Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi (5 total)

MHE.VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:-
Baada ya Serikali kutoa tamko la elimu bure wananchi wamekuwa wagumu sana kutoa michango mbalimbali ya kuboresha elimu.
Je, Serikali ina mikakati gani ya kumaliza tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa na vyumba vya maabara katika shule za msingi na sekondari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Elimu Msingi bila Malipo unazingatia uendeshaji wa shule bila ada na michango kutoka kwa wazazi au walezi. Hata hivyo, mpango huo haujaondoa dhamira na uzalendo wa jamii kuchangia shughuli za maendeleo ya nchi yao kwa hiari. Kwa uzalendo wa wananchi walioonesha hivi karibuni Serikali imefanikiwa kupiga hatua za maendeleo katika sekta mbalimbali. Mfano, katika kufanikisha utengenezaji wa madawati kwa asilimia 97.2 kwa shule za msingi na asilimia 100.3 kwa shule za sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa rai kwa wananchi wote ambao wamekuwa wagumu katika kushiriki shughuli za maendeleo wabadilishe mwenendo wao na kuwa na uzalendo kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mkakati wa kupunguza tatizo la nyumba, vyumba vya madarasa na maabara, Serikali katika bajeti ya mwaka 2016/2017 imetenga shilingi bilioni 29.3 kwa ajili yya ujenzi wa vyumba vya madarasa 3,306 kwa shule za msingi na shilingi bilioni 16.3 zimetengwa kujenga vyumba vya madarasa 1,047 kwa shule za sekondari. Aidha, kupitia MMES II zimetengwa shilingi bilioni 23.6 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vyumba 1,642. Kwa upande wa maabara Serikali imetenga shilingi bilioni 18.9 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba 2,135 vya maabara. Serikali itaendelea kutenga bajeti kila mwaka wa fedha na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo katika kufanikisha upatikanaji wa elimu bora hapa nchini.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:-
Wenyeviti wa Mitaa, Madiwani, Wabunge na Rais huchaguliwa na watu wanaoishi katika eneo la mipaka yake na wote hawa wanafanya kazi ya kuwahudumia wananchi katika maeneo yao.
Je, Serikali imeridhika na malipo wanayopata Wenyeviti wa Mitaa pamoja na Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji katika kusimamia shughuli za maendeleo. Majukumu yanayotekelezwa na viongozi hao ni utekelezaji wa dhana ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi ambapo mipango yote na usimamizi yanafanywa katika ngazi za msingi za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiboresha maslahi ya Waheshimiwa Madiwani kadri uchumi wa nchi unavyoruhusu. Kwa mfano posho ya Madiwani ilipandishwa mwaka 2015 kutoka shilingi 120,000 hadi shilingi 350,000 kwa mwezi. Kwa vipindi tofauti hususani Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilipokutana na Waheshimiwa Madiwani katika mkutano wa ALAT hoja hii imekuwa ikijitokeza. Hata hivyo Serikali inalifanyia kazi jambo hili kulingana na mwenendo wa Kifedha wa nchi na jambo hili litakapokamilika utekelezaji wake utafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa hulipwa posho kutokana na asilimia 20 ya makusanyo ya ndani inayopaswa kurejeshwa kwenye ngazi ya msingi katika kata na vijiji. Kila Halmashauri imetakiwa kuhakikisha fedha hizo zinapalekwa kwenye vijiji kwa ajili ya shughuli za utawala ikiwemo kulipa posho na shughuli za maendeleo. Aidha, Halmashauri zimetakiwa kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani ili kujenga uwezo wa kulipa posho hizo kupitia makusanyo yanayofanyika.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:-

Uvuvi haramu bado unaendelea licha ya adhabu kubwa inayotolewa kwa watu wamaojihusisha nao.

(a) Je, Serikali ina mkakati gani katika kuwasaidia wananchi wake fursa zilizopo badala ya kutoa adhabu kali zinazowaumiza?

(b) Je, Serikali inavisaidiaje vikundi vya Beach Mananagement Unit vinavyojihusisha kuona faida ya kazi wazofanya?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mikakati mbalimbali ya kuwasaidia wananchi wake wanaojihusisha na uvuvi ikiwemo:-

(i) Kufata kodi mbalimbali ili kuwapunguzia wavuvi mzigo kama vile Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye injili za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu, nyavu za uvuvi na vifungashio kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2011 na Sheria ya Mamlaka ya Mapato (VAT Act) ya mwaka 2014.

(ii) Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile tunao mkakati wa kupunguza au kuondoa ushuru na tozo mbalimbali kama vile ushuru wa usajili kwa vyombo vya uvuvi vilivyo chini ya mita 11 na tozo ya cheti na afya nazo zimeondolea.

(iii) Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati mwingine ni kuhakikisha wavuvi wanaanzisha vyama vya ushirika ili waweza kunufaika na programu mbalimbali, mfano wavuvi scheme iliyopo katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa (NSSF).

(iv) Kufanya maboresho ya sheria na kanuni za uvuvi ili ziweze kuendena na mazingira na hali ya sasa ya uvuvi nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inafanya yafuatayo ili kuvisaidi vikundi vya vya uvuvi shirikishi wa mazingira ya bahari na maziwa yaani BMUs.

