Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dunstan Luka Kitandula (25 total)

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa kifuta jasho kwa wahanga walioathirika na wanyamapori ikiwepo laki moja tu kwa heka nzima ya mazao yaliyoharibiwa au shilingi laki mbili kwa mtu aliyejeruhiwa, laki tano kwa aliyepata jeraha la kudumu na labda milioni moja kwa familia ya aliyeuawa na wanyama pori na pengine kuchelewesha kutoa malipo hayo kwa wahanga.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu matukio hayo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku pengine kuwa mzigo mkubwa kwa Serikali na kushindwa kuwalipa kama ilivyo nchi ya jirani ni kwa nini sasa Serikali isione umuhimu wa kuanzisha huu mfuko wa fidia kwa wahanga?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Serikali yetu ya Tanzania bado inatoa kifuta jasho kwa wahanga, haioni sasa ni muda mwafaka kurejea na kubadilisha baadhi ya mafungu katika Sheria hiyo ya Wanyamapori ya mwaka 2011 hasa kuongeza nyongeza hii ya fidia angalau iendane na hali ya maisha ya sasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli imekuwepo changamoto ya viwango vya fidia au kifuta jasho kuwa vidogo. Vilevile ni kweli kwamba wakati mwingine imechukua muda mrefu kwa wananchi hao kufidiwa. Serikali imeliona hili na imelifanyia kazi na tuko kwenye hatua za mwisho za kuona kwamba kanuni zinafanyiwa marekebisho ili wananchi waweze kulipwa stahiki zao kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hili la kusema tuanzishe mfuko maalum. Serikali imefanyia kazi jambo hili na imefanya utafiti kwa nchi jirani ambazo zimekuwa na mfumo huu na imejiridhisha kwamba wenzetu wamepata matatizo kuendana na mfumo huu unaopendekezwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali inajielekeza kuweka mikakati ya dharula ambayo itatuhakikishia kwamba tunaondokana na tatizo hili, nakushukuru.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata nafasi. Wako wananchi wangu wa Kata ya Maore, Karemawe, Bendera nakadhalika ambao wameuawa na Tembo takribani miaka miwili sasa lakini Serikali haijatoa kifutajasho wala chochote.

Je, hauoni kwamba Serikali inaonekana kama inawathamini Tembo zaidi kuliko ambavyo inawaona wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imechukulia kwa umuhimu na uzito mkubwa maisha ya Watanzania. Kutokana na changamoto hizi ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa tembo kuvamia na kupoteza maisha ya wananchi wetu, Serikali imeandaa mkakati wa dharura ambao utatuondoa kwenye changamoto hii. Naomba tuipe Serikali muda, ndani ya kipindi mfupi tutaona matokeo ya utekelezaji wa jambo hili.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nampongeza sana; lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imeonesha wazi kwamba wameweka hiyo dawa. Hata hivyo, tatizo la popo katika maeneo ya Upanga, Sea View, Leaders Club, Kinondoni, Oysterbay, Masaki, Msasani Peninsula na maeneo mengine ya ukanda wa pwani linaongezeka siku hadi siku na kusababisha popo hao mpaka wanavunja vioo vya madirisha kwenye nyumbani.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza hiyo dawa ili popo hawa waweze kuondoka na kuwaondolea adha wananchi wa maeneo hayo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa changamoto inayowapata wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam katika maeneo ya Upanga na mengineyo, pia inawakuta wananchi wa Dodoma kuvamiwa na nyuki katika maeneo mbalimbali hasa maeneo ya Area D katika majengo ya TBA, Makole yote pamoja na maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma nyuki wanavamia na kuhama hama hovyo hovyo;

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaondolea wananchi wa Jiji la Dodoma adha ya kuvamiwa na nyuki?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye swali la msingi, hatua ya kwanza ya kukabiliana na popo hawa ilikuwa ni kufanya utafiti wa kujua kiwango cha ukubwa wa tatizo na aina ya dawa ambayo inaweza kutumika ili kukabiliana na changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, utafiti huu umekamilika, sasa jukumu lililopo mbele yetu ni kuhakikisha kwamba wadau wote wanaohusika na kukabiliana na jambo hili, zikiwepo Halmashauri zetu zinachukuwa hatua ya kuhakikisha tunasambaza dawa hizi kwa wananchi ili tuweze kukabilianana tatizo hili. Niombe wadau wote wanaohusika tushirikiane ili tuweze kuondokana na tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la tatizo la uvamizi wa nyuki kwenye Mkoa wa Dodoma. Nitumie fursa hii kuwaagiza wataalamu wetu wa idara ya nyuki kushirikiana na wenzetu wa jiji la Dodoma ili kufanya tathmini ya haraka na kuona ukubwa wa tatizo hili na kuchukua hatua za haraka za kuangamiza nyuki hawa, ahsante sana.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri na kumpongeza, tunafanya kazi vizuri kwa pamoja na nimpongeza kwa majibu mazuri sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuongezea majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa upande wa popo, tayari tumeagiza dawa nyingine za majaribio ikiwemo Pepzol na Super Dichlorvos ambazo zinapatikana Marekani na Kenya. Imeonekana kwamba dawa hizo zikitumika ndani ya miezi miwili mpaka mitatu popo hao wanaweza wakatoweka.

