ambavyo wale Wasaidizi ambao wanaikwamisha hata NDC ionekane ni taasisi ambayo haina uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha, jana nilivyofuatilia pale Hazina nikaona kwamba ile exchequer leo ndiyo ilikuwa inatoka ili baada tu ya sikukuu wananchi wale waweze kwenda kulipwa fidia. Kwa hiyo, niliweza kuwashawishi wale wananchi kwamba waniamini na kitendo cha Mheshimiwa Waziri wa Fedha kukamilisha ile exchequer siku ya leo, naamini baada ya sikukuu hii wananchi wale watakwenda kulipwa fidia na atakuwa ametuondolea aibu mimi na Mkuu wangu wa Mkoa ambao tulikwenda kuwahakikishia wale wananchi kwamba fidia watalipwa lakini mpaka leo miezi karibia minne, mitano imepita bila kulipwa fidia. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iweze kusimamia jambo hili tuweze kuhitimisha fidia za wananchi hawa ambazo wamezisubiri toka 2015 na tuende mbele, mpaka sasa makaa ya mawe yana soko kubwa sana duniani kwa wafanyabiashara ambao wataweza kusafirisha makaa ya mawe waweze kuongeza Pato la Taifa na uchumi wa Wilaya yetu ya Ludewa uweze kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru pia Mkurugenzi wa NDC kwa kukubali ushauri wetu tulioutoa kwamba vile vitalu walivyovihodhi kwa muda mrefu wafanye apportionment, wavigawe katika vipande vidogovidogo, wavitangaze, waweze kukaribisha wawekezaji wengi zaidi waweze kuchimba mkaa na kuuza sasa hivi ambapo una thamani kubwa duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri ule ameufanyia kazi na wamekwenda kugawa vitalu vile, tunawaomba sana katika kugawa vile vitalu wasiangalie tu matajiri wengine wa maeneo ya nje ya Mkoa wa Njombe, waangalie pia wale wachimbaji wadogo ambao wako maeneo yale ili nao waweze kushiriki kwenye uchumi. Waangalie Halmashauri iweze kushiriki uchumi huu na wawekezaji wengine wa ndani ya Mkoa. Namna hii itawezesha wananchi wale waweze katika kushiriki katika uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ikiwezekana hawa wachimbaji wanavyokwenda haya maeneo mengine ya sasa, waweze kuwaruhusu wananchi wale wakilipwa fidia waweze kununua hisa kwenye haya makampuni ili nao waweze kupata manufaa yatakayodumu vizazi na vizazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na uwekezaji huu wa Liganga na Mchuchuma kuna ile reli inayotoka Mtwara mpaka Mbamba Bay na tawi lake Mchuchuma na Liganga. Kuna wawekezaji ambao wanataka kujenga kwa mfumo wa PPP. Niliwasiliana na Ndugu Kafulila, Mkurugenzi wa PPP anaendelea nao kuwasikiliza. Kwa hiyo, ninaomba sana ikionekana wanao uwezo wa kujenga ile reli waweze kupewa nafasi hiyo ili waijenge na iweze kubadilisha kabisa uchumi wa ukanda huu wa Kusini miaka na miaka na kuongeza Pato la Taifa. Itatupunguzia hata kwenda kutegemea mikopo ambayo mingine ina masharti yasiyo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, reli hii ikikamilika inaweza kuchangamsha hata shughuli zingine za kiuchumi. Sambamba na hili nilikuwa nazungumza na Waziri wa Ujenzi. Changamoto kubwa ya makaa ya mawe kule yaliko mpaka kwenye Bandari ya Mtwara, kuna changamoto kubwa ya logistics, usafirishaji kuyatoa pale mpaka kufikisha bandarini. Kwa hiyo, ni muhimu sana reli hii ikajengwa ili iweze kusafirisha malighafi za chuma na makaa ya mawe mpaka bandarini na kwenda mpaka kwenye masoko ya Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili kutoka pale Ludewa kuna daraja moja ambalo lipo Kata ya Ibumi linaunganisha Wilaya ya Mbinga na Wilaya ya Ludewa. Daraja hili likijengwa itakuwa ni njia nzuri na ya mkato ya kuweza kupeleka makaa ya mawe bandarini Mtwara kuliko wakizunguka kilometa nyingi gharama za usafiri zitakuwa zimeongezeka sana. Kwa hiyo, naomba sana daraja hili liweze kujengwa ili lirahisishe usafirishaji wa makaa ya mawe vilevile shughuli za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili lina ekari ambazo Halmashauri wamezitenga 3,500 ambazo zinafaa sana kwa kilimo cha umwagiliaji, kwa hiyo daraja hili likijengwa litarahisisha sana hata ajira kwa vijana katika sekta ya kilimo, mfumo ambao Waziri wa Kilimo ameuanzisha wa BBT ni mfumo mzuri sana ambao utapunguza kero ya ajira. Tutafute sasa mfuko maalum ambao utaweza kuwakopesha vijana fedha wale wanaotoka JKT na wale wanaomaliza vyuo vikuu hasa vya kilimo na vyuo vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasoma ripoti ya Mkaguzi inaonesha kwamba kuna Halmashauri 106 zilikuwa na Idara na Vitengo ambavyo vinaongozwa na watumishi 747 wasio na sifa. Wabunge wengine wamezungumzia hapa kwamba kuna tatizo kubwa sana la ajira, ninaamini Wabunge wengi wana vijana na wazazi wao kutoka kule Majimboni wanatutumia message kila siku na kutupigia simu. Kwa hiyo, naomba vilevile hizi nafasi za ajira ambazo zinaonekana zina matatizo ziweze kufanyiwa uchambuzi na kutangazwa. Kule wazazi wamesomesha vijana wao wako kijijini hawana shughuli. Kwa hiyo, maeneo kama haya ya miradi ya kilimo cha umwagiliaji wakipewa mikopo vijana wale wanaomaliza Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) wanaweza wakatengeneza ajira na wakalisha hata nchi hii kwa kutumia haya maeneo ambayo yanafaa kwa kilimo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine…

