Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, na mimi kwa namna ya pekee naomba kwa kweli kuwapa hongera nyingi sana Waziri Engineer Kamwelwe, Naibu wako Waziri, Katibu Mkuu Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu Engineer Kalobero na Wakurugenzi wote wakiongozwa na ndugu Mafuru mnafanya kazi nzuri, hongereni sana. Mnafanya kazi katika mazingira magumu na kwa kweli ukiangalia taarifa ya Kamati na hotuba ya bajeti kwa kiwango kikubwa mmefanyia kazi zile shilingi bilioni 158 za Mfuko wa Maji ambazo zimekuwa ring fenced, hongereni sana kwa kazi nzuri ambayo mmefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa kwenye Kamati ya Maji kipindi kilichopita, najua uwekezaji mliouweka ni mkubwa sana katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam. Mmefanya kazi kubwa sana, miradi mikubwa mliyowekeza sasa muisimamie iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la takwimu, katika ukurasa 214 na 215 kwenye skimu za umwagiliaji na katika skimu zilizoko katika Mkoa wa Kigoma kuna skimu moja muhimu sana hamkuiweka pale, nafikiri ni oversight, Skimu ya Maji ya Msambala ni muhimu sana pale na iko katika Mji wa Kasulu. Ninaomba kwenye kumbukumbu zenu muiweke sikuiona humu na inawezekana katika mfumo wa kibajeti na yenyewe mkawa mmeisahau, nilikuwa nakumbusha tu jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, nianze na fedha za India, miradi ya miji 17 ambayo umeitaja kwenye kitabu chako. Naomba Mheshimiwa Waziri najua juhudi zinakwenda, Serikali imeshapiga hatua kubwa kuhusu fedha za mkopo kutoka Serikali ya India kwa miji ile 17 na miji hiyo 17 ni pamoja na Mji wa Kasulu. Kwenye kitabu chako hiki cha hotuba umeeleza kwamba, itakwenda kwa phases, kuna phase one Zanzibar na miji mingine mitatu/minne, halafu phase two na miji mingine iliyobaki. Sasa sikuelewa logic kama mradi wa maji unatekelezwa Zanzibar au unatekelezwa Njombe unazuia vipi mradi wa Kasulu usitekelezwe?

Mheshimiwa Spika, sikuelewa logic sikuiona hata kidogo, kwa hiyo nilikuwa nafikiri good practise kwa sababu hii miradi tumeisubiri muda mrefu na itakuwa na fedha za kutosha, hii miradi ingeanza simultaneously. Kama unatekelezwa Zanzibar, unatekelezwa Makambako na utekelezwe na Kasulu kwa wakati huo huo kwa sababu wahandisi tunao wa kutosha wa kufanya kazi hii. Sikuona logic ya kuanza kuweka kwa phase kwamba hii ni phase one na phase two, maana kwa tafsiri hii ni kwamba phase two sisi pamoja na Mji wa Kasulu itabidi tusubiri miaka mingine mitatu minne tungoje phase. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa uweze kuliweka vizuri na wataalam wako wananisikiliza. Tunataka miradi hii, tumeisubiri sana, ianze mara moja katika maeneo yote kwa sababu kuna wakandarasi na wahandisi wengi wa kutosha. Nilifikiri nianze na jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulisema kwa sauti kubwa kwa kweli ni kukushukuru sana. Waziri ninakushukuru sana wewe na timu yako, mmefanya kazi kubwa sana. Katika Jimbo langu nimepokea shilingi bilioni 1.3 kwa kweli zimefanya kazi kubwa sana. Tumejenga chanzo kipya cha maji katika Mji wa Kasulu ambacho hakikuwepo katika eneo la Kimobwa, Kijiji cha Heru Juu chenye wakazi zaidi ya 15,000 sasa wanapata maji safi na salama. Kijiji cha Muhunga mradi unakwenda vizuri, tunahitaji fedha nadhani watakuwa wameshakuletea certificate ili uweze kutupa fedha nyingine kukamilisha mradi ule, kazi ni nzuri na tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, again kwenye kitabu chako hiki kuna miradi ambayo imetengewa fedha, nimeona kijiji cha Muganza, nimeona mradi wa maji Marumba unaendelea, kuna miradi Mheshimiwa Waziri ile nimekuwa nikisema sana kwenye Wizara yako, miradi ya siku nyingi, kule kwetu ilianzishwa na watu wa NORAD Water Project. Kuna miradi ya siku nyingi sana na jambo hili nimeshazungumza na hata na Katibu Mkuu wako na Ndugu Kalobero. Tuna mradi mkubwa sana wa Kijiji cha Ruhita - Kanazi ni miradi wa siku nyingi inahitaji tu kufanyiwa rehabilitation. Ninafikiri mwaka huu wa fedha ungetafuta fedha, mradi huu ni muhimu sana unahudumia vijiji vitatu kwa mara moja, unahudumia zaidi ya wakazi 50,000 katika vijiji vile. Kwa sababu system ipo ni suala la kupeleka wataalam na kuangalia namna bora ya ku-rehabilitate ili hatimaye wakazi hawa waweze kupata maji.