Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Khamis Mtumwa Ali (4 total)

MHE. KHATIB SAID HAJI (K.n.y. KHAMIS MTUMWA ALI) aliuliza:-
Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inafanya ukaguzi katika Taasisi za Tanzania Bara na Zanzibar:-
Je, Ofisi hii inashirikiana vipi wakati wa kufanya ukaguzi wa Taasisi za Muungano na Ofisi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khamis Mtumwa Ali, Mbunge wa Jimbo la Kiwengwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inafanya ukaguzi katika Taasisi zote za Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Ibara ya 143 (2)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya mwaka 1977. Ibara hiyo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, mamlaka ya kufanya ukaguzi wa hesabu za mihimili yote mitatu ya dola, Serikali, Bunge na Mahakama na kutoa ripoti ya ukaguzi angalau mara moja kila mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mipaka ya kufanya kazi baina ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Jukumu la ukaguzi wa Taasisi za Muungano lipo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Wakati jukumu la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Zanzibar ni kukagua Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mipaka hiyo ya kazi, kumekuwepo na ushirikiano katika kufanya ukaguzi wa pamoja kati ya Ofisi hizi kuu mbili kwa lengo la kujenga uwezo na kubadilishana uzoefu. Kwa mfano ukaguzi wa ujenzi wa Ofisi za Wabunge kwenye Majimbo, ukaguzi wa bahari ya kina kirefu na mradi wa kupambana na UKIMWI Zanzibar. Ukaguzi wa miradi hii ulifanywa kwa ushirikiano wa pande zote mbili.
MHE. KHAMIS M. ALI aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa baadhi ya wakuu wa Vituo vya polisi hasa Zanzibar hutumia pesa ao za mishahara kulipa huduma za umeme katika vituo hivyo;
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwalipa au kuwarejeshea pesa wanazotumia kulipa umeme katika vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khamisi Mtumwa Ali Mbunge wa Kiwengwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikirejesha fedha hizo za umeme endapo askari amelipia au amenunua umeme kwa ajili ya kituo cha polisi kwa kupitia utaratibu wa kujaza fomu za madai na kuambatisha risiti ya malipo hayo kisha kuziwasilisha kwa mhasibu kwa ajili ya malipo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Wizara yangu imekuwa ikijitahidi kupeleka fedha za kulipia umeme kwa wakati ili kuondoa usumbufu unaojitokeza kwa askari walioko vituoni na makambini kadri ya hali ya uwezo utakapokuwa unaruhusu.
MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI (K.n.y. MHE. KHAMIS MTUMWA ALI) aliuliza:-

Serikali ilizuia sherehe za kuadhimisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuelekeza kusheherekea kwa kufanya usafi wa mazingira. Wakati zuio hilo linatolewa maandalizi ya sherehe hizo yalikwishaanza na gharama mbalimbali zilitumika ikiwemo mafunzo ya halaiki ya watoto:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwafidia wale waliotumia gharama binafsi wakiwemo wakufunzi wa maandalizi ya sherehe hizo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khamis Mtumwa Ali, Mbunge wa Kiwengwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maadhimisho ya sherehe za miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 2016 yalifanyika kwa wananchi kupumzika siku hiyo na kuendelea kutafakari umuhimu wa Muungano wetu ambao unazidi kuimarika na hivyo kufanya shughuli mbalimbali kama vile usafi wa mazingira, kujitolea katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali haina kumbukumbu zozote za watu binafsi waliotumia rasilimali zao kwa maandalizi ya sherehe hizo. Maandalizi hufanyika baada ya idhini kutolewa na viongozi wakuu hivyo hakuna mtu, kikundi au taasisi itakayofidiwa kwa namna yoyote ile.
MHE. KHAMIS MTUMWA ALI aliuliza:-
Taasisi za Muungano zinafanyiwa ukaguzi na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Je, ni mara ngapi Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imeshirikiana na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukagua Taasisi za Ubalozi zilizoko nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khamis Mtumwa Ali, Mbunge wa Kiwengwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali imeanzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambapo majukumu ya ofisi hii yameainishwa katika Ibara ya 143(2) ya Katiba hiyo, ambayo inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi angalau mara moja kila mwaka na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali, Bunge na Mahakama. Aidha, majukumu hayo pia yameanishwa katika kifungu cha 10 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 na Kanuni zake za mwaka 2009.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukaguzi wa Balozi unafanyika chini ya Fungu 34, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, kwa kuwa na Ofisi zote za Ubalozi ni sehemu ya Fungu 34. Hivyo basi, ukaguzi wa Balozi kama ilivyo kwa taasisi nyingine za Muungano unafanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali wa Zanzibar majukumu yake yameanishwa kwenye Ibara ya 112(3) ya Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1984. Kutokana na maelezo hayo Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kila moja ina mipaka yake ya kufanya ukaguzi. Jukumu la ukaguzi wa taasisi za Muungano lipo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijawahi kumhusisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ukaguzi wa Balozi au ukaguzi wowote ule kama wa Umoja wa Mataifa kwa sababu hakuna ulazima wa kufanya hivyo kikatiba na kisheria. (Makofi)