Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namshukuru Mwenyezi Mungu, Subhanah Wataalah kwa kupata fursa kuchangia juu ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na ulinzi wa amani. Sisi kama Tanzania kama wanachama wa Umoja wa Mataifa, tunaendelea na taratibu zetu hizo, lakini katika ukurasa wa 26 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu ulinzi wa amani huko DRC Kongo, kuna wanajeshi 19 ambao wamepoteza maisha na 66 ambao wamejeruhiwa. Katika maelezo, Mheshimiwa Waziri alisema ni shambulio la kushtukiza na pia Maafisa Askari wetu walichelewa kupata msaada stahiki kwa wakati kutoka kwa MONUSCO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Waziri, suala la kupata msaada unaostahili kwa wakati, naomba mara hii iwe ni mwisho, kwamba vifo vimetosha; wanajeshi wetu wako vizuri. Ni kwamba hapa inaonekana bado kuna peace keeping, siyo enforcement keeping. Katika mtandao wa UN wa Peacekeeping wameleta jina la Private Mohamed Haji Ally ambaye tangu tarehe 7 Desemba, 2017 haonekani kule DRC, mbali na hawa 19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari imesambaa kwenye mitandao ya kijamii. Wazazi wake wametupa maelezo haya tumuulize Mheshimiwa Waziri, Private Mohamed Haji Ally, je, yuko hai au ni miongoni mwa waliokufa? Maana hapa Pemba na Unguja hayupo. Maiti yake haijaletwa. Tunaomba maelezo wakati wa kuhitimisha hili jambo. Hilo lilikuwa la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, baada ya vifo kutokea, wale wajane wanaopaswa kupata stahiki, wanapata kutoka kwenye UN na baadhi ya fedha nyingine kwenda kwenye Serikali. Kama Askari huyu angekuwa hai, angekwenda kupatiwa mafao yake, wakati wa kustaafu anapata pensheni. Wajane hawa inaonekana hawapati pensheni kwa kipindi ambacho mume wake kama angekuwa hai au angestaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, wakati anafanya majumuisho, atupe utaratibu stahiki, kuna malalamiko mengi. Je, baada ya vifo hivi 19 kutokea, wale wajane wataendelea kupata fedha wanayostahiki na pensheni mpaka umri wa kustaafu wa waume zao waliokufa? Hilo jambo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba, mara nyingi Serikali imekuwa ikisema inawahurumiwa wananchi. Katika jambo linalowakera wananchi ni tathmini ya fidia ya malipo kwa wananchi wa maeneo yaliyochukuliwa na Jeshi. Tangu mwaka 2016, Serikali imekuwa ikiahidi hapa Bungeni itatoa fidia kwa maeneo waliyoyachukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mara kadhaa wamekuwa wakitenga shilingi bilioni 27, fedha hazitolewi. Safari hii nashukuru zimetengwa shilingi bilioni 20.9, lakini kwenye hotuba, nashukuru Mungu wamesema kwamba Rasi Mshindo, Mji Mdogo wa Kilwa Masoko, Vitongoji vile vya Chomolo na Kisangi vipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nasisitiza, katika maeneo haya ya Rasi Mshindo, Mji Mdogo wa Kilwa Masoko, vitongoji vya Chomolo na Kisangi, fedha zitolewe haraka. Wananchi wengine wameshakufa, wamepoteza maisha, fedha hizi hazitolewi, Jeshi limechukua maeneo mengi kwa wananchi na fedha za maendeleo hazitolewi. Mheshimiwa Waziri, jambo hili limekuwa ni kubwa sana. Wananchi wamekata tamaa, wanasema wameshanyang’anywa, wamedhulumiwa na Jeshi. Ikiwa miaka na miaka, tangu miaka takriban 18 au 20, fedha hazitolewi, wananchi tayari wamepoteza imani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi shilingi bilioni 20.9 zitolewe. Mbona mambo mengine Serikali wanafanya, mtashindwa na hili, kwa nini? Nashangaa!

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye JKT, wametenga shilingi milioni 225, wanataka kulipa fidia kwa maeneo ambayo yamechukuliwa na Jeshi. Ni jambo jema, lakini hizi fedha nazo zitolewe. Nashukuru sana, namwomba Mheshimiwa Waziri, fedha hizi nazo shilingi milioni 225 ambazo zimetengwa, zitolewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala zima la Sheria ya Ulinzi. Imezungumzwa kidogo hapa, tangu mwaka 1966 hadi leo miaka 52, Sheria hii haijabadilika, haijafanyiwa maboresho. Tunaambiwa ipo katika mchakato, sijui rasimu tayari, lakini kama Jeshi ambalo linaendana na taratibu za kisasa, ikifika miaka 52 halina maboresho, ni tatizo. Hii inasababisha mpaka athari ya mafao kwa wastaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wale walio katika cheo cha private mpaka Brigadier General ni tatizo kubwa. Mafao yao wanapostaafu yanakuwa ni madogo sana. Tatizo ni kwamba sera haipo, sheria haijabadilishwa, Wanajeshi wanapata taabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri akija hapa leo kufanya majumuisho, atuambie kuhusu michakato hii, kwa sababu inaathiri mafao hasa wanapostaafu. Leo Askari private mpaka Brigadier General fedha anazopata wakati anastaafu ni aibu. Sasa watuambie, sisi tuko hapa kwa ajili ya wananchi. Kila mara michakato, mipango iko mbioni, nashangaa! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amezungumza alama za mipaka (beacons) akaeleza taratibu nzuri za kule Uganda. Mbona hatuambii urejeshaji wa alama za mipaka (beacons) kati ya Tanzania na Kenya, yaani Migori na Tarime? Kuna vijiji vimetajwa miaka kadhaa, kuna viashiria ambavyo siyo vizuri; Vijiji vya Panyakoo, Ronche na Ikoma, vimetajwa lakini hawarejeshi. Mheshimiwa Waziri hajatuambia kwenye hotuba yake.