Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Haji Hussein Mponda (19 total)

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Niliuliza swali kwa niaba ya Mheshimiwa Obama mimi mwenyewe naitwa Dkt. Hadji Mponda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, kwa kuwa mkataba kati ya Halmashauri ya Buhigwe na ile Hospitali ya Mission umesitishwa kwa sababu ya fedha, sasa ni nini Serikali wana njia mbadala ya kutoa huduma za afya bure kwa makundi haya ya wazee na watoto?
Swali la pili, mkataba kama huo huo uliofanyika Buhigwe na mwaka 2011 - 2013 ulifanyika katika Wilaya ya Ulanga ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga waliingia mkataba na Hospitali ya Lugala, ni Hospitali ya Mission, lakini mkataba ule ulidumu kwa muda wa miezi sita mpaka leo umesitishwa. Sasa swali langu ni lini Halmashauri hiyo ya Malinyi pamoja na TAMISEMI wataufufua mkataba ule kwa kurudisha huduma hizi bure kwa makundi haya mawili ya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano?
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza katika sehemu ya (a) ni kwamba nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, mkataba huu haujasitishwa, kilichotokea ni kwamba kuna fedha za quarter ya kwanza ambayo imekuja mpaka mwezi Disemba ambapo tunarajia sasa kuna pesa zingine zitakuja mpaka hivi sasa na nimesema pale mwanzo kwamba matarajio zile pesa zikishafika Halmashauri, basi lazima zielekezwe katika sehemu hizi tatu ilimradi wananchi waendelee kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili, kwa sababu hili ni suala la Hospitali ya Lugala Mission sijakuwa na taarifa nayo za kutosha, lakini nina imani kwamba mikataba yote kilichozingatiwa ni kwamba, inakwenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwezekano ni kwamba naomba nishauri hasa Baraza la Madiwani hasa katika vikao vyao vya Kamati ya Fedha. Lazima fedha zinapokuja, wasimamie fedha hizi maelekezo yake ni wapi, kwa sababu sehemu zingine inawezekana fedha zikapita lakini watu katika kufanya maamuzi wakaelekeza pesa sehemu ambazo siyo muafaka mwisho wake wakati mwingine mikataba inavunjika wakati kumbe kuna watu hawajatimiza majukumu yao. Imani yangu ni kwamba, kila mtu atatimiza wajibu wake ilimradi wananchi wetu waweze kupata huduma bora kwa ajili ya kuhakikisha afya ya mama na mtoto inaimarika katika nchi yetu.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Vile vile naishukuru Serikali kwa majibu mazuri kuhusu daraja hilo na mwendelezo wa ujenzi wake lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Daraja hili la Kilombero unahusisha pia ujenzi wa barabara zinazoingia kwenye daraja hilo. Barabara hizo za maingilio ya daraja zinaunganishwa na barabara itokayo kwenye mto huo kwenda Lupilo – Malinyi - Kilosa - Mpepo - Londo - Lumecha hadi kwa Mheshimiwa Naibu Waziri Namtumbo. Barabara hii niliyoitaja hadi sasa haipitiki kabisa kutokana na uharibifu mkubwa uliofanywa na mvua na mkandarasi yupo site hawezi akamaliza ukarabati wa uharibifu ambao umefanyika. Je, Serikali ina mpango gani wa dharura kusaidia kunusuru hali mbaya ya usafiri katika barabara hiyo ambayo nimeizungumzia?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kivuko cha Mto Kilombero baada ya kukamilika daraja lile, tumekubaliana kupitia Mfuko wa…
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Baada ya kukamilika kivuko kile tulikubaliana kiende kwenye Kivuko cha Kikove, je, ni lini Serikali wataanza ujenzi wa gati hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni jirani yangu lazima akiri kwamba, katika mipango ya kunusuru maeneo ya dharura hatuwezi tukaanza sisi majirani kwa sababu maeneo yenye matatizo ni mengi sana. Hata hivyo, simaanishi nawakatisha tamaa wananchi wa Namtumbo ambao ndiyo wamenileta hapa pamoja na majirani zao wa Malinyi, sina maana hiyo, maana yangu kubwa ni kwamba tatizo hili la kukatika mawasiliano ni la Tanzania nzima. Maadam mvua imeanza kupungua, tunaamini sasa kazi ya kurejesha mawasiliano itafanyika kwa kasi kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naomba nichukue nafasi hii kuwaelekeza TANROADS Mikoa yote sasa tuanze kuelekeza nguvu ya kurudisha mawasiliano katika maeneo yaliyokatika kwa sababu mvua sasa zimepungua. Fedha tutakazotumia hazitapotea bure kwa sababu mvua imepungua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili, naomba Mheshimiwa Dkt. Mponda turudi kule tulipokubaliana ambapo ilikuwa katika kikao cha Mkoa na sisi tuliwakilishwa na watu wa TEMESA tuangalie kama mahitaji ya TEMESA Mkoa hayatoshi, wao watatuletea Kitaifa halafu tutaangalia utekelezaji wa hilo suala.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali nayo pia imeahidi ujenzi wa barabara ya Ifakara – Lupilo – Malinyi – Londo - Lumecha - Namtumbo Songea katika kiwango cha lami. Sasa ni muda barabara hiyo bado haijaanza kujengwa.