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha naomba umalizie.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia. Kwa hiyo, baada ya kusema hayo machache kwa sababu nitapata nafasi ya kuchangia kwenye Wizara nyingine ninashukuru sana kwa kunipa nafasi naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya hata wananchi kule Ludewa wanaziona na leo wamefurahi kuona kuna Wananchi wa Ludewa walipewa mwaliko wa Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya mikopo ya maboti. Hili ni jambo la kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumpongeze pia Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na Katibu Mkuu Professor Shemdoe, hongereni sana kwa kazi nzuri. Sisi Ludewa tuna kata nane ambazo zimezunguka Ziwa Nyasa, kuna Kata ya Lumbila, Kilondo, Lifuma, Lupingu, Iwela, Manda na Ruhuhu. Kwa hiyo, kuna idadi kubwa sana ya wananchi ambao ajira yao inategemea maji, inategemea kwenye uvuvi. Kwa hiyo, bajeti hii ni muhimu sana ndiyo maana nimesimama niweze kuwasemea wale wavuvi wa jimboni kwangu na wa maeneo mengine hapa nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisoma ile Hotuba ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri nimeona amezungumzia mwaka 2021, Sekta ya Mifugo ilikua kwa 5% na kuchangia 7% ya Pato la Taifa. Hii ipo kwenye ukurasa wa 69 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Vilevile ameonesha kwamba Sekta ya Uvuvi kwa mwaka 2022 ilikua kwa 2.5% na ilichangia 1.8% kwenye Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na Wabunge wenzangu waliozungumzia Sekta hizi mbili kwa maana ya Uvuvi na Mifugo kwamba sekta hizi zinazo nafasi na uwezo mkubwa wa kuchangia zaidi kwenye Pato la Taifa iwapo zile changamoto ambazo zinaikabili Wizara hii kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameainisha na kamati imeainisha zikafanyiwa kazi na kuongezewa fedha kama ambavyo Wajumbe wengine wamependekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake amezungumzia ana upungufu mkubwa wa wafanyakazi. Hili hata kule Ziwa Nyasa Jimboni kwangu tuna watumishi wawili tu ambao ni wataalamu wa uvuvi katika kata nane. Kwa hiyo kutegemea hapa tutapata tija ni changamoto sana. Kwa hiyo, ningeiomba sana Serikali iweze kuongeza watumishi kwenye Sekta ya Uvuvi ili waende kusimamia tija kule kwa wananchi ambako wanafuga samaki na wanavua kutegemea asili kwenye Ziwa Nyasa na maziwa mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia hata vyuo ambavyo vinatoa mfaunzo ya uvuvi ni vichache sana hapa nchini hasa hizi kada za kati. Ukienda pale Sokoine utaona wana kitengo wanafanya vizuri lakini hizi kada za kati wale ndiyo hasa ukimwambia nenda Lumbila ukahudumie wananchi wa kule atakwenda na atafanya kazi yake kwa uaminifu mkubwa. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Serikali kuongeza hizi kozi za kati ngazi ya cheti, ngazi ya diploma ili tupate wataalamu wengi zaidi na hii itasaidia sana kuongeza mchango wa Sekta ya Uvuvi kwenye Pato la Taifa vilevile kuongeza ajira kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile imebainika kwamba Watanzania milioni 4.5 wanategemea Sekta ya Uvuvi. Hii ni idadi kubwa ya Watanzania ambao tunatakiwa tulinde ajira zao kwa nguvu zote. Kwa hiyo, tukiwaongezea wataalam tukawapa vitendeakazi, sekta hii kwa kweli inaweza ikakua kwa kasi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine ambalo ningependa kulizungumzia ambalo Wabunge wengi pia wamezungumzia ni eneo la kuanzisha kwa mamlaka ambayo itasimamia Sekta ya Uvuvi, itasimamia Sekta ya Mifugo. Tukiangalia upande wa maliasili, samaki ni maliasili, misitu ni maliasili. Kwa hiyo, misitu, wanyamapori wana mamlaka ambazo zinasimamia kwa sababu kule kunakuwa na wataalam ambao wao kazi yao wakilala wakiamka wanafanya mambo kwa utaalamu kwa kuzingatia tafiti tukamwacha Mheshimiwa Ulega anahusika na sheria na mambo ya sera. Hii mamlaka sasa ndiyo itasimamia kule kwenye uvuvi kwa sababu samaki nao tumesema ni maliasili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watapewa mafunzo kwa sababu shughuli ya kwenye maji inahitaji ukakamavu kidogo. Kwa hiyo, ni muhimu wakapata pia mafunzo kama ambavyo imefanyika kwenye Sekta ya Misitu. Kwa hiyo, tukiangalia mwaka ule 2009 katika Gazeti la Serikali Na. 135 ilianzisha hiyo Mamlaka ya TAWA kwa hiyo nimshauri sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na Sekta hii ya Mifugo na yeye nimeona kwenye ukurasa wa 106 wa hotuba yake amezungumzia dhamira yake ya kuanzisha hii mamlaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo hili ni muhimu sana ambalo Serikali ningeishauri iweze kutoa msukumo wa dhati kuhakikisha mamlaka hii inaanzishwa ili Sekta hii ya Mifugo, Sekta ya Uvuvi iweze kuajiri Watanzania wengi zaidi ambao vijana wetu sahizi wanahangaika ajira lakini vilevile itoe mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa letu. Hii 7% bado tuko chini sana ukizingatia takwimu zinaonesha kwamba nchi yetu ni nchi ya tatu kwa wingi wa mifugo barani Afrika. Kwa hiyo, nadhani tulipaswa tunufaike sana na idadi hii kubwa ya mifugo ambayo tunayo hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo ningependa kushauri Serikali ni eneo la uhifadhi wa mazingira kwenye maziwa yetu haya ili kuweza kuhifadhi maeneo ya kuzalia kwa samaki, mazalia. Kwa sababu wananchi wengi bado wanategemea ule uvuvi wa asili (nature). Kwa hiyo, ningeishauri Serikali kupitia Wizara hii ya Mifugo ishirikiane na Wizara inayohusika na mazingira waweze kuhifadhi vizuri yale mazalia ya samaki kwenye maziwa yetu ili kuweza kufanya samaki wawe wengi zaidi na wakati ule mpango mwingine wa ufugaji wa samaki nao unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo maeneo yote ambayo yanafaa kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwenye vizimba labda kama watatumia njia ya kufuga nchi kavu. Kwa mfano kama Ziwa Nyasa lina mawimbi makali sana kwa hiyo kuna maeneo ambayo yanahitaji Wizara iende ikayafanyie utafiti zaidi iweze kuongeza nguvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tulisema hizi sheria za uvuvi ndizo zinazosimamia ufugaji wa samaki. Hii ni changamoto kubwa sana, kwa hiyo ningeshauri Serikali iweze kufanyia marekebisho tuwe na Sera, kanuni na sheria zinazosimamia eneo la ufugaji wa samaki kwa sababu utaangalia kuna nyavu ambazo zinatumika kutengeneza vizimba. Ukija kuangalia kwenye Sheria ya Uvuvi ni nyavu haramu. Kwa hiyo, tunakuwa tunajichanganya na hapa nchini hazipatikani kwa hiyo wananchi wanahangaika kwenda kununua nchi jirani kwa njia za magendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunaona hapa kuna umuhimu mkubwa sana kwa Serikali kufanyia kazi hizi kanuni licha ya kuwa walifanyia mabadiliko mwaka 2020 lakini hili eneo sasa la ufugaji wa samaki ni vyema lilkawa na sheria zake mahususi na kanuni zake ikiwezekana na sera yake ambayo itaenda kuangalia.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa maoni yangu na mchango wangu kwenye bajeti hii ya Wizara ya Kilimo. Niungane na Wabunge wenzangu wote waliotangulia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada kubwa anazozifanya na kuuona umuhimu sana wa Wizara hii ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi humu ambao tunatokea maeneo ya majimbo ambayo yana wananchi wengi wakulima tusipozungumzia sekta hii ya kilimo tutakuwa tumewasaliti wakulima.

Mheshimiwa Spika, niungane na Wabunge wengine waliompongeza sana Mheshimiwa Bashe na Naibu wake Mheshimiwa Anthony Mavunde, Kaka yangu na wasaidizi wao wote kule Wizara. Kwa kweli wanajitahidi wanafanya kazi vizuri na wana maono nazuri. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikisoma malengo ya Wizara, Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake ameandika ni kuongeza tija na uzalishaji katika Sekta ya Kilimo. Ili kuongeza tija, maana yake nini? Maana yake tunaangalia mkulima sasa kwa ekari, akipanda ekari moja atapata mavuno kiasi gani. Hili jambo ni muhimu sana tukaliangalie ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata matokeo ya kile ambacho wanakifanya.

Mheshimiwa Spika, tutafikiaje hapo sasa? Ili tuweze kufikia kwenye tija ni muhimu sana kuboresha huduma za ugani kule kwenye vijiji. Sasa hapa maana yake tunaenda pamoja na kuangalia idadi ya watumishi walioko pale. Kule Ludewa nashukuru sana Wizara hii tumeongezewa watumishi, tulikuwa na watumishi 41, tumeongezewa Maafisa Umwagiliaji watatu na maafisa wengine watatu. Kati ya hao graduates ni tisa. Kwa hiyo niishukuru sana Serikali kwa kutuongezea watumishi kwenye Sekta ya Kilimo watumishi sita na kwenye Sekta ya Mifugo watumishi 10.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sasa hivi maana yake tija tunayoitaka anayozungumza Mheshimiwa Waziri itakuwa ni rahisi kuweza kuipata. Maana yake wale watumishi sasa wataenda kuwaelimisha wakulima. Sasa ili wapate tija lazima tunaangalia hata muda ambao wanapanda, je wakulima hawa wanapanda kwa wakati? Kwa hiyo tunatarajia watumishi hawa ambao wameletwa waweze kwenda kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanapanda kwa wakati, lakini vile vile wanatumia mbegu bora.

Mheshimiwa Spika, sasa hapa kwenye eneo la mbegu, ningependa sana kuishauri Serikali, mbegu bado kwa mkulima wa kijijini, bado ni ghali sana. Kwa hiyo Serikali ingefaa iweze kuwekeza fedha kwa kushirikiana na vyuo vikuu vya kilimo na taasisi mbalimbali za utafiti, ili waweze kuandaa mbegu ambazo mkulima atazipata kwa gharama nafuu kuliko hali ilivyo hivi sasa. Kwa sababu wakati tunakua tuliona wazazi wetu, mbegu kama alipanda mwaka jana, mwaka huu anachagua anarudia tena. Hii ilikuwa inawapunguzia gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi zile mbegu za asili tumezipoteza. Kuna Mbunge mmoja alisisitiza hapa kwamba kuna umuhimu wa kuja kuhangaika pia kuhakikisha kwamba hizi mbegu tunaweza tukaziandaa na kuzihifadhi. Kwa hiyo, eneo la mbegu bado ni ghali, kwa hiyo Serikali iwekeze, ishirikiane na vyuo vikuu vya kilimo na taasisi za utafiti kuhakikisha kwamba mbegu inashuka bei na ikiwezekana tuweke ruzuku pia kwenye mbegu na yale madawa ya kuua wadudu na yenyewe tuweke ruzuku ili yapatikane kwa bei nafuu sana.