Mheshimiwa Spika, pia nitoe rai kwa Halmashauri zetu za Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri nyinginezo katika maeneo ya miti ya barabarani waweze kununua dawa hizo ili waweze kupiga kwa ajili ya kuweza kufukuza na kudhibiti popo hao.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa Jiji la Dodoma kuhusu suala la nyuki, kama ambavyo Naibu Waziri ameeleza, nako pia tutoe rai kwa Halmashauri ya jiji Dodoma nao watenge fedha ili waweze kununua dawa hizo ili pale tutakapokuwa tumepata tathmini ya kuweza kujua ni dawa gani zinaweza kufanya kazi vizuri katika kudhibiti basi waweze kununua dawa hizo na kuweza kutumia.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia taasisi ya TAWIRI tutaendelea kushirikiana na wananchi pamoja na taasisi katika kuhakikisha kwamba tunadhibiti tatizo hili. Tuombe ushirikiano kwa wale wenye makazi pia waweze kununua dawa hizi katika maduka mbalimbali yanayozalisha dawa hizi. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na popo katika Mkoa wa Dar es Salaam, kuna tatizo kubwa la kunguru ambao wamekuwa wakitapakaa kila mahali, wanajerui watoto; na hasa katika fukwe, ambako wamekithiri, na hivyo kuharibu utalii wetu. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wanadhibiti kunguru hao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba kujibu swali la nyongezala la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na tatizo la kunguru katika maeneo mbalimbali nchini. Serikali kupitia Wizara imekuwa ikifanya jitihada ya kuja na mipango mbalimbali ya kuweza kuondokana na tatizo hili. Changamoto tunayoiona ni kwamba wenzetu kwenye maeneo ya halmashauri zetu wameliacha jambo hili kuwa ni jambo la Wizara peke yake. Tunawaomba sana wadau wenzetu katika maeneo ya halmashauri, kwa kutumia teknolojia iliyoandaliwa na Wizara tushirikiane ili kupambana na tatizo hilo. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Natumia nafasi hii kuipongeza Wizara na Serikali kwa ujumla kwa jitihada zinazofanywa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Napongeza Wizara kwa kutumia TTB na kuratibu ziara ya waandishi wa habari kwa ajili ya kubaini vivutio hivi. Hata hivyo, huwezi kutenganisha utalii na rika mbalimbali kwenye eneo husika kwa maana ya watu wazima, wazee, rika la kati na watoto katika kubaini na kuendeleza utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ziara hii imefanikiwa, lakini bahati mbaya sana kuna rika la watu wazima, kuna kikundi cha KUMIDEU na vinginevyo ambavyo vinafahamu zaidi utamaduni, mila na desturi za watu wa Ukerewe, walitakiwa kuhusishwa. Nini sasa mkakati wa Serikali ili wakati mwingine vikundi kama hivi vishirikishwe ili kupata