Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba niende moja kwa moja Ulanga. Jimbo la Ulanga au Wilaya ya Ulanga kwa ujumla ina kilometa za mraba 11,000 na inakadiriwa kuwa na watu 200,000; lakini asilimia 47 ya eneo hilo ni hifadhi na eneo lililobaki ni milima mikali na mabonde makali na eneo lingine ni madini, kama unavyoijua Ulanga ilivyo, lakini hiyo sio shida. Maeneo ya hifadhi ambayo tumezungukwa, tumezungukwa na Selous Game Reserve, Bonde la Mto Kilombero na Hifadhi ya Ilumo na hifadhi ndogo ndogo 14.

Mheshimiwa Spika, shida inakuja kwenye mipaka, upande ambao tumepakana na Selous Game Reserve kuna Kata tatu, Ilonga, Ketaketa na Mbuga, lakini kama kawaida ilivyo ya watu wa maliasili wameongeza mipaka kinyemela katika hizi kata tatu. Kuongeza mipaka sio shida, watu hao maeneo ya kijiji watu ambao walikuwa wanalima wakikanyaga hayo maeneo wanakamatwa na kuachiwa wanatozwa faini ya shilingi 500,000 hadi shilingi 1,000,000.

Mheshimiwa Spika, nilikuja kwa Waziri, Waziri akafanya mawasiliano watu wa Selous wakamthibitishia hilo eneo sio la Selous na wakasema pia, sio eneo la kijiji. Waziri akawauliza mamlaka ya kuwakamata watu na kuwatesa mnayatoa wapi? Wakashindwa kumjibu na Waziri ameniahidi ataenda, ili kutatua mgogoro huu kuangalia nini kilichopo, hilo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, upande mwingine tumepakana na Bonde la Mto Kilombero ambayo ni Kata ya Ilagua, Lupilo, Minepa pamoja na Milola. Mwaka 2012 Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Halmashauri waliweka mipaka, lakini leo hii Wizara wamekuja wanaondoa watu katika yale maeneo ya ile mipaka ambayo iliwekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali leo tunafanya hivi kwesho tunaamka na hili, hii mpaka lini? Kwa hiyo, naomba Waziri Kigwangalla, najua wewe ni mahiri sana, naomba ulifuatilie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ni operation ya tokomeza. Operation ya tokomeza iliumiza watu wengi sana katika Jimbo langu la Ulanga, lakini mpaka leo hii kuna watu ambao walihakikiwa kwa ajili ya kulipwa hawakulipwa, hasa katika Kata ya Iputi nina wananchi wangu sita ambao mpaka leo hii hawajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jimbo langu la Ulanga kama nilivyosema limebarikiwa kuwa na hifadhi nyingi. Kuna vijiji ambavyo vimefuata taratibu zote kwa ajili ya uvunaji wa mbao, lakini tatizo kubwa Wizara mpaka leo hii hawataki kutupa nyundo. Mkurugenzi wangu leo hii yuko hapa na anasema ikifika Jumatatu kama hamjatupa nyundo nitaita Madiwani wote pamoja na wananchi wangu wa Ulanga tutakaa tutaweka kambi katika Wizara mpaka mtupe hiyo nyundo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la mkaa, nchi yetu, kama tunavyojua maisha yetu ya vijijini sio watu wote wenye uwezo wa kutumia gesi, lakini Wizara wakimkamata mtu ana debe moja la mkaa wanamtoza faini shilingi 500,000. Sasa kama mnaona hawa wauza mikaa wanafaidi si Wizara ya Maliasili nawashauri mchome ninyi mikaa muweke ma-agent watu wawe wanaenda kununua huko kwenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ni suala la utalii, ulitutuma China, tulienda tukaangalia pamoja na fursa za utalii, China wana mnyama mmoja tu anaitwa panda, lakini wanapata mamilioni ya pesa kwa ajili ya huyo mnyama.

Mheshimiwa Spika, Tanzania tuna wanyama wa kila aina, lakini hatutangazi na nikabaini hata sisi wenyewe ni fursa kwa utalii, tulienda na Mheshimiwa Kanyasu, Mbunge wa Geita, kwa urefu wake Wachina walikuwa wanamshangaa na mimi nikapiga chapuo hapo hapo nikawaambia kuwa huyu ni mfupi Tanzania wako warefu kuliko huyo. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.