Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ally Mohamed Kassinge (23 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nikushukuru kwa nafasi, lakini pia kwa sababu nachangia kwa mara ya kwanza, nami nitumie fursa hii kuanza kwa kumshukuru Allah Mwenyezi Mungu Subhanah Wataala, lakini pia kuishukuru familia yangu, wapigakura wangu wa Jimbo la Kilwa Kusini, pamoja na Chama changu Chama Cha Mapinduzi kilichonipa dhamana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo naanza kuchangia nikianzia na sekta ya viwanda. Sekta ya Viwanda katika nchi yetu ipo malighafi ambayo bado hatujaweza kuitumia na hapa nazungumzia malighafi ya gesi asilia. Katika Wilaya ya Kilwa eneo la Songosongo tunazalisha gesi pale ambayo inatumika kuzalisha umeme au kufua umeme, lakini mabaki yanayotokana na gesi asilia bado hayajaweza kutumika kwa ajili ya viwanda na hapa nazungumzia viwanda vya mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri kupitia Mpango huu Kiwanda cha Mbolea Kilwa Masoko kitakachotokana na malighafi ya gesi asilia kiingie katika Mpango huu tunaoenda kuutekeleza kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nije kwenye Sekta ya Kilimo; eneo mahususi ambalo tutawasaidia wakulima wetu ni kuhusianisha kilimo pamoja na Sekta ya Viwanda. Mosi, viwanda vya kuwawezesha wakulima wetu kupata mbolea kwa urahisi vianzishwe karibu na maeneo ambayo viwanda hivyo vitawasaidia wakulima kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyanda za Juu Kusini ambapo kwa kiwango kikubwa wenzetu ndiyo wakulima wakubwa wanaozalisha kwa ajili ya kulisha nchi na ziada mpaka tunaambiwa kwamba kuna chakula au mahindi yamebaki huko yamekosa soko, nashauri kupitia Mpango huu kuanzishwe kiwanda cha mbolea Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoani Njombe ambapo tayari wananchi wametoa eneo la kutosha. Kwa kufanya hivyo tutaweza kupunguza changamoto ya pembejeo ya mbolea katika msimu wa kilimo. Wizara ya Kilimo itakuwa inapunguza kazi ya kutoa bei elekezi kwa sababu ya mbolea inayotokana na sekta binafsi, tukianzisha kiwanda pale tutasaidia Mikoa ya Njombe, Mbeya, Iringa, Ruvuma na Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kuna eneo la sekta ya uvuvi, Mpango unaelezea suala zima la uvuvi katika kuanzisha bandari za uvuvi lakini hii iende sambamba na masoko ya samaki. Wilayani Kilwa hususani Kilwa Kivinje ni miongoni mwa maeneo ya uzalishaji mkubwa wa sekta hii ya uvuvi ikiwa ni pamoja na Mafia. Nashauri kupitia Mpango huu tuanzishe bandari za uvuvi Kilwa Masoko na Mafia na tuanzishe soko kubwa la samaki pale Kilwa Masoko kwa sababu nchi jirani na hususani Congo wanakuja kununua samaki tani kwa tani lakini Serikali hatujaweza bado kuratibu eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huu, naunga mkono Mpango huu na nashauri upitishwe kwa mujibu wa mapendekezo tunayoyatoa Wabunge hapa Bungeni. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa neema ya uzima hata nikapata nafasi ya kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Rais- TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutufanyia makubwa sisi wananchi wa Jimbo la Kilwa Kusini. Kupitia TARURA, tumeweza kuongezewa fedha za barabara kutoka wastani wa shilingi milioni 500 kwa mwaka mpaka wastani wa shilingi bilioni 1.5 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ongezeko la bajeti ya barabara tumeweza kujenga barabara kwa kiwango cha changarawe ili angalau zipitike kipindi kirefu cha mwaka. Kwa kutolea mfano wa barabara hizo ni kama vile Hoteli Tatu – Pande – Lihimalyao; Naiwanga - Likawage na Kikole - Mitole. Aidha, tumeweza kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Lumumba hadi Mnazi Mmoja kiasi cha kilometa 0.7 pale Kilwa Masoko. Napendekeza barabara hii iongezewe fedha kwa mwaka huu wa 2023/2024 ili ifike Kilwa Sekondari kwa kiwango cha lami. Napendekeza pia barabara ya Dodoma One (Dodoli) iunganishwe na barabara hii ya Sekondari.

Mheshimiwa Spika, tunaomba bajeti ya TARURA iongezwe ili kuendelea kukarabati barabara zetu ili zipitike kipindi kirefu cha mwaka.

Mheshimiwa Spika, tunashukuru kwa upande wa Hospitali yetu ya Wilaya ya Kinyonga tumeweza kupatiwa jengo la dharura na kupokea fedha shilingi milioni 900 kwa ajili ya kujenga maabara, jengo la upasuaji na x-ray. Tunaomba kuongezewa fedha kwa bajeti hii ili kujenga uzio na kukarabati wodi.

Mheshimiwa Spika, niombe kupitia bajeti hii Kata za Likawage na Lihimalyao ziweze kujengewa vituo vya afya kwani ni kata za pembezoni na ziko mbali kutoka maeneo ya vituo vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, tunashukuru kwa kupata Shule ya Sekondari Ngome pale Kilwa Masoko kupitia Mpango wa SEQUIP. Tunaomba Serikali ikamilishe shilingi milioni 130 zilizobaki ili kukamilisha miundombinu katika shule hii. Tunaomba mpango huu uendelee kwa kujengewa shule ya sekondari katika eneo la Singino, Kata ya Kivinje - Singino ili kupunguza mrundikano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Kivinje.

Mheshimiwa Spika, katika mpango wa Serikali kupeleka magari ya kusafirisha wagonjwa ambayo TAMISEMI itapeleka angalau gari moja kwa kila halmashauri, naomba Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ipatiwe magari mawili ili gari moja lipelekwe kwa ajili ya Kituo cha Afya Nanjirinji.

Mheshimiwa Spika, mwisho nitumie fursa hii kuipongeza Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kuanzia na Waziri wa Nchi Mheshimiwa Angellah Kairuki, Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Deo Ndejembi na Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange. Nimpongeze pia Katibu Mkuu na Naibu wote pamoja na Wakuu wa Mikoa akiwemo RC wangu Mheshimiwa Zainabu Telak. Nipongeze pia Wakuu wa Wilaya akiwemo DC wangu Mheshimiwa Christopher Ngubiagai na Mkurugenzi wangu Bwana Ngilangwa na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, kwa kweli wanachapa kazi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Nikianza kwa kumpongeza mwenye Ofisi yake kwa maana ya Mheshimiwa Rais. Pia, niwapongeze wanaomsaidia kwa maana ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene, tuna imani kubwa naye, Waziri senior na mjomba wangu Ridhiwani Kikwete tuna imani naye, ni mweledi katika eneo ambalo Mheshimiwa Rais amekupa majukumu hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipompongeza mtangulizi wa Mheshimiwa Simbachawene, Dada yangu Jenista Mhagama amefanya kazi ambayo imeacha legacy katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu ambao kwa kweli tunaikumbusha Serikali kuwafikiria wale ambao waliondolewa katika Utumishi wa Umma kwa sababu zisizokuwa na ulazima wowote, Mheshimiwa Jenista Mhagama amefanya kazi kubwa asilimia kubwa wamerudi, kwa sababu kauli ya Mheshimiwa Rais anasema kazi iendelee ninaomba Mheshimiwa Simbachawene endeleza pale ambapo Mheshimiwa Jenista ameachia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wachache ambao wamebaki wakiwemo wale ambao walikuwa na qualification za Darasa la Saba naomba Mheshimiwa Waziri shughulikia warudi katika Utumishi wa Umma kwa sababu ilikuwa ni haki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo mimi nianze na ajira. Wachangiaji wengi wamezungumzia katika mfumo ule wa Central Government kwa maana ya ajira ambazo zinafanywa na Sekretariati ya Ajira katika Utumishi wa Umma. Nianze na ajira ambazo zinafanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo kimsingi zimekasimiwa na Sekretariati ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira ambazo zinafanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ni za kisheria lakini sheria hiyo inawataka watu wa Sekretariati ya Ajira wasimamie mchakato wa mwenendo huu, lakini mimi nieleze masikitiko yangu kwamba usimamizi wa mchakato wa ajira unaofanywa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa unatuondolea imani sisi tunaotoka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, bado tunahisi kwamba kuna viashiria vya ubaguzi, kuna viashiria vya upendeleo na kuna viashiria vya kuonea watu wa Mamlaka za Serikali husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na case study kutoka katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Kilwa, michakato kadhaa ya ajira imefanyika, karibu mitatu nyuma kutoka sasa lakini hata wale wenye sifa za msingi wanaotoka katika Halmashauri za Wilaya ya Kilwa wamekosa kupata ajira kwa kisingoizio tu kwamba hawakufaulu mtihani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna jambo la kufanyia kazi Serikali na nitoe wito au ushauri kwa Serikali kwamba hebu tukachunguze ajira tatu zilizofanywa kwa mfululizo katika Halmashauri ya Kilwa kama zili-base on merit, kama sheria zilizingatiwa na kama weredi ulitumika katika mchakato wa ajira huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba watumishi wale ambao ni wakazi na wazawa wa Halmashauri wanapokuja katika mitihani ya practical wanafanya vizuri lakini inapokuja katika theory wanaonekana wamefeli, watumishi wanotoka nje ya Kilwa wanapokuja kwenye theory wanafanya vizuri kulikoni? Hii kama ni bahati mbaya kwa nini iwe ni bahati mbaya au by accident wa ajira tatu mfululizo hata mmoja hapati, hata wale watumishi ambao wamekuwa wakijitolea pale kwa mfano, hata kada ya madereva tu wanakosa ajira sifa za msingi wanazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo la kufanyia kazi Serikali. Nimetoa ushauri kwamba likafanyiwe kazi kabla sisi Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa maana mimi Diwani mmojawapo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa na Madiwani wenzangu hatujachukua hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nije katika stahiki za Watumishi. Hapa nitazumzia watumishi waliopo katika Utumishi wa Umma na Wastaafu. Pamoja na juhudi ambazo Serikali imeendelea kuzifanya lakini bado katika eneo la matibabu, masomo likizo malimbikizo ya mishahara na disturbance allowance kwa wastaafu bado imekuwa ni kizungumkuti katika kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanapata stahiki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano kwa kadhia ambayo imekuwa ikiwakumba wastaafu. Ninayo orodha ya wastaafu waliostaafu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa tangu mwaka 2018 mpaka leo, ninasikitika kusema kwamba hawajalipwa mafao yao ya kustaafu kulikoni? Nikiwataja kwa uchache wao hapa angalau kwa mfano tu, kuna Mwalimu Mstaafu Omari Mcheula kuna Mwalimu Mstaafu Khadija Bungurumo kuna Mwalimu Mstaafu Salma Kaisi tangu 2018 mpaka leo hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha wakati wengine hebu tuuvae uhusika, just imagine kwamba ni wewe ndiyo umetumikia nchi hii kwa weledi kwa mapenzi makubwa tangu 2018 umestaafu mpaka leo hujalipwa, hii ni kadhia lazima Serikali ifanye jambo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo niseme tu kwamba Mifuko ya Pensheni na hapo kwa upeke yake nauzungumzia mfuko wa PSSSF umekuwa ukichelewesha mafao ya watumishi wastaafu, hebu Serikali ichukue hatua katika eneo hili. Mstaafu anastaafu miaka mitano nyuma anakaa tu anahangaikia tu, hili kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nije katika suala la madaraja. Ninashukuru Serikali ya Awamu ya Sita imeweza kupandisha madaraja watumishi lakini kitu ambacho ninaomba kuikumbusha Serikali ni kwamba zoezi hili halikufanyika kwa umakini tulioutarajia. Kilichofanyika ni kwamba watumishi ambao pengine kwa miaka mitano na kidogo hivi hawakupandishwa vyeo wakapandishwa kwa mkupuo, tafsiri yake ni kwamba kwenye eneo la utumishi wa umma tunakosa ile dhana ya seniority, mtumishi ambaye alikuwa wa kwanza kuajiriwa anajikuta yuko daraja moja na aliyefuatia kuajiriwa, hii itakuja kuleta athari kwenye utaratibu wa kustaafu na kwenye taratibu za mafao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ushauri pamoja na kwamba Serikali imefanyia kazi eneo hili, ushauri wangu ni kwamba ikafanye review ya taratibu zote za upandishaji wa madaraja ili kila mtumishi akae kwenye daraja lake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nizungumie suala la motisha kwa Walimu. Huko nyuma tulikuwa na kitu ambacho kwa Walimu kilikuwa kinaitwa teaching allowance haitolewi kwa nini Serikali imeondoa teaching allowance, nadhani Serikali ambayo ilikuwepo wakati huo iliweka teaching allowance kwa Walimu kwa kuzingatia uzito wa jukumu la kazi ya ualimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nikumbushe tu kwamba mwalimu pamoja na kufundisha, ambapo watu wengi tunadhani kwamba kazi yake ni kufundisha tu, ana kazi kubwa ya kuandaa mpango mzima wa ufundishaji wa mwaka au muhula mzima ambao kiualimu unaitwa scheme of work, lakini mwalimu anajukumu la kuandaa lesson plan, mwalimu ana jukumu la kuandaa teaching aid, utaona walimu kama watatu hivi wanacheza wanaandaa midoli, midoli hivi ndiyo kazi ya Mwalimu na anaifanya nje ya muda wa kazi. Walimu wana kazi ya kuandaa lesson plan na sasa hivi wameongezewa kitu kinachoitwa KPI. Hii load kubwa yote kwa nini Mwalimu asilipwe teaching allowance wakati watumishi wengine wanalipwa kitu kinachoitwa responsibility allowance, ration allowance, on call allowance kwa nini Mwalimu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalizungumza hili kwa masikitiko makubw,a tutunze heshima ya Walimu katika nchi hii, viongozi wengi wakubwa katika nchi hili wamekuwa ni walimu, kwanini hatumheshimu Mwalimu? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wengi wakubwa katika nchi hii wamekuwa ni walimu, Baba wa Taifa ni Mwalimu, Mzee Alli Hassan Mwinyi ni Mwalimu, Hayati Magufuli ni Mwalimu, Waziri Mkuu wa sasa hivi Kassim Majaliwa ni Mwalimu, kwa nini hatutunzi heshima ya Walimu? Spika wa Bunge ni Mwalimu, tutunze heshima ya walimu kwa kuhakikisha kwamba walimu tunawatendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbushwa hapa kwamba Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ni Mwalimu, pia nakumbushwa kwamba Waziri wa Elimu ni Mwalimu, nakumbushwa pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu mwingine ni mwalimu, sasa Ndugu zangu ni kwa nini hatuwatendei haki walimu, rudisheni teaching allowance kwa walimu. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya masuala ya kwamba performance na nini na nini hayana mpango wowote, muwezeshe mwalimu, toa motisha kwa walimu, elimu itapanda katika nchi hii. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza haya kwa masikitiko makubwa, nimesahau hata Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, ndugu yangu Mheshimiwa Jumanne Abdallah Sagini ni mwalimu. (Kicheko/Makofi)

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ally Kassinge muda wako ulikuwa umekwisha lakini kwa mamlaka niliyonayo nakuongeza dakika nyingine moja ili uweze kumalizia na pengine ufahamu pia na Kiongozi wa Muhimili huu pia ni mwalimu. (Makofi)