uhalisia wa vivutio vya utalii vilivyopo pale Ukerewe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali, lakini tunakosa kiungo kinachoweza kuratibu mambo haya ya utalii. Halmashauri zetu zingeweza kutoa msaada mkubwa sana, lakini bahati mbaya sana hazina watu specific wanaoshughulika na utalii zaidi ya utamaduni. Je, ni nini mkakati wa Serikali sasa kuhakikisha Halmashauri zetu zote zinakuwa ama na idara au na vitengo vinavyohusika na utalii ili kuweza kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais katika kukuza Sekta ya Utalii? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ulimwenguni kote, custodian wa mila na desturi ni Machifu wakienda sambamba na wazee wa mila na desturi. Kwa bahati mbaya kwenye halmashauri zetu kumekuwa na upungufu wa kubaini makundi haya ya wazee wa mila na desturi. Natoa rai kwa halmashauri zetu, ziwe na mikakati ya kuwatambua wazee wa mila na desturi ambao ndio custodian wa tamaduni zetu ili tunapofanya jukumu la kutambua na kutangaza vivutio vilivyopo kwenye maeneo yetu, basi wazee hawa waweze kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa halmashauri zetu, zijielekeze kwenye kutambua maeneo yote yenye sifa za kiutalii, wawasiliane na Wizara ili maeneo haya yaweze kusajiliwa tuweze kuweka mpango mkakati wa pamoja wa kutangaza maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili la uhaba au kukosekana kwa kiungo, kwa kukosekana wataalam kwenye halmashauri zetu. Mamlaka ya ajira ya watumishi kwenye ngazi ya halmashauri, ni Wizara ya TAMISEMI. Naomba sana halmashauri zetu zijielekeze kwenda kuomba vibali vya ajira kwa TAMISEMI ili jambo hili liweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kwa kutambua gap lililopo, Wizara ya Maliasili inao wataalam kwenye kanda zetu. Kwa mfano, kwenye Kanda ya Ziwa Victoria, tunao wataalam wetu wawili walioko Mwanza, Kanda ya Kusini, tunao wataalam watatu wapo Iringa, Kanda ya Kaskazini, tunao wataalam sita wapo Arusha, Kanda ya Pwani, tunao sita wapo Dar es Salam lakini vilevile hapa Makao Makuu tunao wataalam. Tunaomba halmashauri zetu ziwatumie wataalam hawa wakati wakijiandaa kupata vibali vya ajira kutoka TAMISEMI.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Hifadhi za Taifa, Hifadhi za Misitu pamoja na Mapori ya Akiba, tumeanzisha kwa ajili ya kuhifadhi uoto wa asili na kulinda viumbe hai pamoja na wale ambao wako hatarini kutoweka. Hali kadhalika kwa kuwa hivi karibuni maeneo mengi ya hifadhi na mapori ya akiba, aidha tumeyamega ya kuyateremsha hadhi baadhi yake. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba utaratibu huu wa kumega maeneo na kuteremsha hadhi maeneno ya hifadhi haujirudii tena?

