Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, katika Bunge la Kumi niliwasilisha Bungeni maelezo binafsi kuhusu tathmini ya ukusanyaji wa kodi ya majengo Jijini Dar es Salaam uliokuwa unafanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kulinganisha na wakati ambapo ukusanyaji huo ulikuwa ukifanywa na Halmashauri. Maelezo hayo yalieleza bayana kwamba kodi ilikusanywa kwa ufanisi zaidi na Halmashauri zaidi ya TRA.

Aidha, maelezo hayo yalipendekeza hatua za kuchukuliwa kuboresha kasoro ndogo katika Halmashauri ili kuongeza ufanisi. Wizara ya Fedha irejee maelezo hayo na kuleta marekebisho wakati wa Muswada wa Sheria ya Fedha ili kurejesha ukusanyaji wa mapato hayo kwa Halmashauri. Kitendo cha TRA kukusanya shilingi bilioni 20.2 tu wakati makadirio yalikuwa shilingi bilioni 47.6 pekee ni ushahidi kuwa yale niliyoyaeleza kwenye maelezo binafsi kwa TRA haiwezi kuwa wakala bora wa ukusanyaji wa kodi hizi.

Mheshimiwa Spika, izingatiwe kuwa hata makadirio ya shilingi bilioni 47.6 kwa nchi nzima ni madogo kwa kuwa hata Halmashauri na Jiji la Dar es Salaam ikiwemo ya kwetu ya Ubungo zingepewa mamlaka ya kukusanya kodi ya majengo zingevuka malengo yaliyowekwa na TRA. Hatua hii ya kurejesha kodi ya majengo ichukuliwe pia kwenye ada za mabango na vyanzo vingine vya mapato ambavyo Serikali Kuu imeamua kuvihodhi/kuvitwaa. Kitendo cha kuminya vyanzo vya uhakika vya mapato vinafanya Halmashauri kushindwa kutumia ipasavyo dhamana za Serikali za Mitaa (Municipal bonds) kujipatia fedha za vitega uchumi na miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka za kurejesha Tume ya Mipango na kufanya marekebisho ya sheria kuipa mamlaka zaidi kuwa chombo huru. Hatua ya sasa ya masuala ya mipango kuwa kama sehemu ya Wizara ya Fedha kumefanya masuala ya mapato na matumizi kupewa kipaumbele bila mipango thabiti.

Mheshimiwa Spika, hali hii imeathiri pia bajeti za Wizara kwa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Dira ya Taifa kutokuzingatiwa kwenye vipaumbele. Aidha, ni muhimu Kitabu cha Mapato (Volume 1) kipewe kipaumbele na utengwe muda wa kutosha na Bunge kujadili kuhusu mapato kabla ya kujikita katika matumizi.