Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Alexander Pastory Mnyeti (15 total)

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga soko kubwa la Samaki Lindi Manispaa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa naomba nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kila kitu, pia ninaamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Hassan Suluhu kwa imani yake kubwa kwa kunipa nafasi hii nimsaidie kumuwakilisha katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya uvuvi nchini, ikiwemo masoko ya samaki katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi, kwa kuzingatia upatikanaji wa maeneo na rasilimali fedha. Changamoto iliyopo ni upatikanaji wa maeneo katika Halmashauri zetu kwa ajili ya ujenzi wa masoko. Kwa sababu hii, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwa nafasi yake, asaidie kupatikana kwa eneo la ujenzi wa soko hilo katika Manispaa ya Lindi na mara likipatikana, Wizara yangu itafanya tathmini za awali ikiwa ni pamoja na kuandaa michoro na gharama za ujenzi. Aidha, baada ya kukamilika kwa hatua hizo, Wizara itatafuta fedha za ujenzi wa soko hilo katika vyanzo vya ndani, yaani bajeti ya Wizara au miradi kwa ajili ya kuanza ujenzi.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuharakisha uwekaji samani kwenye maktaba na maabara Chuo cha FETA Mikindani?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024 Serikali kupitia Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) inaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia katika Kampasi zake ikiwemo ujenzi wa maabara na maktaba katika kampasi ya Mikindani. Pindi tuu ujenzi wa majengo hayo ya maktaba na maabara yatakapokamilika katika kampasi ya Mikindani, Serikali itaweka samani kwenye miundombinu hiyo muhimu. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza: -

Je, lini Serikali itatoa elimu kwa wafugaji kuhusu matumizi ya biogas ili kuhamasisha ufugaji wa kisasa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikitoa elimu ya ufugaji bora ikiwa ni pamoja na matumizi ya samadi kuzalisha biogas ambayo ni nishati mbadala ya kupikia na rafiki kwa mazingira.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya nishati mbadala ya biogas ambayo inatokana na kinyesi cha mifugo ikitumika vizuri, itapunguza matumizi ya kuni na mkaa hivyo kuboresha maisha ya wafugaji na kuhifadhi mazingira. Kutokana na umuhimu huo, Wizara kupitia Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA), inatoa mafunzo ya utengenezaji wa biogas kwa wanafunzi wanaosoma katika vyuo vyake katika ngazi ya cheti na diploma ili watakapohitimu masomo hayo, wawe na ujuzi wa teknolojia ya biogas na waweze kuwafundisha wafugaji matumizi sahihi ya teknolojia hiyo pia. LITA hutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wafugaji au vikundi vya wafugaji vinavyohitaji mafunzo hayo katika kampasi za Mpwapwa na Tengeru.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR aliuliza: -

Je, ni kwa kiwango gani bahari zinachangia kukua kwa uchumi kupitia uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bakar Hamad Bakar, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Uvuvi hutoa mchango katika uchumi wa nchi kupitia uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali zinazozalishwa ndani ya sekta. Aidha, baadhi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa hutumika kama mali ghafi katika uzalishaji ndani ya sekta nyingine kama vile viwanda na kuwa na mchango mkubwa zaidi katika sekta hizo. Katika mwaka 2022, sekta ya uvuvi ilichangia asilimia 1.8 ya Pato la Taifa huku ikikua kwa asilimia 1.9.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2022/2023, mazao ya uvuvi kutoka baharini yalichangia jumla ya tani 54,823 sawa na asilimia 10.6 ya mazao ya uvuvi ambayo ni tani 513,525. Vilevile, maduhuli ya Serikali ya shilingi bilioni 1.8 yalikusanywa kutoka katika shughuli za uvuvi baharini. Kiasi hicho cha mazao ya uvuvi kilichozalishwa kutoka baharini kilitokana na uvuvi mdogo na kilikuwa na thamani ya shilingi bilioni 356.3. Naomba kuwasilisha.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa mradi wa lambo Kata ya Nsimbo, Kijiji cha Mwenge, Halmashauri ya Nsimbo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo hapa nchini, Serikali ilianza ujenzi wa mabwawa manne ya maji kwa mifugo likiwemo bwawa la Isulamilomo lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo. Aidha, ujenzi wa Bwawa la Isulamilomo haukukamilika katika muda uliopangwa kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi, ikiwemo kukosekana kwa barabara ya kusafirisha mitambo kwenda eneo la mradi na kipindi kirefu cha mvua nyingi katika eneo la mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto hizo, Mkandarasi aliomba kuongezewa muda wa kukamilisha ujenzi wa bwawa hilo ambapo ujenzi unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2023. Kwa sasa, Mkandarasi yupo katika eneo la mradi akiendelea na kazi ya ujenzi wa tuta na njia ya utoro wa maji. Naomba kuwasilisha.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -

Je, lini mabwawa ya mifugo yatachimbwa Kata za Lagama, Masanga Mwamalasa, Ngofila, Bunambiyu, Mwasubi na Somagedi – Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo katika Jimbo la Kishapu. Kazi ya ujenzi wa mabwawa hufanyika kwa hatua kuu tatu ambazo ni; kutafuta chanzo cha maji (water source), kufanya usanifu na kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa kutambua changamoto ya upatikanaji wa maji katika jimbo la Kishapu hususani katika kata alizozitaja Mheshimiwa Mbunge, naomba kutoa wito kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kushirikiana na wataalam wa Wakala ya Huduma na Usafi wa Maji Vijijini (RUWASA), kuanza kazi ya kutafuta chanzo cha maji katika maeneo husika, kuandaa michoro (design) na mchanganuo wa gharama (BOQ) ili kuweza kupewa kipaumbele kwenye mpango na bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutoa wito kwa wafugaji na wadau wengine, kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya maji ya mifugo ili kusaidia kupunguza changamoto ya maji kwa ajili ya mifugo hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -

Je, lini Serikali itafanya marekebisho ya sheria zisizo rafiki kwa wavuvi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024 Serikali imepanga kuendelea kupitia na kufanya marekebisho ya Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 ili kukidhi mahitaji ya hali halisi ya sasa ya shughuli za uvuvi. Aidha, Serikali ina utaratibu wa kufanya maboresho ya kanuni mbalimbali za uvuvi mara kwa mara ili kuondoa kero na kuboresha mazingira ya biashara kwa wadau wa uvuvi. Kwa mfano, katika mwaka 2019 Serikali ilirekebisha kanuni kuruhusu leseni ya uvuvi iliyokatwa kwenye Wilaya moja kutumika katika Wilaya zote katika ziwa husika au ukanda wote wa bahari. Pia mwaka 2020 Serikali ilirejelea kanuni za uvuvi kuruhusu ongezeko la kina cha nyavu za makila katika Ziwa Victoria kutoka macho 26 mpaka macho 78 kwa uvuvi wa samaki aina ya sangara.

