Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Zainabu Nuhu Mwamwindi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyeniwezesha kusimama na kuweza kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Naunga mkono maoni na ushauri uliotolewa na Kamati.

Mheshimiwa Spika, ili tuwe na utalii endelevu lazima tutunze vivutio vyetu. Mkoa wa Iringa ndio kitovu cha utalii katika Nyanda za Juu Kusini. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendeleza utalii kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Spika, ninatambua mchango mkubwa wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa nchi yetu. Hifadhi ya Ruaha inayopakana na vijiji 21 vinavyofaidika na uhifadhi kupitia Mbomipa. Pamoja na hayo kuna vijiji ambavyo bado ni maskini sana na ndivyo vinavyotumika kwenye ujangili wa wanyamapori.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Rais amekubali kutujengea barabara kwa kiwango cha lami itokayo Iringa kwenda Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye urefu wa kilometa 130, ninaomba kuishauri Serikali kupitia Wizara hii wawe wanatoa elimu ya ujirani mwema, wasaidie kutoa elimu ya ujasiriamali kama ilivyo Hifadhi za Manyara na Ngorongoro ili kuweza kutengeneza soko la bidhaa za asili kwa kuwatengea eneo ili wageni wanapopita kuelekea hifadhi waweze kusimama na kununua bidhaa na wananchi hawa watafaidika moja kwa moja na kuwapunguzia umasikini.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie makumbusho ya Chifu Mkwawa ambayo yameachwa kwa muda mrefu na hivyo kuendelea kupoteza mapato ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kuona umuhimu wa kutembelea makumbusho ya Chifu Mkwawa. Ninaomba yaweze kuendelezwa ili wageni wanaopata nafasi ya kupumzika Iringa Mjini wapate fursa ya kutembelea makumbusho yetu na kuongeza kipato kwa Taifa na pia kuwanufaisha wananchi wa Kalenga.

Mheshimiwa Spika, naomba pia Serikali imalize mgogoro uliopo kati ya familia ya Mkwawa kuhodhi Makumbusho haya ya Taifa.

Mheshimiwa Spika nashukuru, naunga mkono hoja, naomba kuwasilisha.