Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Halima James Mdee (8 total)

MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE) aliuliza:-
Serikali ilitoa kauli kuwa itapanga gharama za karo elekezi kwa shule zote za binafsi hapa nchini:-
(a) Je, Serikali imegundua kiwango cha gharama kwa kila mwanafunzi (unit cost) kwa shule za bweni na za kutwa ni kiasi gani?
(b) Je, kiwango hiki hakitasababisha kuporomoka kwa ubora wa elimu ambayo ilikuwa ikitolewa hapo awali na shule binafsi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Kawe, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imefanya utafiti kuhusu gharama za kumsomesha mwanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari. Kupitia utafiti huo, imebainika kuwa ada zinazotozwa katika shule za binafsi zinatofautiana kwa kiasi kikubwa kulingana na huduma zinazotolewa, aina ya shule na miundombinu iliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utafiti huo, Wizara yangu ilifanya mazungumzo na baadhi ya taasisi zinazosimamia shule zisizo za Kiserikali na kukubaliana namna ya kufikia viwango vya ada elekezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, taasisi ambazo tumefanya nazo mazungumzo ni pamoja na Umoja wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), Kamisheni ya Huduma za Jamii za Kikristo (CSSC) na Baraza la Sunna Tanzania (BASUTA). Kutokana na tofauti za ubora na idadi ya huduma zinazotolewa na shule, Wizara sasa imeanza zoezi la kupanga shule hizi kwa makundi ili kuweka viwango vya ada kwa kuzingatia ubora na huduma na hivyo kutoathiri kiwango cha elimu inayotolewa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inatarajia kuwa utaratibu wa ada elekezi hautaathiri ubora wa elimu katika shule binafsi kwa sababu ada hiyo itapangwa kulingana na ubora na huduma na miundombinu iliyopo shuleni.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
Serikali iliwaahidi wananchi wa Jimbo la Kawe kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Chuo Kikuu cha Ardhi - Makongo - Goba na barabara ya Tegeta Kibaoni - Wazo Hill – Madale:-
Je, ni lini ujenzi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Kawe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Chuo Kikuu cha Ardhi - Makongo - Goba pamoja na barabara ya Tegeta Kibaoni - Wazo Hill - Madale Goba ni kati ya barabara ambazo zimo kwenye mpango wa Serikali wa ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam ambao utekelezaji wake ulianza mwaka 2010 na unagharamiwa na Serikali za Tanzania kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambazo ujenzi wa kiwango cha lami umekamilika ni Ubungo Bus Terminal - Kigogo Roundabout ambayo ni kilomita 6.4, Ubungo Maziwa - Mabibo External kilomita 0.65 na Jet Corner - Vituka - Davis Corner ambayo ni kilomita10.3. Aidha, barabara zinazoendelea kujengwa ni pamoja na Tangibovu - Goba kilomita 9, Kimara Baruti - Msewe - Changanyikeni kilomita 2.6, Kimara - Kilungule - External kilomita 9 na Tabata Dampo - Kigogo kilomita 2.25.
Mheshimiwa Naibu Spika, usanifu wa kina wa barabara ya Tegeta Kibaoni - Wazo Hill -Madale - Goba na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi umekamilika. Aidha, usanifu wa kina wa barabara ya Chuo Kikuu cha Ardhi - Makongo - Goba utafanyika sambamba na ujenzi wa barabara hiyo yaani design and build.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara za Chuo Kikuu cha Ardhi - Makongo - Goba na Tegeta Kibaoni - Wazo Hill - Madale - Goba umepangwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
Jimbo la Kawe ni miongoni mwa Majimbo ambayo (baadhi ya maeneo) yamekuwa yanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama kwa kipindi kirefu ambayo ni Kata ya Mabwepande (Mtaa wa Mbopo, Mabwepande na Kinondo), Kata ya Makongo (Mtaa wa Changanyikeni na baadhi ya maeneo ya Mtaa wa Makongo Juu), Kata ya Wazo, Mbweni na Mbezi Juu; na changamoto hii sugu ilitarajiwa kupungua na kumalizika kabisa baada ya mradi mkubwa wa maji wa Ruvu chini kukamilika ambao kwa sasa tayari umeshakamilika:-