Swali langu, ni lini sasa hii kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina itakamilika na barabara hii kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dokta Hadji Mponda, Mbunge wa Malinyi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie Wabunge wote wanaohusika na barabara hii ya kutoka Ifakara - Malinyi - Namtumbo - Songea kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kuanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Labda nimhakikishie tu kwamba kazi iliyofanyika hadi sasa ni kubwa. Unafahamu kwamba kipande kile cha kutoka Lumecha - Londo kimeshakamilika kwa maana kufunguliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile tumebakabiza kilometa 4 tu kukamilisha kuifungua hii barabara, wakati kazi ya feasibility study na detail design ikiendelea kufanyika. Nikuhakikishie kazi hii ya feasibility study na detail design pamoja na kipande hiki cha kilometa 4 kilichobaki cha kufunguliwa barabara hii itakamilika katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 unaoanza Ijumaa.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Migogoro ya ardhi ambayo inajitokeza kati ya hifadhi na wananchi nayo yanajitokeza katika Pori Tengefu la Bonde la Kilombero. Tumeiomba Serikali, naomba niwaulize hapa Serikali, ni lini sasa mtarudisha ardhi ile ya Buffer Zone katika Pori Tengefu la Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza niseme kwamba Buffer Zone tafsiri yake ya moja kwa moja isiyohitaji utaalam mwingi sana ni eneo ambalo linapaswa kuwa siyo la yeyote kati ya pande mbili zinazopakana. Eneo hilo kwa mujibu wa kanuni na taratibu, linapaswa kuwa ni eneo ambalo shughuli za uhifadhi zinakuwa mild, lakini pia shughuli za matumizi ya kibinadamu na zenyewe zinakuwa mild kwa maana ya kwamba siyo eneo ambalo linatumika moja kwa moja kwa asilimia mia moja na pande zote mbili zinazopakana. Kwa hiyo, kusema kwamba lirudishwe kwa wananchi, pengine inaweza kuwa siyo sahihi sana kwa sababu halijawahi kuwa kwa asilimia mia moja upande wa hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kusema na ninarudia tena, mazoezi haya yote ya kupitia hifadhi baada ya hifadhi; iwe hifadhi ya misitu, iwe hifadhi ya wanyamapori au hifadhi nyingine yoyote ile chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii; maeneo yote hayo yameorodheshwa kama sehemu ya migogoro ya ardhi na yameorodheshwa hivyo na Wizara ya Ardhi. Pia tunakwenda kufanya team work miongoni mwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi yenyewe, TAMISEMI, eneo ambalo sasa Mheshimiwa Mbunge atashirikiana na Serikali ya Wilaya pale, lakini pia Wizara ya Nishati na Madini, pale patakapokuwa panahusika na mambo ya madini; lakini pia masuala ya maji kwa sababu tunahusika pia. Kwa kutunza misitu tunatunza pia vyanzo vya maji, basi pale itakapobidi kwamba kuna chanzo cha maji tunataka kukifanya kiwe endelevu, kukilinda, basi na Wizara ya Maji itahusika. Kwa kuanzia ni Wizara hizo tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba wananchi wote na kupitia swali hili la Mheshimiwa Mbunge, wawe wavumilivu katika kipindi hiki ambacho ni kipindi cha mpito ambapo Serikali sasa inakwenda kutafuta majibu ya kudumu kwenye migogoro hii ya mipaka na hifadhi na migogoro ya ardhi kwa ujumla.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya wakazi wa Wilaya ya Malinyi, Wilaya ya Ulanga na Kilombero, tunaishukuru Serikali na tunawapa pongezi kutekeleza ahadi ambayo wametuahidi ya ujenzi wa daraja la Kilombero ambayo imekuwa jawabu kubwa la kero ya miundombinu katika Wilaya hizo tatu. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, ujenzi huo wa daraja la Kilombero unahusisha pia na barabara za maingilio na barabara hiyo ya maingilio inaunganisha barabara inayotoka Ifakara, Lupilo, Malinyi, Kilosa Mpepo, Londo, Lumecha, Namtumbo mpaka Songea. Barabara hii kipindi cha masika inachafuka sana kutegemea na mazingira ya mvua maeneo yale na inakuwa inapitika kwa tabu sana. Sasa, je, Serikali inajipangaje na ukarabati wa kudumu wa maeneo korofi katika barabara hiyo niliyotaja?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; barabara hii niliyotaja inajulikana kwa T16, barabara hiyo iko katika upembuzi yakinifu unaosanifu kwa kina ambao umekamilika. Barabara inatakiwa ijengwe kwa kiwango cha lami. Ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hiyo inayotoka Ifakara, inatobokea mpaka Songea ambayo itakuwa sio kwa ajili ya mkaazi wa Morogoro itasaidia pia na ndugu zetu majirani wa Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Njombe?