Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Katani Ahmadi Katani (1 total)

MHE. KATANI A. KATANI: Naitwa Katani Ahmad Katani, Mbunge wa Jimbo la Tandahimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Tandahimba ina vyanzo vingi vya maji ukiwepo Mto Ruvuma na Mahuta lakini bado wananchi wake wanapata tatizo kubwa la maji.
Je, Wizara ina utaratibu gani wa kuhakikisha inaleta mashine ikafunga pale watu wake wakapata maji ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pale Tandahimba kuna mto na ni kweli wana changamoto ya maji. Kama nilivyosema pale mwanzo kila jambo lazima tuwe na mchakato wa upatikanaji wa fedha.
Kwa suala hili katika kikao chetu cha juzi tulifanya maamuzi tukasema lazima Wizara ya Maji na TAMISEMI utendaji wetu wa kazi uwe wa karibu sana. Katika haya nini cha kufanya?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema kila Halmashauri kwanza angalau itenge bajeti ya kuanza kushughulikia yale mambo ya awali mfano kufanya upembuzi yakinifu sehemu ambayo chanzo cha maji kinaweza kupatikana. Hali kadhalika katika mchakato wa bajeti, naomba nizielekeze Halmashauri zote zihakikishe katika bajeti zao ajenda ya maji ni ya msingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba ajenda kubwa ya Serikali ni kuhakikisha inatatua tatizo la maji kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Katani hili ulilolizungumzia Serikali imesikia na inalichukua na lengo kubwa la Mheshimiwa Rais wetu amesema ni lazima tuhakikishe tunamtua ndoo mama, suala hili tutakwenda kulifanyia kazi.