Swali la Pili, kwa kuwa upoteaji wa uoto wa asili unaenda sambamba na upoteaji wa viumbehai, mimea na wanyama ambao wako hatarini kutoweka. Je, Serikali ina mpango gani wa kuainisha na kuwea kutenga utaratibu maalum wa kuweza kuhifadhi viumbe adimu na wale ambao wako hatarini kutoweka? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliridhia kuachia maeneo yenye migogoro vilevile kushusha hadhi baadhi ya mapori na hifadhi zetu baada ya kubaini kwamba ipo migogoro isiyokuwa na tija iliyokuwa inahatarisha usalama wa wananchi wetu. Serikali ilifanya hivyo baada ya kufanya utafiti wa kina kuona kiasi cha matumizi endelevu ya maeneo hayo, jinsi ambavyo yanaweza kutumika na kama yalikuwa yanatumika kwa jinsi ambavyo ilivyokuwa imekusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale inapoonekana kwamba pori au hifadhi imepoteza sifa yake ya awali ya msingi, basi maeneno hayo hushushwa hadhi na kuwa misitu ili tuweze kuendelea kutunza maeneno haya. Katika kujipanga kuhakikisha kwamba hali hii haijitokezi tena, Serikali inajipanga kutoa elimu kwenye maeneo yote yanayozunguka maeneo ya hifadhi zetu na mapori tengefu ili kujenga uelewa wa wananchi kuhusiana na umuhimu wa rasilimali hizi, vilevile Serikali imejipanga kuongeza doria katika maeneo haya ili uvamizi usijitokeze tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, Serikali inajitahidi sana kuhakikisha kwamba pale ambapo mimea imetoweka au wanyama wametoweka Serikali imekuja na mkakati wa kupanda miti kwenye maeneo yale yaliyoathirika, kwa mfano kupitia TFS tumeaza kupanda miti kule Mkoani Geita, vilevile tumeanza kupanda miti Mkoani Kigoma zaidi ya hekta 139,000 zimepandwa ili kuhakikisha uoto ule haupotei.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pale ambapo tunaona kwamba kuna aina fulani ya wanyama inatoweka, tunakuwa na mkakati wa kuweka maeneo maalum ya kuhakikisha tunadhibiti kuzaliana kwa wanyama wale ili wasije wakatoweka. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Hifadhi ya Msitu wa Kihesa - Kilolo pia imekutana na athari hizo. Je, Serikali iko tayari kutusaidia na sisi kuja kupanda miti ili kuendela kuhifadhi eneo lile?

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, tumelichukua, wataalam wetu wataenda kufanya tathmini na kuona jinsi ambavyo tunaweza kusaidia.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, Sera ya Ugatuaji ni Sera ya Kitaifa. Suala la mapato ya taasisi zetu na maduhuli ya Serikali kwenda moja kwa moja hazina inaenda kinyume na hii Sera ya ugatuaji. Ndio inayosababisha miundombinu muhimu kwenye hifadhi zetu kutotengenezwa mara kwa mara. Je, Serikali haioni wakati umefika sasa wa kurudisha walau asilimia 20 ya mapato kwenye hifadhi zetu, ili washughulikie miundombinu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Serikali inakiri kufunguliwa kwa geti hili katika Kata ya Kilangali na Tindiga kunaenda kufungua fursa za kiuchumi. Je, wamewaandaa vipi wananchi wa Kata za Tindiga, Dhombo, Masanze na Kilangali, ili wasije kuwa wageni wakati fursa hizi ambazo zitatokana na kufunguliwa kwa lango hili zitakapowadia? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto ya kukamilika kwa miundombinu kwenye maeneo yetu kutokana na kukosekana kwa fedha na mabadiliko tuliyokuwa tumefanya ya mfumo wa kukusanya mapato na kuyapeleka moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. Hata hivyo, baada ya jambo hili kujadiliwa kwa kina ndani ya Bunge lako Tukufu na jambo hili kufikishwa Serikalini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuridhia kurejesha tozo ya maendeleo ya utalii ambapo tayari Mheshimiwa Rais ameridhia asilimia tatu ya fedha hizi iweze kutumika kwa ajili ya shughuli hizi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili; jukumu la kutoa elimu kwa wananchi wetu sio jukumu la Serikali Kuu peke yake ni pamoja na halmashauri zetu. Nitoe rai kwa halmashauri husika ziweze kutoa elimu kwa wananchi, tukiwepo sisi Waheshimiwa Wabunge, ili wananchi waweze kuchangamkia fursa za kimaendeleo zinazokuja katika maeneo yetu.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana; je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha lango la kuingia Mlima Kilimanjaro la Kidia kwani lango hili litakuwa linatumiwa na watu maarufu kupanda Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii ina mchango mkubwa katika kuongeza mapato katika nchi yetu. Kwa hiyo, ni makusudio ya Serikali kuboresha malango katika hifadhi zetu zote za Taifa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, katika hili la Kidia, tayari Serikali inaendelea na kuboresha eneo lile. Tayari tunavyozungumza barabara ya kilometa karibu 28 ya watembea kwa miguu kwenye eneo lile imeboreshwa. Barabara karibu kilometa tisa inajengwa kwa kiwango cha changarawe na katika bajeti ya mwaka huu kupitia TANAPA zimetengwa karibu milioni mia tisa kwa ajili ya kujenga mageti kwenye eneo hilo.
