Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Edwin Enosy Swalle (20 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba za Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu leo ni mara yangu ya kwanza kuzungumza ndani ya Bunge lako Tukufu, naona basi ni vema nikatumia nafasi hii pia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Joseph Pombe Magufuli na Mwenyekiti wa Chama chetu cha Mapinduzi na Halmashauri Kuu ya Chama chetu cha CCM kwa kuwa na imani kubwa na kupitisha jina langu kuwa Mbunge wa Bunge hili la Kumi na Mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu amekuwa akiacha alama kila mahali. Ameacha alama kwenye nchi lakini pia ameendelea kuacha alama kubwa kwa sisi vijana wa nchi hii kwa kutuamini na kutupa nafasi. Mheshimiwa Rais ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi sana napenda nitumie kama dakika moja pia kuwashukuru sana familia yangu ya Mzee Enosy na kipekee mke wangu mpenzi Tumaini anayelea wanangu wawili kwa ufasaha mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijikite kwenye mchango wa hotuba za Mheshimiwa Rais. Nimesoma hotuba mbili za Mheshimiwa Rais, hotuba hizi zina sura mbili sehemu ya kwanza zinaeleza mafanikio makubwa ya miaka mitano iliyopita, lakini sehemu ya pili inaeleza mipango ya Serikali kwa miaka mitano ijayo. Tunavyompongeza Mheshimiwa Rais kwangu mimi nadhani pia ni muhimu sana kuwapongeza Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wetu na Mawaziri wote waliopita kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa ajili ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sote ni mashahidi, tulishuhudia Waziri Mkuu wetu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Kassim, akizunguka hii nchi nzima kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Mimi ni kati ya Wabunge ambao niliomba sana Mungu Mheshimiwa Majaliwa aweze kuendelea kuwa Waziri Mkuu na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mwenyezi Mungu alimuonyesha akampa nafasi Mheshimiwa Waziri Mkuu ya kuendelea na utumishi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini maombi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuendelea kuwa na nafasi ya Waziri Mkuu nilikuwa na sababu maalum. Pamoja na kazi nzuri sana ambayo Serikali imefanya kwa miaka mitano iliyopita na hasa kwenye kipengele cha kilimo, Waziri Mkuu ameshughulika sana kutatua kero za mazao mengi ya kimkakati. Tumemuona Waziri Mkuu akihangaika na zao la korosho katika nchi hii, pamba, mkonge na mazao mengine katika nchi hii. Hata hivyo liko zao moja ambalo katika miaka mitano iliyopita na hiki pengine ni kiporo ambacho naiomba Serikali katika mpango wake wa kuendelea kukuza ajira kwa wananchi wa Tanzania Serikali kupitia Waziri Mkuu awamu hii ya pili ya miaka mitano ya utumishi watazame katika zao la chai ambalo ni zao la kimkakati la Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Lupembe wananchi walisikiliza hotuba ya Mheshimiwa Rais. Ukiangalia kwenye ukurasa 12 wa hotuba ya Mheshimiwa Rais ya mwezi Novemba 2020, Mheshimiwa Rais aliwaahidi Watanzania pamoja na wananchi wa Jimbo langu la Lupembe kwamba anayo ndoto na angetamani sana wananchi wetu waweze kuwa mabilionea. Wananchi wa Jimbo la Lupembe wako tayari kuwa mabilionea na wamejiandaa kuwa mabilionea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mchango wangu wa hotuba hii wamenituma kumuomba Mheshimiwa Rais mambo mawili ya msingi sana. Jambo la kwanza wananchi wa Lupembe wanasema pamoja na uchapa kazi, wanamuomba Mheshimiwa Rais awasaidie ahadi ya barabara ya lami kuanzia Kibena - Lupembe - Madeke - Morogoro. Barabara hii ikifunguka hata wewe Naibu ukitoka pale Mbeya utapita Jimbo la Lupembe kuelekea Dar es Salaam, lakini hata Waziri Mkuu mwenyewe anaweza kupitia barabara hii badala ya kupita barabara ya Iringa ambayo ni ndefu na ina milima mikali sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo hili la zao la chai kuna changamoto kubwa sana katika Jimbo la Lupembe. Wananchi wengi wa Jimbo la Lupembe hawalipwi fedha zao na viongozi wengi wa Serikali wamekuja Lupembe wakipewa ahadi na wawekezaji kwamba wangelipa fedha hizi kwa wakati lakini mpaka leo tunavyozungumza Makamu wa Rais amekuja kapewa ahadi hii, Waziri Mkuu amekuja kapewa ahadi hii, Waziri wa Kilimo amekuja kapewa ahadi hii nilikuwa lakini utekelezaji hakuna.

Kwa mujibu wa Sheria yetu ya Makosa ya Jinai, kifungu cha 122 ni kosa kwa mtu kumweleza taarifa za uongo kiongozi wa umma na kwa kuwa wawekezaji hao wamekuwa wakitoa taarifa siyo za kweli kwa viongozi wetu wa Serikali, naiomba Serikali sasa ingewaita wawekezaji hawa waeleze ni kwa nini wasichukuliwe hatua kwa kuiambia Serikali au viongozi wetu taarifa ambazo hawawezi kutekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili naomba niseme kidogo sana kwenye ajira. Naomba sana watu wa TRA waweke mazingira rafiki kwa vijana wetu, wanapofungua biashara wapewe grace period ya kuanza kulipa kodi angalau mwaka mmoja au miaka miwili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango huo, naunga mkono hoja, ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niwe mchangiaji wa mwisho kwa mchana huu wa leo kwenye bajeti hii ya Serikali.

Kwanza niseme kwamba naunga mkono kauli ya Mheshimiwa Mbunge wa Singida Mashariki, Mheshimiwa Miraji Mtaturu kwamba wapo watu katika nchi hii wanaona taabu mtu akipongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwakumbushe Watanzania, mtu asiyependa kupongeza ni mtu mwenye wivu au ni mtu msahaulifu kwa mema aliyofanyiwa. Kwa hiyo, nimesoma bajeti hii ya Wizara ya Fedha na nimejiuliza swali moja tu: Je, bajeti hii inajibu kero za wananchi wangu wa Lupembe? Nimekuta jibu ni ndiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti hii imebeba matumaini makubwa, imebeba miradi ya umeme kwa wananchi, imebeba miradi ya barabara, imebeba miradi ya maji ya Kichiwa, Maduma na Tagamenda, Nyombo, Matigangila, na kadhalika. Bajeti hii ya Wizara ya Fedha imebeba fedha ya kupeleka mbolea ya ruzuku kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, hii ni bajeti muhimu. Nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kwa ajili ya Taifa letu. Nami kwa niaba ya wananchi wa Lupembe, namwombea Mheshimiwa Rais afya njema na siha njema ya kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Mchemba, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara hii. Kwa mara ya kwanza Watanzania wameshuhudia kwenye majimbo yetu, tunayo miradi mingi mpaka imefika mahali wakandarasi hawapatikani, fedha ziko nyingi sana. Mambo haya yamefanikiwa kwa sababu, Waziri wetu wa Fedha bila shaka amekuwa ni mshauri mzuri sana kwa Mheshimiwa Rais. Nasi tunamuunga mkono, tuendelee kupeleka fedha wananchi wapate maendeleo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kukishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi, na kipekee namshukuru Katibu wetu wa CCM, Comrade Daniel Godfrey Chongolo kwa kusimamia vizuri Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Wabunge tumeshuhudia mahali pengi, Katibu wetu Mkuu na timu yake wanatembea kwenye majimbo yetu wakitoa hamasa kwa wananchi na kutoa wito wa ilani kutekelezwa. Hongereni sana Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chingolo na timu yako yote ya chama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye mchango wa bajeti. Nianze kwenye eneo la changamoto za wafanyabiashara. Nimesoma kwenye Bajeti hii ya Serikali na nipongeze kwamba Serikali imetambua umuhimu wa kukuza sekta binafsi. Kutambua sekta binafsi ni kwa sababu sekta binafsi inalipa kodi kubwa sana Serikalini. Namwomba Mheshimiwa Waziri, Serikali imefanya uamuzi mzuri. Kwanza tulimsikia Mheshimiwa Rais akiwaambia wafanyabiashara wanaoanza biashara mpya kupewa muda angalau wa mwaka mmoja ndipo waanze kulipa kodi. Huu ni uamuzi mzuri sana kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tumemsikia Waziri hapa ndani akisema anataka wafanyabiashara wenye madai ya kodi wasibughudhiwe, wasifungiwe biashara, badala yake waelimishwe jinsi ya kulipa kodi zao. Haya ni maamuzi mazuri, yanaonesha kulea na kukuza sekta binafsi ya wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, kumekuwa na kero kubwa sana kwa wafanyabiashara. Kule kwangu Lupembe na Mkoa wa Njombe kwa ujumla, wafanyabiashara wengi wanasumbuliwa sana magetini na Maofisa wa TRA. Mageti kama ya Migori na Mikumi, kuna usumbufu mkubwa sana kwa wafanyabiashara, mpaka Wabunge tupige simu ndiyo watu waachiwe. Kwa hiyo, imekuwa kama kufanya biashara kwenye nchi hii ni kero, ni usumbufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri kwa uzito kabisa, kwa sababu Wizara ya Jinsia na Watoto wanalo dawati maalum la kushughulikia masuala ya jinsia, nakushauri Mheshimiwa Waziri, anzisha dawati maalum la wafanyabiashara kwenye Wizara hii, ili wafanyabiashara wapate fursa ya kutoa kero zao moja kwa moja kwako Wizarani. Hili jambo likifanyika hivyo, Mheshimiwa Waziri utakuwa karibu sana na wafanyabiashara na kujibu kero zao kwa wakati. Dawati hili ni muhimu, aajiriwe mtu maalum kupokea kero za Watanzania hasa wafanyabiashara. Hii ni kuhusu wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu kilimo. Nimeongea mara nyingi hapa ndani kwamba Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe ni msemaji wa wakulima, ni mkombozi wa wakulima wa Tanzania. Mheshimiwa Bashe anafanya kazi nzuri sana. Mwaka 2022 Mheshimiwa Bashe ametangaza maeneo kadhaa hapa nchini kwamba, mkulima wa Tanzania aachwe kuuza mazao yake anakotaka. Aachwe kama walivyo wafanyabiashara wengine wa soda, sukari, na kadhalika. Nataka nikuhakikishie uamuzi ule wa Serikali wakulima wetu waliupokea vizuri sana. Sasa ushauri wangu ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa siku za karibuni huu mkanganyiko wa wafanyabiashara kutokwenda kununua haya mazao, hizi taarifa kwamba wamezuiwa kununua mazao na kwenda nje, Mheshimiwa Waziri, asubuhi na jana ametoa kauli nzuri sana hapa ndani kwamba, Serikali haijazuia wananchi kuuza mazao popote wanakotaka. Nimhakikishie Mheshimiwa Waziri, kuna jambo moja kubwa sana nyuma ya hili suala, kuna urasimu mkubwa wa kutoa vibali vya wafanyabiashara wa haya mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wanazinguliwa sana huko maofisini. Vibali havipatikani, leseni hazipatikani. Namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa sababu jambo hili limeshakuwa kero, kule kwangu Lupembe, watu wa Ikondo, Ninga, Mtwango, Kichiwa, Igongolo, Ikula, na kadhalika, mahindi yameanza kushuka bei kutoka shilingi 15,000, wameanza kuuza kwa shilingi 5,000. Ni mporomoko mkubwa sana. Namwomba Mheshimiwa Waziri mambo mawili; jambo la kwanza atangaze mamlaka yetu ya kununua nafaka ianze mara moja kununua nafaka kwa wananchi; pili, atoe bei elekezi, wanunue kwa bei gani kwa wakulima? La tatu,…

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, naomba sana Serikali iongeze fedha za kununua haya mahindi kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa ameamua kuwasaidia wakulima wa Tanzania, afuatilie kwa ukaribu upatikanaji wa vibali vya kununua mahindi na mazao kwa wananchi wetu… (Makofi)

MWENYEKITI: Kabla hujamaliza, nafikiri kuna Taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kuhusiana na hoja hiyo.

TAARIFA

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge wa Lupembe na wakulima wa Tanzania. Wakala wa Chakula wa Serikali (National Food Reserve Agency) ameshaanza kununua mahindi, na bei ya chini anayonunulia ni shilingi 600 mpaka shilingi 700 na tumeanza kufungua vituo katika Wilaya zote na Serikali itatoa tangazo. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili. Mfumo wa kutoa vibali vya export kwa watu wote watakaokuwa na Business License, badala ya kutoa leseni manually, tutaanza kutoa leseni za export na kuuza mazao kuanzia tarehe 1 Julai kwenye mtandao ili kuondoa hiyo adha anayoisema kwamba, Wilayani wanasumbuliwa. Kwa hiyo, leseni zote zitatoka online kuanzia tarehe 1 mwezi wa saba. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Swalle unaipokea Taarifa?

