Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Asha Mshimba Jecha

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa asilimia 100. Naipongeza Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha amani, usalama wa nchi yetu unaendelea kuimarika na wananchi wake kuishi bila ya hofu na kuendelea na harakati za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Makamanda na Wanajeshi wetu wote kwa kutekeleza majukumu yao ya ulinzi wa nchi yetu kwa weledi na ufanisi mkubwa na jeshi letu kutuletea sifa kubwa ndani na nje ya nchi. Hongera sana na Mungu atawalipa kwa uzalendo wao wa kujitoa muhanga kwa ulinzi wa nchi yetu, hakika kazi yao imetukuka na tunaithamini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kuendelea kuliimarisha Jeshi letu hatua kwa hatua na wakati wote jeshi letu limeweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, hata pale zinapotokea baadhi ya changamoto, halikushindwa kukabiliana na changamoto hiyo na tuliweza kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, udhibiti wa sare za jeshi, hivi karibuni kumejitokeza matumizi ya sare za kijeshi na hata za polisi kutumika kwa kufanyia uhalifu na kujipatia fedha kwa njia isiyo ya halali. Hivyo, tunaomba Wizara kuwa makini na jambo hili, kwani inaonesha baadhi yao huziiba nguo hizi wakati wakiwa kazini na mara wanapostaafu na maisha kuwa duni, huanza kujihusisha na uhalifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wanaojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, wakimaliza mafunzo yao, baadhi yao huajiriwa kwenye Taasisi mbalimbali, lakini wapo wanaobaki mitaani mwetu. Naomba Serikali kupitia Wizara hii kuwatambua vijana hao pamoja na wale wanajeshi wastaafu katika mikoa, wilaya zetu ili kuwa na takwimu zao kwa lengo la kuwatumia pale wanapohitajika, hata kuanzisha vikundi vya uzalishaji na ulinzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Ahsante.