Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii niunge mkono Mapendekezo ya Mpango wa mwaka 2019/2020 pia naunga mkono mapendekezo na maoni ya Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binadamu na wanyama kimahitaji tunafanana ila tofauti binadamu anaufahamu na kujitambua; mnyama ajitambui lakini binadamu anaufahamu wa kujitambua, inapotokea binadamu akajitoa ufahamu wa kujitambua huo ni uvivu wa kufikiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inapotokea Mheshimiwa Mbunge aliyekaa miaka mitatu ndani ya Bunge aliyekaa miaka mitano ya nyuma ndani ya Bunge asitambue yote yanayofanyika huo ni uvivu wa kufikiri kutokuona yote hayo hata huu mpanga bahati nzuri Mheshimiwa Mpango umetuambia vizuri sana jamani eeee naomba tujikite kwenye mpango ili kusudi maoni, ushauri na mapendekezo yenu baadaye sasa iwe mpango sasa wa maendeleo uwigizwe kwenye Mpango wa Maendeleo wa 2019/2020 ulitushauri hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inasikitisha badala ya kuzungumzia mpango wenyewe kwa mfano mimi nitashauri tukiachana na haya mengine Mheshimiwa Mpango nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wa kuthubutu wala kutokuogopa mtu wala nchi yoyote ile kuhusu mradi wa Stiegler’s Gorge na hili Mheshimiwa Mpango, Waziri wa Mipango sisi hapa kama mradi huu ukikamilika tutapata megawatts 2,100 ni tija kwa Taifa hawa wanaosema eti watu wa nje wakichukia, sisi tulikuwa tunaitaji kilometa za mraba 100 wala siyo zaidi ya hapo kilometa 50 urefu na kilometa mbili upana ili tupate megawatts 2,100 hivi kweli hii ni rasilimali ya Taifa rasilimali ya nchi hii tumepewa na Mungu hivi unapoogopa kutumia cha kwako utumie cha nani? Eti kwa sababu watu wa nje watanuna wache wanune hili ni Taifa huru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Mpango katika mpango wako kuna mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma ili nafikiri tangu ukiwa Katibu wa Mipango limekuwepo, tumelisema, tumelisema sasa tuondoe kwenye story sasa tuweke kwenye uhalisia ebu tufike mahala sasa tuamue kwamba je? Huu mradi wa makaa ya mawe Liganga na Mchuchuma bahati nzuri mmewakabidhi NDC hebu sasa tufikie pahala tumalize hili suala baada ya kukaa kila mwaka inakuja, lakini ili tuendane na sekta ya viwanda ni lazima Mheshimiwa Mpango kuna maeneo mawili/kuna viwanda viwili; Kilimanjaro Tools na Mang’ula Tools hizi kama zitaimarishwa zitaenda kulisha mitambo ya viwanda vyetu, naomba hili tusilionee aibu lazima tulitekeleze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ushauri katika kuboresha shirika letu la ndege la Air Tanzania tunategemea ikifika Oktoba 2019 tutakuwa na ndege nane, lakini tatizo kubwa ambalo lipo ni upungufu wa marubani. Marubani waliopo leo ni 33, marubani 16 wameenda mafunzoni na ndege hizi nane zinahitaji jumla ya marubani 70; marubani hao 70 ni lazima wawe wazalendo. Na wewe kwenye kitabu Mheshimiwa Dkt. Mpango umeandika kwamba kusomesha kwa wingi katika fani na ujuzi adimu na maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii fani ya urubani ni fani maalum na adimu na lazima tupate marubani wetu wazalendo ili waje waendeshe ndege zetu hizi ili kupunguza gharama. Tukitegemea marubani wa nje gharama itakuwa kubwa zaidi.

Nimuombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, hili la marubani nafikiri ni jambo jema tukapata marubani wetu wakaenda wakafanya mafunzo kwa sasa kabla ndege zingine hazijaja hizi maana zingine zikafika mwezi wa kumi na moja nyingine mwakani. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Mpango, ndege hizi zitahitaji marubani wazalendo wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Dkt. Mpango, Kanda ya Ziwa tunalima sana pamba, lakini bahati mbaya hatuna viwanda vya nguo sasa mazao yanayotokana na pamba hivi tunafurahia sisi kusafirisha marobota kutoka Sumve kuyapeleka Dar es Salaam.

Kwa hiyo nikuombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango katika mpango wako kwa sababu hii ni Serikali ya viwanda na mazao yale yapo sasa kama pamba hebu tuwe na utaratibu agalau wa kusimamia Wizara ya Viwanda na Uwekezaji hebu Bwana Mwijage aje na mpango maalum na kamati yake kuhusu mazao ya biashara pamba, korosho, kahawa ili mazao hayo ikiwezekana yawe yanabanguliwa humu ndani na kufanya packing humu ndani ili baadae tuuze sasa badala ya kuuza raw material tuuze bidhaa ambayo imechambuliwa tayari na kwenda nchinje kwa ajili ya kuongeza thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni kuombe sana suala la Mkoa Mwanza, Simiyu, Mara lazima tuwe na kiwanda kinchotengeza nguo na inawezekana basi angalau kimoja tu Mheshimiwa Mpango kimoja tu kanda ya ziwa angau kwa kuanzia ili zao lile la pamba liweze kutumika badala ya kusafirisha marobota, tupate kiwanda kimoja cha kutengeneza nguo na mahitaji ni makubwa sana ya nguo za aina mbalimbali huo ndio ulikuwa ushauri wangu Mheshimiwa Mpango na nikushukuru sana na nikuombe usiogope hizi kelele za huyo, huyo, huyo, wewe songa mbele tu watu wapige kelele lakini si tunajua tutafika wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono.