Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa uthubutu mkubwa wa kuwa na nia ya kujenga Tanzania ya viwada. Vilevile niipongeze sana Wizara kwa jitihada zake chini ya Waziri, Mheshimiwa Mwijage, Naibu wake, Mheshimiwa Stella Manyanya, pamoja na Katibu Mkuu, Profesa Elisante, kwa kweli jitihada zenu zinaonekana. Hivyo basi, tunazidi kuwatia moyo, tupo nyuma yenu, tutazidi kuwashauri kadri tuwezavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya yote nipende kumkumbusha Mheshimiwa Waziri kwamba Mkoa wa Mwanza uko tayari kwa ajili ya uwekezaji mpya wa viwanda vipya. Kila Wilaya imeshatenga maeneo kwa ajili ya viwanda. Kwa mfano Magu imeshatanga maeneo Isangijo, Bundirya; Wilaya ya Ilemela imeshatenga Nyamongolo na Sangabuye, na Wilaya nyingine hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua kwamba Wanamwanza ni wakarimu, hali ya hewa ya Mwanza ni nzuri, lakini vilevile tupo tayari kuwakaribisha hawa wafanyabiashara wawe wadogo ama wakubwa. Kwa hiyo tunaomba Mheshimiwa Waziri utusaidie sana kutukaribishia na kutupa ushirikiano katika kuwaalika wawekezaji hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ilemela ina Kiwanda cha Ngozi cha Mwanza Tanneries. Mwaka jana nilisimama hapa nikaomba Serikali iweze kumnyang’anya yule mwekezaji aliyekuwa amepewa kwa sababu alikuwa amekitelekeza. Ninaishukuru sana Serikali, kupitia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imeweza kukiridisha mikononi mwake. Sasa ninachoomba ni kwamba mtuletee mwekezaji katika kiwanda kile kwani maeneo yale kuna chuo na wanachuo wale wanakosa sehemu ya kufanya field. Kwa hiyo, vilevile itasaidia wanafunzi kupata field na itatoa ajira kwa akina mama na vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua, pamba ni ajira lakini ni uchumi hususani katika Mkoa wetu wa Mwanza, na wanawake na vijana wanategemea kipato kutoka katika zao hili. Hivyo basi, nichukue fursa hii kumkumbusa Mheshimiwa Waziri kuhusu ule mpango wa kuvifufua viwanda vya kuchambua pamba vya Nyambiti Ginnery na Ngasamo Ginnery ambavyo tunaamini kabisa vitaongeza ajira kwa vijana lakini pia pamba yetu itaweza kuchambuliwa pale pale na kutengeneza nyuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri, kwa sababu hili suala lipo mezani kwake kwa muda mrefu, atakapokuja ku-wind up atueleze ni lini viwanda hivi vitafufuliwa, kwa sababu wananchi wa Kwimba wamekuwa wakihangaika kupeleka pamba yao mbali wakati viwanda vipo pale na vina uwezo wa kufufuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme Wizara hii ya Viwanda imekuwa ikionesha nia nzuri na imekuwa ikifanya kazi nzuri, lakini nashindwa kujua ni kwanini Mheshimiwa Waziri anashindwa kuwa muwazi? Yapo masuala ambayo yanawakwamisha na sisi tunayaona lakini kwa namna moja ama nyingine yeye inabidi admit na aseme na awe aggressive juu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano zipo hizi associates za Wizara yake kwa ajili ya kujenga viwanda. Kwa mfano iko TRA, TFDA, NEMC, TBS, OSHA na mengineyo kama yapo; hizi taasisi ni muhimu sana katika ujenzi wa viwanda. Pia zimekuwa zikiangusha sana Wizara hii. Kwa nini nasema hivyo zimekuwa na mlolongo mrefu, urasimu mrefu sana wa kutoa vibali. Vilevile kwa namna hiyo tumekuwa tukiwakatisha tamaa wafanyabiashara na wawekezaji wengi sana. Hivyo basi Mheshimiwa Mwijage simama kifua mbele uzikemee na uwe aggressive kama navyosema. Ni lazima useme ili yaweze kusunga mbele kama kweli tuna nia ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kutimiza azima yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa mfano leo hii unataka kufungua kiwanda na unapaswa kupata certificate ya TFDA utaambiwa lazima uje ukagulie premises zako. Kitendo cha kumpata afisa kuja kukagua premises inaweza ikachukua miezi miwili/mitatu na bado akifika pale atasema sawa naomba urekebishe hiki na hiki na hiki ukimaliza niite. Kitendo cha kumuhitaji tena inaweza ikachua miezi kama ile ile bado
bidhaa yako umeipelekea TFDA, ipo kule inakaguliwa, kitendo hicho nacho kinaweza kikachukua miezi mingi. Mimi napenda ku-declare interest, kwamba mimi ninakiwanda changu ndiyo, lakini leo ni miaka miwili ninashughulikia kupata leseni na mpaka hivi naambiwa leseni yangu nembo yangu ya TBS ipo tayari lakini mpaka leo hivi sijaipata na hapo mimi ni Mbunge, je, wale wananchi wa kaaida wanafanyaje? Ni lazima tutafakari haya masuala ili tuweze kuisaidia nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masoko, bado Serikari haijaonesha nia ya kulinda bidhaa za Kitanzania kwa sababu kumekuwa na mambo ambayo yanakwamisha bidhaa hizi. Tukianza katika kodi nyingi ambazo zinatozwa juu ya bidhaa hizi, tukiangalia malighafi ambazo zinaletwa ndani ya nchi zinatozwa kodi nyingi katika bandari yetu. Leo hii bidhaa za kitanzania ni gharama kuliko hata bidhaa zinazotoka nje, hivi unategemea nini? Kwa na namna hii tunauwa viwanda na tunawakatisha tamaa wawekezaji wadogo kwa wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshauri Mheshimiwa Waziri, lakini si ushauri kwa sababu ni jambo ambalo nalifahamu, nikukumbueshe kwamba tunao mabalozi wetu nje ya nchi unaweze kuwatumia kututafutia masoko. Vilevile mkae muangalia namna ya kuweza ku-regulate hizi kodi ndogo ndogo ili tuweze kumwezesha Mtanzania kuuza katika bei nzuri na bidhaa zao ziwe katika soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na malalamiko mengi sana juu ya TRA, hasa pale inapojipangia bei ya bidhaa za wafanyabiashara wanazoagiza kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wafanyabiashara wengi wamekuwa forced kususia bidhaa zao bandarini kwa sababu wana-estimate bei kubwa ambazo wanajua wao lakini kodi pia inakuwa kubwa. Kwa hiyo, kunakuwa hakuna haja ya mfanyabiashara yule kutoa kodi kubwa na bidhaa ile isiwe na faida. Kwa hiyo, iko haja ya Serikali kukaa na kutathmini ufanyaji kazi wa hizi taasisi. Tunazipenda sana, tunafahamu umuhimu wake katika kuijenga Tanzania ya viwanda. Hata hivyo kama haitafanya kazi zake kwa ufasihi ni lazima tuzirekebishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa machache hayo naomba kuunga mkono hoja.