Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jacquline Andrew Kainja (14 total)

MHE. JACKLINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii niweze kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na kwamba tunajua Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inajitahidi kupunguza ajali za bodaboda, tukiangalia kwa mwaka 2019 tulikuwa na ajali 567 lakini mwaka 2020 tuna 240. Je, Jeshi la Polisi lina mpango gani wa kuhakikisha ajali hizi zinapungua zaidi? Tukiangalia wahanga wakubwa ni vijana na wanawake ndiyo wanaopata shida ya kupoteza vijana ambao ni nguvukazi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; utafiti unaonyesha askari wastaafu wanachelewa kupata mafao yao, je, Wizara husika ina mpango gani wa kuhakikisha askari hawa baada ya kustaafu wanapatiwa mafao yao kwa haraka ili kuepusha wanapokuwa kazini kuchukua rushwa ili kujilimbikizia akiba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika jibu la msingi inaonekana Mheshimiwa tumempa sababu moja au njia moja ambayo tunaweza tukaitumia katika kuepuka hizi ajali. Zipo njia ambazo tumeshazichukua kama Serikali na nyingine tuko mbioni kuzichukua kwa kushirikiana na Wizara nyingine au kushirikiana na taasisi nyingine kuhakikisha kwamba hizi ajali za barabarani zinapungua. Cha kwanza tumefikiria kuendelea kuwafundisha zaidi hasa vijana wa bodaboda namna ya kutumia alama za barabarani ambazo zina uwezo mzuri wa kuwaeleza kwamba wanakoelekea wanaweza wakapata ajali.

Mheshimiwa Spika, lingine tuna mpango sasa wa kutengeneza mfumo wa kufunga au ku-control ajali kwa kutumia vidhibiti mwendo, ambapo tunahisi hivi vinaweza kupunguza ajali. Pia tuna mpango wa kufanya marekebisho ya sheria ambayo yanakwenda moja kwa moja kwenye masuala ya faini na adhabu katika mambo haya ya usalama barabarani.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge atusaidie pia kuwaelimisha vijana kwa sababu naamini katika mkoa wake vijana wa bodaboda wapo, basi azidi kuwaelimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kujibu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kuhusu mafao ya Askari. Kwa kweli Wizara inajitahidi sana kuhakikisha kwamba tunawalipa wastaafu posho zao mara tu baada ya wao kustaafu. Katika kipindi cha 2018/2019 tumejitahidi kati ya wastaafu 591; jumla ya wastaafu 479 tayari tulishawapatia mafao yao na sasa hivi wengi wanaishi maisha mazuri.

Mheshimiwa Spika, kikubwa kinachokuwa kinatukabili kama sehemu ya changamoto, inafika wakati inakuwa OC nazo na bajeti nayo inakuwa mtihani, kwa hiyo, ndiyo maana kuna wakati wanachelewa kidogo kulipwa. Hata hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kama itakuwa kuna mtu ambaye hajapata mafao yake na amestaafu, basi tukitoka hapa tuonane, tuone tunamsaidia vipi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na jitihada nzuri za Wizara inavyofanya kuzitangaza zao la asali nchini, lakini bado hatujafanya vizuri kwa masoko ya nje ambayo inapelekea wafanyabiashara wengi wa nchini wanashindwa kufanya vizuri kwa masoko ya nje hususan ni Mkoa wa Tabora na tukiangalia kinamama wengi wa Mkoa wa Tabora wamejikita kwenye uvunaji wa asali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Wizara inakuja na mkakati upi kuhakikisha soko la nje la zao la asali linafanya vizuri kama ambavyo zao la asali linafanya vizuri ndani ya nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, pamoja na jitihada nzuri zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuhakikisha zao la asali linaendelea kuwa na thamani, mpaka kupata wafadhili kutoka Umoja wa Ulaya.

