Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Timotheo Paul Mnzava (2 total)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Kutokana na muitikio mkubwa wa wananchi wa Tanzania kulima mazao ya kimkakati ili kukuza uchumi wa nchi yetu, upo uwezekano baada ya miaka michache tukaongeza sana uzalishaji kwenye mazao haya. Kwa sasa sehemu kubwa ya mazao haya ya kimkakati soko lake ni nje ya nchi yetu, jambo ambalo linaminya kidogo fursa za ajira, lakini pia soko likiyumba kule, inaleta shida kwa wakulima wetu na kwa uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujua, ni upi sasa mkakati maalum na mahususi wa Serikali kuhakikisha kwamba inawezesha uwekezaji kwenye viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa kwa mazao haya ya kimkakati kama zao la mkonge ili kuwasaidia wananchi wapate uhakika wa masoko na pia kuendelea kutengeneza ajira kwa wananchi wetu wa Tanzania? Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo: -

Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, nilikuwa nae kwenye kampeni za kufufua zao la mkonge Mkoani Tanga kwenye kikao cha wadau na tulifanya ziara kwa pamoja kwa siku tatu mfululizo kupitia mashamba, viwanda, vinavyochakata zao la mkonge. Zao la mkonge ni miongoni mwa mazao yale ya kimkakati, tulianza na matano, tumeongeza mazao mawili kuwa saba na mazao hayo ni mkonge yenyewe pamoja na mchikichi ambao unalimwa sana Mkoani Kigoma na maeneo ya Ukanda wa Pwani. Tunapohamasisha kilimo cha mazao haya na kuyapa hadhi ya mkakati, mazao haya ni mazao yanayolimwa na jamii pana kwenye maeneo yake na mazao haya ndiyo yanayoleta uchumi wa mtu mmoja mmoja kwenye maeneo yanayolimwa, lakini pia hata uchumi wa kitaifa kwa kupata fedha nyingi kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, lakini bado mkakati wa Serikali ni kuhakikisha tunahamasisha kilimo si tu cha mazao haya ya kimkakati pamoja na mazao mengine ya chakula na biashara tunataka pia usalama wa chakula nchini uwepo, watu wapate chakula cha kutosha, lakini pia na mazao haya ya kibiashara yakiwemo haya ya kimkakati na mazao mengine ambayo hatukuyaingiza kwenye mkakati lakini tunatamani mazao haya yalimwe ili wananchi waweze kuuza, wapate uchumi wa kutosha na sisi pia tuwe na uwezo wa kupata fedha.

Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Mbunge anataka kujua mkakati wa kutafuta masoko. Ni kweli mkakati tunao, kila zao tunajua maeneo ambako soko lipo, lakini tunapoupeleka kwenye masoko haya jambo la kwanza ambalo tunalizingatia ni kuongeza thamani ili wakulima wapate faida kubwa na mazao haya tunaposema kuongeza thamani tunakwenda sasa kwenye wito wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa ujenzi wa viwanda ndani ya nchi. (Makofi)

Kwa hiyo, moja kati ya mkakati ambao tunao ni kuhakikisha kwamba tunakaribisha uwekezaji kwa Watanzania na walioko nje ya nchi kuja kuwekeza kwenye viwanda kwa sababu tuna uhakika tuna ardhi ya kutosha, lakini pia malighafi ya mazao hayo tunaweza pia na tuna labour ya kutosha nchini kwa maana ya kwamba tunaweza kutengeneza ajira nyingi kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema.

Mheshimiwa Spika, sasa mkakati huu nilipokuwa ziara ya siku tatu mkoani Tanga tumepita kwenye viwanda na tumeona na kumesikia, sehemu kubwa ya viwanda vingi vinafanya kazi, lakini pia vingine havifanyi kazi kwa sababu ya uchakavu. Tunahitaji kubadilisha teknolojia ili tuwe na teknolojia ambayo sasa inaendelea vizuri.