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa heshima kubwa sana. Nilisema hapa ndani kwamba, mzigo mzito wa kulima amepewa Mnyamwezi, Mheshimiwa Bashe, hongera sana, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye suala zima la ajira. Hili jambo la ajira limesemwa mara nyingi na watu wengi hapa nchini. Sisi kama chama, tumeahidi ajira milioni nane kwa Watanzania. Kwa takwimu zilizopo, kila mwaka karibu Watanzania milioni moja wanaingia kwenye soko la ajira kutafuta ajira, lakini uwezo wetu wa kuajiri hauzidi 70,000 pengine. Sasa maana yake kundi kubwa halipo kwenye mfumo rasmi wa ajira. Ushauri wangu ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, juzi hapa ndani tumetunga sheria kama Bunge ya kuanzisha Tume ya Mipango kwa ajili ya kushauri mipango mbalimbali ya Serikali. Ninaomba Serikali kupitia tume hii ikaanzishe mpango maalum wa kufufua viwanda vingi ambavyo vimekufa. Sisi kule Njombe kwa mfano, tulikuwa na kiwanda cha maziwa ambacho kingetoa ajira nyingi sana, kimekufa. Tulikuwa na kiwanda cha parachichi (Urivado) kimekufa. Viwanda vya chai vina hali mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipoweka mpango wa kufufua viwanda vilivyokufa, hatuwezi kuongeza ajira. Serikali duniani kote haiwezi kuajiri wananchi wote wakapata ajira rasmi Serikalini. Kwa hiyo, hili ni jambo la kwanza ambalo Tume yetu ya Mipango lazima iliangalie kwa ajili ya kuongeza ajira kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nataka niseme kuhusu barabara yangu ya muhimu sana; barabara ya Kibena – Lupembe mpaka Madeke. Hii barabara imekuwa na ahadi ya muda mrefu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mwaka 2022 Rais wetu amekuja Njombe na Mheshimiwa Waziri alikuwepo. Barabara hii Mheshimiwa Rais ameagiza ianze ujenzi. Nimeambiwa mchakato wa kuandaa tenda umeanza. Nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenye bajeti hii ambayo mimi naiunga mkono, barabara hii ianze kujengwa kwenye bajeti hii ya 2023/2024 ili kusudi mwakani tukija hapa tukupongeze kwa kazi nzuri ambazo unafanya huko Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, naona umeinua mic, natoa rai kwa Waziri wetu wa TAMISEMI pamoja na watu wa fedha, wananchi wetu wanayo maboma mengi ya zahanati, maboma mengi ya madarasa, vituo vya afya, na kadhaliak. Wekeni mpango maalum wa kumaliza maboma haya ili kuwatia moyo wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Mpango huu wa Miaka Mitano wa Serikali. Niende moja kwa moja kwenye Mpango ambao umewasilishwa na Serikali. Kwanza nipongeze sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kuwasilisha Mpango huu kwa niaba ya Waziri wa Fedha, ameuwasilisha vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Mpango huu mzima Mpango wetu ni mzuri sana na umeweka vipaumbele vyote vizuri. Na ukisoma kwenye ukurasa wa 88 wa mapendekezo ya Mpango huu wa Miaka Mitano, Serikali imetamka wazi kwamba sekta ya kilimo itaendelea kuwa kitovu cha ukuzaji wa viwanda na maisha ya watu. Huu ni ukweli ambao Wabunge wote humu ndani tunaujua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mchango ufuatao kuhusu sekta ya kilimo; wakati fulani ukitazama takwimu za Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Nchi yetu, utakuta kwamba kwenye kilimo zilipelekwa fedha bilioni 188 tu. Sasa kama kilimo ndio kitovu cha kukuza viwanda, unaweza kuona ule msemo ambao alikuwa anasema Rais wetu wa Nne, kwamba zilongwa mbali, zitendwa mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? Ukitazama kwenye sekta ya kilimo, iko mipango mizuri imewekwa hapa kwamba Serikali itaboresha suala la utafiti mbegu bora, Maafisa Ugani na kadhalika. Naishauri Serikali kwa sababu maeneo mengi ya kilimo ambapo mazao ya kimkakati kama kahawa, chai, korosho, pamba na mazao mengine, haya maeneo hatuwezi kuweka kipaumbele cha kupeleka mbegu bora na wataalam na utafiti wakati miundombinu yake haiwezeshi kilimo kile kuwa na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali kwenye maeneo ambayo kuna mazao ya kimkakati, Mpango huu ubainishe kwamba yatapewa kipaumbele cha miundombinu kama ya barabara, miundombinu ya umeme, miundombinu ya afya, ili kusudi kama unasema Jimbo la Lupembe kwa mfano lina zao la mkakati ambalo ni chai na eneo hili linalo viwanda, lakini wakati huo huo kwenye eneo hilo barabara hazipitiki, umeme hakuna, maji hakuna, Mpango huu hauwezi kufanikiwa. Ushauri wangu ulikuwa ni huo kwamba Mpango huu uendane na maeneo ya vipaumbele ili kusudi uakisi uhalisia wa mpango wenye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ambayo napenda kuchangia kwa ufupi, lipo jambo limesemwa na Wabunge wengi humu ndani, Wabunge wengi tumetoa maoni kwamba Serikali haina fedha na Wabunge wamependekeza njia mbalimbali za kupata fedha. Nataka niseme eneo lingine ambalo wengi hatujalisema shida yetu kwenye utekelezaji wa hii Mipango ya Serikali kwa maoni yangu siyo fedha tu, lipo tatizo lingine la kutofanya maamuzi kwa wakati kwa watu wenye mamlaka ya kufanya maamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwa mfano, yuko Mbunge mwenzangu wa Njombe Mjini amezungumza hapa, kwa mfano yupo mwekezaji wa zao la chai ambaye yeye anashindwa kuendesha kiwanda kwa sababu tu watu wa Hazina wanashindwa kufanya maamuzi wa jinsi yeye aweze kusamehewa kodi na kuendesha biashara yake ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo pia mengine, mfano eneo kama la Kilolo, kuna mashamba ya chai yametelekezwa ni mapori, kwa sababu tu maamuzi hayajafanyika ni nani akawekeze maeneo haya. Kwa hiyo, naomba sana watu wa Serikali wafanye maamuzi, decision making ni kipaumbele muhimu sana kwa utekelezaji wa Mpango huu wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, natoa ushauri kwa Serikali kuwa itoe ajira za kudumu kwa Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba Wilaya. Msingi wa hoja hii ni kuongeza uhuru wa Mabaraza haya, (independence of the tribunals).

Mheshimiwa Naibu Spika, ni maoni yangu kuwa kitendo cha kuajiri Wenyeviti hawa kwa mikataba ya miaka mitatu, mitatu ni kumweka Mwenyekiti katika hali ya kukosa uhakika wa ajira. Kwa mfano, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wamepewa security of tenure ili kulinda uhuru wa Mahakama. Maisha ni ardhi, ardhi ni mali. Hatuwezi kulinda mali muhimu ya wananchi ambayo ni ardhi inayosimamiwa na kuamuliwa na mtu ambaye hana uhuru, freedom ya ajira yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufikia lengo la kutoa hamasa na elimu kwa Watanzania kulipa kodi, natoa ushauri kuwa Wizara ibuni mfumo wa mabalozi wa kulipa kodi bila shuruti.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kuwa umma ukipata hamasa ya kulipa kodi itakuwa rahisi watu wengi kuona fahari kulipa kodi. Tunataka watu wapate hamasa ya kudai na kutoa risiti. Hii iwe ni kampeni ya nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi najitolea kuwa balozi wa kwanza. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Wizara ya TAMISEMI, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri wake Mheshimiwa Silinde na Mheshimiwa Dkt. Dugange kwa kazi nzuri ambayo wanafanya. Pia kwa upekee kabisa, nimpongeze sana Katibu Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI Profesa Silas Shemdoe. Amekuwa na ushirikiano mzuri sana na Wabunge kwa kadri ambavyo tunakwenda kumuona na hata ukimpigia simu usiku anapokea na kujibu changamoto mbalimbali. Nampongeza sana Profesa Shemdoe. Na nimhakikishie wananchi wa Jimbo la Lupembe tuko na yeye, tunamuunga mkono sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaongea masuala machache, Halmashauri ya Njombe DC kwenye Jimbo la Lupembe sisi kama jimbo tunazo changamoto nyingi sana hasa katika eneo zima la kutengewa bajeti ya Serikali Kuu. Kwenye bajeti ya mwaka 2020/2021 Halmashauri ya Njombe DC imepokea fedha kwa kiwango cha asilimia sita tu. Maana yake nini? Zaidi ya asilimia 90 halmashauri hii inajiendesha kwa mapato ya ndani.

Mheshimiwa Spika, ombi la wananchi wa Lupembe pamoja na kwamba Serikali yetu ina majukumu mengi inafanya na inafanya kazi nzuri ya kuhudumia Watanzania mahali pengine, tunajua sungura ni mdogo lakini pia wananchi wa Lupembe wanaiomba Serikali katika bajeti hii mpya ya mwaka 2021/2022 wananchi wa Lupembe waangaliwe kwa jicho la pekee sana hasa katika fedha za Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tuliomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya utawala. Jimbo la Lupembe kwa maana ya Halmashauri ya Njombe DC tumehamia kwenye halmashauri yetu kutoka Njombe Mji. Watumishi wa Halmashauri wanakaa kwenye majengo ya shule ya msingi, hakuna vyoo, hakuna sehemu ya kula na hawana majengo ya utawala. Tunaiomba sana Serikali itoe kipaumbele kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa makao Makuu ya halmashauri.

Mheshimiwa Spika, liko jambo lingine upande wa TARURA, tunaiomba sana Serikali waongeze bajeti zaidi kwenye Mfuko wa TARURA. Jimbo langu la Lupembe kwenye maeneo mengi kuna barabara za vijijini halina barabara ya lami hata kilometa moja. Wananchi wa maeneo ya Kata za Kichiwa, Igongolo na Sovi pale Mtwango barabara ni mbaya sana hazipitiki. Ziko barabara kama ya Igongolo – Ninga na barabara ya Nyombo - Ninga – Lima – Itovo - Ikondo wakati wa mvua hazipitiki, wananchi hawana zahanati wanapata shida sana. Naiomba Serikali kwenye bajeti hii watazame kwa jicho la huruma kwa ajili ya kusaidia wananchi wa Jimbo la Lupembe.

Mheshimiwa Spika, lakini pia niwapongeze sana watumishi wa Halmashauri ya Njombe DC wanafanya kazi nzuri sana. Pamoja na kwamba hatupati fedha ya halmashauri kuu sisi kama halmashauri, tumekuwa tukikusanya mapato ya ndani kwa zaidi ya asilimia 100 na tunajiendesha kwa asilimia zaidi ya 90 kwa mapato ya ndani. Naiomba Serikali iwatie moyo watumishi hawa waendelee kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine watumishi hawa wanadai fedha kwa ajili ya uhamisho kutoka Njombe Mji kwenda Njombe DC. Tunaomba wapewe fedha…

SPIKA: Mna makusanyo ya kiasi gani kwa mwaka? Mapato ya ndani Lupembe ni kiasi gani?

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ni zaidi ya shilingi bilioni moja na milioni mia tisa.

SPIKA: Bilioni 1.9?

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Kumbe ni hela ya kawaida tu.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ni hela ndogo sana. Kwa hiyo, naomba sana Serikali waliangalie Jimbo hili ili kusudi waweze kufanya kazi nzuri za maendeleo.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tunao uhaba mkubwa wa watumishi wa umma. Jimbo hili kwa maana ya halmashauri tuna upungufu wa watumishi zaidi ya 442, unaweza kupata picha namna ambavyo jimbo hili lilivyo na hali mbaya. Tunaiomba sana Serikali kwenye mpango huu wa bajeti mpya ya mwaka huu Jimbo la Lupembe litazamwe kwa upekee na wananchi wamenituma ndani ya Bunge lako kuja kuwanusuru wananchi hawa katika hali hii ambayo wanayo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, limesemwa sana humu ndani jambo la watumishi wa Serikali za Mitaa kwa maana ya Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji. Nilipokwenda kwenye kampeni na nilipokwenda kwenye ziara wananchi na viongozi hawa ndiyo wanaofanya kazi kubwa ya kusimamia maendeleo, wanaomba Serikali iwaangalie, iwape posho kwa ajili ya kujikimu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Edwin Swalle. Hivi Jimbo la Lupembe ni halmashauri gani?

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, Njombe DC.

SPIKA: Njombe Vijijini.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Yes.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Naibu Mawaziri wake wawili. Lakini pia nimpongeze sana Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mfugale, kwa kazi nzuri ambayo ameifanya kwa nchi hii katika ujenzi wa barabara katika sehemu mbalimbali za nchi yetu; nampongeza sana mzee Mfugale.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mkurugenzi wa SUMATRA kwa kudhibiti usafiri wa majini na nchi kavu. Ajali nchini zimepungua sana, kwa hiyo, nampongeza sana Mr. Gilliard Ngewe kwa kazi nzuri hapo SUMATRA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye mchango wangu katika Wizara hii. Hayati Dkt. Joseph Pombe Magufuli alitufundisha kwamba msemakweli ni mpenzi wa Mung na mimi naomba nisema ukweli kwenye jambo hili. Waziri wetu wa Ujenzi na Uchukuzi bajeti hii imeanza vibaya na haina matumaini kabisa kwa Watanzania walio wengi. Huu ni ukweli ulio wazi, Wabunge wote wanalalamika na nimekuwa nikimtazama Waziri wangu pale na yeye mwenyewe amekata tamaa, bajeti hii haina matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wananchi wa Jimbo la Lupembe viongozi wa Serikali tangu wakati wa Mheshimiwa Mkapa wamekuja Lupembe kutoa ahadi ya barabara ya Kibena mpaka Madeke kilometa 125. Wananchi wamekuwa wakifurika mara kwa mara kwenye kampeni wanapiga makofi, wanashangilia kwamba barabara ipo Kibena inakuja. Mwaka jana Wizara hii ya ujenzi wameitengea barabara hii shilingi bilioni 5.9 wakatuambia wapo mbioni kutangaza tender.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ndiye alikuwa Katibu Mkuu akatupatia shilingi bilioni 5 leo Wizara ileile imepunguza fedha kutoka shilingi bilioni 5 mpaka shilingi bilioni 2. Mheshimiwa Waziri hebu nisaidie kujua nini kimekusibu kupunguza kutoka shilingi bilioni 5 mpaka shilingi bilioni 2? Wananchi wa Lupembe tumekosa ni nini? Fedha hii umeiondoa Lupembe umeipeleka wapi na kwa nini? Hilo nitaomba kwenye majibu yako utusaidie kujua ili tujue kwa nini fedha imepunguzwa, imepelekwa wapi kwenye umuhimu zaidi kuliko wananchi wa Lupembe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, sisi watu wa Mkoa wa Njombe kwenye Ilani tumeahidiwa ujenzi wa uwanja wa ndege. Mheshimiwa Rais alipokuja Njombe tulifanya maombi, tukapiga na magoti tukaahidiwa kujengewa Uwanja wa Ndege Njombe. Nimeangalia kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri uwanja wa ndege hakuna lakini kwenye Ilani upo. Mimi nashindwa kujua mpango huu unatekeleza Ilani au hii bajeti mpya, siwezi kujua. Naomba Mheshimiwa Waziri utuambie ule mpango wa kujenga Uwanja wa Ndege Njombe umeishia wapi ili watu wa Njombe waweze kujua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la tatu na la mwisho, naomba kushauri Serikali, tumeona kuna kazi kubwa inaendelea ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, bila shaka mizigo itaanza kuwa mingi na mizigo mingi ya bandarini inakwenda Mikoa ya nyanda za Juu Kusini hasa kwenda Zambia, Malawi na kadhalika. Naiomba Serikali wawekeze jitihada kubwa kufanya upanuzi wa barabara ya kutoka Igawa kuelekea Tunduma. Mimi napita Mbeya mara nyingi, barabara ya Mbeya ina msongamano mkubwa, haipitiki, kuna malori, bajaji na daladala. Kama tunapanua Bandari ya Dar es Salaam kuongeza mizigo hatupanui tunakopeleka mizigo kazi hii itakuwa ni bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, asante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii muhimu ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kuungana na Wabunge wenzangu kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wake na timu nzima ya Wizara hii. Hata mimi ni shuhuda ambaye nimekuwa nikiongea na Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, wamekuwa ni wasikivu sana.

