Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Martha Nehemia Gwau (3 total)

MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, la kwanza. Je, ni mamlaka gani hasa inayosimamia uingizaji wa zebaki nchini?

Mheshimiwa Spika, lakini kingine, Serikali iko tayari kutenga fedha kwa ajili ya kwenda kutoa elimu ya madhara ya kemikali hiyo ya zebaki kwa wananchi wanaojihusisha na uchimbaji wa madini, hususan Mkoa wangu wa Singida, Ikungi na Wilaya ya Iramba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza swali lake la kwanza ni mamlaka gani inayohusika na kusimamia uingizaji wa kemikali hizi nchini:-

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema kwenye swali la msingi, ni Mkemia Mkuu wa Serikali, lakini ili tuweze kufanikiwa kwenye hili ni suala ambalo linahitaji kushirikisha mamlaka mbalimbali. Kwa hiyo, kikubwa ni kwamba, kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mamlaka mbalimbali ambazo zinahusika zitashirikishwa, ili kuhakikisha kunakuwepo na udhibiti wa kina.

Mheshimiwa Spika, lakini swali lake la pili. Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu suala hilo:-

Mheshimiwa Spika, ni swali zuri, na nafikiri iko tayari na kwa sababu tunahitaji kwakweli kutoa elimu pamoja na kudhibiti kwa maana ya kuwasajili watu kama hao wanaoingiza, lakini vilevile kuna umuhimu wa ufuatiliaji, ili zebaki isiweze kuingia kwa njia za panya. Lakini wakati huohuo kwenda kutoa elimu hasa kwenye maeneo ya madini ambayo wanachimba dhahabu, kwenye makaa ya mawe ambao wanahitaji kutumia zebaki. Wakati huohuo kwenye hospitali zetu ambazo vilevile zenaki inatumika, kuhakikisha kwamba, wakati wa ku-despose hivyo vitu vinakuwa disposed vizuri. Vilevile kuwajulisha wananchi namna nzuri ya kutumia, lakini kununua vifaa ambavyo wakati wachimba madini wanapokuwa wanatumia basi kuwe na mashine na vifaa maalum ambavyo vinasababisha hivyo vitu visiweze kutoka na kuingia kwenye jamii.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nafikiri swali lake Serikali iko tayari na nafikiri kwa ajili ya kufanya hatua hiyo fedha zinahitajika.
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa katika mikoa 12 iliyotajwa ya hizo nyumba, Mkoa wa Singida siyo miongoni mwa Mikoa iliyo na hiyo huduma. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha nyumba hizo katika Mkoa wa Singida?

Swali la pili, kwa kuwa ukatili kwa watoto bado unaendelea siku hadi siku. Je, Serikali imefikia wapi au ina mpango gani wa kuanzisha Vituo vya Kulelea Watoto (ECD Centers) ili kuhakikisha kwamba wazazi wanakuwa wanawaacha watoto kwenye mikono salama? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Nehemia Gwau: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kujenga nyumba salama katika Mkoa wa Singida, ni dhahiri kwamba iko mikoa mingi kweli ambayo haina nyumba salama, hapa ni mitano tu inayo, na wizara inafanya jitihada za kuwasiliana na wadau ambao wamekuja kutusaidia katika mapambano haya ya kutokomeza ukatili. Andiko hilo likipita, tutapeleleka hizi rasilimali katika maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa ikiwemo huko Singida.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kupitia mwongozo huu, tunaomba mamlaka za Mikoa na Halmashauri na wadau walioko huko waone umuhimu wa kuanza kuanzisha nyumba hizi wakati Wizara inakuja kuongezea nguvu. Vilevile kwenye bajeti zinazokuja; mwaka ujao tutaendelea kutenga fedha kidogo katika ngazi zote kwa ajili ya kuchochea ujenzi wa nyumba Salama hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu maelezi ya Watoto, ni kweli, mpango wa Serikali ni kuhakikisha watoto wanalelewa vizuri kwa kuwajengea vituo vya kuwalea na kuwakuza katika maeneo ya jamii. Sasa tuna vituo 200 tumeshirikiana na wadau kuvijenga. Formular ni ile ile, tunahamasisha wadau waliopo kwenye Halmashauri zetu waendelee kujitokeza na kuchangia fedha kwa ajili ya vituo hivi, lakini kwenye bajeti zetu tutatenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hivi sasa Wizarani tuna kikao kinaendelea cha resource mobilization. Hivyo, tukiipata, tutaanza kuwapelekea wale ambao wameshamiliki na wameanza huku tukiwaelimisha wengine ambao bado hawajaona umuhimu huo, kuamka na kujipanga kwenye bajeti za mwaka unaokuja, ahsante.
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Kwa kuwa Mkoa wa Singida ni jirani kabisa na Mkoa wa Dodoma ambao ndiyo Makao Makuu ya nchi: Je, ni lini Kiwanja cha Ndege Singida kitakamilika ili wananchi wa Singida wapate huduma; lakini pia uwanja huo wa Singida utumike kama uwanja wa dharura kama Dodoma kuna changamoto? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Singida ni mkoa ambao uko karibu na Dodoma na Serikali tayari imeshafanya usanifu wa Uwanja wa Singida ili uweze kujengwa, kwani unaweza ukatumika sana pale ambapo kunatokea changamoto katika viwanja vya Mkoa wa Dodoma, ahsante. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi kwa kunisaidia. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya usanifu kukamilika, hatua inayofuata sasa ni kujua mahitaji halisi kwa ajili ya fidia ili hatimaye tuweze kuanza kufanyia kazi huo uwanja. (Makofi)