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ushauri wa bure na wa nia njema, hatuzungumzi kwa namna ya kufurahisha Bunge lakini ni ushauri wa bure na wa nia njema, hebu tutunze hali ya mwalimu katika nchi hii, turudishe teaching allowance kwa walimu. Ufaulu utaongezeka kwa kumwezesha na kumpa motisha Mwalimu na siyo vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kuniongezea muda na wewe utawekwa katika alama ya kumbukumbu kwamba ulimwongezea muda Mbunge anayechangia hotuba hii kwa kuhakikisha kwamba walimu wanapewa fursa ya kusikilizwa na haya yakifanyika tutakuweka katika kumbukumbu, wekeni alama Mheshimiwa Simbachawene, Mheshimiwa Waziri wa Elimu wekeni alama kwa kuhakikisha kwamba mnarudisha motisha kwa kwa Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi/Vigelegele)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE: ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi asubuhi ya leo ili nami niweze kuchangia hoja ya Waziri wa Fedha na Mipango inayohusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka uliopita Mpango wa Maendeleo kwa mwaka ujao lakini pia Mpango wa Mapato na Matumizi kwa mwaka ujao wa fedha wa 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze sana Wizara ya Fedha kwa kuja na mpango na bajeti ambayo inakwenda kugusa matarajio ya Watanzania. Bajeti ya mwaka huu tutakayoipitisha ni bajeti ambayo imezingatia kwa ukamilifu wake masuala ya maendeleo na ya huduma za jamii pongezi sana Wizara ya Fedha na Mipango. Wakati unatuletea mpango huu pamoja na mambo mengine tulizingatia Mpango wa Tatu wa Maendeleo ambao tuliupitisha hapa Bungeni. Mpango huo wa Tatu wa Maendeleo pamoja na mambo mengine ulikuja na mikakati ya kuhakikisha kwamba tunajenga bandari za uvuvi katika maeneo yetu ya mwambao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru sana Serikali kwamba katika eneo hili tumeanza na Kilwa, na ninayoheshima kutoa taarifa kwamba mkataba wa kujenga bandari ya uvuvi pale Kilwa Masoko umesainiwa na tayari mkandarasi wa kutoka China ameanza kuoneshwa eneo la kufanyakazi. Hii ni faraja kubwa sana kwa Tanzania kwa ujumla wake lakini kwawana Kilwa kwa upekee wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo la bandari pamoja na mambo mengine ambayo Wizara ya Uvuvi na Mifugo imejiandaa ninayo ya kupendekeza. Jambo la kwanza ujenzi wa bandari ya uvuvi uendane na uwepo wa miundombinu mingine rafiki au taasisi zingine rafiki zitakazoendosha au zitakazowezesha bandari ya uvuvi kufanyakazi vizuri. Taasisi au miundombinu hiyo ni pamoja na hizi zifuatazo: -

Jambo la kwanza tunapendekeza chuo cha uvuvi kijengwe pale Kilwa Masoko ili bandari ya uvuvi na masuala ya kuelimisha watu masuala ya uvuvi yawe maeneo hayo hayo ya karibu. (Makofi)

Jambo la pili; tunapendekeza kwamba miundombinu ya barabara ya uhakika kutoka Bandarini Kilwa Masoko pale mpaka Nangurukuru kwenye Barabara Kuu (highway) ya Dar es Salam mpaka Mikoa ya Kusini ya Lindi Mtwara na Ruvuma iimarishwe ili iendane na mahitaji na kukidhi haja ya bandari ambayo tunakuja kuijenga. (Makofi)

Suala la tatu ambalo tunapendekeza; nimepitia mpango wa Wizara ya Uvuvi katika ujenzi wa bandari hii na nimeona kwamba tutajenga Soko la Uvuvi pale Kilwa Masoko. Mapendekezo yangu ni kwamba pale Kilwa Masoko tujenge kituo cha kukusanyia samaki au mazao ya bahari, badala yake soko la samaki likajengwe Kilwa Kivinje ambako kuna fursa za kutosha na kuna wadau wengi wachuuzi wengi, wavuvi wengi pale Kilwa Kivinje ambao ni mji jirani na Kilwa Masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne katika mapendekezo haya nipendekeze kwamba Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko uimarishwe na ujengwe katika viwango vya kukidhi matakwa ya kimataifa. Hi ni kwa sababu sasa tunapojenga bandari ya uvuvi maana yake ni kwamba tunakuja kufungua fursa za kimataifa. Hatuwezi kufungua fursa za kimataifa kwa uwanja wa ndege tulionao sasa hivi ambao ni wavumbi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulikuwa na mpango wa kujenga uwanja huu wa ndege kwa kiwango cha changarawe. Uwanja huu unamita 1,800, Serikali imeweka changarawe mita 1,000 tu bado mita 800. Sasa niseme kwamba mita 800 zile zimaliziwe lakini tuwe na mpango sasa wa kujenga Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tuendane na kwenda kuwalipa fidia. Kulikuwa na mpango wa muda mrefu, na ninaomba niukumbushe hapa; upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko ambapo wakazi wengi maeneo ya mashamba pamoja na nyumba zao zimewekewa alama, kwamba zitabomolewa ili kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wakalipwa fidia na utekelezaji wa uwanja huu uanze mara moja kadri ambavyo Serikali itakuwa imejipanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoka kwenye eneo hilo la masuala ya uvuvi na miundombinu yake rafiki nije katika eneo la menejimenti ya utumishi wa umma, usimamizi wa utumishi wa umma. Utumishi wa umma usimamizi wake unaanzia katika mchakato wa ajira mpaka mtumishi anastaafu. Hata hivyo kwa experience ambayo imejitokeza tokeza tumeona kwamba watumishi wa umma hawako katika hali ya kufurahi sana; kuanzia ajira zao mpaka ukomo wa ajira wanaishi maisha yaliyo ya mashaka mashaka kutokana kutosimamia vyema eneo hili la utumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano eneo la pension kwa watumishi wa umma hivi tunavyozungumza bado kuna watumishi hawajalipwa mafao yao ya pension ilhali wamestaafu miaka miwili, miaka mitatu bado hawajalipwa. Vilevile kuna eneo la usafirishaji wa mizigo mtumishi baada ya kustaafu. Wapo watumishi wamestaafu miaka mitatu sasa, miaka minne bado hawajalipwa. Niikumbushe Serikali kwamba mwaka 2008, 2009 mpaka 2010 Ofisi ya Rais, Menajimenti ya Utumishi wa Umma ilikuwa na zoezi la kusafisha taarifa za watumishi maarufu kama data cleaning ili watumishi wenye sifa waweze kuwepo katika utumishi na taarifa zao zikawe sawa katika utaratibu wa kimtandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika dhana hiyohiyo ya kusafisha taarifa za watumishi data cleaning niombe sasa Serikali ijisafishe yenyewe kwa kuhakikisha kwamba watumishi hawaidai Serikali yao. Sambamba na hilo kwenye eneo hilo la usimamizi wa menejimenti ya utumishi wa umma nigusie kidogo masuala ya uteuzi na utenguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uteuzi katika eneo hili uko wa namna mbili; wapo wanaoteuliwa kupata nafasi za uteuzi ndani ya utumishi wa umma, lakini wapo wanaopata nafasi nje ya utumishi wa umma. Niiombe Serikali kwamba treatment za makundi mawili haya zisiwe sawasawa. Kwa vyovyote vile mtumishi wa umma anapoteuliwa kwenye nafasi ya utumishi maana yake ametoka kwenye ajira anakwenda kule kwa mkataba utumishi wake huku haujakoma na sheria ndiyo inaelekeza hivyo tofauti na yule ambayo ameteuliwa nje ya utumishi wa umma ambaye anakwenda kwenye mkataba, ukiisha mkataba wake inakuwa basi atarudi kwenye shughuli ambayo alikuwa akiifanya awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mtumishi wa umma anapoteuliwa baadaye mkataba wake wa uteuzi au mamlaka ya uteuzi ikasema kwamba sasa inatosha halafu anaachwa arudishwi kwenye majukumu yake hili lazima tulizungumze kwa masikitiko; kwasababu limetokea, watumishi wameathirika sana kisaikolojia na familia zimeathirika. Hata hivyo, nilishukuru sana, dada yangu Jenista alivyoingia tu katika Wizara hii jambo la kwanza kushughulikia ni kurudisha watumishi wote ambao walikuwa na sifa za kurudi kazini; ahsante sana Mheshimiwa Jenista. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika dhana hiyo hiyo ya kufanya data cleaning, niiombe Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma, ifanye data cleaning kwa kuhakikisha kwamba watumishi waliobakibaki wale waliokuwa Ma-DAS, Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Wilaya lakini walitoka kwenye utumishi wa umma, mamlaka ya uteuzi ikasema sasa inatosha wapo wachache wamebaki Wizara izingatie ifanye data cleaning kuhakikisha wale waliobaki wanarudi katika utumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la watumishi walioteuliwa utakapokoma muda wao wa uteuzi kushushwa; hili limezungumzwa na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba Dkt. katika hotuba yake ya bajeti. Niikumbushe Serikali, kwamba utumishi wa umma unazingatia haya yafuatayo; Sera ya Menejiment na Ajira ya Mwaka 1999, Sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2002 na mabadiliko yake, Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003, Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009, Kanuni za Utendaji Bora, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini na miongozo mbalimbali inayoongoza utumishi wa umma. Kama hivyo ndivyo Serikali tunakwama wapi? Sheria hizi, miongozo hii tuliitengeneza wenyewe, tulitunga wenyewe, kwanini hatuzingatii hizi taratibu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumishi anapoteuliwa kwenye nafasi ya uteuzi aidha alikuwa afisa daraja la kwanza, afisa mwandamizi, au afisa mkuu, anapopata barua yake ya uteuzi inasema kwamba yahusu kuteuliwa na kupandishwa cheo kuwa... Sasa unapomteua na kumpandisha cheo maana yake ni kwamba unamtoa katika daraja lile na kwa maana hiyo maslahi anayopata ikiwa ni pamoja na mshahara ni kwa sababu ulimteua na kumpandisha cheo. Utumishi au uteuzi wake unapokoma nafasi yake ya kupandishwa cheo ndiyo inayomfanya abaki na mshahara huo wa nafasi aliyoteuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, kwa dhati kabisa ninapendekeza kwamba watumishi hawa wanaoteuliwa pindi wanapotenguliwa wasishushwe mishahara yao kwa sababu wamepandishwa cheo; na kupandishwa cheo ndugu zangu siyo adhabu, kupandishwa cheo ni tija na ni faraja na niheshima inakuwaje mtu anayepandishwa cheo baadaye unamvunjia ile heshima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri sana Serikali eneo hili mpango wake wa kuwashusha mishahara watumishi waliotumbuliwa isiendelee nao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kwanza kukushukuru binafsi kwa kuniona. Pili, kushukuru kwa hotuba nzuri ya Wizara ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ikiwa ni sambamba…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge tusikilizane, huyu anayeongea ndiye aliyechukua Jimbo la yule Mbunge ambaye alikuwa anajiita Bwege. Sasa mbadala wake ni Mheshimiwa Kassinge, karibu sana hiyo ndiyo bunduki mpya ya CCM. (Makofi)

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, niendelee kupongeza Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa mawasilisho ya hotuba ya bajeti, lakini kwa kuaminiwa na mamlaka katika timu zote kuanzia Mheshimiwa Waziri na Wasaidizi wake, lakini pia Katibu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo langu la kwanza la uchangiaji ni kuishauri Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuja na sera ya ugatuaji ili maeneo ya mgawanyo wa madaraka katika maeneo yote ya siasa, utawala, fedha yabainike baina ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, katika eneo la mapato ya halmashauri, kuna eneo la mapato ya ushuru wa mazao produce cess. Ushuru huu umekuwa ukitofautiana kati ya halmashauri moja na halmashauri nyingine. Niishauri Ofisi ya Rais, TAMISEMI iweze ku-harmonies ili ushuru huu uwe sawa na halmashauri zote na kuondoa mgogoro au mgongano ikiwa ni sambamba na kurudisha asilimia tano ya ushuru wa mazao badala ya asilimia tatu ya sasa hivi, kwa sababu utafiti umebainisha kwamba wanaochangia halmashauri katika ushuru huo wa mazao asilimia tatu ni wanunuzi na si wakulima.

Mheshimiwa Spika, pili, kuna eneo hili la property tax ambalo baadhi ya Wabunge hapa wamelizungumzia. Kimsingi hili ni eneo la ushuru au mapato ya Local Authority, lakini hali ilivyo sasa hivi inakusanywa na halmashauri lakini ina hesabika kuwa ni mapato ya Serikali Kuu. Nishauri eneo hili lirudishwe halmashauri na hayo ni mapato ya halmashauri ili zikajenge barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna ushuru wa halmashauri wa kimazoea (traditional) wa siku nyingi, ushuru mdogo mdogo wa wajasiriamali, wauza vitumbua, wauza mahindi ya kuchoma na kadhalika.

Lengo la Serikali kutoa vitambulisho kwa wajasiriamali lilikuwa ni lengo zuri na kazi hii inafanywa vizuri na Watendaji wa Halmashauri kukusanya fedha kupitia vitambulisho 20,000 kwa mwaka, lakini mapato yanahesabika si mapato ya halmashari bali ni mapato ya Serikali Kuu, yanakwenda Hazina moja kwa moja. Niishauri Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Serikali kwa ujumla, mapato yanayotokana na wajasiriamali wadogo wadogo yarudi halmashauri yakajenge barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kushauri masuala ya kisera sasa nije katika eneo langu la uongozi na uwakilishi kwa maana ya changamoto zilizopo katika Jimbo la Kilwa Kusini, nikianza na eneo la barabara zinazohudumiwa na TARURA. Naomba hapa nitoe takwimu; kuanzia mwaka 2017/2018 – 2019/2020, Halmashauri ya Kilwa imekuwa ikipata fedha za barabara billioni moja plus kidogo hivi, lakini kuanzia 2021 imekuwa ikishuka ni mpaka kufikia Sh.984,000,000 na hali hii imeendelea kushuka mpaka bajeti hii tuliyonayo. Kwa hali halisi ya urefu wa barabara za Kilwa ambazo ni zaidi ya kilomita 1,000, Sh.984,000,000 hazitoshi.

Mheshimiwa Spika, nashauri tuongeze bajeti hii ili ikahudumie barabara zile. Hapa naomba nizungumze barabara mahsusi na naomba hizi zipewe kipaumbele. Barabara ya kutoka Hoteli Tatu - Pande, Hoteli Tatu – Lihimalyao, sisi Wanakilwa hii ni barabara ya kimkakati inaenda kuhudumia wakazi wapatao 30,000 ambao ni wazalishaji wakubwa wa korosho, kwa hiyo itakuwa ni barabara ambayo itajenga uchumi katika eneo hili. Nishauri kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, barabara isiingie katika utaratibu wa maintenance, badala yake iingie katika utaratibu wa development na itengewe fedha za kutosha ili ipitike kipindi chote cha mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho Sekta ya Afya. Hospitali yetu ya Wilaya ya Kilwa imechakaa vya kutosha…

