Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge (15 total)

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE Aliuliza:-

Miradi mikubwa ya ujenzi nchini inafanywa na kampuni kutoka Bara la Asia wakati wahandisi nchini wanasoma uhandisi kwa mitaala ya Uingereza na Marekani.

(a) Je, Serikali haioni haja ya kuongeza mitaala ya Asia katika mitaala ya Vyuo vya Uhandisi ili Wahandisi wetu wapate utaalam katika miradi ya ujenzi?

(b) Je, suala la kubadilishana weledi limepewa kipaumbele gani katika miradi inayoendelea kujengwa hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Uhandisi ni fani ya Kimataifa ambayo mitaala yake haitofautiani kijiografia. Kwa muktadha huo mitaala ya shahada za uhandisi katika vyuo vyetu nchini nayo ni ya viwango vya kimataifa. Hata hivyo, ni kawaida kuhuisha mitaala mara kwa mara ili kuingiza utaalam mpya kwenye fani. Hivyo basi ni nia ya Serikali yetu kuhuisha (review and update) ya mitaala ya kihandisi na fani nyingine za kipaumbele kwenye Tanzania ya viwanda kama tunavyoongozwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025, Ibara ya 80 Ukurasa 130 Kipengele (c) ambayo inaagiza “kuhuisha Mitaala (curriculum review) na kuanzisha programu kulingana na mahitaji ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili wahitimu wawe na stadi stahiki za kumudu kufanya kazi mbalimbali za kuajiriwa na kujiajiri na hasa kwa kuzingatia Mapinduzi ya Nne ya Viwanda”.

(b) Mheshimiwa Spika, suala la kubadilishana uweledi wa kihandisi kati ya miradi mikubwa inayoendelea tayari linatekelezwa ambapo wahitimu wetu wa uhandisi hupata nafasi za utarajali katika miradi yetu mikubwa ya Kitaifa ili kupata weledi. Kwa mfano, kupitia Bodi ya Usajili wa Wahandisi (Engineers Registration Board) wapo wahandisi wahitimu 197 ambao wanashiriki kwa sasa katika miradi mikubwa mbalimbali mfano Mradi Umeme wa Mwalimu Nyerere na Mradi wa Reli ya Mwendo Kasi. Hivyo, Serikali itaendelea kuweka mfumo wa kuhakikisha kuwa katika miradi mikubwa inayotekelezwa nchini suala la kubadilishana uweledi linaendelea kupewa kipaumbele. Ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza:-

Mwaka 2018 KFW Germany walisitisha udhamini kwa huduma za Afya kwa Mama na Mtoto Mkoani Tanga: -

(a) Je, ni juhudi gani zimefanyika kuhakikisha Mdhamini huyo anaendelea na udhamini wake Mkoani Tanga?

(b) Je, Serikali ina mpango gani kupata Mdhamini mwingine?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya KFW ilianzisha mpango wa Bima ya Afya kwa akinamama wajawazito na watoto. Mpango huo ulitekelezwa kwa makubaliano ya kipindi maalum toka 2012 hadi 2018. Mpango huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa wa dhana na umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya katika jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali inakamilisha Rasimu ya Muswada wa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambao utawasilishwa Bungeni mwezi Juni 2021, swali la Mheshimiwa Mbunge lenye kipengele (a) na (b) litaenda kupata suluhisho. Hata hivyo, Serikali inaendelea kuwahamasisha wadau mbalimbali katika kuchangia miradi ya Sekta ya Afya, ikiwemo Bima ya Afya kwa Wote.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO K.n.y. MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza:-

Je, ni kwa namna gani Serikali imetumia fursa ya makubaliano ya TICAD kati ya Tanzania na Japan ili kupata wawekezaji nchini?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD) ni chombo kilichoanzishwa na nchi ya Japan mwaka 1993 kwa lengo la kukuza mahusiano, maendeleo na kuondoa umaskini Afrika. Vipaumbele vya TICAD vinaenda sambamba na agenda ya 2063 ya Umoja wa Afrika na agenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Mheshimiwa Spika, kupitia TICAD Serikali ya Tanzania imeweza kuandaa mfumo wa blueprint unaoboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini na hivyo kupelekea kukuza sekta za uzalishaji, ujenzi wa miundombinu na huduma ikiwemo nishati na kujenga uwezo wa wajasiriamali. Sekta hizo huandaa miradi mbalimbali na kuiwasilisha TICAD, ili kupata ufadhili wa kifedha chini ya uratibu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Spika, miradi ya kiuwekezaji ambayo imetekelezwa nchini kutokana na TICAD ni pamoja na maboresho ya Bandari ya Kigoma, uendelezaji wa huduma za usambazaji wa maji Zanzibar, ujenzi wa kituo cha uzalishaji na usambazaji wa umeme kwa kutumia nishati ya gesi mkoani Mtwara, maboresho ya barabara jijini Dodoma na utoaji wa mikopo nafuu kwa wajasiriamali.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kukuza mahusiano mazuri ya kibiashara baina ya Tanzania na Japan ili kuendelea kunufaika na TICAD katika kuvutia wawekezaji zaidi wa ndani na nje ya nchi.
MHE. CECILIA PARESSO K.n.y. MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -

Je, ni lini ahadi ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege Tanga aliyoitoa Mheshimiwa Rais wakati wa uzinduzi wa Bomba la Mafuta pale Chongoleni Mkoani Tanga itaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’azi Ulenge, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kiwanja cha Ndege cha Tanga ni miongoni mwa viwanja 11 vya ndege vinavyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Transport Sector Support Project.

Mheshimwa Spika, Benki ya Dunia imeonesha nia ya kufadhili upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Tanga kupitia programu iitwayo Development Corridor Transport Programme.

Mheshimwa Spika, kwa sasa majadiliano kati ya Serikali na Benki ya Dunia kuhusu malipo ya fidia kwa wananchi watakaopisha utekelezaji wa mradi wa upanuzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Tanga, mapitio ya awali ya ripoti ya mradi huu pamoja na maandalizi ya taarifa mbalimbali zinazohitajika kabla ya mkataba wa mkopo kusainiwa yanaendelea.

Mheshimwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’azi Ulenge kuwa Serikali ina nia ya dhati ya kufanya upanuzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Tanga. Aidha, majadiliano kati ya Serikali na Benki ya Dunia yatakapokamilika utekelezaji wa mradi huu utaanza mara moja. Ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaruhusu usafirishaji wa Viumbe Hai nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge wa Viti Malum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tarehe 17 Machi, 2016 Serikali ilisitisha biashara ya kusafirisha wanyamapori hai nje ya nchi. Tatizo kubwa lililosababisha maamuzi hayo lilikuwa ni matokeo hasi yaliyokuwa yakiendelea kujitokeza kutokana na kufanya biashara hiyo ikiwemo kuhamisha rasilimali ya wanyamapori nje ya nchi. Aidha, Serikali ilirejesha jumla ya shilingi 173.2 ya ada na tozo zilizolipwa awali na wafanyabiashara kabla ya kusitishwa kwa biashara hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya tathmini ya kina kuhusu biashara ya usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi. Kufuatia tathmini hiyo, zuio la biashara litaondolewa ambapo biashara hiyo itafanyika kwa utaratibu ufuatao: -

(i) Wanyamapori hai wataruhusiwa kusafirishwa kwa shughuli za utafiti na kidiplomasia tu.

(ii) Wanyamapori watakaosafirishwa nje ya nchi watakuwa ni wale waliokaushwa au mazao yatokanayo na wanyamapori hao.

(iii) Biashara ya wanyamapori waliokaushwa pamoja na mazao yake itafanywa na wafanyabiashara wenye miradi ya ufugaji wanyamapori ili kuhamasisha uanzishwaji wa miradi ya ufugaji wa wanyamapori.

(iv) Serikali itatoa muda wa miezi mitatu ili kuruhusu wafanyabiashara kusafirisha wanyamapori waliosalia kwenye mazizi na mashamba kabla ya zuio ambao walikuwa wanafugwa kwa lengo la kuwasafirisha nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -

Je, nini kauli ya Serikali kutokana na mkanganyiko uliotokea kuhusu fidia katika barabara ya Tanga – Pangani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Tanga – Pangani yenye urefu wa kilomita 50 ni sehemu ya barabara ya Bagamoyo kuanzia Makurunge – Saadani – Pangani hadi Tanga ambayo ina urefu wa kilomita 256. Awali Benki ya Maendeleo ya Afrika ilionesha nia ya kufadhili barabara yote ya Bagamoyo kuanzia Makurunge – Saadani – Pangani hadi Tanga urefu wa kilomita 256.