Mheshimiwa Spika, Sera yetu ya Umeme inasema Umeme kila Kijiji. Hata kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri inaeleza idadi ya vijiji ambavyo bado kupata umeme lakini sisi katika Jimbo la Lupembe bado tupo kwenye shida ya kupata umeme kwenye ngazi ya kata. Zipo kata ambazo hazina umeme hata katika level ya kata, achilia mbali vijiji.

Mheshimiwa Spika, Kata kama za Ukalawa, Ikondo, Mfiriga na Idamba, hakuna umeme. Maeneo haya palikuwa na mtu binafsi alikuwa na umeme unaitwa umeme wa Sefa ambapo watu wa Wizara waliwapa nafasi ya kutoa umeme kwa baadhi ya vijiji. Hata hivyo, kwa masikitiko makubwa sana ule umeme ambao ni wa Sefa kwanza ni wa bei ghali sana kwa sababu ni wa mtu binafsi, lakini pili umekuwa na changamoto nyingine, ule umeme hauna uwezo wa kuendesha hata mashine ya kukoboa na kusaga.

Mheshimiwa Spika, viko baadhi ya vijiji kwa mfano sehemu za Image, ikifika jioni saa 02.00 wananchi wamerudi mashambani wakiwasha TV zao haziwezi ku-operate kabisa kwa sababu umeme hauna nguvu, hata redio za kawaida, TBC au redio ndani ya mkoa umeme huu hauna uwezo wa kuziendesha. Kilichobaki sasa wananchi hawa wanaendesha hizi mashine na redio kwenye sehemu za starehe kwa kutumia mafuta. Kwa hiyo, nashauri sana Serikali katika karne hii ya 21 kwa muda ambapo tupo katika Sera ya Viwanda kuwa na jimbo ambalo hata umeme kwenye kata haujafika, hatutendi haki kwa wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Lupembe lina fursa nyingi za utajiri kwa ajili ya viwanda; Lupembe tunalima sana zao la chai kuna viwanda zaidi ya viwili vinahitaji umeme, Lupembe inalima sana matunda, hasa nanasi, wako watu wengi wana nia ya kuwekeza kwenye nanasi maeneo ya Madeke lakini kwa sababu hakuna nishati ya umeme wanashindwa kuweka viwanda ambavyo vingetoa ajira nyingi sana kwa vijana wetu. Pia kulikuwa na fursa nzuri ya kuweka viwanda vya parachichi kwenye jimbo hili lakini kwa sababu ya changamoto ya umeme wawekezaji wengi hawaji tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishauri sana Wizara ya Nishati pia kwenye maeneo ambayo kuna umeme wa REA kiasi kuna shida kubwa na mara kadhaa nimeongea na Naibu Waziri, Mheshimiwa Byabato kwamba umeme ambao upo umekuwa na wenyewe ni kero kuliko hata usingekuwepo. Wananchi wana mashine zao mfano, mteja amekuja kusaga unga kabla hujamaliza kusaga umeme umekatika. Kwa hiyo, mwananchi anashindwa kwenda kufanya kazi nyingine anasubiria mpaka umeme urudi na hajui unarudi saa ngapi.

Mheshimiwa Spika, pia kuna wananchi wa mashine ndogo au viwanda vidogo vya kuranda mbao. Kuna msiba, inabidi watu warande mbao kwa ajili ya shughuli ya msiba, umeme unakatika. Kwa hiyo, tatizo la kukatika umeme kwa nchi nzima ni kubwa na namuomba sana Waziri kama walivyoongea Wabunge wengi humu ndani, hii ni shida kubwa ukiachilia mbali kupeleka umeme kwenye kila kijiji, lakini kuwa na umeme ambao hauna uhakika pia ni kero kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu wako wananchi wamepata hasara sana, wameunguza redio, kuna mwananchi wangu mmoja mpaka nyumba yake imeungua kwa sababu ya kero ya umeme kukatika. Kwa hiyo, nimuombe Waziri pamoja na sifa nyingi ambazo tumetoa kwenye Wizara yake lakini tatizo la umeme kukatika, kutotabirika, kutokuwa na nguvu, Wizara hii itoe kipaumbele wasiweke tu kipaumbele kupeleka umeme kwenye kila kijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa ajili ya nafasi ya kuchangia bajeti hii muhimu sana ya Serikali. Nianze kwa kunukuu maneno ambayo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameyasema kwenye ukurasa ule wa 116 wakati akiwasilisha bajeti yake ndani ya Bunge lako Tukufu. Pengine kabla sijanukuu maneno hayo, niseme tu kwamba napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Nchi yetu, Samia Suluhu Hassan. Pia nawapongeza sana Waziri wetu wa Fedha, Naibu wake pamoja na timu nzima ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza, kwanza kwa kusikiliza maoni ya Waheshimiwa Wabunge, lakini pia nawapongeza sana kwa sababu wamekuwa ni wasikivu na kujibu kilio cha wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia bajeti hii, ukiitazama sura nzima inaakisi kauli mbiu ya Rais wetu, kwamba kazi iendelee. Hii ni kwa sababu bajeti hii ya kwanza imezingatia kuendeleza miradi yote mikubwa ambayo ndiyo imekuwa moyo wa Watanzania katika kupata maendeleo yao. Kwa hiyo kauli mbiu ya kazi iendelee imeakisiwa vizuri sana katika hotuba hii ya Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea kwenye ukurasa wa 116, Mheshimiwa Waziri alisema, naomba kumnukuu: “Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amenituma niwahakikishie Watanzania kupitia hotuba hii kuwa, tunaendelea kuijenga nchi, ije mvua, lije jua, tunaendelea kuijenga nchi, uwe usiku au mchana, tunaendelea kuijenga nchi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Lupembe, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Rais kwamba sisi wananchi wa Jimbo la Lupembe, iwe usiku, iwe mchana, tutaendelea kumuunga mkono kwa kazi nzuri ambayo ameanza kuifanya inayoleta matumaini makubwa sana kwa Watanzania wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Lupembe wamenituma nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwamba zile milioni 500 kwa ajili ya barabara za vijijini zimewafikia na kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya Wizara hii kuhusu kutoza fedha kwenye mafuta kwa ajili ya barabara za vijijini, wananchi wa Jimbo la Lupembe wanayo matumaini makubwa, kwamba barabara ambazo kwa muda mrefu zimekuwa na shida; Barabara kama ya Nyombo – Ikuna – Kichiwa – Mtwango – Welela sasa itakwenda kupata ufumbuzi. Pia barabara ambayo imekuwa na kero ya muda mrefu ya kutoka Ninga – Lima – Ikondo, kwa bajeti hii itakwenda kupata ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo machache ambayo nataka sasa niishauri Wizara hii. Sehemu ya kwanza ni kuhusu sehemu ya TRA. Nilizungumza na Mheshimiwa Waziri wiki mbili zilizopita, kwamba wananchi wa Mkoa wa Njombe, hasa wajasiriamali wadogo wa biashara ya mbao kumekuwa na biashara kubwa sana kwenye biashara ya miti ya mbao. Siyo Njombe tu, mikoa mingi ya Nyanda za Juu Kusini kumekuwa na kero kubwa kwa wasafirishaji wa biashara ya mbao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa, nilimwambia Waziri hapa, kwamba kumekuwa na hitaji la kisheria la watu ambao wanafanya biashara ya mbao kusajiliwa kwenye VAT. Mfanyabiashara wa mbao akisajiliwa kwenye VAT anakwenda kununua mbao kwa wakulima wadogowadogo kule vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yuko babu yangu, au mtu ambaye ana msitu, ameufuga kwa zaidi ya miaka kumi, anauza mbao mara moja tu kwa miaka kumi au 15, lakini kwa mujibu wa sheria hii, inamtaka huyu mkulima mdogo anavyouza huo msitu wa mbao awe na mashine ya EFD. Kwa hiyo huyu mfanyabiashara aliyesajiliwa kwenye VAT akienda kwa yule mwananchi wa kule chini hana risiti ya EFD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake hapa ni nini? Kumekuwa na udanganyifu mkubwa wa wafanyabiashara na kukwepa kodi ya Serikali. Pia Maafisa wa TRA ambao siyo waaminifu wamejenga mazingira ya kuchukua fedha kwa wafanyabiashara wa mbao. Kwa hiyo biashara ya mbao Mkoani Njombe imeshuka na baadhi ya wafanyabiashara wameamua kuacha kabisa hii biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, nilimwomba Waziri na leo namwomba tena, tukimaliza Bunge hili la Bajeti afike Mkoani Njombe akazungumze na wafanyabiashara hawa ili kutatua changamoto ya VAT na biashara ya mbao ambayo kimsingi imekuwa na shida sana. Wafanyabiashara wako tayari kulipa kodi lakini wanahitaji uwekwe mfumo mzuri ambao utakadiriwa na wakajua kwamba ukipakia mbao kiasi fulani, malipo yake ni kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo napenda kuishauri Serikali ni kuhusu elimu kwa mlipakodi. Nimesoma kwenye bajeti hii kuna suala ambalo halijasemwa vizuri. Makamu wa Rais akiwa Waziri wa Fedha aliongea ndani ya Bunge hili kwamba alipokwenda kugombea jimboni aligundua wananchi wengi ni maskini na aligundua kuna ukwepaji mkubwa sana wa kodi na ubadhirifu wa fedha za umma kwenye miradi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla hajawa Makamu wa Rais, aliahidi Bunge hili kwamba angetoa elimu kwa Wabunge tujue mianya ya upotevu wa fedha za umma. Naomba nimshauri Waziri; kwa sababu ahadi hii aliitoa Makamu wa Rais wa sasa, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atoe semina kwa Wabunge na Madiwani ambao ni wasimamizi wa shughuli za maendeleo kwenye majimbo haya, wapate semina kujua mianya ya ubadhirifu wa fedha za umma kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia sana kudhibiti upotevu wa fedha ambao Serikali kwa siku za karibuni wanapeleka fedha nyingi sana kwenye halmashauri, lakini bila kuwa na usimamizi fedha hizi zitakwenda kupotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo napenda kusema ni kwamba, naishukuru sana pia Serikali kwa kutupia macho Mradi wa Liganga na Mchuchuma kule Njombe. Ninachomwomba Waziri wa Fedha, kwa kuwa Rais ameonesha mwelekeo wa mradi huu ukamilike mapema, Mkoa wa Njombe hauna uwanja wa ndege, na nilishauri kwenye mpango wa Serikali kwamba ni vizuri vipaumbele vya Serikali vikaendana na maeneo muhimu ambayo Serikali imekusudia kuweka fedha nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mkoa wa Njombe ambao sasa unafungua uchumi mkubwa kwenye Mradi wa Liganga na Mchuchuma na ule mkoa una biashara kubwa ya matunda ya parachichi na ni mkoa wa tatu kwa uchumi nchini, hauna uwanja wa ndege. Kwa hiyo namwomba sana Waziri kwenye bajeti yake hii basi aendelee kutazama maeneo ambayo kuna mambo mengi ya kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba pia kulisema ni kuhusu suala zima la kuwasaidia wananchi kuwa na uelewa wa kudai risiti baada ya kupata huduma. Siku za karibuni kumekuwa na kujisahau kwa Watanzania wengi kudai risiti. Ukienda kwenye sheli sasa hivi, sheli nyingi hawatoi risiti kwa wanaoweka mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na bajeti hii kuwa nzuri ni vizuri akajielekeza kutoa elimu kwa Watanzania ili wajue kodi wanayolipa ndiyo kodi ambayo inawafanya wao kupata maji safi na salama; kodi wanayolipa wanapata elimu bora; kodi wanayolipa ndiyo wanapata maji na kadhalika. Bila kutoa elimu hii kwa Watanzania wakawa sehemu ya kusimamia uchangiaji wa fedha hizi hakutakuwa na maana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata Waheshimiwa Wabunge sisi kama sehemu ya kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi ni vizuri pia tukawa na sehemu kubwa ya kuwaelimisha wananchi wetu waone furaha kulipa kodi kwa sababu kodi ni maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kwanza kuchangia taarifa ya Kamati hii ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kukushukuru sana wewe kwa kuniamini na kuniteua kuwa kwenye Kamati hii ya Sheria Ndogo ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ulivyosema kwenye utangulizi, kwa mujibu na mifumo ya nchi yetu, sheria ndogo ndio sheria ambazo zinagusa kwa kiasi kikubwa wananchi walio wengi kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, na nitumie nafasi hii kuipongeza sana Kamati ya Sheria Ndogo kwa kufanya kazi kubwa sana katika uchambuzi wa sheria hizi ambazo katika uchambuzi huo imebainika dhahiri kwamba kulikuwa na dosari muhimu za kurekebisha hasa kwenye kulinda tasnia ya sanaa, tasnia ya walimu, tasnia ya watu wa bodaboda na wananchi mbalimbali kwenye kilimo na kadhalika. Kwa hiyo, niwapongeze sana Kamati ya Sheria Ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kamati na ripoti ambayo imetolewa hapa ni dhahiri kwamba ziko changamoto mbalimbali hasa kwenye ushirikishwaji wa wananchi kwenye kutoa maoni kwenye sheria hizi ndogo. Sote tunajua kwamba katika nchi yetu yapo maeneo kadhaa kumekuwa na mvutano na wafanyabishara wadogo pamoja na watu wa bodaboda wakilalamikia baadhi ya sheria ambazo zimekuwa zikitungwa na mamlaka ambazo zinatunga sheria ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali na mamlaka ambazo zinahusika na utungaji wa sheria hizi ndogo ni vizuri sheria hizi kwa sababu walaji na waathirika wa sheria hizi ni wananchi wa kule chini, kabla ya sheria kuanza kutekelezwa ni muhimu sana wadau hawa wakasikilizwa na ndiyo maana kwenye ripoti ya Kamati imeabainika dhahiri kwamba kwenye Sheria ya Bodi ya Walimu kwa mfano walimu walikuwa na maoni yao ya msingi sana ya kuboresha Bodi ya Taaluma ya walimu. Lakini kwa sababu tu ya kutokushirikishwa vizuri na kutoa maoni yao kwa ufasaha kumeleta mvuta usiokuwa wa lazima na kupelekea Kamati ya Sheria Ndogo kutoa mapendekezo ambayo imewatoa ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni muhimu kwenye siku za usoni, mamlaka hizi za kutunga sheria ndogo wafahamu kwamba sheria hizi ni kama huduma kwa wale walaji wasiposhirikishwa wale ambao ndiyo sheria inawagusa inaleta shida nyingi sana kwenye maeneo mbalimbali. Na ndiyo maana Kamati ilibaini mfano; kule Mbeya kulikuwa na sheria ndogo ambayo ilikuwa inaweka faini kwa watu wa bajaji kwenye fedha ambayo ni karibu sawa na mtu anayemiliki basi.

