Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon Sagini Jumanne Abdallah (128 total)

MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawatambua watu wenye haki ya Uraia ili wapate Vitambulisho vya Taifa pamoja na kuwapa Uraia watu ambao siyo raia lakini wameishi nchini kwa zaidi ya miaka kumi na tano?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwa na afya na leo kushiriki kwenye kikao cha Bunge.

Mheshimiwa Spika, pia nimshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuniamini kuwa mmoja wa wasaidizi wake katika nafasi ya Naibu Uwaziri. Ahadi yangu kwake ni kutekeleza majukumu haya kwa uadilifu, uaminifu na bidIi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, nikupongeze kwa kuchaguliwa kwa kura zote kuwa kiongozi wetu wa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo sasa, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na zoezi la kuwatambua na kuwapatia vitambulisho wale wote wanaostahili. Aidha, zoezi hili ni endelevu kwa kuwa kila mwaka idadi ya watu wanaofikisha umri na vigezo vya kutambuliwa na kusajiliwa inaongezeka. Aidha, idadi ya wageni wakazi na wakimbizi wanaoingia nchini imekuwa ikiongezeka na hivyo kuhitaji kusajiliwa na kutambuliwa ili kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utaratibu wa kuwapatia uraia wa Tanzania (Tajnisi) wageni ambao wanaomba uraia wa Tanzania ikiwa wamekidhi sifa na vigezo vya kutajnisiwa uraia kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Sura ya 357, Toleo la Mwaka 2002 na Kanuni zake. Ahsante.
MHE. HAJI AMOUR HAJI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuwa na Chombo Maalum (Agency) kitakachosimamia shughuli zote za kampuni binafsi za ulinzi ili kuongeza wigo wa kiutendaji pamoja na kuwepo kwa sheria itakayosimamia kampuni hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Amour Haji, Mbunge wa Pangawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali haioni sababu ya kuanzisha chombo maalumu (Agency) cha kusimamia makampuni binafsi ya ulinzi. Jeshi la Polisi linatosha kusimamia shughuli za makampuni hayo kama ilivyo sasa kwa sababu ndiyo taasisi iliyopewa mamlaka kisheria ya kutoa leseni na hati za umiliki wa silaha hapa nchini ambazo pia humilikiwa na makampuni hayo. Utaratibu huo hutoa urahisi wa kufuatilia mwenendo wa makampuni katika utunzaji na matumizi ya silaha hizo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa sheria itakayosimamia makampuni binafsi ya ulinzi. Tayari mapendekezo ya kutungwa kwa sheria hiyo yapo kwenye hatua zaa awali za mawasiliano baina ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Baada ya maridhiano kati ya Serikali zetu mbili kufikiwa, maandalizi ya sheria hiyo yataendelea kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya ziara kwenye Vituo vya Polisi vya zamani na nyumba za kuishi Askari Unguja na Pemba ili kushuhudia uchakavu uliopo na ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya Vituo vya Polisi nchini kwa Mwaka 2021/2022?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilishatembelea na kuona uchakavu wa vituo vya polisi na nyumba za makazi ya askari huko Zanzibar na maeneo mengine ya Tanzania Bara. Zoezi la kufanya tathmini ya uchakavu kujua gharama zinazohitajika ili kufanya ukarabati zinaendelea nchi nzima. Zoezi hili litakapokamilika, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ukarabati kulingana na upatikanaji wa fedha kwa mwaka ujao (2022/2023) kama ilivyofanyika mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi 2,000,000,000 kwa ajili ya ukarabati wa Vituo vya Polisi na ujenzi wa nyumba za askari. Ahsante sana.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vya Polisi katika maeneo ya mpakani wilaya ya Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya mpakani mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika Wilaya ya Nkasi kuna vituo vitano vya Polisi vya daraja C, ambavyo ni kituo cha Wampembe, kituo cha Namansi, Kipili, Kilando na Kabwe. Vituo hivi vinatoa huduma kwa wananchi kwa saa 24. Pia kuna tarajiwa kujengwa kituo kingine cha Polisi cha Daraja C katika eneo la Mpasa. Vituo vyote hivyo vinakidhi mahitaji ya kutoa huduma katika eneo la mpakani kando ya ziwa Tanganyika katika Wilaya ya Nkasi. Aidha, Serikali imepanga kuimarisha huduma kwenye vituo hivyo kwa kuvipatia usafiri stahiki hatua kwa hatua kulingana na upatikanaji wa fedha. Nakushukuru.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italeta Muswada Bungeni ili kuboresha Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 kutokana na Sheria hiyo kupitwa na wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kupitia na kuboresha Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973. Maboresho ya sheria hiyo yamefanyika ambapo muswada wenye marekebisho hayo ulisomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Mbili, tarehe 30 Juni, 2021. Muswada huo uliwasilishwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama tarehe 17 Agosti, 2021 ambapo ushauri na maoni ya Kamati yalizingatiwa. Hatua inayofuata ni kufikishwa Bungeni ili kusomwa kwa mara ya pili na tatu hatimaye kuridhiwa.
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS aliuliza: -

Je, ni sababu gani iliyopelekea vituo vidogo vya Polisi Kidongo Chekundu, Jang’ombe na Beit El Ras visifunguliwe na kufanya kazi kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis, Mbunge wa Kuteuliwa (Baraza la Wawakilishi), kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vituo vya Polisi vya Kidongo Chekundu kilichojengwa mwaka 1993, Jang’ombe kilichojengwa mwaka 2018, na Beit El Ras kilichojengwa mwaka 1994 ni vituo vidogo vya polisi vilivyoko Wilaya ya Mjini Magharibi. Vituo hivi vilifungwa mwaka 2019 kutokana na upungufu wa askari. Kwa sasa Kituo cha Polisi Jang’ombe kimefunguliwa na kinafanya kazi saa 24 baada ya kupangiwa askari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pindi askari walioko Shule ya Polisi Moshi watakapohitimu mafunzo ya awali, kipaumbele cha ugawaji wa polisi hao kitakuwa kwenye maeneo yenye upungufu wa askari ikiwemo Wilaya ya Mjini Magharibi ili kuwezesha vituo vilivyofungwa viweze kufunguliwa tena. Nashukuru.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itanunua Magari ya kisasa ya Zimamoto ili kunusuru maisha ya raia na mali zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa mpango mkakati wa kuimarisha huduma za zimamoto na uokoaji nchini kwa kuimarisha na kuongeza vifaa vya kisasa vya utendaji kazi katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Vifaa hivi vya kisasa vitaenda sambamba na upelekaji wa huduma ya zimamoto na uokoaji katika wilaya zote ambazo hazina huduma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini imetenga bajeti ya maendeleo ya shilingi bilioni 2 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kununua magari mapya ya kisasa ya zima moto. Lengo la ununuzi wa magari haya ni kuongeza ufanisi kwenye shughuli za kuokoa maisha na mali za wananchi, pindi patokeapo ajali za moto na nyingine. Taratibu zote za ununuzi zikikamilika, magari ya kuzima moto yatapelekwa mikoa isiyokuwa na huduma ya zimamoto na uokoaji. Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka ili kuliwezesha vitendea kazi stahiki Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuhamisha Gereza la Mkoa wa Iringa ili kuondoa muingiliano uliopo kati ya Gereza hilo na Hospitali ya Mkoa wa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali bado ina mpango wa kuhamisha Gereza hilo kwani eneo kwa ajili ya kuhamishia Gereza hilo, lilishapatikana maeneo ya Mlolo na Mbunge anafahamu jambo hilo. Kwa kuanzia Jeshi la Magereza lilishafungua kambi ijulikanayo kwa jina la Kambi ya Mlolo. Katika kambi hii zimejengwa nyumba 20 za watumishi na mabweni manne, kwa kutumia bajeti kidogo iliyokuwa inatengwa na Serikali kupitia vyanzo vya ndani vya Jeshi.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa iliyokuwepo ni ufinyu wa bajeti hali inayopelekea kushindwa kutekeleza mpango huu. Aidha, kwa sasa gharama za ujenzi wa Gereza hilo zimeshaanza kupitiwa upya ili ziweze kuwekwa katika Mpango wa Maendeleo kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapenda kutoa pongezi nyingi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa juhudi zake kupitia Mkuu wa Magereza wa Mkoa ambapo amekuwa mstari wa mbele kufuatilia maendeleo ya mpango huu. Aidha, natoa rai kwa wadau mbalimbali wa maendeleo waweze kujitokeza kuunga mkono juhudi za Serikali katika utekelezaji wa mpango huu. Nashukuru. (Makofi)
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -

Je ni lini Serikali itafanya ukarabati wa nyumba za makazi ya askari wa Jeshi la Polisi kwenye Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Igunga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba nyumba za makazi ya askari Kituo cha Polisi Wilaya ya Igunga ambazo ni nyumba nne zenye kuishi familia 20 zimechakaa. Tathmini kwa ajili ya kubaini kiwango cha uchakavu na gharama za ukarabati imefanyika na kubaini kuwa kiasi cha shilingi 165,000,000.00 zitahitajika. Serikali imepanga kuanza kufanya ukarabati wa vituo na makazi chakavu ya askari wa jeshi la polisi, yakiwemo ya kituo cha polisi Wilaya ya Igunga kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga kituo kipya cha Polisi katika Wilaya ya Chakechake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge Wa Chakechake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi lina eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Shehia ya Vitongoji lenye ukubwa wa mita za mraba 1,496. Mpango wa Serikali ni kutenga fedha katika bajeti ya mwaka ujao 2023/2024 ili ujenzi uanze. Nashukuru.
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA K.n.y MHE. JANEJELLY J. NTATE aliuliza: -

Je, ni lini serikali itamaliza ujenzi wa Kituo cha Polisi Mbande Kata ya Chamazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi cha Mbande ambacho ni cha Daraja B kilianza kujengwa kwa kutumia Shilingi 16,000,000 zilizochangwa na wananchi mwezi Agosti 2016. Kwa kutumia Shilingi 38,000,000 zilizochangwa na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mradi wa SONGAS na Kampuni ya Tatu Mzuka ujenzi uliendelea hadi upauaji mwaka 2020.

Mheshimwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi, ilitoa Shilingi 30,826,500 mwezi Juni, 2022 ili kuendeleza na kukamilisha ujenzi huo. Hadi sasa milango, grills za madirisha, mfumo wa majisafi na majitaka, umeme na blundering vimekamilishwa. Ni matarajio yetu kuwa Kituo hicho kitakamilika na kuanza kutumika kabla ya mwezi Novemba, 2022. Ninakushukuru.
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA K.n.y. MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kurahisisha upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kuhakikisha watu wote wanaokidhi vigezo vya usajili na utambuzi wanasajiliwa kwa urahisi. Ili kufikia lengo hilo, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inatekeleza mikakati ifuatayo: -

(i) Kufungua ofisi za usajili na utambuzi katika Wilaya zote Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo jumla ya ofisi 152 zimefunguliwa katika Wilaya 150;

(ii) Kuendelea kufanya usajili na utambuzi wa wananchi kupitia ofisi za Mamlaka za Wilaya na kuendesha mazoezi ya usajili wa watu wengi (Mass registration); na

(iii) Ugawaji vitambulisho kwenye ngazi za msingi yaani Kata/Shehia na vijiji ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati hiyo husaidia kupunguza usumbufu na gharama za usajili kwa wananchi. Nashukuru.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -

Je, Serikali inaweza kuongeza uhai wa paspoti za muda wanazopewa Madereva hadi kufikia Miezi sita?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Pasipoti za muda wanazopewa madereva ni hati za dharura za safari (Emergency Travel Documents) ambazo kwa mujibu wa Sheria ya Pasipoti na Hati za Safari ya Mwaka 2002, hutolewa kwa safari moja kwa muda ulioainishwa ndani ya hati husika. Aidha, hati hii ya safari hutolewa kwa waombaji wenye safari za dharura.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa suala la kuongeza muda wa hati za dharura za safari litahitaji mabadiliko ya sheria endapo itaridhiwa, Serikali inawashauri madereva kuomba pasipoti ili kuepuka usumbufu wa kuomba hati za dharura za safari mara kwa mara kwa vile safari zao siyo za dharura. Nashukuru.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -

Je, ni ipi kauli ya Serikali juu ya ajali zinazosababishwa na bodaboda kwa kutoa sight mirror?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Fakharia Shomar Khamis Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya usalama barabarani Sura ya 168 ya mwaka 1973 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, Kifungu 39 (1) inayotumika Tanzania bara, na sheria ya usafiri barabarani Sura ya 7 ya mwaka 2003, Kifungu cha 22 inayotumika Zanzibar zinatamka kuwa ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kuendesha chombo cha moto barabarani ikiwemo gari na pikipiki bila kuwa na vifaa kamili ikiwemo sight mirrors kwani chombo hicho kitahesabika kuwa ni kibovu.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kuwa, mtu yeyote anayeendesha chombo cha moto zikiwemo pikipiki za biashara (bodaboda) kufuata sheria na kutotoa sight mirror kwenye pikipiki. Kitendo cha kutoa sight mirror ni kukiuka sheria na mhusika atapaswa kukamatwa na kutozwa faini ya papo kwa papo au kufikishwa mahakamani na chombo chake kuzuiwa hadi akirekebishe.
MHE. GRACE V. TENDEGA K.n.y. MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Mkalama?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mkalama ni Kituo cha Daraja A. Ujenzi wake ulianza mwezi Juni, 2015 na ulisimama kutokana na kukosekana kwa fedha. Katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi 467,148,000 ili kukamilisha ujenzi wa kituo hiko. Nashukuru.
MHE. SAADA MONSOUR HUSSEIN aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kunusuru maisha ya vijana wa kike kwa kudhibiti wimbi la mauaji Visiwani Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saada Mansour Hussein, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kufuatilia kwa karibu matukio ya mauaji yanayotokea maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo Zanzibar. Matukio haya tumebaini yanasababishwa na migogoro ya ardhi, wivu wa kimapenzi na migogoro ya ndoa, imani za kishirikiana, wananchi kujichukulia sheria mikononi, ulevi, na matukio ya uhalifu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba 2022 jumla ya matukio manne (4) ya mauaji ya wanawake yametokea Zanzibar. Matukio haya yamehusishwa na wivu wa mapenzi na migogoro katika ndoa.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi itaendelea kutoa elimu kwa jamii kufuata sheria za nchi na njia sahihi za kutatua migogoro ya aina hiyo. Tunawashauri wahusika kuzishirikisha familia zao, viongozi wa dini, viongozi wa jamii, viongozi wa siasa, wazee wa mila, watu maarufu na wenye ushawishi katika jamii pamoja na Ofisi za Serikali za Mitaa ili kupunguza athari za migogoro hiyo. Aidha, kwa migogoro inayoshindikana ifikishwe katika vyombo vya dola hususan Polisi na Mahakama ili kupata suluhisho la kisheria.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanzisha Vituo vya Polisi katika Tarafa za Gonja na Mamba/Vunta?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na vituo vya Polisi katika maeneo mbalimbali nchini. Katika Tarafa ya Gonja kuna Kituo cha Polisi cha Daraja B kinachoongozwa na Mrakibu Msaidizi wa Polisi na kina Askari 16 na gari moja. Tarafa ya Mamba haina Kituo cha Polisi wala haijatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo na makazi ya Askari. Hivyo tarafa, hiyo hupata huduma za Polisi toka kituo cha Polisi Gonja na vituo vidogo vya Polisi vya Kihurio na Ndungu vilivyo katika Tarafa ya Mamba.

Mheshimiwa Spika, ni ushauri wetu kwa Mheshimiwa Mbunge kushirikisha Halmashauri ya Wilaya ya Same kutenga eneo katika Tarafa ya Mamba kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi, pamoja na nyumba za makazi ya Askari ili Serikali iweze kuingiza katika mpango wa kukitengea bajeti ya ujenzi.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati wa Kituo kidogo cha Polisi cha Chaani Lungalunga.?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, Mbunge wa Chaani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo kidogo cha Polisi cha Chaani, Lungalunga kilichopo Wilaya ya Kaskazini A ni kituo kilichojengwa kwa kushirikisha jitihada na nguvu za wananchi. Jengo la kituo hiki ni chakavu na haliwezi kufanyiwa ukarabati kwa sababu kuta zake zimeweka nyufa nyingi na kingo za jengo zimebomoka.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi Kamisheni ya Zanzibar imeshaandaa mchoro na makadirio kwa ajili ya kujenga Kituo kipya cha Daraja C katika eneo hilo. Kiasi cha fedha, shilingi 82,530,960 kinahitajika kwa ajili ya ujenzi huo, na zitaingizwa katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 kulingana na upatikanaji wa fedha. Nashukuru.
MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya usafiri katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asya Sharif Omar, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022 Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba umepatiwa magari matatu yaliyonunuliwa na Serikali ili kupunguza uhaba wa magari katika Mkoa huo. Serikali itaendelea kununua magari na pikipiki kila mwaka na kuzigawa katika Mikoa na Wilaya zenye uhitaji mkubwa ikiwemo Mkoa wa Kaskazini na Kusini Pemba. Nashukuru.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Vituo vya Polisi vya Nyamagana, Keza na Djululigwa vilivyojengwa na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini jitihada na michango ya wananchi katika kujenga vituo vya Polisi nchini. Vituo vidogo vya Polisi vya Nyamagana, Keza na Djululigwa ambavyo viko Wilaya ya Ngara, ni vituo vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi. Tathmini imefanyika na kubaini kuwa kiasi cha shilingi 125,000,000 kitahitajika ili kugharamia uwekaji wa mfumo wa umeme na maji, kupiga plasta, kuweka sakafu, dari, milango, madirisha, samani na kupaka rangi. Serikali kupitia Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau inatafuta fedha ili kuweza kumalizia kazi ya ujenzi huo.
MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati wa Kituo cha Polisi cha Konde katika Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Saidi Issa, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uchakavu wa Kituo cha Polisi cha Konde ambacho jengo lake lilijengwa wakati wa ukoloni. Tathmini kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho imefanyika na kubaini kwamba kiasi cha fedha Sh.42,000,000/= kinahitajika ili kugharamia ubadilishaji paa, kubadilisha mfumo wa umeme, maji safi na maji taka, kuziba nyufa, kubadilisha dari na kupaka rangi. Ukarabati huo utafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Serikali inawahamasisha wadau walio tayari kushirikiana na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wilaya katika kuboresha vituo vya Polisi vilivyo kwenye maeneo yao.
MHE. MOHAMED ABDULRAHMAN MWINYI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi Jimbo la Chambani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdulrhman Mwinyi Mohamed Mbunge wa Chambani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Chambani liko katika Wilaya ya Mkoa wa Kusini Pemba. Wilaya hii ina vituo vya polisi vine ambavyo ni Mkoani, Kengeja, Mtambile, na Mkanyageni. Wananchi wa Chambani wanapata huduma ya polisi kwenye vituo vya Mtambile na Kengeja ambavyo viko ndani ya kilometa sita.

Kwa sasa Serikali kupitia Jeshi la Polisi linatarajia kujenga Vituo vya Polisi maeneo ya vitongoji, Pujini, Wesha na Gombani Wilayani Chakechake ambayo ina kituo kimoja tu cha Polisi katika mkoa wa Kusini Pemba.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA K.n.y. MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kulipatia Jeshi la Polisi magari mapya kama moja ya vitendea kazi ili litekeleze majukumu yake ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kulipatia Jeshi la Polisi magari kama nyenzo ya kutendea kazi. Mkakati wa Serikali ni kutenga fedha kwenye Bajeti yake kila mwaka ili kununulia vitendea kazi muhimu yakiwemo magari na pikipiki. Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Jeshi la Polisi limetengewa kiasi cha Shilingi Bilioni 15 kwa ajili ya ununuzi wa magari 101 na pikipiki 336. Nashukuru.
MHE. HAJI AMOUR HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutunga Sera na Sheria ya Kampuni Binafsi za Ulinzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Amour Haji, Mbunge wa Pangawe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa Sheria na Sera inayosimamia kampuni binafsi za ulinzi. Kwa sasa Waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu mapendekezo ya kutunga Sheria ya Huduma za sekta binafsi za ulinzi umekamilika na utawasilishwa katika Baraza la Mawaziri kwa ajili ya maamuzi baada ya kupata maoni ya kina ya wadau wa pande zote mbili za Muungano juu ya Rasimu ya Sheria hiyo. Baada ya kukamilika kwa hatua hizo, muswada wa sheria utawasilishwa Bungeni.
MHE. CHARLES J. MWIJAGE aliuliza: -

Je, ni kwanini katika Tarafa ya Kamachumu mlalamikaji hulazimishwa kumgharamia mahabusu kwa kumsafirisha kwenda na kurudi rumande?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Charles John Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Polisi (Police Force and Auxiliary Service Act) Sura ya 322 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 na Kanuni 353 na 354 ya Kanuni ya Jeshi la Polisi (Police General Order) zinazosimamia watuhumiwa/mahabusu walioko kwenye Vituo vya Polisi, utaratibu wa kuwasafirisha watuhumiwa/mahabusu kwenda Mahakamani hutekelezwa na Jeshi la Polisi. Pia jukumu la kuwasafirisha watuhumiwa/mahabusu toka rumande Gerezani kwenda Mahakamani ni jukumu la Jeshi la Magereza kwa mujibu wa Kifungu cha 75 cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 ya mwaka 1967 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha mlalamikaji kulazimishwa kugharamia usafirishaji wa mtuhumiwa/mahabusu kwenda na kurudi rumande ni kukiuka Sheria na Kanuni zilizopo na kinatakiwa kuachwa mara moja. Wizara imefanya mawasiliano na Wakuu wa Vyombo vyetu, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mkuu wa Jeshi la Magereza (CGP) ili wawaelekeze wasaidizi wao ngazi za Mikoa na Wilaya kuzingatia sheria hiyo. Ninashukuru.
MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati katika Kituo cha Polisi Matangatuani Wilayani ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naenda kujibu swali la Mheshimiwa Asya Sharif Omar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi cha Matangatuani kilichopo Wilaya ya Micheweni ni kituo kilichojengwa siku nyingi na jengo lake ni chakavu. Katika tathmini iliyofanyika jengo hilo halifai kufanyiwa ukarabati kutokana na udhaifu wa kuta za jengo hilo. Serikali ina mpango wa kujenga Kituo kipya cha Polisi cha daraja "C". Michoro na makadirio yameshafanyika na kiasi cha Shilingi 427,604,929 kinahitajika kwa ajili ya kujenga Jengo la Kituo pamoja na nyumba mbili za makazi ya Askari. Fedha za ujenzi zinatarajiwa kuombwa kwenye Bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 kutegemea na upatikanaji wa fedha.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE auliza: -

Je, Serikali ni lini italeta Bungeni Muswada wa Sheria ya Kampuni Binafsi za Ulinzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa Sheria inayosimamia kampuni binafsi za ulinzi. Kwa sasa Waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu mapendekezo ya kutunga Sheria ya Huduma za Sekta Binafsi za Ulinzi umekamilika, na utawasilishwa katika Baraza la Mawaziri kwa ajili ya Maamuzi baada ya kupata maoni ya kina ya wadau wa pande zote mbili za Muungano juu ya rasimu ya sheria hiyo. Baada ya kukamilika kwa hatua hizo, Muswada wa Sheria hiyo utawasilishwa Bungeni. Nashukuru sana.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: –

Je, kuna mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi Tarafa ya Kintinku Manyoni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na Kituo cha Polisi pamoja na nyumba za makazi ya askari katika Tarafa ya Kintinku. Kwa sasa wakazi wa eneo hilo hupata huduma toka Kituo Kidogo cha Polisi kinachotumia jengo lililokuwa ghala la mazao ya kilimo waliloazimwa na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.

Mheshimiwa Spika, Serikali inamshauri Mheshimiwa Mbunge, ashirikiane na Uongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, kutenga eneo mahsusi kwa ajili ya kujenga kituo na nyumba za askari ili Serikali iweze kukiingiza kituo hicho katika mpango wake na kukitengea fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanzisha vituo vya Polisi katika Tarafa za Gonja na Mamba/Vunta?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge Wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na vituo vya Polisi katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi. Tarafa za Gonja na Mamba/Vunta hazina vituo vya polisi wala maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya polisi na Nyumba za Makazi ya Askari. Wananchi wa Tarafa za Gonja na Mamba/Vunta hupata huduma za polisi toka vituo vya polisi vya Same mjini na Gonja, na vituo vidogo vya polisi vya Kihurio na Ndungu.

Mheshimiwa Spika, ni ushauri wangu kwa Mheshimiwa Mbunge kushirikisha Halmashauri ya Wilaya ya Same kutenga maeneo katika tarafa za Mamba na Gonja kwa ajili ya kujenga kituo cha Polisi pamoja na Nyumba za Makazi ya Askari, ili Serikali iweze kuweka kwenye mpango wake wa Bajeti kwa ajili ya utekelezaji. Nashukuru. (Makofi)
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya ukosefu wa magari na nyumba za Askari Polisi Kituo cha Polisi Nungwi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki, Mbunge wa Nungwi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi Nungwi ni kituo cha Daraja C na kipo Mkoa wa Kaskazini Unguja. Pamoja na kufanya kazi mbalimbali za kipolisi, hushughulikia pia na kusimamia majukumu ya utalii.

