Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa na mimi kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Aidha, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuandaa hotuba hii ya bajeti.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika na wengi tunaifahamu kwamba sekta ya utalii imekuwa ikiingizia pato kubwa sana nchi yetu kwa asilimia 25 pesa ya kigeni. Lakini iwapo sekta hii itafanyiwa marekebisho na ukafanyika usimamizi madhubuti ninaamini kabisa pato hili linaweza likaongezeka zaidi.

Mheshimiwa Spika, wenzangu wamezungumzia kwamba Tanzania ina eneo kubwa sana la fukwe, takribani kilometa 1000 ukianzia Tanga hadi Mtwara. Hata hivyo kwa masikitiko makubwa ni kwamba aina hii ya utalii katika nchi yetu bado haijapewa kipaumbele cha kutosha, kwa hiyo tuna kila sababu ya kutumia tunu hizi.

Nilikuwa naomba niishauri Wizara wafanye utaratibu wa kuwapeleka watalaam wetu katika nchi za Seychelles, Egypt, Tunisia na zile ambazo zimefanikiwa katika utalii huu wa fukwe. Kwa sababu mimi naamini kabisa pia tukiongeza katika utalii wa fukwe pato letu linaweza likaongezeka mara dufu na hivyo sekta hii ikaingiza pesa zaidi.

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 52 wa hotuba hii umezungumzia pia masuala ya cultural tourism. Napongeza sana juhudi za Serikali kwa kuhamasisha hii cultural tourism. Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo bado kuna mambo makubwa sana ya kufanya, kwa sababu mengi sisi nchi yetu haijafanya. Nchi kwa mfano kama Kenya, wenzetu wako hatua kubwa sana, Morocco, Jordan, India pamoja na Uturuki. Katika hili pia nilikuwa natamani niishauri Serikali ifanye utaratibu wa kuona jinsi gani watalaamu wetu wanakwenda kujifunza na kuleta yale mema na sisi tuweze kufanya hii cultural tourism. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia sambamba na hilo na wenzangu baadhi ya wenzangu wamelizungumza, tuna makabila mengi hapa nchini kwetu, nichukulie katika mkoa wa Dodoma. Mkoa wa Dodoma jamii ya Wagogo ni wachezaji wazuri wa ngoma, lakini pia wana utamaduni wao wa kuzungusha shingo ambayo naamini hakuna kabila lingine lolote Tanzania hii wanaoweza kufanya.

Mheshimiwa Spika, sasa kama wakiendelezwa hawa wenyeji wa Mkoa wa Dodoma na wakawa ni kivutio cha utalii mimi naamini kabisa tunaweza tukapata pato kubwa sana. Si wa Dodoma tu, kuna makabila kama Wamakonde wanacheza vizuri sana, Wasukuma, Wanyamwezi, Wangoni, Wafipa, Waha na makabila mengine mengi. Kwa hiyo, iwapo kama utawekwa utaratibu makabila haya yakaonesha mila na desturi zao na tamaduni zao watalii watakuja kwa wingi, mimi naamini kabisa tukikuza jambo hili litatusaidia sana katika hii cultural tourism. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nizungumzie kuhusu vyuo vyetu vya utalii, ni vichache sana katika nchi hii. Sambamba na hilo mafunzo ambayo yanatolewa katika vyuo hivi hayaendani na ukuaji wa utalii katika dunia.

Kwa hiyo, nilikuwa naomba niishauri Serikali kwamba wajaribu kuangalia upya ile mitaala ili kusudi iendane na hali ya sasa hivi. Kwa sababu ukiangalia katika sekta ya utalii Watanzania wengi wanafanya zile kazi za chini, zile kazi ambazo ni za juu hasa katika hoteli za kitalii zinafanywa na wageni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naamini kabisa tumekuwa na tatizo kubwa sana la ajira, vijana wetu iwapo watapewa mafunzo ya kutosha mimi naamini kabisa hizi nafasi ambazo zinashikwa na wageni badala ya kushikwa na wageni zitachukuliwa na vijana wetu wa Kitanzania. Kwa hiyo, nilikuwa naomba nitoe shime kwa Wizara waone kwamba ili kupata ufumbuzi ni vizuri kurekebisha hili mitaala ili kusudi iendane na mahitaji ya kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 17 wa hotuba hii Mheshimiwa Waziri amezungumzia kuhusu uwindaji wa kitalii. Ni kweli kabisa kuna baadhi ya vitalu vimetolewa, lakini Serikali imetoa wazo kwamba baada ya shughuli za uwindaji wa kitalii yaani ule msimu ukiisha ufanyike utalii wa picha.

Mheshimiwa Spika, mimi nadhani hili ni wazo zuri sana, lakini pamoja na kuwa wazo zuri hebu sasa Serikali ione jinsi gani itarekebisha miundombinu katika maeneo haya kwa sababu tatizo la miundombinu ni kubwa. Mimi nimekuwa Mkuu wa Wilaya katika eneo la Manyoni na kule kuna Rungwa, Kizigo, Mhesi Game Reserves, lakini miundombinu yake ni mibaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna zile posts ambazo ziko ndani katika haya mapori ya akiba, hebu Serikali ione ni jinsi gani ya kuzirekebisha ziwe katika hali nzuri zaidi ili kusudi wafanyakazi wetu waweze kukaa kule katika yale maeneo ya hizi game reserves. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni jinsi ya kupata taarifa za jinsi watalii wanavyoingia nchini. Mimi nilikuwa napenda kushauri, kwamba ni vizuri kukawa kuna taarifa ambazo zitasaidia ni idadi ya watalii wangapi wameingia nchini, na watalii hawa wametoka katika nchi zipi. Hii itawasaidia baadhi ya wafanyabiashara ambao wanafanyabiashara za utalii wakajua hitaji la soko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakitumia social media, tunafahamu kabisa kwamba watu wengi sasa hivi wanatumia social media, kwa hiyo, taarifa hizi zikiwekwa katika social media na watu mbalimbali wakasoma ina maana ya kwamba wale ambao katika nchi zao inaonekana kabisa kwamba utalii upo katika hali ya chini basi hata wafanyabiashara wanaweza wakafanya utaratibu maalumu wa kuona ni jinsi gani wakaweka mkakati kutafuta watalii katika maeneo yale ili sasa kupitia hiyo mitandao ya kijamii tuweze kupata watalii wengi zaidi katika nchi yetu. Sambasamba na hilo tukitumia hivyo inaweza ikatusaidia tukajua kwamba wapi tumejitangaza zaidi na wapi ambapo tunahitaji tujitangaze zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine ambalo nilitaka kulizungumzia ni kuhusu professionals katika hizi Balozi zetu nje ya nchi. Nilikuwa napenda niishauri Serikali yangu kwamba kwa kuwa inavyoelekea kwamba utalii ndio unatangazwa lakini haujatangazwa kwa kiwango kile ni vizuri basi kule katika balozi zetu kukawa attached na baadhi ya wataalam ili waweze kusaidia kutangaza utalii. Kwa sababu ukienda maeneo kama Dubai kwa mfano wenzetu wamefanikiwa sana kwenye suala la utalii kwa sababu ya matangazo, wenzangu wengi wamelizungumzia. Kweli matangazo yapo lakini hata hivyo hapa kwetu matangazo hayatoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilikuwa nashauri ikiwezekana Serikali iweke utaratibu wa kupeleka professionals katika balozi zetu mbalimbali ili waweze kusaidia kutangaza utalii wa nchi yetu na hatimaye tuweze kupata…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana naunga mkono hoja.