Sasa sheria hizi kama ambavyo kamati imebainisha ni kwamba hazina uhalisia wa mazingira ya wananchi na biashara ambazo wanafanya. Kwa hiyo, ni rai yangu mimi kama Mbunge basi mamlaka za kutunga Sheria ziweke mazingira ya wazi ili sheria zisiwe na malalamiko makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kama ambavyo taarifa ya Kamati imesema, imeonesha ndani ya sheria ambazo zimefika kwenye Kamati kulikuwa na shida ya kiuandishi kwenye sheria karibu 15. Hii tafsiri yake nini? Na nimaoni yangu mimi kama Mbunge pengine mamlaka ambazo zimekasimiwa kutunga hizi sheria ndogo ni vema wakawa na muda wa kutosha wa kupitia sheria inayohusu utungaji wa sheria ndogo kwa ufasaha ili kusudi kuipunguzia mzigo kamati wa kuchambua kazi ambayo ingefanywa na mamlaka husika kwenye utungaji wa sheria yenyewe. (Makofi)

Kwa hiyo, ni vyema basi kwenye siku za usoni ambako tutakwenda baadaye na nimuombe sana Waziri wetu wa Sera Bunge, Kazi na Ajira Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na kazi nzuri ambayo anafanya ya kusimamia utaratibu mzuri wa sheria ndogo basi asaidie pia hizi mamlaka zinazotunga sheria ndogo wajitahidi sana kufuata utaratibu ambao tumejiwekea kama nchi kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kulichangia kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa hapa ni kuhusu hoja mahususi ya hizi sheria zinazohusu watu wa filamu. Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ni dhahiri kwamba sanaa ya muziki nchini ni sanaa inayoajiri vijana wengi sana na vijana hawa wanafanya kazi hizi kwa ubunifu wao wenyewe, ni rai yangu kama Mbunge kwamba sekta ya sanaa nchini inahitaji kupewa ulezi na nafasi ya kukuzwa badala ya kuwekewa mazingira ya kudidimiza.

Kwa hiyo, ushauri ni kwamba Serikali ichukue hatua, inapotunga sheria za kusimamia sekta hii ya sanaa na muziki nchini basi sheria zake ziweke mazingira ya kuhamasisha sekta badala ya kuwavunja moyo wasanii wetu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na nimatumaini yetu kwamba kama sekta hii ya muziki na sanaa itakuzwa kwa kiasi kikubwa itachangia sana kwenye pato la Serikali, lakini pia itachangia ajira kwa vijana wengi ambao nchi nzima sasa hivi wanafanya ubunifu katika sanaa na muziki. Kwa hiyo, niipongeze sana kamati kwa kazi nzuri walioyoifanya kwa ajili ya kuboresha kanuni za kusimamia filamu sanaa pamoja na muziki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia niwapongeze upande wa Serikali kwa Mawaziri ambao walienda kwenye Kamati ni dhahiri kwamba walitoa ushirikiano mzuri sana na hii imetoa picha kwamba dhamira ya Serikali imekusudia kuboresha maisha ya Watanzania na kuwapeleka Watanzania katika maisha bora zaidi. Kwa hiyo, hili ni jambo jema na niipongeze sana kwa hiyo kwa sababu ni sura nzuri, kwamba kama Taifa sasa na Serikali inatazama zaidi maslahi ya wananchi walioko kule chini ili kusudi kama Taifa tuweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako, kwenye Kamati hii ya Sheria Ndogo ameeleza vizuri sana utayari wake wakushirikisha wadau mbalimbali kwa ajili ya sekta ya elimu na tumeona wiki iliyopita ameanza kutekeleza kwa kuanza kukaa na wadau mbalimbali kwenye hii sekta ya elimu katika kutekeleza maoni ya Kamati ambayo imeanza kuyatoa hii ni sura nzuri na tukiendelea hivi kama Bunge basi mbele ya safari kazi itakuwa nzuri na nyepesi sana.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, baada ya hayo nakushukuru sana naunga mkono ripoti ya Kamati. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuwa mchangiaji wa pili kwenye taarifa hii ya Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuunga mkono taarifa nzuri ya Kamati ya Sheria Ndogo na niipongeze sana Kamati kwa kazi kubwa ambayo wameifanya ya uchambuzi wa Sheria 487.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili pia nimshukuru sana Mheshimiwa Spika, kwa kuipa muda wa kutosha Kamati ya Sheria Ndogo na hii inaashiria kwamba Ofisi ya Mheshimiwa Spika inatambua na kujali madhara ya Sheria Ndogo ambazo ndiyo zinatumiwa kwenye shughuli za kila siku za wananchi wetu wa Tanzania. Wakiwemo wale wavuvi na watu wa chini katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirejea kwenye taarifa ya Kamati kama ambavyo imesomwa na Mwenyekiti wa Kamati, ukitazama kwa ujumla unaweza ukapata picha kwamba katika uchambuzi ambao Kamati imefanya kumekuwa na kosa ambalo mara nyingi linafanywa na mamlaka za utunzi wa hizi Kanuni au Sheria Ndogo. Hii inapelekea kwamba mtazamo wa utunzi wa Kanuni hizi wakati fulani unaangalia kuwa na lengo la kukataza, lengo la kuzuia, lengo la kutoa adhabu na lengo la kukataza watu wasifanye shughuli mbalimbali za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndiyo maana miongoni mwa Kanuni ambazo zimebainika kuwa na dosari ni Kanuni ya Wanyamapori na Uhifadhi kwenye Kifungu cha 24. Kanuni hii ambayo inahusu ajira za Wahifadhi Wanyamapori ilikuwa inataka mtu akiajiriwa kwenye Uhifadhi wa Wanyamapori asifanye shughuli nyingine yeyote ya kumuingizia kipato chake halali. Kanuni hii kama ingeachwa kama ilivyo tafsiri yake ni kwamba mtu anayefanya kazi ya ulinzi kwenye hifadhi hataweza kufanya hata shughuli zingine za kumuingizia kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Kamati inakuwa je, kama asifanye shughuli yoyote ya kumuingizia kipato ina maana kwamba haruhusiwi kuwa na duka lake binafsi, ina maana kwamba haruhusiwi kuwa na shamba lake binafsi. Kwa hiyo, Kanuni hii ilikuwa haitoi taswira sawa sawa kwamba asifanye shughuli nyingine binafsi maana yake nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Kamati imeona hii dosari kwamba kwa mujibu wa Katiba yetu ukisoma kuanzia Ibara ya 12 hadi ya 30 ni wazi kwamba Watanzania wanayo haki ya kufanya kazi na wana haki ya kupata ujira. Kwa hiyo, ni maoni ya Kamati kwamba Kanuni hii ilikuwa na dosari hiyo kwa hiyo pamoja na kuzuia shughuli maalum ya ulinzi, lakini Mlinzi ana haki ya kufanya shughuli zingine za kumuingizia kipato kama raia wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo lingine kwenye Kanuni ya Misitu inayohusu uzalishaji, usafirishaji na uuzaji wa mkaa mbadala. Waheshimiwa Wabunge wote mnajua dunia sasa hivi inatazama uhifadhi wa mazingira na siku za karibuni Mheshimiwa Rais alikuwa kwenye mkutano mkubwa duniani unaozungumza kuhifadhi mazingira, maana yake ni kwamba kuelekea kwenye kanuni za kutengeneza mkaa mbadala ni kitu muhimu cha kuhimiza wananchi wetu watengeneze mkaa mbadala badala ya kuharibu maliasili ya misitu kwa maana mkaa wa asili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kanuni hii ya Tisa ukitazama kwenye maudhui yake inatoa katazo au inatoa mamlaka kwa Mhifadhi wa Misitu kwamba anaweza kusitisha leseni ya mtu anayefanya kazi ya uzalishaji wa mkaa mbadala au usafirishaji au uuzaji na haitoi akisitisha hicho kibali, atasitisha kwa muda gani na haielezi atarudishiwa kwa namna gani akikidhi masharti ya kibali husika. Kwa hiyo, hii pia ilikuwa ni dosari kubwa tunadhani ni wakati sasa Kanuni zetu nyingi ziwe ni Kanuni za kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo badala ya kukataza na kutoa adhabu peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho na la muhimu napenda pia kuishauri Serikali kwamba inapoendelea kutunga hizi Kanuni na Sheria Ndogo ndogo tuwe na mtazamo zaidi wa kutunga Sheria na Kanuni za kuwezesha shughuli za wananchi kuendelea badala ya kuwa na sheria ambazo kazi yake kubwa ni kukataza, kuzuia na kutoa adhabu peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Jenista Mhagama Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba hata Mawaziri walipokuja kwenye Kamati ya Sheria Ndogo wakati wote ilipobainika dosari ya kufanyia marekebisho walikuwa tayari na kutoa ushirikiano mkubwa sana kwa ajili ya ujenzi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kwanza kuweza kuchangia taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo. Kwanza nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kututeua kuwa kwenye Kamati hii ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati hii ya Sheria Ndogo kwa kufanya kazi nzuri ya kusoma hotuba ya Kamati hii ya sheria ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kusema kwamba wajibu wa kutunga sheria za nchi hii ni mamlaka ya Bunge lako tukufu, na wajibu huu wa kutunga sheria tumepewa kama Bunge kwa mujibu wa Ibara ya 4 na Ibara ya 64 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na wajibu huu sisi kama Bunge tunao wajibu wa kuulinda kwa wivu mkubwa pale ambapo Bunge linakasimu haya madaraka kwa mamlaka zingine kutunga kanuni mbalimbali za kuendesha taasisi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kama ambavyo taarifa imesomwa hapa, Bunge lako kwa mujibu wa Ibara ya 97 inayo Mamlaka ya kukasimu madaraka ya utunzi wa sheria ndogo kwa mamlaka zingine za Serikali, na miongoni mwa hizo mamlaka ni pamoja na Wizara mbalimbali na taasisi mbalimbali za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kumekuwa na shida kidogo siku za karibu, Bunge likitunga sheria mama ndani ya Bunge na kutoa mamlaka au kukasimu madaraka kwa mamlaka zingine kutunga kanuni, mamlaka hizi nyingine zimekuwa zikitunga kanuni ambazo wakati fulani zinakinzana na dhamira ya Bunge lako tukufu. Kwa sababu mamlaka ya utunzi wa sheria ni ya Bunge zinapokwenda kutungwa kanuni zingine na hizo mamlaka zikileta mkanganyiko kwa wananchi lawama zinakuwa ni kwa Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa kuanza tu naomba nitoe wito na rai sana mamlaka za Serikali zinazokasimiwa mamlaka na Bunge kutunga kanuni mbalimbali za uendeshaji wa shughuli zihakikishe zinatunga kanuni ambazo zinasaidia wananchi wetu kufanya kazi vizuri kwenye maeneo yao. Kwa sababu kumekuwa na kero nyingi kwenye kanuni na sio sheria za Bunge. Kwa mfano Bunge lako tukufu hapa ndani lilitunga sheria ya Bunge ambayo ni sheria ya watu wa EWURA ikitoa mamlaka kwa Wizara kutunga kanuni kuratibu uendeshaji bora wa vyombo vya usafirishaji wa abiria. Lakini kwenye utunzi wa kanuni kwenye mamlaka husika imekwenda kutungwa kanuni ambayo inaitwa The Land Transport Licensing Private Hire Regulations, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kanuni hii, kwenye kanuni ndogo ya 15(d) kanuni imeweka utaratibu kwamba wanaomiliki leseni za vyombo vya moto vya usafirishaji wa abiria kwa mfano wakiwemo watu wa bodaboda, watu taxi na kadhalika na watu wa bajaji, kila mmoja afunge mita kwenye chombo chake cha moto, ifungwe mita kwa ajili ya kukokotoa nauli za abiria. Kamati yako inajiuliza unafunga mita kwenye bodaboda kukokotoa nauli gani ya abiria. Kwa hiyo, sisi kama Bunge tunadhani waliokwenda kutunga hizi kanuni wanaweza kwenda kuleta kero kwa wananchi, na ikienda kuwepo kero inakuwa ni lawama kwa Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa hiyo kwakuwa Bunge lako lina mamlaka ya kufuatilia utunzi wa kanuni hizo, na kama zimetungwa kinyume na utaratibu au haziwezi kuwa na ufanisi mzuri Bunge lako linayo mamlaka ya kuitisha kanuni hiyo na kuirekebisha na ndio maana taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Ndogo inaliomba Bunge leo hii, kwenye moja ya maazimio yake ni kwamba tunataka mamlaka husika ikarekebishe na kufuta makosa haya ambayo yamekwenda kujitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili, Bunge hili linapotoa maazimio kwa mamlaka ambazo zinatunga sheria ndogo mwaka jana mwezi Novemba Bunge liliazimia hapa ndani kwamba baadhi ya makosa ambayo yalionekana kwenye kanuni au sheria ndogo yakarekebishwe, lakini kama ambavyo taarifa imesomwa hapa leo, tangu mwaka jana mwezi Novemba hadi leo mwezi Septemba hizi kanuni hazijarekebishwa, tafsiri yake ni nini. Azimio la Bunge halijafanyiwa kazi. (Makofi)