Pili, viko viwanda ambavyo wawekezaji wamejenga vinakwama kupata masoko mazuri kwa sababu kuna bidhaa zisizokuwa na sifa zinazoingia nchini. Ili kuendeleza uwekezaji huo, moja kati ya jambo kubwa tunalolifanya ni kuhakikisha kwamba tunadhibiti bidhaa za kutoka nje ili kuwezesha uwekezaji wa ndani kukua na kuuletea manufaa makubwa kwa kupata fedha za kutosha na ajira. Hayo yote tunayazingatia ili tuweze kuhakikisha kwamba uwekezaji unakuwepo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani, mpango wetu ni kuhakikisha kwamba tunaongeza hamasa ya ujenzi wa viwanda, lakini pia tunavilinda viwanda vya ndani. Kwa mfano tuliouona kwenye zao la mkonge, tunacho kiwanda kinazalisha nyuzi nchini kupitia zao la mkonge, na kiwanda hiki inazalisha bidhaa mbalimbali za nyuzi zenye ukubwa tofauti lakini pia tunazo bidhaa za plastiki zinaingia nchini huku Tanzania tukiwa tumeshazuia kuingiza plastiki. Kwa hiyo, nimeagiza Wizara ya Kilimo kufanya mapitio kwenye viwanda vyote vinavyozalisha nyuzi za plastiki huwa tukiwa na viwanda vinavyozalisha nyuzi za mkonge tunaoulima hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulishapiga marufuku matumizi ya plastiki lakini tulisema tutaenda kwa awamu. Tulianza na plastiki za kubebea mizigo na zile za viroba. Sasa tutaenda mbali zaidi tunaingia kwenye nyuzi kwa lengo la kumlinda mwekezaji wetu aliyejengwa kiwanda nchini, lakini pia anayetumia zao letu la mkonge kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo na nyuzi lazima tumlinde ilia pate faida na sisi tunufaike kwa kupata soko zuri, kupata ajira kwa watu wetu lakini pia kuhakikisha kwamba wakulima sasa wanahamasika kulima kwa sababu ya uhakika wa soko. Huo ndiyo mpango wetu wa Serikali kwenye eneo hili. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; moja kati ya jambo litakalosaidia sana utekelezaji wa Sera hii ya Elimu na kuendeleza maendeleo ya elimu yetu, ni maelekezo na uamuzi wa Serikali wa Elimu Msingi Bila Malipo. Hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya shule kuwa na utitiri mkubwa wa michango kiasi cha kupelekea kuondoa ile dhana ya Elimu Msingi Bila Malipo. Ni nini kauli ya Serikali juu ya jambo hili?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Korogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, msimamo wa Serikali umebaki vilevile kwamba michango holela hairuhusiwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaposema michango holela, tunajua tuna michango inayokubalika kwenye jamii. Hizi shule zetu za msingi na sekondari ni shule za jamii, ziko kwenye meneo hayo. Tumeunda Kamati ya Shule kwa Shule za Msingi lakini tuna Bodi ya Shule kwa Sekondari. Wajumbe wa Bodi hizi ni wale walioko kwenye maeneo yale kwa lengo la kuwa wanapaswa kusimamia maendeleo ya shule, kushauri mwenendo wa shule na pia kupata changamoto zinazotokana na mwenendo wa kila siku, nao washiriki katika usimamizi wa uendeshaji au uendelezaji wa shule hiyo na taaluma yake kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, Kamati ya Shule inajua inawajibika kwenye ile shule kufuatilia maendeleo yake na pia mahitaji yake. Inaweza kutokea kwa mfano, choo cha shilingi milioni mbili kimebomoka. Siyo lazima kusubiri Serikali ije kujenga choo. Jamii inaweza ikaweka mpango mkakati wa kujenga choo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, michango holela na michango inayokubalika, hapa iko ya aina mbili. Michango inayokubalika ni hiyo ya maendeleo; ya choo kimebomoka, Kamati ya Shule inakutana, wanasema kuna choo kimebomoka tunataka kijengwe kwa haraka watoto wetu waanze kukitumia kesho. Badala ya kusubiri kuandika barua, bajeti ipangwe mpaka TAMISEMI, wanaweza kukubaliana kwamba bwana, tuchangie hapa shilingi mia tano, mia tano, mchango ambao unaenda kwenye choo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, michango hii pamoja na maamuzi hayo tumeidhibiti kidogo. Pamoja na maamuzi yenu ninyi Kamati ya Shule na Kijiji kwa ajili ya jambo la maendeleo, bado mwenye idhini ya kuanza kuchangisha ni Mkuu wa Wilaya. Tumeiweka hiyo kuondoa pia watu kukaa pamoja kutengeneza michango ambayo pia haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, msimamo wa Serikali umebaki pale pale kwamba hatuhitaji michango holela. Michango holela ni ile ambayo wakati wote ninapokuwa ziara huwa natoa mifano. Mtu mmoja tu anakurupuka anasema, kesho kila mmoja awe na shilingi mia mbili mia mbili, hazina maelekezo, hazina maelezo. Michango kama hii ndiyo ile holela ambayo haikubaliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeagiza pia kwamba Mamlaka ya Serikali za Mitaa, kusimamia kutokuwepo kwa michango holela inayokwaza wazazi katika kuendesha shughuli au usimamizi wa mtoto kupata taaluma. Hiyo ndiyo maana ya michango holela na michango rasmi ambayo pia nayo tumeidhibiti na msimamo wetu umebaki pale pale kwamba michango holela haikubaliki. (Makofi)