Je, Wizara imeweka mikakati ipi na mipango madhubuti ya kutenga pesa kwa ajili ya kuhakikisha mradi huu walioweka kusaidiwa na Umoja wa Ulaya unaweza kuendelea hata kama mradi ule, hata kama wafadhali watachelewesha pesa au hawatoleta pesa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jacqueline, Mbunge wa Viti Maalum Tabora kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tabora Mheshimiwa Jacqueline kwa kuona umuhimu wa zao hili la asali. Ni kweli Tanzania tunafaidika kwa asilimia kubwa kwa soko hili la asali kuuza ndani na nje ya nchi. Mkakakati wa Wizara na Serikali kwa ujumla ni kuhakikisha kwamba asali yetu inakuwa na ubora zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba kwa sasa hivi wizara inashikirikiana na Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani kupeleka sampuli za kemikali za asali ambazo huwa zinachakatwa na kuangalia ubora wa asali ya Tanzania. Na kwa asilimia 90 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 tulipeleka asali yetu ya Tanzania na ikaonekana kwa asilimia 90 ni nzuri na inafaa kuuzwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Tanzania sasa itaanza kupeleka asali kwenye nchi za Ulaya na Marekani kwa kuwa tumekidhi vigezo vya viwango vya ubora wa asali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwenye mikakati ya kutenga fedha nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa sasa tuna mkakati wa kuanzisha viwanda vitano. Viwanda vitatu tayari vimeshajengwa na viwili tunakarabati. Lakini pia hii ni mwanzo wa kuhakikisha kwamba tayari tuna vyanzo vyetu sisi wenyewe bila kutegemea misaada mingine ambavyo vitaweza kukusanya asali yote nchini na itachakatwa kwenye viwanda hivi na kuhakikisha soko la ubora wa asali linapatikana na tunaweza kuuza nje na ndani ya nchi. Ahsante. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Kutokana na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri yanayowapa matumaini wafanyabiashara wa usindikaji wa mbogamboga hasa kwa Mkoa wa Tabora hususan kinamama.

Je, ni lini Serikali kushirikiana na FAO inaweza kuanza mradi huu wa kuwawezesha kina mama kuweza kufanya biashara ya Kitaifa na Kimataifa?

Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi kuwezesha mazao haya ya usindikaji wa mbogamboga ambayo wakinamama wengi wa Mkoa wa Tabora wamejikita katika biashara hiyo kuhakikisha kwamba yanakuwa yana masoko ndani ya nchi na ukizingatia unaweza ukaenda kwenye hoteli nyingi hatuna mboga za asili, tunatumia mboga ambazo ni roast na zilizoungwa ungwa zaidi. Naomba kupata jibu, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naoba kumjibu Mheshimiwa Jacqueline maswali yake ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, lini tunaanza mradi wa FAO, tunaaza mwaka wa fedha unaokuja; ni mradi wa miaka mitano, tunaanzia majaribio katika Wilaya ya Kaliua ndipo tutakapoanzia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kuwasaidia wakinamama wa Mkoa wa Tabora na Watanzania wote kuweza kuingia katika masoko. Sasa hivi tunapata project pamoja na wenzetu wa SIDO ili waweze kukidhi vigezo vya viwango vinavyoweza kuwasaidia kuingia katika masoko ndio maana mmesikia katika Mkoa wa Tabora tumesema kwamba Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Umoja wa Wanyabiashara sasa hivi pamoja na SIDO inatafutwa eneo moja ambalo litakuwa ni center ya kina mama kwa ajili ya kukaushia na hapo kuweza kufanya packaging waweze ku- meet standard za masoko. Kwa hiyo, ni hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo la msingi sio tu kuzalisha, je tunachokizalisha kinaweza kukidhi vigezo vinavyotakiwa vya sokoni, hiyo ndio kazi tunayoifanya katika sekta ya mbogamboga na matunda.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwamba na wewe umeweza kuona hili swali halijajibiwa na mimi nimegundua hivyo, lakini nimpongeze Waziri kwa majibu mazuri yanayoonyesha namna gani Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan imeendelea kupanga bajeti kuendelea kuhakikisha maboma ambayo yanatakiwa kukamilishwa yakamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tu nipatiwe majibu mazuri, ambayo yanaendana na swali langu ili niweze kuridhika sasa kwamba ni lini Serikali inaweza ikaona kuna mpango mzuri kwenye hizi Kata ambazo ni kubwa hazina zahanati ili wananchi hawa waweze kupata zahanati na siyo kwamba kuna maboma hakuna hata hayo maboma ambayo yanatakiwa kukamilishwa yaani ni ujenzi mpya, Serikali ina mpango gani na njia ipi madhubuti kuhakikisha kwamba Kata ambazo ni kubwa mfano, Kata hii ya Ng’ambo ambayo iko Tabora Mjini na zingine nyingi ambazo sijaziainisha zinaweza kupata ufumbuzi huo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa sasa Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwanza tunamaliza ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Tarafa zote nchini. Tangu uhuru tulikuwa tuna Tarafa 570 na tulikuwa na Tarafa 363 tu pekee ambazo zilikuwa na Vituo vya Afya na katika Awamu ya sasa hivi tulikuwa na Vituo vya Afya kama 207 ambavyo Serikali tayari imeshapeleka fedha kwa awamu mbili ambazo nafikiri kila Mbunge anazo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tukija kwenye level ya zahanati kwa kila Kijiji lengo la Serikali ambalo tumeliweka na ndiyo maana nimejaribu kuelezea hapa fedha ambazo tumezitenga ni kwa ajili ya kwenda kumalizia zahanati ambazo zimeanzishwa na nguvu za wananchi na nyingine zimeanzishwa na mapato ya ndani ya Halmashauri na ndiyo maana kwenye swali hili la msingi lilipokuwa linaulizwa, tumemshauri Mbunge wa Jimbo na Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Tabora kwamba, hamasisheni wananchi mkishirikiana na vyanzo vya ndani muanze ujenzi ili sisi kutoka Serikali Kuu tulete fedha kwa ajili ya kumalizia hiyo zahanati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukisema kwamba tutajenga zahanati vijiji 12,000 kwa wakati mmoja kwa sasa hivi hatuwezi kudanganya kwenye hilo, ukweli wetu ni kwamba tunamaliza Vituo vya Afya Tarafa zote, tunamaliza Hospitali katika Halmashauri zote halafu kwenye ngazi ya vijiji tutapeleka fedha, kwenye vijiji vyote ambavyo zahanati wananchi wamepeleka nguvu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hilo ndiyo jibu letu, ahsante. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa jibu zuri la Serikali, lakini kutokana na umuhimu wa hospitali hii ya Kanda ambayo inajumuisha mikoa mitatu; Kigoma, Katavi na Tabora; nataka majibu ambayo yataweza kutuonesha Wana-Kanda ya Magharibi ni lini hasa hospitali hii itaanza kujengwa kutokana na kwamba eneo lilishatengwa kama ambavyo amesema na katika Kata ya Magili kwa hekari 200? Hii itasaidia wananchi wasianze kufanya shughuli za maendeleo kwa kuzingatia ni muda mrefu mchakato huu walishasema utafanyika lakini bado haujafanyika.