Naomba kutao rai kwa niaba ya kamati ya Sheria Ndogo, maagizo ya Bunge Kwenda kurekebisha kanuni sio hisani, ni maelekezo ya Bunge na ni lazima yatekelezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lipo jambo lingine ambalo pia limesemwa kwenye taarifa ya Kamati kwamba Bunge limetunga sheria mama kuweka adhabu kwa watu mbalimbali ambao watakiuka taratibu kwenye sheria ya The Energy and Water Utilities Regulatory Act Namba 414; kwenye kifungu cha 8 cha sheria hii kimetoa adhabu ambayo ni kiasi cha shilingi 300,000 au kifungo cha miezi 15 na kikaitaka mamlaka husika wa watu wa maji wanapokwenda kutunga kanuni zao za kuratibu vizuri zoezi hili la shughuli za maji wamekwenda kutuma kanuni ambayo imeongeza adhabu baada ya Bunge ambalo limeweka adhabu ndogo ya shilingi 300,000 wao wameweka shilingi 3,000,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge limesema adhabu isizidi miezi 15 kwa maana ya kifungo, wao wamekwenda kuweka miezi 15. Tunaomba kutoa rai tena kwamba tunaomba mamlaka zinazokasimiwa utunzi wa kanuni na sheria ndogo wazingatie maelekezo ya Bunge kwa ustawi wa nchi na wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Naomba kuunga mkono hoja taarifa ya Kamati kwamba tunaliomba Bunge likubali na kutoa maazimio kwamba kwa kuwa hizi dosari ni kubwa na zipo kwenye taarifa ya Kamati, tunaomba ifikapo mwezi Novemba, 2022 marekebisho haya yakafanyiwe kazi. Na mwisho kama ambavyo taarifa imesema marekebisho ya mwisho yafanyike mwezi Desemba, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Bunge mfano mwaka jana hapa kupitia serikali na mapenzi mema ya Mheshimiwa Rais tumepunguza hata faini kwa watu wa boda boda kutoka shilingi 30,000 hadi shilingi 10,000 ili bodaboda wetu wafanye kazi vizuri, wafanye kazi kama Watanzania wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini inapofika mahali kunakuwa kuna kanuni ambazo badala ya kusaidia kazi nzuri ya bodaboda zinakwenda kuanzisha utaratibu wa kufunga mita, naomba Bunge hili lisikubali na lazima haya mambo yafike mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho naliomba sana Bunge lako tukufu, sisi kama Wabunge na wawakilishi wa wananchi tuendelee kufuatilia kanuni zote ambazo zimekuwa ni kero kwa wananchi wetu, na sisi kama Kamati yako ya Sheria Ndogo kwa niaba ya Bunge hili tukufu tutaendelea kufanya kazi hii, ili kusudi wananchi wetu waendelee kufanya kazi nzuri za uzalishaji kwa ajili ya maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa upekee sana naomba mamlaka zote ambao wanatunga sheria ndogo wasitunge sheria za udhibiti tutunge sheria za kuwezesha wananchi kufanya majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kuhusu mchango huu ambao ni maoni ya Mpango wa Bajeti ya Serikali. Kwanza niseme jambo mmoja, tangu juzi Wabunge wamejadili humu ndani mambo mbali mbali lakini mmoja kubwa ambalo Wabunge wengi tumejiuliza ndani ya Bunge lako Tukufu ni kwamba tunayo maji ya kutosha, tunayo ardhi ya kutosha, tunao watu, Wabunge wanasema, kwanini mambo hayaendi mbele? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, aliwahi kusema wakati fulani, na pengine hilo huwenda likawa ndilo jibu. Alisema kuna msemo Wakwere wanasema ‘zilongwa mbali zitendwa mbali’; yaani yanayosemwa na yanayokwenda kutekelezwa ni tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu wa Mheshimiwa Waziri wa Fedha ukiusoma ni mpango mzuri sana, na hata ukisoma takwimu ni takwimu nzuri sana; lakini utajiuliza ni kwa nini kila mwaka tukija hapa ndani tunarudia mambo yale yale ndiyo maana jibu lake likawa zilongwa mbali zitendwa mbali. Ukitazama michango ya Wabunge, wamechangia maeneo mazuri sana kwenye kuboresha mpango huu. Wametoa maoni mengi sana kwenye Bunge lako Tukufu, lakini unaweza kuja kushangaa tukija mwakani hapa, kwenye mpango wenyewe ukaona hakuna hata moja ambalo wenzetu wa Wizara wameyaweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe wenzangu Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Spika utuongoze Bunge lako, tulioyasema humu ndani ya Bunge, tunatamani kuyaona kwenye mpango wenyewe. Tunaolala na wagonjwa ni sisi, ndio tunaojua wanapoumwa. Sisi ni Wabunge tunajua shida za wananchi wetu, tuwaombe sana wataalam watusikilize, watusikilize na waamini kwamba tunayoyasema ndiyo matatizo ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hasa nianze kwenye kilimo, jambo la kilimo tangu wakati wa Mwalimu Nyerere, tumesema kilimo ni siasa, kilimo cha kufa na kupona na kadhalika, lakini miaka yote hii kilimo kimekuwa kinasuasua. Nitumie nafasi hii kwa mara ya kwanza kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye yeye ameamua kuondoka kwenye kauli ya zilongwa mbali zitendwa mbali ameamua kufanya kwa vitendo kwa kuongeza bajeti ya kilimo kuanzia bilioni 294 hadi bilioni 959, zaidi ya zaidi ya mara tatu. Rais ana dhamira njema ameamua kufanya kwa vitendo, lakini nimwombe sana Waziri wa Kilimo na hili nasema na Bunge liweke Kumbukumbu. Tumemuongezea Waziri wa Kilimo fedha kwa ajili ya mbolea, mbegu, ujuzi na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, nataka kuamini tutakuja mwakani hapa, tutakuwa na wakulima wengi ambao wamelima mazao yao lakini hakuna soko. Mwaka jana kabla ya kuongeza bajeti tulikuja hapa, tukaiomba Serikali itafute fedha za dharura kwenda kununua mahindi kwa wakulima. Namuomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, wameshauri Waheshimiwa Wabunge humu ndani, mpango mzuri unaokwenda nao, tusaidie kuweka mkakati wa kutafuta masoko kwa ajili ya mazao haya ya wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kule Lupembe wananchi wangu wamehamishwa sana kulima parachichi, tunavyozungumza wamelima parachichi wameuza zaidi ya miezi sita hawalipwi kwenye mazao yao, soko hakuna. Kwa hiyo naomba kabla hatujatengeneza crisis ya soko tujipange mapema, tuandae soko, wananchi wakilima mahindi au mazao watakwenda kuuza wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo Tusaidie kutuondolea watu wababishaji na wafanyabiashara uchwara kwenye kilimo. Sisi Lupembe kwa mfano tunalo zao la chai, zao ambalo ni kubwa sana kwenye nchi hii. Linaingiza fedha za kigeni na lina uwezo wa kutoa ajira nyingi sana kwa wananchi wetu. Linaweza kutoa ajira kwa mkulima mwenyewe kwa mzalishaji, watu wenye magari, wasafirishaji na kadhalika. Lakini zaidi ya miaka 20 wananchi wa zao la chai Lupembe wamezidi kuwa maskini, wanalia na Serikali kila siku wanaomba kiwanda chao kirudi kifanye kazi sababu hakifanyi kazi. Tunaongea habari ya ajira hapa, mtapataje ajira?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, wananchi wa Lupembe wamelia kilio kama mamba majini machozi yao yanakwenda na maji. Naomba wapatie matumaini wananchi wangu wa Lupembe, kile kiwanda cha Lupembe Tea factory Kirudishwe kifanye kazi na mwekezaji aliopo pale tuondolee kama ni mzigo, atoke pale, wananchi wangu wapate ajira na Serikali ipate fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni kuhusu…

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Edwin Ennoy Swalle kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo.

T A A R I F A

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa tu taarifa Mheshimiwa Mbunge wa Lupembe na wananchi wake, kwamba Serikali imeshachukua hatua dhidi ya muwekezaji wa kiwanda cha Lupembe Tea Company Dhow Merchantile, na sasa Bodi ya Chai imeshamuandikia notice ya kumfutia leseni kwa sababu makubaliano yote aliyoingia na Serikali ameamua kutokuyafuata. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Swalle, unaipokea taarifa hiyo.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili kwa niaba ya Wananchi wa Lupembe. Ninachoomba kauli hii ya Mheshimiwa Waziri isiwe zilongwa mbali zitendwa mbali. Nakushukuru sana Mheshimiwa Bashe kwa jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni kuhusu jambo la mazingira. Nimesoma kwenye mpango wa Serikali, jambo la mazingira limesemwa kama jambo la mzaha hivi. Jambo la mazingira; naishauri Serikali tusitegemee fedha za wahisani tu, tuanzishe mpango maalum angalau kwenye halmashauri zetu waanze kutenga fedha kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji. Hata hapa Dodoma hali ya hewa imekuwa ikibadilika siku hadi siku, na wananchi yetu wanaendelea kuongezeka, tusipoweka mkakati wa muda mrefu wa kutunza mazingira, wakutunza maji, suluhu ya muda mfupi ya kuhamisha wananchi kwenye mabonde haiwezi kusaidia. Suluhu ya kudumu ni kutunza mazingira, tuwashirikishe wananchi wapande miti, watunze vyanzo vya maji wawe sehemu ya kuhifadhi mazingira yetu. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumesaidia nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere pale leo, linategemea maji, Mikoa ya Kusini ndio mwanzo wa maji haya. Tumeingiza trilioni sita pale lakini mpango wa Serikali wa kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kutumia fedha za ndani kwenye halmashauri upo wapi? Juzi pale kwangu Mtwango wananchi wangu wamelima kwenye maeneo ya mabonde, wamefyekewa mazao yote pale, lakini kufyeka mazao haiwezi kuwa suluhu ya kuhifadhi maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuwa na mpango wa Serikali wa kukwamua utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji. Napendekeza kama itakuwa jambo jema, Serikali ikiona inafaa, waziagize halmashauri, kwa kuwa mmeagiza kutoa asilimia kumi kwa ajili ya wanawake, vijana na wenye ulemavu, agizeni halmashauri watenge hata asilimia mbili kwa ajili ya fedha za kuhifadhi mazingira na kutunza vyanzo vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ambayo umenipa ili nami niweze kuchangia Wizara hii ya TAMISEMI. Kwanza kabisa nitumie nafasi hii kumpongeza sana Waziri, Mheshimiwa Innocent Bashungwa pamoja na Manaibu Mawaziri wake; Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mheshimiwa Festo John Dugange na wataalamu wote wa Wizara hii ya TAMISEMI. Naomba ifahamike wazi kwamba, Wizara hii ni muhimu sana na ni roho ya wananchi wa Tanzania na tunawategemea sana.