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea kwa niaba ya Serikali pongezi alizotupa na kwa kweli ni wajibu wetu kutekeleza ahadi zote ambazo tumezitoa katika Ilani ya Uchaguzi ya 2015/2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoongelea nayo iko katika Ilani ya Uchaguzi ya 2015 hadi 2020 ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Upembuzi na usanifu wa kina haujakamilika – physically umekamilika lakini taarifa bado haijakamilika na tunatarajia hiyo kazi itakamilika mwezi Mei, 2017. Kwa sasa taarifa ya rasimu imeshawasilishwa TANROADS wanaipitia kwa kina ili hatimaye wamrudishie maoni yule Mhandisi Mshauri ambaye ni kampuni ya Kyong Dong na baada ya hapo ndio atakuja kukamilisha kuandika taarifa ya mwisho. Kwa ratiba ilivyo ataiwasilisha taarifa ya mwisho mwezi Mei, 2017. Baada ya hapo Serikali itaanza kujipanga kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la ukarabati wa maeneo korofi kwa sasa ili iweze kupitika muda wote; nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Hadji Mponda Mbunge wa Malinyi na wananchi wote wa Malinyi hadi Kilosa kwa Mpepo kwamba Serikali ina mkakati kabambe na kila mwaka tunatenga fedha na nafahamu mwaka huu kuna wakandarasi wawili wako site katika maeneo korofi wanafanyia ukarabati wa hali ya juu ili kuhakikisha barabara hiyo inapitika mwaka mzima bila matatizo.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo yanayowakumba wakazi wa Lulindi, Masasi, yanafanana kabisa na wakazi wa Wilaya ya Malinyi katika kata za Sufi, Kilosa Mpepo; swali langu, kata hizo ninazozitaja ni kwamba kama alivyosema jibu la msingi Mheshimiwa Waziri, kwamba, kupitia Mfuko wa Fursa ya Mawasiliano kwa Wote (UCAF), wamejenga minara miwili katika Kata ya Ngoeranga na kata ya Sufi, lakini minara hiyo ambayo imejengwa chini ya Tigo haifanyi kazi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali nangu. Je, ni lini Serikali watarekebisha minara hiyo na vilevile kumalizia Kata zile mbili ambazo hazina mawasiliano kabisa, kata ya Sufi na kata nyingine?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwakikishie kwamba kata hizo mbili alizozieleza ambazo hazina mawasiliano kabisa ikiwa ni pamoja na kata ya Kilosa Mpepo, tutahakikisha kwamba tunazifikishia mawasiliano kwa kadri tutakapopata fedha na maadamu ulishawasilisha hilo mapema Mheshimiwa Mponda nadhani utakumbuka Mheshimiwa Waziri wangu alivyokujibu na nikuthibitishie lie jibu alilokupa Waziri wangu na mimi nitalifuatilia utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mponda kuhusiana na kata mbili ambazo…
Alitaja kata nne na nimeongelea kata mbili, kata hizo mbili ambazo Tigo wamejenga minara nitazifuatilia kuhakikisha kwamba minara hiyo inafanya kazi.
MHE. DKT. HAJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Nabu Spika, usimamizi na ushauri wa kitaalam wa jinsi ya uendeshaji wa Skimu hii ya Itete unafanywa na wataalam ambao wanakaa Makao Makuu Malinyi, kilometa 80 kutoka ilipo skimu hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umbali huo na uhaba mkubwa unaoikabili Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi watumishi hao, wataalam hao wanashindwa kutekeleza majukumu yao ya kikazi. Je, Serikali hasa Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji mnaisaidiaje Halmashauri ya Malinyi, ili kuwezesha skimu hii ifanye kazi kwa kiwango chake hata kuwapatia gari lililotumika tu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, eneo hili la Malinyi lina neema kubwa ya mito ambayo inatiririka maji masika na kiangazi ambayo kama ikitumika vyema tutaweza kumaliza kabisa tatizo la uhaba wa chakula katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu fupi sana; Serikali ina mpango gani sasa kuweza kuongeza skimu nyingine katika Wilaya ya Malinyi kwenye mito kama ya Sofi, Laswesa, Mwatisi, Fuluwa pamoja na Mto wa Mafinji ambayo kama itawekewa skimu tatizo la uhaba wa chakula hasa mpunga, litakuwa limeondoka kabisa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza anazungumzia habari ya usimamizi wa scheme ambayo tayari imeendelezwa na Tume yetu ya Taifa ya Umwagiliaji. Katika mwaka huu wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya kufanya mapitio ya kuangalia hizi scheme zote ambazo zimejengwa kwa miaka mingi na kuweza kupanga namna bora ya kuziendeleza ikiwa ni pamoja na kuzisimamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunajipanga katika mwaka wa fedha huu unaokuja tuweze kuangalia scheme zile kubwa ambazo kwanza kulingana na sera tulikuwa tunakabidhi kwa Halmashauri au jumuiya ya watumiaji kuziendesha, lakini maeneo mengi tumeona kwamba hayaendi na jinsi tunavyopanga. Kwa hiyo, tunafanya mapitio na kuona namna bora ya kuweza kuweza kuziangalia namna ya kuzisimamia scheme hizi kwa ajili ya faida ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili; ni kweli Wilaya yake ina mito mingi na ndio maana tumesema Tume ya Taifa inafanya kazi ya mapitio ya mpango kabambe wa sera yetu ya Umwagiliaji na kuona namna gani bora tunaweza kuyaendeleza maeneo haya kwa kuweza hata kuwakaribisha wawekezaji wakubwa ili wajenge miradi mikubwa ya umwagiliaji katika maeneo ambayo maji yanaweza kupatikana kwa urahisi.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa mchakato ambao unaendelea katika maeneo yale.