Mheshimiwa Spika, niishukuru sana Serikali kwa kuweka ruzuku kwenye mbolea. Kule Ludewa tulipata shida kidogo kutokana na changamoto ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezieleza, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake. Kuna mtaalam mmoja anaitwa Mablanketi, nafikiri aliniunganisha Naibu Waziri mpaka tuligombana, lakini baadaye alifanya kazi nzuri tukaweza kupata lori zaidi ya 15 zenye mifugo 600 kila moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kutokana na ruzuku ile ya mbolea leo lazima niwe muungwana niweze kuishukuru sana Serikali. Nami niombe tu zile changamoto za kukosekana kwa maghala, mawakala kule wilaya za pembezoni yaweze kutatuliwa mapema.

Mheshimiwa Spika, vile vile nipongeze sana Serikali kwa kuifufua ile TFC na kuipa fedha iweze kuagiza mbolea. Nimesoma kwamba awamu ijayo mbolea itakuja mapema na hii kwa kweli sisi kule Mkoa wa Njombe alizungumza ndugu yangu Mwanyika. Tunalima mara kwa mara viazi vinalimwa misimu miwili au mitatu, lakini kuna kilimo cha bustani vitunguu, nyanya, mboga mboga. Kwa hiyo muda wowote mbolea zinahitajika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nitaomba hawa watu wa TFC waweze kuleta mbolea mapema iweze kupatikana muda wote. Vile vile kuna wazee ambao hawana uwezo wa kumudu kununua mbolea ya mfuko 70,000. Wao wakipata hela kidogo wanakwenda ananunua kwenye kilo. Naomba pia hilo liweze kuzingatiwa kwa sababu hali za wananchi wetu hazifanani, tusiwalazimishe wote kununua mbolea kilo 50 na kuendelea.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ni muhimu sana, Ludewa tumepata mahindi mengi, tumelima hekta 51,000, tunaomba masoko yaweze kuandaliwa kwa sababu tutakuwa na mavuno mengi. Tani laki tano hazitoshi, naomba Serikali ionge fedha.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa upendo mkubwa kwa wananchi wa Jimbo la Ludewa na Watanzania wote, kazi zake tunaziona. Sambamba na hilo, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na Mheshimiwa Dada yangu Naibu Waziri wake, hongera sana, kazi zenu ni nzuri na zinaonekana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Ludewa akifika kiongozi au Mheshimiwa Mbunge akienda kuwatembelea wana kawaida za kuandaa nyimbo zao za utamaduni, kuna nyimbo na ngoma za asili, wanaimba, wanacheza na wanakueleza mambo mazuri ambayo Serikali imefanya kupitia kwako Mbunge na mambo ambayo bado hayajafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilivyokwenda Kijiji cha Kisaula na Kijiji cha Lutala, wananchi walibeba maji machafu kwenye makopo wanacheza ngoma wakawa wanaomba maji, wanaomba sana. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kumuomba sana Mheshimiwa Waziri. Ninakushukuru ulimtuma Naibu Waziri alikwenda kule akawaahidi wale wananchi wa Lutala kwamba ule mradi wa Iwena ambapo Serikali ilifanya kazi nzuri sana, mradi wa bilioni moja na milioni mia mbili, kuna matenki mawili ambapo maji yanamwagika, Mheshimiwa Naibu Waziri aliwaahidi wananchi wa Lutala kwamba ule mradi utakuwa extended kwenda kuwahudumia wale wananchi wa Lutala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuishukuru sana Serikali kwa dhamira hii njema kuwakomboa wale wananchi, kwa kweli wapo kwenye changamoto kubwa sana, ule mradi unaweza pia ukahudumia na pale Kisaula, ni muhimu sana. Kwa sababu Jimbo la Ludewa lina tarafa tano, kuna hii Tarafa ya Masasi kidogo ina changamoto na inahitaji uangalizi wa karibu na msaada. Nilipanga kusema mengi lakini nashukuru Mheshimiwa Waziri nimekaa nae ameniahidi atakuja Ludewa kwa ajili ya kusaini mkataba wa mradi wa maji Ludewa Mjini wenye thamani ya bilioni saba. Kwa hiyo, naamini nitapata muda zaidi wa kuongea naye pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuishukuru sana Serikali kwa miradi mingi ya maji Ludewa. Tulipata bilioni 1.5 kwa ajili ya Mradi wa Maji Mavanga, tulipata bilioni moja kwa ajili ya mradi wa maji Mavala, tulipata bilioni 1.5 kwa ajili ya Mradi wa Kijiji cha Luvuyo, kule ambako na wenzetu wa Njombe wamechukulia maji pale Igongwi, tulipata milioni 900 kwa ajili ya mradi wa Lifua – Manda na miradi mingine mingi sana. Kwa hiyo, nipende kuishukuru sana Serikali. Niombe tu kwamba waendelee kuiangalia Ludewa kwa karibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo yako Mheshimiwa Waziri kwamba wakandarasi waweze kulipwa fedha naomba ulisimamie sana, maana yake pale Mawengi tulipata mradi wa bilioni mbili, umesinzia kidogo Mkandarasi alikuwa anadai fedha, mradi wa Mavala ulikuwa pia umesinzia kidogo. Kwa hiyo, maelezo yako hayo ya kwamba wale wakandarasi waweze kulipwa naamini yatakwenda kutengeneza furaha kubwa sana kwa wananchi wa Mavala. Hata ziara yako utakapokuja Mheshimiwa Waziri itakuwa yenye baraka sana, utakuta ngoma zile za asili za kioda na mganda zina ujumbe wenye furaha na kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Tarafa ya Mwambao, Kata ya Lumbila, Kata ya Kilondo, Kata ya Makonde, na Kata ya Lifuma. Hawa wananchi bado wanategemea maji kwenye asili (nature), wanakwenda kuteka Ziwa Nyasa. Ndiyo maana nilileta swali kuomba Wizara ifanye usanifu kuona ni jinsi gani wanaweza wakatumia maji ya Ziwa Nyasa kwa baadhi ya kata kuweza kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba mradi huu unaweza kuwa na gharama kubwa kwa sababu utahitaji pumping ya maji kwa kutumia umeme, ndipo yaweze kuhudumia wananchi. Tusiangalie gharama kwenye kuokoa uhai wa wananchi, kwa sababu anayepewa kazi ya kumpa mwanadamu maji, anapewa kazi ya kulinda uhai wa mwanandamu huyu. Kwa hiyo, naomba wananchi hawa kama wengine ambao tunashukuru, nao ifike siku waweze kutoa shukrani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna mamlaka ya bonde la Ziwa Nyasa, naomba sana waweze kufanya utafiti kwenye hili Ziwa kuangalia mabadiliko ya tabianchi, kwa sababu mwaka huu maji yameongezeka sana kwenye ziwa. Ukiongea na wale wazee wenye umri mkubwa, wanasema hali hiyo ilionekana mwaka 1976. Kwa hiyo, kwa kuwa wataalam wapo, watusaidie waweze kwenda kufanya utafiti tuweze kujua chanzo. Kwa sababu kuna historia, kuna mwaka nchi jirani iliwahi kufunga mto maji yakaleta shida kidogo. Kwa hiyo, ni vizuri tukajua ili tuweze kuwaeleza wananchi chanzo cha maji kujaa kwa kiwango kile: Je, ni mvua tu au kuna sababu nyingine, ili wananchi waweze kuishi kwa amani kando ya Ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo, niangalie huu mradi sasa wa pale Kipingu. Kijiji cha Kipingu kwenye Mto Ruhuhu kumekuwa na matukio ya wananchi kuliwa sana na mamba. Hivi sasa ninavyoongea, tunauguza mwananchi mmoja, na vifo vingi vimetokea kwa wananchi kukosa maji. Namshukuru Mwenyekiti wangu wa Mkoa wa Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Deo Sanga na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Anthony Mtaka, walifanya ziara pale, waliweza kwenda kuwapa pole wananchi na kuwafariji. Kwa hiyo, waliahidi kwamba watashirikiana nami Mbunge, kuhakikisha wale wananchi wa Kipingu wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliongea na jirani zetu, Wilaya ya Nyasa, wanaweza wakachukua maji pale, inahitajika kama roll kumi tu, wakavusha kwenye daraja la Mto Ruhuhu tukaweza kuwasaidia wale wananchi wasiende kuteka maji kwenye Mto Ruhuhu. Isitoshe, maji ya Mto Ruhuhu siyo salama sana. Kuna uchimbaji mkubwa wa madini eneo la Amani kule, Ibumi, Nkomang’ombe, Lihugai, wanachimba sana makaa ya mawe na dhahabu. Kwa hiyo, yale maji siyo salama sana. Kwa hiyo, ni vizuri wale wananchi wakatafutiwa chanzo mbadala ili waweze kupata maji ya uhakika