(a) Je, mikakati ya usambazaji maji pamoja na Mabomba (katika maeneo ambayo hayana mtandao wa mabomba) ikoje ili kutatua kero husika?
(b) Je, ni miradi gani inayotarajiwa kutekelezwa, muda wa utekelezaji, gharama za kila mradi na nani anayewajibika katika utekelezaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mkubwa wa maji wa Ruvu Chini umekamilika na umeanza kutumika rasmi tarehe 23 mwezi Machi, 2016. Mradi huu ulihusu upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini na ujenzi wa Bomba kuu kutoka Ruvu Chini kwenda Dar es Salaam. Hivi sasa uzalishaji wa maji kutoka Ruvu Chini ni mita za ujazo milioni 270 kwa siku ikiwa ni ongezeko la mita za ujazo milioni 90 kwa siku. Kutokana na kukamilika kwa mradi huu, kumekuwa na ongezeko la upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa hayapati maji licha ya kuwa na mabomba ya DAWASCO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Kwanza, Serikali inatekeleza mradi wa uboreshaji na usambazaji wa maji unaogharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 32.772 kutoka Benki ya Exim-India. Katika Jimbo la Kawe la Mheshimiwa Mbunge, mradi huu utatekelezwa katika maeneo ya Changanyikeni, Makongo, Salasala, Wazo, Tegeta, Ununio, Bunju na Mabwepande. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kusukumia maji katika Kata ya Mabwepande na matanki ya kuhifadhia maji katika Kata za Makongo na Wazo pamoja na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu utatekelezwa kwa muda wa miezi 15 chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA).
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-
Barabara mpya ya Mwenge - Tegeta kwa kiwango fulani imesaidia kupunguza tatizo la foleni ingawa ina changamoto kadhaa kama kukosekana kwa taa za kuongoza magari kunakosababisha ajali za mara kwa mara; nyakati za mvua barabara hujaa maji sababu ya udogo wa mapokeo na matoleo ya maji ya mvua hususan eneo la Makonde - Mbuyuni hali inayohatarisha uhai wa wananchi na barabara yenyewe; kuna maeneo hatarishi sana ambayo Serikali inatakiwa ama kuweka matuta au vivuko vya waenda kwa miguu ili kuzuia ajali, miongoni mwa maeneo hayo ni eneo la Bondeni (Jeshini Kata ya Mbezi Juu) karibu na njia panda ya kwenda Kawe:- Je, ni lini changamoto hizi zitapatiwa ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge Halima James Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua umuhimu wa taa za kuongoza magari kwenye makutano ya barabara zetu ili kusaidia kupunguza ajali hususan barabara ya Mwenge -Tegeta. Mkandarasi wa ujenzi wa taa za kuongoza magari kwenye makutano ya Afrikana tayari amepatikana na anatarajia kuanza kazi wakati wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu udogo wa mapokeo na matoleo ya maji ya mvua yanayosababisha kero katika eneo la Makonde hadi Mbuyuni, Serikali inakamilisha taratibu za kusaini mkataba wa ujenzi wa mtaro mkubwa eneo la Mbezi Samaki Wabichi ambao utatatua kero ya barabara kujaa maji nyakati za mvua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la kivuko cha waenda kwa miguu eneo la Kawe Bondeni hadi Jeshini, Kata ya Mbezi Juu na Kawe tayari limeshapatiwa ufumbuzi. Serikali itajenga daraja la juu kwa ajili ya kivuko cha waenda kwa miguu (Over- Head Pedestrian Bridge) eneo la Kawe Bondeni. Kwa sasa mkandarasi wa kujenga daraja hilo yupo kwenye hatua za maandalizi (mobilization) kwa ajili ya kuanza ujenzi.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA (K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE) aliuliza:-
Kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu sana unaohusu eneo lenye ukubwa wa ekari 357.5 Boko Dovya – Kawe – Kinondoni baina ya wananchi na watu wanaojitambulisha kuwa wamiliki halali wa eneo hilo maarufu kama SOMJI; wananchi katika hatua mbalimbali wamepeleka malalamiko Serikalini kuanzia ngazi ya Wilaya, Wizara ya Ardhi na hata kwa Waziri Mkuu lakini mpaka sasa hakuna utatuzi uliofanyika.