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kumekuwa na wimbi kubwa la tembo kuvamia makazi ya watu na mashamba, lakini kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kuna askari wanatokea Ngara. Tumekuwa tukitoa taarifa ya uvamizi wa tembo huwa inachukuwa zaidi ya siku mbili mpaka nne kwenda kutatua tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali mtanipa lini askari watakao kaa katika Jimbo la Igalula siyo hao wa Ngara na siwajui na sijawahi kuwaona?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, tumekuwa na uvamizi na uharibifu wa mali za wananchi na mwaka jana tulikwenda kufanya tathmini wananchi zaidi ya hao 17 walivamiwa na uharibifu mkubwa. Lini mtawalipa fidia wananchi waliopata athari hizo? Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli nchi yetu imekuwa na wimbi kubwa la matukio ya wanyama wakali na waharibifu kushambulia maeneo ya wananchi wetu. Serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kwamba pale tunapopata taarifa tunawatuma askari wetu kwa haraka kwenda kusaidia kukabiliana na changamoto hizi.

Mheshimiwa Spika, sasa tathmini iliyokuwa imefanyika ilionekana kabisa askari hawa tuliokuwa nao kwenye eneo lile wana uwezo wa kushughulikia jambo hili, lakini kwa sababu ya concern ya Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki cha leo nitakaa nae tuweze kuona ni jinsi gani tunaweza kushirikiana na halmashauri kutoa mafunzo kwa maafisa wanyama pori wa vijiji ili waweze kushirikiana na wale wa Serikali kuondokana na changamoto iliyopo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuwalipa hawa wananchi ambao wamepata madhara haya kama nilivyosema kwenye jibu la msingi tuko kwenye hatua za mwisho za kufanya tathmini ili tuweze kuwalipa. Tathmini hii ikikamilika nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wale watakaostahili kulipwa watapata malipo yao kwa wakati.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana ninalo swali moja la nyongeza. Kwanza, niishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri ya kutia moyo. Kwa kuwa umekiri kuwepo kwa maporomoko hayo ambayo ni kivutio lakini yamepotea baada ya uchepushaji kwenye mradi wa umeme Rusumo. Je, huoni sasa ipo haja kupitia Wizara yako na Wizara ya Nishati mshirikiane kurejesha maporomoko hayo yawe kama awali ili yaendelee kuwa kivutio katika Wilaya yetu ya Ngara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Semguruka kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kwa kushirikiana na kampuni ya umeme ambayo itapewa jukumu la kuendesha mradi ule wa umeme pale Rusumo tayari wanamkakati wa kupanda miti katika eneo lote lile la ukanda wa mradi ule, ni imani yetu kwamba baada ya kufanyika upandaji wa miti ule hali ya upatikanaji wa maji katika eneo lile itaimarika na hivyo uwezekano mkubwa wa kivutio hiki kuendelea kutumika.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kutoa ajira kwa mkataba wa muda mfupi kwa askari wa VGS ilikuweza kupunguza tatizo kubwa ama uhaba wa askari wa wanyama pori nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inao mkakati wa kuhakikisha kwamba pale ambapo mafunzo ya askari wa vijiji yamefanyika na kumekuwa na uhitaji wa askari hawa kupatiwa ajira, tunashirikiana na halmashauri kuona jinsi ambavyo kupitia miradi mbalimbali tulioyonayo akari hawa badala ya kupewa ajira wanaanzishiwa miradi itakayowaingizia kipato ili wakati wakifanya shughuli hii ya uhifadhi lakini vilevile waweze kujiongezea kipato.