Je, Serikali inaweza kutueleza ni lini hasa kazi hii inaweza ikafanyika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ambavyo nimeshaeleza kwenye swali la msingi kuhusu tathmini; kwanza fedha za kwanza ambazo makadirio ya kuanza, kwa sababu ni fedha ambazo hazitamaliza, lakini zimeshatengwa shilingi bilioni 10 za kuanza, lakini kazi inayofanyika ni kuangalia kwenye mikoa hiyo kuhusu umbali, kwa sababu hatuangalii tu Hospitali ya Kanda kwamba tunaweka Magharibi au wapi, tunaangalia ni mikoa ipi na ni mkoa upi upo mbali na facilities kama hizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukiangalia kutoka Tabora kuja Benjamin Mkapa ni Kilomita ngapi? Tabora kuja hospitali nyingine ya Kanda ni Kilomita ngapi? Hii itasaidia tuweze kuamua eneo sahihi ambalo huduma itawasogelea wananchi walio wengi na tuangalie eneo ambalo vile vile huduma nyingine ziko mbali na wananchi ambazo wengine wako karibu nazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, upembuzi bado unafanyika ili kutambua eneo ambalo hospitali itaenda kuwekwa kwa kutumia busara kusogezea huduma wananchi walio wengi zaidi. Ahsante.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha usanifu wa matenki na michoro ya miundombinu katika Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria inayoenda katika Miji ya Urambo, Sikonge na Kaliua inaisha? Kwani usanifu huu ulitakiwa uishe Desemba, 2022 na ukizingatia Miji hii tayari ipo kwenye exemption ya kodi ili Mkandarasi aweze kwenda site na wananchi wa maeneo haya waweze kupata maji kwa urahisi. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jacqueline, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, usanifu ulipaswa kukamilika Desemba na sasa ni Januari, tuko mwishoni kabisa kukamilisha na lengo letu ni kuhakikisha dhumuni la kupeleka maji maeneo haya aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge tunakwenda kukamilisha kwa wakati.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nishukuru majibu mazuri ya Serikali. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali bado tuna changamoto nyingi hasa kwenye upande wa magari katika taasisi hii ili waweze kufanya kazi zao vizuri na kurahishisha kazi zao;

Je, Serikali ina mpango gani kuhusiana na masuala mazima ya magari ya usafiri kwa Taasisi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili;

Je, Seriikali ina mpango gani wa kuongeza watumishi katika Taasisi hii, ambao bado maeneo mengi tuna changamoto kubwa ya watumishi kwenye taasisi hii, ili waweze kufanya kazi vizuri na tukiangalia Taasisi hii ina - deal na masuala ya rushwa na bado tuna changamoto nyingi sana katika nchi hii kuhusu suala la rushwa?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto ya usafiri, hili linachukuliwa umuhimu wa pekee, na hata kwenye bajeti ijayo tunaomba nafasi ya kuongeza vyombo vya usafiri, ili kuwasaidia maafisa wetu wa TAKUKURU kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile suala la kuongeza watumishi tunaendelea nalo ni zoezi endelevu. Kwa ushahidi Waheshimiwa Wabunge wote mnajua hata mwaka huu TAKUKURU ilipata nafasi na mpaka sasa kwenye kipindi hiki, bado wanaendelea na mchakato. Tangazo lao la mwisho lina kama wiki mbili hivi bado wanaendelea kufanya mchakato wa kupata watumishi zaidi. Kwa hiyo hili zoezi la kuongeza watumishi ni zoezi endelevu kulinganna na upatikanaji wa fedha na namna Serikali itakavyopata nafasi ya kuongeza nafasi zaidi.
MHE. JACQUELINE K. ANDREW: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili. Swali langu la kwanza; katika mikoa yetu ambayo ina hifadhi changa, Wakuu wetu wa Mikoa wamejitahidi kujitokeza

