Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dunstan Luka Kitandula (12 total)

MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanzisha Mfuko wa Fidia kwa wahanga wanaoathirika na wanyamapori wakali na waharibifu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la kama ulivyonielekeza.

Mheshimiwa Spika, kwa hii ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu baada ya Mheshimiwa Rais kunipa heshima hii ya kuniteua kuwa Naibu Waziri, naomba nitumie fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye imempendeza niweze kutumika kwenye nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pili nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kunipa heshima hii ya kuitumikia nchi yetu. Naahidi kutekeleza majukumu yangu kwa uwezo wangu wote na kwa vipawa vyote alivyonipa Mwenyezi Mungu, naahidi sitamwangusha.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba ushirikiano wako na Wabunge wenzangu nawaahidi ushirikiano naomba tushirikiane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikilipa kifuta jasho na kifuta machozi kama mkono wa pole au faraja kwa wananchi wanaopata madhara kutokana na wanyamapori wakali na waharibifu. Malipo hayo yamekuwa yakifanyika kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta Jasho na Machozi za mwaka 2011 na kwa kadri ya upatikanaji wa fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, kanuni hizo zilianza kutekelezwa mwaka 2012 ambapo katika kipindi cha kuanzia 2012/2013 hadi 2022/2023 jumla ya shilingi bilioni 11.3 zimelipwa kwa wananchi walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu. Hata hivyo, suala hili limekuwa ni changamoto kubwa kwa nchi nyingi za Afrika ambapo limesababisha baadhi ya nchi kuondokana na utaratibu wa kulipa kifuta jasho na machozi. Lakini Tanzania imeendelea kuona umuhimu wa kuwafuta jasho na machozi wananchi kwa madhara wanayoyapata kutokana na wanyamapori hao. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaondoa popo waliopo maeneo ya Upanga ili kulinda afya za wakazi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kudhibiti popo katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuchukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufanya soroveya (survey) ya kuangalia ukubwa wa tatizo, maeneo yaliyoathirika, mbinu gani ambazo ni rafiki kwa mazingira zitumike kudhibiti na pia kubaini aina ya popo wanaosumbua. Imebainika kuwa kuna aina mbili ya popo wanaosumbua, ambao ni popo wanaokula matunda (hawa wanaotumia miti kama maeneo yao ya makazi) na popo wanaotumia mapango au magofu ya nyumba kama makazi yao.

Mheshimiwa Spika, katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, majaribio ya dawa tano za kunyunyizia yalifanyika ili kufukuza popo katika makazi hayo. Kati ya dawa hizo; dawa mbili (Napthalene na Bat CRP) zimeonekana kuwa na uwezo wa kuwafukuza popo hao. Juhudi zaidi zinaendelea kwa kushirikiana na wadau kwenye maeneo husika.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, nini mkakati wa Serikali kuvifanya vivutio vya mapango ya Handebezya na jiwe linalocheza kuwa na tija kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuendeleza, kukuza na kutunza vivutio vya utalii vilivyopo Ukerewe vikiwemo Mapango ya Handebezya na Jiwe linalocheza vinavyopatikana katika Kisiwa cha Ukerewe. Mikakati hiyo ni pamoja na kutangaza vivutio hivyo kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari.

Mheshimiwa Naibu Spika, mathalan, Wizara kupitia TTB iliratibu ziara ya Kituo cha Televisheni cha ITV kwenda kutembelea baadhi ya vivutio vya utalii vilivyopo Ukerewe vikiwemo Mapango ya Handebezya na jiwe linalocheza kwa ajili ya kuandaa documentary ambayo itakapokamilika itaonyeshwa katika kipindi cha ITV cha Chetu ni Chetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mafunzo yanaendelea kutolewa kuhusu uanzishwaji wa utalii wa utamaduni ambapo hadi sasa kuna vikundi vya utalii wa utamaduni vikiwemo Ukerewe (Ukerewe Cultural Tourism Enterprises) na Nansio (Nansio Cultural Tourism Enterprises).

