Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Katani Ahmadi Katani (1 total)

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Waziri Mkuu, nakushukuru. Swali langu la nyongeza ni je, wale wakulima ambao korosho zao zimepotea zikiwa ghalani na Serikali ndiyo ilifanya uzembe kwa kuweka dhamana ndogo kwa mwendesha ghala, Serikali iko tayari sasa kuwalipa wakulima wale ambao pesa zao bado wanawadai?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Katani, Mbunge wa Tandahimba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli uko uendeshaji wa hovyo wa Vyama vya Msingi, pamoja na Vyama Vikuu, vinavyosimamia korosho na ndiyo sababu Serikali imesimamia kidete kwenye mazao yote; korosho, pamoja na mazao mengine, kuweka usimamizi wa dhati wa kuhakikisha kwamba wakulima sasa wanapata tija kwenye masoko ambayo wanapeleka mazao yao ili waanze kunufaika na mazao waliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Katani anataka kujua wale waliopoteza korosho. Mifumo inayotumika pale, mara nyingi haisimamiwi na Serikali bali na Vyama vyao wenyewe vya Ushirika ambapo wao wenyewe wamechagua ushirika wao, ukisimamiwa na Mrajisi ambaye ndiye pia tumemtaka asimamie kwa dhati namna ya kuuza mazao hayo, pamoja na kutafuta masoko yake ili
wakulima waweze kupata fedha. Sasa wakulima wote ambao wamepoteza korosho, wajibu wao wa kwanza ni kuwauliza viongozi wao wa Chama cha Msingi na Chama Kikuu, kupitia mikutano yao. Wanayo mikutano yao ya haki kabisa na ya msingi na wanayo nafasi ya kuwahoji viongozi wao wa ushirika wa Chama cha Msingi AMCOS pamoja na Chama Kikuu, kwa vyama vile vikuu vinavyoongoza zao hilo la korosho.
Mheshimiwa Spika, pale itakapoonekana hawajaridhika na majibu hayo, wanachama wenyewe wanao uwezo wa kuwapeleka Mahakamani ili Sheria iweze kufuata mkondo wake. Mahakama maamuzi yake yatakayotolewa, ndiyo yale ambayo yataweza kuwawajibisha viongozi wa hovyo, ambao pia wanawasababishia wakulima kupoteza mazao yao. Hii sasa siyo kwa korosho tu; kwa mazao kama pamba, tumbaku, kahawa; yote haya ni mazao ambayo yanauzwa kwa utaratibu ambao sasa tunataka tuusimamie, tuhakikishe kwamba wakulima wanapata tija. Mazao haya ndiyo yanaipatia pato Serikali, lakini wakulima ndiyo wanategemea sana katika kuendesha shughuli zao.