kuhakikisha wanatangaza utalii katika hifadhi hizi changa. Je, Serikali ina mpango gani katika kuhakikisha inasaidia viongozi hawa wa mikoa ili kuweza kukuza utalii katika hizi hifadhi changa na tukizingatia bado miundombinu ni mibovu, magari pia hayatoshi, wanapata wakati mgumu hasa wanapokuwa wanafanya kazi za kutangaza hifadhi hizi kujikuta sasa inabidi waazime magari kutoka sehemu zingine, tunaonaje kama Serikali tuweze kusaidia kutangaza sekta hii ya Maliasili na Utalii?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; bado tunachangamoto nyingi kwenye upande wa ajira. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha ajira zinapatikana na kukuza sekta hii ya utalii hasa katika hifadhi hizi changa, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jacquiline Kainja, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali kwa sasa imejikita katika maeneo mapya ya utalii zikiwemo hifadhi hizi ambazo imezitaja na malengo makuu ni kuhakikisha kwamba tunapanua wigo wa namna ambavyo watalii wataweza kufika katika maeneo hayo. Mikoa yote ya Tanzania tumeendelea kuwahimiza waendelee kuhamasisha utalii ikiwemo utalii wa ndani lakini pia tumejikita kuboresha miundombinu zikiwemo barabara, maeneo ya malazi na chakula ili sasa iwe rahisi kwa watalii kuweza kufika katika maeneo hayo. Kwa hiyo tunaendelea kuwahimiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya waendelee kuhamasisha masuala mazima ya utalii.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ameongelea kuhusu ajira. Tumeendelea kuwasiliana na Ofisi ya Rais, Menejimenti Utumishi na Utawala Bora kuangalia namna ya kuongeza watumishi ambao tutawasambaza katika maeneo mapya yaliyoko katika hifadhi hizo.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuulizwa maswali mawili ya nyongeza.

Swali langu la kwanza, je, ni kiasi gani GST imewezeshwa kufanya kazi?

Swali langu la pili, je, Serikali ina mpango gani mahsusi kuhakikisha Watanzania wananufaika na madini haya yanayopatikana nchini Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jacqueline Kainja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la kwanza GST katika bajeti hii ambayo ilipitishwa na Wizara ya Madini imetengewa kiasi cha fedha shilingi bilioni mbili na milioni mia nne kwa ajili ya shughuli zake mbalimbali ikiwemo kipande kidogo kwa ajili ya utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli hizi za utafiti zinahitaji fedha nyingi sana kwa hiyo shilingi bilioni 2.4 peke yake haitoshi, wenzetu wa GST tayari wameshaanza kufanya proposal za kupata fedha kutoka maeneo mengine ili kuweza ku-complement kwenye zile fedha ndogo ambazo wanazo kwa ajili ya kukamilisha hii kazi ambayo wamepatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili ni mkakati wa Serikali ambao unafahamika wazi kwamba madini yanayochimbwa Tanzania yanawanufaisha Watanzania wote, uniruhusu nitoe mfano mmoja kwa juzi Barrick imetoa CSR kiasi cha shilingi bilioni 30 ambayo kwa kuanzia imetoa Shilingi Bilioni 10, hata sisi ambao hatuko katika yale maeneo ya mgodi tumepata fedha hiyo. Kwa hiyo, Watanzania wote Serikali imeweka mpango wa kuhakikisha kwamba kila mmoja anayetakiwa kunufaika nayo ananufaika kwenye eneo lake.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, ni pikipiki 85 zilizotoka kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii zimetoka kwa Mikoa 21 na Mkoa wangu wa Tabora zimetoka pikipiki nne. Pikipiki mbili zimeenda Wilaya ya Urambo kwa Kata ya Kazaroho na Uyumbu na zingine zimeenda Kaliua. Sasa Serikali ina mpango gani kuhakikisha inatenga pikipiki nyingi za kutosha kwa ajili ya kuwezesha Afisa Maendeleo, kwa ajili ya kazi hizi za kufatilia mikopo?

Swali la pili, Kanuni ya utoaji mikopo Februari 2021 iliwaagiza Wakurugenzi kutenga pesa 500,000 hadi milioni 5,000, 000 kwa ajili ya ufuatiliaji wa mikopo lakini siyo kila Halmashauri ina uwezo wa kuwa na pesa za kutosha. Swali langu kwa Serikali, haioni kama na Serikali yenyewe ni chanzo cha mikopo hii chefuchefu ambayo tunashindwa kukusanya na kufuatilia vikundi hai na ambavyo siyo hai.

