Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Selemani Said Bungara (23 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye amenipa mimi umaarufu na kuwa Selemani Bungara Bwege, pia kwa kukupa Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa mjanja kwa hiyo, namshukuru Mwenyezi Mungu. Pili, nawashukuru wapiga kura wa Jimbo langu la Kilwa Kusini, mwaka 2010 nilishinda kwa kura 500 kuna watu wakasema wewe umemuonea tu Madabida nitamwita Mhindi Bin Asineni, mwaka huu nimempiga kwa kura 5,595. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba CCM mjiandae mumlete mgombea mwingine nimpige tena. Kwa mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili mambo mengi yamesemwa hapa, lakini naomba vijana wangu wa upande wa UKAWA msiwe na wasiwasi, humu ndani sasa hivi hatupambani na Serikali ya CCM, humu tunapambana na Serikali ya Magufuli na tunapambana na Serikali ya Mapinduzi, CCM hamna Tanzania sasa hivi, hii ni Serikali ya Magufuli na Serikali ya Mapinduzi.
Sasa mkitambua kwamba tunapambana na Serikali ya Magufuli, tusimlaumu sana Magufuli kwamba ndiyo kwanza anaanza na wamekubali wenyewe Serikali ya CCM kwamba tulifikia hapa na udhaifu huu ni kwa ajili ya Serikali iliyopita ya CCM, hii sasa ni Serikali ya Magufuli. Kwa hiyo, tutamwona Mheshimiwa Magufuli kwa miaka yake hii mitano atafanya nini akishindwa na yeye tutamwajibisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nawashukuru sana vijana wangu wa UKAWA tushirikiane tuzidi ili 2020 tuielekeze kibla Serikali ya Magufuli maana yake CCM tena hakuna nchi hii. Waheshimiwa nimepokea pole, kuna watu hapa wametaka kulia hapa eti kwa sababu…
Bunge lisioneshwe live wanataka kulia, aah, mimi nilifikiri wanataka kulia kwa sababu watu hawapati maji vijijini…
TAARIFA....
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Taarifa siipokei kwa sababu anapingana na mwenyewe Mheshimiwa Magufuli, kila siku anasema kwamba Serikali yangu, wakati mwingi anasema Serikali yangu hasemi Serikali ya CCM, kwa hiyo siipokei taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, dakika zangu bado saba ilikuwa tatu tu, narudia kusema kwamba napenda sana Wabunge msililie kwamba Bunge lisioneshwe live mlie kwa kuwa watu hawapati maji, hawapati tiba vizuri, hawapati elimu. Nashangaa sana mtu anayelia anaomba kulia, mimi ninavyojua kulia kuna mambo mawili tu, utamu au uchungu, na ukipata utamu au uchungu huombi kulia unalia tu, ukimwona mtu anaomba kulia au anatamani kulia hataki kulia huyo. Ahsante. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naanza na mambo ya viwanja vya ndege, katika kitabu ukurasa wa 99 nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, kwamba anaanza mchakato katika Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko, nimefurahi sana, lakini Uwanja wa Kilwa Masoko walikuja kutathmini mwaka 2013 na tathmini ya uwanja ili upanuliwe bilioni mbili, milioni themanini, laki nne na sitini elfu mia mbili na sitini mpaka leo, wametathmini watu wale hawajawalipa. Leo wanasema wanafanya mchakato ili wapanue sasa kabla bado hawajafanya mchakato huo wakawalipe wapiga kura wangu, 2,080,460,260, mkawalipe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2013/2014, 2015/2016, wanawaambia wasiendeleze majumba wala wasilime mashamba yao mwaka wa tatu sasa hivi au wa nne. Naomba sana katika majumuisho ya Mheshimiwa Waziri aniambie kwamba lini watakwenda kuwalipa wale watu ili waendelee na mchakato wa kuupanua uwanja huo. Kama hawakuniambia lini wanataka kuwalipa nashika shilingi. Najua mtapiga kura nyinyi mko wengi, lakini shilingi mimi nitaishika safari hii isipokuwa katika majumuisho yake akiniambia watawalipa lini kesi imekwisha kwa sababu Serikali ya Magufuli ndiyo kwanza inaanza, sisemi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili barabara, katika ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyepita kulikuwa na ahadi ya barabara ya kwa Mkocho – Kivinje, lakini mpaka leo. Mheshimiwa Majaliwa alikuwa Waziri akasema kabla ya Uchaguzi, uchaguzi umekwisha, naomba Waziri Profesa, Msomi leteni hela hizo barabara ya kwa Mkocho – Kivinje ijengwe, maana yake kuna watu hapa wa CCM wanasema Majimbo upinzani usipeleke hela, jamani ehee mimi nilipata kura elfu kumi na tano, Asineni elfu kumi, Mheshimiwa Magufuli alipata elfu kumi, Mheshimiwa Lowassa alipata elfu kumi na nne, haya hizi elfu kumi za Mheshimiwa Magufuli ndiyo zimemfanya yeye ashinde. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukisema kwamba Jimbo la Kilwa huleti maendeleo kwa sababu Magufuli hakushinda mnawaumiza elfu kumi waliomchagua Magufuli, haki sawa kwa wote timizeni. Sina wasiwasi, kama hamkuleta hayo nitashinda zaidi kwa sababu kila ukimuumiza mtu wa Kilwa basi anazidi kupata uchungu anaipiga CCM, leteni Maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Nangurukuru – Liwale itiwe lami, sisemi sana amesema Mheshimiwa Bi Lulida hapa, Naiwanga – Nainoko – Ruangwa mtengeneze, mjenge. Kilanjelanje na Njilinji mmepanga milioni 85, jamani ehee milioni 85 haifai, haitoshi tuongezeni hela, mvua ya mwaka huu, mafuriko ya mwaka huu barabara yote imekufa tunaomba hela iongezwe, naomba sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, siisemi sana Serikali ya CCM kwa sababu tayari ishashindwa na wenyewe Mawaziri mmesema kwamba Serikali yetu ilikuwa dhaifu, ilikuwa haikusanyi hela, ilikuwa hivi, lakini Serikali ya Magufuli inakusanya hela haina udhaifu, wala siilaumu Serikali ya CCM iliyopita, najua nitailaumu Serikali ya Magufuli mwakani siyo mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, kuna vijiji kumi havina mawasiliano ya simu Nainokwe, Liwitu, Kikole, nawaomba Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri watuletee mawasiliano watu wapige simu.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya, bandari, nimeangalia humu Bandari ya Kilwa haipo, lakini gesi ya Kilwa akisimama Mheshimiwa Muhongo hapa, gesi ya Kilwa italeta mambo, ehee, lakini watu wenyewe wa Kilwa thuma amanu thuma kafara. Naomba bandari nayo muiangalie, sasa gesi hiyo mngeipitisha wapi? Naomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, sisi watu wa Kusini mnatuonea, maendeleo yote mnawapa watu wenye maneno mengi tu huku. Sisi wengine hatujui kusema, wanyonge, tunaomba Serikali ituangalie. Kuna mradi wa maji, kuna wafadhili kutoka Ubelgiji, basi mpaka leo hawataki kutuletea, tangu mwaka 2014, Mbelgiji amesema anatuletea maji hamtaki kutuletea maji. Kwa sababu gani, sisi watu wa Kusini tu! Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, amani iwe kwa Mheshimiwa Waziri. Awali ya yote napenda kumshukuru Allah (SW) kwa kuniwezesha kuwepo leo hii na nikiwa na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwake ni malipo ya wananchi wa Mji Mdogo wa Kilwa Masoko Sh.3,662,108,122.00 kwa ajili ya fidia. Mheshimiwa Waziri naomba asimamie madai yetu hayo.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuletea mafuriko katika Wilaya ya Kilwa na familia au kaya 4,000 hazina mahali pa kulala, kaya 4,000 hazina chakula, kaya 4,000, Allahu Akbar!

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunamshukuru Mwenyezi Mungu na nawapa pole wahanga wote wa mafuriko Mkoa wa Lindi. Ninaomba wasamaria wema wote wa Tanzania pamoja na Bunge lako tukufu mtusaidie katika mchango.

Mheshimiwa Spika, nawaomba Wabunge wote tuwasaidie wananchi waliopata mafuriko, tunaomba sana. Hili liangalie sana, hali siyo nzuri. Mimi nimekwenda Kilwa, nimekaa siku nne, lakini wananchi hali siyo nzuri.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, naomba tufanye mchango tuwasaidie watu hawa. Hata ukisema aaah, lakini tulipata tetemeko la ardhi Bukoba Wabunge tulichanga.

MBUNGE FULANI: Aaah!

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Sasa wewe unayesema, aah, kwa kuwa tumepata mafuriko sisi watu wa Kilwa, sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu kwa mujibu wa Katiba, inasema wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani. Kama kweli nchi yetu tumejenga misingi ya udugu na watu wa Kilwa na Lindi wamepata mafuriko, wewe unasema aah! Basi ile misingi ambayo tumejiwekea kwa mujibu wa Katiba na sisi tumeapa kwa mujibu wa Katiba tumeishika Biblia, na Misahafu, halafu unasema aah, basi Inshaallah.

Mheshimiwa Spika, nasema tena, angalia sana, hali siyo nzuri Kilwa.

SPIKA: Mheshimiwa, si utoe hoja basi uone wangapi wanakuunga mkono?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, nachangia, nitatoa hoja baadaye.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa misingi hiyo ya uhuru, haki, udugu na amani itatekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambapo Serikali yake husimamiwa na Bunge lenye Wajumbe waliochaguliwa na wananchi, pia yenye Mahakama huru zenye wajibu wa kutoa haki bila uoga wala upendeleo wowote, hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa, kulindwa kwa wajibu wa mtu anayetekelezwa kwa uaminifu;

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo basi, Katiba hii imetungwa na Bunge Maalum la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya wananchi. Unajua nchi yetu, sisi tumeapa. Mimi sikuapa kuilinda Katiba ya CUF, sikuapa hivyo! Wala mtu wa CCM hajaapa kuilinda Katiba ya CCM, hatukuapa hivyo. Sisi tumeapa kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini ndani ya mijadala yetu hii sasa hivi hapa ni kwa uchama tu, sijui CCM itashinda! Nyote ndani mtakuwa CCM, CUF mtashindwa!

Mheshimiwa Spika, huko Zanzibar hakuna CUF hata mmoja, hakuna CHADEMA hata mmoja? Mko CCM watupu! Kinachofanyika kitu gani? Haya, mwakani muwe ninyi nyote CCM, Bunge lenu, maana mnasema mtashinda, mtashinda; haya, wote muwe CCM watupu, sisi wengine tusiwepo ndani. Jambo lenu mtasimamia Katiba tu, wala hamsimamii CCM. Tena mtapata taabu sana kwa sababu wa kuwasokola mtakuwa hamna ndani. Mtasokolana wenyewe kwa wenyewe. Badala ya kutushambulia sisi, mtashambuliana wenyewe kwa wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana, tuache mambo ya uchama. CCM imeundwa; imeanza kuundwa Tanzania halafu ndiyo CCM; imeanza kuundwa Tanzania halafu ndiyo CUF. Naomba sana tuache mambo ya uchama. Wangapi walikuwepo humu? Wako wapi sasa hivi? Wangapi? Mtu unakuja ndani humu, Bwege utakuwa sio Mbunge. Kwani mwanzo nilikuwa Mbunge? Hata kama nikikosa Ubunge! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba usalama wa nchi yetu, amani ya nchi yetu na amani haipatikani bila haki. Leo tunaongea hapa, tunasema hapa Serikali inajifanya haisikii. Ndiyo maana pia wameenda kumsema Marekani huko, ninyi hamsikii hapa. Mtu akipambana anapambana kwa njia yoyote ile, ndani ya nchi na nje ya nchi. Akienda nje ya nchi, oh msaliti! Usaliti gani wakati ninyi hamsikii hapa!

Mheshimiwa Spika, mimi niliwaambia Waislamu kule wamepigwa risasi, wameuliwa, Serikali iko kimyaa! Msaliti nani? Tukiwaambia hamsikii. Mnaangalia nani kasema? Hamwangalii kasema nini. Tunaitaka Serikali ijue nini inasema?

SPIKA: Mheshimiwa Bungara nilitaka tu kukukumbusha neno moja…

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Inshaalah. Nikae!

SPIKA: Hapana usikae. Kwa suti uliyopiga leo, blue bahari inataka leo upige taratibu taratibu, maana yaani leo uko vizuri. (Kicheko)

Endelea Mheshimiwa. (Kicheko/Makofi)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, leo tunasimama hapa, Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sio Mbunge wa CCM wewe, wewe ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kazi yako ni kuisimamia Serikali. Siyo kila kitu Serikali ikisema baya, ndiyo! Zuri, ndiyo! Why? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Wabunge sasa hivi mmekuwa kama mbumbumbu; umeshiba? Eeh! Una njaa? Eeh! Why? Unachokisimamia hukijui! (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Jamani Wabunge wote wa CCM mmepigwa ganzi? Hakuna hata Taarifa? (Kicheko/Makofi)

MHE. RICHARD P. MBOGO: Taarifa ipo.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, unanichanganya bwana! SPIKA: Mheshimiwa Bungara unapewa taarifa bwana, tafadhali. (Kicheko) MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Ananipa nani taarifa? Haya.

SPIKA: Nimekuona Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimesimama kwa mujibu wa Kanuni ya 68(8) ambayo inaniongoza niweze kutoa taarifa.

Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa kwamba Wabunge wa CCM kwa wingi wao wamekuwa wakitoa ushauri ndani ya Bunge hili ndani ya Kamati za Kudumu za Bunge na wamekuwa pia wakitoa ushauri kwenye mabadiliko mbalimbali ya sheria kwa kuleta schedule of amendments ambazo zimekuwa zikichangiwa humu ndani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimpe taarifa kwamba tuko vizuri na tuko imara na tunafahamu kazi vizuri. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Bwege, pokea taarifa hiyo, halafu endelea.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, nimemwelewa sana, lakini nataka nimwulize swali moja halafu ukatoe ushauri. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sisi ni nchi ya kidemokrasia ya vyama vingi vya siasa. Sasa katoe ushauri kuzuia mikutano ya siasa, kuzuia Bunge Live! Sasa katoe ushauri huko kwamba ndiyo sheria? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Katiba inasema katika Ibara ya 9 kwamba Sheria za nchi zilindwe na zitekelezwe. Sasa kwa kuwa wewe unasimamia sheria za nchi na zilindwe na kutekelezwa, Sheria ya Mfumo wa Vyama Vingi inavyosema ni kwamba mikutano ya hadhara na maandamano ni haki, wewe unaizuia; kaishauri Serikali yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sheria inasema lazima isimamiwe na itekelezwe. Sasa kwa kuwa wewe unajua kushauri sana na kuisimamia sana Serikali, sisi vyama vingi tunaambiwa mikutano ya hadhara hakuna, Wabunge tunazuiwa; wewe unasemaje kuhusu hilo? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimemjibu taarifa yake, akaishauri vizuri Serikali waifuate Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawaomba sana, nawasifia kidogo kuhusu mambo ya umeme. Aaah, kwa umeme Alhamdullilah! Kwa umeme aah, mnatufikisha mahali pazuri! Kama mtaendelea hivi kuhusu umeme na mkafanya speed katika maji, mkawalipa wakandarasi wa umeme hela zao vizuri, mkawalipa wakulima wa korosho hela zao wote, mkawaongeza mishahara kwa wafanyakazi, kukawa hakuna kesi za kubambikia, kukawa maandamani yapo, aaah, CCM itashinda! Mashehe wale waliokuwa ndani kwa miaka minane mkiwaachia, aaah CCM dole! Ikiwa wenyewe tunalia umeme, Mashehe hawatoki, mishahara hamwongezi, wakulima hamwalipi na kadhalika, aaah, hesabuni kuumia tu 2020. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Bungara, sijui; ninyi Makatibu mbona hamwangalii muda? (Kicheko)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninawaomba Wabunge wote mtuchangie watu wa Kilwa, natoa hoja Waheshimiwa mniunge mkono.