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kushiriki katika maonesho na matamasha mbalimbali yakiwemo Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki na Tamasha la Bulabo yanayofanyika katika Kanda ya Ziwa kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji zilizopo katika ukanda huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara itaendelea kuhamasisha uwekezaji wa miundombinu inayoelekea katika maeneo yenye vivutio vya utalii, ujenzi wa huduma za malazi zenye hadhi pamoja na kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo maji, umeme, huduma za kibenki na mawasiliano.
MHE. MOHAMED JUMAH SOUD aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kupunguza upoteaji wa Uoto wa Asili nchini unaosababisha kupoteza hadhi kwa Hifadhi na Mapori ya Akiba?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Jumah Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kubwa ya kupotea kwa uoto wa asili katika Hifadhi na Mapori ya akiba ni ongezeko la mimea vamizi katika maeneo hayo. Mimea hiyo husababisha mabadiliko ya aina ya mimea katika maeneo yaliyohifadhiwa kwa kutoa fursa kwa mimea isiyoliwa na wanyamapori kustawi zaidi, kuongezeka na kupunguza uoto wa asili ambao ni tegemeo la wanyamapori. Hadi sasa, tafiti zimebaini aina 47 za mimea vamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa. Sababu zinazopelekea kushamiri kwa mimea vamizi ni pamoja na uingizaji wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa, mabadiliko ya tabianchi, shughuli za binadamu na viumbepori wahamao.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada za kudhibiti mimea vamizi, Wizara kupitia Taasisi za uhifadhi inatekeleza mkakati wa kukabiliana na mimea vamizi katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kuondoa kwa kung’oa mimea husika katika hifadhi. Aidha, mikakati mingine ni kuimarisha ulinzi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa kudhibiti shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na uingizwaji wa mifugo hifadhini sambamba na kuwekeza zaidi katika utafiti ili kupata suluhisho la kudumu.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:-

Je, mchakato wa ujenzi wa geti jipya la kuingilia Hifadhi ya Mikumi kutokea Kilangali na Tindiga umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Londo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha tathmini ya awali kwa ajili ya kujenga lango la kuingilia watalii kupitia maeneo ya Kilangali na Tindiga Wilaya ya Kilosa. Kufuatia tathmini hiyo, gharama za ujenzi wa lango hilo na miundombinu ambata ya lango husika ni jumla ya shilingi bilioni 2.8. Aidha, michoro pamoja na BOQ imekamilika. Hatua inayoendelea kwa sasa ni kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa lango hilo. Kwa ujumla, lango husika litafungua fursa za watalii watakaosafiri na treni ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam na Dodoma kuingia Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwa urahisi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali kwa kuona umuhimu wa hifadhi hiyo imejipanga kuongeza malango ya kuingilia watalii katika maeneo yote muhimu ambapo kwa sasa kupitia Mradi wa Kukuza Utalii Kusini (REGROW), malango mawili ya kisasa yanajengwa kwa ajili ya kuingilia watalii katika maeneo ya Doma na Kikwaraza (Mji mdogo wa Mikumi). Ujenzi huo umeanza mwezi Agosti, 2023 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2024.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka Askari na kulipa fidia kwa Wananchi waliovamiwa na Tembo kwenye makazi na mashamba yao Jimbo la Igalula?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeweka askari sita wakiwemo askari wa uhifadhi wawili na askari wa vijiji (VGS) wanne katika kituo cha kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu cha Ndala kilichopo katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora. Aidha, askari hao wamepewa vitendea kazi ikiwemo pikipiki mbili na silaha ambavyo vinawawezesha kudhibiti wanyamapori hao popote wanapoonekana ikiwemo Jimbo la Igalula.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikilipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi wanaopata madhara kutokana na Wanyama pori ambapo kwa upande wa Wilaya ya Uyui ambayo inajumuisha Jimbo la Igalula Wizara imepokea maombi ya wananchi 17 waliopata madhara ya wanyama pori wakali na waharibifu, maombi hayo kwa sasa yanaendelea kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako tukufu niendelee kutoa rai kwa wakurugenzi wa Halmashauri wa wilaya hususan zenye changamoto za wanyama pori wakali na waharibifu kuharakisha kuwasilisha maombi yanayotokana na madhara ya Wanyama pori hao Wizarani ndani ya siku saba ili kuiwezesha Serikali kufanya malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi kwa wakati.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kukitangaza vya kutosha Kivutio cha Maporomoko ya Maji Rusumo ili kuchangia pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kushirikiana na Halmashauri za Wilaya kubaini vivutio mbalimbali vya utalii nchini kwa lengo la kuongeza wigo wa mazao ya utalii, katika kutekeleza hilo mwaka 2021 wataalam wa Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara walibaini vivutio vya utalii na fursa mbalimbali za uwekezaji na shughuli za utalii katika Mkoa wa Kagera.