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na tathmini ya sheria, kanuni, na miongozo iliyopo katika sekta ya uvuvi ili kubaini sheria zisizo rafiki kwa wavuvi nchini na kuzifuta au kuzirekebisha. Aidha, Wizara yangu iko tayari kupokea maoni na ushauri wa wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge juu ya sheria zetu zinazohitaji kufanyiwa maboresho, naomba kuwasilisha.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Masoko ya Kuuzia Samaki katika Kata za Ninde, Wampembe na Kala Wilayani Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuboresha na kujenga miundombinu ya uvuvi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika. Katika mwaka 2023/2024, Serikali inajenga masoko ya samaki saba na mialo mitatu ambapo Wilaya ya Nkasi imepangiwa kujengewa mwalo wa Karungu. Aidha, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeingia Mkataba na Mkarandarasi Nice Construction and General Supplies Ltd. wenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kujenga mwalo wa Karungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalo huo wa Karungu utakaojengwa utakuwa na miundombinu ya soko ikiwemo chumba cha ubaridi, mtambo wa kuzalisha barafu na sehemu ya kuuzia samaki. Aidha, nimuombe Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Nkasi kutumia miundombinu hiyo kwa pindi itakapokamilika wakati Serikali inatafuta fedha za kujenga masoko ya samaki katika kata zingine zilizosalia. Vilevile, Serikali itaendelea kujenga miundombinu ya uvuvi katika maeneo mbalimbali nchini kuendana na upatikanaji wa fedha na mahitaji ya maeneo husika.
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa utambuzi wa mifugo baada ya kusitisha zoezi la utambuzi kwa kutumia hereni za mifugo?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Alexander Mnyeti majibu.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Novemba, 2022 Serikali ilisitisha kwa muda zoezi la utambuzi wa mifugo kwa njia ya hereni ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza ambazo ni pamoja na wafugaji kulalamika juu ya bei ya kuvisha hereni na baadhi ya wafugaji kukosa elimu sahihi ya utambuzi wa mifugo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekamilisha kufanya marekebisho ya kasoro la zoezi hilo la utambuzi zilizojitokeza ambapo bei ya kuvika hereni imeshuka kutoka 1,750 hadi shilingi 1,550 kwa ng’ombe na kutoka shilingi 1,000 kwa mbuzi na kondoo hadi shilingi 900. Pia, Wizara imekamilisha kuandaa mkakati wa utoaji elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa utambuzi wa mifugo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara kwa kushirikiana na wadau wa mifugo, inategemea kuanza awamu ya pili ya utambuzi wa mifugo kwa kuanza na mashamba makubwa ya mifugo ya Serikali, mashirika, watu binafsi, wawekezaji kwenye vitalu vya NARCO, vituo vya unenepeshaji ng’ombe wa maziwa, wafugaji wakubwa na wafugaji watakaokuwa tayari wakati wa zoezi hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. CHARLES M. KAJEGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Malambo ya kunyweshea mifugo katika Jimbo la Mwibara?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Charles Muguta Kajege, Mbunge wa Mwibara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa maji ya mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwa ni katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda; na aidha katika mwaka 2022/2023 Serikali ilianza ujenzi wa bwawa la maji ya mifugo katika Kijiji cha Kihumbo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambapo ujenzi wa bwawa hilo umefikia asilimia 95. Kazi inayoendelea kwa sasa ni ujenzi wa mabirika ya kunyeshea maji ya mifugo kabla ya bwawa kuanza kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali za kujenga mabwawa na kuchimba visima virefu kwa ajili ya maji ya mifugo bado mahitaji ni makubwa. Hivyo nitoe wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya kuhamasisha wafugaji na wadau wengine kuwekeza kwenye miundombinu ya maji kwa ajili ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. ABEID R. IGHONDO K.n.y. MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, ni malambo/mabwawa mangapi yatajengwa katika Halmashauri ya Itigi kwa ajili ya kunyweshea Mifugo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, ikiwemo katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi. Aidha, mwaka 2021/2022 Serikali ilikamilisha ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo katika Kijiji cha Mhanga Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya mabwawa na visima kwa ajili ya maji ya mifugo nchini ni makubwa. Hivyo, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ujenzi wa mabwawa na kuchimba visima katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Itigi. Kulingana na upatikanaji wa fedha, vilevile, ili kukabiliana na upungufu uliopo, na nitoe wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kuhamasisha wafugaji na wadau wengine kuwekeza katika miundombinu ya maji ya mifugo.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: -