Mheshimiwa Spika, Kituo hiki kinacho gari Na. PT. 3388, Toyota Landcruiser ambalo hutumika kwenye kazi za kila siku za polisi. Kutokana na udogo wa eneo la kituo, hakuna sehemu inayoweza kutosheleza kujenga nyumba za makazi ya askari polisi. Hivyo, Serikali inawashauri wadau wenye nyumba za kupangisha wapangishe askari wetu. Aidha, uongozi wa Mkoa Kaskazini Unguja unaombwa ushirikiane na uongozi wa jamii kupata eneo linalofaa kujenga nyumba za askari ili Serikali iingize ujenzi wa nyumba hizo katika mpango.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kudhibiti matukio ya ubakaji wa akina mama uliokithiri katika Jimbo la Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada zake za kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani watu wote wanaojihusisha na matukio ya uvunjifu wa sheria ikiwemo ya ubakaji. Aidha, Jeshi pia hutoa elimu kwa jamii kwa kuwashirikisha viongozi wa dini, mila na watu maarufu ili jamii iache kutenda makosa hayo. Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatoa wito kwa jamii yote kushirikiana kutokomeza matukio ya uhalifu hapa nchini yakiwemo ubakaji kwani yanasababisha athari kubwa kwa jamii, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Ofisi ya NIDA katika Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Jimbo la Wingwi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kujenga ofisi 31 katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa gharama ya dola za Kimarekani 84,924,918 sawa na fedha za Tanzania shilingi 197,094,598,943.58. Fedha hizo zinajumuisha mchango wa Serikali wa jumla ya dola za Kimarekani 14,924,918 na mkopo nafuu wa dola za Kimarekani 70,000,000 kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea ya Kusini. Wilaya ya Micheweni iliyopo Mkoa wa Kaskazini Pemba ni mojawapo ya Wilaya zitakazonufaika kwa kujengewa Ofisi ya Usajili na Utambuzi wa Watu. Ofisi hiyo itajengwa kwenye Kiwanja Na. 10, kilichopo Shehia ya Maziwang’ombe, huko Micheweni, ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, ni lini Vituo vya Polisi vya Tarafa ya Mang'ula na Kidatu vitakarabatiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uchakavu wa Vituo vya Polisi katika Tarafa za Mang'ula na Kidatu. Jengo la Kituo cha Polisi linalotumika Mang'ula ni mali ya Shirika la Reli Tanzania na Zambia -TAZARA, na jengo la Kituo cha Polisi linalotumika Kidatu ni mali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania -JWTZ. Mnamo tarehe 22 Novemba, 2021 Halmashauri ya Mji wa Ifakara ilitoa eneo la ekari nne kwa ajili kujenga Kituo cha Polisi cha Mang'ula na tarehe 23 Januari, 2023 uongozi wa Kata ya Kidatu ulitoa eneo la ekari mbili kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi. Taratibu za upimaji wa maeneo hayo zinaendelea kwa ajili ya kupata hatimiliki ili kuandaa michoro na hatimaye kuomba fedha kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Daraja C.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Mamlaka ya Upimaji (Halmashauri ya Mji wa Ifakara) waharakishe upatikanaji wa hatimiliki hizo ili mipango ya ujenzi wa vituo hivyo iweze kuandaliwa, nashukuru.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma za kipolisi jirani na maeneo ya wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwatum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa madhumuni ya kupeleka huduma za polisi jirani na wananchi, Jeshi la Polisi linatekeleza utaratibu wa kuwapangia kazi Wakaguzi wa Polisi kwenye maeneo ya kata na shehia zote hapa nchini. Mpaka sasa Wakaguzi wa Polisi 2,552 wameshapelekwa kwenye kata hizo 2,552 na...Sorry, naomba kurejea eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi linatekeleza utaratibu wa kuwapangia kazi Wakaguzi wa Polisi kwenye maeneo ya kata na shehia zote hapa nchini. Mpaka sasa Wakaguzi 2,552 wameshapelekwa kwenye kata na 288 wameshapelekwa kwenye shehia kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu ya Wakaguzi wa Polisi wanaopangwa kwenye kata na shehia ni kusimamia hali ya ulinzi na usalama kwenye maeneo yao na kushirikiana na wananchi kuanzisha na kusimamia vikundi vya ulinzi shirikishi, kushiriki vikao na mikutano ya vitongoji, vijiji, shehia na kata na ward ili kutatua changamoto za uhalifu na migogoro katika jamii, pia hushiriki kwenye mikutano ya kamati za maendeleo za kata ili kutoa ushauri kuhusiana na masuala ya ulinzi na usalama, nakushukuru.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaboresha jengo la Kituo cha Polisi Konde, Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk Mbunge wa Tumbe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uchakavu wa jengo la Kituo cha Polisi cha Konde kilichopo Wilaya ya Micheweni. Tathmini ya uchakavu ili kufanya ukarabati imefanyika mwezi Novemba, 2022 na kiasi cha fedha shilingi 92,000,000 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati huo. Fedha hizo zitatengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kilindi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua hitaji la Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kilindi. Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi imeshatoa eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 15,760 kwa ajili ya kujenga kituo daraja B, pamoja na nyumba za kuishi askari. Fedha za Ujenzi zinatarajiwa kutengwa kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/2024; nashukuru.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuzuia matukio ya mauaji, kujiua na ukatili uliokithiri hasa kwa wanawake na watoto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi itaendelea kuwakamata watu wote wanaotenda makosa yakiwemo ya mauaji na ukatili na kuwafikisha Mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. Uchunguzi wa Jeshi la Polisi unaonesha kuwa matukio haya kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na watu kujichukulia sheria mkononi, imani za ushirikina, wivu wa mapenzi, migogoro ya ardhi, migogoro kwenye ndoa, kugombania mirathi, ulevi na mmomonyoko wa maadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi itaendelea kutekeleza mkakati wa kutoa elimu na mafunzo kwa jamii ili wananchi wafuate sheria za nchi katika kutatua migogoro inayojitokeza au wanapodai haki zao. Aidha, wananchi wanaombwa kuwashirikisha viongozi wa kijamii, kimila, kisiasa na kiserikali, wazee au watu maarufu wanaotambulika na kuheshimika ili kuwaasa ipasavyo na hivyo kuepuka kuvunja sheria za nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Mji wa Mangaka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Yahya Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua hitaji la kujengwa Kituo cha Polisi kwenye mji wa Mangaka Wilaya ya Nanyumbu. Tathmini kwa ajili ya ujenzi imeshafanyika na kubaini kuwa kiasi cha shilingi 569,091,050 kinahitajika kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi Daraja B. Fedha hizo zinatarajiwa kutengwa kwenye Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2023/2024; nashukuru.
MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza magari ya kisasa ya zimamoto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salim Mussa Omar, Mbunge wa Gando kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji imekamilisha hatua zote za mkopo wa Euro milioni 4.9 kutoka Nchini Austria kwa ajili ya ununuzi wa magari 12 ya kuzima moto. Kati ya magari yanayonunuliwa mawili ni ya ngazi (Turntable ladder) kwa ajili ya kuzima moto katika majengo marefu. Aidha, Jeshi la Zimamoto na Uokozi linatarajia kupata magari matatu ya kuzimia moto ambayo yalipatikana kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 kutoka Shirika la Nyumbu Tanzania Automotive Technology Center (TATC).
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuwapatia wananchi wa Kyerwa Vitambulisho vya Taifa ili waondokane na adha wanayoipata?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Jimbo la Kyerwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Januari, 2023 jumla ya wananchi 112,518 wamesajiliwa na kutambuliwa Wilayani Kyerwa. Vilevile katika kipindi hicho jumla ya Namba za Utambulisho (National Identification Numbers) 31,897 sawa na asilimia 28.3 ya wananchi wote walioandikishwa zimezalishwa na kugawiwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo. Aidha, jumla ya Vitambulisho vya Taifa 19,614 sawa na asilimia 61.5 ya Namba za Utambulisho vimezalishwa na kugawiwa kwa wananchi wa Wilaya ya Kyerwa.

Mheshimiwa Spika, mkakati unaotekelezwa na Serikali ni kusimamia kwa karibu mkataba uliohuishwa ili fedha shilingi bilioni 42.5 zilizotengwa zikitolewa na kulipwa mzabuni azalishe na kuwasilisha kadighafi 13,000,000 ili uzalishaji wa Vitambulisho vya Taifa uendelee kutekelezwa. Ununuzi wa kadighafi hizo utawezesha mamlaka kuzalisha vitambulisho kwa wananchi wote waliosajiliwa na kutambuliwa ikiwemo wananchi wa Wilaya ya Kyerwa, ahsante.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -

Je, ni nini mpango wa Serikali wa kupambana na majanga ya moto yanayotokea mara kwa mara kwenye masoko nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea na mikakati ya kuzuia majanga ya moto kwa kufanya ukaguzi wa masoko, kutoa ushauri wa kitaalam na utoaji wa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto. Jeshi pia linasisitiza kuwepo kwa vifaa vya awali vya kuzima moto (fire extinguishers) na ving’amuzi vya moto (fire detectors) na uwepo wa walinzi katika maeneo yote ya masoko.

Mheshimiwa Spika, napenda kuitumia fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba masoko yote nchini yamekaguliwa na wahusika kupewa ushauri stahiki. Jeshi pia linafanya ufuatiliaji ili kujiridhisha kama ushauri uliotolewa unafanyiwa kazi.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya katika Jimbo la Singida Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kujenga vituo vya polisi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhudumia wananchi katika kudhibiti uhalifu. Katika tarafa ya Ilongero eneo la Kinyagigi Jimbo la Singida Kaskazini kunajengwa kituo cha Polisi cha Daraja C na kimefikia hatua ya umaliziaji. Kazi iliyobaki ni kuweka miundombinu ya umeme, maji safi na taka, milango na madirisha, dari, sakafu na kupaka rangi. Kiasi cha fedha shilingi 46,000,000 kinahitajika kumalizia ujenzi, na fedha hizo zinatarajia kutengwa kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawapatia uraia wananchi 6000 kutoka Burundi waliokamilisha mchakato wa maombi ya uraia katika Jimbo la Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wananchi wapato 6,000 kutoka Burundi wamekamilisha mchakato wa maombi ya uraia katika Jimbo la Ulyankulu. Wananchi hao walikuwa watoto wa wakimbizi wa Burundi wapatao 162,156 waliopewa uraia mwaka 2009/2010. Wananchi hao pamoja na watoto wapatao 6,620 waliozaliwa baada ya wazazi wao kuwasilisha maombi ya uraia, waliwasilisha maombi ya uraia Serikalini.

Mheshimiwa Spika, kwa ufupi wananchi hao walikamilisha kujaza ipasavyo fomu za maombi ya uraia na kuziwasilisha Serikalini. Maombi yao yalifanyiwa kazi na kwa sasa yapo katika hatua za maamuzi. Mara maamuzi yatakapofanyika, wananchi hao 6,620 watajulishwa hatma ya maombi yao.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, Serikali inatumia vigezo gani kuanzisha vituo vya polisi katika maeneo ambayo idadi ya watu na vitendo vya uhalifu vinaongezeka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohammed Jumah Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vigezo vinavyotumika kuanzisha vituo vya polisi ni ongezeko la watu, ongezeko la matukio ya uhalifu, umbali kati ya kituo kimoja cha polisi na kingine, uwepo wa miundombinu ya Serikali, shughuli za kibiashara pamoja na maeneo ya kimkakati kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi, likini pia uwezo wa kibajeti na utayari wa wananchi na mamlaka zao za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, nia ya uanzishwaji wa kituo cha polisi huwasilishwa kwenye Kamati ya Usalama ya Wilaya. Kikao kikiridhia, hoja hupelekwa kwenye Kamati ya Usalama ya Mkoa, kisha ushauri wao huwasilishwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya utekelezaji ikiwa ni pamoja na mipango ya ujenzi, kupeleka Askari na vitendea kazi. Nashukuru.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza: -

Je, ukaguzi wa magari barabarani unahusisha vitu gani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali na Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Ukaguzi wa magari hufanywa kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 ya mwaka 1973 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002 na kanuni zake. Ukaguzi wa magari uko wa aina mbili, aina ya kwanza hufanywa kwa mujibu wa Kifungu cha 81 ambao ni ukaguzi wa kawaida unaofanywa na askari barabarani. Ukaguzi huu huangalia nyaraka za gari, leseni ya dereva, uwezo wa gari, madai ya tozo za faini, pamoja na hali ya dereva.