SPIKA: Hoja haijaungwa mkono bado. Jamani Mheshimiwa ametoa hoja, mnasemaje?

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MBUNGE FULANI: Tunaomba Mkoa mzima wa Lindi, kama tunachangia Mkoa mzima wa Lindi.

SPIKA: Hilo tutalifanyia maamuzi baadaye Mheshimiwa Bungara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini awali ya yote, napenda kukupongeza kwa kuchaguliwa tena kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Wizara nyeti na muhimu katika Tanzania yetu. Mwenyezi Mungu akuzidishie busara na hekima.
Pia napenda kukupongeza kwa katika hotuba yako ukurasa wa 36 mpaka 37 kwa kuturejeshea mradi wa ujenzi wa kiwanda cha mbolea, mradi utakaogharimu Dola za Kimarekani bilioni 1.98 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 411.24. Natoa shukrani kwa Serikali kwa kutupatia mradi huu mkubwa kwa maendeleo ya Kilwa na Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote hayo, Jimbo la Kilwa Kusini, pamoja na gesi inatoka katika Jimbo la Kilwa Kusini lakini katika mradi wa umeme vijiji REA, kwenye Jimbo la Kilwa Kusini ni Kijiji kimoja tu cha Matanda ndicho kimepata umeme katika mradi wa REA. Mheshimiwa Waziri naomba vijiji vifuatavyo vipate umeme wa REA: Pande, Mtilimita, Namwando, Nakimwera, Nangao Malalani (Kata ya Pande), Rushungi, Kisongo, Ruyaya, Lilimalya Kaskazini na Kusini, Namakongoro (Kata ya Linimalyao), Makangaga, Nakia, Nanjilinji „A‟ na „B‟ (Kata ya Nanjilinji), Likawange, Mirawi, Nainokwe (Kata ya Likawaga) Kilole, Ruatwe, Kisangi, Kimbarambara (Kata ya Kikole).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Wilaya ya Kilwa Jimbo la Kilwa Kusini ndilo Jimbo litowalo gesi asili kwa heshima na taadhima lipewe kipaumbele katika mradi wa umeme vijijini. Natanguliza shukrani. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukuwezesha wewe kuwa Mwenyekiti wa kikao hiki na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpa Urais Mheshimiwa Magufuli na kuapa kwamba atailinda Katiba ya Jamhuri ya Tanzania, lakini kwa bahati mbaya tu Katiba yenyewe kidogo anaipindisha pindisha kwa sababu hatoi haki kwa Vyama vya Siasa kufanya mikutano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si nimetoa shukrani? Mimi nimetoa shukrani tu wala sikumtukana mtu yeyote. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa shukrani hizi kwa Mwenyezi Mungu leo najielekeza kuchangia katika sehemu mbili tu katika hotuba hii. Tunakumbuka 2010 Rais aliyemaliza muda wake Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Mungu amzidishie, aliahidi kwamba katika kampeni yake ya 2010 aliahidi kwamba atatengeneza barabara ya Kwa Mkocho – Kivinje barabara ya kilomita 4.2 kwa kiwango cha lami, mpaka leo nisemavyo barabara kwa mvua za jana tu na juzi gari zilikuwa hazifiki katika Hospitali ya Wilaya kutokana na barabara hiyo kuwa chafu na haipitiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bajeti ya 2016/2017, tulitenga milioni 800 kwa ajili ya barabara hiyo ili ikamilike kwa kiwango cha lami, lakini mpaka sasa hivi nisemavyo ndege zimenunuliwa lakini fedha hizo za bajeti hazijaingia katika Wilaya ya Kilwa ili barabara hiyo itengenezwe. Pamoja na ndege mlizonunua hizo lakini mkumbuke kwamba kuna barabara ambazo ni muhimu sana zinaenda katika hospitali za Wilaya, nazo zikumbukwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri naomba hizo milioni 800 zipatikane ili babaraba ile iishe. Tena kwa bahati nzuri tarehe 2 Machi, 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Dkt. Magufuli alifika Kilwa na nikamwambia tatizo hilo kwamba kuna kiporo cha Rais aliyepita na nikamwomba kiporo hicho amalizie yeye. Akaahidi na kumuagiza Injinia kwamba hiyo barabara iishe.

Naomba sana naomba, kwa kuwa Mheshimiwa Magufuli hasemi uwongo na alisema kwamba barabara lazima naomba barabara hiyo iishe ili watu wapate kutumia barabara hiyo na kufika katika hospitali kwa njia ya usalama. Bila hivyo watu wa Kivinje na Wilaya ya Kilwa kwa ujumla tutaona kwamba hatutendewi haki tunaonewa bila sababu ya msingi. Naomba Mheshimiwa Waziri barabara hiyo iishe na fedha hizo milioni 800 zipatikane katika mizezi mitatu iliyobaki ili barabara hii iishe. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni uwanja wa ndege. Kilwa Masoko kuna uwanja wa ndege, uwanja huo kulifanywa tathmini kwa wananchi wangu tarehe 19 Machi, 2013 ili walipwe fidia ili uwanja upanuliwe. Mpaka leo ninavyoongea tangu 2013 mpaka leo 2017 wananchi wangu hawajapata fidia. Naomba sana katika kuhitisha hotuba yake Mheshimiwa Waziri atuambie hawa wananchi wangu watapata lini fidia hiyo ya uwanja wa ndege na kama haiwezekani mseme kwamba haiwezekani.
heshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ingawa dakika tano hazijatimia lakini imeeleweka.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwingi wa huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya Rais katika Serikali ya Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Kikwete aliahidi kujenga barabara ya Singino (Kwamkocho) - Kivinje ya urefu wa kilometa 4.2, barabara hiyo inaelekea katika Hospitali ya Wilaya. Ahadi hiyo ilitolewa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne kwa umuhimu wa barabara hiyo ya kiwango cha lami, lakini kwa bahati mbaya mpaka leo, hiyo barabara ni tatizo. Katika bajeti ya 2016/2017, ilipitishiwa sh. 800,000,000/= kwa ajili ya kumalizia barabara hiyo lakini hadi leo hakuna kilichopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli, mwaka huu wakati alipotutembelea nilitoa kilio changu hiki cha barabara ya kiwango cha lami katika Hosopitali ya Wilaya. Alimwagiza Meneja wa TANROAD Mkoa wa Lindi amalize kero hii ya muda mrefu. Kwa heshima na taadhima naomba fedha ya bajeti ya 2016/2017, sh. 800,000,000/= zipatikane ili mradi huu wa barabara muhimu ya Kwamkocho - Kivinje ikamilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri, pia asimamie agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli aliyoagiza Nangurukuru kuwa Meneja wa TANROAD kuwa awasiliane na Wizara ili kero hii imalizike. Naomba kwa heshima na taadhima asimamie barabara hii muhimu kwa ajili ya faida ya kiuchumi na kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujaona katika bajeti hii mwendelezo wa Uwanja wa Ndege na Bandari ya Kilwa Masoko. Naomba katika majumuisho ya Mheshimiwa Waziri anipatie taarifa ya Uwanja wa Ndege na Bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vile vile Mheshimiwa Waziri anifahamishe, malipo ya wananchi waliotathminiwa katika eneo la Uwanja wa Ndege. Katika majumuisho yake napenda kujua malipo ya wananchi hawa kwa muda sasa wa miaka mitatu hawajalipwa, ni lini watalipwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho napenda kusisitiza:-

(a) Barabara ya Kwamkocho – Hospitali, ambayo ni ahadi ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Kikwete.

(b) Bandari na uwanja wa ndege.

(c) Malipo ya wananchi waliotathminiwa katika eneo la Uwanja wa Ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ufafanuzi katika hizo kero zangu na naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa hii nafasi. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya kuongea leo kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninachoifurahia Serikali ya CCM kwa kutoa tozo za ng’ombe au wafugaji. Hata hivyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, katika sekta ambazo umeisahahu ni Sekta ya Uvuvi. Sisi wavuvi; mimi mvuvi, ndiyo; sisi wavuvi kuna tozo moja tunatozwa dola 1.5 royalty levy, ni shilingi 3,300 kwa kilo ya dagaa. Na alivyokuja Waziri Kilwa na wavuvi wa Kilwa tuliomba sana hii tozo ipungue, kwa sababu unapoteza dola 1.5 sawasawa na kila kilo moja ya dagaa shilingi 3,500 mvuvi atakuwa hapati bei nzuri na wala hatuwezi kuuza nje ya nchi hawa dagaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, na sababu kubwa kule Ziwa Victoria dagaa hao hao wanatozwa 0.16, shilingi 300 kwa kilo. Kwa hiyo dagaa wa Pwani shilingi 3,600 kwa kilo, dagaa wa Victoria shilingi 300 kwa kilo. Ina maana kwamba dagaa wa Pwani hawatakuwa tena na soko kwa sabbau hawatakwenda nje. Tunaomba sana kwamba hii tozo ibadilishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha pili, wavuvi wa Kilwa wamechomewa nyavu zao. Walikata leseni, wana vyombo vyao halali, nyavu zao ni milimita nane, za halali za kisheria, na mtu ukikata leseni ina maana kwamba mtego wako umekaguliwa na ni halali kuvulia. Sasa cha ajabu zaidi ni kwamba tuliiomba Serikali kwamba hizi nyavu zisichomwe mpaka hiyo kanuni ya milimita nane ipitishwe; Waziri akakubali kwamba nyavu zisubiri. Alivyotoka pale Kivinje kufika Dar es Salaam tu siku ya pili nyavu zikachomwa. Zile nyavu milimita nane zikachomwa halafu mwezi wa tano zikaruhusiwa tena milimita nane zivue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naona ajabu, halafu mnasema Serikali hii ya wanyonge. Kwamba milimita nane tuliomba zivumiliwe Waziri akasema zisichomwe mpaka sheria irekebishwe na alituahidi kwamba itarekebisha mwezi wa tano. Akitoka pale Kivinje anavyotuahidi akifika Dar es Salaam tu kachoma. Alivyochoma mwezi wa tano anaziruhusu zilezile nyavu alizochoma zivue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana kwa kuwa wavuvi walikuwa na leseni zao, vyombo vyao halali na nyavu zao zilezile zilikuwa halali, naomba Mheshimiwa Dkt. Mpango ongeza katika bajeti fedha za kuwalipa fidia milioni 900. Ongeza warudishiwe hela zao kwa sababu mmewaonea, naiomba Serikali wavuvi warudishiwe hela zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kitabu chako ukurasa wa 79 anasema kiongozi achaguliwe anayetoka katika ndani ya chama cha siasa kinachotetea maslahi ya haki ya wanyonge na chama hicho ni CCM. Sifa za wagombea, chakushangaza mna sifa gani ninyi CCM kwamba wanyonge ndiyo mnawatetea ninyi!

Mheshimiwa Naibu Spika, leo mnasema kwamba wafanyakazi wasiongezewe mishahara kwa sababu kuna miradi mitatu mikubwa ya kiuchumi. Wakati mnawaambia wafanyakazi wasiongezewe mishahara sisi Wabunge posho yetu ya siku 30 ni mishahara ya miaka miwili na miezi sita ya mfanyakazi. Tuseme wafanyakazi wadogo wangojee sisi Wabunge tuna mishahara mikubwa na miposho mikubwa wao wangojee. Wanyonge hao, wanyonge mnawanyonga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge leo hata tukikaa miaka mia hatuongezewi mishahara wala hatuna taabu; tunakunywa maji safi na salama, tunasomesha watoto wetu, lakini wanyonge, wafanyakazi wasiokuwa na mishahara mizuri mnazuia kuongeza mishahara mnasema eti mngojee mpaka… hii CCM hii, naomba sana…

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bungara, kuna taarifa; Mheshimiwa Asha Abdullah Juma.

TAARIFA

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Selemani, maarufu Bwege, kwamba alikuwepo wapi mpaka sasa hivi anaona hana nafasi ya kupata katika uchaguzi ujao anasema kwamba mshahara ni mkubwa; alikuwa wapi tangu alipoingia humu Bungeni?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bungara, endelea na mchango wako.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba muda wangu uzingatiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, wala simuelewi anachokisema, naona kababaishababaisha maneno tu. Ninachosema Serikali ya CCM mnasema mchaguliwe kwa sababu mnawatetea wanyonge, wanyonge ni watu ambao wanapokea mishahara midogo…

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: …posho yetu sisi Wabunge…

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Taarifa juu ya taarifa, mimi najibu taarifa hii kwanza. Kwa hiyo…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bungara, kuna taarifa; Mheshimiwa Agness Marwa.

