Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Haji Amour Haji (4 total)

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa vile Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa sheria ya makampuni ya ulinzi binafsi, swali langu ni hili; je, sheria gani kwa sasa hivi inayotumika kuwapatia vibali hayo makampuni binafsi ya ulinzi?

Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa sasa hakuna sheria mahususi kwa ajili ya kazi hiyo, badala yake inatumiwa miongozo inayotolewa na Mkuu wa Polisi Nchini (IGP).
MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa ruhusa yako nina maswali mawili ya nyongeza: -

Swali la kwanza, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo katika jitihada za kuwaita wawekezaji nchini kwetu Tanzania kwa ajili ya kuja kuwekeza nchini mwetu, wakati huo huo pia kuna kuwa na idadi kubwa ya wageni ambao wanakuja Tanzania kwa ajili ya kuja kujifunza.

Je, kwanini vibali vinachelewa?

Swali la pili, ninamuomba Mheshimiwa Waziri kama ataridhia kwake tukaongozana mimi na yeye kufanya ziara ya maksudi kwenda kuangalia mtambo ule ambao ulikuwepo Zanzibar na kuangalia vile vibali walau 100 vilivyochapishwa kwa mwaka huu 2022. Naomba sana hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haji Mbunge wa Pangawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya kuchelewa, kwanza nikiri hii changamoto ipo, lakini changamoto hii inasababishwa zaidi na wananchi wenyewe au wale ambao wanaotaka kuomba vile vibali vyewewe. Sababu moja ni za kimtandao unajua tumeingia katika e-permit kwa hiyo time nyingine inawezekana mtandao ukawa unasumbua ukachelewesha kidogo, lakini sababu nyingine ni kwamba wananchi wenyewe au wale ambao wanaomba zile permit huwa wanafika wakati wanakuwa wanashindwa kukamilisha vigezo na masharti hivi vinapelekea sasa kuchelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa ni kwamba kuna baadhi ya watu huwa wanawapitisha hawa wageni katika njia ambazo siyo rasmi wala siyo sahihi hii inapelekea vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kwa upande wa kwenda kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi tupo tayari kwa ajili ya kwenda huko kukagua huo mtambo huko Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi nina swali langu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kisheria wahusika wakuu wa mfuko wa jimbo kwa upande wa Bara na Wizara inayohusiana na masuala ya Serikali za Mitaa, lakini kwa upande wa Tanzania Zanzibar wasimamizi wakuu ni Wizara ya Muungano inayohusika na masuala ya Muungano.

Swali langu je, ni sababu zipi fedha za Mfuko wa Jimbo kupelekwa katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais zisizimamiwe kupitia Ofisi ya inayoshughulikia masuala ya Muungano? Ahsante sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naomba kujibu swali la kaka yangu; ni kwamba Wizara yetu ni Wizara ya Muungano, lakini katika masuala ya uratibu kwa upande wa Zanzibar ofisi inayohusiana na masuala ya uratibu yote ni Ofisi ya Makamu wa Pili na hata hivi asubuhi nilikuwa naongea na pacha wangu, ndugu yangu Hamza katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo. Kwa hiyo, jambo hili halina mashaka, isipokuwa ni kwamba jambo kubwa linahitajika ni jinsi gani tutafanya kama kulikuwa na changamoto mbalimbali ya utekelezaji wa miradi lengo letu sisi kubwa kuweza kuingilia.

Mheshimiwa Spika, ndio maana nishukuru sana hata hapa nyuma Bwana Abdulwakil pale nilienda mpaka jimboni kwake wakanieleza masuala mbalimbali ya changamoto na tukaanza kuyatatua. Na mimi niwashukuru sana Wabunge wa Zanzibar baada ya kuibua changamoto mbalimbali za fedha za Mfuko wa Jimbo sasa ninaamini japo kama inawezekana matatizo bado yapo lakini naamini sasa hivi angalau kidogo speed ya utekelezaji imebadilika sana ukilinganisha na miaka ya nyuma iliyopita. Kwa hiyo tunaamini kwamba suala la uratibu linaenda vizuri mpaka sasa.
MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza nashukuru kwa jibu lake zuri Mheshimiwa Naibu Waziri, pia nina swali langu la nyongeza.

Katika Jimbo langu la Pangawe kuna kituo kidogo cha polisi kinaitwa Kijitopele. Bahati nzuri kwamba au bahati mbaya kunakuwa na wahalifu wengi sana ambao wanakitumia kituo kile na ukiangalia wahalifu wale maana yake wanakuwa hawana nafasi ya kutosha ndani ya kituo kile. Je, Serikali ina mpango gani kukiboresha Kituo cha Kijitopele? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Haji Amour Haji, Mbunge wa Pangawe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishasema katika nyakati tofauti na bahati nzuri kwa Zanzibar nimeshatembelea vituo hivyo na kubaini kwamba vingine vina hali dhaifu, tutaendelea kupitia Mfuko wa Tuzo na Tozo kuviimarisha vituo hivi na kuwapanga askari watakaotoka vyuoni ili waweze kusimamia usalama wa raia na mali zao kikiwemo hiki kituo alichokitaja Mheshimiwa Mbunge wa Pangawe. Nashukuru.