SPIKA: Kengele imeshagonga. Ahsante sana Mheshimiwa Kassinge.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Kwa hiyo tunaomba hospitali ikarabatiwe, kama si kujenga hospitali mpya.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fadhili zake kuu na neema zake za kila namna. Mwenyezi Mungu ambaye ametujaalia pumzi hata tukapta fursa ya kujadili Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyopeleka fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii pia kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mheshimiwa Dkt. Selemani Jafo kwa namna anavyoingoza Wizara hii akisaidiana na Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kupongeza Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), kwa kuja na mpango wa kujenga kuta katika maeneo yetu ya mwambao na katika visiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe mpango huu uwe endelevu na uangalie maeneo mbalimbali ya pwani ya nchi yetu. Niiombe Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ifikirie kujenga ukuta ili kuzuia athari za kimazingira katika Mji Mkongwe wa Kilwa Kivinje ambao ulijengwa tangu wakati wa utawala wa kikoloni na sasa umebomoka. Kwa kufanya hivi tutaweza kuhifadhi ardhi ya mji huu na kufanya makazi ya watu, taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, maeneo ya biashara na viwanda vilivyopo katika Mji wa Kilwa Kivinje, kuwa salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nianze kwa kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Lakini kwa upekee nianze kutambua changamoto za watumishi hususani kundi la walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, walimu ni sehemu ya watumishi katika nchi hii lakini kama tunawasikiliza vizuri inaweza ikawa ni miongoni mwa kundi lenye changamoto nyingi zaidi ikiwemo kama ambavyo Wabunge wengine wamechangia kucheleweshwa kupandishwa kwa madaraja ikiwemo mapunjo baada ya kustaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nina case study mbili naomba nizitaje; katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, kuna mwalimu anaitwa Mwalimu Hadija Salum Bugurumo alistaafu mwaka 2020; alistaafu akiwa na Daraja F, mshahara aliolipwa ni wa Daraja E, na kwa maana hiyo anadai mapunjo. Pia kuna mwalimu anaitwa Mwalimu Salma Khamis Kaisi, naye kadhalika alistaafu mwaka 2020 lakini alipandishwa daraja tangu mwaka 2017 na amelipwa mafao yake ya kustaafu kwa mapunjo bado wanaidai Serikali mpaka leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa hawa ni walimu wangu ambao wamenifundisha mimi shule ya msingi Mnazi Mmoja, Kilwa Masoko na wamesema mwanangu, mwanangu katusaidie kutusemea huko na hapa nawasemea, Serikali iwasikie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo pia, kama ambavyo Wabunge wengine wamechangia kumekuwa na changamoto kubwa sana ya kupewa gharama za kusafirisha mizigo baada ya kustaafu. Walimu wangu wawili hawa ambao nimewataja kwa mfano tu kwa niaba ya wengine walio wengi nao pia wanakumbwa na kadhai hii hawajalipwa mizigo ya kustaafu bado. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya eneo hilo, nizungumzie pia mazingira ya ufundishaji kwa walimu. Kada zingine hapa Tanzania kumekuwa na namna fulani fulani hivi ya kufikiriwa kimotisha motisha zipo kada ambazo wanalipwa kinachoitwa ration allowance, zipo kada wanalipwa on call allowance kwa maana ya kada ya sekta ya afya, ambayo hiyo on call allowance kwa sababu ya ule muda wa ziada mtumishi wa sekta ya afya anapoitwa kwa ajili ya kwenda kutoa huduma. Lakini walimu hawajafikiriwa, huko nyuma tulipata kuambiwa kwamba kulikuwa na kitu kinachoitwa teaching allowance na hii ilizingatia mazingira ya walimu yalivyokuwa magumu katika kuandaa somo lenyewe, kufundisha na kufuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ualimu hauishii kufundisha tu darasani unaandaa scheme of work ya mwaka mzima kama si kwa muhula mzima, ukitoka hapo unaanda lesson plan, ukitoka hapo unaandaa lesson notes, ukitoka hapo unasahihisha kazi na kufuatilia mwafunzi mmoja baada ya mwingine, lakini pia work load ni kubwa. Mwalimu anatakiwa afundishwe wanafunzi 40 mpaka 45 kwa darasa moja. Walimu wetu hawa wanafundisha wanafunzi mpaka 200 kwa darasa moja hii ni work load kubwa wafikiriwe na wao kupata teaching allowance wapate motisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la watumishi nitumie lugha kwamba wametelekezwa, hawa walikuwa ni watumishi waandamizi wakapata nafasi za kuteuliwa na mamlaka zao, mamlaka zao za uteuzi baada ya kuwaacha katika nafasi hizo hawajarudishwa bado katika utumishi wa umma na ndio maana nimetumia lugha ya wametelekezwa. (Makofi)

Naomba Ofisi ya Rais Utumishi iwafikirie watumishi hawa kwa sababu na wao ni watumishi kama watumishi wengine na wana haki ya kufikiriwa, hawajapata pension zao, hawajapata maslahi yao yoyote, wamebaki kama walivyo kama wakiwa ndani ya nchi yao, hii sio sawa Ofisi ya Rais iwafikirie hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niseme kwamba wale watumishi ambao walifikia nafasi za uteuzi kama vile Wakurugenzi, Ma-DAS na wengine na wakaingia katika mchakato wa uchaguzi, baadhi hawakutoka katika sekta nje ya utumishi wa umma tunafahamu ambao wametoka katika utumishi wa umma na bado wameendelea kutelekezwa miezi tisa kama wenzangu wamezungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa nina case study moja ya mtumishi ambaye alikuwa Mtendaji wa Kata Manispaa ya Kinondoni na baadae akawa DAS - Mbeya na baadae akaenda kugombea mpaka leo hajarudishwa katika utumishi wa umma. Tunaomba Serikali iwafikirie hawa ili tusiandae kundi kubwa la huko mbele ya safari ambao watakuwa ni wa kuipinga Serikali ambayo kwa kweli walihitumikia kwa uadilifu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi. Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, nitumie fursa hii kumpongeza mdogo wangu Mheshimiwa Nape Moses Nnauye kwa kuteuliwa na kuamini na Mheshimiwa Rais kuongoza Wizara hii ambayo kwa kweli Watanzania tuna Imani naye kubwa sana na nadhani ataendeleza pale ambapo rafiki yangu Dkt. Ndugulile aliachia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi, nianze kwa kushukuru Wizara. Jambo langu la kwanza nilipoingia Bungeni ilikuwa ni kuomba mawasiliano kupitia mnara katika Kata ya Likawage, nashukuru Serikali ya Mama Samia imetekeleza hili. Kupitia mchango wangu, niombe kama ambavyo niliomba katika Mkutano wa Sita uliopita kwamba mnara huu ambao umekamilika kule Likawage utakaohudumia Vijiji vya Nainokoli, Likawage pamoja na Liwiti, basi Mheshimiwa Waziri impendeze aende akazindue rasmi na wana wa Likawage wanamsubiri kwa hamu kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo wanasema kushukuru ni kuomba tena. Pamoja na hayo sisi Wanakilwa tunaendelea kuomba tena kwamba, mawasiliano haya ya njia ya simu bado ni changamoto katika Kata zetu za Nanjilinji, Chumo, Kandawale, Kinjumbi, Kipatimu pamoja na Kikole. Iwapendeze wenzetu wa Wizara hii ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika mpango huu wa 2022/2023, Kata nilizozitaja ziingie katika mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umahususi, niseme kwa masikitiko kidogo kwamba, katika Wizara hii eneo la Shirika la TBC, Wilaya ya Kilwa pekee katika Mkoa wa Lindi ndiyo ambao hatuna huduma ya TBC, wilaya nyingine zote zilizobaki wanapata huduma hii. Impendeze Mheshimiwa Waziri mdogo wangu Mheshimiwa Nape, awaelekeze watumishi wake, watendaji wenzake katika Serikali, katika Shirika hili la TBC na siye wana Kilwa tunahitaji kupata taarifa za Habari kupitia TBC FM, TBC Taifa na vyombo vingine vya TBC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nijikite katika ushauri. Tumeona mikakati ya Wizara kupitia taasisi zake zote nane ni mizuri sana. Hata hivyo, kwa upekee nishauri katika eneo hili la mawasiliano kwamba, kwa muda mrefu eneo la mawasiliano limeachiwa sekta binafsi. Imebainika hapa kwamba, muda si mrefu, Mungu akipenda tunapitisha bajeti ya kutosha, lakini pia bado tuna nafasi ya kukusanya makusanyo mengi kupitia taasisi za Wizara hii. Niwashauri Wizara kwamba eneo hili la mawasiliano libebwe na Wizara kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko kutegemea watoa huduma binafsi pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili niseme kabisa kwamba, Wizara itengeneze sera kama ilivyo katika Wizara zingine kwa mfano Wizara ya Maji, Sera mita 400 maji, mita 400 maji; na Wizara hii ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iweke sera kama ni kila kata ama kila kijiji ama kila umbali wa kilometa kadhaa kadri ambayo utafiti na usanifu utakavyofanywa na wataalam na kuja na hayo mapendekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa fadhili zake kuu. Pia nianze na nukuu, wakati nachangia Wizara hii ya Maji Maandiko Matakatifu ya Quran sura ya 21 aya ya 30 ambapo Mwenyezi Mungu anasema: “Wajaalna minalmaa- i kulashai-in-hayaa.” Tumejaalia kutokana na maji kuwa ndiyo chanzo cha uhai wa kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maandiko haya matakatifu tafsiri yake ni kwamba Wizara ambayo anaisimamia Mheshimiwa Jumaa Aweso na timu yake ndiyo uhai wetu sisi na viumbe vingine. Kwa maana hiyo, ni Wizara ambayo ni tegemeo kubwa la maisha yetu. (Makofi)


Mheshimiwa Spika, kwa spirit hiyo hiyo, mimi binafsi sina shaka kabisa na kiongozi wa Wizara hii Mheshimiwa Jumaa Aweso, sina shaka kabisa na Naibu Waziri, dada yangu Mheshimiwa Eng. Maryprisca, sina shaka na Katibu Mkuu, ndugu yangu Eng. Sanga; Naibu Katibu Mkuu pamoja na timu yote ya Wizara, wapo sawa sawa. Hata meneja wangu wa RUWASA katika Wilaya ya Kilwa Eng. Ramadhani Mabula yupo sawa sawa na tunakwenda naye vema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa imani tuliyojenga kwenu Wizara ya Maji, nitumie fursa hii kutoa ushauri ufuatao: kwamba kama ilivyo katika umeme, Wizara ya Nishati imekuwa na jukumu na juhudi za kutafuta vyanzo vya umeme kila angle na maji kadhalika mtafute vyanzo vya maji kila angle; katika chemichemi, katika mito, mabwawa, maziwa, maji ya ardhi kwa maana ya underground water na maji ya vyanzo vya asili.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili, niseme tu kwamba kuanzishwa kwa RUWASA miaka miwili iliyopita kumeleta matumaini makubwa kwa Watanzania, lakini ukiangalia mwenendo na utendaji kazi wa RUWASA ni kama vile unaleta tija zaidi kwenye miradi mikubwa mikubwa na hususan kwenye vyanzo vikubwa vya maji hasa Maziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule vijijini ambako hatutegemei sana kupata maji kutoka vyanzo vikuu, kidogo nitoe ushauri. Kuna Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA), miaka miwili iliyopita nahisi ufanisi wake wa kazi umepungua. Nadhani kuanzishwa kwa RUWASA umeifanya DDCA isiwe mamlaka kamili au wakala kamili, ni kama unit tu hivi ndani ya Wizara. Nashauri kupitia Bunge lako kwamba DDCA ipewe nguvu kamili. Ilikuwa na waatam wa kutosha, ilikuwa na mitambo ya kutosha. Tulikuwa tukiona magari yakipita na ma- drill yakipita na ma-compressor kwa ajili ya kwenda kuchimba visima vijijini.

Mheshimiwa Spika, Mbunge wa Itilima atakuwa mfano moja wapo wa kutoa ushuhuda huo, kuna visima vingi vimechimbwa na DDCA na ilikuwa na uwezo wa kuleta mapato takribani shilingi bilioni 12 kwa mwaka. Haya siyo mapato madogo. Tuitathmini miaka miwili iliyopita kwa mwaka 2021/2022 kiasi gani cha fedha kimepatikana kutoka wakala wa huu. Kimeweza kuchimba visima vingapi katika vijiji vyetu?

Mheshimiwa Spika, nashauri DDCA ipewe nguvu na mamlaka kamili, Wahandisi wale ambao walikuwa ni washauri wa kitaalam, wako wapi sasa hivi? Mitambo ile iko wapi na iko mingapi na inafanya kazi gani? Nitoe kama hadidu za rejea kwa Waziri akaifanyie kazi ikiwezekana aunde Tume au kikosi kazi mahsusi cha kutathmini utendaji kazi wa DDCA kama kuna upungufu uboreshwe kwa lengo la kusaidia hususan visima vijijini.

Mheshimiwa Spika, hapo hapo nikumbushe Wizara ya Maji; katika Wilaya ya Kilwa hususan Jimbo la Kilwa Kusini, tarehe 15 Septemba, 2009 aliyekuwa Waziri ya Maji wakati huo Mheshimiwa Mwandosya aliahidi kuchimba bwawa katika Kijiji cha Limaliyao, ambapo bwawa lile lingechimbwa lingeweza kusaidia upatikanaji wa maji kwa watu takribani 15,000. Naikumbusha Wizara ikafanyie kazi. Tangu agizo lile la Waziri, hakuna ambacho kimefanyika mpaka sasa.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Jumaa Aweso ndugu yangu, ninaimani na timu yake, atume wataalam wake wakafanyie kazi kutafuta eneo ambalo tunaweza tukapata bwawa kwa ajili ya maji ya Wana- Limaliyao, kwa sababu hawataweza kunufaika na mradi mkubwa wa maji kutoka chanzo chochote cha mto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati nikishauri hivyo pia, niendelee kuishukuru na kuipongeza Wizara. Nimeona kupitia kitabu cha bajeti kwamba katika vijiji vyangu kadhaa nitapata miradi ikiwepo Kilwa Kisiwani, nashukuru sana. Pia ikiwemo Likawage, nashukuru sana; pia ikiwemo na Kiu, nashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, ahadi yake ya kunisaidia kisima cha maji katika Kijiji cha Nainokwe, naomba itekelezwe kupitia mpango huu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, pia mpango ule wa miji 28, ukumbuke na Mji wa Kilwa Masoko na Mji wa kilwa Kivinje.

Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 49 na ukurasa wa 88 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia suala la migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Nipongeze Wizara kwa kutatua migogoro hii ambapo Mkoa wa Lindi imetatuliwa migogoro kumi. Aidha, kwa mpango wa mwaka 2022/2023, Wizara itaendelea kutatua migogoro husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kuwa Wizara ijikite kwenye kuzuia migogoro zaidi kuliko kusubiri itokee ndipo watatue. Ni vema Wizara ikafanya tathimini ya mifugo hitajika kila Mkoa au Wilaya na hatimaye kuweka mikakati ya kudhibiti kuongezeka kwa mifugo katika maeneo husika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. ALLY M. KISSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza rafiki yangu Dkt. Faustine Ndungulile kwa kuwa Mtanzania muasisi wa Wizara hii mpya ambapo Mheshimiwa Rais amemdhamini, amemuamini na kwa changamoto ambazo Wabunge tunazielezea katika Bunge lako Tukufu, naamini kabisa rafiki yangu Mheshimiwa Ndugulile ataweza kuitendea haki Wizara hii. Atasaidiana na timu yake Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote katika Wizara hii, tuna imani nanyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu la kwanza la mchango, ni kuishauri Serikali Wizara hii ya Mawasiliano Teknolojia na Habari kupitia taasisi yake ya TCRA. Kimsingi TCRA ni regulator, lakini Watanzania tunahitaji kufahamu ina regulate nini, masuala yote ambayo TCRA inadhibiti yafahamike. Kama ingelikuwa ni mpira tasnia ya kabumbu au kandanda maana yake ni kwamba TCRA ni referee na makampuni ya simu ndiyo timu wachezaji, sisi watumiaji ndiyo washangiliaji na washabiki. Tunataka tujue sisi washabiki nini TCRA ina regulate. Twende mbali zaidi ipendeze zaidi tufikie wakati kwamba sisi washangiliaji, watumiaji, tupate muda wa kupata forum ya kutoa maoni yetu kwa huyu regulator anayeitwa TCRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili gharama za simu. Huko nyuma tulikuwa tunatumia gharama za simu kwa utaratibu wa ukinunua Sh.1000 au Sh.2000 maana yake ndivyo utakavyotumia, lakini kumekuwa na utaratibu sasa wa kununua bando au vifurushi, imekuwa kana kwamba ni lazima ununue vifurushi, hivi utaratibu huu TCRA na Mheshimiwa Waziri wanasemaje, kwamba ni lazima Watanzania tulazimishwe kutumia simu kwa utaratibu wa vifurushi, usipohitaji vifurushi unataka utumie moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, bado kuna matatizo na tunahisi kwamba sisi wadau wa tasnia hii ya mawasiliano kuna kuibiwa kupitia utaratibu wa vifurushi. Kwa mfano, unakuta unajiunga kifurushi cha wiki au kifurushi cha siku cha saa 24, badala ya kutumia akiba yako kadiri ulivyoweka, muda ukifika wa saa 24 imekata, sasa hii iliyokatwa inakwenda wapi, hapa ndiyo ambapo tunamtaka regulator, TCRA asikilize maoni ya sisi wadau ambao ni watumiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa ushauri kwa Wizara hii, nianze sasa kuelezea changamoto ambazo zipo katika Jimbo langu la Kilwa Kusini lakini pia Jimbo la mwenzangu, jirani yangu ndugu yangu, Mheshimiwa Ndulane la Kilwa Kaskazini. Katika Wilaya ya Kilwa, wilaya yenye kata 23, kata 22 hazina uhakika wa mawasiliano. Nitumie fursa hii kumkumbusha rafiki yangu Mheshimiwa Dkt Ndungulile, nimefika ofisini kwake mara kadhaa kumkumbusha kwamba Likawage ambayo ni kilometa zaidi ya 110 kutoka Makao Makuu ya Wilaya hawana mawasiliano, kitu ambacho ni tishio kwa usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukumbuke kwamba Kata hii ya Likawage na Vijiji vyake vyote vitatu vya Likawage na Inoke na Liwiti, ni kata ambayo ipo katika eneo kubwa linazungukwa na Mbuga ya Selous. Wanapata shida ya kwenda kupiga simu mbali karibu na mpakani ukielekea Njinjo kule na usalama wa maisha yao unakuwa hatarini, tunapata shida kupata taarifa za dharura ikiwemo misiba, lakini shida kubwa ni suala la mtandao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alinipokea vizuri ofisini kwake na kupitia sasa katika mjadala wa bajeti yake, nimkumbushe ahadi yake ya kuhakikisha kwamba Wanalikawage wanapata mnara wana uhakika wa mawasiliano. Sambamba na hilo bado zipo kata zingine ambazo mawasiliano ni shida katika Wilaya ya Kilwa ikiwemo Kata ya Nanjilinji hususan Nakiu pamoja na Kigombo, lakini pia ikiwemo Kata ya Lihimalyao hususan Kisongo na maeneo ya Mabanda kule. Pia Kata ya Kandawale, Kipatimu, Miguruwe, Mitole, Kibata, Kinjumbi, Namayuni pamoja na Chumo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Wizara hii inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndungulile awatendee haki Watanzania wa Wilaya ya Kilwa kuhakikisha kwamba wanapata mawasiliano ya uhakika. Mbaya zaidi hata zile sehemu ambazo mawasiliano yanapatikana, uhakika wa 4G haupo. Kwa hiyo tunaomba kwamba minara hii sasa iongezewe nguvu ili watanzania wa Kilwa nao waishi kidigitali kama maeneo mengine ya mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nianze kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwanza kabisa kwa kupongeza uongozi wa Wizara ambao kwa ujumla umeanza kuleta matumaini mazuri kwa Watanzania hususan kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi. Kwa hiyo, nawashukuru na ninawapongeza sana viongozi kuanzia Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Makatibu Wakuu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi ambalo linatupa matumaini ni kwamba uongozi huu umejikita kwenye ubobezi wa sekta wanazosimamia. Ukiangalia Katibu Mkuu wa Uvuvi, amejikita katika masuala hayo, Katibu Mkuu wa Mifugo kadhalika ni mzoefu wa masuala hayo. Ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, Naibu Waziri ni mzoefu wa masuala hayo kitaaluma na pia kimakuzi. Kwa hiyo, Watanzania hatuna shaka katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo nataka kuanza kuchangia katika hotuba hii, kwanza kabisa ijitambue kwamba ni Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi na siyo Wizara ya Mifugo na Kukwaza Uvivu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hivi kwa sababu mengi ambayo wachangiaji wenzangu wamezungumza, niwarejeshe tu katika kanuni za mwaka 2020, kanuni ya 66(1)(d)(f)(g). Vifungu hivi vinakwaza kabisa maendeleo ya uvuvi katika nchi yetu ya Tanzania. Sihitaji nidadavue vinakwaza vipi? Bahati nzuri wachangiaji wenzangu waliotangulia wameelezea. Naomba katika mabadiliko ya kanuni Mheshimiwa Waziri anayokwenda kuyafanya, azingatie haya ambayo kwenye vifungu nivyovitaja yanakwanza uvuvi Tanzania. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba wataalam wa Sekta ya Uvuvi, wanapokwenda kutengeneza kanuni mpya, ziwe ni kanuni shirikishi na pia ziwe ni kanuni zinazoendana na mazingira husika. Kwa mfano, sisi watu wa Pwani, taratibu za uvuvi zinazingatia masuala ya nyakati, nyakati za pepo na miandamo ya miezi. Kwa mfano, unapokataza watu wasivue mchana kwa ujumla wake tu, wakati taratibu za uvuvi wa baharini zinazingatia mwandamo wa mwezi, kuna kipindi cha mwezi mchanga, kuna kipindi cha mwezi mpevu, kuna kipindi cha mwezi mwangavu, hilo lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuna hawa samaki maarufu kama Kambakochi au Kambamiti. Kule Kilwa ni tofauti na Rufiji ambapo Kilwa uvuvi wa Kambakochi unatakiwa uanzie mwezi Januari, lakini leseni ambazo Wizara inatoa inaanzia mwezi Aprili. Maana yake ni kwamba mpira unapigwa huku, golikipa anaangukia huku; tofauti kabisa. Hapa tunaomba izingatiwe pia, ndiyo maana tunasema kwamba sheria hizi na kanuni hizi ziiwe shirikishi, ziulize wazoefu wa maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninaomba ni kukuza Sekta ya Uvuvi na hususan katika Sekta ya Wilaya ya Kilwa, ni kuhakikisha kwamba pale Kilwa Kivinje ambapo nimejiridhisha kabisa samaki wengi ambao wanaliwa Tanzania wanatoka Kilwa; ukiona samaki wanaliwa Dar es Salaam wanatoka Kilwa, ukiona samaki wanaliwa mikoa mingine ya Kusini, wenzetu jirani zetu Mtwara na Ruvuma wanatoka Kilwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi wa hili wale ambao wanatumia barabara hii maarufu kama ya Kibiti - Lindi, ukifika pale Somanga, ukinunua samaki unakuja Dar es Salaam au unakwenda Mtwara au unakwenda Ruvuma maana yake hao ndiyo samaki wa Kilwa. Kama hivyo ndivyo, kuna haja ya kuanzisha soko la samaki la kisasa pale Kilwa Kivinje ili wavuvi wetu wawe na uhakika wa soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe taarifa tu kwenye Wizara hii, katika utaratibu usio rasmi jirani zetu wa Kongo wanakuja Kilwa kununua samaki tani za kutosha. Tumeandaa utaratibu gani wa kuingiza mapato ya Taifa kwa kuuza samaki nje ya nchi? Tuko katika utaratibu usiosimamiwa vizuri na Wizara. Nashauri katika eneo hili, Wizara isimamie inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri, matumizi ya nyavu zilizozuiliwa. Kimsingi nyavu hizi, wananchi wetu wavuvi hawa masikini wa Tanzania wanavua kulingana na aina ya samaki wanaovua. Kwa mfano, dagaa wote tunawafahamu, wanahitaji milimita kumi. Wote tunajua dagaa ni visamaki vidogo vidogo sana, vinahitaji milimita sita, ikizidi milimita saba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tangu kumetolewa zuio la kukataza zuio la kukataza uvuvi wa nyavu hizi, uvuvi wa mchana, wavuvi wetu wamebaki kuwa masikini, wamechomewa nyavu zao, wamechomewa vyombo vyao, vimeangamizwa, hii ni msiba mkubwa katika Taifa hili na siyo haki kufanya katika nchi ambayo iko huru. Malengo na matarajio ya Watanzania ni kuona kwamba kila sekta inasaidia wahusika. Kama ni Sekta ya Kulima isaidie wakulima, Sekta ya Uvuvi isaidie wavuvi, Sekta ya Ufugaji isaidie wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sihitaji nizungumzie kilio cha Wana-Kilwa cha kuchomewa nyavu zao, kuangamiziwa vyombo vyao vya uvuvi, kilichofanywa huko na Waziri ambaye amemaliza muda wake. Nina matarajio mazuri na Mheshimiwa Waziri wewe kaka yangu, hautafanya kama mwenzako aliyekutangulia. Utakuwa ni msikivu, utakuwa ni mwenye huruma kwa Watanzania masikini hususani wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, niseme tu kwamba katika mpango wa Wizara wa kuanzisha bandari za uvuvi, nimeona imetajwa Mbegani hapa, lakini mwanzoni Kilwa ilikuwa kwenye mpango. Tunaomba mpango huu kwa miaka mitano hii, Kilwa isisahaulike. Kilwa Masoko pale kuna kina cha kutosha, kuna bandari ya asili. Kwa hiyo, ule mpango wa miaka mitano ubaki vile vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili nami jioni ya leo nichangie hoja zilipo mezani. Pia kwa upekee wake nitajikita zaidi kwenye hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kama ambavyo imebainisha na taarifa ya CAG kwa hesabu za kuishia Juni, 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya leo nitakuwa na hoja kubwa mbili tu. Hoja ya kwanza ni uwezo wa halmashauri zetu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG kumekuwa na changaomoto katika kutekeleza miradi ya maendeleo katika mamlaka zetu za Serikali za Mitaa, na kwa ridhaa yako naomba nitoe mifano michache;

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na Halmashauri ya Mji wa Newala, sekta ya elimu peke yake Shule ya Msingi Lidumbe mradi wa nyumba ya mwalimu umetelekezwa tangu mwaka 2015. Shule ya Msingi Mnaida, mradi wa nyumba ya mwalimu umetelekezwa tangu mwaka 2012. Shule ya Msingi Mcholimbili, mradi wa nyumba ya mwalimu tangu mwaka 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, madarasa 25 yametelekezwa, nyumba za walimu 37 zimetelekezwa, maabara 26, zahanati 12 na mabwalo ya chakula mawili. Halmashauri ya Kasulu miradi 34 ambayo imeanzishwa na jamii imetelekezwa, haikuweza kukamilishwa. Nimalizie kwa mifano michache na halmashauri ya Kigoma Ujiji, kati ya miaka mitatu hadi kumi na moja, miradi yenye thamani ya shilingi 1,251,000,000/= imetelekezwa bila kukamilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini maana yake hapa? Maana yake ni kwamba, fedha za Watanzania walipa kodi zimeangamizwa bila kuleta tija yoyote. Jambo kama hili, sisi kama wabunge, wawakilishi wa wananchi ambao ndio walipa kodi haipaswi kulinyamazia. Hapa tumezungumzia fedha ambazo zimeingizwa kwenye miradi hii ya muda mrefu ambayo haikukamilika na haitumiki. Maana yake ni kwamba fedha za Watanzania zimekwenda bila kuleta tija. Hilo ni eneo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo kikubwa ni kwamba halmashauri zetu hatujazijengea uwezo katika maeneo mawili; eneo la kwanza ambayo ni usimamizi na eneo la kutoa ruzuku kwa halmashauri zetu katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Baadhi ya Wabunge hapa wamechambua, kwamba kumekuwa na uwiano usioridhisha wa kutoa ruzuku za miradi ya maendeleo katika halimashauri zetu. Zipo halmashauri ambazo zimepata ruzuku zaidi ya asilimia 100 na zipo ambazo zimepata ruzuku chini ya asilimia 40, kwa mujibu wa taarifa ya CAG. Hii imesababisha ndio matokeo ya miradi zaidi ya miaka minane, imetelekezwa na haina tija yoyote.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ni matokeo ya haya ni usimamizi usioridhisha wa mamlaka zetu za Serikali za mitaa kwenye vyombo vyake vya usimamizi. Hapa kwa upekee kabisa niseme, regional secretariat (Sekretarieti za mikoa). Kimsingi, kwa utendaji usioridhisha wa halmashauri zetu, mtu wa karibu kabisa ambaye ndiye mkono wa karibu wa ofisi ya Rais, TAMISEMI wa kusimamia ni Ofisi ya Mkuu wa Mkoa chini ya Sekretarieti ya mkoa. Lakini, ni kiwango gani sekretaieti zetu za mikoa tumeziweshesha kusimamia halmashauri? Ni kwa kiwango gani watendaji pamoja na maafisa waliopo pale kwenye sekretarieti za mikoa wamejengewa uwezo wa kusimamia Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa.? Ni kwa kiwango gani mamalaka zetu za sekretarieti za mikoa watendaji wake wamekuwa na uzoefu wa kutosha wa usimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hili ni janga na ni jukumu la Serikali kuliangalia eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili mahsusi ambalo ningependa kulitolea uchambuzi katika taarifa hii ni mfumo wa ukusanyaji wa mapato. Halmashauri 46, kwa mujibu wa taarifa ya CAG zenye POS 1,355 hazikuwa katika mfumo wa kukusanaya mapato mpaka ripoti hii inatolewa. Pia halmashauri nane zilipoteza POS 34 na halmashauri 27 zilifanya marekebisho ya ankara kiasi cha shilingi bilioni moja milioni mia sita na ushee, bila kiambatisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma kulikuwa na utaratibu katika halmashauri zetu, watendaji wasio na nia njema ya nchi hii kuiba fedha za wananchi wakati tukitumia mfumo wa stakabdhi za kuandika kwa mikono maarufu kama HW5. Kulikuwa na utaratibu wa kupoteza vitabu kwa makusudi wakati tayari fedha zimekusanywa, halafu watendaji wasio na nia njema walikuwa wanapiga hizo fedha. Tulipoleta mifumo hii ya ukusanyaji wa fedha kwa njia za kielektroniki tulidhani utakuwa ndio mwarobaini wa kurekebisha mapungufu haya. Badala yake watendaji hao hao wasiokuwa na nia njema na nchi yetu, wamekuwa wakitumia mifumo hii hii ya kielektroniki, kwa maana ya mashine za kukusanyia mapato lakini bado wanapiga kwa namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoambiwa kwamba halmashauri nane zilipoteza POS maana yake ni kwamba walikusanya halafu fedha za Watanzania zikaenda mifukoni mwa watu binafsi halafu baadaye wanasema POS zimepotea. Hili ni jambo ambalo haliwezi likakubalika. Pia tunaambiwa kwamba katika halmashauri ambazo zimakaguliwa na CAG kwa taarifa ya kuishia Juni, 2021 kiasi cha shilingi bilioni 17 za mapato zilikusanywa na POS lakini hazikupelekwa benki. Maana yake ni kwamba zilibaki kama fedha mbichi na zilitumika zikiwa fedha mbichi bila kupelekwa benki. Sasa haya mambo ni msiba mkubwa sana katika taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwasababu hiyo nilikuwa na mapendekeo yafaatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, kama nilivyosema, kwamba haya yote ni matokeo ya mifumo ya usimamizi isioridhisha. Kwa hiyo jukumu la kwanza kabisa ni kuimarisha mfumo wetu wa usimamizi hususani kuimarisha eneo lile la regional secretariat ili Ofisi ya Rais TAMISEMI isipate shida sana, kwamba Maafisa wa TAMISEMI kuhangaika kuwa wanashuka kwenye halmashauri. Tuna halmashauri 184 nchi nzima, watumishi au maafisa wa Wizara hawatoweza kutosheleza kuzunguka kwenye halmashauri 184 kwaajili kutoa au kujenga uwezo kwa watendaji wetu au kusimamia miradi. Jukumu la regional secretariat ni kuisaidia Ofisi ya Rais TAMISEMI, kwa maana ya Wizara, kwa niaba yake, kuzisimamia hizi halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia uwezo wa kiutendaji na wa kiuzoefu wa maafisa waliopo kwenye regional secretariat zetu unakuwa si kwenye kiwango ambacho wangeweza kuzisimamia halmashauri hizi.

Mheshimiwa Mwenyekti, jambo lingine ambalo nimeliona ni changamoto na nipendekeze hapa ni muundo wenyewe uliopo kati ya watendaji wa halmashauri na muundo wa regional secretariat.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Ofisi ya Rais TAMISEMI ilipitisha muundo ambao ulinakwenda kutekelezwa na watendaji wetu wa halmashauri lakini muundo huu kimsingi si muundo ambao ulikuwa shirikishi. Sisi kama Madiwani, Wabunge hatukushirikishwa katika kupendekeza muundo huu. Hata hapa Bungeni sidhani kama kulikuwa na semina ya kuonesha kwamba tunaenda kutekeleza nuundo huu. Sasa tunapotekeleza muundo ambao umetoka juu na kushuka tu kutekelezwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa bila kuhusisha wadau wakaingiza inputs zao matokeo yake ndiyo haya ambayo CAG anakuja kuyaibua. Utaratibu huu wa mapungufu ya kiutendaji na usimamizi yataendelea kuwa ni mwiba katika nchi hii mpaka pale ambapo muundo wa usimamizi utakapokuwa umekaa vizuri.

Mhehimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa juhudi ya kazi ambayo anaendelea kuifanya, na kubwa zaidi kwa kutuletea dada yetu mahiri katika Wizara hii ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; akisaidiana na mdogo wangu Mheshimiwa Ndejembi, ambaye ninamfahamu kikazi yuko vizuri na kwa maana hiyo, Wizara hii imepata watu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kuchangia nikumbushe waliopewa dhamana ya Wizara hii ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; kwamba, ofisi hii ni ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa kingereza Public Service Management. Kwa Kiswahili fasaha kabisa hii management ni usimamizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa masikitiko sana niseme kwamba, maeneo yafuatayo yanaharibu taswira ya ofisi hii au ya Wizara hii ya eneo lake la usimamizi, badala yake inaonekana kana kwamba, ni Wizara ya kuleta shida kwa watumishi wa umma. Nikianza nae neo la wanaopata nafasi za uteuzi wa Rais, maafisa wakuu ndani ya Serikali na maafisa waandamizi ndani ya Serikali; wanatekeleza majukumu yao mpaka pale mamlaka ya uteuzi inaposema basi, wakapumzishwa kwenye majukumu hayo, ofisi hii imeendelea kuwatelekeza kwa muda usiojulikana. Huu ni msiba mkubwa na inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais Kikatiba ana mamlaka ya kufanya uteuzi maeneo mbalimbali katika idara na taasisi mbalimbali ikiwemo kwenye majeshi, lakini ikiwemo hata humu Bungeni anateuwa humu Bungeni. Na pale ambapo uteuzi wa Rais unapokoma taasisi husika inawarudisha kwenye majukumu yao mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kama ingekuwa Waheshimiwa Wabunge wanaopata bahati ya kuteuliwa na Rais kuwa Mawaziri au Manaibu Waziri na pale ambapo utumishi wao wa uwaziri au unaibu Waziri unakoma ikaonekana kwamba, na Ubunge wao umekoma hapo ingekuwa msiba mkubwa, lakini kwa utumishi wa umma imekuwa ni kinyume chake. Utumishi wao wa uteuzi unapokoma wamebaki wakitelekezwa kwa muda usiojulikana. Nalizungumza hili kwa masikitiko makubwa na ionekane sasa kupitia Bunge hili mabadiliko na marekebisho na maboresho yafanyike katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alipofanya mabadiliko katika kada za wakurugenzi, watendaji wa Halmashauri, makatibu tawala wa wilaya kwa maana ya ma- DAS, pamoja na wakuu wa wilaya, wateule hawa walioachwa kwenye majukumu yao wapo ambao wamekaa bila majukumu yoyote kwa miezi mitatu, wengine miezi mitano, wengine miezi nane, wengine miezi tisa. Sasa kiutumishi huku kupumzishwa kwao kwa miezi mitatu, minne, mitano, mpaka tis ani nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003, kanuni ya 96 na ya 97, likizo inatajwa kama vile likizo ya mwaka, likizo ya uzazi, sabbatical leave na likizo nyinginezo. Sasa hawa waliokaa miezi tisa nje ya majukumu walikuwa kwenye likizo gani, watwambie?

Mheshimiwa Naibu Spika, na katika eneo hili nipongeze Mheshimiwa Dada yangu Mheshimiwa Jenista alivyoingia tu kwenye ofisi ameanza kushughulikia tatizo hili. Na ninayo amani kupata taarifa kwamba, watumishi wote sasa hivi wamerudi kwenye majukumu yao ikiwemo wakurugenzi, ma-DAS, pamoja na wakuu wa wilaya, lakini itakapofika wakati wa kupitisha mafungu hapa nitamuhitaji Mheshimiwa Waziri aje atoe maelezo hawa watumishi walikuwa kwenye likizo ipi na stahili zao ni zipi kwa muda wote ambao walikuwa nje ya utumishi wa umma? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo linaharibu taswira ya Wizara hii ni kucheleweshwa kwa mafao ya wastaafu pamoja na kucheleweshwa kwa kulipwa stahiki za wastaafu, gharama za kufungasha mizigo kwenda makwao. Vilevile wapo watumishi ambao wanastaafu kinyume na madaraja ambayo wanatakiwa wastaafie na kwa maana hiyo, wanakuwa wanaidai Serikali mapunjo. Mbaya zaidi unalipwa kwa mshahara wa nyuma kuliko ule ambao walitakiwa staafie. (Makofi).

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nachangia bajeti mwaka jana nilieleza kilio cha walimu wangu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, nilitaja wachache kwa uwakilishi wa wengine, na ninarudia tena kuwataja. Walimu haw ani pamoja na Hadija Nasoro Bungurumo, Salima Khamis Kaisi, Omari Ahamadi Mcheluya. Watumishi hawa wamestaafu tangu mwaka 2020 bado pamoja na kuwasemea hapa hawajalipwa mafao yao ya kufungasha mizigo, hawajalipwa tofauti zao za mshahara, kwa maana ya mapunjo ya malimbikizo au arrears.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi ni Serikali Sikivu ni Serikali makini. Inakuwaje wanyonge hawa tunawasemea hapa Bungeni halafu Serikali haichukui hatua? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, matarajio yangu hii itakuwa ni mara ya mwisho ya kuwasmea watumishi hawa. Kwa umahiri wako Mheshimiwa Waziri uliyepewa dhamana…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nilitaka nimpe Taarifa mzungumzaji kwamba, sio wastaafu tu ndio hawapewi fedha za kufungasha na kwenda, bali hata ambao bado wanaendelea na kazi wanaohamishwa kituo kimoja kwenda kingine hawalipwi, wanaweza wakahamishwa hata vituo vitatu bila kulipwa mpaka wanastaafu hawajalipwa hizo hela ambazo walikuwa wanahamishwa wakati wakiendelea kufanya kazi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ally, Taarifa unaipokea?

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeipokea. Na ni maeneo ya kurekebisha katika Ofisi hii ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni kuchelewa kufanyika kwa maamuzi kwa watumishi wenye mashauri ya kinidhamu. Ukiangalia sheria na kanuni za utumishi wa umma, ndani ya miezi mitatu inatakiwa mashauri ya kinidhamu yawe yamehitimishwa, mtumishi awe amejua kwamba, anayo hatia na kwa maana hiyo atatumikia adhabu yake au hana hatia, atarudishwa kwenye majukumu yake. Lakini kwa masikitiko makubwa niseme tu kwamba, wapo baadhi ya watumishi wamekaa zaidi ya mwaka mashauri yao ya kinidhamu hayajaamuliwa. Sasa hii ni kinyume kabisa na sheria ambazo tunazitunga hapahapa Bungeni na Serikali ina jukumu la kuzisimamia sheria hizi. Kama tunazitunga na Serikali ndio msimamizi tunatagemea nani akazisimamie? Nani atatoa haki kama si Serikali ambayo ndio inaleta miswada ya kurekebisha au kutunga sheria hapa Bungeni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe taarifa tu kwamba, kuna walimu 48 Tanzania Bara waliombewa kibali cha kurudi kazini tangu mwezi Juni, 2021. Narudia, walimu 48 wameombewa kibali cha kurudi kazini baada ya mashauri yao kuwa yamehitimishwa tangu mwezi Juni mwaka 2021 lakini mpaka leo mashauri haya yako kwenye ofisi hii ambayo bajeti yake tunaendelea kuijadili. Niombe, mtakapochukua hatua za kuwarudisha kazini watumishi hawa kwa upungufu mkubwa wa watumishi, hasa kada ya walimu tulionao, hawa waleteni Kilwa, mimi nitawapokea. Narudia, waleteni Kilwa tukawapangie majukumu tuna upungufu mkubwa wa walimu kule wakatumikie Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni kuhusu motisha kwa kada ya walimu. Walimu, hebu tuangalie ugumu na uzito wa majukumu yao; katika hali ya kawaida inaonekana kama walimu kazi yao kubwa ni kufundisha tu, lakini hapana, walimu hawa kwanza ni walezi wa watoto wetu. Hata pale ambapo watoto wameshindikana kule kwa walimu watoto wananyooshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni nani hajapitia mikononi mwa walimu katika Bunge hili? Hakuna; lakini walimu hawa tumewakumbuka kwa utaratibu gani katika motisha?

Mheshimiwa Naibu Spika, kada zingine wana allowance kulingana na majukumu na uzito wa kazi zao kama vile responsibility allowance, on call allowance pamoja na rational allowance. Sasa hawa walimu ambao wanatumia muda wa ziada kuandaa masomo, kuandaa scheme of service ya muhula mzima au mwaka mzima na shughuli hizi wanazifanya nyumbani. Kama ni mama anaacha baba amelala yeye anaandaa scheme of work, kama ni baba anaacha mama amelala yeye anaandaa scheme of work. Tunachukua hatua gani za kufikiria kuwapa motisha hawa walimu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna kuandaa lesson plan, nje kabisa ya ufundishaji wenyewe. Baada ya hapo unaandaa lesson notice, baada ya hapo unaanza kumfuatilia mwanafunzi mmoja baada ya mwingine. Hebu tufike mahali tupime majukumu mazito ya kazi ya walimu wetu hawa ambao kwa uzalendo mkubwa wanaitumikia nchi yetu na ndio zao la sisi sote na kwa maana hiyo, tuwakumbuke katika motisha. Kama madaktari na sekta ya afya wanapata on call allowance wanapofanya kazi ya ziada…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Ahsante. (Makofi)

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa muda. Na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili na mimi jioni hii niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nikiungana na Wabunge wenzangu waliopata fursa ya kuanza kuchangia na mimi kwa dhati kabisa nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anajitoa kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake ukurasa wa kumi na mbili ametukumbusha Watanzania kwamba mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere megawatt 2115 serikali imetoa bilioni 869.93 na mradi umefikia 83%; hizi ndizo kazi za Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kwamba haitoshi mradi mkubwa wa kusafirisha mafuta kutoka Uganda Hoima mpaka Tanga, kilomita 1443 Serikali imeshatoa bilioni 30.39 kwa ajili ya kulipa fidia waathirika wa maeneo ambayo bomba itapita, hizi ndizo kazi ambazo Watanzania wanafanyiwa na Mheshimiwa Rais Wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upekee wake sisi wana- Kilwa na hususani wana-Kilwa Kusini Rais Samia amefanya ambayo hayajawahi kufanyika, na kwa kweli ameacha alama ambayo kwa kweli hatutoisahau. Kulikuwa na mradi ambao umesuasua kwa muda mrefu wa maji kwenye miji 28 umeanza kutekelezwa katika kipindi hiki cha Dkt. Samia. Pia kulikuwa na ujenzi wa bandari ambao mipango yake ilikuwa ni ya muda mrefu, tulipitisha katika mpango wa miaka mitano ya maendeleo hapa Bungeni. Nitumie fursa hii kuwataarifu Watanzania kwamba mradi huu tayari umeanza pale Kilwa Masoko na unathamani ya shilingi bilioni 266.7; Kilwa hatujawahi kupata mradi mkubwa kama huu tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama kwamba haitoshi Mheshimiwa rais ameendalea kutusaidia wanakilwa katika sekta za barabara. Tumeongezewa fedha kwenye TARURA kutoka milioni 800 ambayo ilikuwa ni kwa ajili ya Wilaya nzima ya Kilwa kwa wakati ule mpaka kufikia karibu bilioni tatu kwa majimbo yote mawili kwa mwaka, Kilwa Kaskazini na Kilwa Kusini. tunamshukuru na kumpongeza sana Rais Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo sasa nije katika baaadhi ya maeneo ambayo nilidhani Serikali ikitekeleza basi tutakuwa tumemsaidia na kumfanya Rais Samia apendeze zaidi kwa Watanzania na wana Kilwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza katika eneo la ujenzi wa bandari, nitoe rai kabisa kwamba wakati Serikali inatekeleza ujenzi huu wa bandari basi ifikirie kuweka miundombinu mingine rafiki itakayoendana na uwepo wa Bandari hii ya Uvuvi pale Kilwa Masoko. Kwa mfano barabara iliyopo kutoka pale bandarini kuelekea Nangurukuru kilometa takribani 30 haiko katika viwango ambavyo vitaendana na bandari hiyo. Nitoe rai katika bajeti hii barabara hii ipanuliwe na ijengwe katika viwango. Lakini pili mundombinu rafiki na taasisi rafiki ambazo zitaendana na uwepo huu wa bandari ikiwemo viwanda vya kuchakata mazao ya Bahari na chuo cha uvuvi pale KilwaMasoko ni vitu ambavyo pia vinatakiwa vifikiriwe katika bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nieleze kwa masikitiko kidogo, kwamba pamoja na utekelezaji wa bandari ambao unaendelea pale Kilwa Masoko lakini wananchi wangu wapatao 54 bado hawajalipwa fidia kupisha upanuzi na ujenzi huu wa bandari. Nitoe rai kabisa, katika kipindi hiki kifupi ndani ya mwaka huu muda si mrefu Serikali ifikirie kuwalipa fidia wananchi wangu wapatao 54 ili masuala ya ujenzi wa bandari yasiingie migogoro ya wananchi kudai fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija katika uboreshaji na upanuzi wa viwanja vya ndege, tulipitisha katika mpango wa miaka mitano, na Kiwanja cha Ndege cha Kilwa Masoko ni miongoni mwa viwanja ambavyo vitapanuliwa na kufanyiwa maboresho. Lakini kwa masikitiko niseme tu kwamba bajeti iliyotengwa kwa mwaka uliopita ilikuwa ni ndogo sana kiasi cha kukarabati runway ile kilometa 800 tu kwa kiwango cha changarawe. nitoe rai kwamba kiwanja hiki cha ndege sasa kijengwe katika viwango vinavyotakiwa, kwa maana kuongeza mita 900 zingine za runway, kuweka uzio wa kiwanja cha ndege na pia kuboresha lile eneo la kupumzikia abiria.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nieleze tu kwamba dhana ya upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kilwa Masoko ni wa miaka takribani miaka 10 iliyopita, na wananchi wangu walifanyiwa tathmini mwaka 2011/2012, na ikarudiwa tena tathmini ili walipwe fidia mwaka 2011/2012 na tathmini hii ilirudiwa tena mwaka jana mwezi wa nne. Kiasi cha wananchi wangu zaidi ya 412 wamefanyiwa tathmini hii lakini bado hawajalipwa fidia hii. Nitoe rai kabisa, Serikali ifanye hima kuwalipa fidia wananchi wangu hawa ili ujenzi utakapokuwa umeanza wa kuboresha na kupanua Kiwanja cha Ndege pale Kilwa Masoko kusiwe tena na malalamiko ya wananchi wetu kudai fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija katika eneo la maji, pamoja na kushukuru kupatiwa mradi ule wa maji kutoka Mto Mavuji kwa ajili ya Miji ya Nangurukulu Masoko na Kivinje niseme tu kwamba bado tunahitaji kupanua wigo wa upatikanaji wa maji vijijini pamoja na mijni. Hapa kwa upekee wake nizungumzie kata moja ambayo kwa kweli haijawahi kupata kunufaika na mradi wa maji wa aina yoyote ile; na hii si kata nyingine isipokuwa ni Kata ya Lihimalyao iliyopo katika Jimbo langu la Kilwa Kusini. Nitoe rai kwa kata ya Lihimalyao kwa upekee wake, hebu Serikali ione uwezekano wa kujenga mabwawa kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Kata jirani ya Pande kuna maji ya kutosha. Serikali ione uwezekano wa kutoa maji kwa utaratibu wa mtiririko kupeleka katika Kata hii ya Lihimalyao ndani ya kipindi cha mwaka huu wa bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitoe rai tu kwa Serikali; kwamba ili kupunguza kama si kuondoa kabisa tatizo la maji, si tu Kilwa lakini mikoa yote ya Kusini, kwa nini tusiwe sasa na mpango wa kupanua wigo matumizi ya maji ya Mto Rufiji? Badala ya kupeleka maji ukanda wa Dar es salaam peke yake tawi lingine lije Ukanda wa Kusini ili Mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara pamoja Ruvuma inufaike. Mradi huu wa Mto Rufiji kama utatekelezwa kuanzia kipindi hiki nakuhakikishia kwamba wananchi wa mikoa yote ya kusini niliyoitaja tatizo la maji au changamoto ya maji litakuwa ni baibai na hapo itakuwa kwamba kweli tumewatendea haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika miradi ya kimkakati. Sisi pale Kilwa tuna miradi mingi ya kimkakati lakini kwa muktadha wa mchango wangu leo niuzungumzie mradi mmoja tu ambao ni mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Stendi ya Nangurukuru. Tunaomba kupitia halmashauri miaka mitatu katika bajeti yetu kama maombi maalum; lakini niombe mwaka huu maombi yetu yale maalum ya bajeti ya kupanua ujenzi wa stendi ya nangurukuru kama mradi wetu mkakati uweze kuidhinishwa na Bunge hili na hatimaye wana-Kilwa waweze kunufaika na stendi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikumbushe pia Bunge lako kwamba katika mpango wa miaka mitano wa maendeleo tulioupitisha hapa bungeni tulipitisha ujenzi wa kiwango cha lami Barabara ya Kiranjeranje Nanjirinji mpaka Ruangwa, lakini pia Barabara ya kutoka Nangurukuru mpaka Liwale. Ninayo furaha kusema kwamba kazi za upembuzi yakinifu na usanifu zimekamilika. Ni wakati muafaka sasa barabara hizi zianze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipendekeze barabara ya Nangurukuru mpaka Liwale ambayo kimsingi inahudumia majimbo matatu, Jimbo la Kilwa Kusini, Kilwa Kaskazini pamoja na Jimbo la mtani wangu Kuchauka kule, Liwale ianze kutekelezwa ndani ya mwaka huu angalau kilometa 50 kutoka pale Nangurukuru. Tukifanya hivyo tutakuwa tumeyatendea haki majimbo hayo matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niseme tu kwamba tunaendelea kupongeza na kushukuru juhudi za Mheshimiwa Rais Samia katika kuboresha miundombinu katika sekta za huduma ikiwemo afya na elimu. Katika elimu tumepata madarasa ya kutosha. Hata hivyo, nitoe rai, bado tuna tatizo kubwa la nyumba za walimu lakini pia bado tuna tatizo kubwa la madawati katika maeneo yetu ya halmashauri zetu. Niombe katika bajeti hii kwamba tatizo la nyumba za walimu pamoja na madawati liwekewe kipaumbele ili tatizo la ujumla la miundombinula shule zetu za msingi na za sekondari tuweze kulipunguza kwa kiwango kikubwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumza haya naomba kuunga mkono hoja.(Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante awali ya yote niungane na wenzangu kukupongeza wewe kwa kuchaguliwa na Bunge hili kuwa Spika wetu na kwa kweli sisi Wabunge tuna imani kubwa. Tunaomba Mungu akusimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo ambazo pia zimfikie Mheshimiwa Zungu Naibu Spika, nianze sasa kwa kuchangia hoja au taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kama ambavyo imewasilishwa na Mwenyekiti wetu, mama Grace Tendega, ikiwa ni hesabu za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuishia mwezi Juni, 2020. Ni ukweli kwamba Serikali imekuwa na juhudi za dhati kabisa kupeleka fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, sekta ya elimu na sekta nyinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kumekuwa na utaratibu wa kupeleka fedha kwa utaratibu wa flat rate kwa kila halmashauri, kwa mfano, Serikali imekuwa ikipeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni kwenye shule zetu za sekondari. Hapo awali ilikuwa ni Shilingi milioni 75 na baadaye ikawa ni shilingi milioni 80, lakini kumekuwa na namna tofauti tofauti katika utekelezaji wa eneo hili.