ili wajiepushe na magonjwa mbalimbali ambayo yatawagharimu sana uchumi wao. Fedha watakazozipata badala ya kwenda hospitali, basi zitawasaidia kufanya mambo mengine iwapo watapata maji salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba pia lile eneo la Mchuchuma na Liganga ambapo nimetoka kuishukuru sana Serikali kwa kushughulikia suala la fidia ambalo lilikwama, tunatarajia litakuwa na wananchi wengi sana. Pale Amani, Mundindi, namshukuru Mheshimiwa Waziri nimeona kwenye bajei ameweka mradi. Pale Njelela kulikuwa na tenki lita 100,000 ambalo kuna Padre alituletea, ila tulikosa mtaalam wa ku- survey maji na kuyaongoza yakafika kwenye tenki. Nakushukuru umetuletea Engineer mzuri sasa hivi, kwa kweli nakupongeza kijana, wananchi wana matumaini na mategemeo makubwa sana nawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huu mradi ambao umeupeleka hapa Njelela na Mundindi, utakwenda kusaidia wawekezaji wale wa Mchuchuma na Liganga. Hata hivyo, mradi uliopelekwa bado ni mdogo, hauwezi kutosheleza idadi ya watu ambao tunawatarajia watakwenda eneo lile la Amani pale Mundindi, na eneo la Njelela. Kwa hiyo, kadhalika na kule kwenye makaa ya mawe, Mchuchuma, Makaa ya mawe yana athari. Ukisoma ripoti za kimazingira. Kwa hiyo, wananchi wanatakiwa wapewe maji mbadala. Kwa hiyo, wale wananchi wa Lifua, Liugahi, Nkomang’ombe, Malamba, nao wanahitaji wapewe maji mbadala na tuweze kuangalia idadi ya watu ambao watakwenda kuishi pale kutokana na uwekezaji mkubwa ambao Serikali inakwenda kuufanya pale. Halikadharika kule Liugahi iwapo wananchi wale watatumia maji yale ya kwenye mito ambapo makaa ya mawe yanatiririsha maji, ni hatari sana kwa afya zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja, na nina imani kubwa sana na Mheshimiwa Waziri, kwani ametutoa mbali. Alipotukuta na sasa kuna mabadiliko makubwa. Kule Ludewa tumepata miradi mingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia mjadala wa bajeti hii. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Nampongeza sana kwa kuwa kazi anayoifanya kwenye eneo hili ni kubwa sana ni lazima tuweze kumpongeza. Vilevile nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Nape Nnauye, Mheshimiwa Naibu Waziri wake, Mheshimiwa Kundo na taasisi zao zote. Kuna TCRA, kuna UCSAF, kuna yule dada yangu Justina, kwa kweli anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachomshukuru Mheshimiwa Nape, kwa sababu anapafahamu pale Lupingu kuna mwaka alienda akiwa Mwenezi wa Chama Taifa, na nilipoenda kumwomba mnara wa simu, alimtuma Naibu wake tukaenda mpaka pale wakapanda boti mpaka sehemu inaitwa Igha. Aliwaahidi wananchi wale kwamba atawasha mnara mapema. Nitumie nafasi hii kuishukuru sana Serikali, sasa hivi Kata yote la Lupingu, wananchi hata wakiwa kwenye maji wanavua Samaki, wanaweza kuwasiliana. Likitokea tatizo lolote, ajali yoyote, mawasiliano yanakuwa ya mapema kwa sababu kuna mnara pale ambao unaweza kusaidia kutoa taarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni ishara kwamba wizara hii inatambua kwamba mawasiliano ya simu siyo anasa, ni hitaji la muhimu kwa dunia ya leo, wananchi wanatumia kwa manufaa mbaliambali kuweza kupeana habari kwa ajili ya biashara mbalimbali, fursa mbalimbali kupitia mitandao ya simu. Vilevile kwenye shule zetu za msingi, walimu wanasajili wanafunzi wa Darasa la Saba kwa kutumia mitandao ya simu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kule, zahanati zetu hii mitandao inatumika kwa ajili ya matumizi ya shughuli za kila siku. Kwa hiyo, na kule Ludewa maeneo mengi ambayo yako pembezoni tuna zahanati nyingi ambazo zinahitaji mawasiliano ya simu. Tuna shule za msingi zaidi ya 100 ambao walimu walikuwa wakitembea umbali mrefu sana kwenda kusajili wanafunzi wale wa Darasa la Saba. Nafurahi kwamba tokea nimekuwa Mbunge Serikali hii ya awamu ya sita imeweza kunisaidia kupata minara 15.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipata mnara pale Madope, tayari unafanya kazi; tulipata mnara Kijiji cha Ilawa Kata ya Madilu, unafanya kazi; Tulipata mnara Mkongobaki, Ibumi, Lupanga na Galawale pale Kata ya Ludewa ambao unahudumia hadi Nindi kule; Kuna mnara Mkumbili, kuna mnara Mkomang’ombe, Mapogoro ambao unaenda kujengwa sasa mnara wa Tigo; kuna mnara Shaurimoyo na Mdiligili ambao unakwenda kujengwa sasa wa Vodacom; kuna mnara Kitowele; na Lupande ambao unakwenda kujengwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, hapa Lupande alikwenda, alifanya mkutano na aliwaahidi wananchi kwamba atakwenda kujenga mnara, Serikali itapeleka mnara pale. Kwa hiyo, nafurahi sana siku ya utiaji saini mikataba ile 758 mimi nilikwenda pale kwa niaba ya wananchi wa Ludewa na niliona hawa wananchi wa Kitewele na Lupande sasa watakwenda kupata mnara kama ambavyo Mheshimiwa Waziri aliweza kuahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo tunapata mnara ni Mapogoro, mnara wa Tigo, kuna eneo la Ludende mnara wa Vodacom, kuna Iwela tumepata mnara wa TTCL na Igalu. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Ludewa kuishukuru sana sana Serikali. Hata mimi Mbunge mmenipa heshima sana, nikipita kwa wananchi naonekana Mbunge wa maana kwa sababu ya Mheshimiwa Nape Nnauye na Serikali ya Awamu ya Sita. Kwa sababu kule kwetu minara ilikuwa changamoto kubwa sana ila sasa hivi kwa mwendo huu, naamini tutafika mbali zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuiomba Serikali iendelee kuangalia ile Kata ya Ibumi, eneo lile lina utajiri mkubwa wa madini, kuna migodi mikubwa inaenda kuanza pale. Kwa hiyo, mawasiliano yatakuwa muhimu sana hasa Kijiji kile cha Masimavalafu, kuna reserve kubwa sana za copper na makaa ya mawe, kwa hiyo, kuna wawekezaji kule. Naishukuru Serikali mwaka huu kupitia TAMISEMI, wataenda kutujengea daraja pale ambalo linaunganisha Kata ya Ibumi na Kata ya Itumbandyosi ambayo iko kule kwa Mheshimiwa Benaya. Kwa hiyo, maeneo haya, mawasiliano yatakuwa muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Kijiji kile cha Masimavalafu kiweze kupata mawasiliano ya simu. Tunao mnara pale wa TTCL na umewashwa kipindi nikiwa Mbunge, kwa hiyo, naishukuru sana Serikali, lakini coverage yake bado ni ndogo. Siku ile niliongea na Mkurugenzi yule wa TTCL akaniahidi atatuma wataalam. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba sana msaada wako, hawa watu wa TTCL waweze kwenda pale kuongeza uwezo wa ule mnara ili uhudimie kile Kitongoji kile cha Nyamalamba na maeneo jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika, Tarafa ya Mwambao Kijiji cha Lumbila Kata yote ya Lumbila, Kata ya Makonde na Kata ya Kilondo, wana mnara ule wa Halotel ambao nao kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wameeleza, unategemea teknolojia ya umeme wa jua (solar). Sasa kukiwa na hali ya hewa kidogo ya mawingu mawingu, wananchi wanakosa mawasiliano. Kabla ya Mheshimiwa Naibu Waziri wataalam walishaenda na vipimo wakaweza kutambua maeneo yote. Kwa hiyo naomba tu utekekelezaji ufanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, nashukuru sana. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi. Nianze kwa kuishukuru sana Serikali kwa sisi Ludewa kwenye ile barabara inayoanzia Njombe kwa maana ya Itoni Ludewa mpaka Manda tumeweza kupata mkandarasi kwa ajili ya kujenga lami kiwango cha zege. Mradi huu unakadiriwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni 95 na pia nishukuru ule mradi mwingine wa Mawengi hadi Lusitu nao ujenzi wa lami kwa kiwango cha zege unaendelea vizuri na sasa umefikia asilimia 86.