Swali la kwanza, kupitia huo Mradi wa KILORWEMP, wadau tulikaa mwezi Oktoba, 2016 katika Mji Mdogo wa Mikumi. Tulichokubaliana ni kwamba urejeshaji upya wa mipaka ile utazingatia ushirikishi wa wananchi. Serikali wamefanya hilo lakini changamoto hapa, tunapojadiliana, tunapokubaliana katika urekebishaji wa ile mipaka lakini wakienda site watumishi/wataalam wale wa Serikali wanagoma, wanaelekeza kuweka mipaka kama wanavyotaka wao. Kwa mazingira hayo bado wataendeleza mgogoro. Kwa nini sasa makubaliano yale na wananchi na wadau kwenye kijiji hayatekelezwi wanapokwenda kuweka upya ile mipaka? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali sasa mnafanya zoezi la kuondoa mifugo kwenye hifadhi kwa maeneo yale ya lile Bonde la Ardhi Oevu la Kilombero. Mifugo ile itakapotoka kule inakuja kwenye ardhi ya vijiji, ardhi ya vijiji ndiyo yenye vyanzo vya maji katika bonde lile la Kilombero. Je, Serikali mnavisaidiaje vijiji hivi kukabiliana na msukosuko huo wa ile mifugo itakapotoka kule kwenye lile bonde kuja kwenye ardhi ya vijiji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: MheshimiwaSpika, swali lake la kwanza linasisitiza juu ya umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi jambo ambalo kwenye majibu yangu ya msingi nimelifafanua kirefu kwamba kwa mujibu wa mipango ya Serikali ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kufanya uhifadhi uweze kuwa endelevu na kuweza kutimiza masharti ya sheria, kanuni na taratibu bado utekelezaji wake unaendelea kusisitizwa na kwamba Serikali itaendelea kuona umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi. Katika mradi huu wa KILORWEMP tayari tunao mpango huishi unaoitwa intergrated management plan ambao kwa mujibu wa Kanuni za Mkataba za RAMSAR Convention tunapaswa kuuzingatia.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nipokee maelezo yake ambayo nayasikia kwa mara ya kwanza hapa kwamba makubaliano yanayofikiwa katika vikao mbalimbali vilevile vya ushirikishwaji wa wananchi wakati wa kwenda kuyatekeleza kule site yanakuwa yana kasoro au yana upungufu. Hili naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa niaba ya Serikali tunalipokea ili tuweze kufika kule kwenye maeneo yanayohusika tuweze kuona pengine katika utekelezaji, utendaji unakuwa una kasoro. Kwa hiyo, tukifika kule tutakwenda kushirikiana kuona namna gani tunaweza kuondoa hizo kasoro ndogo ndogo zinazoweza kukwamisha dhamira kuu ya Serikali ya kuweza kufanya uhifadhi uwe na mafanikio.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili linalohusiana na uondoaji wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na changamoto zake, anataka kujua kwamba uondoaji wa mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa na mahsusi katika suala hili ni suala la Bonde la Mto Kilombero kwamba mifugo ile hasa ng’ombe wanapokwenda katika maeneo ya vijiji wanakwenda kusababisha changamoto nyingine ambazo na zenyewe zinakuwa ni kubwa vilevile pengine ni kubwa zaidi kuliko wanapokuwa wako kwenye hifadhi kwa mujibu wa maelezo yake.
Napenda nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba na hili nalo ni suala vilevile la ushirikishaji wa pande zote mbili kwamba Serikali na wananchi kwa pamoja tunapaswa kufanya kazi hizi kwa pamoja kwa kushirikishana ili kila mmoja atambue umuhimu wa uhifadhi lakini katika kusimamia uhifadhi, changamoto tunazokutana nazo wakati wa kusimamia tuweze kuzitatua kwa pamoja. Kwa hiyo, katika safari hiyohiyo ninayosema tutakuja tuweze kuona nini kiko site, tutaweza kuliangalia tatizo hili la mifugo inayoondoka katika maeneo ya hifadhi ya Mto Kilombero ili tuweze kuona namna ya kutatua changamoto hizo katika maeneo ya vijiji wanamoishi wananchi.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu la msingi Waziri amezungumzia kwamba baadhi ya Halmashauri tayari wameshamaliza ujenzi wa maabara katika shule za sekondari na mojawapo ya Halmashauri hii ni Halmashauri ya Malinyi tumeshamaliza karibu asilimia 90 ya maabara ya masomo ya sayansi katika shule za sekondari na baadhi ya majengo haya sasa hivi yanaanza kuharibiwa na wadudu wau ndege aina ya popo.
Je, ni lini Serikali watakamilisha utaratibu wa kupeleka vifaa ili maabara hizo zianze kutumika rasmi.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba tuliweza kununua vifaa kwa ajili ya maabara zaidi ya 1,000, tumeweza kuvisambaza. Ninafahamu Mheshimiwa Dkt. Mponda hata tulivyofika kule kwako Malinyi tuliona kweli ulitoa concern hiyo.
Kwa hiyo, tutafanya kila liwezekanalo kuona jinsi ya upelekaji wa vifaa. Hata hivyo, katika ile shule ambayo ulisema ina changamoto kubwa, kabla ya mwezi wa pili nadhani tutafanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba shule ile tunaiboresha, wananchi wa Malinyi ambao wana changamoto kubwa sana waweze kupata elimu vizuri.(Makofi)
