Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Abdallah Haji Ali (4 total)

MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS (K.n.y MHE. ABDALLAH HAJI
ALI) aliuliza:-
Usafiri wa bodaboda unatoa ajira kwa vijana walio wengi na kurahisisha usafiri, lakini zimekuwa zikisabaisha ajali nyingi mara kwa mara:-
Je, ni watu wangapi wamepoteza maisha na wangapi wamejeruhiwa na ajali za pikipiki kuanzia mwaka 2010 hadi 2017?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu ndugu yangu Abdallah Haji Ali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pikipiki za matairi mawili yaani bodaboda na matairi matatu yaani bajaji zilianza kutumika kubeba abiria kuanzia mwaka 2008. Mwaka 2010 Serikali ilipitisha kanuni na masharti ya usafirishaji wa pikipiki pamoja na bajaji. Aidha, katika kipindi hicho hakukua na utaratibu wowote wa kusimamia biashara ya uendeshaji pikipiki pamoja na bajaji zinazobeba watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha kuanzia Januari, 2010 hadi Februari, 2017 kumekuwa na jumla ya ajali 31,928 zilizosababisha vifo vya watu 6,529 na majeruhi 30,661.
MHE. ABDALLA HAJI ALI aliuliza:-
Uzalishaji wa mafuta na gesi ni suala la Muungano na kwa kuzingatia ukweli kwamba visima vya gesi vya songosongo na Mnazi Bay Mkoani Lindi na Mtwara vimekuwa vikizalisha gesi muda mrefu sasa:-
(a) Je, uzalishaji wa gesi kwa siku kwa visima hivyo ni mita za ujazo kiasi gani?
(b) Je, tangu uzalishaji ulipoanza mapato ya fedha yamekuwa kiasi gani kwa mwaka na yanatumikaje?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y WAZIRI WA NISHATI NA MADINI) alijibu:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdalla Haji Ali, Mbunge wa Kiwani, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wastani jumla ya futi za ujazo milioni 145 za gesi asilia huzalishwa kwa siku katika visima vya uzalishaji gesi asilia vya Songosongo na Mnazi Bay ambako kiasi cha futi za ujazo milioni 90 huzalishwa kwenye visima vya Songosongo na kiasi cha futi za ujazo milioni 55 huzalishwa katika visima vya Mnazi Bay.
Mheshimiwa Naibu Spika, gesi asilia inayozalishwa hutumika kuzalisha umeme katika mitambo ya SONGAS megawatt 189; Kinyerezi, megawatts 150; Ubungo I megawatts 102; Ubungo II megawatts 129; Somangafungu megawatts 7.5; Tegeta megawatts 45; na Mtwara megawatts 18. Aidha, kiasi kingine cha gesi asilia hutumika kama chanzo cha nishati kwenye viwanda 42 vilivyounganishwa pamoja na matumizi madogo kwenye nyumba kwa ajili ya kupikia na kuendeshea magari.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha jumla ya shilingi bilioni 488 zimekusanywa kutoka kwenye mauzo ya gesi asilia kwa miaka sita tangu 2011 hadi 2016 sawa na wastani wa kiasi cha shilingi bilioni 81.3 kwa mwaka. Mapato haya huwasilishwa Hazina kwa mujibu wa taratibu husika.
MHE. ALI SALIM KHAMIS (K.n.y. MHE. ABDALLAH HAJI ALI) aliuliza:-
Mfumo wa vyama vingi Tanzania ulirudishwa nchini hata baada ya Tume ya Nyalali kubaini ni asilimia ishirini tu ya Watanzania ndio waliotaka mabadiliko.
(a) Je, baada ya miongo miwili na nusu ni faida gani za mfumo huo zilizopatikana?
(b) Je, ni changamoto zipi ambazo zimejitokeza na kuwa mtihani katika suala hili la vyama vingi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Haji Ali, Mbunge wa Kiwani lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kama ilivyokuwa mfumo wa demokrasia ya chama kimoja cha siasa una faida na changamoto zake. Tangu mfumo huo uliporejeshwa mwaka 1992 kumekuwa na faida zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; mfumo umewezesha kupanuka kwa wigo wa demokrasia ya siasa ya vyama vingi ambapo hadi sasa kuna vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; kuongezeka kwa ushiriki wa wananchi katika chaguzi za kisiasa kwa ngazi zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu; kumekuwepo kwa ongezeko la uhuru wa kuchagua wagombea wa vyama vya siasa vilivyonadi na kushindanisha sera zao wakati wa kampeni za uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne; ni kuongezeka kwa uwazi na uwajibikaji katika utendaji wa Serikali.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizojitokeza zikiambatana na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; ni kuongezeka kwa gharama za kuendesha chaguzi za kisiasa katika ngazi mbalimbali za uchaguzi. Aidha, kuongezeka kwa gharama za ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu na uwakilishi Bungeni na katika ngazi ya Serikali za Mitaa wawakilishi katika Baraza la Madiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; kuibuka kwa makundi ndani ya baadhi ya vyama vya siasa ambapo viongozi wamekuwa hawafanyi siasa za kistaarabu na kuchochea vurugu katika jamii, hasa nyakati za Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge, Chaguzi ndogo za marudio pamoja na Chaguzi za ngazi ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu; ni kushuka kwa uzalendo wa wananchi kutokana na baadhi ya wanasiasa kushabikia mitazamo na kampeni hasi dhidi ya Serikali iliyopo madarakani.
MHE. ABDALLAH HAJI ALI aliuliza:-

Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo (CDCF) hutolewa kila mwaka kwa Majimbo yote ya Uchaguzi Tanzania lakini fedha hizi zimekuwa zikichelewa sana kutolewa kwa upande wa Zanzibar tofauti na Tanzania Bara:-

Je, ni sababu zipi za msingi zinazofanya fedha za mfuko huo kuchelewa kupelekwa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba nichukue fursa hii kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Haji Ali, Mbunge wa Kiwani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ulianzishwa kwa lengo la kuchochea maendeleo ya Majimbo ya Uchaguzi ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutokana na makubaliano hayo, Sheria Na.16 ya mwaka 2009 ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo katika kifungu cha 3 inamtaja Waziri anayehusika na Mfuko huo kuwa ni Waziri anayehusika na masuala ya Serikali za Mitaa.

Aidha, kifungu cha 4(2) cha Sheria kinasema kwamba, kwa upande wa Tanzania Bara ni Waziri anayehusika na Serikali za Mitaa na kwa upande wa Zanzibar ni Waziri anayehusika na masuala ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka 2010, Ofisi ya Makamu wa Rais ameratibu na kufuatilia miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa upande wa Zanzibar. Mchanganuo wa mgawanyo wa fedha kwa kila Jimbo kulingana na vigezo vilivyoainishwa vya idadi ya watu katika Jimbo, ukubwa wa eneo na kiwango cha umaskini hufanywa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kuwasilishwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zinatakiwa kufuata utaratibu wa mgawanyo kama nilivyoeleza. Utaratibu huo ni kama ifuatavyo: Fedha zinatolewa na Wizara ya Fedha na Mipango (SMT), baada ya kutolewa, Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hufanya mchanganuo wa kila Jimbo, mchanganuo huo huwasilishwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambapo huwasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango ya SMZ. Wizara ya Fedha na Mipango ya SMZ ndiyo inayoingiza fedha kwenye akaunti za majimbo ya Zanzibar. Hivyo, ni dhahiri kuwa hatua hizo zinaweza kusababisha ucheleweshaji wa fedha ikilinganishwa na fedha zinazotolewa katika majimbo ya Tanzania Bara. Hata hivyo, jitihada za makusudi zinafanyika ili kuhakikisha fedha hizo zinaingia kwenye akaunti za majimbo ya Zanzibar kwa wakati.