Mheshimiwa Spika, aidha, mfadhili alitoa sharti la kulipia fidia kwa mali zote zitakazoathiriwa na mradi ndani na nje ya eneo la hifadhi ya barabara. Hivyo, uthamini wa mali zitakazoathiriwa na mradi ulifanyika kwa kuzingatia sharti hilo. Wananchi walifahamishwa kwenye mikutano ya uelimishaji umma na kujulishwa kuwa endapo mfadhili hataendelea na nia hiyo na Serikali ikajenga kwa fedha za ndani, wale wenye mali zilizopo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara hawatalipwa fidia.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hiyo, na kwa kutochelewesha mradi, Serikali ilianza ujenzi kwa sehemu ya Tanga, hadi Pangani urefu wa kilomita 50 kwa kutumia fedha za ndani.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka, 2017 ujenzi wa aina yoyote hauruhusiwi ndani ya eneo la hifadhi ya barabara. Hivyo, wananchi waliofanya maendelezo ndani ya eneo hilo hawastahili kulipwa fidia.

Mheshimiwa Spika, kwa kufuata matakwa ya sheria za nchi wale wote ambao walikuwa ndani ya eneo la hifadhi ya barabara, hawakustahili kulipwa fidia na waliondolewa kwenye orodha ya malipo kabla ya taarifa ya fidia kuwasilishwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali. Ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -

Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhusu mpango wa kukuza uchumi wa buluu kwa kuzingatia mazao yatokanayo na bahari?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kukuza uchumi wa buluu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya uratibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais na kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo, mashirika ya kijamii, na sekta binafsi tunaandaa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Buluu. Mazao ambayo yamepewa kipaumbele kwenye mkakati huo kwa upande wa baharini ni samaki aina ya dagaa, pweza, kambamiti, vibua, jodari, changudoa, zao la mwani, unenepeshaji wa kaa na ukuzaji wa lulu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 11.51 ambazo zitatumika kununua boti za kisasa zenye engine, kifaa cha kutafutia samaki (GPS) na kasha la ubaridi lenye uwezo wa kubeba tani 1.5 kwa ajili ya kuwakopesha wavuvi. Pia jumla ya shilingi bilioni 20 zimetengwa ambapo kiasi cha shilingi bilioni 3.32 zitatumika kuwezesha pembejeo kwa ajili ya wakulima wa mwani katika ukanda wa bahari ya Hindi. Ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -

Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuunganisha barabara za Mkoa wa Tanga na mikoa jirani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Mwanaisha Ng’azi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Serikali ni kuiunganisha mikoa yote kwa barabara za lami. Mkoa wa Tanga unapakana na Mikoa ya Pwani, Morogoro, Manyara, Kilimanjaro na nchi jirani ya Kenya. Tanga imeunganishwa na barabara zifuatazo: Tanga – Chalinze (Mkoa wa Pwani), Handeni – Tuliani hadi Magole (upande wa Mkoa wa Morogoro), Handeni - Kibilashi – Kibaya, (Mkoa wa Manyara), Tanga – Korogwe hadi Same (Mkoa wa Kilimanjaro) na kwa upande wa Kenya ni Tanga - Horohoro.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, zipo barabara nyingine ambazo zinaunganisha Mkoa wa Tanga na mikoa ya jirani. Ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaboresha kadi ya kliniki ya Watoto chini ya miaka mitano ili kusaidia ufuatiliaji wa wingi wa damu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’azi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadi za kiliniki ya watoto ziliboreshwa tangu mwaka 2011 kwa kuzingatia miongozo ya Shirika la Afya Duniani, ambapo maboresho hayo yamezingatia maeneo yasioacha maeneo hatarishi yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo unaelekeza kutumia mbinu za kitabibu kutambua wingi wa damu kwa mtoto bila kumtoboa na wale wenye dalili za upungufu hupelekwa kwenye vipimo zaidi, ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -

Je, lini Serikali itawahamisha wataalam wa maendeleo ya jamii kuwa chini ya Wizara?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inatekeleza Tamko la Sera ya Ugatuaji wa Madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwa wananchi kwa kushusha madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kusogeza huduma na utalaam karibu na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kufuatia kuundwa kwa Wizara hii ya Maendeleleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ambapo kada za msingi za kitaalam ni Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii, Serikali inaendelea na hatua za kuimarisha mifumo ya uratibu ngazi ya Sekratarieti ya Mikoa na Halmashauri ili kujibu mahitaji ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara hii mpya.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaweka wazi vigezo vya kubaini kaya maskini zinazostahili kupokea msaada wa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kumjibu Mheshimiwa Injinia Mwanaisha Ng’azi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalam, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, vigezo vya utambuzi wa kaya za walengwa viko wazi na vinatambulika. Vigezo hivyo ni kama ifuatavyo ili kuweka record sawa katika Bunge lako:-