Mheshimiwa Spika, tumeanza zoezi hilo kwa mradi wa REGROW ambao unajielekeza kwenye kufungua fursa za utalii katika mikoa ya Kusini tunaamini mafunzo tutakayoyapata kutokana na mradi huu yatatuonesha ni jinsi gani tunaweza kuendeleza katika maeneo mengine.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kwa kuwa kivutio chetu pekee cha maporomoko ya Rusumo sasa kimepunguza mvuto baada ya uwekezaji wa mradi wa umeme pale Rusumo, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuisaidia Ngara kuendeleza vivutio vingine ili Ngara isiondoke kwenye ramani ya kupata watalii, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kivutio cha Rusumo siyo kivutio pekee kilichopo katika ukanda huu tunazo mbuga za wanyama zilizoko katika ukanda huu. Vilevile, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi tunaangalia kutumia uwepo wa mradi wa umeme kuufanya kama sehemu ya kivutio. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika kuendeleza utalii katika ukanda huu tutaunganisha vivutio vingine vyote vilivyopo ili Sekta ya Utalii iweze kunufaisha ukanda huu na nchi yetu kwa ujumla.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, licha ya kupeleka umeme katika Kata za Chenzema, Langala na hizo nyingine zote, naishukuru Serikali kwa sababu inachukua huduma sana kwenye umeme: Je, ni lini vijiji vya Kidunda pamoja na Ngolehanga vitaweza kupatiwa umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini vijiji na vitongoji vya Morogoro vijijini vitaweza kupata umeme? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Morogoro kwa ujumla wake una vijiji vilivyohitaji kupatiwa umeme takribani 668. Vijiji ambavyo vilikuwa vipo katika mpango wa kupelekewa umeme ni vijiji 239. Mpaka sasa tumeshapeleka umeme kwenye vijiji takribani asilimia 90. Makusudio yetu ni kwamba vijiji vyote vya Mkoa wa Morogoro ikifika mwezi Juni mwaka huu viwe vimepatiwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mkakati wetu ni kuhakikisha kwamba tupo katika hatua ya mwisho ya kupeleka umeme kwenye vitongoji 15 vya kila jimbo la nchi yetu na matarajio yetu ni kwamba kazi hii itakamilika, uratibu wa kazi hii utakamilika hivi karibuni na tutaweza kuanza kufanya kazi hiyo.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ndani ya Halmashauri ya Mji wa Njombe Kata ya Kambarage kuna mitaa miwili ya Pemba na Unguja mpaka leo haina umeme: Ni lini mitaa hiyo itapata umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Mwanyika, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itahakikisha kwamba vijiji vyote ambavyo havina umeme, kufika mwezi Juni vinapata umeme na vile vile kufika Juni kazi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote nchini, vile 15 kama nilivyosema awali, itakuwa imefanyika.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni lini Serikali itapeleka umeme katika Kata za Mwamashele, Lagana pamoja na Mwasubi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mnzava, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, makusudio yetu ni kuhakikisha kwamba mikataba yote ya ukandarasi wa kupeleka umeme kwenye vijiji vyetu, ile mikataba iliyowahi kufika mwezi Juni mwaka huu 2024, umeme utakuwa umepatikana. Mikataba ambayo imechelewa tutasogea mbele kidogo ikiwezekana kufika mwishoni mwa mwaka huu wa fedha (2023/2024). (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni lini Serikali itatekeleza mpango wake wa peri urban kupeleka umeme katika mitaa yenye sura za vijiji katika miji yetu ikiwepo katika Manispaa ya Iringa Mtaa wa Ugere, Mosi, Msisina na Mtalagala.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango wa kupeleka umeme kwenye maeneo ya miji yenye sura za vijiji (peri urban) na kazi hiyo inaendelea kwa sasa. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, kazi hii itakamilika, maeneo haya yatapatiwa umeme.