Mheshimiwa Spika, aina ya pili ya ukaguzi hufanywa kwa mujibu wa Kifungu cha 83 ambapo Mkaguzi wa Magari hufanya ukaguzi kwenye maeneo maalum na baada ya kukagua hutoa hati ya ukaguzi kwa maana ya PF 93. Ukaguzi huu wa magari hufanywa ili kujiridhisha na uzima na usalama wa gari kama vile mifumo ya breki, umeme, sterling, matairi na kadhalika. Nashukuru.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -

Je, Bodi za Parole za Mkoa na Kitaifa zinakaa vikao vingapi kwa mwaka na wafungwa wangapi wamepata msamaha kwa mwaka 2020/2021?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Parole ya Taifa na Mikoa iliundwa kwa Sheria Na. 25 ya mwaka 1994 na ikafanyiwa marekebisho na Sheria Na. 5 ya nwaka 2002 kwa lengo la kutaka wafungwa wengi wanufaike na mpango huu. Bodi za Mikoa na Taifa kisheria zinatakiwa kufanya vikao vyake angalau mara nne kwa mwaka.

Aidha, katika kipindi cha mwaka 2020/2021 idadi ya wafungwa waliopata msamaha kupitia Bodi ya Parole nchini ni 70. Nashukuru.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Vituo vya Dawati la Jinsia katika kila Makao Makuu ya Polisi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Dawati la Jinsia na Watoto kuwepo kwenye vituo vya Polisi nchini, kwani husaidia kushughulikia matatizo ya wananchi wa makundi yanayonyanyaswa katika jamii wakiwemo wanawake na watoto. Ujenzi wa ofisi za dawati katika vituo vya Polisi unaendelea nchi nzima na kwa kadri ya upatikanaji wa fedha Serikalini, Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo wa ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa zimejengwa ofisi 70 katika vituo vya Polisi na vinafanya kazi. Kwa Mkoa wa Ruvuma, vituo vya dawati la jinsia na watoto vimejengwa kwenye vituo vya Polisi Songea, Tunduru na Mbinga. Aidha, ramani za majengo ya vituo vya Polisi zimeboreshwa ili kuingiza ofisi za jinsia na watoto. Hivyo, vituo vipya vitakavyokuwa vinavyojengwa kuanzia sasa vitakuwa

vimezingatia umuhimu wa kuwa na Ofisi za Dawati la Jinsia na Watoto.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -

Je, ni ipi kauli ya Serikali juu ya matukio ya moto katika Masoko kwenye maeneo mbalimbali nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, alijibu: -

Mheshimiwa Spika; kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumekuwa na matukio ya moto katika baadhi ya masoko nchini. Uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vingine umebaini sababu mbalimbali za matukio hayo. Sababu hizo ni pamoja na uunganishwaji holela wa mifumo ya umeme, kutokuzingatia tahadhari za moto kwa mama lishe na baba lishe na shughuli za uchomeleaji holela wa vyuma katika masoko.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na vyanzo vya matukio hayo umefanyika ukaguzi wa kinga na tahadhari ya majanga ya moto sambamba na utoaji wa elimu na mafunzo ya matumizi ya vifaa vya awali vya kuzima moto katika masoko nchini. Aidha, Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji inashirikiana na Halmashauri zote kuboresha miundombinu ya kuzima moto katika masoko na kuhakikisha ramani za masoko mapya zinakaguliwa na zinakidhi vigezo vya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kusisitiza uwepo wa vifaa vya awali vya uzimaji moto, uwepo wa ulinzi wa masoko kwa saa 24 na kuzingatia utekelezaji wa mapendekezo ya taarifa maalum za kaguzi zinazotolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Nashukuru.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Tumbatu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kujenga kituo cha Polisi na nyumba za makazi ya askari katika eneo Tumbatu wilaya ya Kaskazini “A” kwani eneo hilo ni kisiwa. Jeshi la Polisi liliomba na kupewa eneo lenye ukubwa wa mita za mraba elfu 47.5 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Polisi pamoja na nyumba za makazi ya askari. Jeshi la Polisi kupitia Kamisheni ya Zanzibar iliwasilisha maombi ya kupewa Hati miliki ya eneo hilo kwenye Mamlaka husika yaani Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “A” kupitia barua yenye Kumb.Na.PHQ/Z/C-5/17/X/41 ya tarehe 4 Aprili, 2020. Kinachosubiriwa ni kupata hati ya umiliki ili kuanza taratibu za kuomba fedha kwenye bajeti ya Serikali kwa ajili ya ujenzi nashukuru.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Chemba uliokwama kwenye ngazi ya lenta kwa miaka mitatu sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Chemba ulianza mwezi Novemba mwaka 2018. Gharama za jumla za ujenzi huu ni Sh.296,000,000. Ujenzi huo umeshirikisha nguvu za wananchi pamoja na Mdau aitwaye Local Investment Climate ambaye alitoa kiasi cha Sh.43,000,000. Ujenzi umefikia kwenye hatua ya lenta na ulisimama kutokana na kukosekana kwa fedha. Kiasi cha Sh.53,000,000 tayari kimeombwa kwenye mfuko wa tuzo na tozo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ili kumalizia ujenzi huo.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. JANETH M. MASSABURI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatunga Sheria kali za kudhibiti madereva wasiofuata sheria za usalama barabarani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Usalama Barabarani, sura 168 ya mwaka 1973 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002 na kanuni zake, inayotumika Tanzania Bara, na Sheria ya Usafiri Barabarani, Sura ya 7 ya mwaka 2003 na kanuni zake, inayotumika Zanzibar, zinatoa adhabu kwa wale wanaokiuka Sheria ya Usalama Barabarani. Serikali inaendelea kuboresha Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Usalama barabarani ambao tayari ulishasomwa kwa mara ya kwanza hapa Bungeni ili kuzingatia mabadiliko yaliyotokea na mahitaji ya sasa.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa Jengo la Kituo cha Polisi Kengeja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Khamis Kombo, Mbunge toka Baraza la Wawakilishi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jengo la kituo cha Polisi Kengeja, Mkoa wa Kusini Pemba ni chakavu na halifai kwa matumizi ya kutoa huduma za Kipolisi. Makadirio ya gharama za kujenga kituo kipya cha Polisi daraja C yamefanyika ambapo kiasi cha shilingi 292,544,139 zitahitajika. Fedha hizo zitaombwa kutoka mfuko wa tuzo na tozo ili ujenzi wake uanze katika mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha Polisi katika kata ya Kala Wilayani Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetoa kiasi cha shilingi 115,809,000 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi Daraja C katika Kata ya Kala Tarafa ya Wampembe Wilaya ya Nkasi. Taratibu za ujenzi wa kituo tayari umeanza mwezi Machi, 2023. Kituo hiki kinajengwa eneo la Mpasa na kitahudumia vijiji vya Mpasa, Kala, Mlambo, Tundu, King’ombe na kilambo cha Mkolechi.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Askari wa Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Kusini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan Mbunge wa Chakechake, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imetoa kibali cha kuajiri askari wapya wa Jeshi la Polisi 4,103. Kwa sasa askari hao wapo kwenye mafunzo ya awali katika shule ya Polisi Moshi. Watakapomaliza mafunzo yao, watagawiwa kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa wa askari ikiwemo mkoa wa Kusini Pemba. Nashukuru.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza msongamano wa watu wanaofuatilia hati za kusafiria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Makame Mlenge, Mbunge wa Chwaka kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji katika kupunguza msongamano wa waombaji wa Hati za kusafiria, imefunga mifumo ya kielektroniki ya utoaji wa hati za kusafiria katika Mikoa yote ya Zanzibar. Ufungwaji wa mifumo hiyo kumeondosha msongamano kwa wananchi katika Ofisi Kuu kwani kwa sasa wananchi wanaweza kuomba na kufuatilia maombi ya Hati za kusafiria katika Mkoa wowote anaoishi. Nashukuru.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo kipya cha Polisi cha Wilaya ya Micheweni pamoja na kupeleka samani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la mheshimiwa Omar Issa Kombo Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Micheweni ina kituo cha Polisi daraja B ambacho kinakidhi mahitaji ya kutoa huduma ya Polisi eneo hilo. Tatizo pekee la kituo hiki ni uchakavu unaohitaji kufanyiwa ukarabati. Tathmini ya uchakavu wa kituo imefanyika mwezi Januari 2023, na kubaini kuwa jumla ya shilingi 65,000,000 zinahitajika kwa ajili ya kubadilisha paa, dari, milango na madirisha, mfumo wa maji safi, maji taka, umeme, kuziba nyufa na kupaka rangi. Fedha hizo zimetengwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/2024 na kiasi cha fedha shilingi 17, 870,000 kwa ajili ya ununuzi wa samani za ofisi zinatarajiwa kuombwa kutoka kwenye mfuko wa tuzo na tozo kwa mwaka 2023/2024 mara ukarabati wa kituo utakapo kamilika.
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA K.n.y. MHE. HASSAN HAJI KASSIM aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu wa kuwa na kitambulisho kimoja chenye taarifa zote za huduma ndani ya kadi moja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Haji Kassim, Mbunge wa Jimbo la Mwanakwerekwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inatengeneza vitambulisho vya Taifa kwa kutumia teknolojia ya smart card ambapo kitambulisho kinakuwa na chip inayokiwezesha kutumika kwa matumizi mbalimbali. Kitambulisho hiki kinaweza kutumika kama pochi ya fedha ya kielektroniki (E-Wallet), Atm card kwa ajili ya kutoa fedha kutoka mashine ya ATM, huduma za Bima ya Afya, Kitambulisho cha Mpiga Kura na mengineyo.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia NIDA inaendelea kufanya mawasiliano na taasisi nyingine zenye vitambulisho ili kuona uwezekano wa kuoainisha taarifa zilizomo katika vitambulisho tofauti kwa madhumuni ya kuwa na kitambulisho kimoja. Mara muafaka utakapofikia wananchi watajulishwa rasmi lini utaratibu huo utaanza kutekelezwa. Ninashukuru.
MHE. MOHAMED ABDULRAHMAN MWINYI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukijenga upya Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mkoani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Abdulrahman Mwinyi, Mbunge wa Chambani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mkoani ni chakavu na halifai kwa matumizi ya kutoa huduma za polisi. Mwezi Desemba, 2022 Serikali ilitoa kiasi cha fedha shilingi milioni 700 kwa ajili ya kujenga kituo cha polisi kipya cha Daraja B eneo hilo na taratibu za ujenzi zimeshaanza. Ujenzi unafanywa na Kikosi cha Ujenzi cha Polisi na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Agosti, 2023. Nashukuru.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO K.n.y. MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza: -

Je, nini mkakati gani wa kumaliza changamoto za ukosefu wa nyumba za askari, magari na ufinyu wa ofisi katika Kituo cha Polisi Mlandizi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi Mlandizi kilichopo Mkoa wa Pwani, kina gari moja PT 4336 Ashok Leyland ambalo linafanya kazi. Kituo hicho kinatekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba mbili za kuishi familia Sita za Askari. Ujenzi wa nyumba hizo ambao umegharimu Shilingi Milioni 106.92 umechangiwa na nguvu za wananchi na wadau. Jengo moja lipo kwenye hatua ya kumalizia na lingine liko kwenye hatua ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kumalizia ujenzi wa nyumba zote mbili kiasi cha shilingi milioni 147.054 kinahitajika. Kuhusu mahitaji ya ofisi, tathmini kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Upelelezi, uchunguzi wa kisayansi na intelijensia ya jinai umefanyika na kubaini kuwa kiasi cha fedha shilingi 82,000,000 kinahitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa nyumba za nyumba za askari, pamoja na ofisi zitaombwa kwenye Mfuko wa Tuzo na Tozo katika mwaka wa fedha 2023/2024. Nashukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakarabati upya Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mkoani Pemba pamoja na nyumba za kuishi askari wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jengo la kituo cha Polisi cha wilaya ya Mkoani, mkoa wa kusini Pemba ni chakavu na halifai kwa matumizi ya kutoa huduma za Polisi. Mwezi Disemba 2022 Serikali imetoa kiasi cha fedha shilingi milioni 700 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi kipya cha Daraja B eneo hilo. Taratibu za ujenzi zimeshaanza na ujenzi unatarajia kukamilika mwezi Agosti, 2023.