(i) Kaya ambazo hazina uwezo wa kupata kwa uhakika angalau milo miwili kwa siku;

(ii) Kaya isiyo na kipato cha uhakika na inayo wategemezi wengi wakiwemo watoto wanaokosa huduma za elimu na afya;

(iii) Kaya zinazoishi kwenye makazi duni yanayohatarisha usalama wa kaya;

(iv) Wazee wasio na msaada wowote;

(v) Watoto wanaoishi wenyewe bila wazazi au walezi.

Mheshimiwa Spika, vigezo hivi ndivyo vimewezesha Serikali kuweza kuhudumia kaya za walengwa 1,378,000 ambao wanaendelea kunufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF).
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza:-

Je lini Serikali itajenga barabara ya mchepuko kutoka barabara ya Tanga - Horohoro - Chongoleani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii inachepuka kutoka barabara ya Tanga - Horohoro kuelekea eneo ambalo kutajengwa bohari kubwa (depot) ya kupokelea mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mradi huu wa bomba la mafuta na ujenzi wa bohari kwa ajili ya upokeaji wa mafuta unaofanywa na Kampuni ya EACOP ambao ndiyo wasimamizi wa mradi huu, waliomba kibali cha kuimarisha barabara ya Chongoleani kwa viwango ambavyo vitaweza kuhimili uzito wa magari na mitambo itakayokuwa inapitishwa katika barabara hii kwa kipindi chote cha ujenzi wa mradi hadi utakapokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo kutokana na hali hiyo kwa sasa barabara hii inahudumiwa na EACOP kupitia Mkandarasi walieingia naye mkataba kwa kipindi chote cha mradi.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -

Je, ni lini Mamlaka ya Viwanja vya Ndege itaruhusiwa kukusanya na kutumia passenger service charge kuboresha viwanja vya ndege ?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) imewekewa utaratibu wa kukusanya moja kwa moja ada za kutua na maegesho ya ndege; ada ya usalama (security fee); tozo za ukodishaji wa ofisi, karakana, majengo ya kuhifadhia mizigo, migahawa na maduka; tozo za maegesho ya magari, na tozo za mabango. Aidha, Sheria ya Huduma za Viwanja vya Ndege (The Airport Service Charge Act) Sura ya 365 inaipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jukumu la kukusanya tozo kwa abiria wanaosafiri kupitia viwanja vya ndege (passenger service charge) na kuwasilisha Hazina.

Mheshimiwa Spika, fedha zinazokusanywa na TRA kutoka kwa abiria na kuwasilishwa Hazina zinatumika kuendeleza miundombinu ya viwanja vya ndege nchini pamoja na kulipa mishahara ya watumishi, matumizi ya uendeshaji wa TAA na kufanya matengenezo ya viwanja. Aidha, Serikali hutoa fedha kila mwaka kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya viwanja vya ndege, ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa bei elekezi ya vifaa vya tiba hasa vya macho, pua na koo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeandaa kanuni za kudhibiti bei za dawa na tayari zimekwishawasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Bei elekezi za vifa tiba zitaandaliwa mara baada ya kukamilika kwa kanuni za bei za dawa elekezi. Ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza:-

Je, nini Mkakati wa Serikali wa kuifanya Bandari ya Tanga iwe na ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu sasa Bandari ya Tanga ilikuwa haihudumii meli na shehena ya kutosha kutokana na changamoto ya kasi ndogo ya huduma za meli na shehena hizo ambazo zilipaswa kuhudumiwa nangani umbali wa kilomita 1.7 kutoka gatini. Hali hii ilipunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Bandari ya Tanga na ushindani wa bandari hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali kupitia TPA, inaendelea na maboresho ya bandari hiyo katika maeneo ya miundombinu, mitambo na vifaa ili kuvutia meli na shehena nyingi zaidi kama mkakati mahsusi wa kuifanya bandari hiyo ifanye kazi kwa ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo TPA ina mkakati mahsusi wa kimasoko kwa ajili ya Bandari ya Tanga ambao lengo lake ni kuteka soko la kaskazini mwa Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda na DRC. Mikakati hiyo ni pamoja na kuwashawishi wateja wakubwa kutumia bandari hiyo kwa kutoa punguzo la tozo.