(i) Kuvipatia elemu na kuvijenge uwezo wa kusimamia rasilimali za uvuvi kwa lengo la kuwa na uvuvi endelevu.

(ii) Kuziagiza Halmashauri za Wilaya zote nchini kuvipatia vikundi vya BMUs uwakala wa kukusanya mapato yatokanayo na uvuvi katika Halmashauri zao.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:-

Serikali katika kuhakikisha inapata watumishi bora na wenye sifa iliamua kuwaondoa watumishi wasio na sifa pamoja na wenye vyeti feki, lakini zoezi hilo lilikumbwa na changamoto mbalimbali ambapo Afisa Utumishi aliwaondoa watumishi kwenye payroll bila sababu maalum na walipofuatilia Wizarani walirudishwa kazini:-

(a) Je, kwa nini Serikali isiunde timu maalum ili ipite kila Halmashauri kupitia taarifa juu ya zoezi hili ili haki itendeke hasa kwa wale ambao hawana uwezo wa kwenda Wizarani?

(b) Wapo watumishi ambao baada ya kuajiriwa kwa kutumia vyeti feki walijiendeleza kielimu zaidi ya Darasa la Saba na wameondolewa kwa kosa la udanganyifu wa vyeti: Je, Serikali haioni kuwa hao ni bora kuliko wale ambao hawakujiendeleza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kushirikiana na waajiri na Baraza la Mitihani la Taifa, Serikali iliendesha zoezi maalum la kuhakiki vyeti vya ufaulu mtihani wa Kidato cha Nne, Kidato cha Sita na Ualimu. Kupitia zoezi hilo, watumishi 15,189 walibainika kuwa na vyeti vya kugushi na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mshahara (payroll).

Hata hivyo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa watumishi na vyanzo vingine kuhusu watumishi kuondolewa kimakosa au kwa uonevu katika orodha ya malipo ya mishahara, Serikali imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa karibu ikiwa ni pamoja na kuunda timu za ufuatiliaji wa utekelezaji wa zoezi hili. Jumla ya watumishi 4,160 waliobainika kuondolewa kimakosa au kwa uonevu wamerejeshwa kazini. Kati ya watumishi waliorejeshwa kazini 3,057 ni Watendaji wa Vijiji/Mtaa na Kata.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wanaojiendeleza zaidi ya Darasa la Saba wanafanya vizuri na Serikali inahimiza watumishi kujiendeleza kielimu. Hata hivyo, kwa mujibu wa Kanuni ile ya D.12 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009, ni makosa kwa mtumishi kujipatia ajira kwa njia ya udanganyifu.

Hivyo Serikali ilielekeza waajiri kuwaondoa kwenye orodha ya malipo ya mishahara Watumishi wa Umma wote walioajiriwa kabla ya tarehe 20, Mei, 2004 ambao katika kumbukumbu zao rasmi za kiutumishi walijaza taarifa za udanganyifu kwamba walifaulu mitihani ya Kidato cha Nne, lakini hawakuthibitisha taarifa zao kwa kuwasilisha vielelezo vya sifa hizo kama vile taarifa binafsi (personal records).

Hivyo, pamoja na watumishi hao kujiendeleza kielimu, uamuzi wao wa kutoa taarifa za udanganyifu unawaondolea sifa ya uaminifu na uadilifu kwa Serikali na hivyo wanakosa sifa za kuendelea kuwa Watumishi wa Umma. Ahsante.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:-

Ikiwa lengo la Serikali ni kuhakikisha inawahudumia na kutatua kero za wananchi, kero hizo zisipotatuliwa katika ngazi za Mitaa, Kata, Wilaya na Mkoa wananchi hao hulazimika kuandika na kushika mabango kila Mheshimiwa Rais anapofika majimboni ili kupaza sauti zao:-

(a) Je, ni kwa nini Viongozi wa Wilaya na Mkoa huzuia mabango hayo yasionekane na kusomwa na Mheshimiwa Rais?

(b) Je, wananchi watumie njia gani kufikisha ujumbe wao kwa Mheshimiwa Rais pale matatizo yanaposhindwa kutatuliwa katika ngazi ya chini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MIAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Serikali kwa ujumla inaamini katika uwazi na uwajibikaji na kwamba, ni haki ya msingi ya wananchi kueleza matatizo yao kwa sauti au kwa maandishi pindi wanapotembelewa na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Rais. Kama kuna Viongozi wa Mikoa au Wilaya wanawazuia wananchi, hayo sio maelekezo ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI wala Serikali na wanapaswa kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa, wananchi wana haki ya kueleza changamoto zao kwa Viongozi wa Kitaifa.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inao utaratibu na mfumo wa kuhakikisha kero za wananchi zinatatuliwa na viongozi. Mfumo huo unaanzia ngazi ya Kitongoji hadi Taifa, utaratibu ambao unawawezesha wananchi kufikisha kero zao kwenye ngazi mbalimbali kwa ajili ya kuzitafutia utatuzi. Nazielekeza Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa kuimarisha madawati ya kupokea kero na malalamiko katika maeneo yao ili kuwawezesha wananchi kufikisha kero na changamoto zao kwa wakati. Ahsante.