TAARIFA

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, natoa taarifa kwa muongeaji anayeongea kwamba Serikali imesema kwamba wafanyakazi wasiongezewe mishahara kwamba Mbunge haruhusiwi kuongea uwongo Bungeni, atuelezee kwamba ni nani aliyetamka hayo matamko.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, aliyetamka ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na clip tunazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo katika Nchi za SADC tulikubaliana kwamba kilimo kisipate chini ya asilimia 10 ya bajeti. Leo mkulima mnyonge mnampangia asilimia 1.5, eti Serikali ya CCM ya wanyonge. Serikali ya CCM leo watu wanatekwa, wanapigwa risasi, wanyonge, hawafikishwi mahakamani, na wanaopigwa risasi wanakufa, eti Serikali ya wanyonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo mkulima wa korosho kalima korosho zake mpaka leo hajalipwa, Serikali ya wanyonge. Leo wavuvi wanachomewa nyavu zao ilihali ... Serikali ya wanyonge; mnyonge gani? Leo wafanyabiashara wadogowadogo wanalipishwa shilingi 20,000 kila mtu, Serikali ya wanyonge; wanyonge gani? Nashangaa sana ninyi mtapitaje katika uchaguzi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wanalia, wavuvi wanalia, wakulima wanalia, wafanyakazi wanalia; Serikali ya wanyonge mtapita wapi? Tunajua mnataka kupita ninyi kwa kutumia rungu yenu ya dola, polisi, wanajeshi wasimamie uchaguzi ili mshinde, lakini kwa wanyonge wa nchi hii kuichagua CCM, ng’ooo! Mnyonge gani! Leo tunakula tunaomba sana Serikali ya CCM siyo ya wanyonge, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, mnyonge hapati haki mpaka mwenye nguvu atake, wenye nguvu ndio ninyi Serikali ya CCM, manawaonea wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kimechanwa kitabu juzi hapa kwa kuwa sijui kitabu cha wanyonge mmeacha tu; mikutano ya hadhara inazuiliwa kwa sababu sisi wanyonge, acheni bwana. Naomba sana Serikali ya CCM ijirekebishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge posho yake ya mwezi mmoja mishahara ya miaka miwili na nusu ya mnyonge. Soko hilo hilo, shule hizo hizo, anaposoma mtoto wa mnyonge na mtoto wa Mbunge hapohapo; soko la mnyonge na soko la Mbunge hilohilo lakini mshahara 350,000. 350,000 kwa mwezi sisi posho siku moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania Nyerere alisema, mwisho nasema, kasema mtu mmoja hapa eti nchi yetu ina uhuru, Nyerere alisema nchi yoyote isiyoweza kujitegemea haiwezi kuwa huru. Ndiyo maana tulisema ujamaa na kujitegemea, kama hukujitegemea ujamaa hautekelezeki na tutakuwa chini ya mabeberu mpaka kiama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutwa ombaomba tu na mtu anayeombaomba hawi huru, kwa hiyo, sisi hatupo huru tuna uhuru wa bendera tu. Naomba sana…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: …naomba sana, naona kasimama mama pale.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bungara kuna taarifa. Mheshimiwa Jenista, naona kengele yake imegonga hapo.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimesimama kabla kengele haijagonga.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge huyu ndio Waziri mwenye dhamana ya ajira, kwa hiyo Mheshimiwa Jenista Mhagama.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu
Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Bungara. Amesema kwamba nchi yoyote ambayo inataka kujitawala ni lazima ijenge uchumi wake yenyewe, na ame-quote maneno ya Baba wa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumthibitishia Mheshimiwa Bungara, na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli imeamua kubeba concept ya Baba wa Taifa kuhakikisha inakuja na miradi mikubwa ya kimkakati ili kuhakikisha nchi yetu inajenga uchumi wa ndani na uchumi ule wa ndani ndiyo utakaomaliza kero nyingi za wananchi wanyonge wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huohuo, tukiendelea na miradi mikubwa ya kimkakati, miradi ile ya kuwanufaisha wanyonge kama ujenzi wa zahanati, ujenzi wa vituo vya afya, elimu bure kwa wanafunzi, hayo yote yameshakwenda kwa wananchi wanyonge. Mheshimiwa Bungara anajua hata wananchi wa jimbo lake wanapata elimu bure na kitu hicho hakikuwepo katika muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninataka kumpa taarifa Mheshimiwa Bungara.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yake kwanza ni nzuri sana.

NAIBU SPIKA: Muda ulishaisha Mheshimiwa Bungara. Waheshimiwa Wabunge, mtakumbuka…

(Hapa Mheshimiwa Selemani Bungara alikuwa akipiga kelele)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bungara tafadhali!

Waheshimiwa Wabunge, mtakumbuka kuna wakati taarifa za kifedha zikiwekwa wazi huwa kuna watu wanalalamika hivi. lakini maneno kama haya yakizungumzwa pengine ni muhimu watu wafahamu ni fedha kiasi gani Wabunge wanapata ili irahisishe wananchi huko nje kuona uhalisia wa mambo haya. Kwa sababu mtu anaweza akasema jambo halafu akitoka hapo nje anadaiwa 50,000 miezi sita mtu hajalipa wakati analipwa hela ambayo ni posho ya siku moja mtu analipwa mshahara.

Kwa hiyo pengine ni muhimu Waheshimiwa Wabunge kama mnakubaliana na Mheshimiwa Spika, atangaze Wabunge tunapata kiasi gani inaweza ikarahisisha mchango wa Mheshimiwa Bungara ili wananchi wafahamu, inaweza kutusaidia kidogo maana naona Wabunge walikuwa wananiangalia hapa kama ni kweli ama vipi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa shukurani kwa kunipa nafasi hii ili nichangie. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameumba mbingu na ardhi ili tuitumie sisi binadamu katika maendeleo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia habari ya maji na kila kiumbe ana asili ya maji, sisi binadamu tumepatikana kutoka na asili ya maji. Hata hivyo miaka 56 ya Serikali ya CCM tunazungumzia habari ya maji. Tunakwenda vijijini kuomba kura ajenda yetu kubwa ni kwamba mkinichagua kuwa Mbunge mtapata maji, miaka 56.

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema Mheshimiwa wa Mtama hapa, Ilani ya CCM mliwaahidi Watanzania kwamba mtapata maji kutoka asilimia 67 mpaka 85. Mimi Jimbo langu au Wilaya yangu ya Kilwa maji vijijini ni asilimia 48.3. Tunaomba sana maji safi na salama. Tunaomba sana, bajeti ya maji lazima iongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa 2016/2017 tulipangiwa au tulipitisha bajeti ya bilioni mia tisa hamsinitukapata asilimia 19, mwaka huu bilioni mia sita sasa ukipata asilimia 16 utajua mwenyewe itakuwa shilingi ngapi maana itapungua. Naomba sana bajeti hii ya maji irudi iende ikaongezwe fedha kama zilivyoongezwa mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia Mradi wa Maji wa Mavuji. Katika bajeti ya 2016/2017, ukurasa wa 142 kulikuwa na mradi wa maji katika Mji wa Kilwa Masoko. Kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa chanzo, mitambo ya kusafishia na kutibu maji, ulazaji wa mabomba, ujenzi wa matanki, ukarabati wa upanuzi wa mabomba ya kusambaza maji. Mahitaji ya fedha euro milioni 61.67. Maelezo, majadiliano ya Serikali na Ubeligiji kupitia kampuni ya Aspec international yanaendelea. Usanifu umekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya! Nataka nijue toka kwa Mheshimiwa Waziri, mazungumzo kati ya Aspec na ninyi yameishia wapi? Mradi huu ungesaidia upatikanaji wa maji katika miji midogo miwili ya Kilwa Kivinje na Mji Mdogo wa Kilwa Masoko, lakini sasa hivi ni miaka mitano maneno tu, maneno tu, kesho, kesho kutwa, kucha maneno tu. Oh haa! Mheshimiwa Waziri leo nataka aniambie mchakato huu umefikia wapi ama sivyo kwa mara ya kwanza nataka nitoe shilingi;.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana. Serikali ya CCM kwa miaka 56 imeshindwa, tunataka kuiangalia Serikali ya Magufuli, maana Serikali CCM haipo, sasa hivi kuna Serikali ya Magufuli. Tunataka tuione Serikali ya Magufuli kwa miaka hii mitano itamaliza tatizo la maji? Kama haikumaliza tatizo la maji katika Tanzania, basi Magufuli bye bye (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Serikali ya Magufuli ikishindwa kutatua tatizo la maji bye bye mwaka 2020, kwa herini. Waheshimiwa maji si mchezo, huwezi kuishi bila maji, huwezi kulala na mama bila maji. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana, bila maji hakuna kila kitu, watoto hawapatikani bila maji. Tunaomba hilo jambo la maji na hii bajeti lazima irekebishwe ili Watanzania tupate maji. Naunga mkono kabisa; utampata wapi mtoto bila maji? (Vicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kule Kilwa kuna mradi wa maji tangu mwaka 1992, Kilwa sehemu ya Mpala. Watu walitathminiwa lakini tangu 1992 mpaka leo hawajalipwa fidia, mpaka leo! Maji wameyachukua Mpala wameyapeleka Masoko lakini Mpala penyewe pale maji hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana katika majumuisho leo Mheshimiwa Waziri aniambie watu wa Mpala fidia yao watalipwa lini? Naomba sana na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji alikuja Mpala na akawaahidi watu wa Mpala kwamba lazima hela zao watapata, nataka nijue leo Serikali sikivu ya Mheshimiwa Magufuli mtoe kauli leo nisikie kama si hivyo sijapata jibu sawasawa nasema kweli Serikali ya Mheshimiwa Magufuli si Serikali sikivu. Kama sikivu kweli nijue kwamba watu wale fidia zao zimetoka au zitatoka lini. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, naomba sana msimtie aibu Mheshimiwa Magufuli, Magufuli ni mzuri pengine wabaya ni ninyi hapo. Magufuli mzuri ana tatizo moja tu, anabinya demokrasia, hapo tatizo analo, lakini mengine hana matatizo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana; kuna matatizo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu. Naomba kujua ahadi ya Rais ya barabara ya Kwa Mkocho – Hospitali ya Wilaya ya Kilwa na ahadi ya Rais ya kujengwa kiwango cha lami kilometa nane katika Mji Mdogo wa Kilwa Masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua malipo ya wananchi waliothaminiwa katika maeneo ya mradi wa Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko. Naomba kwa heshima na taadhima wananchi hao walipwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua Bandari ya Kilwa Masoko upo mpango upi wa kuiendeleza kwa kuwa ni bandari muhimu hasa kwa kuwa upo mpango wa kujengwa kiwanda kikubwa cha mbolea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji Mdogo wa kihistoria wa Kivinje miundombinu ya barabara ni mibaya. Mifereji, barabara na madaraja ya Mji Mdogo wa Kivinje, hakuna bajeti wanayopanga. Naomba Mji Mdogo wa Kivinje utengewe fedha za kujenga miundombinu ya barabara, mifereji na madaraja.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wa Masoko tuna kiwanja cha ndege. Kutokana na Mji wa Kilwa Masoko na Kilwa kwa ujumla kukua ni muhimu kuimarishwa na kupanuliwa kwa uwanja huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na taadhima, naomba Mheshimiwa Waziri azingatie maombi na ushauri wangu. Natanguliza shukrani, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameleta mafuriko ameleta Ugonjwa wa Corona; Mwenyezi Mungu ambaye amewapenda Watanzania kwa kuuchelewesha Ugonjwa wa Corona kuja Tanzania kwanza na ugonjwa huo kuanzia China. Huu ni mpango maalum wa Mwenyezi Mungu.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naona mlimshangaa Mheshimiwa Bungara, hajakosea, imeandikwa tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kila jambo. Endelea Mheshimiwa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, hivi walikuwa na matatizo hapo? Kheri shari minallahi taalah. Kwa hiyo, tunamshukuru Mwenyezi Mungu, kama lingekuwa jambo hili limeanzia Kariakoo na hali hii tuliyokuwa nayo sisi hii, aah saa hizi Tanzania ilishateketea! Kwa kuwa imeanzia China ili sisi huku tujipange. Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika watu ambao wamenufaika katika Awamu ya Tano, ah, basi Jimbo langu mimi Alhamdulillah. Katika Vituo vya Afya, nina vituo vya afya vitatu, aah, vizuri vyote! Nanjilinji mambo safi, Pande mambo safi, Masoko mambo safi. Barabara ya kwa Mkocho imekwisha, barabara za lami pale Masoko zimejengwa; aah, mambo Alhamdulillah! Mahakama nzuri kabisa, Chuo cha Maedeleo, aah, utasema watoto wako Chuo Kikuu cha nanii, kizuri kabisa! Hakika katika sifa ambazo Chama cha Mapinduzi kinasifiwa, basi Kilwa Alhamdulillah, hasa Kilwa Kusini! Mambo mazuri kabisa. Ninaamini kabisa kwa juhudi za Serikali ikisimamiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haya mambo ndiyo yametimia.

Mheshimiwa Spika, maana yake kuna wengine wanasema sijui Serikali Chama cha Mapinduzi; hapana, kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali na kuishauri Serikali. Kwa hiyo, haya yote yanayofanyika ni kwa sababu Bunge lako liko strong. Wala siyo CCM, CCM ilikuwa zamani tu, haya hata hayakufanyika. Hayakufanyika haya! Hii inatudhihirishia sasa, kumbe CCM hii ikitesa kwa makusudi, lakini miaka minne tu mambo mazuri eti. Miaka 50 ya CCM imeshindwa. Ingelikuwa speed hii mnayoifanya ya miaka hii minne kama mngelianza miaka 50, sasa hivi tusingeongea habari hizi. Yangekuwa mengine kabisa, lakini mmetuchelewesha. CCM imetuchelewesha! (Kicheko/Makofi)

MBUNGE FULANI: Sana tu!

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kama mngelifanya haya, kwa speed hii kwa mpangilio huu, aah, sasa hivi Tanzania kama Ulaya.

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Kwa hiyo, mimi nashukuru sana.

SPIKA: Mheshimiwa Bungara, kuna taarifa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Muda wangu, muda wangu jamani.

SPIKA: Aah, tunauchunga. Maana ulianza vizuri, halafu unataka kuharibu tena! (Kicheko)

Mheshimiwa Waziri tafadhali. (Kicheko)

T A A R I F A

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Bungara ambaye anaendelea kuongea sasa hivi kwamba Chama cha Mapinduzi wananchi walikikubali kikamchagua Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ndio Rais wa Tanzania, hakuna Rais mwingine. Rais alichaguliwa na wananchi wote mpaka hao wa Kilwa. Ndiyo maana Rais wetu hana upendeleo na katika kauli zake thabiti amesema maendeleo hayana chama, ndiyo maana katika uongozi wake ametekeleza maendeleo maeneo yote, ilimradi ni Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliona nimpe ndugu yangu, Mheshimiwa Bungara, hayo ili aweze kujua anachokiongea, ni kwamba imetekelezwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Rais wa Watanzania wote.

SPIKA: Anachosema Mheshimiwa Bungara ni kwamba Serikali hii imetekeleza miradi yote hii bila upendeleo pamoja na kwamba wapinzani mlipiga kura mfululizo kwa miaka yote ya hapana kwa bajeti hiyo. Ndicho anachosema tu.

Endelea Mheshimiwa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, mimi naona hatugombani sana kwa sababu kasema; nami nilisema zamani kwamba hii Serikali siyo ya CCM, ni ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli. Kwa hiyo ananiunga mkono tu. Kwa hiyo, wala sina matatizo na hilo. Mimi nilichosema, Serikali ya CCM miaka 50 imeshindwa, lakini ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli si ndiyo imefanya! Sasa tunapishana wapi? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitunzie muda wangu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mazuri haya na safari hii mimi nitapiga kura ya neutral, inaitwaje ile?

