Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mungu kwa ulinzi, nguvu na afya aliyonijalia mimi na Wabunge wenzengu wote humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia zaidi ya 65 ya wananchi wa Tanzania ni wakulima. Ni kweli kwamba kaulimbiu yetu ni kufikisha nchi yetu kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na ili kufika huko tunakotaka kwenda ni lazima tufufue viwanda vyetu. Mazao ya kilimo ndiyo malighafi ya kufanya viwanda vyetu vizalishe, vitoe ajira, vituletee fedha za kigeni na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu sasa Wizara ya Kilimo ilikuwa haipewi kipaumbele kabisa, pamoja na kuwa ndiyo Wizara pekee ambayo ina uwezo mkubwa wa kuondoa umaskini wa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kwa dhati ya moyo wangu juhudi kubwa ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ninatambua nia ya dhati ya Mawaziri wa Kilimo ya kuleta mapinduzi ya kilimo, lakini ifike mahali watalaam wa Wizara hii wafikiri njia bora na sahihi ya kumkomboa mkulima huyu maskini anayevunja shamba kwa mikono yake, anayepanda, kupalilia na kuvuna mazao yake kwa gharama na jasho jingi, ni kwa namna gani kazi yake hiyo itamlipa? Kwani wakati akilima hakusaidiwa na mtu wala Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa wafanyakazi wa nchi hii wanapopokea mishahara yao baada ya kufanya kazi kwa mwezi mzima, ni kwa nini mkulima huyu abebe gharama zake mwenyewe halafu baadae apangiwe wapi akauze?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kilimo cha mahindi kimeshamiri sana hapa nchini, mbali na kuwa zao la chakula, lakini sasa hivi zao hili limekuwa la kibiashara, pia na wananchi wengi wanalima kama zao la biashara. Mwaka 2017 Serikali ilipofunga mipaka ili mahindi yasiuzwe nje, wakulima wengi wamepata hasara kubwa sana. Mahindi mengi yameoza na yaliyobaki yanauzwa kwa debe moja shilingi 5,000, gunia ni shilingi 25,000. Kumbuka mbegu ya mahindi kilogramu mbili ni shilingi 12,000, weka gharama za kilimo, palizi na kuvuna. Kwa heka moja mkulima anapoteza zaidi ya shilingi 600,000, lakini leo anauza mahindi kwa debe shilingi 5,000 kuna tija gani hapo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mkulima huyu aliyelima mbaazi na bado mbaazi inakosa soko huko India, mkulima huyu amelemewa.

Naomba Serikali ione ni kwa namna gani sasa mkulima huyu atasaidika. Suala la pamba kuuzwa kwenye ushirika nalo ni janga lingine. Ninaomba sana Serikali yangu iangalie kwa upya jambo hili na ikiwezekana ijipe muda kidogo wa kufanya utafiti ili kujiridhisha vilivyo ili hatimaye tusije kutukamuumiza tena mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli bajeti iliyotengwa mwaka 2017/2018 yenyewe ilikuwa ndogo lakini kinachouma zaidi ni kiasi kidogo sana kilichopelekwa. Kama kweli tunataka kutoka hapa tulipo kiuchumi, ni lazima tuwekeze vya kutosha katika kilimo chenye kuleta tija hasa kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote zilizoendelea katika uchumi wa kilimo, wamewekeza zaidi katika kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni na mpaka sasa bado mvua kubwa zinaendelea kuleta mafuriko makubwa na maafa, lakini inashangaza sana kuona kuwa hatuwekezi kwenye utengenezaji wa mabwawa ili maji hayo yaweze kutumika katika kilimo cha umwagiliaji. Pamoja na kwamba hii siyo njia pekee, tunahitaji kuchimba visima virefu ili kutekeleza azma hiyo. Naishauri Serikali, Wizara ya Maji ifanye kazi sambamba na Wizara ya Kilimo ili uwekezaji huo wa kilimo cha umwagiliaji, kiweze kufanikiwa ili tupate malighafi ya kutosha ya viwanda vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi waliomaliza vyuo va kazi na Vyuo Vikuu hawana ajira. Nashauri Serikali itenge maeneo yanayofaa kwa kilimo, vijana hawa wakopeshwe zana kama matrekta na kadhalika ili waweze kujiajiri kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema nashukuru sana. Naunga mkono hoja.