Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Marwa Ryoba Chacha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi hii Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi, ni moja ya Wizara hewa. Katika Wizara hewa ambazo zimewahi kuundwa ni hii na nina sababu. Nenda ukurasa wa nane wa hotuba walitengewa development bilioni nne, ukisoma pale anasema hadi kufika mwezi Aprili 2018 hakuna fedha iliyokuwa imetolewa, yaani maana yake sifuri, walipewa sifuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unajua mimi ni Mwalimu, ukisahihisha ukamwekea mtoto sifuri, maana yake hewa, hakuna kitu. Sasa najiuliza kwa nini waliamua kutoa hii Wizara iliyokuwa pamoja na kilimo ili iwe peke yake! Sasa nimejua kwamba ilikuwa ni kutafutia washikaji ulaji, haikuwa na maana yoyote. Kama Wizara ya Mifugo na Uvuvi huwezi kutenga fedha za maendeleo maana yake ni nini? Wabunge wote mko hapa maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba hawataki kusikia biashara ya wafugaji, hawataki kusikia habari ya samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niwaeleze wafugaji, Serikali hii ya CCM haina mpango na nyie. Hivi can you imagine wafugaji wanaoteseka nchi hii, kwa wale wafugaji ambao wako kandokando ya hifadhi na mapori ya akiba, ng’ombe akikanyaga hifadhini, ng’ombe mmoja laki moja ndiyo Sheria inasema.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi hapa mfugaji mmoja kutoka Jimboni kwangu Serengeti, ng’ombe 300 wote wamepigwa mnada amebaki maskini. Ng’ombe akikanyaga hifadhini laki moja, tembo akila heka tano shamba la mahindi mtu anapewa laki moja, hii ndiyo Serikali ya CCM. Tembo akila shamba la hekari tano, laki moja; ng’ombe akikanyaga tu pale hifadhini akakamatwa, ng’ombe mmoja fine laki moja, hutaki kulipa wanapiga mnada Mahakamani, hiyo ndiyo Serikali ya CCM. Kwa hiyo, hii Wizara kazi yenu ni nini? Kama hamuwezi kutetea wafugaji wa nchi hii kazi yenu ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wafugaji wanateseka, unajua tumekaa hapa kuna watu wanakula nyama tu hawajui tabu ambayo wafugaji wanakula. Utakwenda pale canteen utakuta kuna Wabunge wanakula hata hajui ng’ombe anavyofugwa, lakini ukimkuta anavyopinga ng’ombe humu. Wafugaji wetu wanapata shida, sasa nilikuwa naangalia kwenye ule ukurasa sijui watafanya nini mwaka huu, watatoa wapi hela? Ulega atatoa wapi hela? Haya wanayosema watafanya hela watatoa wapi? Kama mwaka uliopita wameshindwa kupewa hata mia, afadhali waje hata naweza kuwafadhili, kama Magufuli ameshindwa kuwapa hela, waje nitawasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye uvuvi ni balaa, yaani Ulega na Mpina wanataka wananchi wa Kanda ya Ziwa wale nini? Tulizoea kula dagaa, kula samaki sasa hivi hawataki kabisa na mitego yote, nyavu zote wamechoma na kuteketeza. Hata zile ambazo ziko kwa mujibu wa Sheria walikuwa wameigiza, ziko pale mpakani Sirari Mpina amezikataa. Akija hapa atuambie kwanini zile nyavu ambazo ziko pale mpakani amezikataa. Nataka majibu leo toka kwa Mpina, kama hatatupa majibu, mimi nitakamata shilingi yake na Wabunge wote wa Kanda ya Ziwa tutamsulubu kesho.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka majibu, kwa nini nyavu za wafanyabisahara zile ambazo ziko pale Sirari amezikataa ambazo ziko kwa mujibu wa sheria. Sasa hivi dagaa wameadimika Kanda ya Ziwa hakuna dagaa, hakuna samaki. Nilikwenda pale naulizia samaki wananiambia elfu 30, samaki mmoja shilingi elfu 30. Hivi Mheshimiwa Mpina anatoka Kanda ya Ziwa au anatokea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli niwaombe Wabunge wa CCM kama wataunga mkono hoja, uchumi wa Kanda ya Ziwa ni samaki, uchumi wa Kanda ya Ziwa ni ng’ombe, ng’ombe wamepigwa mnada wamekwisha, samaki nao hawataki, sasa wanataka wafanye nini, wakaibe? Mheshimiwa Mpina wakaibe?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kimsingi nashangaa Wizara hii, hivi kazi yao ni nini?