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa nikukumbushe Mheshimiwa Waziri ni mradi wetu mkubwa wa maji unaofadhiliwa na Serikali ya Ubelgiji chini ya BTC. Ule ni mradi mkubwa sana kwa watu wa Kigoma, una-cover Wilaya zote za Mkoa wa Kigoma, unaanzia Kigoma, Kasulu, Kibondo mpaka Kakonko. Ule mradi inaonekana umekwama na nimezungumza na RAS ananiambia tatizo kubwa ni kwamba Serikali ya Ubelgiji inataka procurement procedures zifuate Sheria ya Ubelgiji ya Procurement, haikuingia kwenye kichwa changu Mheshimiwa Waziri, wewe mwenyewe kwa juhudi zako umeshafanya mawasiliano na watu wa Kigoma, nilikuwa nafikiri kuna haja ya ku-fast track jambo hili. Ule mradi tuna uhitaji sana, fedha zipo, Waziri wa Fedha ameshasaini ile Financial Agreement tayari, kwa hiyo tuna fedha zetu kupitia Serikali ya Ubelgiji ambazo zinahitaji fast tracking na control ya aina fulani ili mradi ule uanze.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani mradi wa maji usubiri miaka miwili kufanyiwa procurement, it is just too long. Ni muda mrefu sana na wananchi hawa wanataka maji. Huu mradi wa Ubelgiji pale Kasulu Mjini ni muhimu sana kwetu kwa sababu una-cover vijiji vitatu, Vijiji vya Nyasha, Nyatale na Kijiji cha Kigondo ni vijiji vyenye wakazi wengi sana ningependa sana miradi hii Mheshimiwa Waziri ikamilike.

Mheshimiwa Spika, najua muda hautoshi nizungumzie pia suala hili la kulinda vyanzo vya maji. Hili jambo hata mwaka jana nimelisema. Nakushauri Mheshimiwa Waziri wa Maji wewe na mwenzako wa Mazingira hata Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Kigwangalla, muangalie njia nzuri ya ile mito mikubwa tuliyonayo katika nchi hii. Nimeona kwenye kitabu chako kuna mito michache ume-identify hapa ukurasa 107. Ukiangalia ukurasa wa 107 kuna mito umeitaja pale, lakini mito hiyo hamjautaja Mto Malagarasi wala hamjataja Mto Kilombero na nimeshangaa sana hata Mto Rufiji hamkuutaja nimeshangaa kidogo. Hiyo ni mito mikubwa sana, mmetaja Ruaha, Wami, Ruvu na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu naomba Serikali nzima mkae chini na muangalie namna ya kulinda mito hii mikubwa. Katika nchi hii mito mikubwa ni mito 14 tu, mito mikubwa sana. Mnahitaji kufanya kama mlivyofanya kwa Ruaha Mkuu mito hii ilindwe kwa sababu ina uhakika wa maji na pengine hii ya kufikiria kwamba maji yatatoka tu Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria pengine itakuwa si sawa sana, wakati kuna mito mikubwa 14 katika nchi hii ambayo tunaweza tukailinda. Kama Serikali mkawa na strategy kabisa ya kulinda mito hii ambayo tunataka iendelee kuwepo kwa manufaa ya vizazi vijavyo ni jambo la muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho niwakumbushe tu tulitembelea miradi mikubwa sana mmewekeza katika Jiji la Dar es Salaam. Tumetembelea Ruvu Juu, Ruvu Chini lakini unakumbuka Mheshimiwa Waziri watu wa DAWASCO na DAWASA wakati ule kabla ya hizi fikra za kuwaunganisha walikuwa na changamoto zao nyingi sana, baadhi ya miradi ilikuwa haijakamilika. Miradi ya Changanyikeni, Salasala, miradi mikubwa sana. Kujenga matenki makubwa sana kwa ajili ya kuondoa shida ya maji katika Jiji la Dar es Salaam. Nilikuwa nashauri strongly uwekezaji ule uliowekwa katika Jiji la Dar es Salaam na Mheshimiwa John Mnyika hiyo kamati ndiyo tulikuwa wote pamoja uwekezaji ni mkubwa sana umewekezwa katika miradi ile. Ilikuwa ni matumaini yangu kwamba Wizara kwa kushirikiana na DAWASCO off course na DAWASA miradi ile ni mikubwa sana ikamilike kwa wakati ili kuondoa shida ya maji kabisa katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nilikuwa namkumbusha ndugu yangu Mheshimiwa Mnyika kwamba tulikuwa naye kwenye Kamati ya Maji, hakuna uwekezaji mkubwa kama uwekezaji uliofanyika katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa namkumbusha tu. Nakushukuru sana.