Mheshimishiwa Spika, miongoni mwa vivutio vilivyobainishwa ni Maporomoko ya Maji ya Mto Rusumo ambayo yanatoa fursa ya uendelezaji wa shughuli za utalii. Hata hivyo, tathmini ya awali iliyofanywa na watalaam wa Wizara imebaini kwamba kiasi kikubwa cha maji ya maporomoko hayo kimechepushwa kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na hivyo kupunguza mvuto wa utalii wa maporomoko pekee.

Mheshimishiwa Spika, kwa mujibu wa ushauri wa watalaam, mara baada ya kukamilika kwa mradi wa uzalishaji wa umeme na kukabidhiwa Serikalini, tathmini mpya itafanyika ili kuunganisha utalii wa maporomoko ya maji na utalii wa uzalishaji wa umeme. Endapo tathmini hiyo itaonesha uwezekano wa eneo hilo kutumika kama kivutio cha utalii wa maporomoko ya maji na utalii wa uzalishaji umeme, Serikali itajielekeza kwenye kufanya maboresho ya miundombinu katika maporomoko hayo na kuyatangaza ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuvutia watalii kutembelea katika kivutio hicho.

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako tukufu niendelee kuwahamasisha Watanzania wenzangu kuwa na utamaduni wa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii. Aidha, nitoe wito kwa Mheshimiwa Mbunge, uongozi wa Mkoa na wadau wengine kwa ujumla kuhamasisha uwekezaji wa huduma ikiwemo huduma za malazi na miundombinu mbalimbali katika vivutio vya utalii vilivyopo katika Mkoa wa Kagera.
MHE. EMANNUEL L. SHANGAI aliuliza:-

Je ni sheria ipi inawaruhusu Watumishi wa TANAPA, TAWA na NCAA kutoza mifugo shilingi 100,000 pindi iingiapo hifadhini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emannuel Lekshon Shangai, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi za Uhifadhi za TANAPA, NCAA na TAWA zinaongozwa na Sheria mahususi za kusimamia rasilimali za wanyamapori. Mathalan, Sheria ya TANAPA Sura 282 Kifungu cha 28(1)(a) kama kilivyorekebishwa na Sheria ya Marekebisho Mbalimbali (Na. 11) ya mwaka 2003 ambayo imeongeza kifungu 20A cha Sheria hiyo kwa kuwapa mamlaka watumishi wa TANAPA kutoza faini isiyozidi shilingi 100,000 kwa kila kosa pale mkosaji anapokiri na kukubali kwa maandishi kulipa faini kwa kosa husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 116 cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori, Sura ya 283 hutumika katika kutoza faini pindi mifugo inapoingizwa kinyume cha sheria, ndani ya mapori ya akiba. Kifungu hiki kimebainisha utaratibu wa kulipa faini ambapo mkosaji atalipa faini mara baada ya kukubali na kukiri kosa. Aidha, sheria imeelekeza kuwa kiwango cha faini hakitapungua shilingi 200,000 na hakitazidi shilingi 10,000,000. Mkosaji hukiri kosa kwa maandishi na kulipa faini hiyo, na endapo hatakuwa tayari kulipa faini, hufikishwa Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Wananchi kwa ujumla kuwa Serikali itaendelea kuhifadhi na kusimamia rasilimali za wanyamapori kwa kushirikiana na jamii. Hivyo, tunawaomba wote watoe ushirikiano katika kufanikisha jukumu hilo na kuwasihi wazingatie sheria ili kuepusha migongano isiyo ya lazima baina yao na Wahifadhi.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -

Je, lini Serikali itafanya mapitio ya viwango vya malipo ya ujira kwa wapagazi, wapishi na waongoza watalii Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu,

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya viwango vya malipo ya ujira kwa wapagazi, wapishi na waongoza watalii katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. Aidha, katika kutatua changamoto hizo, Wizara kwa kushirikiana na vyama vya mawakala wa utalii yaani waajiri imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali kwa ajili ya kufanya maboresho ya viwango hivyo vya malipo ya ujira.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua hiyo, Wizara imefanya kikao na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na kujadili kuhusu viwango vya ujira kwa wapagazi, wapishi na waongoza watalii.

Mheshimiwa Spika, hatua inayofuata ni Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kufanya kikao kazi baina ya wadau hao na waajiri wao kwa lengo la kupendekeza viwango stahiki, ili viweze kuwasilishwa katika Bodi ya Utatu yenye dhamana ya kumshauri Waziri mwenye dhamana ili makubaliano hayo yawe ya kisheria. Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika katikati ya Novemba, 2023 kule Arusha.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani wa kupunguza athari hasi zitakazojitokeza kutokana na kuondolewa kwa buffer zone katika hifadhi na mapori?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maeneo ya kinga za hifadhi za wanyamapori husaidia wanyamapori kupata mahitaji yao ikiwemo malisho na hivyo kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

Mheshimiwa Spika, katika kupunguza athari za kutokuwa na maeneo ya kinga, Wizara kupitia taasisi zake za uhifadhi (TANAPA, TAWA na NCAA) inatoa elimu kwa wananchi kuhusu kutokuanzisha shughuli za kibinadamu kama vile kilimo na makazi kwenye maeneo ya karibu na hifadhi ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori.