MHE. EMANNUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Nashukuru kwamba, ameshindwa kuthibitisha kwamba mifugo inatakiwa kutozwa shilingi 100,000 kwa kichwa cha ng’ombe wanapoingia hifadhini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wafugaji wengi Tanzania wamekuwa wakitozwa shilingi laki moja kwa kichwa cha ng’ombe wanapoingia hifadhini na kuna wananchi wametozwa mpaka shilingi milioni sabini kwa wakati mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza nini kauli ya Serikali kwa Watumishi wa TANAPA, TAWA pamoja na NCAA ambao wamekuwa wakitoza shilingi laki moja kwa kichwa cha ng’ombe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili je, Serikali ipo tayari kurejesha fedha za wananchi ambazo wametozwa zaidi ya shilingi milioni kumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shangai kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimeonyesha sheria inataka nini? Lakini sambamba na eneo hilo niseme tu kwamba, kosa la kuingiza mifugo kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi ya Taifa lipo pia katika Kanuni Na. 7(1) ya Kanuni za Hifadhi ya Taifa GN Na. 255 ya mwaka 1970 kama ilivyorekebishwa ambavyo Kifungu kinazuia kuingiza mifugo Hifadhini na adhabu ya kosa kuingiza mifugo ni kwa kila mfugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nchi yetu, Serikali yetu ina heshimu Utawala wa Sheria na chombo ambacho kimekasimiwa kutafsiri sheria pale ambapo kuna changamoto ni Mahakama zetu. Nitoe rai kwamba wale wote wanaoona kwamba imepita hukumu ambayo wanaona haikuwatendea haki basi twende kwenye mfumo wa kisheria ili sheria iweze kutoa haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili la kurejesha bado narudi pale pale yeyote anayehisi kwamba hakutendewa haki tuzitumie Mahakama zetu ili haki iweze kutendeka. (Makofi)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, naomba niulize swali moja la nyongeza, ila niruhusu nijieleze kidogo.

Mheshimiwa Spika, wakati kunatokea moto kwenye mlima watu wanaokimbizana kuuzima ni wale wanaoishi kandokando ya ule mlima; pale Marangu wanabebwa, wanasombwa, wanalazimishwa kwenda kuzima moto. Sasa tulikuwa tunaomba Serikali itoe kauli kuhusiana na uwezekano wa kutoa mwongozo ili wale tour operators wawe na uwiano fulani tuseme asilimia 70 ya wahudumu wanaopandisha watalii wawe wanatoka kwenye eneo lile la pale Marangu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, tumepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na tunaenda kuufanyia kazi tuone ushauri wa kitaalam utatuelekeza vipi. (Makofi)
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuondoshwa kwa maeneo ya kinga (buffer zone) kunasogeza zaidi wananchi karibu na hifadhi na kuwahatarisha na wanyama wakali na waharibifu: Je, Serikali haioni haja ya kuja na mikakati zaidi ya kutoa elimu ili kuwasaidia wananchi hawa kuwaepusha na hiyo hatari? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa buffer zone kitaalam inalenga kuwatenga wananchi na maeneo ya hifadhi na hivyo, kupunguza vitendo vya uharibifu na vitendo vya uvamizi.

Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha kwamba, utaratibu huu wa kuondoa buffer zone katika maeneo ya hifadhi haujirudii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohammed Soud Jumah, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, Wizara inajielekeza sana kwenye kutoa elimu. Sambamba na hiyo, kwenye maeneo ya namna hii vilevile tuna mikakati ya kuwahamasisha wananchi kufuga nyuki kwenye maeneo hayo. Vilevile, kuendesha utalii wa kiutamaduni, kupanda au kutunza misitu ili waweze kuja na mfumo wa biashara ya uvunaji wa Hewa ya Ukaa. Tunaamini wananchi wakijielekeza kwenye maeneo haya, basi huo muingiliano utapungua athari zake.

Mheshimiwa Spika, katika swali la pili, ni kweli kwamba maeneo haya ya buffer zone yanalenga kuwatenga wananchi na maeneo ya hifadhi ili kuwaondolea athari ya madhara ya uvamizi na hivi. Pamoja na kutoa elimu, Wizara inajielekeza kwenye kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uhifadhi na kutoa elimu kwa viongozi na wananchi. Imani yetu ni kwamba, elimu hii ikiwaingia wananchi na wakazingatia maelekezo haya, basi migogoro hii itaondoka. (Makofi)
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa wanyama hao walioko katika maeneo yetu ya uhifadhi, mara baada tu ya kuvuka kwenye buffer zine wanaingia kwenye ardhi za vijiji.