Mheshimiwa Spika, nitumie pia, nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake mahiri wa mwaka mmoja ambao umekwenda kupita sasa. Tunapompongeza Mheshimiwa Rais, wako baadhi ya watu wanadhani pengine tunafanya utani.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kwa upande wa Jimbo la Lupembe, ndani ya huu mwaka mmoja wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, tulikuwa na Kata kama ya Ikondo ambayo tangu kuumbwa kwa ulimwengu wa dunia hii hakujawahi kuwa na kituo cha afya wala shule ya kata, lakini Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amewafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikuwa hatuna shule shikizi kwenye maeneo kama ya Madeke na maeneo ya Itova. Ndani ya mwaka mmoja, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewafikia wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, wananchi wangu wa Mtwango pale Lunguya wamekuwa na shida ya muda mrefu ya barabara ya Lunguya kwenda Welela. Ndani ya mwaka huu mmoja tu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amewafikia wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, Njombe DC tulikuwa hatuna Makao Makuu ya Halmashauri, Mheshimiwa Silinde alikuja mwaka 2021 kule; tulikuwa hatujaanza hata kujenga msingi, lakini ndani ya huu mwaka mmoja pekee, Mheshimiwa Rais ametuletea fedha shilingi bilioni 1,900 na hivi sasa ujenzi wa makao makuu upo kwenye level ya lenta. Nani kama Samia Suluhu Hassan? Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais tunapompongeza Mheshimiwa Rais tunamaanisha na kazi anazifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaposhukuru hivi, ni ishara pia ya kuomba tena. Unaposhukuru ni kwamba, unataka kuomba tena. Halmashauri ya Njombe DC, pamoja na kazi nzuri ambazo Mheshimiwa Rais na Serikali imefanya, tunazo changamoto katika maeneo kadhaa ambayo napenda kuyabainisha. Kwanza alipokuja Mheshimiwa Silinde, Naibu Waziri, ikapendekezwa kujenga Makao Makuu ya Halmashauri. Eneo hili halina kituo cha afya. Kwa hiyo, eneo ambalo tunakwenda kujenga Makao Makuu ya Halmashauri patakuwa na watumishi wengi sana. Tunaiomba Serikali ipeleke Kituo cha Afya katika Kata ya Kidegembye.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, alipokuja Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Ummy, alituahidi kutupatia kituo cha afya kwenye Kata ya Ikuna na tulishauriwa kwamba, tusiendelee na ujenzi wa kile kituo cha afya badala yake tuelekeze nguvu kwenye ujenzi wa kituo cha afya kikubwa cha pale Mtwango kwa mapato ya ndani. Napenda kutoa taarifa, Halmashauri ya Njombe DC chini ya usimamizi wa Mkurugenzi wetu mahiri sana, Dada Sharifa Yusufu Nabarang’anya, tumeshajenga kituo cha afya kwa mapato ya ndani chenye majengo zaidi ya nane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Halmashauri yetu imejenga kituo cha afya kwa mapato ya ndani kwa majengo zaidi ya nane, naiomba sana Serikali iwasaidie wananchi wa Mtwango, Ilunda, Welela, Sovi na Itunduma, kupata vifaatiba kwenye hospitali hii. Kama itapendeza pia wananchi hawa wangepata watumishi wa afya na vifaatiba na vifaa tendanishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba ya Waziri amezungumza mafanikio mengi sana ambayo yamepatikana. Nilikuwa napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri kwamba ufanisi huu wa TAMISEMI unasaidiwa pia na Wakurugenzi kwenye Halmashauri zetu. Napenda kutoa ushauri kwa Wizara, wapo Wakurugenzi ambao wamemwelewa sana Mheshimiwa Rais na wanafanya kazi nzuri sana, akiwemo Mkurugenzi wangu wa Njombe DC, dada yangu Sharifa. Nilikuwa namshauri, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, tunakokwenda, aanze kutoa zawadi maalum kwa Wakurugenzi wanaofanya vizuri kwa ajili ya motisha. Hili jambo litakuwa ni muhimu sana kuwatia motisha ili na Wakurugenzi wengine wajifunze kufanya kazi kwa ufasaha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naomba kushauri kuhusu asilimia 10. Kwenye mchango uliopita hapa ndani, Mbunge wa Makete alisema kwa ufasaha kwamba fedha nyingi za mfuko za asilimia 10 hazirudishwi kwenye Halmashauri zetu. Ninayo maoni kwamba, utaratibu huu wa kutoa fedha kwenye vikundi pengine hauwezi kuwa na ufanisi sana. Nilikuwa napendekeza, hivi sasa wako wananchi wengi binafsi wenye uwezo wa kuwa na mawazo ya biashara, wanaoweza kubuni mradi, na kadhalika, badala ya kuendelea kutoa fedha kwenye vikundi vya watu watano hadi kumi, tungeruhusu hizi fedha akopeshwe mtu mmoja mmoja ambaye ana wazo zuri la biashara. Ninaamini mtu mmoja mwenye wazo zuri la biashara anaweza kuajiri hata watu 100 kuliko watu kwenye vikundi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunayo historia katika nchi hii, hizi biashara za watu wengi zimeshindikana huko nyuma. Tulikuwa na mashamba ya vijiji, tulishindwa kuyaendesha; tulikuwa na matrekta ya vijiji, tulishindwa kuyaendesha. Biashara ya watu wengi ni ngumu sana kufuatilia. Kwa hiyo, napendekeza tubadili sheria, tuanze kutoa mikopo kwa mtu mmoja mmoja mwenye ujuzi au mwenye mradi mzuri ilimradi tu ana sifa za kupewa mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale mwanzo palikuwa na hofu kwamba, kuwafuatilia itakuwa ni vigumu. Dunia inakwenda mbele. Sasa hivi tupo kwenye mchakato wa kuandikisha anuani za makazi. Wananchi wetu wana vitambulisho vya NIDA vya Taifa. Watu hawa wanajulikana waliko, tuwaamini, tuwakopeshe waweze kufanya maendeleo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye taarifa za Kamati ya Katiba na Sheria pamoja na Kamati ya Sheria Ndogo.

Kwanza na mimi niungane na Wajumbe wenzangu ambao wameshachangia, kuwapongeza sana Wenyeviti wa Kamati hizi zote mbili kwa kazi nzuri ambayo wamefanya kuwasilisha hizi mada ndani ya Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili niseme pia kwamba ninaunga mkono maazimio yote ya Kamati zote mbili ambazo Wenyeviti wamewasilisha ndani ya Bunge lako tukufu. Mimi nitachangia maeneo yote mawili, nikianza na sehemu ya Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu asubuhi tumesikia ndani ya Bunge lako tukufu Wabunge wengi ambao wamechangia hapa wameonesha dosari mbalimbali kwenye sheria ndogo ambazo nyingi zinatungwa na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa, Wizara mbalimbali na mamlaka mbalimbali za nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tumesema hapa ndani, mamlaka ya kutunga sheria zote za nchi hii ni kazi ya Bunge na Katiba imesema vizuri sana, imesema mamlaka yote, imetumia neno yote kwa maana kwamba Bunge hili ndio lenye mamlaka ya utunzi wa sheria zote za nchi hii. Kwa hiyo, hata kama kuna sheria ndogo kwenye Manispaa, kwenye Majiji au kwenye Halmashauri, kama inaumiza watu maana yake Bunge hili tunawajibika kuirekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake nini? Wajumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo kwenye Taarifa ya Kamati hapa, imetolewa wazi kwamba yako maazimio ya Bunge yaliyotolewa ya Mkutano wa Sita na wa Saba, lakini mpaka leo hayajatekelezwa na sheria hizi bado ziko mtaani.

Nilikuwa naomba kutoa rai, kama ambavyo Wabunge wamesema kwamba kwa sababu mamlaka ya utunzi wa sheria hizi ni kazi ya Bunge haitegemewi mamlaka nyingine yoyote ya Serikali au Halmashauri zetu za Mitaa kuendelea kupuuza maazimio ya Bunge hili ambayo sisi tumeazimia mambo yafanyiwe marekebisho, na tukiruhusu hili Bunge hili tutakuwa hatufanyi wajibu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili ambalo naomba kuchangia hapa, napenda kusema kwamba pia sisi kama Bunge tunapotunga sheria mbalimbali kwa ajili ya nchi yetu tunaunga mkono kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais anaifanya kwa ajili ya nchi yetu. Rais wetu tangu ameingia madarakani kati ya maeneo muhimu anayofanyia kazi ni kurekebisha mifumo ya sheria ili watu wetu wapate uhuru zaidi, ili watu wetu waishi kwa amani katika maeneo yao. Na Mheshimiwa Rais juzi wakati anaongea na Tume ya Kurekebisha Haki Jinai aliongea maneno yafuatayo na naomba kumnukuu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Rais amesema; “Hakuna kitu kibaya kukichepusha duniani kama kuchepusha haki ya mtu.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais anaamini kwamba kuchezea haki za wananchi ni kitu kibaya sana, na sisi kama Bunge na mimi kwa maoni yangu ninaamini, haki za wananchi zinaweza kuchepushwa katika maeneo mawili; sehemu ya kwanza zinaweza kuchepushwa na mamlaka ambazo zinasimamia haki za wananchi wetu zikiwemo Mahakama, vyombo vya polisi, TAKUKURU na kadhalika; lakini eneo la pili linaloweza kuchepusha haki za wananchi ni sisi Bunge kutokutunga sheria bora za kusimamia wananchi wetu. (Makofi)

Kwa hiyo, naliomba Bunge lako tukufu tutumie mamlaka yetu vizuri ya kutunga sheria, ziwe na tija, zisaidie kuboresha huduma za wananchi badala ya kuweka ugumu kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, naomba nichangie mahususi kwa ajili ya Law School, kabla sijaenda mbele kwanza ni-declare interest kwamba mimi nimesoma Law School ya Tanzania, na ili kuweka mchango wangu vizuri, mimi nimesoma Law School na nilifaulu katika first sitting, sikufeli kama wanafunzi wale wengine. Nataka huu mchango ukae vizuri, kwa hiyo, ninapochangia kuhusu Law School sichangii kuipaka matope nachangia kwa ajili ya kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu ya Katiba na Sheria, kwenye maoni yao, wameshauri kwamba ili kupata wanafunzi bora wa sheria ni vema kuwe kuna mitihani ya kuingilia kusoma Law School ya Tanzania. Tafsiri yake ni kwamba, wale ambao watafeli mitihani ya kuingia Law School hawatakwenda kusoma Law School.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na azimio hilo, lakini mimi nakwenda mbali zaidi na Waziri wa Katiba yuko hapa ndani, naomba hili jambo alisikie na alifanyie kazi. Wanafunzi wengi wa sheria Tanzania hivi sasa wamekuwa kama watoto yatima, degree za sheria nchini sasa hivi mwanafunzi akikaa darasani miaka minne, miaka mitatu, ni kama hajasoma shule kwa sababu matangazo yote ya Serikali huwezi kupata ajira nchi hii sasa hivi kama hujasoma Law School. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba kusoma Law School Tanzania imekuwa ni jambo la lazima, suala ambalo sio sawa na hii sio haki. Mwanafunzi aliyeuza ng’ombe, ameuza mahindi, amejibana akasoma degree miaka minne, miaka mitatu, unamwambia bila Law School hupati ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naamini kwa kuwa Katiba yetu, Ibara ya 22 inasema kila raia wa Tanzania ana haki ya kufanya kazi katika nchi hii, ninaliomba Bunge lako tukufu na Waziri wa Katiba na Sheria, suala la kusoma Law School liwe ni optional, sio lazima. Sio kila mwanasheria ana mpango wa kuwa wakili kama mimi, sio kila mwanasheria ana mpango wa kuwa kwenye mambo haya. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninampongeza Kaka yangu Mheshimiwa Ulega pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara hii na timu yote ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Nimekwenda kwenye mabanda pale nje kumenoga kweli kweli, kwa kweli Mheshimiwa Waziri umetuthibitishia kwamba hii ni Wizara ya vitoweo, hongereni sana kwa ubunifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia kwenye eneo la sekta hii ya maziwa. Jimbo la Lupembe na Mkoani Njombe kwa ujumla wake huko nyuma tulikuwa na kiwanda kizuri sana cha maziwa, kiwanda hiki cha maziwa kilikuwa kinatoa ajira nyingi kwa wananchi wetu, kilikuwa kinatoa kodi kwa Serikali na kadhalika, lakini kiwanda hiki ambacho kilikuwa ni msaada mkubwa kwenye kuchakata mazao ya mifugo leo hii kimefungwa. Mkoa wa Njombe tangu wakati wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kule Makete ranch ya Kitulo kulishakuwa na ranch nzuri kwa ajili ya mifugo na Mheshimiwa Waziri anajua, ranch hii ya Kitulo ilikuwa ni kwa ajili ya kunenepesha ng’ombe tulikuwa na ng’ombe wakitoa maziwa mpaka lita 40 kwa siku, ranch hii imeendelea kushuka imeendelea kuwa haina tija kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu amekuja kuipa nguvu sekta hii ni vizuri akaenda Mkoani Njombe akasaidie kufufua kiwanda cha maziwa kilichoko Njombe, Serikali kupitia Waziri kwa sababu mnayo nia njema ya kupeleka mbele sekta hii ya mifugo na uvuvi ninaamini kiwanda hiki ambacho kinapigwa danadana, kimejawa na mambo mengi, wataalam wako Mheshimiwa Waziri ukiwauliza wanajua, ukifia Njombe utakuja kukikwamua kiwanda hiki ambacho kipo na mitambo ipo, badala ya kupanga mambo mapya ningeomba bidhaa tulizonazo, vifaa tulivyonavyo tukaboreshe vianze kutoa ajira kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nataka nitumie nafasi hii pia kupitia wewe nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake njema ya kuboresha sekta ya mifugo na uvuvi. Halmashauri ya Njombe kwa mara ya kwanza Halmashauri ya Njombe DC tumepata mradi wa mabwawa manne ya kufuga Samaki, huu ni mpango ambao sekta hii ya uvuvi na mifugo imeamua kwenda mbele na kuboresha maisha ya wananchi wetu. Nikuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu umeanza vizuri, utakapokuja Njombe utembelee mabwawa haya ili uone pia namna ya kuongeza fedha na kuongeza tija kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la lingine ninataka pia niseme kuhusu mifugo kwamba ni kero. Nakubaliana na Waziri kwamba mifugo ni utajiri, mifugo ni uchumi lakini mifugo pia ni kero. Zipo kero tatu kwenye mifugo, kero ya kwanza hii mifugo imekuwa sababu ya ugomvi kati ya wakulima na wafugaji. Jambo la pili, kero kwenye mifugo ni kwamba mifugo imekuwa ni sababu ya ajali mbalimbali barabarani, Wabunge ninyi mnakumbuka Mheshimiwa Kigwangalla yuko hapa alipata ajali kwa kugongana na mifugo barabarani, Mheshimiwa Waziri ujumbe wangu ni nini, tunakuomba uibadili sekta hii ya mifugo…

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Mwita Getere.

TAARIFA

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba mifugo siyo kero, ila wanaotunza mifugo hiyo ndiyo wana kero, kwa hiyo watu waelimishwe tu kwamba mifugo haina akili watu ndiyo wanaitumia.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Edwin Swalle unaipokea hiyo taarifa?