MBUNGE FULANI: Abstain,

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Abstain; sisemi hapana wala ndiyo, kwa sababu kuna mazuri halafu kuna mabaya. Kwa hiyo, nitakaa kati kwa kati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pamoja na maendeleo haya yaliyokuwepo lakini sisi Waheshimiwa tunaishi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunaapa hapa kuwa tutailinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunachukua misaafu na nini, tunalinda, tunaapa! Ukiapa hapa ina maana kuilinda Katiba ni pamoja na kukaa katika Ubunge miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kuna watu wameapa hapa, nitailinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; katikati ya miaka mitatu wameshuka, wametoka Bungeni amekwenda CCM.tatizo lililokuwepo, walipokwenda kule wakaahidiwa watapata Ubunge. Kwa hiyo, wakaacha Ubunge. Waliapa kwamba sisi tutakuwa katika Bunge miaka mitano, halafu wakatoka wakaingia CCM, halafu kufika CCM kule, wakaomba Ubunge. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kitendo kile cha kuomba Ubunge; na kwa kuwa waliahidiwa kwamba watapata Ubunge, wakasimamia, ndipo tunaposema Tume sio huru sasa. Tume sio huru hapo. Wakahakikisha lazima Mheshimiwa Maulid Mtulia awe Mbunge tena. Kwa kuwa wapinzani tulikuwa tuna nguvu, wakafanya figisufigisu kwa sababu wamevunja Katiba ya Jamhuri, akapigwa mtu risasi; alivyopigwa mtu risasi ni kwa sababu ya huyu Mtulia aliyevunja Katiba…

SPIKA: Samahani kidogo Mheshimiwa Bungara. Nilikuwa nawatafuta baadhi ya watu humu ndani; hivi Mheshimiwa Lusinde yupo! Ndio mchangiaji atakayefuata baada ya hako wewe. Nilitaka kumpa taarifa tu.

Endelea Mheshimiwa Bungara. (Kicheko)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, anapokuja leo Mheshimiwa Mtulia akasema Chama cha CHADEMA kifutwe kwa sababu ya kuua, lakini sababu ilikuwa Mtulia. Aliacha Ubunge ndani humu Mheshimiwa Mtulia wa Kinondoni huyu. Tunaposema tume siyo sawasawa, huyu Mtulia akapita bila kupingwa kwa tume kusema kwamba watu wa CHADEMA na CUF hawakupeleka fomu, akapita bila kupingwa.

Mheshimiwa Spika, tunaposema tume siyo huru wala halali, kwetu Kilwa sisi Madiwani wetu wamerudisha fomu kabisa, Mkurugenzi akasema fomu hazikurudishwa, wamepita bila kupingwa. Tunaposema tume siyo halali, siyo kwa sababu tu tume siyo huru; pale Maalim Seif anaposhinda na anaposema kwamba mimi naongoza ukafutwa uchaguzi. Tunaposema tume siyo halali ni hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana, tume huru ipo lakini watu sio huru. Sijui mnanielewa! Tume huru katika Katiba ipo, imeandikwa tume huru, lakini watu sio huru na wasimamizi sio huru. (Makofi)

SPIKA: Samahani kidogo. Tume hiyo hiyo inapomtangaza Selemani Bungara zaidi ya mara moja kwamba ameshinda uchaguzi, ni huru siyo huru?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, inakuwa hivi, lazima utoe kongoro kwenye mchuzi. Inaitwa kongoro mumchuzi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunavyoongea hapa tumesema mengi katika Bunge hili kuiambia Serikali, lakini miaka mitano imepita sasa hivi hali si nzuri. Nilisema hapa kuna watu wamepigwa risasi katika msikiti, Mheshimiwa Ismail Bweta kapigwa risasi msikitini; tumesema kwa Waziri Mkuu, kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, hamna chochote kinachofanyika, hali mbaya.

Mheshimiwa Spika, juzi wamekamatwa watu, wamechukuliwa watu na watu wasiojulikana, watu sita njia nne hapo; mtu wa kwanza Juma Selemani Farahan, Omary Kassim Mkwachu, Rashid Abdallah Mwinyigoha, Nurdin Ally Mnyiwiwa, Selemani Sefu, Yussuf Ramadhan, tarehe 15 Januari, wamechukuliwa hatujui wapi walipopelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaposema kwamba, Serikali ya CCM hamuwezi kushinda Masheikh wetu mpaka sasa hivi wako gerezani miaka sita, hamuwezi kushinda! Tunaposema Serikali ya CCM haiwezi kushinda sio kwa sababu ya kujenga barabara, barabara hata Afrika Kusini zipo, Marekani huko zipo na watu wanatolewa vilevile, barabara nini? Sisi Kilwa Kivinje barabara tulikuwanayo tukaikataa CCM, barabara sisi hatuchagui barabara tunataka utawala bora, utawala wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo watu wanatekwa wanapotea, wanapigwa risasi, Serikali ya CCM imekaa kimya tu. Katiba inasema kabisa kila mtu ana haki ya kuishi, nataka Serikali ya CCM Masheikh watoke Mahakamani; hatuna matatizo kukamatwa kwa watu, tuna matatizo mkiwakamata! Muwapeleke Mahakamani. Watu wetu wamekamatwa hawa sita Mheshimiwa Waziri Mkuu tarehe 15 wamekamatwa watu sita hatujui waliko na wamechukuliwa na watu, nini jamani? Halafu ninyi mchukue nchi ninyi? Mchukue nchi kwa kitu gani? Kwa barabara? Kwani Afrika Kusini barabara zilikuwa hakuna? Umeme ulikuwa hakuna? Walienda watu wakaenda wakamtoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana Waziri Mkuu tunakuomba sana. Tena Waziri Mkuu hata Kilwa hujaja kila siku unatuongopa tu nakuja leo, nakuja leo; njoo Kilwa tuje kukuambia mambo…

SPIKA: Mheshimiwa Bungara nchi hii kubwa anazunguka kila mahali atakuja tu.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, na Kilwa si katika nchi? Au Kilwa sio nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana vijana hawa sita hawa wamechukuliwa eti Serikali ya CCM miaka mitano mnashindwa watu kuwajua watu wasiojulikana, mnashindwa kuwajua ninyi? Kweli mnashindwa kuwajua ninyi? Intelijensia ninyi, mkutano wa Bwege mnauzuwia, intelijensia, watu wanachukuliwa vijana wetu…

MBUNGE FULANI: Wamechukuliwa na nani?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA:…Hamuwawezi, hamuwezi kuwakamata?

MBUNGE FULANI: Wamechukuliwa na nani?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA:…kuna nini Mheshimiwa, sikiliza, kuna kitu gani? Kuna siri gani?

Mheshimiwa Spika, tuliambiwa na Mkurugenzi wa Upelelezi hapa wa Usalama wa Taifa hakuna jambo linalofanyika Tanzania Usalama wa Taifa hawalijui, hapa kuna nini hapa? (Makofi)

SPIKA: Labda kulisaidia Bunge japo muda wako umeisha, wamechukuliwa na nani hawa watu?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, na watu wasiojulikana.

SPIKA: Hawa vijana sita?

MHE. SELAMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, watu wasiojulikana, lakini CCM mnawajua, mnawajua. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Bungara muda wako umeisha. Ahsante sana Mheshimiwa Selemani Bungara. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimefurahi sana kwa kuwa umerudi salama kutoka katika matibabu, tunakuombea Mwenyezi Mungu afya yako izidi kuimarika na Inshallah itaimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nitazungumzia sana habari za siasa na hususan hali ya kisisasa katika nchi yetu. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye utangulizi pale, misingi ya Katiba na kwa kuwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, undugu na amani. Kwa hiyo, Katiba yetu inazungumzia uhuru na haki ndiyo jambo la kwanza ili nchi yetu tuwe na mapenzi, kupendana, undugu na amani, lakini kama nchi yetu haitokuwa na uhuru na haki undugu na amani hautokuwepo katika nchi yetu, ndiyo msingi kwa Katiba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nia yetu ni nchi yetu na jamii yetu ijengwe kwa msingi huo, kwa hiyo kwa msingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambayo Serikali yake huamini Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na Mahakama iliyowakilisha kwa nchi pia yenye Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ukurasa wa saba inasema, nchi yetu inaendelea kuwa na amani na utulivu ili hali mimi kwa utafiti wangu naona hizi habari siyo za kweli kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina matatizo sana, kama hatukubali kama nchi ina matatizo naomba tutegemee kwamba nchi yetu huko mbele tunakokwenda hali itakuwa mbaya sana. Mimi mwenyewe nilimuandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani, kuna gari Noah ilifika Kilwa tarehe 29 Novemba, ikampigia simu kijana mmoja anaitwa Abdallah Said Ngaranga wakamwambia njoo uchukue mzigo wako hapa Kilwa Masoko, Mheshimiwa Abdallah Ngaranga alifuatana na Mheshimiwa mmoja anaitwa Hamisi Mtori, kufika pale Kilwa Masoko ile gari ya aina ya Noah nyeusi wakamuita yule kijana njoo ndani uchukue mzigo, alipoingia ndani yule kijana, kijana wa pili akawa yuko nje alivyoingia ndani wakamuita na yule wa pili, yule wa pili kaona hata Noah hii nyeusi siielewi akakimbia na askari mmoja akamkimbiza yule kijana akaingia katika makapa akapiga risasi yule askari, lakini jamaa hakusimama, akaondoka akafika Kivinje.

Mheshimiwa Spika, nikaitwa mimi kwamba mtu wetu mmoja katekwa, kwa bahati nzuri nikapiga simu Polisi Masoko nikaambiwa kwamba kweli yule kijana amekamatwa yuko polisi hapa. Usiku huo wakakamatwa vijana tisa, nikaenda polisi siku ya pili nikaambiwa kweli vijana walikamatwa walikuwepo hapa, lakini hatuwezi kuwaandikia kwa sababu walikuwa wamepitia tu. Nikaandika barua kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, katika vijana hao 11 wakarudishwa tisa na mpaka sasa hivi wako Kilwa, lakini wawili hawajarudishwa mpaka leo. Mmoja anaitwa Ndugu Ally Mohamed Shali na mwingine anaitwa Ndugu Yussuf Kipuka mpaka leo hawajarudishwa, lakini tuna uhakika walichukuliwa, walikuja kituo cha Polisi Kilwa Masoko mpaka leo hawajarudishwa na wazazi wao hawajulikani wapi walipo.

Mheshimiwa Spika, hii ni ukweli kabisa ninataka leo Waziri atupatie vijana wetu wawili hawa, ushahidi upo tarehe 21 Julai, askari hao hao walikwenda Kijiji kimoja cha Chumo wakaenda msikitini usiku saa saba, wakapiga risasi msikitini mle, wakawachukua watu 10 msikitini. Tumekwenda asubuhi damu zimetapakaa ndani ya msikiti, katika watu hao wakarudi wote 10, katika 10 waliorudi mmoja kafa, mmoja hana jicho, mmoja wakamwambia wewe unafuga ndefu wamemchoma ndevu zake, wamemnyoa ndevu kwa kumchoma moto, watu hawa wapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo mnatuambia kwamba nchi hii ina amani na utulivu mimi sielewi? Watu hawa wapo na huyo mtu mmoja amekufa tumemzika na majina yao nitakutajia. Samahani kidogo nimeandika aliyefariki anaitwa Ismail Bwela, aliyetoka jicho anaitwa Mbaraka Masaburi, aliyechomwa ndevu anaitwa Muharam Yalife, wapo! Wamepigwa risasi msikitini, mmoja amekufa na Serikali haijasema chochote mpaka leo na wamerudishwa wako Kilwa pale.

Mheshimiwa Spika, unaposema nchi hii ina amani na utulivu sielewi! Ninawaunga mkono waraka uliotolewa na Maaskofu. Nawaunga mkono Maaskofu mlichokisema ni sawasawa na maneno ya Maaskofu ni maneno ya Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii nchi imeharibika leo waislamu lazima wasiseme, tumetengenezewa jambo tunaitwa magaidi, kwa hiyo Mashekhe wote wa kiislam wakitaka kutetea haki zao kuhusu waislam wenzao tunaambiwa aah!Ninyi magaidi mnawatetea magaidi na ndiyo maana waislam hawawezi kusema sasa hivi, watasema vipi wakati wao wanaambiwa ni magaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawapongeza Maaskofu sasa hivi matumaini kwa Watanzania ni sehemu mbili tu Mahakama na Maaskofu, lakini waislamu hatuwezi kusema! Akipigwa muislam akisema unaambiwa unatetea magaidi eeh! Waislam wote tumerudi nyuma, tunaomba sana…..

Mheshimiwa Spika, nitunzie muda wangu.

T A A R I F A . . .

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, taarifa nimeipokea. Wewe tulia nitamjibu mwenyewe huyu.

Katika watu wanaolaani kwamba wale watu wamepigwa kwa makosa wale askari pamoja na mimi, lakini siwezi kuacha kusema watu wengine wakionewa haiwezekani!

Mheshimiwa Spika, polisi wakionewa nitasema, wananchi wakionewa watasema! Nia yetu hapa tunataka amani na utulivu ndiyo hoja, sijasema kwamba waliopigwa risasi polisi sijasema hivyo, nimesema polisi wameiniga msikitini wamewapiga watu risasi sasa mkatae kwamba hamkupiga watu risasi.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Rufiji hiyo ilikuwa watu wanapigwa risasi wanauawa, mkatengeneza mazingira kwamba wale wanaopigwa ni wa CCM na mkahalalisha Viongozi wetu wa CUF wamekamatwa na mpaka sasa hivi hawajulikani walipo, nitawatajia watu sita waliokamatwa katika operation mpaka sasa hatujui walipo, nataka tujue wako wapi.

Mheshimiwa Spika, basi nitakuletea majina ya hao watu sita waliokamatwa tunataka tujue wako wapi, ni wa Rufiji nitakuletea majina. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumushukuru Mheshimiwa Waziri kwa kufanikisha malipo ya wapiga kura wangu walio katika Chanzo cha Maji Champala, kwa kweli nakushukuru kwa hili, Mwenyezi Mungu akujalie afya, busara na hekima.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumshukuru Mheshimiwa Waziri naomba sana tatizo la maji katika Mji Mdogo wa Kilwa Kivinje ambapo ipo Hospitali ya Wilaya ambayo ina upungufu wa maji kwa muda mrefu. Nakuomba sana Mji Mdogo wa Kivinje uangaliwe kwa jicho la huruma sana, tena sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, napenda kukukumbusha Mradi wa Maji wa Mavuji ambao upembuzi yakinifu umekamilika lakini tatizo ni upatikanaji wa fedha kwa ajili ya mradi huo. Mradi wa Mavuji utakapopata fedha na kukamilika hilo ndilo suluhisho la upatikanaji wa maji katika Mji Mdogo wa Kivinje/Masoko. Nakuomba sana usimamie mradi huu wa Mavuji ambao upembuzi yakinifu ulifanywa na Wabelgiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba fedha zilizopangwa mwaka 2017/2018 zitolewe katika miradi ya maji na pia fedha zilizolengwa katika bajeti ya mwaka 2018/2019 zipatikane ili matatizo ya maji yapungue. Natanguliza shukrani, ahsante. Tunakuelewa na tunakukubali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah Wataalah. Pili, naishukuru Serikali ya CCM kwa kutufikisha hapa tulipofikishwa.