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na vilevile naishukuru Serikali kwa majibu mazuri na dhamira yao ya dhati kabisa kufanya mradi huo ukamilike. Nina maswali mawili madogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, uchimbaji wa kisima cha mradi huu,ulipangwa kufanyika mwaka 2016 na tafiti zilifanyika ikabainika kuna mafuta ya kutosha kupata mafuta ya kuendesha biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali kwa utaratibu ambao wameuwekeza ukiritimba umezidi mno umesababisha mpaka sasa hivi mkataba kati ya mwekezaji kampuni ya Swala ya Kitanzania na TPDC bado haujakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu ni lini sasa mtakamilisha mkataba huu ili mradi huo wa uchimbaji wa haya mafuta uanze kwa sababu haraka haraka tu pale itaajiri wananchi karibuni 500 kwa kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nakubali mmetoa elimu lakini mafundisho tuliyopata Mtwara mnaelekea huko huko, elimu mnayo toa mnafanya vi semina na mikutano, watu wachache sana wanahusishwa, eneo lengwa tarafa nzima ya Mtimbira lina wakazi karibu 75,000, hizo semina sijui mtaendeshaje nawashauri na baadaye nauliza swali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumieni media, tumieni vyombo vya habari ambavyo vitaweza kusambaza taarifa na habari haraka sana kuliko hizo semina mnazofanya. Katika maeneo yetu kuna redio za jamii mbili…
redio FM Ulanga, je, Serikali mpo tayari kutumia redio hizo za jamii ili kuelimisha jamii katika eneo hilo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kabla ya kujibu maswali napenda nichukue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Mponda anavyofuatilia utekelezwaji wa mradi huu. Mradi utakapoanza kutelezwa utaajiri watanzania takribani 200 hadi 300, Kwa hiyo, Mheshimiwa Mponda hongera sana kwa kufuatilia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika swali lake la kwanza nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba mkataba ulishasainiwa tangu mwezi Februari, 2012 kwa hiyo, kilichobaki ni uekelezaji wa kufanya drilling kwa maana ya uchimbaji na ugunduzi wa mafuta, na katika eneo hilo Mheshimiwa Mponda mafuta yanayotarajiwa kuchimbwa katika eneo hilo yanafikia milioni 180 hadi milioni 200. Kwa hiyo, ni mtaji mkubwa na utakuwa na manufaa kwa wananchi wako na watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa uchimbaji utaanza, kama ambavyo nimeleeza kama ambavyo nimeleleza kwenye hilo la msingi kwamba kinachosubiriwa ni kupata kibali cha mazingira kutoka NEMC na wenzetu NEMC wanalifanyia kazi pamoja na Mamlaka ya TAWA yaani Hifadhi ya Mamlaka ya Wanyamapori, wametuhakikishia kwamba kuja kufika mwezi Julai vibali vimepatikana na mwezi Septemba uchimbaji utaanza rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la pili kuhusiana na elimu, kwa kweli niwapongeze sana TPDC na Swala wametoa elimu katika mkoa mzima wa Morogoro sasa takribani ya watu 350 wamepewa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumepeleka elimu pia katika vijiji vingi, ikiwemo kijiji cha Mheshimiwa Dkt. Mponda, Ipera, Kipenyo, Mtimbira lakini pamoja na maeneo ya Mnazini pamoja na vijiji vingine anavyovijua Mheshimiwa Mbunge na maeneo mengine ya Kijiji cha Kitete na kata zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, takribani ya wananchi 350 walipata elimu, lakini tutaendelea na kutoa elimu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameshauri. Lakini kuhusu vyombo vya habari tumeshaanza kutumia TBC na nimechukua ushauri wake kwamba chombo cha FM media cha Ulanga nacho tutazingatia tutakipa kazi hiyo.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwa kuniona.
Matatizo yanayowakabili wananchi wa Wilaya Chemba kwa kukosa huduma za Hospitali za Wilaya yanalingana kabisa na ya Wilaya ya Malinyi ambapo wananchi hawana Hospitali ya Wilaya. Halmashauri ya Malinyi imeweka utaratibu kuomba TAMISEMI kuifanya Hospitali ya Lugala ambayo inamilikiwa na taasisi ya kidini kuwa Hospitali ya Wilaya, lakini ombi hilo na utaratibu huu TAMISEMI wamesimamisha.
Je, Serikali ina utaratibu gani wa haraka wa kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Malinyi kupata hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ukiangalia Ulanga, Malinyi wana changamoto kubwa ya sekta ya afya. Katika mpango wa haraka Mheshimiwa Mponda, naomba nikuhakikishie kwamba kuna kituo cha afya cha Mtimila ambacho tumekiwekea kipaumbele tunakuja kukiwekea miundombinu muda si mrefu, kuanzia huu mwezi wa sita kwenda mwezi wa saba inawezekana mchakato huo utaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishe wananchi wa Malinyi kwamba Serikali imewaona, tutaenda kufanya kazi kubwa pale ambayo mtakuja kuona ikifika mwezi wa nane hapo Mungu akijalia, inawezekana hali ikawa ni tofauti wananchi watakwenda kupata huduma nzuri sawa sawa na kituo cha afya cha Lupilo katika Jimbo la Ulanga (Makofi)
