Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Irene Alex Ndyamkama (2 total)

MHE. IRENE A. NDYAMKAMA aliuliza:-

Je, Serikali haioni kuwa kuna haja ya kuendeleza kilimo cha zao la miwa kwa Wananchi wa Wilaya ya Kalambo na Nkasi na baadae kujenga kiwanda cha sukari ambacho kitatoa ajira kwa Vijana na Wanawake ndani ya Mkoa wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Irene Alex Ndyamkama, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sukari ni kati ya bidhaa muhimu sana nchini na matumizi yake kwa maana ya majumbani na viwandani. Kwa sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha wastani wa tani 320,000 kwa mwaka kwa ajili ya matumizi ya majumbani na wakati mahitaji halisi tani 485,000 na mahitaji ya sukari kwa matumizi ya viwandani ni tani 145,000. Pengo la takriban tani 165,000 kwa ajili ya matumizi ya majumbani na tani 145,000 kwa matumizi ya viwandani huagizwa kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua ongezeko la mahitaji ya sukari lisiloendana na uwezo wa uzalishaji wa sukari nchini, Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika miradi mipya na upanuzi ya uzalishaji wa mashamba ya miwa uzalishaji katika viwanda vya sukari ikiwemo viwanda vikubwa na vidogo vilivyopo nchini. Mwaka 2015, Bodi ya Sukari Tanzania ilifanya utafiti na kubaini uwepo wa maeneo yanayofaa kwa ajili ya wakulima wadogo na wa kati kwa ajili ya kilimo cha miwa na hatimaye tuweze kuongeza uzalishaji wa sukari. Aidha, Mkoa wa Rukwa ulibainisha maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo na viwanda ili tukipata wawekezaji katika sekta ya sukari waweze kuwekeza.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kitabu cha Mwongozo wa Uwekezaji cha Mkoa wa Rukwa, Mkoa umetenga jumla ya hekta 20 na hekta 15.65 katika Wilaya ya Kalambo na Nkasi Mtawalia kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha miwa. Hivyo, Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha zao la miwa katika maeneo yote yenye sifa za uzalishaji ikiwemo Wilaya ya Kalambo na Nkasi. Pia tunaendelea kuhamasisha kujenga viwanda kwa ajili ya kuchakata miwa ili kukidhi mahitaji ya sukari na pia kutoa ajira kwa Watanzania. Vile vile, Serikali kupitia Bodi ya Sukari inawahamasisha wawekezaji wakubwa na wadogo kuzalisha sukari ili kukidhi mahitaji yaliyopo hapa nchini.
MHE. IRENE A. NDYAMKAMA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakarabati Meli ya Mv. Liemba pamoja na kujenga meli mpya ambazo zitachochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, asante. kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Irene Alex Ndyamkama, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli imetenga kiasi cha shilingi bilioni 135 katika mwaka huu wa fedha 2020/2021 kwa ajili ya kutekeleza miradi tisa ya ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli katika Ziwa Victoria na Tanganyika. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa ukarabati wa meli ya Mv. Liemba ambayo tayari umeshapata mkandarasi na taratibu za kusaini mkataba zinakamilishwa na itasainiwa mwanzoni mwa mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na kutekeleza mradi wa ukarabati wa meli ya Mv. Liemba katika Ziwa Tanganyika, Serikali pia imepanga kutekeleza miradi ya ujenzi wa meli mpya ya kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Tanganyika, ujenzi wa meli mpya ya kubeba shehena ya mizigo katika Ziwa Tanganyika na ukarabati mkubwa wa meli ya kubeba shehena ya mafuta ya MT. Sangara katika Ziwa Tanganyika. Mikataba ya miradi hiyo ipo katika hatua za mwisho kusainiwa mapema mwanzoni mwa mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumai yangu kuwa, kukamilika kwa miradi hii kutaondoa adha ya usafiri kwa njia ya maji katika Ziwa Tanganyika na mikoa jirani na Kigoma. Aidha, kutaimarisha na kuifanya nchi yetu kuwa kiungo kikubwa cha soko pana la pamoja linalokisiwa kuwa na idadi ya watu takribani milioni 10 wanaoishi pembezoni mwa ziwa hili katika nchi za Mashariki na Kati ya Afrika ikijumuisha nchi ya Tanzania, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia, ahsante.