Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Spika, nami nawapongeza Wizara ya Fedha kwa kazi kubwa wanayofanya. Nawapongeza watu wa TRA kwa kazi kubwa wanayofanya.

Moja, ni suala la TR Office, naiomba sana Wizara, kama kuna eneo tukilisimamia vizuri tutapata fedha nyingi kama Taifa ni kwenye TR Office, kwa sababu TR Office ndiye ambaye anakwenda kutukusanyia dividend. Kwa hiyo, ili tupate dividend lazima tuwekeze, lazima tusaidie hayo makampuni.

Mheshimiwa Spika, natoa mfano wa kampuni mbili. Moja ni TIPER. Tujitahidi sana watu wengi watumie facility yetu ya TIPER kwa sababu TIPER sisi tunapata dividend. Kwa hiyo, tunalo jukumu kama Serikali kuwasaidia TIPER.

Pili, PUMA, leo sisi tuna asilimia 50, lakini tumeleta sheria ya local content. Kwa hiyo, ina maana kote kwenye migodi PUMA anaondoka kwa sababu tu ya asilimia 51. Huyu anatupa dividend. Leo tunajenga reli kwa hela nyingi, kazi kubwa tunafanya, lakini kampuni za Serikali hatutaki zipate biashara, kwa sababu gani? Hatusimamii. Namuomba Waziri wa Fedha, nina uhakika dividend hizi anazihitaji. Ili tuweze kuzipata lazima kampuni ambazo Serikali ina share zisaidiwe zipate biashara, ili zikue na tuweze kupata dividends. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu ni suala la PPP. Tumeongea sana kuhusu PPP. Namwomba ndugu yangu Waziri wa Fedha, kama kuna zawadi anayoweza kuwapa Watanzania ni kusimamia miradi ya PPP na mfano tunao. Naomba leo nitoe mfano mmoja. Tuna mfano wa Daraja la Kigamboni, tunatengeneza fedha nyingi sana kwa sababu Serikali haikuweka hela pale, wananchi wamepata huduma, tumepata daraja na pesa tunapata. Hivi leo barabara ya kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma ambayo ni Makao Makuu kwa nini tusiweke road toll? Kwa nini? Tunaongea leo ni mwaka wa 15 mimi niko ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, naomba sana, dunia yetu, kote wenzetu hata Wachina wakubwa wanaondoka kwenye kufanya kila kitu kama Serikali. Baadhi ya mambo yanafanywa na PPP. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la biashara ndogo ndogo. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kama kuna jambo tutawasaidia Watanzania, tukuze biashara. Tukikuza biashara, kodi itaongezeka. Kodi ikiongezeka, tutapata ajira, nchi itaendelea kwa kasi kubwa zaidi kuliko inavyofanya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, ni transit trade. Mungu alituweka Tanzania akatuweka kwenye jiografia yetu hii, haikuwa bahati mbaya. Tunazungukwa na nchi nane. Hiki ndiyo kiwanda kikubwa kuliko kiwanda chochote Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni lazima tuje na sera ambazo zinatasaidia watu wote waje Dar es Salaam, waende Mtwara, waende Tanga. Wanaendaje? Lazima tuweke sera rafiki. Wanaendaje? Kuwe na miundombinu mizuri, tuwe marafiki kwa wafanyabishara ili watu wote waache kwenda China na Dubai, we should create Dubai of Tanzania na ilishaanza hiyo kazi Kariakoo. Sasa kwa trend tunayoenda nayo, tumeanza kutokuwa marafiki. Naomba sana watu wa Serikali, transit trade ndiyo itakayotuondoa hapa kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakupa mfano wa mafuta. Mafuta yanayoenda nje ya nchi tunasema lazima yawe yametoka Tanzania baada ya siku 30, maana yake ni nini?

Maana yake kwa sababu kule nchi za nje kwa wenzetu siku 30 ni chache, ukienda Daban siku 120, ukienda Beira siku 120, ukienda Holdens Bay siku 120, Tanzania siku 30. Maana yake ni nini? Watu hawatokuja. Tukiongeza tukafanya siku 120, maana yake Dar es Salaam ni karibu, watakuja, lakini biashara, transit trade itaongezeka. Malori yatafanya biashara, watu watakunywa mfuta, tutapata kodi, tutapata ajira. Naomba sana wenzetu wa Wizara ya Fedha tulisimamie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwaunga mkono kwa kila wanachokifanya, lakini niwaombe sana, dunia hii inaenda kwa kasi sana. Tukiendelea kujiuliza kila siku, wenzetu watatuacha.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naomba niunge mkono hoja.