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Waziri wa Fedha, hivi karibuni wameweza kulipa shilingi bilioni 45 kwa hiyo nishukuru sana Serikali kazi inaendelea vizuri. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuiomba Serikali kwamba barabara hii haijafika bado Makao Makuu ya Wilaya imeishia pale Mawengi kutoka pale mpaka Makao Makuu ya Wilaya kwa maana ya Lot III inaanzia Mawengi mpaka Ngalawale pale Ludewa Mjini unafika Ngalawale. Kwa hiyo naomba sana barabara hii iweze kuendelea iweze kufika Makao Makuu ya Wilaya ili mwananchi anavyotoka Makao Makuu ya wilaya ya Ludewa kwenda Mkoani apite kwenye lami.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika ninapende kuishukuru Wizara ya Ujenzi, Wizara hii ndiyo Mawaziri wake wamekuja Ludewa mara nyingi Zaidi, Mheshimiwa Kasekenya Naibu Waziri wa Ujenzi amekuja Ludewa mara mbili tokea mimi nimekuwa Mbunge. Ninamshukuru sana tulikwenda nae daraja la Luhuhu pale na Waziri wa Ujenzi halikadhalika tulikuwa naye Ludewa hasa ambacho napenda kushukuru baada ya kupata maafa ya madaraja kukatika nashukuru Serikali iliweza kumtuma Naibu Waziri wa Ujenzi, kwa kweli wana Ludewa walifarijika sana kumuona Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi.

Mheshimiwa Spika, hii barabara umeweza kuiona kuanzia pale Njombe mpaka Kipingu darajani, wananchi wanaomba sana barabara hii iweze kufika Manda kwa sababu Wilaya ya Ludewa ina rasilimali nyingi. Tunalo Ziwa Nyasa na sasa wananchi wameelimika wanataka kuanza miradi ya ufugaji wa samaki kwenye vizimba na nimeandika barua kwa Waziri wa Uvuvi kuomba pale watujengee soko la wavuvi pale Manda Nsungu. Hii barabara ikikamilika itafungua sana uchumi wa kule na kwa sabbu Waziri wa Mambo ya Ndani ametuletea Maafisa Uhamiaji pale itakuwa ni rahisi zaidi kuanzisha hata biashara na nchi jirani ya Malawi.

Mheshimiwa Spika, barabara hii ni muhimu sana na sasa tuna uwekezaji mkubwa wa makaa ya mawe ule Mlima Kimelembe kwenye hii barabara inayoanzia Itoni, Ludewa Manda Mlima Kimelembe pale wananchi wengi wa Ludewa wamepata ajali na magari na mabasi ya abiria yameanguka sana na kupoteza maisha ya watu na kuwasababishia wengine ulemavu. Kwa hiyo naomba sana hii barabara iweze kukamilika.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna uwekezaji wa makaa ya mawe, tuna kampuni inaitwa Maxcoal Ludewa wanatarajia kusafirisha makaa ya mawe kuwa na lori 4,000 kwa mwezi. Lori 4,000 kwa mwezi ni nyingi sana. Kwa hiyo tunahitaji ile barabara iweze kukamilika ili iweze kufungua uchumi wa Wilaya yetu.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika kuna barabara nimshukuru Kaka yangu Dkt. Joseph Mhagama Mbunge wa Madaba, asubuhi amezungumzia sana barabara inayoanzia Mkiu kwenda Liganga mpaka Madaba, barabara hii ni muhimu sana. Wananchi wa Ludewa wanaona kama wanaambiwa wale ugali kwa harufu ya nyama choma au kwa picha ya Samaki, kwa sabbu miaka yote tumekuwa tukielezwa kwamba tusubirie mradi wa Mchuchuma na Liganga uanze Mwekezaji ndipo ajenge ile barabara. Wazo hili wananchi wa Ludewa wanaona kama linawacheleweshea maendeleo, wanaamini kwamba inapaswa kuanza barabara ndipo mwekezaji aje. Kwa hiyo tunakuwa tunawekwa pembeni kwenye mipango mingine ya kupata fursa za kujengewa barabara ile kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo ninashukuru sana nimeona tumewekewa pale mita 400 za lami, eneo hili Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi umeupiga mwingi kwa sababu kuna ajali nyingi sana zilikuwa zinatokea pale, kutoka Kibao njiapanda ya Lugarawa unaacha zege unavyokuwa unaenda Lugarawa pale mmetupa mita 400 tunaamini kabla bajeti hii unavyohitimisha utakuwa umetufikiria utuongezee tena kwa sababu mita 400 ni kama viwanja vinne vya mpira, tunashukuru kwa sababu eneo lilikuwa korofi sana ila tunaomba utufikirie tupate hata kilometa Mbili angalau pale tutakuwa tumetibu tatizo.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna barabara inayoanzia Ludewa kwenda Lupingu nayo ilipata maafa sana, milima iliporomoka mimi nilikwenda kuwapa pole wananchi, ule udongo na vifusi, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Njombe na Meneja wa TANROADS tulivyopata maafa haya walihamia kule walikaa na wananchi muda wote, ila sasa tunaomba barabara hii itengewe fedha za kutosha kuweza kutoa vifusi na kujenga mitaro ili isiharibike.

Mheshimiwa Spika, kuna barabara nyingine inaitwa Lupingu - Makonde - Lumbila hii ni barabara ya mpakani, Ziwa Nyasa tunajua historia ya hili Ziwa tumekuwa tukirushiana maneno na nchi Jirani, ndiyo maana Wabunge watangulizi wangu kuanzia Horace Kolimba, Chrispine Mponda na Mathias Kihaule walisisitiza sana kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa ulinzi na usalama wa nchi yetu, na sisi tukakubaliana pale na Mkoa kwamba tuandike barua ofisi ya Waziri Mkuu kuweza kuomba barabara hii ichukuliwe kama ni ya muhimu sana kiulinzi na usalama, hasa jirani yetu maneno yalikuwepo kuwepo hapo nyuma nafikiri mnaelewa vizuri. Kwa hiyo, barabara hii tunaomba sana kwa sababu kule mwambao ule usafiri ambao unategemewa wa meli ile meli imefanya route moja tu kwa mwaka huu ikaharibika mpaka sasa imekuwa matengenezo.

Mheshimiwa Spika, nilimuona Naibu Waziri wa Uchukuzi amekwenda pale alijitahidi kuwakaripia kidogo lakini wananchi wa leo wanauelewa mkubwa sana, wanajaribu kupima wale watumishi walioko pale hivi wanawahurumia wananchi kiasi gani. Kwa sababu wananchi wanazama kwenye maji wanatumia maboti, bei ya vifaa vya ujenzi inakuwa kubwa sana kutokana na kukosekana kwa usafiri wa uhakika, kwa hiyo saruji hata ujenzi wa Serikali miundombinu kwenye mashule, kwenye vituo vya afya na zahanati inakuwa ni changamoto sana, gharama zinaongezeka sana. Tulipata shida sana ujenzi wa madarasa manne shule ya Sekondari Makonde wananchi wanabeba mizigo kichwani, kwa hiyo naomba sana hii barabara Serikali iweze kuipa uzito wa kipekee na kuendelea nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile ile meli ni muhimu sana tumekuwa tukiongea hapa na jirani yangu Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya wananchi kule wametukalia kooni wanaona kama mimi na Mheshimiwa Manyanya hatusemi. Mwanzoni walikuwa wanalalamikia juu ya shape ya ile meli lile Ziwa Nyasa lina mawimbi makali sana.

SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa Kmoga, muda wako umekwisha.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Nakushukuru sana baada ya hayo machache naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Ardhi. Nami niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kupewa tuzo, maana yake mchango wake umetambulika duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Mama yangu Mheshimiwa Angeline Mabula na Naibu wake Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete na niwaambie kwamba wananchi wa Ludewa wanawashukuru sana kwa kuwapa fedha kwa ajili ya kurasimisha makazi kiasi cha shilingi milioni 400 na zaidi ambazo zimetumika pale Mlangali wameshapima zaidi ya viwanja 3,000. Halikadhalika Makao Makuu ya Wilaya Ludewa kazi ya upimaji inaendelea. Kijiji cha Amani wananchi wanawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ingawa baadhi ya maeneo wanamashaka na kwamba tunavyopeleka mipango miji watu wa TANESCO wanadhani wanataka kuwaongezea bei ya umeme yaani maeneo yale ambayo yamepangwa kuwa planning areas watu wa TANESCO wana-charge gharama kubwa za umeme. Lakini tunaendelea kuwaelimisha na wanawaalika sana kwenda kuwatembelea na wanawaomba mshirikiane na Waziri wa TAMISEMI kuhakikisha watu wa TARURA wanasaidia kufungua zile barabara ili Mji wa Mlangali uweze kuwa wa kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Amani ambao wanasubiri sana uwekezaji mkubwa wa Liganga napo paweze kuwa na mji wa kisasa kwamba tusiishie tu kurasimisha, wanaomba tuwasaidie kuhakikisha kwamba barabara zinafunguliwa vizuri ili miji iweze kuwa na mvuto wa kisasa na vilevile wanaomba sana taasisi mbalimbali za kifedha ambazo zinawezesha wananchi kwenda kutoa mikopo kama TADB na CRDB waweze kwenda kuwakopesha pembejeo za kilimo. Kwa sababu sasa Wizara ya Ardhi imeongeza thamani ya ardhi yao kuhakikisha kwamba wanapata hati. Kwa hiyo, hongera sana Mheshimiwa Waziri, wananchi umewatengenezea furaha pale Ludewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika Mheshimiwa Waziri wananchi wa Ludewa wanaomba sana pale Makao Makuu ya Wilaya kulikuwa na eneo la kituo cha mabasi na kulikuwa na soko, kulikuwa na vibanda vimegawanywa kwa wananchi waweze kujenga na kufanyia biashara, ni kama uwezeshaji wa kuchumi kwa wananchi. Sasa bahati mbaya kumetokea hali ya kutoelewana kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa na wananchi wale wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wanaomba sana umtume Kamishna wako wa Ardhi aweze kwenda pale na ikiwezekana utolewe muongozo ambao utaonesha haki na wajibu wa kila upande katika kumiliki viwanja hivi vya maeneo ya stand na soko, vibanda vya biashara, kwamba ukitolewa mwongozo utaepusha migogoro, wananchi kupelekana mahakamani na Serikali kwa sababu wananchi ni mali ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze pia kwa bajeti hii nimeweza kuipitia vizuri. Nimeona mikakati ya Wizara ya Ardhi ni mizuri sana, mipango yao imekaa vizuri ila sasa uwezeshwaji, Serikali inapaswa kuunga mkono sana Wizara hii tuweze kuwaongezea bajeti kwa ajili ya kuweza kupima nchi hii. Kwa uzoefu nilionao, mimi naamini kama Wizara ya Ardhi itawezeshwa kwa fedha na vifaa kuweza kupima nchi hii kama mipango yao ilivyo, tutapunguza migogoro ya ardhi kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kama ardhi inakuwa imepimwa, mwananchi amelindwa kwa kupewa hati miliki, ni nani atakuja pale kwenda kuvamia eneo la mwananchi? Kwa sababu itakuwa hata rahisi kutatua migogoro ya ardhi. (Makofi)

