Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nami nafasi hii ya kuchangia eneo muhimu sana hili la michezo. Pongezi zangu nizipeleke kwa kaka yangu Mheshimiwa Harrison Mwakyembe na Mheshimiwa Naibu wake, Katibu Mkuu, Watendaji wote na Ma-CEO wote waliokuwa katika taasisi zake. Pongezi zaidi nisisahau kuzipeleka kwenye timu yangu ya Simba ambayo inakaribia kuwa bingwa wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako, pongezi zaidi zipelekwe kwa timu yangu ya Simba ambayo inakaribia kuwa bingwa wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mataifa yaliyoendelea, katika eneo la michezo wamekuwa wakiwapa nafasi wachezaji wao. Ni eneo muhimu sana kwa maendeleo ya nchi zao. Mfano, kwenye bajeti zetu hapa tunatafuta hela nyingi za barabara, maji na afya. Mataifa yaliyoendelea yanawekeza kama tunavyowekeza kwenye barabara, afya na elimu. Nini maana yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mtoto aweze kuandaliwa, lazima uanze naye chini. Huyu anaweza kuikimbia, huyu anaweza kucheza mpira, anaweza ngumi, anaweza kutupa tufe; lakini wanaowekeza hivyo kila mwaka wanapofika kwenye mashindano ya Kimataifa utaona wanapokelewa na medani nyingi, wanaongeza uchumi wa nchi yao, wanaongeza pato la nchi yao. Kwa hiyo, katika michezo hii ni ajira, ni mapato, nchi inapata. lakini kwetu hapa sijui sana tunakwendaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye michezo ya Madola, ukienda kwenye michezo ya Olimpiki nchi nyingi, angalia jirani zetu Kenya wanakuja na medali. Hakuna medali inakwenda bure. Kila ukiona medali ni pesa zimeingia kwenye nchi yao. Sasa sisi ukiangalia historia ilivyo, tumeweza kupata medali kama sikosei, ilikuwa mwaka 1980, tulipoenda kushiriki Olimpiki Urusi na medali mbili ndiyo tulipata hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye sports ni 1992 kama sikosei kushiriki mashindano ya Afrika. Kuanzia hapo, shughuli hii ni kama haipo. Ni kwa nini? ni kwa sababu hatujakubali kuwekeza kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachezaji waliokuwa wengi ni sawasawa na waimbaji walivyo. Anajitokeza mchezaji mmoja kwa hiari yake, wanajitumikisha, anafanya nini, anapatikana, anafikia viwango tunaiambia Wizara anaondoka kesho njoo umkabidhi bendera. Huyu mchezaji katengenezwa na nani? Nani anajua alipo? Nani kamfanyia maandalizi? Thamani yake ni ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu katika eneo hili la mchezaji mmoja mmoja ndiyo tunashiriki naye, nchi yetu itaendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa pili, tuelekee kwenye vyuo. Katika nchi yetu Chuo cha Michezo ni Malya na Kaole kinachoitwa Chuo cha Sanaa. Ukiangalia kwenye bajeti ya maendeleo Malya ni shilingi milioni 150. Tuko serious? Tuna nia njema? Chuo hiki kinakufa. Mheshimiwa Mama Ndalichako nataka baadaye anijibu, Chuo hiki ni lini kitaweza kutoa degree katika nchi hii? Kwa nini kinachechemea? Kwa nini hawakithamini? Tunapendaje michezo ambako hatuwezi kuwekeza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende TAMISEMI. Kila mwaka wana UMISETA na UMITASHUMTA. Wanaokwenda kuratibu mashindano haya na kuwapata wachezaji, mnawatoa wapi? Au unamchukua Mwalimu kwenye darasa, anajua kufunga goli, unamwambia wewe ni Mwalimu wa Michezo? Haiwezekani. Chama changu na Serikali yangu tumetamka ndani ya Ilani kuendeleza michezo. Tunaendeleza michezo kwa kusababisha Malya kupata shilingi milioni 150? Chuo pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michezo hii, ukitoka hapo Mzee Mkuchika simwoni humu ndani, lakini naomba wanijibu wakati wanajibu; katika ajira 52,000 nataka aniambie Maafisa Utamaduni ni wangapi? Maafisa Michezo ni wangapi katika ajira hiyo? Katika Halmashauri, Maafisa Utamaduni hawa wapo? Wanafanya kazi hii? Au tunapenda michezo watu wamejishindia wenyewe tunawaita Bungeni kuwapigia makofi hapa! Tumewaandaaje? Tunawaandaa vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na Serikali yangu, haiwezekani. Kama tunataka kusimamia michezo, tuweke msingi kwenye michezo. Michezo hii ni ajira sana. Naomba niwapongeze TFF, bora kidogo wanachokipata tunakiona, wanaandaa timu za vijana under 17, under 20 wanashiriki, bora wapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hebu aniambie TOC hela zao ziko wapi? Mashirikisho yoyote yaliyosajiliwa hapa nchini yanapata pesa kutoka nje. Pamoja na kwamba zile pesa zinatoka nje, wanaziratibu vipi? Wanamsaidia nani? Au ni meza tu watu wemekaa, ukishajili NGO yako, noti zinaingia, mambo yanaendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumempata kwa Mheshimiwa Waziri pale mtu mmoja, nilisikia anamteua Mwenyekiti, Mheshimiwa Leodegar Tenga, mimi namkumbuka kama Mwalimu wangu. Wakati nagombea FAT alikuwa ananihoji, nashinda. Baadaye naye ameenda FAT, TFF, leo amekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawazo yangu kwa Mheshimiwa Waziri, naomba Baraza la Michezo atakalolizindua alipe kazi ya kwenda kupitia sera hii. Sera ya Michezo ni butu. Mpira na riadha katika Tanzania siyo mchezo peke yake. Kuna ngumi, karate, boxing na vitu vingi sana vipo, vinapatikanaje? Vinapatikana wapi? Wanaviandaa vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri wakati mwingine akatae kwenda kutoa bendera, kwa sababu haiwezekani Serikali inatoa bendera, haimwandai anayeenda kushiriki michezo hiyo. Anamwandalia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri anakuja kunijibu, aje na maelezo mazuri ya kuniambaia kama yuko tayari, wanaposema Sera ya Michezo ipo, imekuja lini hapa tukaipitisha ili wakatayarishe kanuni watu wakajua? Kwa sababu ipo ndani ya makomputa, iletwe hapa kwenye Bunge lijalo tuambiwe tunataka kufanya hiki na hiki kwenye michezo ili tuendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tupate mabadiliko ya kweli kwenye michezo. Lazima tukubali kuwekeza kwenye michezo, lakini hatuwezi kuipata michezo bila kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri; haiwezekani bajeti ya maendeleo ikawa shilingi bilioni nane. Kamati inasema tumeongeza. Wameongeza nini? Wameongeza asilimia 20. Nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBC, nataka nitoe mfano. Nilibahatika kutembea kwenye nchi hii nikiomba kura na Mheshimiwa Rais wa nchi hii. Tulikuwa na chombo kimoja kinaitwa Star TV. Tukisema mkutano saa 4.00 anaweka chombo, tunarusha nchi nzima; tukisema saa 7.00, anaweka tunarusha nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBC leo, Mheshimiwa Rais leo yuko Kondoa, Mheshimiwa Waziri Mkuu leo aende Nyasa, Makamu wa Rais aende Zanzibar, TBC haiwezi. Haina vyombo kwamba unaweza kumwona Mheshimiwa Rais ukamwona Waziri Mkuu na Makamu wa Rais. Kwa nini? Chombo hiki ndiyo cha nchi. Hizi hela amepewa hapa shilingi bilioni tano hazitoshi kabisa, yaani hawezi kuiweka TBC ika-compete na watu wengine kwa shilingi bilioni tano. Ni hela ndogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tutailamu TBC, tutawafukuza kila wanaokwenda kila siku, lakini kama hatukuwawezesha, tunategemea lini wafanye kazi vizuri? Nilitaka kusahau pale kwa Mheshimiwa Waziri Jafo, naye anijibu hapa ndani. UMITASHUMTA na UMISETA, wale Walimu wanaoenda kuchuja, wanawapata wapi? Wanawapataje? Au wazazi wanatoa hela, watoto wanaenda kule, majibu hayapatikani? Kwa sababu Wizara hizi ni mtambuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri akifika hapa anijibu, lini Wizara inayohusiana na michezo walikutana kikao? Walikutana wapi? Waliamua nini? Wanaendeleza nini? Kwa sababu hapa kuna elimu, hapa kuna utumishi, hapa kuna TAMISEMI na Wizara yake. Lini wanakutana au kila mtu anafanya lake? Haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie hapa Bungeni, kwenye michezo niliuliza swali, kiti hicho alikuwa amekalia Mheshimiwa Mtemi Chenge...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)