Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Salim Mussa Omar (6 total)

MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza:-

Je, ni nini kinachosababisha mabadiliko makubwa ya bei za tiketi za ndege za Air Tanzania kwa safari za Dar es Salaam na Dodoma ambapo mara nyingi hufika hadi shilingi laki sita?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salim Mussa Omar, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa uuzaji wa tiketi katika biashara ya usafiri wa anga ni mojawapo ya mikakati ya ushindani ili kuvutia wateja. Mashirika ya Ndege hushindana kwa kutumia mkakati huu ambapo tiketi hupangwa katika ngazi mbalimbali kufuatana na vigezo mbalimbali kama vile bei ya tiketi, ujazo wa ndege, muda wa kukata tiketi, masharti ya tiketi na daraja la usafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutumia kigezo cha ujazo wa ndege na muda ambao abiria anakata tiketi, mteja anayekata tiketi mapema na kukuta ndege haijajaa hupata bei ya chini ukilinganisha na mteja anayekata tiketi muda mfupi kabla ya safari yake na kukuta ndege imejaa, ambapo mara nyingi huwa siku chache au muda mfupi kabla ya safari, hupata bei za juu. Mfumo huu unatumika Kimataifa na mashirika yote ya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ATCL bei hizi zimepangwa katika ngazi mbalimbali. Kwa mfano, katika safari ya Dodoma kwenda na kurudi, ATCL ina jumla ya ngazi 13 katika daraja la kawaida (economy class) ambapo bei zake zinaanzia shilingi 331,400/= hadi shilingi 678,400/=. Bei ya juu ya wastani wa shilingi 600,000/= ni viti 10 kati ya jumla ya viti 76 vya ndege nzima sawa na takribani asilimia 13 ya ujazo wa ndege. Hivyo, abiria wakiwahi kukata tiketi wana nafasi kubwa ya kupata bei za chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kuna daraja la biashara (business class) ambalo kuna viti sita tu na ni kwa abiria yeyote ambaye yupo tayari kulipa katika daraja hilo. Daraja hilo linatoa huduma maalum, kwa mfano, mteja anapewa kilo saba zaidi za mzigo ukilinganisha na daraja la kawaida, mteja hupatiwa mhudumu wa kumsikiliza kwa haraka muda wowote akiwa ndani ya ndege, mteja kutokuwa na gharama za kubadilisha safari akifanya mabadiliko hayo kwa mara ya kwanza na pia mteja hupewa kipaumbele wakati wote wa safari kuanzia wakati wa ukaguzi (check in). Kutokana na sababu hizi, gharama za daraja hili ni kubwa kuliko daraja la kawaida. Daraja hili la biashara lina ngazi nne zenye bei kati ya shilingi 721,600/= hadi shilingi 953,000/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maelezo hayo, namwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL kufanya utafiti wa nauli zinazotozwa na mashirika ya ndege washindani kwa safari za ndani ili kuziwianisha na kisha kupanga nauli zinazoweza kuvutia Watanzania wengi kutumia ndege za ATCL. Ahsante. (Makofi)
MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza magari ya kisasa ya zimamoto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salim Mussa Omar, Mbunge wa Gando kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji imekamilisha hatua zote za mkopo wa Euro milioni 4.9 kutoka Nchini Austria kwa ajili ya ununuzi wa magari 12 ya kuzima moto. Kati ya magari yanayonunuliwa mawili ni ya ngazi (Turntable ladder) kwa ajili ya kuzima moto katika majengo marefu. Aidha, Jeshi la Zimamoto na Uokozi linatarajia kupata magari matatu ya kuzimia moto ambayo yalipatikana kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 kutoka Shirika la Nyumbu Tanzania Automotive Technology Center (TATC).
MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza: -

