Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Pia nami nachukua fursa hii kuwapongeza sana mabingwa wa Tanzania Dar Yanga Afrika, wameweza kutuwakilisha vyema Kimataifa na sasa wameingia kwenye makundi. Pia nichukue fursa hii kuwapongeza vijana wetu wa Singida United ambao wamefanya vizuri na sasa wameingia fainali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na taarifa nzuri sana ya Mheshimiwa Waziri, nampongeza yeye na Naibu wake; pia yako maeneo tuna kila sababu ya kushauri. Wizara kama ambavyo wameeleza wenzangu, kwa sasa kuna eneo muhimu sana, tunazungumzia entertainment industry. Kwenye eneo hili la kiwanda, nilitarajia kuiona Wizara inatambua kwamba hapa tuna kiwanda. Tukishazungumza kiwanda, content za kiwanda zinajulikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya vizuri, iko Bodi ya Filamu ya Tanzania, iko Baraza la Sanaa (BASATA), lakini iko BMT. Vyombo vyote hivi vya Serikali havijaonesha ni namna gani vinawekeza kwenye kiwanda hiki? Havijaweka mazingira wezeshi ya wawekezaji kuja kuwekeza, badala yake kwa asilimia kubwa vime-deal sana na maadili ambalo ni jambo jema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe kidogo. Kwenye tasnia hii ya filamu, tulikuwa na Marehemu Kanumba, alifanya kazi kubwa sana kuitangaza Tanzania; lakini hata baada ya kutangulia mbele ya haki, kazi zake zinaonekana. Leo nilitaka kuona Mpango Kazi wa Serikali wa kutuwezesha sasa kuwa na akina Kanumba wengine ili kuweza kui-promote Tanzania. Hatujauona Mpango Kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tukumbuke, sasa hivi kijana wetu Diamond anakwenda kutumbuiza kwenye World Cup. Ni fahari ya Tanzania. Najua wakati anaondoka tutamkabidhi bendera na wakati anarudi tutampokea vizuri, tutapiga picha na vitu vingine. Tunajifunza nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Diamond haendi kuwakilisha Wasafi Record, anaenda kuwakilisha Tanzania. Tunatarajia kwa uwakilishi wake duniani wawekezaji watataka kuja Tanzania. Je, mazingira ya kuwekeza tumeyaweka? Wale wawekezaji hawawezi wakaja wakaenda Wasafi Record, watakuja kwenye Wizara ya Habari na Utamaduni kujua mazingira ya kuwekeza kwenye sanaa hii yakoje? Hakuna mazingira yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, consistency hii haipo. Maana yake hatuna watu wengine ambao tunaweza kuwaandaa wakaweza kuitangaza Tanzania, lakini badala yake tumeweza kusimamia kwenye eneo la maadili ambalo mimi naliunga mkono. Ila tulipaswa kutambua, tusitazame tulipoangukia, tunatakiwa tutazame tulikojikwaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka maadili yamepotoka, mpango huu wa maadili kupotoka Serikali ilipaswa iangalie wapi ambapo maadili yamepotoka? Siyo kurudi kuanza kufunga tu kuangalia maadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ni ushindani na mazingira haya ya ushindani yanawapa wakati mgumu sana wasanii. Ili aweze kutoka na mazingira magumu aliyopitia, ni lazima aangalie nchi nyingine wamefanya nini ili aweze kushindana na hilo soko. Katika ushindani huo, lazima tuingie kwenye mazingira haya. Nasi Watanzania tunataka kuangalia kwa sababu tayari jamii yetu imekuwa ina mtazamo huo, lazima turudi, Serikali ikae na wasanii hawa, ikae na wanamichezo wote, izungumze nao. Wanapitia mazingira magumu sana! Kwa mazingira hayohayo, iwekeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuangalia kazi ya Bodi ya Filamu, eneo kubwa sana ni tamasha, makongamano na kadhalika. Sijaona mahali ambapo inaenda kuwekeza kwa hao wasanii. Itatupa mazingira magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie eneo hili la soka. Sisi wadau wa soka, tunafika mahali tunajivunia eneo ambalo Shirikisho la Michezo la Taifa imelisimamia, tumewapa mzigo mkubwa sana na TFF wanafanya kazi kubwa sana, lakini taarifa yote hii ya Serikali haijatambua hata mchango wa TFF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipaswa kwenye bajeti hii na taarifa ya Serikali ioneshe ni namna gani inaweza kuwasaidia TFF kufikia malengo yaliyotarajiwa. Sasa TFF haiwezi kufika mahali ikaandaa na viwanja ama ikajenga viwanja. Serikali ilipaswa ituoneshe mpango thabiti hapa wa kujenga viwanja, lakini ilipaswa itoe maelekezo kwenye Halmashauri zetu, itenge maeneo ya viwanja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo viwanja ambavyo unaviona, vingi ni vya Chama cha Mapinduzi. Nilitarajia kuiona Serikali iingie ubia na CCM katika uboreshaji wa vile viwanja ili viweze kusaidia kwenye eneo hili la soka. Sasa kama huna viwanja na viwanja vimesimamiwa na mapato ya kiwanja kwenye gate collection ni asilimia 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana Baraza la Michezo la Taifa lenyewe linapata asilimia moja na wanaridhika. Kwenye gate collection wanapata asilimia moja wanaridhika. Sasa utaendeleza michezo Tanzania? Maana yake inaonesha kabisa hakuna link hapa ya Serikali na Chama cha Mpira kwa maana ya Chama cha Soka. Hamna link yoyote! Serikali lazima ilitazame hili; inawezajie kusaidia kwenye eneo hili la soka? Tofauti na hapa, hatutaweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wetu wa Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys, nichukue fursa hii kuwapongeza sana. Hizi ni juhudi binafsi za wazalendo, wanafanya kazi kubwa sana. Nilitarajia kuona mpango wa Serikali utakaowezesha vijana hawa under 17 wengine under 21kwa miaka ijao tuwe na timu ya Taifa bora. Sijaona mpango wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri kama inawezekana, ni vizuri vijana hawa tukawapeleka nje hata kwenye Academy za wenzetu ambako soka limeendelea, lakini tukawapeleka kwa mkopo kwenye timu za nje hata kama ni za daraja la nne na kuendelea wakapikwa kule, hata kama Serikali ikigharamia wale vijana wakaa kule. Wakiwaacha huku wakaja kwenye timu zetu, watakuwa polluted na wala hawatawaona. Nasi Timu yetu ya Taifa hata siku moja hatuwezi kufika mahali tukaweza kuingia kwenye mashindano makubwa tukasema sasa timu yetu ya Taifa itafanya vizuri, hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iliangalie eneo hili. Kwa mazingira haya tunazungumzia uchumi wa nchi. Uchumi wa nchi, hauwezi kujengwa tu na viwanda vingine. Natarajia kumwona na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, anatambua kwamba kuna entertainment industry katika viwanda vyake 3,600.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kiwanda kikubwa kuliko viwanda vyote; na kwa sababu najua huwa anaweka machanganuo mzuri kwamba kuna viwanda vikubwa, vya kati, vidogo na vidogo sana, maana hata kiwanda cha juisi anakiita kiwanda kidogo. Sasa entertainment industry ni kiwanda kikubwa sana. Kimeajiri vijana wengi. Lazima tuwe na mpango kazi na lazima tujitathimini wenyewe kabla ya kuamua kukwamisha kazi zao. Ndugu zangu, kazi hii ni ngumu mno. Sisi wanamichezo tunajua huko tunakoelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejikita kwenye UMISETA na UMITASHUMTA. Sisi Walimu tunajua lile ni somo, lakini je, Serikali kama inajua hili ni somo na imesimamia kule, imewezesha kwa kiwango gani maeneo haya hizi shule zikafanya vizuri? Siyo tu kufanya vizuri, mwisho wake nini? Wale vijana wanapoenda kwenye mashindano yale wakamaliza, mwisho wake nini? Maana siyo wanaenda kwenye mashindano wanarudi, biashara imeisha. Ni lazima kuwe na mpango kazi wa Serikali utakaoendeleza michezo mashuleni. Watoto wale wakimaliza wanaenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitarajia kuona hata kama hatuwezi kujenga Academy, uwepo mpango tu kwamba Serikali imeweka mpango wa kuwa na Academy, watoto wanatoka shule wanaingia kwenye Academy tunaendeleza vipaji vyao. Leo tutakuwa tunazungumza habari ya eneo hili la michezo, tutalizungumza tu, lakini...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.