Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kuendelea na shughuli za Bunge letu. Nawatakia Waislam wote heri ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Spika, operatation tokomeza na wafugaji/wakulima. Kama kuna wakati Serikali ilikosea ilikuwa ni katika kipindi cha operatation tokomeza, kwa kuwa ulifanyika ukatili na unyama wa kutisha kwani wanyama katika hifadhi walikuwa na thamani zaidi ya binadamu na mapori tengefu nayo pia yalikuwa na thamani kuliko mifugo na binadamu katika maeneo yaliyo karibu na mapori hayo. Cha kushangaza, hawa wananchi walikuwa toka enzi za kabla na baada ya ukoloni ndio waliokuwa walinzi na rafiki wa wanyama, kwa mfano, Wamasai, Wahadzabe na Wasandawe.

Mheshimiwa Spika, Serikali badala ya kuwaelimisha ili wajue faida zipatikanazo na utalii, Serikali inawatumia askari wa wanyamapori (game rangers) kuwapiga, kuwatesa na hata kuwaua kwa risasi kwa kisingizio cha uvamizi wa hifadhi na mapori tengefu, lakini pia wawindaji haramu. Hii si sawa na ni kinyume cha haki za binadamu. Ni vyema Serikali ikatoa elimu na kuwashirikisha wananchi wa maeneo yaliyo karibu na hifadhi, mapori tengefu na mbuga zetu ili wajue kwamba mbuga za Serikali ni mali yao na wajulishwe faida zinazopatikana kutokana na utalii.

Mheshimiwa Spika, migogoro ya ardhi katika mbuga/ hifadhi na wakulima; migogoro haitaisha katika mbuga na hifadhi kwa kuwa watu wetu (wakulima na wafugaji) hawapangiwi mipango shirikishi ambayo ingeweza kugawa maeneo machache ya kulisha mifugo na maeneo mengine yabaki kuwa ya hifadhi. Ukipatikana ushirikiano wa pamoja ungeleta mafanikio kwani hifadhi/mbuga na mapori tengefu ni mali ya Watanzania, ni mali yetu. Tabia ya kuwanyang’anya ng’ombe iachwe.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali; watu huongezeka, ardhi haikui; Serikali ijue wazi wananchi wakiamua kugoma watalii wasipite katika miji yao, wakiamua kufanya hujuma dhidi ya utalii, hakutakuwa na utalii. Hivyo ni vyema Serikali ikawapa elimu na ushirikiano na iache kuwafanyia ukatili wakulima na wafugaji ili Wizara hii iendelee kuwa chanzo cha mapato ya Serikali ambayo ni 17.6% Pato la Taifa (GDP) = USD 2.3 billion per year.

Mheshimiwa Spika, unyang’anyi unaofanywa na game rangers katika utalii kwa Watanzania (wakulima/ wafugaji) kuwapiga ng’ombe mnada kisha fedha inayopatikana ni shilingi ngapi, iko wapi na inafanya nini? Je, hii ndiyo Serikali ya wanyonge au ni Serikali ya kuwaonea wanyonge?

Mheshimiwa Spika, wosia wangu kwa Serikali, rasilimali tulizonazo tumezipata kwa mapenzi yake Mwenyezi Mungu, lakini badala ya kuwaneemesha Watanzania imekuwa ni NAKAMA, hivyo Serikali ijitathmini, ishirikishe wananchi zaidi, badala ya wageni.

Mheshimiwa Spika, utalii kimataifa (cultural tourism) (Sukuma, Makonde, Ngoni, Bondei, Digo). Zipo kabila katika nchi yetu, ni utalii kwa kutumia mavazi yao (Wamasai), ngoma mbalimbali, taarab (Zanzibar) pamoja na picha za kuchora. Vyote hivi wanapokuja watalii wa nje huzinunua na kuzifurahia, lakini tujiulize makabila haya yananufaika vipi kutokana na utalii? Hawanufaiki zaidi ya mifugo yao na wao wenyewe kupigwa na kufungwa magerezani.