Je, ina mpango gani kuhakikisha sekta hii ya Maafisa Maendeleo ya Jamii wanapata vitendea kazi vya kutosha? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Jacqueline Kainja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la kwanza la utengaji wa pikipiki hizi nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utengaji au upatikanaji wa pikipiki hizi kigezo cha kwanza ni upatikanaji wa bajeti. Kwa hiyo, kama Serikali tutaendelea kutenga bajeti ili tuweze kuwafikia wananchi wote ikiwezekana Kata zote au Wilaya zote za Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili kwamba Halmashauri nyingine hazina uwezo wa kutenga pesa kwa ajili ya kupeleka Maafisa wetu kwenda kuangalia au kufuatilia vikundi hivyo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa haya pia ni maelekezo ya Serikali kwamba Wakurugenzi wote katika Halmashauri zote wahakikishe kwamba wanaendelea kutenga fedha kama ambavyo imeelekezwa na wale ambao watashindwa maelekezo yetu ni kwamba wawasiliane na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kuona ni jinsi gani tunatatua tatizo hilo. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa majibu mazuri ya Wizara, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuweka motisha kwa Walimu walioko vijijini, ili tuweze kupata Walimu wengi waweze kwenda kuajiriwa vijijini ili tuweze kuondokana na upungufu maeneo ya vijijini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Serikali haioni kuna haja ya ajira hizi zinazotoka nyingi zielekezwe vijijini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza aliyouliza Mheshimiwa Kainja. La kwanza hili la motisha kwa Walimu vijijini, tayari Serikali inalifanya hili kwa kupitia Wakurugenzi wa Halmashauri husika, kuna Halmashauri ambazo Walimu wanaporipoti kazini wamekuwa wakipatiwa magodoro na vifaa vingine vya kuweza kuwapa motisha kubaki katika maeneo yao ya kazi. Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kule imekuwa ikifanya hivyo na maeneo mengine nchini na tutaendelea kuona ni namna gani tunatoa motisha kwa Walimu hawa wanaoenda vijijini kadri ya upatikanaji wa fedha na uwezo wa Serikali na bajeti kuruhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, la haja ya ajira hizi hawa Walimu kwenda vijijini. Walimu hawa wanaajiriwa kutokana na upungufu uliopo kwenye maeneo husika hasa maeneo haya ya vijijini. Sasa naomba nitoe rai hapa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ambao ndio waajiri wa Walimu hawa na wale wa Mkoani Tabora kule anakotoka Mheshimiwa Kainja vile vile, kuhakikisha kwamba hawa wanaopangiwa maeneo haya kwenda kufundisha wanabaki kule kwenye maeneo yale kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma. Kwa sababu Serikali ilifanya review ya maeneo yote yenye upungufu wa Walimu na ndiyo maana hawa wanaajiriwa kwenda kuziba mapengo yale yaliyokuwepo kwenye maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kila mmoja akiomba kuhama, ina maana mapengo yale yanazidi kuwepo. Vile vile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote Serikali itaendelea kuajiri Walimu hawa kwa ajili ya kuziba mapengo haya na upungufu uliopo kadri ya bajeti itakavyoruhusu.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza; kwa nini Serikali inapotenga pesa za majengo ya zahanati na vituo vya afya isitenge sambamba na pesa za vifaa? Kwa sababu mara nyingi majengo yanafunguliwa wakati vifaa hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; nini tamko la Serikali kwa majibu mazuri yaliyojibiwa hapa kwamba kuna pesa zimetengwa kwa ajili ya vifaa, tamko la Serikali katika Mkoa wetu wa Tabora kwa zahanati ambazo hazina vifaa na tayari wananchi wanachangishwa pesa za mabenchi kama Zahanati ya Goweko, Kalangale, Wilaya ya Uyui lakini vilevile Wilaya ya Igunga, Kagongo, Kata ya Itunduru na Ibuta - Kata ya Mbutu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, la kwanza, kwa nini Serikali isitenge fedha ya vifaa tiba kwanza; kimekuwa ni kipaumbele cha Serikali kujenga miundombinu kwanza ili huduma zile za msingi ziweze kuanza kutolewa na baada ya kuwa majengo yale yamekamilika na huduma za msingi kuanza kutolewa, ndipo Serikali inatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na kuvipeleka kwenye zahanati hizo.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilisema kwenye majibu yangu ya msingi, katika mwaka huu wa fedha ambao tunaumaliza, Serikali ilitenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba ambapo tayari bilioni 12.90 imeshanunua vifaa tiba hivyo na vimeanza kusambazwa katika zahanati zote nchini.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili; tamko la Serikali kwa zahanati kupata vifaa tiba katika Mkoa wa Tabora anaotoka Mheshimiwa Mbunge, Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika kuhakikisha vifaa tiba vinakuwa katika zahanati zote, vituo vyote vya afya vilevile katika hospitali za wilaya kote nchini katika kuhakikisha afya za Watanzania zinaboreka.

