Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Timotheo Paul Mnzava (2 total)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:-

Katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 wananchi wa Korogwe waliahidiwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Korogwe - Dindira – Bumbuli.

Je, ni lini ujenzi huo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara ya Korogwe - Dindira hadi Bumbuli inayopita kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya biashara na matunda imeanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa lengo la kujenga kwa kiwango cha lami barabara yote ya Soni – Bumbuli – Dindira - Korogwe yenye urefu wa kilomita 77 ikiwemo sehemu ya Bumbuli - Dindira - Korogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina sehemu ya Soni - Bumbuli yenye urefu wa kilomita 21.7 imekamilika mwezi Juni mwaka 2018. Hivi sasa Serikali ipo katika hatua ya ununuzi wa kumpata mtaalam mshauri wa kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sehemu iliyobaki ya Bumbuli-Dindira-Korogwe yenye urefu wa kilomita 5.3. Kiasi cha shilingi milioni 130 zimetengwa katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya kuanza kazi hiyo. Usanifu utakapokamilika na gharama za ujenzi kujulikana, fedha za ujenzi zitafutwa ili ujenzi wa kiwango cha lami uanze kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:-

Wananchi wa Tarafa ya Mombo wamekuwa na hitaji la kuwa na skimu kubwa ya umwagiliaji katika Bonde la Mto Mkomazi na mara kadhaa viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa ahadi ya kukamilisha jambo hilo.

Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi wa umwagiliaji katika Bonde la Mto Mkomazi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Mnzava Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijiji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 1980 Serikali kupitia na washirika wa maendeleo, yaani Wakala wa Ushirikiano wa Kitaalam wa kimataifa wa Serikali ya Ujerumani (Germany) Agency for Technical Cooperation Limited) ulifanya upembuzi yakinifukwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Mkomazi katika tarafa ya Mombo, Halmashauri ya Korogwe. Hata hivyo taarifa ya upembuzi yakinifu na usanifu zilibaini kuwa ujenzi wa bwawa hilo ungesababisha kuongezeka kwa maji katika Ziwa Manga na kupelekea kuzama kwa Kijiji cha Manga Mikocheni pamoja na mashamba ya wakulima.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hiyo katika mwaka 2014/2015 wataalam wa Ofisi ya Kanda ya Umwagiliaji ya Kilimanjaro walifanya mapitio ya upembuzi yakinifu upya na usanifu wa kina uliofanywa katika eneo hilo kwa lengo la kuepusha uwezekano wa kufurika kwa Ziwa Manga, kuzama kwa Kijiji ca Manga Mikocheni na mashamba ya wakulima kutokana na ujenzi wa bwawa hilo. Mapitio hayo yalibaini uwezekano wa ujenzi wa bwawa na mradi wa umwagiiaji katika eneo hilo bila kuathiri wakazi wa eneo hilo. Mapitio ya usanifu huo yalibaini kuwa ujenzi wa bwawa pekee utagharimu shilingi bilioni 1,543,736,877.

Mheshimiwa Spika, Serikali iko katika mchakato wa kufanya ukaguzi na tathmini ya kina ya miradi yote ya umwagiliaji nchini ili kufanya uhakiki wa eneo la umwagiliaji kwa lengo la kubaini ubora wa miradi, thamani ya fedha, gharama za miradi na mahitaji halisi ya sasa ya kuboresha, kuendeleza na kuongeza miradi mipya ya umwagiliaji. Aidha, baada ya tathmini hiyo Serikali itaendelea kutafuta fedha ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha mabwawa na skimu za umwagiliaji nchini ikiwemo mradi wa umwagiliaji katika Bonde la Mkomazi zinaendelezwa na kuwanufaisha wananchi wa Mombo na taifa kwa ujumla.