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Jibu la Serikali limeeleza kwamba kwa muda huu Wilaya ya Malinyi inapata huduma za Kibenki kupitia mawakala wa fahari ambayo ni Malinyi SACCOS na Zidua Shop. Huduma hizi hazitoshelezi kabisa, kwa sababu mawakala hawa wawili wana changamoto kubwa ya mtaji. Je, Serikali kupitia hiyo benki CRDB wanawawezeshaje kwa mikopo isiyokuwa na masharti magumu kuongeza mitaji kwa mawakala hawa wawili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani yupo na maeneo haya ya Malinyi ndio wazalishaji wakubwa wa Mpunga wa Brand inayojulikana ya Kilombero au Ifakara. Wananchi hawa kwa kukosa huduma za kibenki wanalazimika kwenda Mahenge au Ifakara kupata huduma hizi za kuweka na kutoa fedha. Sasa matokeo yake kutembea na fedha nyingi wanahatarisha maisha yao na usalama wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na matukio kwa muda wa miaka mitatu iliyopita zaidi ya matukio kama kumi hivi, ni kwamba kati ya Lupilo, Ilagua na Itete kuna matukio ya ujambazi yanayotokea mara kwa mara wananchi wanapora fedha na kuhatarisha maisha yao. Je, Wizara ya Mambo ya Ndani wanawasaidiaje Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro hususani Wilaya ya Malinyi kukabiliana na ujambazi huo? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mponda kwa swali lake zuri na anaonekana analielewa vizuri Jimbo lake na ndio maana wananchi wameendelea kumchagua. Niseme tu Wizara ya Mambo ya Ndani kwanza tumejipanga kuwasaidia usafiri watu walioko maeneo yale ambayo yanahitaji doria zinazohitaji kuzunguka mwendo mrefu kama ilivyo kwenye Jimbo lake na Majimbo mengine ya aina hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapokuwa tumeimarisha usalama, tutakuwa tumeweka ushawishi pia kwa taasisi za kifedha kuweza kuweka benki zao huku wakijua kwamba kutakuwepo na usalama wa kuweka benki hizo na fedha zao zitakuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya hiyo pamoja na Majimbo hayo ni wazalishaji wakubwa, sina mashaka kuhusu upatikanaji wa wateja ambao unaweza ukavutia benki hizo kuweza kuweka matawi yao kwa namna hiyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutalifanya hilo na mimi binafsi nitatembelea huko ili kuweza kutekeleza haya tunayoyasema. (Makofi)
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pia ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri ya swali la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri hao wote wawili wa Wizara hii; Waziri na Naibu wake wamefika eneo hilo. Mara ya mwisho mwezi wa pili Mheshimiwa Naibu Waziri amefika na wana Malinyi tumempa jina la Dogo Janja. Ameona hali halisi pale katika Skimu ya Itete, kwa kuwa imetokana na usanifu wa kina ambao haukuwa mzuri na hata ujenzi ule uliofanyika haukuwa mzuri imesababisha skimu ile inashindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, skimu ile haina barabara za kuingia kwenye mashamba, skimu ile wakati wa kiangazi haina maji ya kutosha kumwagilia mashamba yale na Serikali wameadhidi kwamba watafanya marekebisho swali langu la kwanza, ni lini mtafanya marekebisho ambayo mmehaidi kwenye Skimu ya Itete?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, menejimenti ya skimu ile inasimamiwa na injinia ambaye anakaa Malinyi kilometa 50 kutoka pale kwenye skimu mpaka anapoishi yule injinia; tuliomba ombi maalum apatiwe usafiri injinia yule, ni lini sasa ombi hili litatekelezwa? Nakushukuru sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nimefika pale Itete na Mheshimiwa Naibu Waziri amefika. Tatizo moja kubwa la Itete ni kwamba skimu ipo haijakamilishwa ujenzi lakini inafanya kazi. Tatizo lililo kubwa ni kwamba sasa hivi baada ya kumaliza huu mpango kabambe tunataka kujenga bwawa kubwa ambalo litatunza maji ili wananchi waendelee kulima wakati wote. Tatizo lingine lililokuwepo ni kwamba ile Kamati iliyokuwa imeundwa ambayo inasimamia kilimo kile cha mpunga ilikuwa na makosa kidogo, tukaivunja na sasa hivi tumeweka nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ombi lake la kwamba injinia sasa awe sehemu ya karibu kwa ajili ya kusimamia ile skimu tutalitekeleza tuwasiliane Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kumpatia huyo injinia. (Makofi)
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Ulanga na Malinyi ni walewale. Suala hili la miundombinu la mifugo tumelipigia kelele muda mrefu na tumeielekeza na kuishauri Serikali watumie Mfuko wa Maendeleo ya Mifugo (Livestock Development Fund) ambayo inakusanywa kutokana na minada waweke percentage ili kuwa na uhakika wa kuhudumia miundombinu hiyo pamoja na malambo na majosho. Ni lini Serikali watatekeleza maagizo haya ambayo mara nyingi tumetoa hapa Bungeni?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni muda mfupi sana sasa hivi Waziri wa Mifugo na Mvuvi atawasilisha hotuba yake, masuala yote yamesheheni humo ataona mipango yetu madhubuti kabisa ambapo sasa mifugo nchi hii haiwezi kufa tena kwa kukosa malisho na maji. (Makofi)
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza kama yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, buffer zone inayozungumziwa hapa katika Bonde la Kilombero ni pana sana, linaanzia kilometa tatu mpaka 12. Mheshimiwa Rais aliahidi angalau kuwasaidia wananchi hawa kipande kidogo tu cha hii buffer zone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hili la uwekaji wa mipaka limeshakamilika kwa Wilaya ya Malinyi lakini bado kuna malalamiko mengi yamejitokeza na busara alizotumia Mheshimiwa Waziri wa Maliasili, ameunda tume lakini hata hiyo tume haiwashirikishi kabisa wananchi.
Swali langu, kwa nini sasa Serikali wasione busara kuanzisha upya tena mipaka hiyo kama walivyoanza mwaka 2016 kwa dhana ya kuwashirikisha wananchi kwa kikamilifu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi hawa sasa wanatoka kule kwenye buffer zone wanarudi kwenye ardhi ya vijiji, ardhi ya vijiji ndiyo vyanzo vya mito ambayo inatiririsha maji kwenye Mto Kilombero.