Je, Wizara au Serikali haioni kwamba kuna haja sasa ya Wizara kukaa na vijiji vinavyozunguka maeno ya hifadhi ili kwa pamoja waweze kuweka utaratibu rafiki wa namna ya kusimamia wanyama pori nje ya hifadhi za Taifa na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ole-Sendeka kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara imekuwa ikifanya jambo hili ambalo Mheshimiwa Ole-Sendeka amelishauri. Sambamba na hilo, tumekuwa tukishirikiana vilevile na Wizara ya Ardhi katika kufanya mipango ya matumizi bora ya ardhi. Tunaamini kwa kufanya hivyo tutaepuka changamoto tunazokabiliana nazo.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, naomba sasa niwe na swali moja tu la nyongeza. Kwa kuwa maelezo ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri umeyaeleza, vikundi vingi vilivyopewa mizinga hiyo ni vya Wilaya ya Iringa lakini kutoka Iringa Vijijini na Iringa Manispaa ni lango la utalii Kusini.

Je, mpo tayari sasa kutupatia na Iringa Manispaa ili angalau uoto wa asili urudi kwa kufuga nyuki? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mara tutakapopata orodha ya vikundi vilivyoanzishwa kwa jambo hili, Wizara itaona jinsi ambavyo inaweza kushirikiana na hamashauri ili kuweza kuwapatia mizinga. (Makofi)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa kuwa tayari Ngara kuna mkandarasi anayeendelea kujenge miundombinu ya kupeleka umeme maeneo ya Ngoma, Kata ya Bugarama, Kibogora, Mganza na Keza, na kwa kuwa mkandarasi huyu mpaka sasa hajapeleka umeme kwenye kata hizo na vijiji ambavyo viko viko kwenye kata hizo, ni upi mpango wa Serikali wa kumsukuma mkandarasi huyu ahakikishe anakamilisha kazi yake ya kupeleka umeme kwenye maeneo haya, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya Serikali, yako wazi kwa wakandarasi wanaoendelea na miradi ya kupeleka umeme vijijini kwamba wanapaswa kuheshimu mikataba yao. Wale ambao hawataweza kupeleka umeme kwa mujibu wa mikataba yao, basi wanakuwa wamejiweka kwenye mazingira ambayo hawatapata mikataba mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwakumbusha wakandarasi wote, wafanye kazi walizopewa kwa mujibu wa mikataba yao, maana kushindwa kufanya hivyo wanajihakikishia kwamba hawatapata mikataba mipya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, natoa maelekezo kwa watendaji wetu katika mkoa ule, wamsimamie kwa karibu mkandarasi huyu ili aweze kutimiza wajibu wake. (Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nimemwelewa vizuri sana Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kwamba Serikali imekubali kutoa hekta 2943.8 kwa wananchi wa Kisiwa cha Maisome. Kwa niaba ya wananchi hao naomba niwasilishe furaha yao kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa Bunge lako Tukufu kwani kwa muda mrefu wameishi kwa mateso sana wakiwa hawana eneo la malisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu ni moja tu ni lini? Ni lini? Ni lini, kwa mara tatu mchakato huu wa kuweka mpaka utatekelezwa ili wananchi waifurahie Serikali yao? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria, zoezi hili linapaswa kuchukua miezi sita. Siku 90 za kuweka mipaka, kutengeneza ramani na vilevile siku 90 ambayo ndiyo itahusisha lile tangazo nililolisema. Tumefika hatua nzuri, naomba Mheshimiwa Mbunge atupe muda, tunalikamilisha muda siyo mrefu.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni Septemba niliuliza swali Na. 76 juu ya wananchi ambao wamevamia Msitu wa Bono uliopo Kijiji cha Mswaki kwenye Kata ya Msanja na Serikali ilisema itawaondoa itakapofika Desemba 30, kwa maana ya mwaka 2022. Nataka kujua: Ni nani ambaye anazuia kuondoa wananchi wale ambao wanafanya uharibifu mkubwa na msitu huo tunaoutegemea kwa ajili ya mvua? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Serikali inasimamia maazimio yake yale kwamba wananchi wale wataondolewa kwenye msitu ule. Naomba Mheshimiwa Mbunge, atupe fursa tulifanyie kazi ili tutekeleze kusudio letu.