Mheshimiwa Spika, matangazo kimataifa; yapo matangazo katika ligi ya Uingereza (England Premier League) peke yake ambayo hayakidhi haja, ni vyema tungekuwa na matangazo katika Bundesliga (German) Laliga (Spain), Series A (Italy), French-League na kadhalika. Pia CNN, BBC, Sky News, Reuters, DW – Deutsche Welle, Aljazeera, kote tutangaze nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, hata katika World Weather Condition Tanzania majiji yetu hayaonekani, tunaona tu Cape Town, Johannesburg, Cairo, Kampala, Kigali, Nairobi, Bujumbura lakini huoni Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Mbeya na Mwanza, kwa nini?

Mheshimiwa Spika, utalii wa bahari (ocean tourism), Tanzania tumejaaliwa ufukwe wa bahari wenye urefu wa kilometa 1,425 kutoka Jasini – Mkinga (Tanga) hadi Msimbati (Mtwara) lakini tunapata mapato kidogo ukilinganisha na mapato ya Kenya ambao ufukwe wao hauzidi kilometa 180 kutoka Mombasa – Vanga (Kenya). Tujiulize tunakwamia wapi?

Mheshimiwa Spika, fishing tourism & surfing; upo utalii wa kuvua samaki wakubwa na kuogelea kwa vidani pamoja na mashindano ya ngalawa (boat). Mashindano haya yanafanyika katika nchi za Dubai, Mozambique, Kenya, South Africa, kwa nini Tanzania tusifanye ambapo watalii wanapokuja wanakaa kwenye hotels na wanatumia huduma mbalimbali zinazotolewa na wenyeji, hii ni ajira, lakini tunashindwa kuweka vivutio (attractions).

Mheshimiwa Spika, VAT na tozo nyingi katika utalii Tanzania; Tanzania tumejaliwa mbuga, mapori, mito, maziwa, vijito na bahari; vyote hivi vipo na Mwenyezi Mungu ametaka tuvitunze na tuvitumie vizuri, vinahitajika vitupatie pia manufaa kwa Serikali na wananchi. Katika nchi sita za Afrika Mashariki, Tanzania ni ya kwanza kwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii, lakini kimapato, kimipango, kitaratibu na mazingira tunashindwa na nchi jirani zetu. Hata kwa watalii wengi kuja katika mbuga tunashindwa. Tunazo mbuga ambazo ni unique. Kwa mfano mbuga ya Saadani (Saadani National Park) ni mbuga pekee inayopakana na bahari na watalii wanapenda kuja kuitembelea lakini kodi zimezidi mno. Kwa mfano VAT, Kenya imeondolewa hali ambayo imekuwa ni kivutio kwa watalii kwenda Kenya zaidi kwa kuwa gharama ni nafuu. Hivyo na Tanzania tuondoe VAT/kodi lukuki

Mheshimiwa Spika, maliasili za misitu, katika nchi zote za SADC ni Tanzania pekee ndiyo pembezoni mwa barabara kumekuwa na magunia ya mkaa na kuni ambayo ni biashara iliyoshamiri.

Mheshimiwa Spika, kwa nini biashara hii imeshamiri? Ni kwa sababu Tanzania ndiyo nchi ambayo umeme na gesi ni bei ghali kuliko nchi zote duniani. Kama tunavyojua asilimia 75 ya Watanzania ni wakazi wa vijijini (wakulima na wafugaji). Je, hivi wakulima na wafugaji wanaweza kumudu kununua umeme wa luku na gesi kwa ajili ya kupikia?

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali ipunguze bei ya umeme, iondoe VAT na pia iondoe utitiri wa kodi, kuokoa muda na kuvutia watalii na pia kuwanufaisha Watanzania katika maisha yao ya kila siku.