Mheshimiwa Spika, juzi niliwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba hata firauni alikuwa mbaya, lakini watu wake waliokuwa nyuma yake, wanamuunga mkono. Sasa huyu firauni aliota ndoto kwamba ataondolewa katika ufalme wake na akaamua kwamba kila nyumba kumi kuwepo na watu, kila atakapozaliwa mtoto wa kiume auliwe ili ufalme wake uendelee. Bahati nzuri akazaliwa Musa akamlea yeye mwenyewe na ndio yeye akamwangamiza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ina maana kubwa sana Waheshimiwa, hayo mnayoyatetea katika upande wa Serikali ya CCM, leo Waheshimiwa wawili wamesema CCM tunakufa eeh! Na mimi naamini kwamba CCM itajiua yenyewe kama alivyosema Nyerere. Naomba sana Serikali ya CCM muendele na hayo mnayoyafanya. (Makofi/Kicheko)


Mheshimiwa Spika, pia Serikali ya CCM mnatutaka Wapinzani lakini hamtutaki, lakini sisi hatuwataki lakini tunawapendeni. Tukiwaambieni maneno mazuri ndiyo tunawapenda hivyo, mfanye. Mkifanya tu mambo mazuri tu Tanzania, naomba sana Serikali ya CCM muwe wasikivu, moja hiyo.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie habari ya mifugo kwanza, Kilwa mmetuletea mifugo, tulikuwa hatuijui mifugo tunashukuru sana sasa hivi tunapata maziwa mengi, lakini hamjawatendea haki wafugaji walikwenda kule, hawana malambo wala hakuna majosho. Naomba sana Serikali ya CCM kwa kuwa mliwatoa mlikowatoa kuwaleta Kilwa hebu tuleeteeni malambo na majosho ili wakae vizuri wale wafugaji, hilo ni ombi la kwanza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi la pili kwetu Kilwa tuna maeneo ya ng’ombe wale, kuna vijiji vingine vimeambiwa wafuge ng’ombe wengine wawe wakulima Mheshimiwa Ulega najua. Kwa mfano, kijiji cha Nakiu ni kijiji cha wakulima lakini kuna ng’ombe siyo chini ya 2000 tunawaomba kila siku ng’ombe hao waende katika sehemu husika hawaendi, tatizo kubwa inawezekana viongozi wa Mkoa na Wilaya kama wamepata rushwa hivi, Mkuu wa Mkoa huyu na Mkuu wa Wilaya ninawasiwasi wamepata rushwa, kwa sababu Mkuu wa Wilaya kaandika barua kwamba ng’ombe wa kijiji cha Nakiu watolewe mwezi wa Novemba waondoke, lakini mpaka leo hawajatolewa na ukimuuliza Mkuu wa Wilaya anasema hela za kuwatoa sina. Ukiwaambia polisi wakawatoe wanasema hela hatuna na kijiji cha Nakiu kimewahi kutoa shilingi 1,500,000 kuwapa polisi kwamba hawana posho, hela wamechukua ng’ombe wapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali hii sasa Jeshi la Polisi hawana uwezo mpaka kijiji kitoe hela kiwape polisi, hela wamechukua na ng’ombe mpaka leo wapo, kweli hii Serikali, kwamba polisi hawana hela mpaka wanakijiji watoe hela na wanatoa hela halafu ng’ombe hawajatolewa? Mkuu wa Wilaya kala rushwa, Mkuu wa Mkoa kala rushwa, polisi wamekula rushwa na kama hawakula rushwa tuwaone ng’ombe watoke, leo bila hivyo wamekula rushwa! (Makofi/ Kicheko)

T A A R I F A . . .

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kusema na nipe dakika moja tu nisema. Nimesema kijiji kimetoa fedha kwa ajili ya kuwapa polisi kuja kutoa ng’ombe, lakini fedha wametoa na ng’ombe hawakutolewa kwa mazingira haya nina wasiwasi watu wamepewa rushwa na kama kutoa rushwa basi ng’ombe wale watoke, kama hawakutoka wamepewa rushwa. Ndiyo hoja yangu mimi, nina uhakika kijiji kimetoa hela na ng’ombe hawajatoka. Sasa kama hawajatoka hela ile ndiyo rushwa, sasa kama wewe unasema habari hizi ni za uongo thibitisha wewe, tuende kijijini mimi na wewe kama hela hazikutolewa.

Mheshimiwa Spika, mimi mwanasiasa eeh!
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupa akili Watanzania lakini hatuwezi kuitumia sawa sawa. Pili, ninakushuru wewe leo kwa kutumia busara kwa kuwasamehe wale waliokuja kupima samaki kwa kutumia ruler; na ndivyo inavyotakiwa kwamba mzee kama wewe uwe na busara. Tuwasamehe watu kama hawa; hawajui walitendalo, wanasema watu wengine huko.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono Waraka wa Maaskofu na Mashekhe, ili Serikali ya CCM irudi katika mstari unaotakiwa. Nawapongeza sana Mashekhe na Maaskofu, na Serikali muwe wasikivu myafuate yale waliyoyasema. Sisi wengine si Wachumi, sisi wengine wanasiasa. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema ili tuendelee tunahitaji vitu vinne, ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Tatizo ninaloliona mimi ni siasa safi na uongozi bora; hapa ndipo penye matatizo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siasa yetu ya mfumo wa vyama vingi, siasa ambayo ilikuwa kama tungeitumia vizuri maendeleo yangepatikana kwa haraka sana. Hata hivyo, kutokana na uongozi wa nchi hii, ambao unatumia sana ubaguzi katika siasa zake nina wasiwasi hatutafika lengo tunalotegemea la maendeleo ya nchi hii. Sisi watu wa kusini tulikuwa nyuma sana kimaendeleo na ndiyo sababu Mkoa wa Lindi tuko draw sasa hivi CCM wanne Wabunge na CUF wanne Wabunge ngoma draw; na kwa kuwa tuko wanne kwa wanne, mambo yako safi sasa hivi Mkoa wa Lindi; upo safi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia Mkoa wetu wa Lindi mimi ndiye Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Lindi, mimi hapa ndiye Mwenyekiti; na tunafanya kazi vizuri na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Waziri Mkuu kwa upande mwingine lakini katika mambo ya ubunge mimi ndiye Mwenyekiti wake. Tunakaa, tunapanga kwa pamoja na mambo mazuri kabisa yanapatikana katika Mkoa wa Lindi sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, ndiyo nakupa taarifa hiyo ndiyo Mwenyekiti mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo kutokana na mchanganyiko huu wa CUF droo na CCM mambo mazuri wakulima wetu sasa hivi wanapata leo ufuta bei inauzwa Sh.2,750. Tunakaa pamoja na Waziri Mkuu mimi nikiwa Mwenyekiti hapa. Tunapanga, tunaongea, tukishamaliza; leo tumeanzisha jambo lingine jambo jipyaa. Siyo stakabadhi ghalani, ni malipo ghalani ya ufuta. Jana tumeuza Sh.2,750 kwa kilo, siyo CCM huo ni mpango wa Mkoa wa Lindi. Kwa kuwa tunakaa pamoja tunashauriana tunamkosoa; Waziri Mkuu hapo sivyo hapo siyo stakabadhi ghalani, tatizo wanunuzi hakuna. Sasa hivi tuna Wachina, tuna Wahindi basi aah mambo yanakwenda vizuri tunakaa pamoja.

Mheshimiwa Spika, kuna njama ya makusudi ya Serikali ya CCM, ya makusudi ya kuturudisha nyuma Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa makusudi na sisi hiyo hatukubali. Leo katika gesi tulikuwa tunapata asilimia tatu wanataka kutuchukulia, service levy wanataka watuchukulie. Halmashauri zetu zilikuwa zinapata asilimia 0.3, leo Mheshimiwa Dkt. Mpango anapanga mpango hela hiyo itolewe katika gesi ije katika Serikali Kuu ili sisi turudi nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, korosho! Serikali hawawezi kuhudumia korosho; tukapanga mpango wetu wa Kusini tuingiziwe fedha kwa mujibu wa sheria, export levy asilimia 65 irudi kule kwa mujibu wa sheria wakachukua, wakaweka, waaa. Bilioni themanini na moja ya mwaka 2017/2018 wamechukua wamekula na wana mpango sasa hivi walete sheria humu kwamba jambo lenyewe kabisa lisiwepo kabisa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nakwambia sisi mpaka tarehe 30 kama hela yetu haikurudi tunakuomba Mheshimiwa Spika uje Mtwara kupokea maandamano ya wakulima wa korosho wa Mikoa ya Kusini. Kwa sababu inaonekana Serikali ya CCM sawasawa na patasi haifanyi kazi mpaka igongwe. Kwa hiyo nakuomba Mheshimiwa Spika tarehe Mosi Julai, ufike Mtwara upokee maandamano ya wakulima wa korosho wanataka fedha zao.

Mheshimiwa Spika, na utuelekeze isiwe kama mpima samaki, utuelekeze Mheshimiwa Spika, tunakupataje, kwa sababu maandamano ya vyama vya siasa yamekatazwa; maandamano ya Wabunge wa Mkoa wa Lindi na Mtwara kutaka hela zetu zirudi. Tunakwambia Mheshimiwa Dkt. Mpango. Tunamwambia Mheshimiwa Mpango fedha zetu atuletee kama hakutuletea tutafanya maandamano Wabunge wa Mkoa wa Lindi na Mtwara mpaka asubuhi na Mheshimiwa hivyo hivyo…

T A A R I F A . . .

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, taarifa yake butu. Namwambia Waziri kwanza mpaka tarehe
30 hela yetu watupe kama hawakutupa tunafanya maandamano, sasa una wasiwasi gani. Kama hakutupa tutafuata sheria zote na tunakuomba Mheshimiwa Spika uje kupokea maandamano ya Wabunge wa Mikoa ya Kusini kwa ajili ya Dkt. Mpango aidha atoe hela au ajiuzulu kama si hivyo; varangati lile la gesi linaanza tena Kusini. Varangati lile lile! Wamandharaba nafsi la yabuki (ajipigaye mwenyewe haliii). Tunakuomba Mheshimiwa Spika utupokelee maandamano yetu, tunaanza upyaaa! Hiyo moja. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, pili, Kiwanda cha Mbolea cha Kilwa kijengwe. Leo sisemi mengi, nawashawishi Wabunge wote wa Mikoa wa Kusini tuungane tupambane na Mheshimiwa Dkt. Mpango, huyu Mheshimiwa ana matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, nasema bajeti hii iongezewe katika mifugo, kilimo, maji; waongeze fedha, kama sivyo nitasema hapana, mkiongeza katika habari hii mwaka huu kwa mara ya kwanza nitasema ndiyo. Wakiongeza bajeti katika kilimo, maji, uvuvi Wallah Mheshimiwa utaona ajabu leo ndiyoooo, lakini kama hamkuongeza katika kilimo, uvuvi, mifugo; hapana!

Mheshimiwa Spika, sisi tunapigiwa kura na wakulima. Wakulima wakisema hawakupigii kura Mheshimiwa Dkt. Magufuli hapiti; na mimi nawajua CCM wajanja kweli kweli, wanataka mwaka 2019 ndipo wakulima wawape, wafanyakazi wawape hela! Nheheheee! Tuseme wanawafanya Watanzania wajinga, waseme mwaka 2019 eeh! Sasa hivi barabara safi ooooh, tunaongeza mshahara. Nasema wakiongeza tutawapiga, wasiongeze tutawapiga, wasitufanye sisi wajinga. Wajanja, wanatuuaua mwishoni, mshahara unaongezwa leo 2019, kuwafanya watu wapate tabu kwa miaka mitano mwishoni akhlini! Wanawazunguka Watanzania. Hizi siasa za hila hila na uongo uongo hizi ziishe mwaka huu; wakiongeza mwishoni tunawachukua tunawaweka, goli. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, mimi leo sisemi mengi leo mimi sisemi mengi, mgeni rasmi ni wewe. Inaonekana Bunge wameshindwa kumdhibiti Mheshimiwa Dkt. Mpango, wanatuambia tutawaletea habari za korosho, sisi maandamano, tutaandamana kweli kweli mwaka huu… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii leo. Pili, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi na uhai ili nichangie katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba yetu, inapambana au inakataza dhuluma na uonevu, lakini katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani inaonesha badala ya kulinda wananchi imekuwa wao ndio kipaumbele cha kuwatesa wananchi. Mtu yeyote mwenye dhuluma silaha zake ni mbili; silaha ya kwanza kutamanisha, maana yake kutoa rushwa, silaha ya pili ni kutisha na kuua. Tumefanikiwa Tanzania kwa kutumia silaha hizo za rushwa kuwanunua Wapinzani na kuwatesa watu, mmefanikiwa Serikali ya CCM kutufikisha watu wa Tanzania kuwa waoga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuoni ajabu kwa watu wa Serikali na watu wa CCM kuitetea Serikali ya CCM ambayo inawatesa Watanzania, hatuoni ajabu. Na hata enzi hizo wakati wa Firauni pamoja na ubaya wake Firauni lakini kulikuwa na wapambe wake waliokuwa wanamtetea; hii ina maana kwamba kila mtawala atatetewa na watu wanaomfuata nyuma yake hata kama akiwa mbaya, kwa hiyo, hatuoni ajabu kwa yote yanayofanyika katika nchi hii kuna watu wanatetea kwamba mambo mazuri tu. Hatuoni ajabu kwa jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.Kwa hiyo tunachoangalia hapa ni amani na utulivu na huu ni wakati wa Wizara ya Mambo ya Ndani. Najielekeza katika mada yangu, lakini ninachosema mikono yenu imeingia damu na sisi tunaweza tusiwape mikono kuanzia leo.

Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, katika hotuba ya Waziri Mkuu nilimwambia kuna vijana wangu wawili ambao wamewachukua mpaka leo hawajawarudisha na alisema atakuja kunijibu katika Wizara yake leo; naomba leo jibu langu nilipate, wako wapi na lazima wapatikane. Vijana hao ni Ali Mohamed Shari na Yusuf Kipuka.


Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna viongozi wamekamatwa kule Rufiji, leo nitakutajia viongozi 12, wamewakamata hatujui walipo. Wa kwanza Ziada Nongwa, huyu ni Diwani wa Viti Maalum kwa Tiketi ya CUF na ana mtoto mchanga, wamemkamata wamemchukua hajulikani wapi alipo, ni mama huyu. Nitaona ajabu sana akinamama wa CCM, mama mwenzenu tena Diwani kakamatwa hajulikani alipo, mseme hiyo ndiyo kazi tu, hapana; kwa hiyo, Ziada Nongwa Viti Maalum. (Makofi)



Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine ni Moshi Mchela, Mwenyekiti wa Kitongoji na ni mwanamke vilevile; Braziluli Lyango na mkewe; Jumanne Kilumeke, Mwenyekiti wa Ikwiriri; Kisangi Athumani, Mwenyekiti wa Kijiji na Katibu wa Vijana wa CUF; Kazi Mtokela, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikwiriri; Mtuko Astella, Katibu wa CUF, Kata ya Ikwiriri; Khamisi Nyumba Mkali, ni Katibu wa CUF, Wilaya ya Rufiji; Baratu Kisongo, Ikwiriri; Kanjoma Mlanzi, mfanyabiashara Ikwiriri; Abdallah Mkiu na Salim Mkiu, Mwenyekiti Mstaafu wa Umwe, wote hao wamewakamata, wako wapi? Waleteni mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Mwigulu Nchemba anapofika hapa atuambie wako wapi na lini watawafikisha mahakamani, wazee wao wanalia watoto wao hawawaoni. Namwomba sana Mheshimiwa Nchemba, tuwajue hawa watu wako wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niongelee kuhusu Mashekhe, sisi ni Waislam na Muislam ni ndugu kwa Muislam mwenzake, ukimuua Muislam mmoja umetuua wote, sisi ni ndugu, hatuwaelewi Serikali ya CCM, hatuwaelewi, kwa nini wanawatesa Mashekhe; kwa nini wanawafunga Mashekhe? Wanawachukua Mashehe wanawaweka ndani hawawapeleki Mahakamani, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waislamu wote tushikamane kama Mwenyezi Mungu alivyosema katika Quran yetu, tupambane na Serikali ya CCM. Mtume amesema mdhalimu yeyote anapofanya udhalimu wake tuseme na tukishindwa kusema tuuondoe udhalimu huo kwa mkono wetu; kasema Mtume. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaambia Waislamu wa Tanzania tuutoe uongozi wa Serikali ya CCM kwa mkono wetu kwa kutumia kura, tutumie kura tuitoe Serikali ya CCM, inatuonea Waislamu kwa nini? Tumekosa nini? Mashekhe wetu Zanzibar wako ndani, Arusha wako ndani, Lindi wako



ndani, kwa nini? Kila Ijumaa tuombe dua Serikali ya CCM itoke madarakani, inatuonea Waislam kwa nini, tuna kosa gani sisi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamandharaba nafsi laa yabuk, ajipigae mwenyewe halii, tuiondoe Serikali ya CCM madarakani, Waislam tuungane, tushikamane na Muislamu yeyote atakayesema kwamba Waislam wakae mahabusu huyu sio Muislam, kafir.

Tunaomba sana Waislam tushikamane, wametugawanya kwa makusudi, wametugawanya. BAKWATA inaisherehekea Serikali ya CCM, wengine sisi tukisema hatuonekani. Tunaomba sana Waislamu kama kuna Waislamu kweli tushikamane, Waislam tunateketea.



Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Mheshimiwa Waziri katika Wilaya ya Kilwa wapo vijana wawili wamechukuliwa na vyombo vya dola (Polisi), vijana hao ni Ndugu Ali Mohamed Shari na Ndugu Yusufu Kiduka. Vijana hawa tangu wamechukuliwa hawajulikani walipo, wazee wao wananiulizia na wamenituma wanataka kujua wapo wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, walikamatwa na Polisi tunahitaji wapelekwe Mahakamani. Pamoja na hawa waliokamatwa Kilwa, pia wapo wananchi wamekamatwa Wilaya ya Rufiji, pia nao hawajapelekwa Mahakamani na jamaa zao hawajui walipo, wengi wao ni viongozi wa Serikali na Chama cha Wananchi ambao ni hawa wafuatao:-

Ndugu Ziada Nongwa, Diwani Viti Maalum; Ndugu Moshi Machela, Mwenyekiti wa Kitongoji; Ndugu Jumanne Kilumike, Mwenyekiti Ikwiriri; Ndugu Kisinga Athumani, Mwenyekiti Kijiji na Katibu wa Vijana CUF; Ndugu Kazi Mtoteka, Mwenyekiti wa Kijiji; Ndugu Mtuku Astera, Katibu CUF, Kata Ikwiriri; Ndugu Khamisi Nyumba na mwanawe Katibu CUF, Wilaya ya Rufiji; Ndugu Blasil Linyago na Mkewe; Ndugu Baruti Kongoi, Ikwiriri; Ndugu Konjoma Mlanzi, Mfanyabiashara, Ikwiriri; Ndugu Abdala Mkuu na Ndugu Salum Mkuu, Mwenyekiti Mstaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hawa wote wamekamatwa, lakini hawajapelekwa Mahakamani kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Mheshimiwa Waziri nahitaji kujua wapo wapi na lini watafikishwa Mahakamani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika majumuisho yako napenda kupata majibu. Mheshimiwa Waziri katika Wilaya ya Kilwa, Kijiji cha Chumo, siku ya Ijumaa tarehe 21 Julai, 2017, Polisi walivamia msikiti wa Ali Mchumo usiku na kushambulia kwa risasi za moto na kusababisha kifo cha muumini Ismaili Bweta na kupoteza jicho kwa muumini Mbaraka Saburi. Je, Serikali inasema nini kuhusu wahanga hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, natanguliza shukrani.
Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi. Leo nakuona kabisa kama Spika kweli kweli! Uko strong, hongera sana. (Makofi)

Msheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi leo na mimi niseme kuhusu habari ya maji. Pili, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji. Tulikuwa tunadai hela tangu mwaka 1992, wananchi wangu walitoa eneo, walikuwa hawajalipwa, lakini kwa Waziri huyu aliyekuja, nilipomwandikia barua moja tu, basi Alhamdulillah vijana wangu wamelipwa hela zao zote. Namshukuru Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema kila siku, tatizo siyo Mawaziri, hakuna Waziri mzigo katika Serikali ya CCM, hakuna! Tena nampongeza Waziri wa Kilimo vilevile vijana wangu walikuwa wanadai, wamelipwa. Naomba sana, Mawaziri hamna makosa, tatizo ni Serikali ya CCM. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilisema siku moja na wakati huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa Waziri wa Ujenzi ndani ya Bunge hili. Nilimwambia Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwamba wewe sio mzigo, mzigo ni Serikali ya CCM. Nikisema hivyo, leo tunasema asilimia 22 ya miradi ya maendeleo ya maji ndiyo imetolewa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, afanye nini Waziri wa Maji wakati asilimia 22 ndiyo aliyopata na asilimia 78 hajapata? Mheshimiwa Waziri tumlaumu wapi? Na sisi ndiyo maana ikija hapa bajeti, tunasema hapana! Siyo hapana hatutaki bajeti ipite, tunasema hapana kwa sababu tunajua ninyi hamuwezi kutekeleza. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, tunasema hapana tunajua tunachokisema ndiyo, hakiwi ndiyo. Kwa hiyo, tunasema hapana kwa sababu tunataka hapana yetu iwe ndiyo, ninyi mjitahidi sasa mseme kwa kuwa Wapinzani wanasema hapana, tufanye mambo haya tuwaone kwamba Wapinzani kama wana…, yale yale, asilimia 22! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana Serikali ya CCM pelekeni fedha katika miradi ya maendeleo. Mkipeleka fedha katika miradi ya maendeleo, sisi tutasema ndiyo. Kama hampeleki fedha, tutasema hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunasema hapana kwa sababu tunajua mnachokisema sicho mnachokitenda. Hii nasema tena, hivi leo mwananchi umuulize ndege na maji nini kianze? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninyi Waheshimiwa Wabunge kama kweli kabisa mnawaonea wananchi huruma, tuwaulize kweli Waheshimiwa Wabunge wa CCM, kununua ndege na kuwapa watu maji, bora nini? Hapa tuseme sasa, wanaosema inunuliwe ndege msimame juu, halafu wananchi wawaone. Halafu wanaosema tuanze maji, wasimame juu halafu tuone kama mtarudi ninyi, mimi sio Bwege. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nakuomba uulize swali hilo, wanaosema ndege inunuliwe wasimame, halafu wanaosema maji yawepo tusimame, halafu tukaoneshe Watanzania huko, he, he, he! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, utaruhusu kidogo tusimame? Naomba sana tuwajali watu wetu, hamna Waziri mbaya, hayupo. Waziri ni Mbunge na anajua matatizo ya wananchi, lakini Serikali ya CCM ni mzigo. Simsemi Mheshimiwa Dkt. Magufuli, ah, ah, Serikali ya CCM ni mzigo. Sio Mheshimiwa Dkt. Magufuli! Mheshimiwa Dkt. Magufuli sio mzigo, Serikali ya CCM ni mzigo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, naomba sana sisi tuna matatizo ya maji katika Mji wa asili wa Kilwa Kivinje, mji mdogo tu wa Kivinje. Mwaka 1980 Mji wa Kivinje tulikuwa tuna mabomba yetu, tunafungua maji, tuliyarithi kwa mkoloni. Leo Kilwa Kivinje kuna Hospitali ya Wilaya. Ndani ya Hospitali ya Wilaya hakuna maji na nilisema siku moja hapa kwamba Hospitali ya Wilaya ya Kilwa Kivinje hakuna maji. Akasimama Mheshimiwa Mkuchika wakachukua matenki ya maji wakaweka hospitalini, wakafungua wakasema Bwege muongo, maji yanafunguka haya. Kumbe wamechukua maji Nangurukuru. (Makofi)

Tunaomba sana, Mji wa Kilwa Kivinje, Mheshimiwa Mkuchika anajua hilo. Wakanisololea sana hapa, lakini Mji wa Kilwa Kivinje hakuna maji. Hospitali ya Wilaya iko Kivinje, watu wananunua maji shilingi 1,000 wanapeleka hospitali. Hospitali ya Wilaya, halafu ninyi mnanunua ndege maskini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri, Hospitali ya Wilaya ipate maji na Mji wa Kivinje na Mji Mdogo wa Kivinje upate maji. Kuna vitongoji saba Nangurukuru, Matandu, Singino, Mgongeni, Magengeni, Mayungiyungi, Kisangi Mjini, Kisangi Shamba, vyote havina maji. Tunaomba sana tupate maji. Kuna vijiji havijapata maji vingi tu, Vimaliao, Pande, Kikole, Luatwe na Nanjilinji hakuna maji. Miaka 57 ya CCM tunaongelea habari ya maji wakati ndiyo nchi ya nne kuwa na maji duniani, lakini hakuna. Hohaa! Serikali ya CCM, amkeni! Hohaa! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hakuna maji, na nimesema hapa Bunge lililopita, kama hatupati maji mwaka 2020 CCM kwaheri, bye, bye, Waheshimiwa! Maji ni uhai, leo mashehe wetu wako Magereza huko, Magereza hakuna maji, na sisi hatuwezi kuswali bila maji. Lazima tutie udhu, tupate maji. Mashehe wako Magereza ya Segerea, maji hakuna. Hawaswali, hawafanyi chochote huko.

Mheshimiwa Spika, tunawaambia kila binadamu kaumbwa na maji, maji ni uhai. Nakusifu sana Waziri wa Maji, namsifu sana Katibu wa Wizara ya Maji Mheshimiwa Kitila Mkumbo, alikuwa huku huku na sijui ilikuwajekuwaje, alikuwa huku huku kwetu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana tuuze ndege mbili tutatue tatizo la maji. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, basi kwa kuwa leo uko vizuri, hebu piga kura, wanaotaka ndege na maji wengi nani? Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kunipa nafasi hii leo na kwa kuwa umeniambia taratibu basi leo nitakuwa taratibu kabisa. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amewapa akili Watanzania na akili kazi zake mbili tu, kujua ukweli na uongo, ndiyo kazi ya akili, hayo mengine kupata Uprofesa na nini, hayo mengine tu, lakini kazi ya akili ni kujua ukweli na uongo, nyeupe na nyeusi, ndiyo kazi yake hiyo hiyo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kwa kusema tunamnukuu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mungu amuweke mahali anapostahili, alisema ili tuendelee tunahitaji vitu vinne; ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Nchi hii vitu vyote hivyo vinne vipo, ardhi ipo ina kila kitu, watu ndiyo wengi tu, tunafika milioni 50 na ngapi sasa hivi, siasa ipo na tangu mwaka 1961 mpaka leo chama cha siasa kinachoongoza katika nchi hii ni Chama cha CCM, kwa hiyo siasa ipo na uongozi upo, lakini unaotakiwa ni uongozi bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mipango yote mnayopanga hii, yote hii, kama siasa haikuwa safi na uongozi haukuwa bora, sawasawa na hakuna. Tangu nimeingia Bunge hili mwaka 2010 mipango inapangwa kweli kweli lakini utekelezaji hakuna. Kwa hiyo, mimi ni mwanasiasa na huwezi ukaendelea kama siasa ikiwa mbaya. Naomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali sikivu, huu uwanja wa siasa kama tukiuchezea hali itakuwa mbaya sana katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango yote hii wanayopanga, angalia sasa hivi, tumepanga mipango mikubwa, limekuja jambo hili la kununuliwa Wabunge, hela zote ambazo tulipangia katika mambo ya maendeleo zinakwenda katika bajeti ya kufanya uchaguzi.