Mheshimiwa Spika, tathimini ya uchakavu kwa ajili ya kufanya ukarabati wa nyumba ya makazi ya askari ya kuishi familia nne ambayo iko eneo la kituo imeshafanyika na kubaini kwamba shilingi milioni 46.27 kinahitajika kwa ajili ya kubadilisha paa, dari, miundombinu ya maji safi, maji taka na umeme, kuziba nyufa na kupaka rangi. Fedha hizo zitaombwa kutoka kwenye mfuko wa tuzo na tozo katika mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuiliza: -

Je, ni kesi ngapi za Wakulima kulishiwa mazao yao zimeripotiwa na ngapi zimepelekwa Mahakamani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mashauri ya kesi za wakulima kulishiwa mazao yao zilizoripotiwa Vituo vya Polisi katika Wilaya ya Mvomero kuanzia Januari, 2022 hadi Machi, 2023, ni jumla ya Mashauri 343. Kesi zilizofikishwa mahakamani ni
184. Kati ya hizo kesi 119 zimehukumiwa, kesi 65 zinaendelea kusikilizwa mahakamani na kesi 159 zipo kwenye hatua mbalimbali za uchunguzi na upelelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaipatia gari Ofisi ya Zimamoto ya Wilaya ya Igunga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa Mbunge wa Igunga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya magari kwa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Nchini. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga bajeti ya jumla ya shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa magari matano ya kuzima moto ambayo yatasambazwa katika mikoa na wilaya zenye upungufu wa magari ya zimamoto na uokoaji nchini ikiwemo Wilaya ya Igunga. Kwa sasa Wilaya ya Igunga inahudumiwa na gari la zimamoto lililopo Mkoani Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuliongezea wataalam na vitendea kazi ikiwemo magari ya kuzimia moto na uokoaji kwa ajili ya kuzifikia wilaya zote nchini kutegemea upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kumalizia ujenzi wa Gereza Chunya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Gereza Chunya ulianza mwaka 2016 kama kambi kwa kujenga na kukamilisha bweni moja la kulala wafungwa, jiko la wafungwa na nyumba mbili za kuishi askari. Vilevile ujenzi uliendelea kwa jengo la utawala na nyumba mbili za kuishi askari ambapo upo kwenye hatua ya msingi. Aidha, katika mpango wa bajeti 2023/2024 Serikali imepanga kutumia kiasi cha shilingi milioni 50 ili kugharamia uendelezaji wa ujenzi wa Gereza Chunya.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuiliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka magari kwa jeshi la polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Ali Omar, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kulipatia Jeshi la Polisi magari kama nyenzo ya kutendea kazi. mwaka 2022, Mkoa wa Kaskazini Pemba ulipatiwa magari matatu (3) yaliyonunuliwa na Serikali ili kupunguza uhaba wa magari katika mkoa huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bajeti yake ya mwaka wa fedha 2022/2023, imetoa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 15 kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kununulia magari na pikipiki. Pindi magari na pikipiki yatakapopokelewa yatagawiwa kwenye mikoa na wilaya zenye uhitaji mkubwa ikiwemo Mkoa wa Kaskazini Pemba, nashukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza ajali zinazosababishwa na magari ya mchanga Wilaya ya Kaskazini B - Unguja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la Kaskazini A na B – Unguja ajali zilizotokea kuanzia Januari, 2021 hadi Desemba, 2021 ni tatu ambazo zimesababisha vifo vya watu wanne na majeruhi mmoja. Ajali zilizotokea kuanzia Januari, 2022 hadi Machi, 2023 ni moja na imesababisha kifo cha mtu mmoja. Kwa jumla kesi zilizofikishwa mahakamani ni nne na zilizopata hukumu ni tatu na kesi moja inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajali zinazosababishwa na magari ya kubeba mchanga zimeendelea kupungua kutokana na Serikali kuweka alama za matumizi ya barabara, kuweka Kituo cha Ukaguzi wa Magari, kukagua leseni za madereva, kuweka utaratibu wa kupima macho na kutoa elimu ya matumizi bora na sahihi ya barabara kwa watumiaji wote, nashukuru.
MHE. JANETH M. MASSABURI aliuiliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kupeleka Maofisa Usalama Barabarani Falme za Kiarabu na Vietnam ili kujifunza jinsi ya kudhibiti ajali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inao utaratibu wa kutoa mafunzo mbalimbali kwa maofisa wa polisi wa usalama barabarani ndani ya nchi na pia kuwapeleka nje ya nchi kujifunza namna bora ya kusimamia na kudhibiti ajali za barabarani.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2023 Serikali imeshawapeleka maofisa wa usalama barabarani 30 kwenye nchi 15 ambazo ni Marekani, Ujerumani, Japan, China, India, Vietnam, Australia, Switzerland, Falme za Kiarabu, Israel, Tunisia, Misri, Ghana, Rwanda na Afrika Kusini ili kujifunza masuala ya usalama barabarani. Mashirika ya kimataifa na wadau kama JICA, UKAID, WFP, WHO, LATRA, TIRA, TRA, NIT na Baraza la Taifa la Usalama Barabarani wanaendelea kufadhili na kutoa mafunzo juu ya udhibiti na usimamizi wa taratibu za usalama barabarani ili kupunguza ajali nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa nafasi za mafunzo ndani na nje ya nchi kwa maofisa wa usalama barabarani ili kupata ujuzi juu ya usimamizi na udhibiti wa ajali kama alivyoshauri Mheshimiwa Mbunge, nashukuru.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kununua Gari la Zimamoto katika Mkoa wa Songwe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Songwe lina magari mawili ya kuzima moto. Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe Wilaya ya Mbozi Mji Mdogo wa Vwawa kuna gari moja aina ya Fuso yenye namba za usajili ZT 0014. Gari hilo linaujazo wa lita 1,500 za maji na lita 500 za foam. Katika Wilaya ya Tunduma kuna gari moja aina ya Mitsubish Canter yenye namba za usajili STL 4914 na lina ujazo wa lita 1,200 za maji.

Mheshimiwa Spika, Aidha, Serikali itaendelea kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuliongezea wataalam na vitendea kazi ikiwemo magari ya kuzima moto na uokoaji kwa Mkoa wa Songwe kwa madhumuni ya kuzifikia wilaya zote kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Moshi Seleman Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi Wilaya ya Tanganyika, Mkoa wa Katavi limepatiwa eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 85,229 na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi daraja B, pamoja na nyumba za makazi ya askari katika eneo la Majalila. Ujenzi wa kituo hicho uko kwenye hatua ya msingi na unashirikisha nguvu za wananchi na wadau akiwemo Mheshimiwa Mbunge. Upimaji wa eneo umeshafanyika na kiasi cha fedha shilingi 20.225 kinahitajika kama gharama za ardhi na maombi yameshatumwa Makao Makuu ya Polisi kwa ajili ya kulipa kwenye halmashauri ya wilaya, ili kupata hati miliki itakayowezesha Wizara kutenga fedha za ujenzi wa kituo na nyumba za makazi ya askari kwenye bajeti ya Serikali katika kuunga mkono jitihada za wananchi na wadau, nashukuru.
MHE. ASYA SHARIF OMAR aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaongeza nyumba za makazi kwa Askari Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asya Sharif Omar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imekamilisha ujenzi wa nyumba moja ya kuishi familia nne za askari katika eneo la Finya, Wilaya ya Wete. Mradi unaoendelea sasa ni ujenzi wa hanga la kuishi familia 18 za askari kwenye Kituo cha Polisi Micheweni. Ujenzi huo umefikia hatua ya kumalizia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imepanga kutumia kiasi cha Sh.270,121,580 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za kuishi familia nne za askari Polisi eneo la Konde Wilaya ya Micheweni. Utaratibu wa kujenga nyumba za makazi ya askari ni endelevu na utakuwa ukifanyika kwa kadri ya upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaimarisha ulinzi na usalama wa maeneo ya maziwa na bahari ili kulinda rasilimali pamoja na wavuvi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi ina wajibu wa kulinda maisha na mali za wananchi wake. Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/2024, tumepanga kutenga shilingi billioni 4.5 kwa ajili ya kununulia Boti 10 za doria zitakazotumika kwenye maeneo ya bahari na maziwa. Pindi boti hizo zitakapofika zitagawiwa maeneo yenye changamoto kubwa za uhalifu wa majini likiwemo eneo ya Rorya.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za Askari Polisi katika Kituo cha Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mahitaji ya nyumba za makazi ya kuishi askari Polisi katika Wilaya ya Micheweni. Mpaka sasa ujenzi unaoendelea ni wa hanga la kuishi familia 18 za askari na uko kwenye hatua za umaliziaji. Kiasi cha shilingi milioni 60,000,000 kinahitajika ili kumalizia na fedha hizo zinatarajiwa kuombwa kutoka Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Serikali itaendelea kujenga nyumba za maofisa na askari kutegemea upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. SALOME W. MAKAMBA K.n.y. MHE. FELISTA D. NJAU
aliuliza: -

Je, nini mkakati wa Serikali wa kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika magereza yetu upo msongamano mkubwa unaosabishwa na idadi kubwa ya mahabusu kuliko wafungwa hususani katika magereza ya mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada zinazochukuliwa na Serikali kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani, ni pamoja na kuhimiza matumizi ya vifungo vya nje kama vile Parole, Extra Mural Labour, huduma kwa jamii na huduma za uangalizi kwa wafungwa wenye viashiria vya kujirekebisha, msamaha unaotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maadhimisho ya sherehe za Muungano wa Tanzania na Uhuru wa Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkakati wa Serikali ni kuendelea kuelimisha na kuhimiza wananchi waishi kwa maadili bora na waepuke kuvunja sheria ili waepuke kufikishwa mahakamani na kufungwa. Aidha, Serikali itaendeleza mpango wa kujenga magereza mapya na kufanya upanuzi kwa magereza ya zamani ili kuongeza nafasi ya kuwahifadhi wafungwa na mahabusu kulingana na mahitaji na kutegemea upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE aliuliza: -

Je, lini warithi wa Askari E2152 aliyekuwa mtumishi wa Jeshi la Polisi watapewa mafao yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimwa Haji Makame Mlenge, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafao ya warithi wa Askari Polisi E.2152 PC Makame Haji Kheir yameshashughulikiwa na Kamisheni ya Polisi Zanzibar, pamoja na Kamisheni ya Utawala wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu Dodoma. Mnamo tarehe 8 Machi, 2023, maombi hayo yaliwasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango baada ya kukamilika kwa nyaraka zote muhimu zilizokuwa zikihitajika kwa ajili ya malipo ambapo taratibu za uandaaji wa malipo hayo zinaendelea na yanatarajiwa kukamilika ndani ya Mwezi huu Mei ambapo warithi wa Askari huyo watalipwa stahiki zao kwa mujibu wa Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. JANEJELLY J. NTATE K.n.y. MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -

Je, nini tamko la Serikali kuhusu Kitambulisho cha Taifa kuwekwa ukomo wa kutumika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Jimbo la Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vitambulisho vya Taifa vilivyotolewa hadi mwaka 2022 vilikuwa na tarehe ya ukomo wa kutumika. Serikali imefanya marekebisho ya Kanuni za Usajili na Utambuzi wa Watu za mwaka 2014 ikiwemo Kanuni ya 7(3)(a) ambayo inaainisha taarifa zilizopo katika uso wa Kitambulisho cha Taifa zinazohusiana na tarehe ya ukomo wa muda wa matumizi ya Kitambulisho cha Taifa. Ili kuondoa ukomo wa matumizi, marekebisho hayo yalitangazwa rasmi katika Tangazo la Serikali (GN) Na. 96 la tarehe 17 Februari, 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ina maana kwamba, Vitambulisho vya Taifa kwa raia ili kuwezesha Vitambulisho vinavyofikia ukomo wake baada ya kipindi cha miaka kumi vitaendelea kutumika baada ya muda huo. Napenda kufafanua zaidi kwamba Namba za Utambulisho (NIN) zilizopo katika vitambulisho hivyo, hazina ukomo wa muda wa matumizi. Aidha, marekebisho hayo hayatahusu muda wa matumizi ya Vitambulisho vya Taifa kwa Wageni Wakaazi (Legal Residents) na Wakimbizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa wito kwa watoa huduma wanaotumia vitambulisho vya Taifa kuwatambua wateja wao, kuendelea kutambua vitambulisho vyenye tarehe za ukomo, nakushukuru.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE K.n.y. MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati na kuongeza uwezo wa Gereza la Dimani Wilayani Kibiti?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itatenga fedha shilingi milioni 350 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa baadhi ya Magereza nchini. Gereza la Dimani Wilaya ya Kibiti ni moja ya magereza yatakayokarabatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali, kupitia mpango na bajeti wa kila mwaka itaendelea kutenga fedha za ukarabati na upanuzi wa Magereza yenye uhitaji huo, ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, lini Mlima Nkongore utarudishwa kwa Wananchi wa Kata ya Katare baada ya kuchukuliwa na Jeshi la Magereza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya hifadhi na milima kama ilivyo kwa Mlima Nkongore, kisheria huwa yapo chini ya Halmashauri ya uendelezaji miji husika. Aidha, mwanzoni mwa mwaka 2016 baadhi ya wananchi walianzisha shughuli za kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo mazao haramu ya bangi katika eneo la kuzunguka Mlima Nkongore uliopo chini ya Halmashauri ya Mji wa Tarime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kilimo kilichokuwa kinafanyika katika maeneo ya Mlima Nkongore, pia kutokana na Sheria ya Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004, kifungu cha 58(1) na (2) kinachozuia kufanya shughuli zozote zinazoweza kupelekea hifadhi ya mlima kuharibiwa kwa kuwa maeneo hayo yanatakiwa yahifadhiwe kisheria. Kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya cha tarehe 11 Novemba, 2017 kiliazimia kuwa eneo la Mlima Nkongore likabidhiwe kwa Jeshi la Magereza ili kuimarisha shughuli za ulinzi na usalama. Kupitia barua Kumb. Na. AB.284/311/01C/59 ya tarehe 17 Novemba, 2017 ni idhini rasmi ya kukabidhi eneo la mlima Nkongore kwa Jeshi la Magereza kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na uhifadhi wa mazingira, ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Tarafa za Kitumbeine na Engarenaibor hususan kwenye migodi ya Rubi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali na Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarafa ya Kitumbeine na Engarenaibor zipo katika Wilaya ya Longido, Mkoa wa Arusha, Tarafa hizi hazina vituo vya Polisi vinavyofanya kazi. Huduma za Polisi hutolewa kwenye kituo cha Polisi cha Wilaya ya Longido kilichopo kilometa 54 toka Kitumbeine na kilometa 35 toka Engarenaibor. Serikali inatambua juhudi za wananchi wa Tarafa hizo mbili kuanza kujenga vituo vya Polisi viwili kwa nguvu zao na kwa kuwashirikisha wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Tarafa ya Kitumbeine jengo la Kituo cha Polisi limejengwa katika Kijiji cha Gelai Lumbwa, Kata ya Gelai Lumbwa lakini bado hawajaanza ujenzi wa nyumba za makazi ya Askari. Katika Tarafa ya Engarenaibor wananchi wamejenga Kituo cha Polisi katika kijiji cha Mundarara, Kata ya Mundarara na ujenzi umefikia kwenye hatua ya lintel.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawapongeza wananchi wa Tarafa ya Kitumbeine na Engarenaibor na itawaunga mkono katika kuchangia nguvu za wananchi ili kukamilisha ujenzi wa majengo hayo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 ili kutoa huduma za Polisi katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. TAMINA HAJI ABASS aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kukarabati nyumba za makazi ya Askari Polisi Kaskazini Unguja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tamina Haji Abass, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tathmini kwa ajili ya ukarabati wa nyumba zote 14 za makazi ya askari polisi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, imefanyika na kiasi cha shilingi 447,065,000 zinahitajika. Fedha hizo zinatarajiwa kutengwa kwenye Bajeti ya Serikali ya 2024/2025, ahsante.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE aliuliza: -

Je, Serikali ina utaratibu gani wa kufanya mazoezi ya utayari katika uokozi wa ajali majini katika Kivuko cha Kivukoni – Kigamboni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lina boti moja ya maokozi iliyopo katika Daraja la Mwalimu Nyerere iliyopo Ofisi ya Mkuu wa Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kigamboni ambayo hutumika kwa ajili ya maokozi ya ajali za majini katika Bahari ya Hindi na kwenye fukwe zote za Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeandaa na kutekeleza mkakati wa utoaji wa elimu na mazoezi katika Wilaya ya Kigamboni kwa kushirikiana na Ofisi ya kivuko cha Magogoni – Feri, Kigamboni Beach Management Unit (BMU) na wavuvi kwa ajili ya utayari wa huduma ya uokoaji wakati wa ajali za majini katika Kivuko cha Kigamboni na maeneo mengine ya jiji. Mkakati huo unatekelezwa pia kwenye sehemu zote zenye bahari kuu, maziwa makuu na mito ikiwemo Mkoa wa Pwani, Mara, Kagera, Geita, Kigoma na Mwanza, nashukuru.
MHE. MOHAMED ABDULRAHMAN. MWINYI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga ofisi ya NIDA katika wilaya ya Mkoani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Abdulrahman Mwinyi, Mbunge wa Jimbo la Chambani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mpango wa ujenzi wa ofisi za usajili za wilaya kwa awamu. Katika awamu ya kwanza Serikali imejenga ofisi 13 na awamu ya pili inatarajia kujenga ofisi 31 kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024. Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa itaendelea kujenga ofisi za usajili kulingana na upatikanaji wa fedha kwa wilaya nyingine nchini ikiwemo Wilaya ya Mkoani, ahsante.
MHE. ALI VUAI KHAMIS aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ali Vuai Khamis, Mbunge wa Mkwajuni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika eneo la Matemwe lenye Shehia sita hakuna sehemu iliyotengwa kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi. Hivyo napenda kutumia fursa hii kumshauri Mheshimiwa Mbunge, aishirikishe Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini A ili itenge eneo kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi pamoja na nyumba za makazi ya askari katika eneo la Matemwe ili Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itenge fedha kwenye bajeti kwa ajili ya ujenzi huo, ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO K.n.y. MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza ujenzi wa Kituo cha Polisi Turiani kilichojengwa kwa nguvu za wananchi?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa kupitia michango mbalimbali ya wananchi inayofikia shilingi milioni 36, Kituo cha Polisi Turiani kimefikia hatua ya lenta. Katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imepanga kutumia fedha toka Mfuko wa Tuzo na Tozo ili kuendeleza ujenzi wa kituo hicho ambacho hadi kukamilika kitakuwa kimegharimu shilingi milioni 110, ahsante.
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID aliuliza:-

Je, kwa nini Jeshi la Polisi haliondoi zuio la kuwahudumia wananchi wanaokwenda kupata huduma kwenye vituo nje ya maeneo yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, Mbunge wa Magomeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Namba 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, kikisomwa pamoja na Kanuni za Jeshi la Polisi (PGO) Namba 309, mtu yeyote aliyetendewa au anayefahamu jinsi kosa lilivyotendeka au linavyotaka kutendeka anatakiwa kutoa taarifa kituo chochote cha Polisi kilicho karibu na taarifa hiyo itachukuliwa na kufanyiwa kazi. Hivyo, hakuna zuio lolote la kuwahudumia wananchi wanaohitaji huduma za polisi kwenye vituo vilivyo nje na maeneo yao, nashukuru.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-

Je, lipi tamko la Serikali kwa watuhumiwa waliopo magereza ya nchi za nje wanaomiliki vitambulisho na hati za kusafiria za Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomari Khamis, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Pasipoti na Hati za Kusafiria, Sura ya 42, pasipoti hutolewa kwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa madhumuni ya kusafiria nje ya nchi. Pale inapothibitika kuwa raia wa nchi za nje wanamiliki hati za kusafiria za Tanzania kinyume na matakwa ya sheria yetu ya pasipoti wanakuwa wametenda makosa na hivyo wanastahili kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kumshauri Mheshimiwa Mbunge kama ana taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa watuhumiwa hao azikabidhi kwa vyombo vyetu ili waweze kuchukuliwa hatua stahiki, nashukuru.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi kwa kumalizia ujenzi wa Vituo vya Polisi vya Itumbi na Kambikatoto, Lupa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Vituo vya Polisi vya Itumbi na Kambikatoto ni vituo vinavyojengwa kwa nguvu za wananchi na mpaka kumalizika ujenzi wake vitagharimu kiasi cha fedha shilingi 279,780,978. Fedha inayohitajika ili kumalizia ujenzi kwa kuunga mkono nguvu za wananchi, ni shilingi 173,447,178. Fedha hizo zitatoka kwenye Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ili kumalizia ujenzi huo kama njia ya kuwaunga mkono wananchi wa Jimbo la Lupa.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza kazi ya kuwapatia wananchi Vitambulisho vya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Jimbo la Sikonge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kazi ya kuwapatia wananchi Vitambulisho vya Taifa ni endelevu kwa kuwa kila mwaka kuna wananchi wanaotimiza umri wa miaka 18 ambao wanastahili kupewa Vitambulisho vya Taifa. Aidha, wapo wananchi wanaopoteza vitambulisho au wenye vitambulisho vinavyoharibika na hivyo kuhitajika vingine.

Mheshimiwa Spika, wananchi ambao walitambuliwa lakini hawajapata vitambulisho vyao, Serikali inatarajia kuwapatia vitambulisho vyao ifikapo mwezi Machi, 2024, nashukuru.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA K.n.y. MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza kulipa fidia kwa baadhi ya wananchi waliopisha uanzishaji wa Kambi ya Gereza la Kilimo Singa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi Singa ilianzishwa mwaka 1983 katika Kijiji cha Singa chini ya Magereza ya Mkoa wa Singida ikiwa na eneo la ekari 500 kama ilivyoombwa kutoka Serikali ya Kijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ardhi (Land Ordinance 03, Cap 113) ya mwaka 1923 iliyokoma mwaka 2003 haikuruhusu ulipwaji wa fidia kwa maeneo yanayotwaliwa na Serikali ambayo hayajaendelezwa. Kwa kuzingatia sheria hiyo, wananchi walio na maeneo yaliyoendelezwa (kwa kupanda mazao ya kudumu) katika eneo lililogawiwa kwa gereza walilipwa fidia zao shilingi 300,000 kwa eneo lenye ukubwa wa ekari 10 na malipo ya mwisho yalifanyika mwaka 1997. Taratibu za umilikishaji rasmi wa eneo hilo kwa Jeshi la Magereza zinakamilishwa na Mamlaka husika, nashukuru.
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO aliuliza:-

Je, lini Serikali itawajengea nyumba za kuishi Askari wa Jeshi la Polisi waliopo Kengeja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Khamis Kombo, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mahitaji ya nyumba za kuishi Askari Polisi katika eneo la Kengeja Mkoa wa Kusini Pemba. Tathmini kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za makazi ya kuishi familia nne za Askari Polisi imefanyika, ambapo kiasi cha fedha Shilingi 368,412,200/= zinahitajika. Fedha hizo zimetengwa katika Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, nashukuru.

MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -

Je, lini Serikali itaweka utaratibu mzuri wa kutambua fire hydrants nchini na kuziwekea alama ili kusaidia wakati wa majanga ya moto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeshirikiana na Mamlaka za Miji na Maji kukagua na kutambua fire hydrants 2,348 ambazo zipo Nchi nzima. Jeshi limeanza kutekeleza utaratibu maalum wa kimataifa wa utambuzi wa fire hydrants ambao ni kuziwekea alama ya FH. Jeshi pia linaziweka fire hydrants hizo katika mfumo wa utambuzi Kijiografia (Geographical Information System – GIS) na kuzijengea mifuniko migumu itakayozuia uharibifu wake. Aidha, Jeshi linawasiliana na mamlaka zinazohusika na ujenzi wa barabara na uendelezaji wa miji kudhibiti ujenzi holela wa makazi na upanuzi wa barabara za mitaa unaohusisha kuzifukia fire hydrants. Lengo ni kuzitunza fire hydrants zilizopo ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji wakati wa kutelekeza majukumu ya kuzima moto yanapotokea majanga, nakushukuru.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, ajali ngapi za barabarani zimetokea kati ya Mikumi na Ruaha Mbuyuni kwa Mwaka 2010 hadi 2022?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi 2022 ajali za barabarani zilizosababishwa na vyombo vya moto katika eneo la Mikumi hadi Ruaha Mbuyuni, barabara ya Morogoro kwenda Iringa ni 128. Mchanganuo wa ajali hizo ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ajali zilizohusisha mabasi ya abiria ni 30, malori 42 na magari madogo 56, nashukuru.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Je, kwa nini Vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo mpakani mwa Ziwa Tanganyika havina Usafiri wa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mahitaji ya vyombo vya usafiri vya uhakika katika kudhibiti uhalifu maeneo ya mpakani mwa ziwa Tanganyika. Kwa dhamira ya kuimarisha upatikanaji wa usafiri, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kununulia magari na pikipiki ambapo mchakato unaendelea. Pindi yatakapofika, pikipiki na magari hayo yatagawiwa wilaya zote zikiwemo zilizopo mpakani mwa ziwa Tanganyika. Pia katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4.5 za kununulia boti 10 kwa ajili ya doria baharini na kwenye maziwa. Baada ya kununuliwa, boti hizo zitagawiwa kwenye maeneo yenye changamoto za uhalifu ikiwemo Ziwa Tanganyika, nashukuru.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Nduguti kwa kuwa ujenzi wake umesimama kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Wilaya ya Mkalama ambacho kinajengwa eneo la Nduguti ni kituo cha Daraja B na ujenzi wake ulisimama ukiwa umefikia hatua ya lenta. Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 ilitenga kiasi cha fedha shilingi 500,000,000 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo hicho. Mwezi Februari, 2023 Serikali ilitoa shilingi 300,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Wilayani Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Wilaya ya Kishapu ni kituo cha Daraja B, na ujenzi wake umesimama ukiwa umefikia kwenye hatua ya umaliziaji. Tathmini kwa ajili ya kumalizia ujenzi imefanyika na kiasi cha shilingi 262,672,520 zinahitajika. Fedha hizo zimepangwa kutolewa kwenye mfuko wa tuzo na tozo katika mwaka wa fedha 2023/2024. Fedha zitakapotolewa ujenzi huo utakamilishwa, ili wananchi wa Kishapu waanze kunufaika na huduma za Polisi kupitia kituo hicho. Nakushukuru.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: -

