Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la haki za kiraia na vifo vinavyotokana na ukatili wa Jeshi la Polisi, kuna baadhi ya Polisi wanafanya matukio ya kikatili kwa raia wa nchi hii. Tunasisitiza kuwa Katiba yetu inaruhusu mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa na sheria zetu zinatoa haki na wajibu kwa vyama hivyo katika kuendesha shughuli zao za kisiasa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila raia yupo na haki ya kujumuika na kujiunga na chama chochote. Vilevile kuna baadhi ya Askari wanawapa mateso baadhi ya raia ambao kwa namna moja au nyingine wanahusiana na Vyama vya Siasa vya Upinzani, bali ni kukiuka haki ambazo sisi wenyewe tumezikubali kama Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 17 Februari, ulifanyika uchaguzi wa marudio katika Majimbo na baadhi ya Kata nchini. Ikumbukwe uchaguzi wowote unatoa wajibu na haki kwa Vyama vya Siasa vinavyoshiriki uchaguzi. Moja ya haki za vyama na Wagombea wanaoshiriki uchaguzi ni pamoja na haki ya kuwa na Mawakala katika kila Kituo cha Uchaguzi na Wakala wa ziada kwa mujibu wa uchaguzi na sheria. Kauli za Jeshi ni kuwa maandamano ni kosa la jinai na hata kusema neno “maandamano” kwa sasa inaonekana ni kosa la jinai huku wakijua ni haki ya kikatiba na kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi linatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria ya Jeshi la Polisi na Wasaidizi wa Polisi na Kanuni za Kudumu za Polisi. Baadhi ya vituo vingi vya Polisi nchini vimegeuka sehemu ya kutesa raia badala ya lengo la msingi la ulinzi na usalama wa raia wa jeshi hilo. Kwa hali hii wananchi wanakosa imani na Jeshi la Polisi na kuamua kuchukua sheria mikononi mwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ukiukwaji wa haki za mahabusu katika Vituo vya Polisi, Askari anapomkamata mtuhumiwa, ni vizuri kumjulisha makosa yake. Ni haki ya mtuhumiwa kujulishwa makosa yake ili ajue sababu ya yeye kukamatwa. Kumekuwa na utaratibu ambao umeanza kuzoeleka katika utendaji wa Jeshi la Polisi ambapo watuhumiwa wanakamatwa bila kujulishwa makosa yao, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya sheria. Mawakili au ndugu wanapohoji ni kwa nini watuhumiwa wanashikiliwa bila kuelezwa makosa yao, wanajibiwa kuwa wanasubiri maelekezo kutoka juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko juu ni wapi? Au Jeshi la Polisi limerekebisha sheria bila kuletwa Bungeni kwa kutengeneza mamlaka nyingine ambazo siyo kwa mujibu wa sheria? Ni lazima mtuhumiwa yeyote yule afikishwe Mahakamani ndani ya saa 24, isipokuwa kwa makosa ambayo adhabu yake ni kifo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masharti haya yamekuwa magumu katika Vituo vya Polisi vingi nchini ambapo Jeshi la Polisi limekuwa likiwashikilia watuhumiwa zaidi ya masaa ambayo yanatakiwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kawaida kwa wanachama au Viongozi wa Vyama vya Upinzani kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu bila kupelekwa Mahakamani, wanarudia kauli ileile ya tunasubiri maelekezo kutoka juu.

Ukiukwaji huu wa sheria siyo tu kwa wanasiasa wa Vyama Upinzani, hata kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Wapo baadhi ya watu wameshikiliwa kwenye Vituo vya Polisi mbalimbali kwa zaidi ya miezi miwili bila kupelekwa Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuhoji kuwa pamoja na ubovu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ambayo kimsingi inatakiwa kufutwa kabisa (kwani hauridhishi), hakuna kifungu chochote cha sheria ambacho kinawapa Jeshi la Polisi mamlaka ya kuwashikilia watuhumiwa wa makosa hayo ya mtandao kwa muda mrefu bila kuwapeleka Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Polisi (Jeshi lisiolojulikana) watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria. Kumeibuka vikundi vya watu ambao hufanya matukio ya utekaji, utesaji, kuua na kushambulia watu mbalimbali. Serikali kupitia Vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama imekuwa ikiwaita watu hao kuwa ni watu wasiojulikana. Zipo taarifa kuwa watu hao wasiojulikana wanaovamia wananchi huwaeleza kuwa ni Maofisa wa Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu suala la haki ya kupata dhamana kuwa kama ni zawadi ya Polisi. Uharaka wa Jeshi la Polisi kuwapeleka Mahakamani watuhumiwa baada ya kupata wito wa Mahakama Kuu ni ishara kuwa hawana sababu wala nia njema ya kuwashikilia watuhumiwa. Huu ni ukiukwaji wa haki wa wazi unaofanywa na Maafisa wa Jeshi la Polisi. Hili limekuwa likijirudia mara kwa mara na kuonekana kama jambo ambalo ni halali mbele yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamana ya Jeshi la Polisi siyo zawadi, ni haki ya msingi kabla mtuhumiwa hajahukumiwa na Mahakama. Vilevile ni vizuri Jeshi la Polisi lisikamate watuhumiwa mpaka pale uchunguzi au upelelezi wao utakapokamilika. Hii ni kwa sababu kumekuwa na
sababu za mara kwa mara zinazotolewa watuhumiwa wengi kuendelea kusota Magerezani kwa sababu za kutokamilika kwa upelelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa mahabusu na Magereza yetu nchini. Magereza yetu nchini yana msongamano mkubwa wa wafungwa, jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ndani ya Magereza kuna wafungwa wengi ambao wamefungwa muda mrefu kwa makosa madogo mdogo na hivyo kusababisha msongamano pasipo ulazima wowote. Yapo makosa mengi yanayofanana katika jamii ambayo yanaweza kabisa kurekebishwa bila watuhumiwa kufikishwa Mahabusu au Magerezani. Vijana wengi ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa, wanaishia Magerezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iendelee kutekeleza adhabu mbadala kwa wafungwa ili kukabiliana na changamoto ya msongamano wa wafungwa na Mahabusu Magerezani. Pia naomba Serikali isimamie marekebisho ya tabia kwa wafungwa ndani na nje ya Magereza na katika maeneo ya jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Askari wa Usalama barabarani wanatakiwa kutoa elimu na kuonesha kuhusu makosa madogo madogo barabarani. Wananchi wengi wanalalamika kutozwa pesa za faini ya makosa ambayo hayahitajiki kupigwa faini zaidi ya kupewa elimu ya kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Askari kupewa idadi ya makosa ambayo wanatakiwa kutoza faini kwa siku. Faini za usalama barabarani zinaweza kuleta chuki katika jamii kwa sababu ya hisia zinazojengeka kwa wamiliki wa magari. Ni vizuri Serikali kuisimamia ipasavyo Sheria ya Usalama Barabarani iliyopo na kurekebisha sheria hiyo ili kudhibiti na kupunguza makosa ya barabarani.