KUHUSU UTARATIBU

HE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema fedha zimetumika katika uchaguzi. Uchaguzi ambao ulikuwa hauna sababu yoyote na hiki kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Mpango, mwenyewe kasema katika ukurasa wa 44 kwamba fedha trilioni tisa hazikupatikana na mambo mengi ya maendeleo hayakufanyika, lakini fedha hizo zilienda katika uchaguzi. Sasa unachosema kwamba kununuliwa hata mimi si nilifuatwa! Hata mimi mwenyewe nilifuatwa, sasa ukitaka ushahidi anaitwa nani yule Mheshimiwa Jenista uje, tukutane baadaye nikwambie walikuja nani na nani walitaka kuninunua mimi nikakataa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Dau alisema jambo kubwa sana katika Bunge hili na mimi nasikitika sana, Waziri Mkuu anachaguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anathibitishwa katika Bunge hili. Kwa hiyo, Waziri Mkuu anachaguliwa na Rais na kuthibitishwa na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dau jana alisema kwamba kuna Waziri mmoja wa Ujenzi alimwambia habari ya boti lakini akajibiwa majibu mabaya na Waziri wa Ujenzi. Sasa hiyo siyo mara moja tu, Mheshimiwa huyu Waziri wa Ujenzi alikuja Kilwa hivyo hivyo nikamwambia kuna mradi wa maji wakati huo alikuwa Naibu Waziri wa Maji, nikamwambia nimeonana na Waziri Mkuu na yeye akanijibu kama alivyojibiwa Bwana Dau, akasema Waziri Mkuu nani, bwana! Mimi namtambua Mheshimiwa Magufuli tu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuseme Waziri Mkuu ambaye amechaguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wwa Tanzania na kuthibitishwa na Bunge hili na mimi nilimpigia kura ili awe Waziri Mkuu. Halafu kuna mtu mmoja ambaye anachaguliwa tu lakini wala hathibitishwi na Bunge anamdhalilisha Waziri Mkuu. Mimi nikifikiri anadhalilisha ninaposema mimi mpinzani tu, kumbe hata akisema Mheshimiwa Dau wa Mafia naye anaambiwa hivyo hivyo hii siyo desturi nzuri Waheshimiwa, huyu ni Waziri Mkuu asidharauliwe na najua watu wa CCM nimewaambia jana vipi wamesema bwana sisi tukisema sana tunaitwa katika maadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nanukuu ya jana. Jana hiyo hiyo kuna Mheshimiwa Sugu hapa kasema kwamba watu wanauliwa akatoka Waziri mwingine akasema hajauliwa. Sasa nina ushahidi kwamba Polisi wa Tanzania wameua watu wangu Kilwa ndani ya msikiti na yule Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alisema kwamba kama kuna ushahidi atoe, mimi ushahidi ninao kwamba Polisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walimuua Ismail Bweta katika Msikiti Chumo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mwigulu akaniita wakati huo akiwa Waziri wa Mambo wa Ndani akaniambia niwalete hao watu, nikaja nao watu kwa Waziri Mwigulu, baba wa marehemu na yule mtu aliyetolewa jicho na Polisi. Mheshimiwa Mwigulu alipopewa taarifa akasema jambo hili zito umpeleke kwa Waziri Mkuu. Namwambia tu huyo Mheshimiwa anasema kwamba Polisi hawajaua watu. Nikawapeleka wale watu Waziri Mkuu wakamwambia, kidogo alie akasema kweli Serikali imefanya kosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hayo mambo yapo nchi hii na mnaua, mnateka na mimi ushahidi ninao, hii yote tunasema ili tuendelee tunahitaji vitu vingapi vinne ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Kitendo cha watu kuuliwa na taarifa mnapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa tena! Tunapanga mipango ya nchi kwamba kama siasa itakuwa mbaya. Nimeanza kusema kwamba siasa mbaya mipango yote itakuwa hakuna kama siasa itakuwa mbaya sasa uelewi tu, mzee mwenzangu huelewi ninachokisema?… (Makofi/Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya namalizia kwamba, naomba sana Serikali muwe makini, muwe wakweli, kwa sababu Mtume anasema utakuja wakati viongozi watakuwa waongo na watu watawajua kuwa waongo, lakini watawapigia makofi na kuwachinjia nyama ili hali watakuwa waongo viongozi hao. Basi msitegemee rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo mwisho wa yote, naomba korosho zote wakanunue kwa sababu waliahidi wakanunue ili mambo…watu wetu wa Kusini mipango yao iende vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake mipango bila korosho kununua hakuna mipango. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. SULEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, dakika tano ni kidogo sana. Kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, nitaongelea mambo mawili tu kuhusu uvuvi na kilimo.

Mheshimwa Spika, Wilaya ya Kilwa ni wavuvi wakubwa wa daga, hususan dagaa mchele na dagaa lumbunga. Kwa kipindi kifupi tumepata mtafaruku mkubwa tulipoingiliwa na operesheni, ikiongozwa na Wanajeshi na kuambiwa kwamba uvuvi tunaotumia ni uvuvi haramu na nyavu tunazotumia ni nyavu ambazo hazitakiwi kuvulia.

Mheshimiwa Spika, wavuvi hao walikuwa na leseni na nyavu zao zilikuwa zinakaguliwa tangu mwaka 2009 mpaka leo. Cha kusikitisha sana nyavu hizo zimeambiwa zisivue. Katika ukurasa wa 37 wa kitabu hiki, wanasema unaweza kumtambua mvuvi anayeshughulika na uvuvi haramu ikiwa mvuvi huyo atatekeleza shughuli zake za uvuvi bila kuwa na leseni. Kwa hiyo, mvuvi haramu ni yule ambaye anavua bila kuwa na leseni lakini wavuvi wetu waliokamatwa waliokuwa na leseni wanaambiwa wavuvi haramu.

Mheshimiwa Spika, naomba jambo hili liangaliwe upya na wale wavuvi waruhusiwe kuvua na nyavu zile kwa sababu leseni wanazo na nyavu zao zilikaguliwa. Hata kama sheria zinasema zile nyavu ni haramu, lakini wananchi walinunua zile nyavu wakapewa leseni. Siyo chini ya wavuvi 3,000 katika Wilaya yangu ya Kilwa wameambia wasivue kuanzia sasa wakati leseni wanazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kwamba pengine zile nyavu ni haramu, lakini leseni wanazo na waliotoa ni Serikali. Naiomba Serikali itumie hekima ili wale wavuvi waendelee kuvua kwa nyavu zile mpaka hiyo sheria itakaporekebishwa. Kwa sababu sisi wengine Waislamu tunasema, nguruwe haramu lakini dharura ikitokea ni halali kula kidogo ili mambo yaendelee. (Kicheko/Makofi)

Mheshimwa Spika, naomba Serikali sikivu ya …

SPIKA: Mheshimiwa Bungara aya ya ngapi hiyo?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Aya ya 150 Surat Maida. (Kicheko/Makofi)

Mheshimwa Spika, kwa hiyo, kwa heshima na taadhima, kwa kuwa Serikali hii sikivu na wale wananchi wavuvi watakuwa hawana kazi, hali zao za kimaisha zitakuwa mbaya, nakuomba Mheshimiwa Mpina uongee na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa wanyonge na hakuna wanyonge nchi hii kama wavuvi, waruhusiwe kuvua ili waende na maisha yao. Hilo moja. (Kicheko/Makofi)

Mheshimwa Spika, pili, nguruwe haramu lakini katika dharura unakula. Basi na nyavu hizo haramu lakini wapewe wavue.

Mheshimiwa Spika, nakuja katika korosho. Sisi tunaishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiongozwa na Mheshimiwa Magufuli kwa kutuambia mtanunua korosho kwa shilingi 3,300; wakulima waliandamana wakafurahi, lakini kilichotokea hali ni mbaya sana. Mpaka leo wakulima bado hawajalipwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Dakika zako zimeisha Mheshimiwa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Allah!! (Kicheko)

SPIKA: Zimeisha kaka.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Namalizia tu. Ninachoomba watu wa Kangomba nao walipwe kwa sababu na wao walipeleka korosho AMCOS zikapokelewa na Serikali wanazo. Kwa kuwa wanazo korosho, za Kangomba walipwe, ndio hoja. Kwa sababu muda wangu umeisha, nilitaka nifafanuliwe sana hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu. Pili, nawashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Kilwa Kusini kwa kuongea nao kwa muda mfupi baada ya sintofahamu ya chama chetu ya muda mrefu na hatimaye mgogoro umemalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Jaji kwa kutumia hekima kuumaliza mgogoro kwa njia ya kisayansi. Sasa chama ni kimoja na Wabunge wa CUF ni Wabunge wa CUF hakuna lile swali la CUF gani, sasa hivi CUF ni moja. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Jaji aliyehukumu kesi hii. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachangia hotuba ya Waziri Mkuu, ukurasa wa 15 umezungumzia hali ya kisiasa na Mheshimiwa Waziri Mkuu amejisifu kwamba hali ya kisiasa ni nzuri na kulikuwa na chaguzi za marudio na CCM imeshinda kata 230, CHADEMA kata moja, CUF hakuna kitu. Mimi siamini kwamba ushindi huu wa kata 230 na CHADEMA kushinda kata moja kwamba uchaguzi huu ulikuwa huru na wa haki. Siamini kabisa na hali ya kisiasa katika nchi yetu ni mbaya mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano katika Wilaya yangu ya Kilwa tulingombea kata tatu na CCM zote wakashinda. Hata hivyo, Polisi waliojaa katika uchaguzi huo wa kata tatu utasema kuna vita ya Vietnam na Marekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchaguzi huo Janjaweed wa CCM waliwateka watu watatu. Tarehe 27 walimteka kijana mmoja anaitwa Abdulrahman Bungara, wakampiga, ni mwanachama wa CUF, wakamnyang’anya saa na hela. Tarehe 29 hao hao watu wa CCM wakampiga kijana mmoja jina lake Shaban Mkongo wakamnyanganya fedha. Tarehe 2 siku ya uchaguzi walimteka Juma Ngondae, wakampiga na wakamfikisha Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wote tulifungua mafaili ya kesi lakini mpaka leo hajakamatwa mtu hata mmoja. Waliokuwa wanafanya matukio hayo wanajulikana na gari waliyokuwa wakitumia kuwateka watu hao inajulikana na gari hiyo ni ya Mbunge mmoja ambaye yupo humu humu ndani. Tumefungua kesi lakini mpaka leo hawajakamatwa lakini mwenye gari tunamjua ni ya aliyekuwa Mbunge wa CUF sasa hivi yupo CCM, gari yake tunaijuwa ndiyo iliyotumika kuteka watu wote hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zikaja kata zingine tatu, wagombea wetu wakarudisha fomu na ndiyo niliyowapeleka kurudisha fomu. Siku ya siku wakasema fomu za CUF zote hazikurudishwa na wagombea wa CCM wamepita bila kupigwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unapojisifu wewe Waziri Mkuu kwamba tulipita, upitishaji wenyewe wa kunyang’anya, hakuna siasa safi na uongozi bora katika nchi hii. Tunaamini kabisa kwa Tume hii ya Uchaguzi 2020 tegemeeni kutakuwa na vita kubwa sana kati ya wananchi na watu wa Tume. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Uchaguzi Mdogo ndiyo mnachukua Jeshi zima, mnapeleka Kilwa Kivinje Jeshi zima, Kilwa Kivinje mnaleta Jeshi zima, je, Uchaguzi Mkuu mna Jeshi ninyi la kusambaza Tanzania nzima, jeshi hilo mnalo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa sana CCM inashindaje? Nyavu za watu mnachoma moto, watu mnawateka, mnawapoteza, korosho zao hamuwalipi vizuri, wakulima mnawauzi, wafanyakazi mishahara hamuwapi, wavuvi…

MWENYEKITI: Wewe na mimi ndiyo nakumalizia hapo hapo, ahsante kwa mchango wako, tunaendelea.

WABUNGE FULANI: Aaaaaa.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Hata bila kengele?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Sasa ikiwa kwamba…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Selemani, muda wako umeisha. Tunaendelea na Mheshimiwa Kubenea.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda ulikuwa bado.

MWENYEKITI: Hapana, tulia Mheshimiwa. Mheshimiwa Kubenea.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kuniwezesha leo kuwa na afya na kuongea katika Bunge lako Tukufu. Pili, nawashukuru wapiga kura na tatu nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na mikutano ya hadhara. Sisi sote pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeapa kuilinda, kuitetea na kuienzi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Cha ajabu Serikali hii ya Awamu ya Tano wanazuia mikutano ya hadhara na maandamano kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi hata pale Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Magufuli aliporuhusu kwa kusema kwamba sisi Wabunge tunaruhusiwa kufanya mkutano kwenye majimbo yetu lakini Jeshi la Polisi sisi Wabunge nao wanatuzuia. Mimi mmojawapo nimezuiliwa mikutano na polisi inayofika mitano. Nikiandika barua ya taarifa wao wazuia, mwisho juzi nimeandika barua nikazuiwa kwa kusema kwamba kwa kuwa Mheshimiwa Mpina amechoma nyavu za wavuvi pale ukifanya mkutano basi hali ya hewa itakuwa siyo nzuri.

Kwa hiyo, mimi naiomba Serikali sikivu, iruhusu mikutano ya hadhara kwa mujibu wa sheria za nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza zaidi ndani ya Bunge hili kuna Kamati ya Katiba na inaona Katiba inasiginwa imekaa kimya. Hatusemi Bunge dhaifu lakini kuna tatizo kidogo kwamba Kamati ya Katiba isimamie jambo hili. Hilo ni jambo la kwanza nililotaka kulizungumzia. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tunasema nchi yetu haina matatizo, ina usalama na amani, lakini mimi naona si sahihi. Kwa mfano, tarehe 20 Aprili, 2019, kuna kijana wangu amekamatwa na amepelekwa Mtwara na sijui kama atarudi. Kwa sababu mwaka jana katika Bunge hili hili nilisema kuna vijana wangu watatu walikamatwa Ali Shari, Yusuph Kipuka na Ali Yusuph Kipuka mpaka leo hatujui walipo. Niliomba sana na Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo alikuwa rafiki yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba lakini hawajapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa wale wanaosema kwamba kuna utulivu na amani katika nchi hii ni kwa kuwa majimboni kwao hawajapata matukio kama haya. Kwa sisi Wapinzani matukio haya yapo, tunaomba Serikali kijana huyu Rashid Salio Rashid aliyepelekwa Mtwara Mheshimiwa Kangi Lugola leo piga simu Mtwara Mheshimiwa huyu kijana aachiwe asipotee kama waliopotea mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema nchi hii ina matatizo. Katika Uchaguzi Mdogo Kilwa Kivinje walitekwa watu watatu na taarifa tukatoa na Mheshimiwa Kangi Lugola ukanielekeza nikafungue kesi, kesi imefunguliwa KLK RB.397 ya 2014. Cha kusikitisha sana walioteka watu hawa wanajulikana, gari ambayo imewateka ya Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoka Liwale inajulikana na kuna gari lingine ambalo lilisaidiana lenye namba T693DDD Toyota Passo ya Mheshimiwa Prosper Rweikiza inajulikana lakini kwa bahati mbaya zaidi…

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bungara, nitakulindia dakika zako subiri tusikilize taarifa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji asipotoshe Bunge kwa sababu Bunge ni chombo maalum/mahsusi. Gari analolitaja kwamba ni la Mheshimiwa Kuchauka ndiyo liliteka watu si kweli.

WABUNGE FULANI: Kweli.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, gari yangu mimi ilikuwa na namba T324 na namba ambayo iliingizwa kwenye mtandao kwamba imehusika na utekaji ule ni namba T024. Sasa namba hizo ni tofauti na tofauti.