Je, hatua gani zimeanza kuchukuliwa ili kero hiyo ya muda mrefu imalizike?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali namba 17 la Mheshimiwa Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, awali shamba hili lililokuwa na ukubwa wa ekari 366 Mbweni maarufu kama Somji Farm lilipimwa na upimaji namba E7/37F na kupewa namba ya upimaji 10,917 ya tarehe 15 Agosti, 1959. Baada ya upimaji shamba lilimilikishwa kwa Ndugu Hussein Somji pamoja na Ndugu Munaver Somji mwaka 1961 na baadae kuandaliwa hati iliyosajiliwa kwa namba 14,573 ya kipindi cha miaka 99.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya shamba hilo, ekari 5.8 zilitwaliwa kwa matumizi mahususi ya Serikali mwaka 1975 na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 670 la tarehe 30 Mei, 1975. Aidha, sehemu iliyobaki yenye ekari 357.5 ilitwaliwa na Serikali tena mwaka 2002 na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 617 la tarehe 27, Septemba, 2002 kwa ajili ya kutumika katika mradi wa viwanja 20,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo eneo hilo halikuingizwa kwenye mradi kutokana na sehemu kubwa kuwa imevamiwa na wananchi. Pamoja na uvamizi huo, wamiliki wa awali walifungua mashauri mahakamani dhidi ya Serikali kupinga eneo lao kutwaliwa; shauri la Kikatiba namba moja la 2003 na shauri la Kikatiba namba 40 la 2010. Uwepo wa mashauri haya ulikwamisha juhudi za Serikali kushughulikia mgogoro huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni mara kadhaa imekaa na wahusika kwa lengo la kuweka utaratibu utakaowezesha wamiliki wa awali kulipwa fidia stahiki kwa fedha iliyopatikana kutokana na wanachi ambao watatakiwa kurasimishiwa maeneo waliyojenga.
Hata hivyo changamoto iliyopo ni katika kumilikisha makubaliano haya kwa wananchi kupitia kamati yao waliyounda, kutokuwa tayari kuchangia gharama za kurasimisha eneo hilo. Jitihada zaidi za wadau wengine akiwemo Mbunge zinahitajika katika kuwaelimisha wananchi kupitia Kamati yao kuwa tayari kushiriki katika upatikanaji wa ufumbuzi wa suala hili.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA (K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE) aliuliza:-
Baadhi ya maeneo katika Jimbo la Kawe yanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama kwa kipindi kirefu. Maeneo kama Kata ya Mabwepande (Mtaa wa Mbojo, Mabwepande, Kinondo); Kata ya Makongo (Mtaa wa Changanyikeni na baadhi ya maeneo ya Mtaa wa Makongo Juu); Kata ya Wazo, Mbweni na Mbezi Juu na changamoto hii sugu ilitarajiwa kupungua na kumalizika kabisa baada ya mradi mkubwa wa maji wa Ruvu Chini kukamilika ambao kwa sasa tayari umeshakamilika.
• Je, mikakati ya usambazaji maji pamoja na mabomba katika maeneo ambayo hayana mtandao wa mabomba ikoje ili kutatua kero husika?
• Je, ni miradi gani inayotarajiwa kutekelezwa, muda wa utekelezaji, gharama za kila mradi na nani anayewajibika katika utekelezaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wananchi wa Dar es Salaam hususan maeneo ambayo hayakuwa na mtandao wanaondokana na kero ya kutopata huduma ya maji, Serikali katika awamu ya kwanza kupitia DAWASA inakamilisha ujenzi wa matanki na mabomba makuu ya kupeleka maji katika maeneo ya miinuko ya Changanyikeni, Wazo na Salasala. Aidha, awamu hii pia itahusu ujenzi wa mtandao wa maji Kata ya Kiluvya na Mbezi Luisi. Mradi huu unatekelezwa chini ya ufadhili wa mkopo wa masharti nafuu kutoka India kwa gharama ya dola za Kimarekani milioni 32.772. Hadi sasa utekelezaji wa awamu ya kwanza umefikia asilimia 82 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2018. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, awamu ya pili ya utekelezaji itahusu ujenzi wa mabomba madogo madogo ya kusambaza maji na kuunganisha wateja katika maeneo yote kuanzia Changanyikeni, Bunju hadi Bagamoyo. Ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kuanzia mwezi Julai, 2018 na unatekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia kwa gharama ya dola za Marekani milioni 45. Mradi huu utatekelezwa kwa miezi 15. Zabuni ya ujenzi wa mradi huo itatangazwa hivi karibuni baada ya kupata kibali kutoka Benki ya Dunia.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE) aliuliza:-