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa heshima ya Mheshimiwa Getere ninachosema ni kwamba Mheshimiwa Waziri ninakuomba uifanye sekta hii kuwa na utulivu tusiache mifugo iendelee kurandaranda kila mahali, leo hapa Dodoma kwa mfano ukiingia katikati ya mji mchana unaweza kuona ng’ombe, hata ukiingia Dar es Salaam unaweza ukaona mbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni nini? Kwa kuwa Serikali yako maeneo mengi tumepanga maeneo kwa ajili ya majumba ya makazi, yako maeneo kwa ajili ya mahoteli, ninayo imani kwamba Mheshimiwa Waziri mnaweza kupanga vizuri maeneo kwa ajili ya malisho na maeneo kwa ajili ya wakulima. Jambo hili Mheshimiwa Waziri linawezekana kwa dhamira njema ambayo unaweza kuwa nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia jambo lingine kwamba mwaka huu kwenye mbio zetu za Mwenge, kauli mbiu za mbio za Mwenge mwaka huu 2023 zinasema;

“Tutunze mazingira, tuokoe vyanzo vya maji, kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa Taifa”. Kauli mbiu hii ya kutunza mazingira inaendana na kudhibiti uzuraraji wa mazao ya mifugo, kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri ujitahidi kuweka mpango mzuri ili kusimamia sekta hii ya Mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu na hili ni muhimu sana, nimesoma kwenye taarifa ya Waziri hapa amesema namna sekta ya mifugo na uvuvi inavyochangia uchumi wa Taifa. Mifugo inachangia uchumi kwa asilimia Saba na lengo la Serikali na Waziri na timu yake yote ninaamini tunataka kulikamata soko la Kimataifa, lakini nitoe wito kwenye Wizara hii kwamba soko la Kimataifa lina vigezo vya kuuza bidhaa za wanyama duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya vigezo hivyo ni kuwatambua wanyama hawa kuwasajili na kujua hawa wanyama ni mali ya nani, huwezi kupeleka biashara kwenye soko la Kimataifa bila kujua mmiliki ni nani kwa usajili alionao. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri umesema kwenye taarifa kwamba mlikuwa na mpango wa kuwatambua wanyama na mpango huu umesimamishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwako mnaweza kukaa kwenye Wizara yenu kama gharama ni kubwa ya kulipia usajili na utambuziwa wa Wanyama, mnaweza kama Serikali kusaidia kama ambavyo tumefanya kwenye sekta yetu ya kilimo, mkatoa ruzuku kwa kiasi fulani ili mkulima alipe bei kidogo. Kwa hiyo, kama ni 1,500 Serikali mnaweza kutoa ruzuku shilingi 1000 na huyu mfugaji akatoa 500 au 300, lakini ni lazima mifugo yetu itambuliwe, ifanyiwe ufuatiliaji ili soko la Kimataifa liweze kutuelewa kwamba tuna sifa ya kuingia kwenye soko la Dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine nataka niseme kidogo kuhusu mpango wa mbele wa kutoa elimu ya ufugaji. Hivi karibuni kumekuwa kuna mpango wa Serikali wa kujenga vyuo vya VETA nchini, vyuo vya VETA ni kutoa ufundi na ujuzi kwa wananchi, ninataka nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Wizara yake kwamba washirikiane na Wizara hii ya Elimu na Sayansi vyuo hivi vya VETA kwenye maeneo mengine ni Mikoa ya wakulima, Jimbo la Lupembe kwa mfano tumepata chuo cha VETA kile chuo ni muhimu kikawa chuo pia cha mifugo na uvuvi ili wananchi wetu wasome habari ya umeme, wasome habari ya ujenzi lakini pia wasome na kilimo kwa sababu kilimo ndiyo shughuli yao ya kila siku kwenye maeneo yale, tukifanya hivyo vyuo hivi vitakuwa na tija kwenye kila eneo ambako vipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine pia kwa kumalizia nitumie nafasi hii kumsihi sana Mheshimiwa Waziri wetu wa Mifugo na Uvuvi, kwamba ubunifu alioanza kuufanya leo kwa kutuonesha kwa vitendo uzuri na ubora wa Wizara hii uigwe na Wizara nyingine huko mbele ambako tunakwenda, ubunifi huu Mheshimiwa Waziri ndiyo kitu pekee ambacho kitakupeleka mbele na ktoa tija kwenye sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo nashukuru sana, naunga mkono hoja.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu sana ya Kilimo. Kwa niaba ya wananchi wa Lupembe na Mkoa wa Njombe kwa ujumla nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa sana ambayo anafanya kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo wa Waswahili unasema, mzigo mzito mpe Mnyamwezi. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais, katika Awamu hii ya Sita amempata Mnyamwezi Waziri wa Kilimo, kaubeba huu mzigo. Mheshimiwa Bashe hongera sana, unafanya kazi nzuri, umetoa matumaini kwa Watanzania, na Bunge tunakuunga mkono. (Makofi)

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuja kwenye Bunge hili la bajeti, nilikuwa ziara jimboni. Wananchi wa Jimbo la Lupembe kwa upekee walinituma nipeleke salamu za pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kuwapelekea mbolea ya ruzuku na wananchi wa Jimbo la Lupembe wameitikia vizuri sana mpango huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Lupembe ni kati ya majimbo ya mfano ambapo wananchi wetu wamelima vizuri na kuna mazao ya kutosha. Kama kuna Mbunge hapa kwao hakuna chakula, waje Lupembe chakula kipo kingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, wananchi wa Lupembe pia walinituma kumwambia Mheshimiwa Waziri mambo yafuatayo: Jambo la kwanza, mpango wa mbolea yetu ya ruzuku umekuwa ni mzuri lakini umeibua changamoto kadhaa. Changamoto ya kwanza kubwa ambayo imeibuka na pembejeo za ruzuku ni vituo vya wakala kuwa vichache…

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wangu wa Jimbo la Lupembe…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Enosy kuna taarifa kutoka Mheshimiwa Almas Maige.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

TAARIFA

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, anayechangia hoja ameongelea ile methali ya kizamani, “Mzigo mzito, mpe Mnyamwezi.” Sisi Wanyamwezi tunapeleka jambo hili kwenye Baraza la Kiswahili ili isemekane “mzigo mzito, punguza, beba mwenyewe.”

MWENYEKITI: Mheshimiwa Enosy taarifa unaipokea.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kazi nzuri ambayo anaifanya Mheshimiwa Bashe, siipokei taarifa hiyo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Wananchi wa Lupembe wamepata shida sana kwenye kupata hizi pembejeo. Yako maeneo wananchi wetu walikuwa wanaamka saa tisa mpaka saa kumi, wanakwenda zaidi ya mara mbili hawapati mbolea, kwa sababu zilikuwa chache na vituo ni vichache. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, kati ya mambo wananchi wetu wanatamani kusikia ni mpango tulionao kwenye msimu wa kilimo ambao unafuata sasa hivi, Serikali imejipangaje kuongeza mawakala wawe karibu na wakulima wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, pamoja na kuongeza wingi wa mawakala, hizi mbolea pia zilikuwa hazipatikani sana, hasa mbolea kama ya Urea na CAN. Wananchi wetu wa Mkoa wa Njombe wameteseka sana. Tungetamani kumsikia Mheshimiwa Waziri aliambie Bunge na nchi kwa ujumla, watu wa kilimo wamejipangaje kupanua wigo wa kupatikana hizi mbolea kwa wingi na kwa wakati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo wananchi wa Lupembe walinituma kulisema kwa Mheshimiwa Rais ni kwamba hizi mbolea za ruzuku kabla ya kuja ruzuku, wananchi wetu sio wote wenye uwezo wa kununua hizi mbolea za kilo 50 kwa Shilingi 70,000/=. Wapo wananchi wengine wamekuwa wakinunua mbolea kwa kupima kwenye kilo na kadhalika. Ushauri wangu kwa Serikali, tunaomba hizi mbolea pia waweke na kilo kama 25 ama 20 ili hata wenye kipato cha chini wamudu kununua hizi mbolea kwa ajili ya maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, amelisema Waziri kwenye hotuba yake naomba nilirudie. Waziri wetu amekuwa ni sauti halisi ya wakulima wa Tanzania, na amesema hapa kwenye hotuba yake vizuri sana. Anasema, “mazao mengi yamekufa nchini kutokana na kushindwa kuwalinda wakulima.” Nataka nikubaliane na Mheshimiwa Waziri kwamba mazao mengi ya kimkakati yameporomoka na mengine kufa, kwa sababu wakulima wetu walikosa mtu wa kuwasemea na kuwalinda kwenye soko lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wananchi wetu maeneo mengi ikiwemo Jimbo la Lupembe wana madai makubwa na wafanyabiashara kwenye mazao yao. Vipo viwanda vingi, wapo wafanyabiashara wanawakopa wakulima, hawawalipi kwa wakati. Jambo hili nitaomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kufunga kwenye bajeti yake atoe tamko la kitaifa juu ya msimamo wa Serikali kwa wafanyabiashara na mawakala wanaowakopa wakulima halafu hawalipi. Wao wanavaa suti, wanabadili magari, lakini wakulima wanaendelea kuwa masikini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Lupembe na Mkoa wa Njombe, yuko mfanyabiashara mmoja wa parachichi anaitwa Olivado, amewakopa wakulima kila mahali. Olivado amekuwa ni tatizo. Zao la parachichi ambalo Mkoa wa Njombe kwa sasa ni zao kubwa sana, lakini wananchi wameanza kukata tamaa kwa sababu wakichuma haya mazao yao hawalipwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, zao kama la parachichi tunaomba Serikali itoe bei elekezi. Wananchi wetu wananunua parachichi, wanauza kwa bei ambazo hazieleweki. Kuna msimu wanauza shilingi 300, kuna msimu shilingi 600, shilingi 1,500 na kadhalika. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa ameanza vizuri, atusaidie kuweka mwelekeo wa Serikali, bei elekezi ya mazao haya muhimu ya wakulima ni nini? Kwa sababu zao la parachichi linachangia sana uchumi na kodi ya nchi yetu kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nataka pia nimwombe Mheshimiwa Waziri, sisi Jimbo la Lupembe na Mkoa wa Njombe, tunayo maeneo mengi, nasi Lupembe tunalo eneo kubwa tumetenga zaidi ya ekari 89,000. Tuko tayari kama Serikali iko tayari, ikafungue kitalu cha mbegu bora kwa ajili ya kilimo. Ardhi ipo, na wakulima wetu wako tayari. Tunaomba utayari wa Serikali tufanye kazi. Nasi Mkoa wa Njombe ni kati ya mikoa ambayo inafanya vizuri sana kwenye kilimo, na ikimpendeza Mheshimiwa Waziri, afanye Mkoa wa Njombe kuwa Mkoa bora wa kilimo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho na siyo kwa umuhimu, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aendelee kupokea maoni ya Wabunge, tutamsaidia kufika mbali sana kwenye hii Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba hii muhimu sana ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Lupembe kwanza nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anafanya kwa ajili ya nchi yetu na kupeleka maendeleo sehemu mbalimbali za nchi yetu ya Tanzania. Kwa sababu ni wazi kwamba sekta nyingi Mheshimiwa Rais anaendelea kuzifungua na hata Jimbo la Lupembe ambalo mimi ndiye Mbunge wake Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana kwenye maeneo ya TARURA na maeneo ya afya na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo hili la barabara, naomba niseme wazi pamoja na Mheshimiwa Waziri kuwasilisha bajeti yake vizuri sana hapa Bungeni leo, nimesoma hotuba nzima ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri kwa wananchi wa Jimbo la Lupembe kuhusu barabara ya Kibena - Stop Lupembe - Lupembe - Madeke. Naomba niseme wazi kwamba sitaunga mkono bajeti hii kwa siku ya leo na kama nitaunga mkono wananchi wangu wa Lupembe hawawezi kunielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya kwa sababu gani? Sababu ya kwanza nimesoma kwenye hotuba hii ya bajeti ukurasa wa 27 wa hotuba hii unasema kwamba barabara ya kutoka Kibena - Stop Lupembe - Madeke - Ifakara kilometa 270 Serikali inasubiri fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili ya kufanya usanifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi katika ukurasa wa 73 – 74 barabara hii ya Kibena – Lupembe - Madeke ilishaahidiwa ipo namba 22 pale inasubiri kuanza ujenzi wa kiwango cha lami. Maana yake ni kwamba wenzetu Wizarani hata Ilani ya Chama cha Mapinduzi hawajasoma wanapoandaa bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sababu ya pili ambayo napenda kusema hapa nimesoma kwenye vitabu vya bajeti mwaka jana Bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali ilitenga shilingi bilioni mbili na niliongea ndani ya Bunge hili kwa ajili ya barabara hii kwamba hii bajeti ilikuwa ni kidogo sana. Mwaka huu wameongeza mpaka shilingi bilioni tano, lakini siyo ya kuanza ujenzi wanazungumza kuendelea ku-mobilize na kutafuta mkandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ya Lupembe imeahidiwa tangu Serikali ya Awamu ya Tatu ya Mheshimiwa Mkapa, imeahidiwa Awamu ya Nne Mheshimiwa Jakaya Kikwete, Awamu ya Tano na bahati nzuri hata Rais wetu akiwa Makamu wa Rais amekuja Lupembe eneo la ujenzi mara mbili amewaahidi wananchi wetu kwamba barabara hii usanifu umeshakamilika inaanza ujenzi. Sasa leo kwenye bajeti hii mwaka wa sita sasa tunazungumza kuendelea kuwa na ahadi ya kutafuta fedha kwa ajili ya mkandarasi na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufunga bajeti yake hii, ili mimi niweze kubadili msimamo wangu wa kuunga mkono hii bajeti au laa, atoe ufafanuzi kwa wananchi wa Lupembe ni lini barabara hii ya Kibena – Lupembe – Madeke inaanza ujenzi? Kwa sababu usanifu ulikamilika tangu mwaka 2014. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, namuomba sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu hii barabara ina ahadi kubwa za Serikali na viongozi wakubwa wa Serikali, namuomba Mheshimiwa Waziri baada ya bajeti yake hii tuondoke mimi na yeye mgugu kwa mguu mpaka Lupembe akawaambie wananchi barabara hii inaanza ujenzi lini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, hii barabara kama ambavyo nimesema imefanyiwa usanifu tangu mwaka 2014 na wananchi wa maeneo ya Nyombo, maeneo ya Kidegembye, Matembwe, Lupembe Barazani, Igombora, Mfilige mpaka Madeke nyumba zao zimewekwa alama za “X” mpaka leo wanasubiri uamuzi wa Serikari. Hawaendelezi wanasubiri Serikali ichukue uamuzi wa kuanza ujenzi wa hii barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inapochukua muda mrefu wananchi hao hawajui sasa wafanye lipi, nyumba zao zina alama ya “X”, hawawezi kuziendeleza. Sasa mimi naiomba Serikali ni vizuri tukajua kwamba tunapokuwa tumewaahidi wananchi wetu kutekeleza baadhi ya masuala yanakuwa na athari kwa wananchi wetu pia. Kwa hiyo, naomba pia kauli ya Mheshimiwa Waziri aseme wananchi hawa ambao nyumba zao zina alama ya “X” tangu mwaka 2014 wanapewa matumaini gani leo zaidi ya miaka 10 sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea mara nyingi ndani ya Bunge lako tukufu. Barabara hii ya Kibena – Madeke ni barabara inayounganisha kati ya Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Morogoro na kwenye sera yetu ya ujenzi wa barabara na Waziri anajua vizuri sana, kama nchi tulikubaliana kwamba barabara za mkoa mmoja na mkoa mwingine ni kipaumbele namba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini barabara hii inaunganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Morogoro. Mkoa wa Morogoro unazalisha mpunga mzuri sana katika nchi hii; Mkoa wa Njombe na eneo la Lupembe mathalani kuna viwanda vikubwa vya chai maeneo haya vinaiingizia Serikali fedha za kigeni, lakini barabara hii wakati wa masika mvua ikinyesha siku mbili magari hayatembei, abiria hawatembei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tupo karne ya 21 wananchi wangu wa Jimbo la Lupembe wakitoka kwenye vijiji mbalimbali kwenye hili Jimbo kufika Njombe Mjini kama wanasafari ya kwenda nje ya Mkoa wa Njombe lazima wabadilishe nguo kwa sababu zinakuwa zimechafuka sana. Katika karne ya 21 hatuwezi kuwa na sehemu ya nchi ambayo ina hali kama hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali na Mheshimiwa Waziri, tumeshauri mara nyingi hapa badala ya kuendelea kupanua maeneo mengine kwa sababu nimesoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ipo mipango ya Serikali baadhi ya maeneo tunapanua upana wa barabara, yapo baadhi ya maeneo tunaunganisha barabara za Wilaya na Wilaya lakini barabara za Mikoa na Mikoa hatujamaliza kwa mujibu wa sera ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali sana barabara hii ya Kibena – Madeke mpaka Morogoro ipewe kipaumbele ili na wananchi wangu wa Lupembe wajisikie kwamba na wao ni sehemu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo napenda kuchangia ni kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege Mkoani Njombe. Kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi pia chama changu kimeahidi vizuri kwamba Mkoa wa Njombe kutokana na hali ya uchumi wake kuwa mkubwa na kuwa na mazao mengi ya biashara ikiwemo parachichi na mazao mengine ya kilimo, lakini pia kutokana na kuwa na hazina kubwa ya Mgodi wa Mchuchuma Naliganga kule Ludewa, Mkoa wa Njombe ni kati ya Mikoa muhimu sana katika nchi hii. Ikiwekewa vipaumbele vya Kiserikali inaweza kuwa ni sehemu ya kuinua uchumi wa Taifa letu. Na kwa maana hiyo Serikali iliona umuhimu mkubwa wa kuahidi kwenye Ilani kwamba uwanja wa Njombe utafanyiwa usanifu ili ujenzi wa uwanja wa ndege uweze kufanyika pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kwenye hotuba sijaona mahali popote ambako jambo hili limeahidiwa na huu ni mwaka wa pili tunazidi kwenda mbele. Namuomba Mheshimiwa Waziri pamoja na kazi nzuri ambazo mnafanya kwenye Wizara hii, tumeshauri kwenye mpango wa Serikali, tunapopanga vipaumbele vya Serikali ni lazima tufungamanishe sekta mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ya uchukuzi na usafirishaji ni lazima ifungamanishwe na sekta ya kilimo. Sasa kama kwenye mikoa ambayo kuna kilimo kikubwa miundombinu haipewi kipaumbele, hatuwezi kukuza uchumi wa nchi yetu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi ndugu naomba niseme kwamba siungi mkono hoja, nitaunga baada ya kupata ufafanuzi ambao nimetoa pale mwanzoni, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba hii muhimu sana ya bajeti yetu ya fedha kwa ajili ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake yote kwa kazi nzuri waliyofanya kwenye kuandaa Bajeti hii ya Serikali. Hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri ambayo ni Bajeti ya Mheshimiwa Rais ya mara ya pili kwenye Bunge lako Tukufu ni ya kihistoria ni hotuba ya kimapinduzi makubwa na uzalendo mkubwa sana kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma hotuba yote, ukurasa kwa ukurasa. Kimsingi bajeti hii imejikita katika mambo yafuatayo; kwanza ni bajeti ambayo imekusudia kuinua kilimo na kumwinua mkulima wa Tanzania. Pili, hii ni bajeti ambayo imekusudia kuhimiza sekta binafsi na biashara pamoja na wajasiriamali wa nchi. Hii ni bajeti ya kihistoria kwa sababu pia imekusudia kukuza ajira nchini; ni hotuba ya kihistoria kwa sababu imekusudia kutoa tija na motisha kwa wafanyakazi wa nchi yetu ya Tanzania; pia ni hotuba ya kihistoria kwa sababu imedhamiria kuboresha huduma za kijamii zikiwemo, afya, maji, elimu, barabara, utalii na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba hii imepokelewa vizuri sana na Watanzania wote nchini kote. Nampongezz Waziri kwani kwenye hotuba hii amedhihirisha wazi kwamba alichukua muda kujiandaa na kufanya utafiti, hongera sana. Pamoja na uzuri wa hotuba hii ya Waziri wa Fedha naomba ninukuu maneno ya Makamu wetu wa CCM Taifa, Comrade Kanali Abdulrahman Kinana aliyoyasema wakati akishiriki sherehe za Iftar tarehe 23 Aprili, 2022 kwenye kuadhimisha miaka 18 ya Kampuni ya Usafirishaji (Silent Ocean Company).

