Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Haji Makame Mlenge (7 total)

MHE. HAJI MAKAME MLENGE aliuliza:-

Je, ni lini warithi wa askari E.152 (Makame Haji Kheir) aliyefariki tangu Mwaka 2003 akiwa mtumishi wa Jeshi la Polisi Kituo cha Madema watapewa mafao yake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haji Makame Mlenge Lengelenge, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi Makao Makuu Dodoma na Ofisi ya Polisi Kamisheni ya Polisi Zanzibar hazijapata kumbukumbu za maombi ya mafao wala nyaraka za mirathi kumhusu Askari tajwa hapo juu kutoka kwa msimamizi wa mirathi. Aidha, kwa sasa Jeshi la Polisi Kamisheni ya Zanzibar limeshafanya jitihada ya kufanya mawasilinao na msimamizi wa mirathi ndugu Mlenge Haji Kheir ili kupata nyaraka zinazohusiana na maombi ya malipo ya mafao ya mirathi ya askari huyo ili ziweze kushughulikiwa. Ahsante.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE aliuliza: -

Je, ni lini Kituo cha Polisi cha Chwaka kitapatiwa gari ili kutimiza majukumu yake kwa ufanisi zaidi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Makame Mlenge, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi linatambua uhitaji wa magari katika Kituo cha Polisi cha Chwaka kama nyenzo ya kutendea kazi. Kupitia mkataba wake na Kampuni ya Ashok Leyland Jeshi la Polisi linategemea kupokea magari 369 toka Serikalini. Pindi magari hayo yatakapofika, kipaumbele kitatolewa kwa maeneo yote ya vituo vya polisi ambavyo havina magari kikiwemo pia Kituo cha Polisi Chwaka.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE aliuliza: -

Je, ni kwa nini wafanyabiashara wanaoweka bustani kando ya barabara hulipishwa fedha nyingi na TANROADS na TARURA?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Makame Mlenge Haji, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Tozo kwa Wafanyabiashara wanaoweka bustani kando ya barabara hutozwa kulingana na Mwongozo wa Udhibiti wa Uwekaji Huduma ndani ya eneo la hifadhi ya barabara (Manual for Control of Utilities Installation within the Road Reserve) ambao unatokana na Kanuni ya 3 (1) ya Kanuni za Barabara (Fedha na Ushirikishwaji wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi) za mwaka 2011 zilizotolewa chini ya Sheria ya Barabara, Na.13 ya mwaka 2007. Kulingana na Mwongozo huo Wafanyabiashara wanaoweka Bustani kando ya barabara hutozwa Shilingi 4,639.5 kwa mita ya mraba kwa mwaka. Fedha hizo hupelekwa Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE aliuliza: -

Je, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inashirikiana vipi na Ofisi ya Makamu wa Rais kuweka mazingira mazuri kandokando ya barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Makame Mlenge, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuweka mazingira mazuri kandokando ya barabara, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inashirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuhamasisha utunzaji wa mazingira ya barabara ikiwa ni pamoja na upandaji miti kandokando ya barabara. Aidha, Wizara inaendelea kuzingatia Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na Miongozo ya Usimamizi wa Mazingira katika kutunza mazingira ya barabara.

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia NEMC inaendelea kuzingatia sheria hiyo kwa kuhakikisha miradi ya barabara inafanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (Environmental Impact Assessment) kabla ya ujenzi na kufanyia kazi matokeo ya tathmini hiyo ili kutunza mazingira ikiwemo kuweka mazingira mazuri kandokando ya barabara, ahsante.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza msongamano wa watu wanaofuatilia hati za kusafiria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Makame Mlenge, Mbunge wa Chwaka kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Idara ya Uhamiaji katika kupunguza msongamano wa waombaji wa Hati za kusafiria, imefunga mifumo ya kielektroniki ya utoaji wa hati za kusafiria katika Mikoa yote ya Zanzibar. Ufungwaji wa mifumo hiyo kumeondosha msongamano kwa wananchi katika Ofisi Kuu kwani kwa sasa wananchi wanaweza kuomba na kufuatilia maombi ya Hati za kusafiria katika Mkoa wowote anaoishi. Nashukuru.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawalipa fedha zao waathirika wa Benki ya FBME iliyofilisiwa tangu Mei, 2017?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, na kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haji Makame Mlenge, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi mwezi Machi, 2023, Serikali kupitia Bodi ya Bima ya Amana - DIB imelipa jumla ya shilingi bilioni 2.43 kama malipo ya awali ya fidia ya Bima ya Amana kwa wateja 3,446 waliojitokeza wa Benki ya FBME iliyofilisiwa mnamo mwezi Mei, 2017. Malipo ya fedha za ufilisi (liquidation proceeds) kwa wateja wenye amana zaidi ya shilingi 1,500,000 yanayotokana na uuzaji wa mali, makusanyo ya madeni na fedha nyingine za Benki ya FBME yatafanyika baada ya Mahakama ya Cyprus kutoa uamuzi kuhusu pingamizi lililowekwa na Benki Kuu ya Cyprus la kuitambua DIB kama Mfilisi wa benki yote ikijumuisha Makao Makuu pamoja na tawi la Cyprus.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, uamuzi wa Mahakama unatarajiwa kutolewa ndani ya mwaka huu wa fedha 2022/2023, ahsante.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE aliuliza: -

Je, lini warithi wa Askari E2152 aliyekuwa mtumishi wa Jeshi la Polisi watapewa mafao yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimwa Haji Makame Mlenge, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafao ya warithi wa Askari Polisi E.2152 PC Makame Haji Kheir yameshashughulikiwa na Kamisheni ya Polisi Zanzibar, pamoja na Kamisheni ya Utawala wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu Dodoma. Mnamo tarehe 8 Machi, 2023, maombi hayo yaliwasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango baada ya kukamilika kwa nyaraka zote muhimu zilizokuwa zikihitajika kwa ajili ya malipo ambapo taratibu za uandaaji wa malipo hayo zinaendelea na yanatarajiwa kukamilika ndani ya Mwezi huu Mei ambapo warithi wa Askari huyo watalipwa stahiki zao kwa mujibu wa Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.