Mheshimiwa Spika, katika baadhi ya halmashauri Shilingi milioni 80 imetosheleza kabisa kujenga bweni moja la wanafunzi kukaa idadi ya watoto 80 ikiwemo facilities za ndani ya bweni hilo, kwa maana ya vitanda, lakini katika baadhi ya halmashauri shilingi milioni 80 hazijatosha na hakuna ambacho kimefanyika na kazi haina viwango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili nina maeneo mawili ya kuzungumzia. Eneo la kwanza ni kuwapongeza wale ambao kwa dhati kabisa wamefanya vizuri ikiwemo, halmashauri ya Wanging’ombe ambayo ni Jimbo la Mheshimiwa Festo Dugange. Wamejenga shule, wamejenga mabweni kule katika Sekondari ya Wanging’ombe, wamejenga bweni katika Sekondari ya Wanike kwa Shilingi milioni 75 na imetosheleza hakuna namna yoyote ya harufu ya ubadhirifu wa fedha. Hata hivyo, katika halmashauri zingine shilingi milioni 80 imezama, mabweni hayajakamilika, vitanda hakuna na bado fedha haitoshelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki ni kiashiria tosha kabisa kuna mazingira ya dalili ya matumizi mabaya ya fedha hizi za umma. Katika hili niseme pia kwamba Serikali imekuwa ikipeleka fedha hizi bila kufanya tathmini ya kina. Katika maeneo mengine ni kweli kumekuwa na dalili za ubadhirifu lakini katika mazingira mengine ambapo facilities zote ikiwemo bidhaa za madukani, zinapatikana kwa urahisi na zile bidhaa ambazo zinapatikana kwenye mazingira halisi ikiwemo mchanga, mawe, kokoto zinapatikana, bado fedha hizi hazijatosha.

Mheshimiwa Spika, sasa niseme tu kwamba wakati Serikali ili kuzipunguzia mzigo wa hoja halmashauri zetu, zinapeleka fedha hizi kwa utaratibu huu wa flat rate, zingefanya kwanza tathmini ya kimazingira ili kujua kila halmashauri na kila maeneo yanahitaji shilingi ngapi? Kwa mfano, katika baadhi ya halmashauri zimekuwa mbali na maeneo ambayo bidhaa za viwandani zinapatikana. Huwezi ukapeleka utaratibu wa flat rate na wakafanya kama vile ambavyo wangeweza kufanya vingine kwa vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa ushauri huu, niunge mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia hoja iliyopo Mezani inayohusu Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika ya Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nami nipongeze sana Wizara hii, nikianza na Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu, Mheshimiwa Eng. Masauni, kwa kazi nzuri ambayo anaifanya katika Wizara hii; na Naibu Waziri, kaka yangu, Mheshimiwa Sagini, ambao kimsingi sisi kama Kamati tumeshirikiana nao vizuri sana katika kuchakata itifaki hii mpaka leo inawasilishwa hapa Bungeni, nasi Wabunge tunapata nafasi ya kuchangia kwa lengo la kuomba Wabunge wenzetu waweze kuridhia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze na nimshukuru pia Mwenyekiti wangu wa Kamati, kaka yangu Mheshimiwa Vita Kawawa kwa namna ambavyo ametuwakilisha vizuri sisi Wanakamati wenzie katika kuwasilisha yale ambayo tulipokuwa kwenye Kamati ndiyo tumekubaliana kama Maoni ya Kamati ya kuwasilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu nitakuwa na mambo machache sana ya kuchangia ambayo yataongozwa na swali moja tu kwamba kwa nini sisi Tanzania kupitia Bunge lako hili tuweke Azimio hili la kuridhia itifaki hii. Jambo la kwanza nature ya ugaidi wenyewe. Kimsingi dhana ya ugaidi si dhana ambayo inafanyika katika utaratibu wa kindani kwa maana locally, kinyume chake ni dhana ambayo inavuka Taifa moja mpaka Taifa lingine kwa maana ni dhana ya kimataifa. Kwa maana hiyo, kama ni jambo la kimataifa hatuwezi sisi Tanzania ambao tunajiita nchi iliyo kamili tukabaki wenyewe bila kushirikiana na nchi zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, sisi Watanzania tukiridhia Itifaki hii, tutakuwa na fursa ya kuweza kushirikiana na nchi zingine za Afrika. Tukumbuke katika wasilisho ambalo Mheshimiwa Waziri amewasilisha hapa ni kwamba nchi 45 za Afrika zimesaini Mkataba huu ikiwemo Tanzania. Katika nchi hizo 45 ni nchi 21 ambazo zimeridhia na kwa maana hiyo sisi Watanzania tukiuungana au tukiridhia tutakuwa tumeungana na nchi zingine za Afrika 21 ikiwa ni pamoja na jirani zetu wa nchi kama za Rwanda, South Africa, Burundi, Lesotho, pamoja na nchi nyingine za Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, kwa nini turidhie? Itakuwa imetupa nafasi au fursa ya kufanya marekebisho ya Sheria yetu iliyotungwa mwaka 2002, Sura Na. 19 ambayo tunasema ni Sheria ya Kuzuia Ugaidi na kwa maana hiyo tutakaporidhia Itifaki hii tutaweza kuwa na fursa ya kubadilisha Sheria yetu na kuwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ambapo sababu sheria zinatungwa hapa Bungeni, Wabunge tutakuwa na nafasi pana zaidi ya kutoa mawanda ya maelezo yetu maana wazoefu katika kuchangia sheria ambayo itakuwa na maslahi kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kwa nini turidhie? Viashiria vya matukio ya kigaidi ni viashiria ambavyo katika nchi yetu tumeanza kuvisikiasikia kipindi kifupi kilichopita, lakini pia miaka kadhaa imepita nchi jirani siyo tu viashiria badala yake ni matukio ya kigaidi yameweza kutokea. Wote tunakumbua matukio ambayo yametokea Kenya miaka kadhaa iliyopita. Hivyo basi, hatuwezi kuwa salama kama jirani zetu au hata ndani ya nchi viashiria hivi vinatokea na sisi tuone kwamba tuko radhi hatuwezi kuridhia Itifaki hii, tukabaki salama hapana. Niombe sana Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono Itifaki hii ili nchi yetu iweze kusaini na kuridhia ili tuungane na nchi zingine za Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nianze kuchangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia kwa juhudi ambazo imeendelea kuzitekeleza kiasi kwamba Watanzania wanashuhudia kwa macho na wenye kusikia wanasikia shughuli mbalimbali ambazo zinatekelezwa, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako hili la 12 katika Mkutano wake wa nne liliazimia kwamba sekta ya kilimo ni sekta ambayo inatakiwa ipewe kipaumbele namba moja katika mpango huu wa tatu wa maendeleo. Na nitumie fursa hii kuipongeza sana Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kile ambacho imeanza kukifanya, kitu ambacho kinaleta matarajio makubwa sana kwa Watanzania hususan wakulima ambao ndio wazalishaji wa mazao yetu ya kilimo, kwa maana ya mazao ya biashara lakini pia mazao ya chakula katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia sekta ya kilimo kabla hatujawagusa wenyewe wakulima tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu. Ni lazima tunapozungumzia kilimo tubainishe maeneo ambayo kweli yatamsaidia mkulima mmoja mmoja na pia kwa vikundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika kilimo kuna suala la ushirika ambalo kimsingi ndilo eneo pekee litakalomsaidia Mkulima. Niishukuru sana hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ukurasa wake wa 29 na 30 amegusia kidogo ushirika na pale ambapo mambo hayakwenda vema Serikali imechukua hatua, na ninaomba ninukuu sehemu ya hotuba hii.