WABUNGE FULANI: Aaaa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, gari anayoitangaza kwamba ni gari yangu siyo kweli. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Bungara.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachosema taarifa nimetoa Polisi na hiyo gari ilikuwepo Kilwa, haikukamatwa kwa sababu walikuwa wanamlinda huyo Mheshimiwa na kama ingekuwa siyo kweli kwa nini isikamatwe? Hiyo namba anayosema ni kweli ilikuwa namba hiyo na tulivyoipeleka ikaoneka gari ya Scania siyo Toyota Land Cruiser. Kwa hiyo, ile gari namba iliyowekwa ilikuwa ya bandia lakini ile gari ni namba yake na ndiyo maana hawakuikamata kwa sababu ilikuwa na namba ya bandia. Mimi naendelea, taarifa yako sikuipokea, ni gari yako na ushahidi upo na kila kitu kipo sahihi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gari nyingine ni T.693 DDD Toyota Passo ya Mheshimiwa Prosper Rweikiza. Taarifa nilitoa Polisi, gari haikukatwa na watu wamepigwa mapanga na watu wao, hii inaonyesha kwamba amani hakuna. Nakuomba Mheshimiwa Waziri Kangi Lugola fuatilia jambo hili na barua niliandika kwa RPC na wewe nikakupa nakala na ninayo hapa, barua hii hapa na Mwenyekiti nitakupa nakala. Mimi sisemi maneno kwa ujinga ujinga na uhakika. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, tulitoa taarifa kwamba kuna watu walipigwa risasi kule Chumo katika Msikiti na Mheshimiwa Mwingulu aliniambia niende kwa Waziri Mkuu. Kwa Waziri Mkuu nikaeenda na barua niliandika nikampelekea Waziri Mkuu. Yeye aliwaambia wale watu atawaita mpaka leo hajawaita na nakala Mheshimiwa Lugola unayo. Naomba Waislamu wale waliopigwa risasi Chumo muwaite muwape fidia kama sivyo tunasema Serikali ya CCM wauaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tukio la utekaji katika Uchaguzi Mdogo, nakuomba Mheshimiwa Lugola uniambie na ushahidi upo. Kama hiyo gari Mheshimiwa Kuchauka anasema sio yake ailete Toyota Cruiser hiyo Kilwa na kwa nini haikukamatwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuthibitisha kwamba Serikali ya CCM inawalinda majambazi, gari hii inayoteka watu ikamchukua iliyemteka wakampeka Polisi na Polisi wanajua kwamba gari hii ndiyo iliyomteka. Pia kwa ushahidi TAKUKURU wakati anatekwa huyo Juma Gondaye walikuwepo na gari waliiona. Mimi nashangaa sana ninyi mnavyosema nchi hii ina amani wananchi mliwapiga risasi, mmewatoa macho, mmewachoma moto kama nao wasingekubali sasa hivi nchi ingekuwa siyo ya amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho Mashekhe wa Uamsho. Mwaka jana alisimama hapa Mheshimiwa Kabudi akasema upelelezi unakamika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WABUNGE FULANI: Aaaa.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Bungara muda wako umeisha.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba jambo hili la Mashekhe lishughulikiwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii leo tarehe 6 Mei. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kufika katika Bunge hili na afya tele. Tatu natoa pole kwa mfanyabiashara Dkt. Reginald Mengi Mungu amuweke mahala pema peponi huyu Mheshimiwa miaka ya 80 huko tulimuita Kilwa akawa mgeni rasmi ni katika kuchangia elimu Wilaya ya Kilwa alitoa shilingi milioni 20, enzi hizo milioni 20 nyingi sana, kwa hiyo, tunatoa pole za dhati watu wa Kilwa na Ishallah Mwenyezi Mungu amuweke mahali anapostahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu 1961 tunapata uhuru mpaka leo miaka 58 Bunge linazungumzia habari ya maji, kila Mbunge anayesimama hapa anasema kwake hakuna maji sio Mbunge wa CCM wala sio Mbunge wa CUF, wala wa CHADEMA. Naomba sana ombi langu kubwa sana katika mfuko wa maji tuongeze shilingi 50 ili yapatikane maji, naona tatizo kubwa ni fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri shilingi 50 iongezwe katika mfuko wa maji ili watu tupate maji. Waheshimiwa maji ndio maisha bila maji kila kitu hakifanayiki kwa hiyo, naomba mheshimiwa Waziri tunawasaidia wafadhili kwamba tutoe shilingi 50 tuingoze katika mfuko wa maji tafadhali, hilo jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili sisi Kilwa kuna miradi ya DCA miradi 17 lakini mpaka sasa hivi vimechimbwa visima vitatu tu tunaipongeza Serikali kwa mfano hivyo visima vitatu vyote vimechimbwa katika Jimbo langu. Lakini katika visima vitatu kisima ambacho kina maji safi na salama ni kisima kimoja tu cha Pande lakini kule Kisongo na Limaliyao visima vyote viwili maji yake ya chumvi na tulisema siku nyingi sana kwamba mazingira ya Limaliyao na Pande tunapenda tuletewe mabwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulisema kwamba kule mazingira yake ukichimba maji lazima yawe maji ya chumvi, tunaipongeza sana Serikali Limaliyao wamechimba visima si chini ya sita lakini vyote ni maji ya chumvi. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali mabwawa yajengwe katika maeneo hayo ya Limaliyao tunaiomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili tunashukuru hiki kisima cha Pande kina maji mengi na mazuri hakina mataatizo kabisa kwa saa moja inatoa lita 14,000. Kwa hiyo, tunachoomba sasa miundombinu yanaweza yakapelekwa maji katika vijiji vitatu katika eneo hilo kwa hiyo tunamuomba Mheshimiwa Waziri Ustadhi Mheshimiwa Profesa Mbarawa onesha ujasiri wako ili tupate maji katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tumepata hela tumeona katika kitabu tumepata hela milioni 300 kwa ajili ya Mji wa mdogo wa Masoko. Lakini Mheshimiwa Profesa kuna Mji mdogo wa Kivinje hakuna bajeti katika mradi wowote wa maji katika Mji mdogo wa Kivinje na Mji mdogo wa Kivinje kuna hospitali ya Wilaya na siku nyingi nasema hiyo hospitali ya Wilaya ina upungufu mkubwa wa maji. Naomba sana Mheshimiwa Profesa uangalieni Mji wa Kivinje ambao una wakati si chini watu 15,000 lakini maji hamna kabisa na hakuna mpango wowote wa maji niliouna katika kitabu hiki ambapo umepangwa mji mdogo wa Kilwa Kivinje isipokuwa Mji wa Kilwa Masoko Alhamdulillah maji yapo na kuna mradi vile vile unakwenda huko, lakini tunaomba sana Mji wa Kilwa Kivinje upatikane maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna vijiji havina maji machache sana kwa mfano Kata ya Kikole kuna Luwate, kuna Kikole yenyewe, kuna kijiji cha Kisange mbalambala , maji nayo hakuna. Pia kata ya Likawage kuna kijiji kimoja kinaitwa Nainokwe kilikuwa katika mradi wa visima 10 kisima kimechimbwa hakina maji hata kidogo tunaomba nacho kijiji hiko kipatiwe maji, naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kijiji cha Mavuji, kijiji cha Mchakama, Kijiji cha Mkondaji katika Kata ya Mandawa navyo maji hakuna lakini nasisitiza sana kuna mradi wa Mavuji ambao mradi huo ulikuwa chini ya Wabeligiji lakini ikaonekana hela ziko nyingi sana, sasa hivi umeingia katika mpango wa msaada wa India.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Profesa sana tena sana mradi huo wa Mavuji kama hautafanikiwa matatizo ya maji katika Mji mdogo wa Kivinje, Mji mdogo wa Masoko utamalizika nakuomba sana na kwa kuwa Serikali hii ni sikivu Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni sikivu naamini kabisa kwamba mradi huu wa Mavuji huu tutafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa Mheshimiwa Dkt. Magufuli sikivu kuna mradi wangu mmoja wa barabara kwa Nkocho Kivinje paka nikaitwa mimi jina langu Nkocho kwa Kivinje, nikamuomba siku moja tu sasa hivi lami ilishakwisha iko moto imekwisha lami, ilishajengwa ni sikivu Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni msikivu. Lakini msimuangushe nakuombe Mheshimiwa Prof. Mbarawa usimuangushe hebu fanya mpango wa maji yawe safi haya ili Mheshimiwa Dkt. Magufuli apate sifa yake hiyo inayotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hayo namuomba Mheshimiwa Magufuli kila kizuri kidogo kutakuwa na kasoro kidogo hawa watu wanaotekwa aseme na yeye kauli aseme kina Mdude hawa nao kukaa kwake kimya kuna…

MWENYEKITI: wewe ongelea hoja iliyo mbele yako tu hapa wewe na muda wako.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naendelea na maji.

MWENYEKITI: Muda wako ndio huo unga mkono upate maji, Mheshimiwa Bungara unga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli upate maji.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Kambi naunga mkono.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru sana kupata nafasi hii, leo kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu ambaye anajua la mtu ambalo liko ndani ya moyo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuniletea miradi, kuhusu afya nimepata vituo vya afya vitatu, na katika jimbo langu kuna vituo vitatu na vyote vimepata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ile barabara ya Kwa Mkocho-Kivinje, ambayo nilipiga kelele kwa muda mrefu sana tangu awamu ile ya nne, alhambulilah barabara imeisha, tunashukuru sana. Jambo lingine ambalo nashukuru sana kuna VETA Chuo cha Maendeleo, kimejengwa, kinaendelea vizuri sana, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuna mahakama ni nzuri kwelikweli, mahakama imekwisha, Alhamdulilah. Kwa hiyo, kwa kweli nashukuru, mengi ambayo nimeomba na niliyasemea katika Bunge hili, yametekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na waswahili wanasema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Sisi ni wanasiasa, kuna wakati jambo likiwa zuri lazima tusifie, lakini kuna jambo likiwa siyo sawasawa, lazima tukosoe, na hiyo ndiyo siasa, hakuna aliyekamilika katika dunia hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba sana, sisi tuna Bandari Kilwa Masoko pale, sijaona katika mpango wako Mheshimiwa Mpango, kama bandari ile ambayo ina kina kirefu tena cha asili, sijaona katika mpango wako kama ipo na itekelezwe. Pia kuhusu habari ya maji, kuna mradi mkubwa sana, Mheshimiwa Mpango naona siku moja tuliyokaa, nakushukuru sana Mheshimiwa Mpango, mradi wa maji ule umeingizwa katika mpango wa Mradi wa India, katika ile miji midogo 29 na ule upo, ni mradi mkubwa sana. Naomba utekelezwe na Inshallah utatekelezwa kwa sababu nimeona katika mpango wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja hayo, yote tunayopanga haya, kama hakuna utawala bora, kama hakuna utawala bora, sawasawa na kutwanga maji katika kinu. Tunakusifieni sana, kwa huduma za jamii mmejitahidi, lakini utawala bora, tatizo na ninamuomba Mheshimiwa Magufuli, aangalie katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania imefika katika hali mbaya, mlianza kwa kutisha, nchi ikawa kuna utekaji mwingi, kuna mauaji mengi, mkazuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, hakika Watanzania tumetishika! Hapo mmefaulu sana katika utawala bora! Tumetishika! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo, katika Wilaya yangu ya Kilwa, Jimbo la Kilwa Kusini, tumesimamisha wagombea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, katika vijiji 15 tulivyosimamisha hata kijiji kimoja hakuna aliye…

MBUNGE FULANI: Kwa chama gani?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: CUF wewe hujui? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameondolewa katika uchaguzi, kuna mtu mmoja kaondolewa, kuna Kijiji kimoja cha Nanjilinji wameondolewa, walisema wao hawajui kuandika kingereza na hawajui kusoma kiingereza! Sasa katika fomu pale unaulizwa, chama chako gani? The Civic United Front, Chama cha Wananchi, ndiyo ameambiwa mmesema uongo! Ninyi mlisema kwamba hamjui kuandika kiingereza mbona mmeandika civic, wameondolewa sababu hiyohiyo tu! (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuseme, wametolewa wajumbe wangu 25 wa Kijiji cha Nanjilinji A kwa kuandika The Civic United Front, ninyi mnasema uwongo! Aa, jamani, sisi tumenukuu tu kadi yetu imeandikwa, sisi tukaangalia tukafuatosha tu, aaa! Mmesema uongo! Wangeliandika CUF, wangelitolewa, kwa sababu hakuna chama kinaitwa CUF, wakiandika The Civic United Front, wanakwambia wewe ulikuwa hujui kuandika kingereza, hujui kuandika kingereza, inakuwaje kuwaje? Imefikia hivyo Tanzania kweli! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mwingine ametolewa katika kinyang’anyiro, kwa kuandika Waziri, binti jina lake Fatuma Waziri Juma, basi katolewa kaambiwa hatujui jina linaloitwa waziri, jina… walah wabilah nayo! Hakuna jina linaloitwa Waziri, waziri ni cheo! Katolewa, walah wabilah watalah. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda wapi? Tunaweka pingamizi, tunaambiwa, pingamizi lako umeandika mwenyekiti, badala ya kuandika uenyekiti, huna sifa! Huna sifa, unaomba nafasi ya uenyekiti! Wengi, hata CCM inawajua, wameandika hivyo hivyo, wengine wameandika uenyekiti, wengine mwenyekiti, basi unaondolewa, kugombea kwa sababu umeandika mwenyekiti, aaa! Lengo si lilelile unayegombea cheo cha uenyekiti, sasa mtu unasemaje! Tuseme nchi hii imefikia hatua hii, kweli jamani! Kukosea neno moja, ndiyo unaondolewa katika uchaguzi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, cha ajabu sasa, twende leo wewe nani huyu, Mhagama wewe, twende mimi na wewe katika Kituo cha Msaidizi, tukachukue fomu za CCM, walah wabilah, wameandika vibaya kushinda sisi, lakini ninachojua, kanuni inasema, mteuzi atakuwa msaidi, na msimamizi masaidizi, aliitwa Ikulu! Sasa mtu kaitwa Ikulu, huyu anataka kusimama, hebu simama wewe. (Kicheko)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge na hasa kwa kusifia kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwenye jimbo lake, na vilevile vazi lake zuri sana na linaakisi Shirika letu la Ndege Tanzania, kwa hiyo, anapongeza pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba, hayo yote anayoyasema, Serikali imeshatoa taarifa, hao wote waliokuwa wanaitwa akina Waziri, wametoka Najilinji, walioandika kina Fatuma, waliondika uenyekiti, mwenyekiti, kama wanaona wameonewa, wakate tu hizo rufaa zitasikilizwa na mwisho wa kuzisikiliza ni kesho!

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile, ninaomba tu nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge, awe tu na subira, kesho, itampa matokeo yoyote yale ambayo yanaweza kuashiria hicho ambacho kimeonekana na ninamshukuru tu anakili kwamba kwamba, mtu amekosea kosa moja, kujaza fomu ya uchaguzi ni kama mtihani, ukikosea umekosea! Kwa hiyo, asubiri tu matokeo ya rufaa yatampa ukweli na uhakika wa kila kitu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bungara unasemaje kuhusu taarifa?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza siyo taarifa, yeye kaniweka sawa tu. Nimekuelewa, nimekuelewa sana, lakini na hili la kusema, The Civic United Front, maana yake hilo la kukosea ndiyo umekosea, ndiyo umeandika sawasawa, lakini kosa lako unaambiwa wewe hujui kingereza, kwa kuwa umeandika kingereza toka, wewe unasemaje hilo, wewe unasemaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huu ni mpango maalum, ni mpango maalum! Naomba sana, naomba sana, sisi watu wazima! Mnakoipeleka nchi siyo sawasawa, mnatutisha, mtu pengine kafumaniwa tu, kaenda kukata shamba la mahindi, kafyeka fyeka siyo sababu ya uchaguzi mnasema, kakata sababu ya uchaguzi, pengine alimfumania.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bungara ahsante sana