Je, lini Serikali itafanya marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani ili kuweka tozo tofauti kulingana na ukubwa wa chombo cha moto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kufanya marekebisho na kuiboresha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 ya mwaka 1973 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002. Kwa sasa Serikali inaendelea kuboresha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani ambao tayari ulishasomwa kwa mara ya kwanza hapa Bungeni. Pamoja na mambo mengine, mswada huo umezingatia mahitaji ya sasa ikiwa ni pamoja na kuweka viwango tofauti vya tozo kulingana na ukubwa wa chombo cha moto kama Mheshimiwa Mbunge anavyoshauri, nashukuru.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka gari Kituo cha Polisi Muhange Wilayani Kakonko?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mahitaji makubwa ya kibajeti, kwa sasa Serikali haitaweza kuvipatia vituo vyote vidogo vya polisi magari. Hivyo, kituo kidogo cha Polisi cha Muhange ambacho kipo Wilaya ya Kakonko kitaendelea kuhudumiwa na Kituo cha Polisi cha Wilaya ambacho kina magari mawili namba PT 1983 na PT 3631 Toyota Land Cruiser kama inavyofanyika kwa vituo vingine vidogo vilivyoko Wilaya ya Kakonko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mkalama ambacho ni gofu la ghorofa kwa muda mrefu sasa ilhali Wilaya haina kituo chenye hadhi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi kinachojengwa katika Wilaya ya Mkalama ni Kituo cha Daraja A na ni cha ghorofa moja. Ujenzi wake umeanza Juni, 2015 na unatarajia kutumia jumla ya shilingi 792,450,000.00 hadi kumalizika kwake. Hadi sasa fedha zilizotumika ni shilingi 100,000,000.00 na kazi iliyobaki ni kumwaga silabu, kupaua na kazi za kumalizia. Katika mwaka ujao wa fedha 2022/2023 zimetengwa fedha kiasi cha shilingi 692,450,000 kwa ajili ya kumalizia kazi ya ujenzi wa kituo hicho. Nashukuru.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Uvinza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaanza kujenga Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Uvinza katika eneo la Lugufu baada ya eneo hilo kupimwa na kupata hati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. JANEJELLY J. NTATE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka Askari Polisi katika Kituo cha Polisi Kata ya Kilungule - Mbagala ili wananchi wa kata hiyo wapate huduma?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dar es Salaam, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari ilishakipangia askari sita kituo kidogo cha Polisi cha Kata ya Kilungule - Mbagala na kinafanya kazi saa 24. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE K.n.y. MHE. AGNESTA L. KAIZA auliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Magereza ili kulinda haki za wafungwa na mahabusu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Magereza limejipanga kukarabati Magereza kwa kutumia fedha za vyanzo vya ndani na fedha inayotengwa kwenye bajeti kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika mwaka 2021/2022 Serikali ilitenga Shilingi 840,000,000/= kwa ajili ya ukarabati wa Magereza matano ambayo ni Gereza Maweni, Isanga, Kondoa, Lindi na Mkuza na limetumia vyanzo vya ndani kukarabati Magereza yafuatayo: Gereza Rombo, Ukonga, Mkono wa Mara, Kwitanga, Idete, Mbigili, Shinyanga, King’ang’a, Butimba, Luanda, Liwale na Babati.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa fedha 2022/2023 Jeshi la Magereza limetenga Shilingi 4,569,000,000/= ili kujenga Magereza sita ya Wilaya za Kilosa, Kaliua, Karatu, Kakonko, Gairo na Msalato.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. (Makofi)
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya Gereza la Liwale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele Mbunge wa Viti Maalum Lindi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Magereza imeanza kuboresha miundombinu ya Gereza Liwale kwa kutumia fedha za vyanzo vya ndani. Jeshi la Magereza limejenga jengo jipya la Utawala na nyumba saba za watumishi kwa ajili ya kuishi askari. Majengo hayo yamekamilika na yamezinduliwa na Mwenge wa Uhuru tarehe 29 Aprili, 2022. Ili kukamilisha uboreshaji wa miundombinu iliyobakia, Shilingi 225,000,000.00 zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023. Aidha, nawashukuru na kuwapongeza Mhe. Mbunge wa Jimbo la Liwale, Mheshimiwa Kuchauka, na Mkuu wa Wilaya ya Liwale kwa kuchangia mifuko ya saruji iliyosaidia ujenzi wa majengo ya utawala na selo moja ya Wanawake.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Dunga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tathmini iliyofanyika imebaini kuwa kiasi cha Shilingi 43,000,000 kinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Dunga kilichoko Wilaya ya Kati, Mkoa Kusini Unguja. Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatafuta fedha hizo ili kumalizia ujenzi huo, kama njia ya kuunga mkono juhudi za wananchi na wadau, hususani katika mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. MAULID ALI MOHAMED aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakifanyia ukarabati Kituo cha polisi Mazizini pamoja na kukarabati nyumba za Askari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Maulid Ali Mohamed Mbunge wa Kiembe samaki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya tathmini ya uchakavu wa kituo na nyumba za makazi za askari polisi Mazizini na kubaini kuwa kiasi cha fedha shilingi 64,484,700 zinahitajika kugharamia ubadilishaji paa, dari, mfumo wa umeme, maji safi, maji taka na kupaka rangi. Ukarabati huo utafanyika kulingana na mpango wa ukarabati kutegemea na upatikanaji wa fedha.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakifanyia matengenezo Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Micheweni na ujenzi wa nyumba za askari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya tathmini ya uchakavu wa Kituo cha Polisi Micheweni na kubaini kuwa kiasi cha fedha shilingi 51,000,000 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho. Aidha, ujenzi wa jengo la hanga la kituo hicho umefikia kwenye hatua za kumalizia na kiasi cha fedha shilingi 57,000,000 zinahitajika. Ukarabati wa kituo pamoja na umaliziaji wa ujenzi wa jengo la hanga utafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA K.n.y. MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa Vitambulisho vya NIDA kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma hususan Jimbo la Muhambwe?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imesajili jumla ya wananchi 975,844 katika Mkoa wa Kigoma wakiwemo wananchi wa Jimbo la Muhambwe na jumla ya vitambulisho 123,962 vimezalishwa kwa ajili ya wananchi wa mkoa huo. Katika Jimbo la Muhambwe ambalo liko katika Wilaya ya Kibondo, wananchi 139,588 walitambuliwa na vitambulisho 5,126 vilitolewa na kugaiwa kwa wananchi. Serikali inatarajia kukamilisha utoaji wa vitambulisho kwa wananchi wote wenye sifa katika mwaka wa fedha 2022/2023. Nashukuru.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya polisi katika Mahakama za Kata nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuwa na vituo vya polisi kila kata na ndio maana imeanzisha utaratibu wa Polisi Kata inayoongozwa na Mkaguzi wa Polisi. Ujenzi wa vituo hivyo utaendelea kufanyika kwa awamu kutegemea upatikanaji wa fedha. Vituo hivyo hutumiwa na mahakama zilizoko kwenye kata husika pindi vinapohitajika, nashukuru.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaboresha miundombinu ya vituo vya polisi vya Ilongero, Ngamu, Ngimu, Msange na Mtinko katika Jimbo la Singida Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Abeid Ramadhan Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uchakavu wa vituo vya polisi vya Ilongero, Mtinko na Ngamu. Tathmini iliyofanyika imebaini kuwa kiasi cha fedha shilingi 46,480,000 zinahitajika ili kugharamia ukarabati wa vituo hivyo. Katika maeneo ya Ngimu na Msange hakuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya vituo vya polisi. Napenda kutumia fursa hii kuishauri Halmashauri ya Wilaya ya Singida itenge maeneo yenye ukubwa stahiki pamoja na kutoa hatimiliki ili kuwezesha Serikali kupanga na kutelekeza kazi ya ujenzi wa vituo vya polisi kwenye maeneo hayo kwa kushirikiana na wadau. Nashukuru.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Gereza la Wilaya ya Igunga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Gereza la Igunga lilianza kujengwa mwaka 2004 na lilifunguliwa rasmi mwaka 2006. Hadi sasa mabweni mawili ya wanaume yenye uwezo wa kulala wafungwa 51 kila moja yamekamilika na ujenzi wa jengo la utawala sambamba na nyumba za askari unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi za kukamilisha ujenzi wa Gereza hili zinaendelea na fedha kiasi cha shilingi 77,694,000 zimetengwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya umaliziaji wa jengo la utawala. Nashukuru.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, ni lini wananchi wa Jimbo la Nkenge ambao hawajapata Vitambulisho vya Taifa au Namba za Usajili watatambuliwa kama raia wenye haki na kupatiwa vitambulisho hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Jimbo la Nkenge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ina jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi ikiwemo wananchi wa Jimbo la Nkenge. Katika Mkoa wa Kagera jumla ya wananchi 1,009,653 wamesajiliwa na kutambuliwa baada ya maombi yao kuhakikiwa. Jumla ya vitambulisho 310,847 vimezalishwa kwa ajili ya wananchi wa mkoa huo. Katika Wilaya ya Misenyi inayojumuisha jimbo la Nkenge wananchi 85,439 wamesajiliwa na kutambuliwa na jumla ya wananchi 32,235 wamepatiwa Namba za Utambulisho ambazo wanazitumia katika kupata huduma mbalimbali. Aidha, vitambulisho 24,694 vimezalishwa na kugaiwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo. Nashukuru.
MHE. SHABAN O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Lushoto ni kituo cha daraja A kilianza kujengwa mwaka 2014 kwa gharama ya shilingi 417,000,000 na hatua iliyofikiwa ni umaliziaji. Ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Juni 2022. Nashukuru.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdulkarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa jengo la Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Manyara ulianza mwaka 2012 kwa kutumia Mkandarasi aitwaye MS Mavonda’s Co. Ltd kwa gharama ya shilingi 862,167,729. Ujenzi huo ulipofikia asilimia 65 zilijitokeza changamoto katika kutekeleza mkataba hali iliyosababisha kuvunjika kwa mkataba huo mwezi Agosti, 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga kukamilisha utekelezaji wa mradi huo kwa utaratibu wa nguvu kazi kwa maana ya Force Account ambapo taratibu zote zimekamilika na tayari kiasi cha fedha shilingi 353,986,150 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo zimepokelewa kutoka Hazina. Ujenzi wa jengo hilo unatarajia kukamilika mwezi Oktoba, 2022. Nashukuru.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI K.n.y. MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -

Je, nini mpango wa Serikali wa kuimarisha Jeshi la Zimamoto hasa katika maeneo ya miji yenye hatari kubwa ya majanga ya moto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika mpango wa kuimarisha huduma za zimamoto na uokoaji nchini kwa kuimarisha na kuongeza vifaa vya kisasa. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 vitajengwa jumla ya vituo saba vya zimamoto na uokoaji kwa kuanza na mikoa isiyokuwa na vituo hivyo. Mikoa hiyo ni pamoja na Songwe, Simiyu, Kagera, Njombe, Manyara, Katavi na Geita. Aidha, kwa kuzingatia ukuaji wa haraka wa Jiji la Dodoma ambalo ni Makao Makuu ya nchi, ujenzi wa vituo viwili Chamwino na Nzuguni utakamilika hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa ajira mpya ya askari 400 ambao kwa sasa wapo mafunzoni. Vilevile Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu kinga dhidi ya majanga ya moto kuanzia shuleni, maeneo ya biashara na yale yenye mikusanyiko mikubwa ya watu. Nashukuru.
MHE. HAJI AMOUR HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na matukio ya uhalifu ukiwemo wizi katika Jimbo la Pangawe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Amour Haji, Mbunge wa Pangawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi itaendelea na kazi ya kulinda maisha ya watu na mali zao kwa kufanya doria, kuendesha operesheni mbalimbali na misako ili kuwabaini na kuwakamata wahalifu. Jeshi la Polisi limewapanga Wakaguzi wa Polisi kila Shehia katika Jimbo la Pangawe ili kusimamia usalama na kuishirikisha jamii kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, uhalifu ni zao la jamii, hivyo naomba kutumia nafasi hii kuwaomba wazazi, walezi, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kuwalea kwa maadili mema vijana wetu ili waepuke kujiingiza katika uhalifu. Aidha, watumie fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa wale watakaokaidi wajiandae kukabiliana na mkono wa sheria. Nashukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: -