Vilevile kuwaelimisha kuanzisha shughuli rafiki kama vile ufugaji nyuki kwenye maeneo hayo. Sambamba na hatua hiyo, jitihada za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu zinafanyika ili kulinda wananchi na mali zao.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kugawa mizinga ya nyuki ili kubadili shughuli za kiuchumi zinazoharibu mazingira kama kukata miti na mkaa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ugawaji wa mizinga na vifaa vingine ni mojawapo ya mikakati ya Serikali katika jitihada za kuwezesha makundi mbalimbali ya kijamii kushiriki katika shughuli za ufugaji wa nyuki hapa nchini. Zoezi la ugawaji wa mizinga lina lengo la kuchochea ufugaji nyuki kwa jamii hasa zile zinazoishi jirani na maeneo yaliyohifadhiwa ili ziweze kujipatia kipato na kuachana na shughuli zinazoharibu mazingira kama kukata miti na kuchoma mkaa.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuimarisha uhifadhi wa maeneo mbalimbali ambapo kupitia Mradi wa REGROW imetoa elimu ya Ufugaji nyuki kwa jamii ya Tungamalenga na kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imepanga kuwagawia mizinga 50 kwa kikundi cha Subira kilichopo Wilaya ya Iringa. Vilevile elimu ya ufugaji nyuki imeendelea kutolewa kwa jamii zinazozunguka hifadhi ambapo kupitia elimu hiyo wananchi wamefundishwa namna bora ya kufanya shughuli za ufugaji nyuki kwa tija.

Mheshimiwa Spika, mathalan kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Wizara ilitoa mizinga 269 yenye thamani ya shilingi milioni 26.9 kwa vikundi 19 vya wafugaji wa nyuki katika Wilaya za Iringa, Kilolo na Mufindi. Vilevile Mfuko wa Misitu Tanzania umetoa ruzuku ya shilingi millioni 20 kwa vikundi viwili vya ufugaji Nyuki vilivyopo Wilaya ya Iringa. Pia, wadau wa maendeleo wametoa mizinga 260 kwa wafugaji nyuki katika Mkoa wa Iringa.

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo, itaendelea kutoa elimu ya uhifadhi na mbinu bora za ufugaji nyuki ili jamii iweze kufuga nyuki kibiashara. Aidha, Mfuko wa Misitu Tanzania umekuwa ukitoa tangazo na kupokea maombi ya ruzuku zitolewazo kwa wadau wa misitu na ufugaji wa nyuki. Hivyo, Mfuko unaendelea kupokea maombi ambayo yanachakatwa ili waombaji waweze kunufaika na ruzuku hizo ikiwemo kupatiwa mizinga ya kufugia nyuki.
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: -

Je, lini Serikali itawamegea eneo Wananchi wa Visiwa vya Maisome katika Hifadhi ya Kisiwa cha Maisome?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mhehimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo: -

Mhehimiwa Mwenyekiti, katika kutatua changamoto ya mwingiliano wa shughuli za uhifadhi na zile za kibinadamu, Serikali iliwasilisha taarifa ya umuhimu wa kumega hifadhi hiyo kama sehemu ya utatuzi wa migogoro ya Vijiji 975. Katika maelekezo ya Baraza la Mawaziri; Baraza liliridhia hifadhi imegwe na vijiji kupatiwa maeneo ya kuendeshea shughuli zao kwa uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshachukua hatua katika kutekeleza maelekezo ya Baraza la Mawaziri kwa kufanya mapitio ya mpaka wa msitu wa Hifadhi ya Maisome ambapo hekta 2,943.8 zimetolewa kwa wananchi na eneo hilo na kubakiwa na hekta 9,319.2. Kwa sasa taratibu za kubadili mpaka kisheria na kupata ramani mpya zinaendelea. Mara zoezi hilo litakapokamilika, Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi watajulishwa ambapo watakuwa na muda wa siku 90 kutoa maoni yao kabla ya tangazo rasmi la kutangaza eneo jipya la hifadhi baada ya mabadiliko niliyoyasema hapo juu.