Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rose Vicent Busiga (3 total)

MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nami naomba niulize swali la nyongeza.

Je, katika hizo fedha shilingi bilioni 8.75 Kituo cha Afya cha Nkhomola kitakuwa ni miongoni mwa vituo vya kupatiwa hizo pesa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rose, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, fedha hizi ambazo zimetengwa shilingi 8,750,000,000 zitakwenda kuainisha vituo vya afya 20 vyenye uchakavu wa hali ya juu zaidi. Kwa sababu sina orodha hapa naomba kwa ridhaa yako baada ya kipindi hiki nitaangalia na kuona kama kituo hicho ambacho amekitaja Mheshimiwa kipo kwenye orodha hiyo, ahsante.
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza: -

Ni lini Serikali itapeleka umeme katika Kata ya Ng'homolwa, Kijiji cha Nkweni?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rose Busiga, Mbunge wa Viti Maalum Geita, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba naamini kijiji hicho na kata hiyo ipo katika mradi wetu wa REA III Round Two, na kabla ya mwaka huu kuisha kijiji hicho kitakuwa pia kimepata umeme kwenye baadhi ya vitongoji na sasa maendeleo yataendelea kwenye vitongoji ambavyo vitakuwa vimebaki.
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naomba niulize swali la nyongeza. Katika Mkoa wetu wa Geita kuna nyumba nyingi sana za Askari ambazo ni chakavu; je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kukarabati nyumba hizo za askari ili askari wetu wa Mkoa wa Geita waweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema hapo awali kwamba kwa sasa Serikali tunatafuta fedha na zitakapopatikana, pamoja na maeneo mengine yenye uchakavu wa nyumba na vituo, tutahakikisha kwamba Mkoa wa Geita nao tunautazama, lengo na madhumuni sasa wananchi waweze kupatiwa huduma hizo vizuri zaidi, nakushukuru.