Mheshimiwa Spika, na kwa ajili ya kutekeleza hilo, Serikali imetenga shilingi bilioni 112 kwenye mwaka wa fedha 2023/2024 na vifaa tiba hivyo vitaanza kununulia mara moja mwaka wa fedha unapoanza, na tutaanza kuvisambaza katika maeneo yote nchini ya zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya, yakiwemo maeneo yale ambayo ameyataja Mheshimiwa Jaqueline Kainja.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi. Kwa kuwa Mkoa wetu wa Tabora una maeneo mengi ya kutosha na wafugaji ni wengi; nini mpango wa Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye viwanda vya maziwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kweli kama nilivyosema Tabora pia ni eneo ambalo kuna wafugaji wengi na ng’ombe wengi, kama nilivyosema hamasa kubwa ni kuona tunaendelea kuhamasisha uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani pia hata wa nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwaomba watanzania wenzangu hata Wabunge wenzangu kuendelea na kushiriki, kutumia fursa hizi zilizopo katika maeneo yetu. Bahati nzuri, Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kodi nyingi kwenye maeneo haya kwenye viwanda vya maziwa, kwenye storage facilities. Kwa hiyo, tutumie fursa hii kuwekeza huko ili tuweze kukwamua au kuwasaidia wafugaji ambao wanakosa soko la kuuza maziwa yao ambayo naamini tukizalisha bidhaa zinazotokana na maziwa tutapata fursa kubwa ya kuuza ndani ya nchi pia nje ya nchi kwa sababu tayari bidhaa hii inahitajika sana, nakushukuru sana.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi. Kwa kuwa Mkoa wetu wa Tabora una maeneo mengi ya kutosha na wafugaji ni wengi; nini mpango wa Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye viwanda vya maziwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kweli kama nilivyosema Tabora pia ni eneo ambalo kuna wafugaji wengi na ng’ombe wengi, kama nilivyosema hamasa kubwa ni kuona tunaendelea kuhamasisha uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani pia hata wa nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwaomba watanzania wenzangu hata Wabunge wenzangu kuendelea na kushiriki, kutumia fursa hizi zilizopo katika maeneo yetu. Bahati nzuri, Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kodi nyingi kwenye maeneo haya kwenye viwanda vya maziwa, kwenye storage facilities. Kwa hiyo, tutumie fursa hii kuwekeza huko ili tuweze kukwamua au kuwasaidia wafugaji ambao wanakosa soko la kuuza maziwa yao ambayo naamini tukizalisha bidhaa zinazotokana na maziwa tutapata fursa kubwa ya kuuza ndani ya nchi pia nje ya nchi kwa sababu tayari bidhaa hii inahitajika sana, nakushukuru sana.