Je, ni kwa nini hadi sasa Wilaya ya Chakechake ina kituo kimoja cha polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wilaya ya Chakechake ina kituo kimoja cha polisi. Sababu ya hali hiyo ni kwamba, Wilaya ya Chakechake ilikuwa na idadi ndogo ya matukio ya uhalifu na hivyo kituo hicho kilionekana kinatosheleza.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu pamoja na shughuli za kiuchumi ikiwemo biashara, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imepanga kujenga vituo vya polisi katika maeneo ya Vitongoji, Pujini, Wesha na Gombani. Tayari Idara ya Ardhi imetoa eneo la mita za mraba 1,496 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi eneo la Vitongoji. Serikali itaanza kujenga kituo hicho kulingana na mpango wake wa ujenzi hususani katika mwaka wa fedha 2023/2024. Nashukuru.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Dunga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tathmini iliyofanyika imebaini kuwa kiasi cha Shilingi 43,000,000 kinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Dunga kilichoko Wilaya ya Kati, Mkoa Kusini Unguja. Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatafuta fedha hizo ili kumalizia ujenzi huo, kama njia ya kuunga mkono juhudi za wananchi na wadau, hususani katika mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. MOHAMED JUMAH SOUD aliuliza: -

Je, ni vigezo gani hutumika kuanzisha Vituo vya Polisi maeneo yenye idadi kubwa ya watu pamoja na vitendo vya uhalifu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Jumah Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vinavyotumika kuanzisha Vituo vya Polisi ni ongezeko la watu, ongezeko la matukio ya uhalifu, umbali kati ya Kituo kimoja cha Polisi na kingine, uwepo wa miundombinu ya Serikali, shughuli za kibiashara pamoja na maeneo ya kimkakati kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi, uwezo wa kibajeti na utayari wa wananchi na Mamlaka zao za Serikali za Mitaa ni vigezo vingine tunavyovitumia. Hatua inayofuata ni mapendekezo ya uanzishwaji wa kituo husika kuwasilishwa kwenye Kamati ya Usalama ya Wilaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa na kisha ushauri wao huwasilishwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya utekelezaji. Nashukuru.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Ofisi ya Polisi Jamii Shehia ya Kendwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshiniwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdalla Rashid, Mbunge wa Kiwani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa Ofisi ya Polisi Jamii inayojengwa Jindamiti katika Shehia ya Kendwa, inajengwa kwa nguvu na michango ya wananchi na wadau na ujenzi wake umefikia hatua ya lenta. Lengo la kujenga ofisi hiyo ni kutumiwa na vikundi vya ulinzi shirikishi vya Shehia ya Kendwa. Wajibu wa Serikali ni kujenga Ofisi na Vituo vya Polisi ambavyo hutumiwa na Askari Polisi katika kudhibiti uhalifu.

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kumshauri Mheshimiwa Mbunge aendelee na jitihada za kuwahamasisha wananchi na wadau kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo ili iweze kutumiwa na vikundi vya ulinzi shirikishi kama walivyofanya wananchi wa Chambani, ahsante.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka Gari la Zimamoto Handeni Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea na jitihada za kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga bajeti ya jumla ya shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa magari matano ya kuzima moto ambayo yatagawiwa katika Mikoa na Wilaya zenye upungufu wa magari ya Zimamoto na Uokoaji, ukiwemo Mkoa wa Tanga, hususan Wilaya ya Handeni, nashukuru.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. JANETH M. MASSABURI aliuliza: -

Je, magari mangapi ya Zimamoto yanahitajika kukidhi mahitaji halisi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linahitaji jumla ya magari 237 ya kuzima moto, magari 168 ya uokoaji, magari 28 ya HAZMAT, Crane 38, ambulance 168 na magari 28 ya ngazi ya kuzima moto katika majengo marefu (Turn table ladder). Serikali imeendelea kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kutenga fedha za maendeleo katika bajeti kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa magari ya kuzima moto pamoja na vifaa vingine vya uokoaji ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Jeshi limetengewa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa magari matano ya kuzima moto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kupata mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 100 utakaowezesha kupata vitendea kazi mbalimbali ikiwemo magari zaidi ya 100 ya kuzima moto na uokoaji kwa nchi nzima, ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU aliuliza: -

Je, lini Serikali itatenga fedha kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Kijiji cha Magungu – Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Olelekaita Kisua, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Magungu Kiteto ulianza mwaka 2015 kwa kutumia michango na nguvu za wananchi. Ujenzi huo ulisimama ukiwa kwenye hatua ya lenta kutokana na kukosa fedha. Wakati ujenzi unasimama kiasi cha shilingi 20,000,000 zilikuwa zimetumika. Tathmini ya kumaliza ili kuunga mkono nguvu za wananchi imeshafanyika na kiasi cha fedha shilingi 33,985,000 kinahitajika. Fedha hizo zitatengwa kwenye mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kurejesha kwa wananchi eneo la Namajani - Masasi kwa vile Jeshi la Magereza limeshindwa kuwalipa fidia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu,

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi Serikali iliwaelekeza wataalam wa ardhi wa Jeshi la Magereza na wataalam wa ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kupima eneo lililovamiwa na kubaini kuwa na ukubwa wa ekari 2,054 na eneo ambalo halikuwa limevamiwa na wananchi lilikuwa na ekari 1,696.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza kwa sasa linaendelea kumiliki eneo la ekari 1,696 ambazo hazikuwa na mgogoro. Kama hatua ya muafaka wa kumaliza mgogoro, Serikali ilikubali kuwaachia wananchi eneo lenye ukubwa wa ekari 2,054 lililokuwa tayari linatumiwa. Mwafaka huo ulifikiwa kwa kuwashirikisha wananchi wa Kijiji cha Ngalole, uongozi wa wilaya na Mkoa wa Mtwara, Wizara ya Ardhi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, nashukuru.
MHE. STANSALAUS H. NYONGO aliuliza: -

Je, lini jengo la Mahabusu katika Gereza la Maswa litakarabatiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu,

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Gereza la Maswa ni miongoni mwa magereza makongwe yaliyojengwa tangu kipindi cha ukoloni ambapo miundombinu yake inahitaji ukarabati.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Jeshi la Magereza inaendelea kuyafanyia ukarabati mdogo magereza nchini likiwemo Gereza la Maswa kwa kutumia fedha zinazotokana na vyanzo vya ndani. Gereza la Maswa limepangwa kuanza kufanyiwa ukarabati katika mwaka huu wa fedha 2023/2024, ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha jengo la Makazi ya Askari Polisi lililopo Kata ya Buyekera Bukoba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu,

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni moja kutoka kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2023/2024 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa jengo la makazi ya Askari Polisi lililopo Buyekera - Bukoba Mjini. Ujenzi huo unatarajiwa kuanza mara baada ya Wizara ya Fedha kuhamishia fedha hizo Jeshi la Polisi.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka Gari la Zimamoto Handeni Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea na jitihada za kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga bajeti ya jumla ya shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa magari matano ya kuzima moto ambayo yatagawiwa katika Mikoa na Wilaya zenye upungufu wa magari ya Zimamoto na Uokoaji, ukiwemo Mkoa wa Tanga, hususan Wilaya ya Handeni, nashukuru.
MHE. ABDI HIJA MKASHA aliuliza:-

Je, lini Kituo cha Polisi Micheweni kitakarabatiwa ili kiendane na hadhi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdi Hija Mkasha, Mbunge wa Micheweni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi ilifanya tathmini kwa ajili ya kubaini kiwango cha uchakavu na gharama za ukarabati wa jengo la Kituo cha Polisi Micheweni na kubaini kuwa jumla ya shilingi milioni 65 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati huo. Fedha hizo zimetengwa kupitia Mfuko wa Tuzo na Tozo katika mwaka wa fedha 2023/2024. Mara fedha hizo zitakapopokelewa, zitatumwa katika kituo hicho ili ukarabati wake uanze kufanyika, nashukuru.
MHE. NG’WASI D. KAMANI K.n.y. MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza:-

Je, lini Serikali itatoa idhini kwa Makampuni binafsi kutoa elimu ya kujikinga na majanga ya moto kwa Wananchi na Taasisi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa makampuni binafsi kushiriki katika shughuli za huduma ya zimamoto na uokoaji nchini, kama vile ufungaji wa mifumo ya kuzima moto, usambazaji na matengenezo ya vifaa vya kuzima moto kwa wananchi na taasisi. Serikali itafanya marekebisho madogo ya kanuni ya ukaguzi, tozo na cheti ya mwaka 2008 ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kutambua na kujumuisha makampuni binafsi katika utoaji wa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto kwa masharti na vigezo vitakavyowekwa na Serikali, nashukuru.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA aliuliza:-

Je, maombi mangapi ya usajili wa Taasisi na Madhehebu ya Dini yamewasilishwa tangu 2016 na hazijapatiwa usajili na sababu za kutosajiliwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2016 hadi Septemba, 2023, jumla ya maombi ya Usajili wa Taasisi na Madhehebu ya Dini 1,858 yalipokelewa katika Ofisi ya Msajili wa Jumuiya. Kati ya maombi yaliyopokelewa, Taasisi na Madhehebu ya Dini 419 yamesajiliwa, maombi manne yamekataliwa na maombi 1,435 yapo katika hatua mbalimbali za usajili. Sababu zinazosababisha baadhi ya Taasisi na Madhehebu ya Dini kuchukua muda mrefu kusajiliwa au kotosajiliwa ni pamoja na baadhi ya Taasisi na Madhehebu ya Dini kukosa vigezo vya kusajiliwa, kubadili anwani za Posta au Makao Makuu ya Taasisi bila kutoa taarifa na hivyo kukosekana kwa mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, baadhi ya Taasisi na Madhehebu kukosa maeneo stahiki ya kuendeshea shughuli zao na kuingia katika migogoro ya ndani, migogoro na jamii inayozunguka taasisi hizo au Mamlaka za Serikali zilizopo katika maeneo hayo au kukabiliwa na kesi katika mamlaka za utoaji haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya, inaendelea kushughulikia maombi ya Usajili wa Taasisi na Madhehebu ya Dini na kutoa usajili kwa wakati kwa taasisi zenye sifa stahiki na kuhakikisha kuwa Serikali haisajili taasisi na Madhehebu ya Dini ambayo yanaweza kuleta madhara kwa jamii au kuhamasisha vitendo ambavyo ni kinyume cha mila, desturi, utamaduni na maadili ya Kitanzania, nashukuru.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatatua tatizo la usafiri kwa ajili ya kusafirisha mahabusu na wafungwa katika magereza nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto iliyopo ya magari ya kusafirisha mahabusu na wafungwa kwa kuwapeleka Mahakamani na kuwarudisha gerezani. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Jeshi la Magereza ilitenga kiasi cha shilingi 878,125,000.00 katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya ununuzi wa magari matano ya kusafirishia mahabusu na wafungwa katika Magereza nchini. Aidha, katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga fedha, kiasi cha shilingi bilioni 1.93 kwa ajili ya ununuzi wa magari 14 kwa ajili ya kusafirisha mahabusu na wafungwa katika magereza nchini. Nashukuru.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -

Je, lini Serikali itamaliza Mgogoro wa Shamba la Gereza la Mollo – Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka ya nyuma kabla ya mwaka 2018 kulikuwepo na mgogoro wa mipaka ya ardhi kati ya gereza la kilimo Mollo na vijiji vya Msanda, Muungano, Malonje, Songambele na Sikaungu vinavyopakana na gereza hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikao cha Tarehe 24 mwezi Novemba 2023 kilichowahusisha Mheshimiwa Jerry William Silaa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na wataalamu wa ardhi kilimaliza mgogoro uliyokuwepo kati ya Gereza la Mollo na vijiji husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumaliza mgogoro huu ilikubalika na pande zote kwamba Jeshi la Magereza libakie na eneo lenye ukubwa wa ekari 8,989.4 na vijiji vibakie nae neo lenye ukubwa wa ekari 1,800. Baada ya makubaliano hayo Jeshi la Magereza lilipima na kubainisha mipaka ya eneo lake huku vijiji pia vikitambua maeneo yao. Hivyo kwa sasa hakuna mgogoro tena baina ya Gereza la Mollo na vijiji vinavyopakana nalo. Ahsante. (Makofi)