Sasa, je, Serikali ina mpango gani mahusus (commitment) kupitia taasisi zake za TAWA au TANAPA kuwezesha Wilaya ya Malinyi kutengeneza schemes za umwagiliaji kwa ajili ya kilimo na mifugo katika eneo hili ili kuendeleza ustawi wa hilo Bonde la Kilombero? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza kwa jinsia ambavyo amekuwa akilifuatilia hili suala na ambavyo amekuwa akishirikiana na Serikali katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ushirikishwaji wa wananchi ni suala pana na ni suala ambalo pengine bado linahitaji ufafanuzi; lakini tuna lengo kubwa kwamba lazima wananchi wote wa maeneo yote kwenye migogoro washirikishwe kikamilifu kupitia wananchi, viongozi wao, Serikali kwa ujumla na wadau wengine wote lazima washirikishwe na hilo ndiyo tumekuwa tukilifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, katika Wilaya ya Malinyi wakati tunaweka mipaka tulifanya vikao 27 na wananchi wakaelimishwa kwa nini tunahitaji kuhifadhi eneo lile na kwa nini lazima kuwe na buffer zone. Katika hivyo vikao tukafanya mikutano 12 na wananchi na katika hao wananchi walioshiriki katika hilo walikuwa ni 1,382; kwa hiyo, kwa ujumla walishirikishwa kwa mapana na marefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama kuna upungufu, namuomba Mheshimiwa Mbunge basi tutakaa tena tuangalie kama kunahitaji ushirikishwaji wa zaidi ya hapo basi tutafanya kama alivyoomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la scheme ya umwagiliaji; ni kweli kabisa kwamba kumekuwa na matumizi mabaya ya maji katika eneo lote zima katika Ramsar Sites.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunataka tuhakikishe kwamba lazima kuwe na matumizi endelevu ya maji katika lile bonde kwa sababu pale ndipo vyanzo vya maji ya Mto Kilombero ambao ndiyo utaenda kuzalisha umeme mkubwa kule Stiegler’s Gorge, kwa hiyo, lazima tuhifadhi vizuri na tuhakikishe kwamba wananchi wanaelimishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza hilo basi tutashirikiana na wananchi, Serikali, Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Wizara ya Kilimo na kuona ni aina gani ya scheme zianzishwe katika maeneo yale ya juu kusudi wananchi wale waweze kunufaika na ule mradi. Zaidi ya hapo tutashirikiana pia na Bodi ya Bonde la Mto Rufiji ambayo ipo kule kwa ajili ya kuhamasisha na kuhakikisha kwamba wananchi hawaharibu vile vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo ninaamini wananchi watafaidika na huu mpango wa scheme ambao Mheshimiwa Mbunge anapendekeza.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa mchakato unaoendelea kuibadilisha barabara hii kuwa kiwango cha lami. Barabara hii kuanzia Ifakara – Lupiro – Malinyi mpaka Kilosa kwa Mpepo kutokana na mvua za mwaka huu, barabara hii kwa kiasi kikubwa sana imeharibika sana na bajeti ambayo tumeipitisha hapa ya Wazara ya Ujenzi haitoshelezi kabisa kipande kile ambacho wamewekea bajeti. Swali langu hapa, Je, Waziri yupo tayari kutumia hela ya dharura kuongezea bajeti kipande hicho cha barabara kuanzia Ifakara mpaka Malinyi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sera ya barabara inaelekeza Makao Makuu ya Wilaya zote zijengewe barabara kwa kiwango cha lami. Wilaya yetu ya Malinyi haina hata chembe ya lami; je, Serikali ni lini watatekeleza sera hiyo ya ujenzi wa barabara ya lami katika Makao Makuu ya Malinyi?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nizipokee pongezi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitoa kwa sababu nafahamu kwamba sasa ujenzi wa barabara hii muhimu kama unavyosema umekwishaanza na unakwenda kwa hatua na tupo hatua nzuri. Pia nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia barabara hii muhimu na katika kufuatilia kwake nilipita barabara hii ili kujionea mwenyewe namna changamoto ilivyokuwa, lakini tunaendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kuhusu swali lake lwa kwanza ni kweli fedha hazitoshelezi kwa mujibu wa bajeti na kwa hali ya mvua iliyokuwa imetokea katika kipindi hiki na niseme tu kwamba tulikuwa tumetoa maagizo kwa Mameneja wa TANROADS mikoa yote ili kuweza kutumia hiyo fursa ya bajeti tuliyokuwa nayo kwenye dharura kuweza kutengeneza maeneo korofi nchini kote ili kuhakikisha kwamba barabara zinapitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niendelee kusisitiza kumwomba Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Morogoro kwa namna tunavyoendelea kwamba aendelee kutazama kwa macho mawili barabara hii na kwa sababu tumeshatoa maelekezo naamini kwamba utaratibu wa kukurejeshea hali ilivyoharibika unaendelea. Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi Mheshimiwa Mponda na wananchi wa Malinyi na nitahakikisha kwamba maeneo ambayo yamekuwa korofi tunaendelea kuyashughulikia wakati utaratibu wa kujenga kwa kiwango cha lami unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kweli Serikali ina mpango wa kuunganisha Makao Makuu ya Wilaya na Makao Makuu ya Mikoa na niseme tu eneo hili la Malinyi na mwenyewe nilipita kama ninavyosema nimeona hiki kipande kidogo sana kwenda kuunganisha na Makao Makuu ya Wilaya hii ambapo pale njia panda ya kwenda Londo, Kilosa kwa Mpepo kuna kipande hiki cha barabara ambacho ni korofi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nielekeze tu kwamba kwenye mipango yetu upande wa TANROADS Mkoa wa Morgoro, tutaendelea kuitazama ili tuweze kutibu eneo hili tuweze kuunganisha ili wakati tukipata barabara hii inayokwenda Lumecha kule Namtumbo basi itukute tayari kipande hiki cha barabara kuunganisha na hii barabara kubwa kinaunganika ili Wilaya hii ya Malinyi iweze kuunganika kama ilivyokuwa kwenye sera yetu ya Serikali. (Makofi)