Mwezi Novemba, 2018, Rais aliutangaza ulimwengu kwamba Serikali yake itanunua korosho zote kwa bei isiyopungua shilingi 3,000/= kwa kilo.

(a) Je, mpaka sasa ni kiasi gani kimetumika na kimetoa chanzo kipi na je, tani ngapi zimenunuliwa?

(b) Je, Wakulima/Vyama vya Msingi vingapi vimelipwa na vingapi bado havijalipwa?

(c) Je, zoezi hilo linatarajiwa kukamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Jimbo la Kawe lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, makadirio ya uzalishaji wa korosho msimu wa 2018/2019 ni zaidi ya tani 240,000 za korosho ghafi. Hadi kufikia tarehe tarehe 30 Januari, 2019, Serikali imekusanya jumla ya tani 214,269.684 za korosho ghafi zenye thamani ya Sh.707,089,957,200 sawa na asilimia 89.3 ya lengo la uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, ununuzi wa korosho unafanywa na Taasisi ya Serikali ya Bodi ya Nafaka na mazao mchanganyiko ambapo malipo yaliyolipwa na kuingizwa kwenye akaunti za wakulima hadi tarehe 30 Januari, 2019 ni kiasi cha Sh.424,849,405,110 zilizotokana na korosho za wakulima kiasi cha tani 134,535,904. Aidha Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko ni Taasisi ya kibiashara yenye lengo la kupata faida na mtaji wake unatokana na ruzuku kutoka Serikali na mikopo kutoka Taasisi kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), NMB, CRDB na Benki zinginezo.

(b) Mheshimiwa Spika, jumla ya wakulima laki 390,466 wamekwishalipwa hadi kufikia tarehe 30 Januari 2019. Aidha Vyama vya Msingi 603 vimelipwa kati ya Vyama vya Msingi 605 vilivyohakikiwa.

(c) Mheshimiwa Spika, zoezi la operesheni korosho linaendelea vizuri na linatarajia kukamilika ifikapo tarehe 15 Februari, 2019.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:-

Jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na tatizo sugu la uchimbaji mchanga na uchafu uliokithiri;

Je, Serikali ina mikakati gani ya muda mfupi na muda mrefu kukabiliana na kero hiyo sugu na hatarishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ridhaa yako naomba kwanza nichukue fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa George Simbachawene kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, lakini pia Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Maziringira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Kawe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna changamoto kubwa ya uchimbaji wa mchanga Dar es Salaam. Aidha, yapo machimbo ya mchanga yaliyoruhusiwa kisheria na kupata vibali kutoka mamlaka husika kama Serikali za Mitaa (Halmashauri za Jiji na Manispaa), Ofisi za Mamlaka ya Mabonde na Wizara ya Madini. Hata hivyo, upo uchimbaji holela hususan katika maeneo ya mito na machimbo mengine ya mchanga ambayo si rasmi yanayoanzishwa na wananchi katika maeneo mbalimbali. Uchimbaji wa madini ya mchanga usio rasmi ni kosa kwa mujibu wa Kifungu 6 (1) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchimbaji huu huleta athari ikiwa ni pamoja na mmomonyoko wa kingo za mito, uharibifu wa maji na miundombinu, mwingiliano wa maji ya bahari katika nchi kavu (sea water intrusion), kubadilika kwa mkondo wa mto kutoka uelekeo wa asili, kuharibika kwa uimara wa mto (channel instability), uharibifu wa mimea ya asili ambayo husaidia kupunguza mmomonyoko na uharibifu wa mazalia ya viumbe hasa wakati kina cha maji kinapoongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na hili hatua zifuatazo zinachukuliwa:

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kuelimisha wananchi kuhusu athari za uchimbaji holela wa mchanga na kuzuia uchimbaji holela. Aidha, mamlaka mbalimbali zikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, Mamlaka za Mabonde na Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Madini Mkoa wa Dar es Salaam zimekuwa zikifanya ukaguzi wa mara kwa mara na hatua stahiki kwa mujibu wa sheria
huchukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, Serikali inaandaa mkakati wa muda mrefu utakaotokana na Mapendekeo ya Kamati Maalum ya Wadau iliyoundwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupendekeza hatua za kuchukuliwa ili kuwa na uchimbaji endelevu wa mchanga usiokiuka sheria za nchi; na kufanya tafiti na kuendeleza teknolojia za ujenzi zinazoweza kutumia mchanga kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchafuzi wa mazingira uliokithiri, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 Kifungu 139(1) imetoa mamlaka kwa Serikali za Mitaa kuzuia au kupunguza taka ngumu, taka vimiminika, gesi taka na taka zenye madhara. Serikali itaendelea kuelimisha wananchi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria. Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia programu ya Elimu kwa Umma inatoa elimu kuhusu usimamizi na udhibiti wa taka kuanzia ngazi ya jamii, viongozi na wadau hasa katika eneo la urejelezaji wa taka ngumu. Natoa wito kwa Serikali za Mitaa kuwajibika kwa kuweka mipango endelevu na usimamizi wa taka kama ilivyobainishwa katika Kifungu 139(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004.