Kwa hiyo, naomba sana Serikali iweze kuwaongezea fedha Wizara hii ili waweze kufikia malengo ya kupanga, kupima nchi hii ili kuweza kuepusha migogoro, lakini vilevile kuwawezesha wananchi kiuchumi. Wananchi wanakuwa na dhamana ambayo inawatambua, inawafanya watambulike kwenye taasisi mbalimbali za fedha nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile nimepitia hotuba ya bajeti hii ukurasa wa 174, nimebaini Wizara hii ina upungufu mkubwa sana wa watumishi. Naomba nitoe mfano hapa, kwa upande wa Maafisa Ardhi mahitaji ni Maafisa 1,206 waliopo ni 605, upungufu ni watumishi 601, kwa hiyo, waliopo ni asilimia 50.2 ya mahitaji. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iweze kutoa vibali vya ajira ili maafisa hawa, kwa sababu mitaani wamo. Chuo cha Ardhi - Tabora kinazalisha wale Maafisa Ardhi Wasaidizi wazuri, Chuo cha Ardhi Morogoro na Chuo cha Ardhi Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba vibali viweze kutolewa kwa sababu hata hawa Wapima ambao tunatarajia hizi fedha tunazopeleka wao ndio watakaoenda kufanya kazi. Mahitaji ni Wapima 1,978; Wapima waliopo ni 618, upungufu ni 1,360. Kwa hiyo, naomba Serikali iweze kuangalia jambo hili kama tatizo ili iweze kuajiri wataalam. Hata halikadhalika wa Mipango Miji naona nao mahitaji ni 1,036, waliopo ni 330, upungufu ni 706, waliopo ni asilimia 22 ya mahitaji yote. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iweze kutoa vibali ili tumuongezee nguvu Mheshimiwa Waziri na Naibu wake Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete waweze kutimiza malengo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika kule Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi; nashukuru naona na Ludewa wameikumbuka tunaweza kupata hapo vijiji vichache. Naomba sana nao waweze kuongezewa fedha ili waweze kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuepusha muingiliano wa watumiaji mbalimbali wa ardhi. Hii itasaidia sana kuepusha migogoro ya ardhi na niwapongeze kwa kuanzisha ofisi za Kanda. Naomba wazisimamie vizuri ili ziweze kupanga na kupima vijiji, ile mipango kina ya vijiji iweze kuandaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba sana Wizara hii ya Ardhi iweze kushirikiana na watu wa TRA, ile kodi ya majengo uaami ule utaratibu tuliouweka mwaka jana kwamba tuta-charge kupitia LUKU, mita zile za umeme. Pale nafikiri hela nyingi bado hazikusanywi, kwa hiyo, naomba tuweze kutumia wataalam wetu kuhakikisha mapato yale tunaweza kuyapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie bajeti hii na niungane na Waheshimiwa Wabunge wote walioendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri pamoja na Mheshimiwa Waziri January Makamba na Naibu wake Mheshimiwa Stephen Byabato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba nimekutana na Mheshimiwa Waziri na changamoto zangu ameweza kunisikiliza vizuri, lakini bahati mbaya wakati nazungumza na Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Ludewa walionituma hawakuwepo, kwa hiyo, hawakusikia. Kwa hiyo, naomba nirudie niliyoyaongea kwa Mheshimiwa Waziri. Nikiri pia kwamba nimezungumza na Mkurugenzi wa REA changamoto zangu ameweza kuzisikiliza vizuri na nipongeze sana Wizara hii kwa kuandaa wataalam wote kuja hapa viwanja vya Bunge kuweza kutusikiliza. Kwa hiyo changamoto zetu tumeziwasilisha tunaamini zitafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa maana ya wananchi walionituma wasikie nikiwasemea, naomba nianze kwa kumuomba sana Mheshimiwa January Makamba kule Jimboni kwangu Ludewa hasa Tarafa ya Masasi, Serikali imefanya kazi nzuri sana ya kusambaza umeme isipokuwa ni ngazi ile ya vijiji kwenye vitongoji mbalimbali bado kuna malalamiko sana na nilifanya ziara kwenye vijiji vyangu vyote 77 vikiwemo hivi vya Tarafa ya Masasi. Nilikwenda Kitongoji cha Chingole pale Manda kuna wananchi walikuwa hawajaunganishiwa umeme. Kwa hiyo, naomba sana na vitongoji vingine vya Manda viweze kuunganishiwa umeme pamoja na Tarafa yote ya Masasi. Huu mradi wa vitongoji naomba Ludewa nao iweze kupewa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna mradi wa REA ambao uko kwenye tarafa ya Mwambao, kuna mkandarasi mmoja alipewa kazi kwenye Kijiji cha Mkwimbili, Kata ya Makonde, Kata ya Lifuma, mkandarasi huyo anashindwa kuwasha umeme tokea mwezi Aprili kwa sababu niliomba Serikalini wapewe umeme mkubwa wa KV 33, lakini sasa umeme uliotoka Makao Makuu ya Wilaya ya Ludewa kwenda Lupingu ni KV 11. Kwa hiyo sasa waliomba na nashukuru niliongea na engineer wa TANESCO Ludewa amekiri kwamba Mheshimiwa Waziri ameshatoa maelekezo, kwa hiyo naomba amsisitize ili aweze kubadilisha hiyo KV 11 Kuwa 33 ili wananchi wa Mkwimbili, wananchi wa Makonde na wananchi wa Lifuma waweze kuwashiwa umeme mapema iwezekanavyo, kwa sababu zile nguzo tokea ziwekwe wamekuwa wakipiga nazo picha mwaka sasa umeisha, wanatamani sana umeme uweze kuwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa Tarafa ya Mwambao, kuna vitongoji ambavyo vina idadi kubwa ya watu, kuna Kitongoji cha Ndamba na Kitongoji cha Kilindi, Kitongoji cha Ndamba kipo pale Kata ya Makonde na Kitongoji cha Kilindi kipo Lifuma, ni vitongoji ambavyo vina idadi kubwa ya wananchi ambao wapo willing na wameupokea mradi vizuri, lakini hawa wameachwa, naomba nao wafikiriwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Tarafa hii ya Mwambao kuna mkandarasi mwingine ambaye amepewa Mradi wa Kusambaza Umeme Kata ya Lumbila, Kijiji cha Ndoa, Kitongoji cha Kimata, Kitongoji cha Kitewele na Liunji, Mkandarasi huyu bado hajapeleka nguzo kwa muda mrefu sana tokea asaini mkataba. Nilivyozungumza naye alikuwa amezungumza kwamba ameshawasiliana na watu wa meli ya mizigo pale Itungu kwa sababu ipo vizuri inafanya kazi, watapeleka. Naomba ahimizwe ili aweze kufanyakazi ili kule mwambao kwote waweze kupata umeme kama maeneo mengine ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Kijiji cha Kitewele ambacho kipo Kata ya Mawengi, eneo hili lipo jirani na mzalishaji binafsi umeme wa JUHUMA. Kwa hiyo nilishauri ili waweze kufikisha umeme huu ni vizuri wakaingiza kile Kijiji cha Mawengi kwenye Mradi wa REA ili waweze kupata uelekeo mzuri wa kupeleka umeme katika Kitongoji cha Liunji na Kitongoji cha Kitewele. Kwa hiyo kwa Tarafa ya Mwambao tutakuwa tumemaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika niliweza kuzungumza na Mheshimiwa Waziri na Mkurugenzi wa REA kwamba wananchi kwenye vijiji 20 vya Jimbo langu la Ludewa ambao wanategemea umeme wa mzalishaji binafsi Kampuni ya Madope, kwa kweli tunaomba sana Serikali isaidie Kampuni hii ya Madope, kwa sababu jukumu la msingi la Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na namwona Mwanasheria Mkuu wa Serikali pale, najua atatusomea kama si Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, kama ilivyofanyiwa marekebisho yake mara kadhaa, inasema jukumu kubwa la Serikali ni ustawi wa wananchi. Kwa hiyo umeme ni ustawi wa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa jukumu hili ni la Serikali, naomba sana Serikali iweze kumsaidia huyu mzalishaji binafsi Kampuni ya Madope kwa sababu vijiji 20 ni vingi sana kupata mgao wa umeme wa masaa zaidi ya 12. Naamini kabisa wakipewa nyaya kwa sababu ule mradi wa mwanzo zile nyaya zilizowekwa zilikuwa ni aluminum millimeter 50. Wamejitahidi wao kwa nafasi wameweza kuhakikisha Mkiu ile Kata ya Lubonde wanapata umeme masaa yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili waweze kutatua tatizo hilo Kata ya Madilu na Kata ya Mlangali, wanahitaji kupata nyaya ili waweze kubadilisha ile miundombinu, waweze kufikia na Kata ya Madope na Lupanga. Kwa hiyo naomba sana Wizara hii, nikiri kwamba baada ya kuwasiliana na Mkurugenzi wa REA, Bodi ya REA imefika pale wameona hizi changamoto, hilo lazima niwe muungwana, Mkurugenzi mwenyewe amekwenda ameona changamoto na yeye atakubaliana na mimi kwamba kuna haja REA na mimi Mbunge na wale wazalishaji wa Kampuni ya Madope tuna kila sababu ya kupita kwa pamoja na watalaam wa REA kwenda kuzungumza na wananchi, kuwapa uhakika kwamba wale ambao wateja wapya hawajaunganishiwa umeme kule Lupanga wawe na uhakika kwamba hadi lini matatizo haya yatakuwa yametatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niendelee kuishukuru Serikali, tulikaa kikao na Mkurugenzi wa REA kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri waliweza kutoa Shilingi Milioni 307, Milioni 150 zilitolewa lakini hizo zilizobakia wamewadhamini Kampuni ya Madope kuweza kuchukua nyaya kwa mzalishaji. Naomba Mkurugenzi wa REA atusaidie kuongea na yule mzalishaji ili nyaya hizi ziweze kutolewa haraka ziwawezesha Kampuni ya Madope kuunganisha umeme kwenye gridi ya Taifa, ule mkataba ambao wanauzia Serikali, itawasaidia kupata mapato yatakoyoweza kutatua changamoto ndogondogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukitatua tatizo la mgao wa umeme kwenye hivi vijiji 20 na tukaenda kusaidia yule mzalishaji binafsi wa JUHUMA ambaye anazalisha umeme pale Mawengi, unakwenda Milo itasaidia sana kuweza kumaliza kero za umeme kwenye Jimbo la Ludewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya ninayoyasema ni maeneo ya uzalishaji mkubwa sana. Pale Mlangali idadi ya watu ni kubwa, pamekaa kibiashara, kwa hiyo, kukosa umeme pale kwakweli ni kuwaadhibu sana wale wananchi. Nimepita juzi wakanisimamisha, nilikuwa natoka kwenye ziara jimboni, kilio chao kikubwa wananchi wa Mlangali, Madilu, Madope, Lupanga na pale Lugarawa ni umeme na katika maeneo haya kuna vituo vya afya, kuna taasisi, kuna chuo cha afya, kuna chuo cha VETA pale Shaurimoyo kinajengwa na Serikali imetoa bilioni tano na milioni mia nne, kipo kwenye Kata hii ya Lugarawa. Kwa hiyo, kuna taasisi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili niendelee kuomba sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Nape ametuwekea booster pale Milo ya TBC lakini pale hakuna umeme. Nimshukuru Meneja wa TANESCO, Mkoa wa Njombe ameshawasilisha kwenye bajeti hii na ndiyo maana naunga mkono hoja kwa sababu kuna fedha nimeona zinakuja jimboni kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja, naomba tu changamoto zote za Jimbo la Ludewa ziweze kutatuliwa na kukatika kwa umeme kuweze kuisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma wa Mwaka 2023.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kuwapongeza sana wezetu wa Serikali, kwa kuona haja ya kuboresha Sheria hii ya Ununuzi wa Umma. Kwa sababu sheria ya mwanzo ilikuwa na mapungufu makubwa na tukijua kwamba asilimia 70 ya bajeti ya nchi yetu inaenda eneo la ununuzi wa umma. Kwa hiyo, kutokana na mapungufu ya sheria ya mwanzo ilikuwa inatoa mwanya kwa Serikali kupoteza fedha nyingi sana. Mara zote tumekuwa tukishuhudia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ikionesha ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi, upotevu wa fedha nyingi. Kwa hiyo sasa ile sheria ni ishara kwamba ilikuwa imeshashindwa kusimamia eneo hili la ununuzi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia huu Muswada wa sasa una ibara zipatazo 131 ambazo zote ukizisoma, unaona sasa zinakwenda kusimamia vizuri eneo hili la ununuzi na ugavi. Kama ambavyo taarifa ya upande wa Serikali na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti wameeleza ni kwamba sheria ya mwanzo ilikuwa haijasema mambo mengi sana kuhusiana na eneo la Ugavi. Hii ya sasa hivi ukiangalia utaona inakuja kuongeza uwezo wa sheria kusimamia sehemu ya ugavi na hata kwenye short title unaona pale eneo la ugavi limeweza kuongezwa. Kwa hiyo, ni jambo la kuipongeza sana Serikali kwa kuboresha sheria hii.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia utaona kifungu cha 64 cha sheria ya mwanzo, kilikuwa tu kimetoa tafsiri ya matumizi ya ile force account. Kule halmashauri kuna miradi mingi ambayo ilikuwa inatekelezwa kwa force account, sasa tumeona changamoto nyingi sana ambazo zilikuwa zinajitokeza kwenye force account. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna miradi mingine ilikuwa miradi mikubwa sana ambayo Serikali ilikuwa inatoa fedha kadri ya upatikanaji. Unakuta mradi wa Shilingi Bilioni sita, Shilingi Bilioni tano unawekwa kwenye force account na Serikali inatoa fedha kadri inavyokusanya, lakini kumbe miradi ile mikubwa akipewa Mkandarasi anafanya kwa fedha yake. Kwa hiyo, mradi unakamilika kwa wakati, wananchi wanaendelea kupata huduma wakati Serikali inaendelea kufanya malipo. Ile ya kusubiri Serikali mpaka ipeleke fedha ilikuwa inaleta changamoto nyingi.