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri, nashukuru kwa majibu mazuri, lakini angalizo langu la kwanza naomba uwe makini na uende kwa kina zaidi kwani hicho kitengo cha kudhibiti panya hakiko sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Serikali kupitia Chuo cha Utafiti cha Sokoine, wamefanya utafiti njia mbadala ya kudhibiti hao panya kwamba wamegundua mkojo bandia wa paka unaoweza kuwadhibiti panya hao bila madhara makubwa kama tunavyotumia sumu ya kawaida. Swali langu, ni kwa namna gani Serikali kwa haraka inaweza ikasambaza matokeo ya utafiti huu, maana yake huo mkojo bandia wa paka huweza kukabiliana na adha hiyo ya panya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Hiyo hiyo Wilaya ya Malinyi takribani sasa ni mwaka wa tano tunasumbuliwa na ugonjwa wa virusi kwa ajili ya zao la mpunga, Kiingereza wanaita Rice Virus Disease ambapo kule kwetu jina maarufu Wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi tunaita Kimyanga; unashambulia mpunga, kipindi ambacho karibu unataka kuzaa unakuwa na rangi ya njano baadaye unaathiri kabisa uzalishaji. Sasa Serikali mna utaratibu gani kusaidia wananchi hawa wakabiliane na huo ugonjwa wa Kimyanga ambao ni adha kubwa sana kwa wakulima wa mpunga kwa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili suala la Rice Virus Disease ambalo linaathiri Wilaya ya Malinyi, Wizara kupitia TARI, sasa hivi wataalam wetu wa TARI wanafanya special investigation kuweza kujua njia bora ya kuweza kudhibiti virus huyu asiweze kusambaa na hivi karibuni tutawasiliana na Mheshimiwa Mbunge na Halmashauri ya Mkoa wa Morogoro kwa ujumla ili kuweza kuwapa mbinu mbadala za kuweza kupambana na virus huyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili la Chuo cha Sokoine, kwa kuwa liko ndani ya docket yetu ya Wizara na sisi ni interested party, nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalichukua na tutalifanyia kazi. Hatua zozote ambazo zinaweza kutusaidia kupambana na changamoto ya panya, ingawa katika Mikoa ya Mtwara ni fursa kwao lakini tutahamasisha wenzetu wa Mtwara waje maeneo ya Malinyi kuweza kuwatega. Vilevile sisi kama Wizara tutashirikiana na SUA kuweza kutumia njia mbadala walioweza kugundua kuondoa hili tatizo.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza wana-Malinyi tunampongeza Mheshimiwa Waziri wa Maji, mwezi wa Nane alikuja Wilayani akaahidi kutatua matatizo ya maji katika Wilaya ya Malinyi ndani ya miezi miwili na nusu. Mheshimiwa Waziri ahadi hiyo mpaka leo haijatimizwa.

Swali la kwanza, katika Kijiji cha Igawa mradi wa Bonde la Mto Rufiji wamechimba kisima kwa njia ya utafiti, lakini kisima hicho wamekitelekeza. Halmashauri Wilaya ya Malinyi tumeomba zaidi ya mara mbili kibali cha kutumia kisima hiki ili tutengeneze miundombinu kusambaza maji, kutatua kero ya maji kwa wananchi wa Kata ya Gawa. Sasa Serikali inasema nini juu ya kuomba kibali hicho cha kutumia kile kisima walichochimba Rufiji Basin?

Swali la pili, pia Mheshimiwa Waziri aliahidi Tarafa ya Mtimbila; Kata ya Mtimbila yenye vijiji saba ipate maji ya mtiririko. Maji yale hayatoshelezi na kuna mpango pale wa kuboresha ule mradi na Mkandarasi ameteuliwa lakini mpaka leo hajafanya chochote. Vile vile Mheshimiwa Waziri aliahidi kwamba ndani ya miezi miwili na nusu atamwondoa Mkandarasi, atafanya utaratibu wa force account ili mradi ule ukamilike. Nini kauli ya Waziri kwenye ahadi hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji
wake, lakini kikubwa tunatambua maji ni uhai na sisi kama Viongozi wa Wizara ya Maji hatupo tayari kupoteza uhai wa Wana-Malinyi. Kubwa namwomba Mheshimiwa Mbunge kutokana na concern yake na jitihada kubwa ambazo zinafanyika pale kuwasimamia wale Wakandarasi, tukutane leo saa 7.00 ili tuweze kutoa uamuzi wa haraka ili wananchi wake waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya maswali mawili ya ngongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa majibu mazuri na tunaona mikakati wa Serikali kuelekea Tanzania ya viwanda.

Swali la kwanza, tayari katika mikakati hiyo shule nyingi za sekondari zimejenga maabara ili kutengeza wataalam kwa ajili ya Tanzania ya viwanda, ni lini sasa Serikali watapeleka vifaa vya maabara katika shule za sekondari ambazo zimeshatekeleza ujenzi wa maabara?

Swali la pili, katika Wilaya Malindi tuna Chuo cha Maendeleo Sofi nashukuru Serikali wanakifanyia ukarabari chuo kile lakini kina uhaba mkubwa wa walimu. Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu katika chuo cha Sofi ambapo ukarabati wake karibu unakamilika? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni lini Serikali itapeleka vifaa vya maabara katika maabara ambayo imekamilika naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumekuwa tukipeleka vifaa vya maabara mara kwa mara kadri maabara zinapokamika. Naomba nimhakishie kwamba kwa shule zile ambazo sasa zimekamilisha Serikali inataendelea kupeleka vifaa vya maabara na hata kwenye bajeti ambayo Bunge hili imepitisha vilevile tumeweka fedha za maabara ili kuhakisha kwamba vifaa vinapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Sofi naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu ule wa kukarabati vyuo vya wananchi (FDC’s), hauishii tu kwenye ukarabati vilevile inaenda kwenye mambo mengine ya kuboresha mazingira yote ya kujifunzia na kufundishia ikiwa ni pamoja na kuajiri walimu, wakufunzi lakini na wafanyakazi ili vyuo vile viweze kuendeshwa kwa uzuri zaidi ndiyo maana tulifanya kitu kinachoitwa conditional survey ya kujaribu kuangalia ni mahitaji yapi yanahitajika ili vyuo vyote viweze kupata mahitaji yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie kwamba tayari tulishafanya tathmini ya nini kinahitajika na punde ukarabati utakapokamilika vilevile nimhakikishie kwamba watapata wakufunzi. (Makofi)