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kinana anasema hivi, “nataka vikao vizae matunda. Nchi hii imeharibiwa na “vikao,” nchi hii imeharibiwa na “mchakato,” nchi hii imeharibiwa na “tutafanyia kazi,” nchi hii imeharibiwa na “tupeni muda,” nchi imeharibiwa na “tutasikiliza,” nchi hii imeharibiwa na “tutakwenda kutatua kero.” Makamu wa CCM anasema yote tumesikia, tunataka vitendo. Huyu ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa uzuri wa hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri kwa kutembea kwenye maneno ya Kiongozi wetu wa CCM Taifa ni kwamba, hotuba hii ni nzuri sana, imejaa mapinduzi makubwa, imejaa uzalendo mkubwa, lakini haitakuwa na maana kama haya ambayo yamesemwa hayatakwenda kwenye maneno hayo ambayo Makamu wa CCM anasema, tusiendelee kusema “mchakato unaendelea, tunakwenda kufanyia kazi.” Tunakuomba Mheshimiwa Waziri, hotuba hii ikatekelezwe ili ionekane wazi kwamba tumetafsiri kwa vitendo maono ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na sehemu ya kilimo. Kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, ukisoma kwenye ukurasa wetu wa 29 utaona wazi kwamba Mheshimiwa Rais anatembea kwenye Ilani ya CCM. Ukurasa wa 29 ile sehemu ya kwanza inasema katika miaka mitano ijayo CCM itaielekeza Serikali kuongeza fursa za ajira katika sekta rasmi na isiyo rasmi zisizopungua milioni saba kwa kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani yetu inasema kuchochea ukuaji wa uchumi hususan katika sekta ya viwanda vinavyotumia malighafi za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, maliasili na sekta ya huduma za kiuchumi ikiwemo utalii. Tumemwona Mheshimiwa Rais akitekeleza maono haya ya Ilani ya CCM kwa vitendo. Rais wetu kwenye sehemu hii ya kilimo kwenye hii bajeti yetu ameongeza zaidi ya shilingi bilioni 700 kwenye kilimo. Kwenye sekta ya Utalii peke yake Rais wetu amezunguka nchi mbalimbali akitangaza Royal Tour ambayo sasa imeanza kuzaa matunda makubwa kwa ajili ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa upande wa ajira, kwa mara ya kwanza kwa miaka mitano iliyopita Mheshimiwa Rais wetu ametoa ajira kwa vijana wetu zaidi ya 30,000 katika mwaka huu wa fedha. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba Mheshimiwa Rais amedhamiria kuboresha huduma mbalimbali kwa mujibu wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. Kwenye maneno haya ambayo nimesema kwamba tunaomba vitendo, naomba Mheshimiwa Waziri, kwenye hotuba yako amependekeza maeneo mbalimbali ya kuwabana watumishi na kufuatilia kodi na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo ambayo yako chini ya uwezo wetu kama Serikali ambayo tunaweza kuongeza mapato. Kwa mfano, wananchi wa Jimbo la Lupembe kwa mfano, wana Kiwanda cha Chai ambacho Serikali imekitelekeza kwa muda mrefu. Nimekuwa naongea mara nyingi humu ndani nikisema kwamba Kiwanda hiki kama Serikali ingekuwa na nia thabiti ingeweza kuingiza fedha nyingi sana kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimemwambia Waziri juzi kwa barua, kwamba kwenye Wizara yako Mheshimiwa Waziri kuna jambo limekwama kuhusu Kiwanda Lupembe. Naibu Msajili au Msajili wa Hazina amekalia maamuzi ya Mahakama yanayomtaka atekeleze uamuzi wa Mahakama wa kumtaka Mwekezaji wa Kiwanda cha Lupembe Do Mecan TYRE aweze kuachilia kile kiwanda ili Serikali iweze kuendelea.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Naunga mkono hoja ya Serikali. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichangie wasilisho la Waziri kwenye hii Finance Bill.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitumie nafasi hii tena kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa namna ambavyo amejielekeza kuhakikisha kwamba anapanua wigo mkubwa wa walipa kodi.

Mimi niseme kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Lupembe spirit ya kuhamasisha Watanzania kulipa kodi ni jambo la msingi sana. Kwa kweli Waziri katika eneo ambalo amelifanya vizuri ni kutoa hamasa kubwa kwa wananchi kuona kulipa kodi ni fahari na kulipa kodi ya nchi ni kujiletea maendeleo wenyewe. Mheshimiwa Waziri alisema kwenye hotuba yake kwamba ni bora kuwa unpopular, lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Waziri kwa mipango hii mizuri ya kutanua wigo wa kodi wananchi watakavyoona mafanikio makubwa kwenye sekta mbalimbali atakuwa popular badala ya kuwa unpopular. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi, ninalo jambo moja ambalo napenda kuchangia kwenye Muswada huu. Tumezungumza ndani ya Bunge hili kwamba kati ya sekta ambayo nchi yetu haifanyi vizuri ni sekta ya kilimo. Sekta hii ya kilimo kwa muda mrefu imekuwa ikitengewa bajeti kidogo sana na hata katika mipango ya Serikali tulisema ndani ya Bunge hili kwamba pengine katika miaka hii mitano tujaribu kuiinua na kuikuza zaidi sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi katika hii Finance Bill ninayo concern moja kwenye issue inayohusu Withholding Tax kwenye mazao ya kilimo. Sisi kule Jimbo la Lupembe kwa mfano tunao wakulima wadogo wadogo kwa asilimia 95, wengi wanalima mazao ya chai, maharagwe, mihogo, matunda na miti ya mbao na wanauza mazao haya kwa watu binafsi kwa maana mtu mmoja mmoja na wananchi wengi wa aina hii hawapo kwenye AMCOS. Withholding Tax kwa ufahamu wangu hii ni Income Tax ni kodi, lakini tu mode ya kuikusanya inakusanywa kama Withholding Tax kwamba amishna wa TRA anamwambia agent kwamba kusanya kodi kwa niaba yangu kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mambo machache ya kuzungumza, jambo la kwanza, ukisoma kwenye mapendekezo haya bila shaka huyu withholding agent atahitaji kupeleka TRA statement inayoonyesha jina na TIN la huyu ambaye anatakiwa kukatwa hii Withholding Tax, wananchi wa kule vijijini hawana TIN Number za biashara. Nikisoma huu Muswada sioni namna ambavyo Wizara imejipanga kwamba ni kwa namna gani wakulima wadogo wote watakuwa identified kwenye TIN Number ili watambulike kwamba wamekatwa Withholding Tax, hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, kwa mujibu wa taratibu zetu za kodi zilivyo mtu anayepaswa kulipa Income Tax ni lazima awe na turnover ya four million per year. Wakulima wadogo wadogo walio wengi hawawezi kufika turnover hiyo kwa mwaka, maana yake walipaswa kwenda ku-recover pesa ambayo walikatwa kwenye Withholding Tax, Kamishna wa TRA atawa-identify vipi kwamba kodi hii ilikatwa kwa fulani na siyo kwa fulani. Kwa hiyo, kwenye jambo hili la Withholding Tax naona kama kuna ukakasi mkubwa sana jinsi ya kwenda kulitekeleza na litakwenda kuleta matatizo makubwa kwa wakulima wetu wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nataka niishauri Serikali na kwa sababu bajeti hii inaanza kutekelezwa mwezi Julai, kwa vyovyote vile TRA sina uhakika kama wamendaa mazingira mazuri ya kutekeleza jambo hili kwa ufanisi unaotakiwa. Pamoja na nia njema ya kutanua wigo wa kodi kwamba watu wengi wachangie kwenye mapato ya Serikali kwenye mazao haya ya kilimo hasa kwa wakulima wadogo ambao wengi wao hawana TIN Number na kwa kweli wanauza mazao kwa kubangaiza, naomba sana kwenye utaratibu huu wa kutanua wigo wa kodi wasiwemo au la wadau mbalimbali wapewe muda wa kutoa maoni yao ili Serikali itafute njia bora zaidi ya kusimamia hawa withholding agent ni jinsi gani kodi hii itaweza ikakusanywa. Hofu yangu mimi ni kwamba inawezekana withholding agent wakaenda kwa wakulima waka-withhold hii tax, lakini wasiweze ku-remit TRA kwa sababu mazingira ya kuwa-monitor na ku-verify kodi hii wamemkata nani na ataidai vipi yakawa ni magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mchango wangu huo naiomba sana Serikali kwa kuwa tumekusudia kuinua mazao ya kilimo na kuinua kilimo nchini hebu tujikite zaidi kuboresha kilimo chenyewe badala ya kuanza ku-impose kodi kwa wakulima wetu hawa wadogo. Nina uhakika wananchi wadogo kama kule kwangu wakulima wa chai, mahindi na mbao kodi hii itakwenda kuwaathiri sana kwa sababu ni wakulima wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huu, nasema ahsante sana. (Makofi)