Mheshimiwa Spika, hata uwezo wa baadhi ya wataalam wetu kusimamia hii miradi ulikuwa upo chini sana. Kwa hiyo, unakuta kuna halmashauri nyingine zilikuwa hazina wale watu wa kuandaa ule mchanganuo wa gharama za ujenzi, wakadiriaji majenzi, hamna wahandisi. Kwa hiyo, unakuta mradi mkubwa wanapewa watu ambao uwezo wao kitaaluma upo chini, lakini kwa sheria hii utaona hapa inamwelekeza Waziri mwenye dhamana kuja na kanuni ambazo zitatoa mwongozo sasa, kwamba ni miradi ipi iweze kutekelezwa kwa hii force account na miradi ipi iweze kwenda kwa wakandarasi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nafikiri hii itaongeza sana ufanisi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Ukiangalia hata kule vijijini ambapo miradi ya madarasa ipo, vituo vya afya na zahanati, wapo vilevile mafundi wale wenyeji kule ambao nao walikuwa wanaweza wakapata kipato kupitia hii force account. Serikali imeweka utaratibu wa kutambua wale wenye ujuzi na kuwapa vyeti. Kwa hiyo wakitambuliwa wale mafundi ambao ni wazoefu wanafanya kazi, kwa sababu nayo ni namna ya kupeleka ajira kwa wananchi, kwa hiyo fedha ndogondogo zitakuwa zinabaki kwa wananchi katika maeneo yaleyale.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba hili pia Serikali liende sambamba na kutambua ujuzi na uwezo wa mafundi wale waliokuwa vijijini na kuwa na utaratibu maalum wa kuwapa mafunzo na ujuzi zaidi ili waweze kutekeleza hii miradi ya kutumia rasilimali za ndani, ambayo inajulikana kama force account.

Mheshimiwa Spika, tukiangalia ibara ya 75 ya muswada tunaona imeenda kuboresha kile kifungu cha 64 cha sheria ya mwanzo, imeweka utaratibu mzuri na mwongozo mzuri ambao utakwenda kuwarahisishia Maafisa Masuuli, kwanza kufuata hizi procedures ule utaratibu wa kutangaza zile kazi kuwapata watu wa kufanya kazi na hata usimamizi wake. Kwa sababu sheria imeeleza mambo mazuri.

Mheshimiwa Spika, vile vile ukisoma ibara ya 75, ibara ndogo ya nne inasema; “Kwa madhumuni ya kifungu kidogo cha kwanza, fundi maana yake ni fundi ujenzi ambaye ana ujuzi wa kitaaluma katika fani ya ujenzi ingawa hajasajiliwa na chombo kinachohusika na usajili wa wataalam wa ujenzi au ambaye hana ujuzi na maneno mengine yanaendelea.”

Kwa hiyo, vitu kama hivi vitaenda kutengeneza ajira kwa wananchi wanaozunguka hiyo miradi.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni ibara ya 63 ya Muswada ambao sasa unakuja kuwa sheria iwapo tutapitisha. Eneo hili linazungumzia kwamba kila Afisa Masuuli, aweze kutenga fedha kwa ajili ya vikundi vya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, eneo hili sasa kama kutakuwa na utekelezaji mzuri wa eneo hili la ibara ya 63, tunaona kwamba tutakwenda kutengeneza ajira kwenye jamii wakati miradi yetu vilevile tunaendelea kuitekeleza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutakuwa tu tunasimamia ubora wa kazi, lakini sio fedha zote zitakwenda maeneo mengine na watu wetu wanaweza kupata ajira. Nitatoa mfano watu wa TARURA kule jimboni kwangu wana vikundi vya akinamama zaidi ya 15 na vikundi vya vijana vilevile na tayari wameweza kuwapa mafunzo, kazi ndogo ndogo za ukandarasi, kama kufyeka line ya TANESCO. Vikundi hivi vidogo vidogo wanaweza siyo kazi zote zinahitaji uandisi au ujuzi wa hali ya juu sana. Kufyeka barabara kwenye kazi za TANROADS, siyo lazima wakandarasi wakubwa. Kwa hiyo, vikundi vya vijana wanaweza wakapewa hizo zabuni wakasimamia na wakafanya kazi. Kwa hiyo, sheria hii imekuja kuweka vizuri sana eneo hilo na ndiyo sababu na mimi pia naunga mkono hoja hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia lengo la hii sheria ni zuri sana. Kwa hiyo, imekuja kuboresha sasa kasoro ambazo zilikuwepo kwenye ile Sheria ya Ununuzi ya mwanzo na vilevile kuna eneo linazungumzia matumizi ya mifumo, tuliona takwimu zinaonyesha kwamba sheria mpya ilisababisha kutokana na kuwa loose ni asilimia 18 tu ya kazi ndiyo ilitumika kwa kufuata mifumo, lakini asilimia kubwa zilikuwa zinafanyika manually. Kwa hiyo, sasa hili linakwenda pia kuhakikisha kwamba mifumo inayotumika katika ununuzi wa umma inaboreshwa na inasomana na mifumo mingine.

Mheshimiwa Spika, hii itaongeza sana ufanisi katika miradi, lakini vile vile itaongeza uwazi kwa sababu, mwananchi yeyote anaweza kuingia tu kwenye mfumo akapata taarifa. Vilevile itaokoa muda ambao mtu anautumia katika kuandaa nyaraka za zabuni, kuomba hizo kazi na tender mbalimbali. Kwa hiyo, muda utakuwa mchache, lakini hata gharama ile ya kuandaa makabrasha ambayo ni ya gharama kubwa kidogo ilikuwa inaweza ikaleta changamoto.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya mifumo nina imani yatakwenda kusimamiwa vizuri kwa sababu ni takwa la kisheria. Tutaondokana na ile hali ya kufanya mambo manually. Kwa hiyo, niipongeze sana Serikali kwa hatua hiyo na nasema kwamba naunga mkono sana.

Mheshimiwa Spika, vilevile ukiangalia hii sheria inakwenda kwenye eneo la ugavi, Serikali inakuwa na mali ambazo ni chakavu kama magari na bidhaa mbalimbali. Kwa hiyo, sasa namna ya kuziondoa zile kuzipeleka ilikuwa na urasimu sana, kwa sababu mwongozo wa kisheria haukukaa vizuri. Kwa hiyo sasa hili, inakwenda kurekebisha hiyo hali na kuhakikisha kwamba kunakuwa na ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, nitamke kwamba naunga mkono hoja na niwashawishi Wabunge wote tuweze kuiunga mkono sheria hii ili iweze kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)