“Hatua mbalimbali za kisheria zimechukuliwa dhidi ya wote waliohusika na ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji wa vyama vya ushirikia ikiwemo vitendo vya wizi wa mali na fedha za ushirika”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera kwa Serikali kwa hatua hii. Lakini wakati hatua hizi zinachukuliwa kwa masikitiko makubwa nielezee kilio cha wakulima wa Nanjilinji katika Jimbo langu la Kilwa Kusini wanaotokana na Chama cha Msingi cha Nanjilinji ‘A’ ambao kwa msimu wa kilimo uliopita wa 2021/2022 wamedhulumiwa mazao yao, mpaka tunazungumza katika Bunge hili wakulima hawa bado hawajalipwa mazao yao. Wmezalisha kiasi cha zaidi ya tani 40 lakini hawajalipwa mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi kumekuwa na matumizi mabaya ya nafasi za watu ikiwemo viongozi wa chama cha msingi wakishirikiana na viongozi wa ushirika au watendaji wa Idara ya Ushirika Wilayani; ambapo wameandikia hati hewa watu ambao hawahusiki katika kulipwa mazao haya. Mbaya zaidi hizi hati hewa ambazo zimekwenda kwenye malipo hewa zinawagusa viongozi na watendaji wa Serikali, na mpaka sasa tunavyozungumza wakuliwa hawa wapatao 40 wameendelea kulalamika na hawajasaidiwa mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo heshima kutoa taarifa hii, na wakulima hawa walipwe fedha zao za msimu uliopita mara moja ili waweze kujikimu na kuanza tena shughuli za Kilimo kwa msimu ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka kwenye sekta ya kilimo nije katika sekta ya afya. Niendelee kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia, wote tumeshuhudia namna ambavyo Vituo vya Afya vimeboreshwa, katika baadhi ya maeneo, kadhalika zahanati zimeboreshwa, lakini katika wilaya mpya hospitali za wilaya zimeendelea kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili nipongeze, katika Jimbo langu la Kilwa Kusini kuna Hospitali yetu ya Wilaya, ipo Kilwa Kivinje, inaitwa Kinyonga. tumepata Shilingi milioni 300, fedha kwaajili ya jengo la emergence, na kwakweli ujenzi unaendelea vizuri; tunaendelea kuipongeza na kuishukuru Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika eneo hili niiombe Serikali, kwamba Hospitali hii ya Wilaya ya Kilwa Kinyonga ni Hospitali chakavu, ni ya tangu miaka ya sitini na kwa maana hiyo miundombinu yake si ya kuridhisha. Wakati tunaendelea kuboresha miundombinu katika maeneo mengine katika mpango huu niombe kabisa kwamba ifikirie kutenga fedha za kutosha kwaajili ya ukarabati na uboreshaji wa miundombinu katika Hospitali ya Wilaya ya Kinyonga pale Kilwa Kivinje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningeweza kupongeza ni mwendelezo wa ujenzi wa barabara nchi nzima; na hapa kwa upekee wake kabisa nipongeze kwa barabara ile ya mwendokasi inayojengwa kutoka Mbagala Rangi Tatu Dar es Salaam kuelekea mjini. Barabara hii itakuwa ni ufumbuzi na utatuzi wa kero kwa wakazi wa Mbagala ambao sisi watu wa kusini wengi ndio tunaishi maeneo haya. Kwa hiyo, tunaipongeza sana Serikali kwa eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika eneo hili nisikitike tu kwamba, kuna usumbufu mkubwa ambao unafanywa na mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa jina Halmashauri ya Manispaa ya Temeke. Halmashauri hii imelazimisha abiria wanaotoka Kilwa Kivinje na Kilwa Masoko kutumia stendi inayoitwa Biansi kinyume na utaratibu wa kutumia stendi ya mabasi ya kusini iliyopo pale Rangi Tatu, maarufu kama stendi ya mjini. Huu ni utaratibu ambao unaleta usumbufu usio na lazima. Niiombe Serikali iingilie kati jambo ili abiria waendao Kilwa na maeneo mengine ya Mikoa ya Kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma watumie Stendi ya Mkoa iliyopo pale Mbagala Rangi Tatu na si stendi za pembezoni, ambazo zinaleta usumbufu mkubwa kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niendelee kuipongeza Serikali kwa kuleta miradi ya kuboresha miji yetu, manispaa na majiji yetu, kama vile mradi wa TSCP umeboresha miundombinu ya miji nchini, mradi wa ULGSP umeboresha miundombinu ya miji, mradi wa DMDP Dar es Salaam inapendeza sasa hivi na sasa hivi tupo katika mradi wa TACTIC. Rai yangu katika mradi huu wa TACTIC na miradi mingine ya kuboresha miji, itakayoendelea, kuwe na uniformity katika nchi, ili isije ikawa unaenda katika miji mingine imedorora haipendezi na miji mingine inapendeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kutoa mapendekezo, kwamba katika mpango huu wa tatu wa maendeleo miji mingine iliyopo ndani ya nchi yetu ya Tanzania ikumbukwe katika miradi hii ikiwemo Mangaka, Ifakara, Chalinze, Mafinga, Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje, Tarime, Mpanda na mingineyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ushauri huu naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi jioni hii ili niweze kuchangia hoja za kamati mbili; Kamati ya Bajeti na Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu nitajikita zaidi kwenye Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Nikianza kwa kupongeza kwa dhati kabisa viongozi wa wanaoongoza Wizara zinazosimamiwa na Kamati yetu hii ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama; nikianza na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje, mama mchapakazi Mheshimiwa Tax pongezi sana kazi nzuri na kwenye kamati kwa kweli umeonesha ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Balozi Mbarouk Naibu Waziri ameonesha ushirikiano wa kutosha kwenye Kamati na yote ambayo tumeyaleta kwenye Bunge ni mchango wa pamoja kati ya sisi Wanakamati pamoja na viongozi wetu hawa wakisaidiana na watendaji wao. Lakini Mheshimiwa Waziri, rafiki yangu wa Ulinzi Bashungwa naye ameonesha uwezo mkubwa sana. Nadhani katika historia ya nchi hii anaweza akawa labda ni Waziri wa pili kijana kuongoza Wizara hii nyeti na ameonesha kumudu. Nikupongeze sana ndugu yangu Bashungwa wewe pamoja na watendaji wako Wizara inakwenda vyema na sisi wanakamati hatuna shaka na wewe kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipongeze vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kutekeleza majumu yao kiasi kwamba Watanzania tumeshazoea kuwa nchi yetu ni nchi shwari, nchi yetu ni nchi ya amani, nchi yetu ni nchi yenye mtangamano, haina shida yoyote mashaka yoyote ukilinganisha na baadhi ya nchi katika bara letu la Afrika au kwingineko duniani. Haya yote hayajafika hapa Tanzania kwa bahati nasibu isipokuwa ni kazi ya dhati kabisa inayofanywa na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi mimi nitandoa kwa uchache sana katika maeneo machache ambayo yamelegalega katika wizara zetu mbili hizi; kwa maana ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pia pamoja na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na maeneo haya kimsingi hayakulegalega kwa sababu ya utendaji usioridhisha wa Waziri au watendaji katika Wizara isipokuwa ni kwa kukosa ushirikiano miongoni mwa Wizara zingine ambazo zilipaswa zisaidie kuwezesha kazi za Wizara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kulikuwa nae neo la kulegalega kwa utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kama ambavyo taarifa yetu imesema. Eneo hili limelegalega kwa sababu ya kukosekana kwa coordination. Nitoe ushauri kabisa katika Bunge hili, kwamba ili diplomasia ya uchumi iweze kutekelezwa ipasavyo lazima kuwe na utaratibu wa ku-coordinate miongoni mwa Wizara, kwa maana ya Wizara za Uzalishaji pamoja na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Wizara hiyo ya Mambo ya Nchi za Nje kumekuwa na kulegalega katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwa mfano katika balozi zetu kuna majengo 47 yanahitaji ukarabati mkubwa. Pia kuna majengo tisa yamechakaa, pia kuna majengo 11 hayako katika hali nzuri kabisa kiasi kwamba yanatweza hadhi ya nchi yetu Tanzania huko nchi za nje. Haya yote hayakufanywa kwa sababu ya uzembe katika wizara isipokuwa ni kwa sababu wizara haikuwezeshwa kutoa fedha za kutosha kwa wakati kutekeleza miradi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwa kipindi cha kuanzia Julai 2022 hadi Januari 2023, wakati taarifa yetu sisi ndiyo tunaijadili kwenye Kamati yetu hakukuwa na fedha yoyote iliyopelekwa kutekeleza miradi hiyo. Huu ni msiba na ni si jambo ambalo linatakiwa watanzania au Wabunge tulitazame kwa mtazamo mwepesi mwepesi lazima tutazame kwa mtazamo mzito katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kukosekana hivyo jambo hili limeikumba pia Jeshi la Magereza. Bajeti ambayo tuliipitisha mwaka jana kwenye Jeshi la Magereza mwaka 2023 ni bilioni 21.369 lakini mpaka tunajadili taarifa ya Wizara ya kuanzia Julai 2022 mpaka Desemba 2022 hakuna fedha yoyote iliyopelekwa kwenye Jeshi letu la Magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kufanya hivyo tafsiri yake ni tafsiri yake ni kwamba Jeshi la Magereza limeshindwa kutekeleza mipango yake ya usalama, mipango ya Ofisi za Magereza, mipango ya ujenzi au uanzishaji wa mashamba ya magereza pamoja na mpango wa kuboresha upatikanaji wa maji katikamagereza yetu. Hali hii si hali ambayo inaridhisha na inapendeza katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwamba haitoshi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambayo fungu lake la fedha ni fungu 14, bajeti ambayo Bunge hili liliidhinisha ilikuwa ni shilingi bilioni 9 .93, lakini mpaka Julai Desemba hakuna fedha yoyote iliyopelekwa kwa ajili ya Jeshi la Uokoaji na Zimamoto. Huu ni msiba mkubwa. Inapotokea majanga ya moto au majanga mengine ambayo yanahitaji msaada wa jeshi hili Watanzania tumebaki tukiwa tunalaumu kuwa Zimamoto wameshindwa kufika kwa wakati, lakini kumbe ni kwa sababu hawajawezeshwa kupata vifaa vya kisasa kuweza kuokoa majanga kwa kipindi yanapotokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, lakini hapa nitagusia fungu moja tu ambalo ni Fungu 39 katika kamandi ile ya Jeshi la Kujenga Taifa. Kamandi ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa kipindi cha Julai mpaka Desemba hakuna hata senti tano ambayo imepelekwa kwenye Kamandi hii ya Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali ya kujiuliza ni kama ifuatavyo; kwa nini sasa Wizara hii inaitwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilhali hatuwezeshi JKT kufanya majukumu yake? Kwa nini Jeshi limeweka Kamandi ya Jeshi la Kujenga Taifa ilhali hatuwezeshi JKT kufanya majukumu yake? Kwa nini kila mwaka tunachukua vijana ili waende JKT wakafanye National Service kule ilhali JKT haijawezeshwa kufanya yake? Huu ni msiba na kama ni msiba si jambo ambalo tunatakiwa tulijadili kwa wepesi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nitoe assignment question kwa Serikali; is Tanzania, the United Republic a country or Nation state discuss. If it is a country, it is well and good to leave these armed forces without to incapacitate them. But if it is a National state should you, the Government please provide enough fund to the National Service, enough fund to armed forces, provide enough fund to the immigration forces in order for Tanzania to be a country a National state, United Republic and Sovereign State. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii jioni ya leo na mimi niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji nikianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nikianza kwa maneno Matakatifu ya Mwenyezi Mungu kutoka katika Kitabu cha Quran sura ya 21 Aya ya 30 inasema na ninanukuu, “Wajaalna minalma kula shain hayi” tafsiri yake ni kuwa, tumejaaliwa kutokana na hayo maji kuwa ndiyo chanzo cha uhai wa kila kitu hapa ulimwenguni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa spirit hiyo Mheshimiwa Waziri na timu yake watambue kabisa wao wamepewa dhamana na jukumu la kusababisha uhai wa kila kitu hapa ulimwenguni katika ardhi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo nitumie fursa hii kwa upekee kabisa kwa dhati kabisa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Aweso, amekuwa ni Waziri kijana wa mfano wake katika kazi na kwa kweli anaishi kwa yale ambayo anayanena hapa Bungeni kila siku anapopata nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, hivi karibuni tuliona sakata na ameishi katika msemo wake wa “ukinizingua tutazinguana” kule Handeni ameshafanya vitu vyake majuzi mwezi uliopita. Baada ya watumishi wasio na dhamira njema na Mkandarasi asiye na dhamira njema aliyetaka kudhulumu kodi ya Watanzania kwa kulipwa zaidi ya Shilingi Milioni 600, bila kazi yenye tija Mheshimiwa Aweso amefukuza watumishi hao amewasimamisha Mkandarasi amemuweka pembeni uchunguzi unaendelea. Hivyo ndivyo tunavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, spirit ya Mheshimiwa Samia Rais wetu ya hapa kazi iendelee na kweli kazi inaendelea ndiyo namna hiyo, huko ndiko kumsaidia kwa ukweli Mheshimiwa Rais hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kana kwamba haitoshi timu nzima ya Wizara hii ya Maji wasaidizi wako wakiwemo Naibu Waziri Dada yangu Engineer Maryprisca ni Dada na Mama makini katika kazi. Katibu Mkuu rafiki yangu Engineer Sanga makini katika kazi, Naibu Katibu Mkuu makini katika kazi na Watendaji wote kwa ujumla wa Wizara hii kwa kweli wanakusaidia ipasavyo. Ni matarajio na matumaini makubwa kwa Watanzania ambao kwa muda mrefu tumekuwa na shida ya maji katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa spirit hiyo hiyo niendelee kupongeza Wizara yako lakini nimpongeze Mheshimiwa Rais na nimshukuru Mheshimiwa Rais, kupitia mpango wa mapambano ya COVID na ustawi na maendeleo Jimbo langu la Kilwa Kusini tulipata Shilingi Milioni 473 kwa ajili ya kuendeleza na kustawisha miundombinu ya maji Kilwa Masoko. Kwa maana hiyo, ninayo furaha kukuambia kwamba kwa fedha hizi Shilingi Milioni 473 tunakwenda kutatua changamoto ya maji kwa asilimia zaidi ya 90 Masoko Mjini, Dodoma One, Nangurukuru, Mpara, Nangurukuru Ndogo, Mnazimmoja, Ngome, Utabiri, Mihina na maeneo mengine ya mjini Kilwa Masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa spirit yako ya “ukinizingua tutazinguana” naomba nikupe taarifa kwamba fedha hizi Shilingi Milioni 473 bado zimekaliwa huko kwenye Wizara yako hazijafika bado. Mkandarasi amefanyakazi kwa asilimia 80 hajalipwa chochote sasa swali langu ni nani anayekuzingua huko Mheshimiwa Waziri? Naomba usimamie hili ili wananchi wa Mji wa Kilwa Masoko waweze kunufaika na neema ya fedha hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nipongeze kwa fedha ambazo Serikali yetu inakopa Serikali ya India kwa ajili ya maji katika Miji 28 na Miji yangu miwili ya Kilwa Kivinje na Kilwa Masoko ni sehemu ya kunufaika na mradi huu. Hapa ndio sehemu pakee ambapo Mheshimiwa Waziri utakuja kuweka alama ambayo kwa miaka sita ilikuwa inashindikana na wengine walikuwa wanabeza. Naomba nikupe taarifa katika maeneo ambayo walikuwa wanabeza na walikuwa hawaamini katika mradi huu ni pamoja na Kilwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri kabisa amesema kwamba mikataba itasainiwa kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha. Maana yake ni kwamba kabla ya tarehe 30 Juni niombe na niungane na wengine kwamba mikataba hii ikasainiwe site huko ili wananchi wakashuhudie na inapowezekana basi tuma timu ya wataalam wako katika Wizara waende wakasimamie mikataba hii na sisi kwa niaba ya wananchi tutakwenda kuisimamia mikataba hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuishauri Wizara hii ni kujengea uwezo RUWASA, tunafahamu kwamba kwa mfano, mimi binafsi Meneja wangu wa RUWASA Engineer Mabula pale Kilwa anafanyakazi vizuri, anajituma sana kijana wa watu, lakini kinachopungua kwake ni mambo matatu tu na inawezekana hili ikawa na wengine pia. Jambo la kwanza bado anakaimu kama ilivyokuwa kwa wengine, jambo la pili ana timu ndogo ya watendaji wanaomsaidia kazi, lakini jambo la tatu vitendea kazi ikiwemo magari hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba utakapokuja kuhitimisha hapa kesho utoe majawabu ya changamoto hizi tatu za upungufu wa watumishi, Mameneja wanaokaimu pamoja na vitendea kazi ikiwemo na magari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo nilitaka nichangie katika bajeti ya Wizara ya maji ni kuhusiana na ahadi ambayo ilitolewa na aliyekuwa Waziri wa Maji wakati ule, katika Kata ya Limalyao, ilikuwa ni mwaka 2009 wakati Waziri wa Maji akiwa Mheshimiwa Prof. Mwandosya. Kata ya Limalyao Mheshimiwa Waziri ndio kata pekee katika Jimbo la Kilwa Kusini ambayo haina uhakika wa maji hata tone. Na Mheshimiwa Waziri Mwandosya wakati ule aliahidi kuchimba bwawa la kuweza kutosheleza kata nzima. Naomba nikumbushe tena ahadi hii iwe katika maandiko na kumbukumbu za Wizara na iwekwe katika mpango wa utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niendelee kupongeza Wizara. Wewe binafsi Mheshimiwa Waziri umekuwa ni mwenye kutembea nchi nzima. Naibu wako Mheshimiwa Engineer Maryprisca amekuwa ni mwenye kutembea nchi nzima. Kwangu Kilwa Naibu Waziri amefika pale Nangurukuru akasikiliza changamoto za maji za wana- Kilwa pale na tulimpa changamoto ya Kilwa Singino ambako kulikuwa na shida ndogo sana, naomba nitoe taarifa tu kwamba, naishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwamba, changamoto ile ya tatizo la maji Singino imekwisha Mheshimiwa Waziri, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nitakuwa mchoyo wa shukrani bila kushukuru wadau wengine wa maendeleo. Pale Kilwa sisi tumepata mdau wa maendeleo katika eneo hili la maji ambaye ni Green World Foundation Jimbo la Kilwa Kusini peke yake ametuchimbia tukishirikiana na viongozi Madiwani na Wenyeviti wangu wa Vijiji, Wenyeviti wangu wa vitongoji tumeshirikiananaye vizuri tumepata visima 83 ambavyo vinakwenda kutatua tatizo au kupunguza changamoto yam aji katika Kata ya Kivinje, Kata ya Masoko pamoja na Kata ya Kikole. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nikumbushie ahadi ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri aliahidi hapa Bungeni nikiwa nimeuliza swali la nyongeza mwaka jana kuhusiana na ombi langu mahususi la kupatiwa kisima cha maji katika Kijiji cha Nainokwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe taarifa kwamba, ahadi ile bado haijatekelezwa, nimekuwa nikifuatilia mpaka kwa Katibu Mkuu, lakini ananiambia Habari za mipango, leo nimeamua niizungumze hapa bungeni. Mheshimiwa Waziri anayekuzingua kutekeleza ahadi ambayo Naibu Waziri aliahidi kunipa kisima cha maji kimoja NaiInokwe ni nani huko Wizarani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha huu, tarehe 30 Juni, tupatiwe maji kisima kimoja Nainokwe, ili tukatengeneze uhai na tukasababishe uhai kwa wana-Nainokwe na wana-Kilwa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kupata fursa hii ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Awali ya yote nianze kwa kuwapongeza sana mawaziri wote wawili, kwa maana ya Mheshimiwa Ulega na Mheshimiwa Naibu Waziri Silinde, ndugu zangu hawa, kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kuongoza sekta mbili hizi za Mifugo na Uvuvi. Mimi kwa upande wangu, kama mimi, binafsi sina shaka kabisa na Waheshimiwa Mawaziri hawa lakini pili niishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza kile ambacho sisi Wabunge tulipitisha katika Bunge lako kama mpango wa maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipitisha ujenzi wa bandari ya uvuvi pale Kilwa Masoko, nitoe tu taarifa kwamba ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ambayo mkataba wake ulisainiwa mwaka
jana mwezi wa sita unaendelea kwa kazi kubwa sana pale Kilwa Masoko; pongezi sana kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Wanakilwa kwa ujumla wao, lakini wana. Kilwa Masoko kwa upekee wanaomba sana itakapofikia hatua yoyote ile ama ya kuweka jiwe la msingi au kuzindua bandari hii Mheshimiwa Waziri tunaomba ushauri mamlaka husika, Mheshimiwa Rais aje afanye kazi hiyo pale wananchi waje wampe pongezi wakiwa live pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi wa Bandari ya Uvuvi pale Kilwa Masoko kulikuwa na changamoto ya wapiga kura wangu 54 kutolipwa fidia. Niliwahi kuzungumza katika Mkutano wa Nane wa Bunge hili, lakini pia niliwahi kuzungumza katika Kikao cha Pili cha Mkutano huu wa Kumi na Moja katika Bunge hili. Vilevile tarehe nne mwezi wanne nilizungumza na Mheshimiwa Waziri Ulega ofisini kwake kuhusiana na wananchi 54 ambao bado hawajalipwa fidia; tuliweka sawa mambo pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kutoa shukrani sana kwa Serikali lakini kupitia Wizara ya Uvuvi na kupitia kwa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana husika, Mheshimiwa Ulega. Ninayo furaha kumjulisha kwamba wananchi wangu 54 wakiwemo Fatma Musa Mjaka, Bibi Mwanawetu Zarafi, Mwanafadhila Sudi pamoja na Bwana Said Bungara a.k. a Bwege tayari wameshalipwa fidia ya bilioni 8.5. Sasa mambo ni mazuri hakuna tena mgogoro kati ya wananchi wangu na Serikali ya Awamu ya Sita. Pongezi sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge hili katika mpango wetu wa maendeleo wa miaka mitano, lakini kwa upekee wake katika bajeti ya Wizara hii mwaka jana tulipitisha kwamba tutajenga masoko ya samaki Kilwa Kivinje pamoja na Kilwa Somanga. Nielezee kwa masikitiko tu kwamba mpaka tunaelekea mwishoni mwa mwaka huu, sasa hivi tuko robo ya nne tumeianza hii hatujapata fedha yoyote kwa ajili ya ujenzi wa masoko ya samaki, Kilwa Kivinje na pale Kilwa Samanga. Nitumie fursa hii kuikumbusha Wizara sisi wana-Kilwa Kivinje na wana-Kilwa Somanga bado tunahitaji masoko haya kutokana na uzalishaji mkubwa wa samaki katika maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti,nielezee mambo ambayo nimeyazungumza kupitia Wizara hii na kupitia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu mara kadhaa hapa Bungeni kuhusiana na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 20202 ambazo zimekuwa kikwazo kwa wavuvi wetu. Niliwahi kuuliza swali la msingi hapa ili kufahamu ni lini Wizara ya Mifugo na Uvuvi itabadilisha kanuni hizi; Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana sasa hivi Mheshimiwa Ulega wakati huo akiwa Naibu Waziri alijibu swali hili kwamba muda si mrefu kanuni hizi zinakwenda kubadilishwa. Kwa masikitiko niseme kwamba kilichofanywa na Wizara ni kubadilisha kanuni za tozo peke yake lakini kanuni za usimamizi wa masuala ya Bahari ambazo ni kikwazo kwa wavuvi wetu bado hazijabadilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme tu kwamba wakati anajibu vile Mheshimiwa Ulega alikuwa ni Naibu Waziri, sasa ni Waziri kamili; nenda kabadilishe kanuni hizi kwa maslahi ya wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge hili bajeti ya mwaka jana ya Wizara hii tulipitisha hapa kwamba Wizara hii itakwenda kununua boti 320 kwa ajili ya kukopesha wavuvi wetu, lakini taarifa ya hotuba ya Waziri hapa leo anatuambia mpaka sasa hivi boti zilizogawiwa ni 150 tu. Hizi zingine zaidi ya 150 zinasubiri nini kupelekwa kwa wavuvi wetu katika maeneo mbalimbali katika ukanda wetu wa Bahari lakini pia katika ukanda wa maziwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapenda kuona wavuvi wetu wasotee kule Mkuranga kwa Mheshimiwa Ulega wanapata boti hizi. Tunapenda kuona wavuvi wetu wa Mafya kule Bwajuu kwa Mheshimiwa Kipanga wanapata boti hizi, tunapenda kuona wavuvi wetu wa Msanga Mkuu kule Mtwara kwa Mheshimiwa Mtenga wanapata bodi hizi. Tunapenda kuona wavuvi wetu wa maeneo ya Pwani, Kibiti, Tanga, Dar es Salaam na kwenye maziwa yetu wanapata boti hizi; ndio utakaokuwa ukombozi pekee kwa wavuvi wetu kuinua uchumi katika sekta hii ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nizungumzie suala la migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji. Migogoro ya ardhi ya wakulima na wafugaji hili lipo ndani ya Wizara hii. Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakiratibu vema na Wizara zingine ikiwemo TAMISEMI, migogoro hii wanaimaliza. Nieleze tu kwamba juhudi kadhaa zimefanyika na Serikali lakini migogoro hii bado ipo. Nitoe tu mfano hapa, mimi katika jimbo langu la Kilwa Kusini bado migogoro hii bado ipo, ukienda Kikole migogoro ipo, ukienda Nanjirinji migogoro ipo, ukienda Kilanjelanje migogoro bado ipo; lakini hata jimbo jirani kwa jirani yangu pale kwa Mheshimiwa Ndulane kule Kilwa Kaskazini ukienda Nginjo, Mitole, Miguruwe, Kandalale bado migogoro ipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti,tatizo ni nini? Wakati utaratibu wa kupeleka mifugo unafanyika katika maeneo yote mikoa ya kusini; utaratibu na makubaliano ulikuwa kwamba Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi ikaweke maandalizi ya kupokea hawa wafugaji, lakini mandalizi hayo hayajafanyika, kulikoni? Nitumie fursa hii kuikumbusha Serikali hebu wakaweke utaratibu wa kupokea hii mifugo ili wafugaji waishi vizuri, malambo yawepo, majosho yawepo na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji ikomeshwe na imalizwe kabisa na Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti,baada ya hapo naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia neema ya uhai na uzima. Nitumie fursa hii kumpongezaza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujitoa yeye mwenyewe kwa kucheza filamu ya Royal Tour ambayo imeinua sekta ya utalii hapa nchini. Nipongeze pia uongozi wa Wizara kwa kazi za kutumikia Watanzania kwa moyo na bidii kubwa.

Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwakumbusha kuwa Wizara hii imepewa jukumu kubwa la uhifadhi wa maliasili zetu. Uhifadhi huu ni kwa aijili ya matumizi na manufaa kwa Watanzania. Tungependa kuona kuwa uhifadhi huu unawasaidia Watanzania na usiwe kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, pale Kilwa Kisiwani kumetangazwa kuwa ni sehemu ya urithi wa dunia na Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori (TAWA) imepewa jukumu la usimamizi wa eneo hili la utalii ambapo Serikali imeboresha miundombinu ili iwe rafiki kwa aijili ya watalii wanaokuja Kilwa kujionea historia ya Kilwa Kisiwani mji ambao ulikuwa wa kwanza katika Pwani ya Afrika Mashariki kujitengenezea fedha zake yenyewe. Tunachokumbusha hapa ni kwamba Serikali itimize wajibu wake wa kutoa CSR kwa Wana-Kilwa Kisiwani kwa kuwajengea miundombinu ya shule ya msingi na zahanati kama ambavyo tumetarajia.

Mheshimiwa Spika, Kilwa Kivinje ni miongoni mwa maeneo yenye historia kubwa hapa nchini; Kilwa Kivinje ndipo palipokuwa na soko la watumwa; Kilwa Kivinje ndipo palipokuwa ni njia ya kusafirisha watumwa; na Kilwa Kivinje ndipo palipokuwa makazi ya Waarabu na baadae Makao ya Wajerumani. Serikali ichukue hatua ya kukarabati soko lile lililokuwa la watumwa ili liendelee kubaki katika uhalisia wake kulinda historia. Pia Serikali ikarabati na kuhifadhi magofu ya Kilwa Kivinje ili kulinda historia na kuifanya Kilwa Kivinje kuwa ni sehemu ya utalii katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, mwisho, katika Kijiji cha Mchakama, Mavuji, kuna msitu wa hifadhi unaosimamiwa na TFS kwa upande wa Kusini Mashariki mwa kijiji. Kwa upande wa Kusini-Magharibi, kijiji kimepitiwa na Mto Mavuji ambao ni chanzo cha maji na tunachoendelea kukihifadhi kwa kuzingatia sheria ya kutoingilia eneo la mita 60 kutoka ukingo wa mto. Kwa muktadha huo, kijiji kimebakiwa na eneo dogo la makazi na taasisi za pale kijijini. Wananchi wanakosa eneo la kufanya shughuli za kiuchumi. Wananchi wangu kutoka Mchakama walituma uwakilishi wao mwaka jana kuja Dodoma kukutana na Waziri wa Maliasili na Utalii kwa lengo la kuomba wapatiwe sehemu ya hifadhi ya msitu kwa ajili wa shughuli za kiuchumi. Niliongozana na uwakilishi huo hadi ofisini kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mary Masanja na kukabidhi barua ya maombi yetu yakiambatana na muhtasari wa kijiji.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa bado Wana-Mchakama hawajajibiwa ombi lao na hatujaona hatua ya Wizara ya kugawa eneo la hifadhi ili wanakijiji wapate kufanya shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo bila kukiuka sheria. Tunakumbusha hapa, maombi yetu yafanyiwe kazi ili wananchi wale wapate eneo kufanyia shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Wizara hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili nami jioni hii ya leo niweze kutoa mchango wangu wa maoni katika Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, kwa upande wangu binafsi, kipekee kabisa lazima niishukuru Wizara na Uongozi wa Wizara kwa maana kile ambacho nilikiwasilisha mwaka 2021, karibu asilimia 66 kimechukuliwa na Wizara na kufanyiwa kazi. Naishukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upekee kabisa niishukuru na niipongeze Serikali ambapo mwaka 2021 wakati nachangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara hii, nilishauri kwamba katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo, lengo la Serikali la kujenga Bandari za Uvuvi, Kilwa Masoko ifikiriwe na iwekewe kipaumbele kwa sababu kuna kina cha asili. Nashukuru Wizara imepokea hili na limefanyia kazi na mpango huu sasa unakwenda kutekelezwa. Pongezi sana kwa Rais Samia, Serikali ya Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini rai yangu katika mpango huu wa Bandari ya Uvuvi ambayo inakwenda kuanza kujengwa mwishoni mwa mwezi huu kama ambavyo Hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeelezea katika ukurasa wa 104, kwamba ameshapatikana Mkandarasi ambaye ni China Harbour Engineering Co. Limited, na mchakato wa kuanza ujenzi unaanza mwisho wa mwezi huu wa Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu nini katika hili? Moja, ni kwamba wakati tunajenga bandari hii, ilikuwa ni finyu kwa mahitaji ya wakati huo na kwa maana hiyo sasa hivi inakwenda kupanuliwa. Kwa maana hiyo, pembezoni mwa eneo la bandari na gati kuna miundombinu mingine ikiwemo makazi pamoja na nyumba nyingine kwa matumizi mbalimbali. Tafsiri yake ni kwamba kunahitajika kulipia fidia kwa waliokuwa wanahusika na maeneo haya. Naomba Wizara ikahakikishe inalipa fidia kwa wakati ili kuepukana na migogoro tunapokwenda kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kama hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu ya pili katika eneo hilo, bandari hii inakwenda kufungua fursa nyingi sana ikiwa ni pamoja na viwanda vya kuchakata samaki pamoja na mazao mengine ya bahari. Naomba na nitoe rai sana kwa Wizara, viwanda hivi visiende kutengenezwa au kujengwa kilomita 100 kutoka maeneo ya uzalishaji. Itakuwa ni jambo la ajabu, na la kituko, na la kuongeza gharama zisizo na sababu. Sisi Kilwa tuna ardhi ya kutosha ya kuweza kupanua viwanda hivi vya kuchakata, kusindika, mazao ya bahari pamoja na samaki kwa sababu uzalishaji utakuwa mzuri kwa kuwa bandari iko pale pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu nyingine, tunapozungumzia bandari ya uvuvi, tafsiri yake ni kwamba tunakwenda sasa kunasibisha pamoja na masuala mengine yanayoendana na uwepo wa bandari ya uvuvi ikiwemo Chuo cha Uvuvi. Tunapozungumza, tuna chuo chetu kikubwa maarufu cha uvuvi Mbegani, pia kuna chuo kingine kidogo cha Mtwara Mikindani. Kwa fursa hii ya uwepo wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko, naomba Chuo cha Uvuvi kijengwe Kilwa Masoko na eneo la kutosha tunalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho katika rai yangu kwenye eneo hili la bandari, litaendana na uwepo wa miundombinu mingine rafiki kwa ajili ya kuwezesha bandari yetu sasa ifanye kazi vizuri. Hapa sasa nakusudia kuzungumza kwa Kimatumbi, maana yake tunahitaji access roads to the port. Kwa maana hiyo sasa, barabara tuliyonayo ya kilomita karibu 30 kutoka bandarini Kilwa Masoko mpaka Nangurukuru ilikuwa ya viwango vya wakati huo kwa matumizi ya kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, ihakikishe kwamba kilomita 30 hizi za kutoka Bandari Kilwa Masoko mpaka Nangurukuru, zinakuwa katika viwango kwa ajili ya matumizi bandari kubwa ya uvuvi. (Makofi)

Mheshmiwa Naibu Spika, baada ya eneo hilo la bandari ya uvuvi, niendelee kukumbusha rai ambayo niliitoa mwaka 2021 wakati nachangia Wizara hii, kwamba kutokana na uzalishaji mkubwa wa samaki Kilwa, hususan Kilwa Kivinje, tunahitaji soko la samaki pale Kilwa Kivinje. Bahati mbaya sana katika mapitio ya mpango wa bajeti hii inayoishia Juni, sijaona utekelezaji wala mipango.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na nikumbushe kwamba Soko la Samaki pale Kilwa Kivinje ni muhimu. Kama macho yangu hayakupitia vizuri wakati napitia bajeti na randama, basi Waziri atakapokuja kufanya sum-up aelezee hilo kwamba tuna mpango gani sasa wa kujenga Soko la Samaki pale Kilwa Kivinje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe takwimu; hatuzungumzi kwa ajili tu ya kupendelea kwa sababu Kilwa Kivinje tunahitaji Soko la Samaki, hapana, Mkoa wa Lindi peke yake, wavuvi ni zaidi 6,000. Katika wavuvi zaidi ya 6,000 wa Mkoa mzima wa Lindi, wavuvi zaidi ya 5,000 wanapatikana Wilaya ya Kilwa. Ndiyo maana tukasema ni fursa ya kutengeneza Soko la Samaki Kilwa Kivinje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, nije sasa katika Sera, Sheria na Kanuni kama ambavyo Hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeelezea ukurasa wa 109 mpaka 110. Kwenye eneo hili, nashukuru hatua za awali zimeanza. Mwaka 2021 wengi tulichangia sekta hii ya uvuvi na tulikuwa tukilalamikia mabadiliko ya Kanuni za uvuvi za mwaka 2020, ndiyo kilio kikubwa cha wavuvi wetu. Masuala ya makatazo ya uvuvi wa usiku, makatazo ya ring net na mambo mengine mengi ambayo tuliyajadili, ni kwa sababu ya mabadiliko ya kanuni ya mwaka 2020. Hapa mmesema mnakwenda kubadilisha Kanuni za Mwaka 2009, hazikuwa na matatizo makubwa sana, matatizo makubwa yalijitokeza kwenye mabadiliko au marekebisho ya Kanuni hizi za mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upekee wa mwaka 2021 nilitoa kifungu ambacho ndiyo kimeleta changamoto zote hizi. Naomba nirudie hapa, hiki ni Kifungu cha 66 au Kanuni ya 66 ya mabadiliko ya Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2020, Kanuni ndogo ya kwanza na kifungu dada (d) na Kifungu gaga (g), vikaangaliwe kwa umakini. Mmeitisha wadau wa uvuvi, mmeitisha Kamati ya kupitia mapendekezo yenu, Kamati ya Sheria Ndogo; nilitamani sana sisi ambao tunaotoka kwenye sekta za uvuvi tungealikwa ili tutoe hizi inputs ambazo sisi ndio wadau husika, tunajua taratibu za uvuvi. Kama mtaitisha tena Kamati ya kupitia, kwa maana ya Kamati ya Sheria Ndogo, nitoe rai sana, sisi tunaotoka kwenye sekta za uvuvi tualikwe tukatoe maoni yetu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa, ni kengele ya pili. Ahsante.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, muda umeisha! Basi mengine nitachangia kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)