Je, kuna Mwongozo unaosema kuwa Zanzibar Insurance Corporation haipaswi kushiriki kukata Bima za Miradi mikubwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI K.n.y. WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Omar Salim, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Bima la Zanzibar (Zanzibar Insurance Corporation) limesajiliwa kwa kupewa leseni Na. 00000821 na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) chini ya Sheria ya Bima Na. 10 ya Mwaka 2009. ZIC inafanya biashara za bima sehemu zote Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya bima nchini ni huria na inaendeshwa kwa jumla ya makampuni 31 ya bima ikiwemo ZIC. Aidha, kampuni zote zina haki sawa ya kutoa kinga ya majanga kwa miradi mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar. Hivyo, hakuna Mwongozo wowote unaokataza Zanzibar Insurance Corporation kushiriki katika biashara ya kukata bima za miradi mikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muktadha huo, Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), kama ilivyo kwa kampuni nyingine yoyote ya bima iliyosajiliwa chini ya Sheria ya Bima Na. 10 ya Mwaka 2009, inaruhusiwa kuweka kinga ya bima kwa miradi mikubwa. Ahsante.
MHE. KASSIM HASSAN HAJI K.n.y. MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuandaa Filamu zenye kueleza Historia ya Nchi?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salim Mussa Omar, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Filamu Tanzania kwa kushirikiana na wadau imewezesha uzalishaji wa filamu zinazohifadhi na kuelezea historia ya nchi yetu.

Mfano Makala ya Uzalendo iliyoandaliwa na Bodi ya Filamu mwaka 2021 kupitia muandaaji filamu Bwana Adam Juma inaelezea historia ya viongozi wetu na ushujaa wao katika kuipambania nchi. Pia, mwaka 2022 Bodi kupitia Studio za Wanene iliandaa makala inayotangaza mandhari ya kupiga picha za filamu na kuelezea maeneo ya kihistoria yaliyopo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Bodi ya Filamu inaendelea na maandalizi ya filamu inayohusu maisha ya Chifu Mkwawa iitwayo Mkwavinyika. Pia kwa kushirikiana na wadau wa filamu, Bodi inaratibu mpango mahsusi wa uandaaji wa filamu zinazohusu maisha ya viongozi wetu, ambapo itaanza na filamu ya Bibi Titi Mohammed, ikifuatiwa na ya Chifu Kingalu, Mtemi Mirambo pamoja na Mwalimu Nyerere.
MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza:-

Je, lini Shirika la Ndege Tanzania litaanza safari za Pemba?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kutujalia afya njema. Pili, kwa sababu ninasimama kwa mara ya kwanza hapa, nitumie nafasi hii kwa unyenyekevu mkubwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi. Kwa unyenyekevu mkubwa nimepokea uteuzi huu na ninaahidi kufanyakazi kwa juhudi, maarifa kwa ajili ya maslahi makubwa ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee ninakushukuru wewe kama mlezi na Kiongozi wangu kwa ushirikiano mkubwa ulionipatia nikiwa Msaidizi wako kwa nafasi ya Mwenyeketi wa Bunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Kilimo na Mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, ninaomba sasa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi kujibu swali la Mheshimiwa Salimu Mussa Omar, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ATCL itaanza safari za Pemba baada ya kupata ndege za kutosha kuweza kutoa huduma bila kuharibu ratiba za safari za sasa na urukaji kwa wakati. Kwa kuwa mwisho wa Septemba, 2023 ATCL inatarajia kupata ndege mpya moja aina ya Boeing B737-9MAX na ndege ndogo aina ya Dash 8 Q300 matengenezo yake yanatarajiwa kuwa yamekamilika na kurejea katika ratiba zake za utoaji wa huduma. Uwepo wa ndege hizo kutaiwezesha ATCL kuanzisha safari zake katika kituo cha Pemba kwa tija na ufanisi mkubwa.
MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza kodi kwa kampuni changa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salim Mussa Omar, Mbunge wa Jimbo la Gando kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na utaratibu wa kuzingatia misingi ya utozaji kodi, Serikali imetoa unafuu kwa biashara na kampuni changa kwa kuzitoza kodi miezi sita baada ya kuanzishwa kwake na kodi ya mapato kwa kampuni hizo huanza kutozwa baada ya kuanza kutengeneza faida ambayo hukokotolewa kulingana na faida iliyopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na zoezi la mapitio ya mfumo wa kodi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya bajeti ya mwaka 2023/2024. Mwelekeo wa Serikali ni kuboresha zaidi mazingira ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji hasa kwa kampuni changa ikiwemo uboreshaji wa mifumo ya usimamizi wa kodi, kufanya tathmini ya tozo mbalimbali zilizopo kwa lengo la ama kupunguza viwango au kuzifuta kabisa pale ambapo zinaonekana ni kero kwa biashara au kampuni changa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.