Je, lini elimu ya uvuvi na mikopo ya vifaa vya kisasa vitatolewa kwa wananchi wa Manda, Ruhuhu, Iwela, Lupingu, Lifuma, Makonde, Kilondo na Lumbila?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika awamu ya kwanza ya mradi wa kuwawezesha wavuvi boti za kisasa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa jumla ya boti nne za kisasa kwa wavuvi wa Ziwa Nyasa. Kati ya boti hizo, boti mbili zimetengwa kwa wanufaika wa Halmashauri ya Ludewa ambazo nitazikabidhi kwa wanufaika hao hivi karibuni. Aidha, katika hatua za awali za upatikanaji wa wanufaika wa mikopo hiyo, wavuvi wa Ludewa Kata za Manda, Ruhuhu, Lumbila, Lupingu na Ludewa walipatiwa elimu na mafunzo ya uvuvi endelevu na utaratibu, upatikanaji na urejeshaji wa mikopo yaliyofanyika Tarehe 16 - 25 Oktoba, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2023/2024, Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi boti za kisasa ambazo zitatolewa kwa wavuvi wa maeneo yenye shughuli za uvuvi hapa nchini ikiwemo Halmashauri ya Ludewa. Aidha, katika mwaka huu wa fedha, Wizara itaendelea kutoa elimu na mafunzo ya uvuvi endelevu, ujasiriamali katika uvuvi na namna ya kunufaika na fursa za mikopo kutoka taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo TADB kwa wananchi wa maeneo ya uvuvi ikiwemo Ludewa. Ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha muundo wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu¬: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agness Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, muundo (organization Structure) wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi yaani Fisheries Education and Training Agency - FETA uliokuwa ukitumika ulipitishwa tarehe 1 Oktoba, 2018. Muundo huo ulikuwa unaendana na matakwa ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi yaani National Council for Technical and Vocational Education and Training - NACTVET, ambalo ndio linaratibu vyuo vya ufundi stadi ikiwemo FETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto ya vyuo vinavyoratibiwa na NACTVET kuwa na miundo isiyofanana, NACTVET walihuisha miundo ya vyuo wanavyo viratibu ili kuongeza tija katika utoaji elimu na pia kupunguza gharama za uendeshaji. Hivyo, kufuatia uhuishaji huo wa NACTVET, muundo mpya wa FETA uliidhinishwa Novemba, 2022 na kwa sasa Serikali inaendelea na taratibu za kujaza nafasi za uongozi katika muundo huo mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Majosho kwenye Vijiji vya Gwandi na Takwa – Chemba?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa majosho nchini ili kudhibiti magonjwa yanayoenezwa na kupe na wadudu wengine. Kupitia mpango huo, jumla ya majosho mapya 747 yamejengwa kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2020/2021 hadi Juni, 2023 yakiwemo majosho matano yaliyojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba katika Vijiji vya Tumbakose, Mlogia, Mondo, Msaada na Masimba ambapo ujenzi umekamilika na yameshaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Sipika, kwa kutambua umuhimu wa majosho katika kudhibiti magonjwa ya mifugo nchini, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali itaendelea kutenga fedha za ujenzi wa majosho maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya Vijiji vya Gwandi na Takwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa msaada wa kitaalamu kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu ili kuongeza idadi ya samaki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha samaki wanaendelea kuwepo na wanaongezeka katika maeneo yote ya maji, ikiwemo Bwawa la Nyumba ya Mungu. Mikakati hiyo ni pamoja na kufanya tafiti na kuimarisha ushirikishwaji wa jamii na taasisi zisizo za kiserikali katika kusimamia na kulinda rasilimali za uvuvi kupitia Halmashauri, Serikali za Vijiji na Vikundi vya kijamii vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU).

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kufanya tafiti za kujua wingi na mtawanyiko wa samaki katika maziwa makuu na imejipanga kutanua wigo wa kufanya tafiti (frame survey) kwa maziwa madogo ili kutambua hali halisi ya uvuvi katika maziwa hayo. Aidha, tafiti hizo zinatoa taarifa sahihi ili kuiwezesha Wizara kutekeleza mikakati ya kuongeza wingi wa samaki ikiwemo uwezekano wa kupandikiza samaki.

Mheshimiwa Spika, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa, Wizara itaendelea na utoaji wa elimu ya Huduma za Ugani kuhusu athari za uvuvi haramu ili kulinda mazalia ya samaki na kuruhusu samaki kukua na kuongezeka kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.