Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Immaculate Sware Semesi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ili nitoe maoni yangu katika Wizara hii husika na nitajikita katika eneo la mazingira. Katika eneo hili nitagusia maeneo matatu ambayo ni Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira; hali ya misitu nchini na athari za mazingira yaani environmental impact assessment ambayo inaratibiwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Miradi kupitia NEMC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuzungumzia kuhusu Mfuko wa Mazingira na naomba ni- quote hotuba ya Waziri akisisitiza kwamba sekta zote za uzalishaji mali zinategemea mazingira na hivyo rasilimali zinazotokana na mazingira zina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi na hivyo shughuli zisizo endelevu za uzalishaji mali zimechangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira.

Nilikuwa nataka tujikumbushie pia siyo tu kwenye mali au kwenye uchumi lakini sekta zote za kimazingira ndiyo uhai wetu, ndiyo tunachokitegemea. Ni hewa tunayoivuta, maji tunayoyanywa, ni vyakula tunavyovipata kutoka kwenye ardhi au wanyama au mimea yoyote. Cha kushangaza hiki tunachokitegemea ili tuwe hai, wenye afya na wenye uchumi mzuri wa binafsi na wa nchi hatuupi kipaumbele na kipaumbele hiki jinsi kilivyo chini kimekuwa reflected kwenye bajeti inayotengewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko huu wa mazingira ambao unasimamia dhamana ya uhifadhi wa mazingira nchini mwaka unaoenda kuisha 2017/2018 ilikuwa umetengewa shilingi milioni 300 tu na hawakupata hata senti. Mwaka huu wa fedha unaokuja 2018/2019 imetengewa shilingi milioni 500 tu. Sasa sijui kati ya hizo shilingi milioni 500 zinaenda kufanya nini na probability ya kuzipata haipo wakati hili ni eneo nyeti ambalo ndiyo linalotuweka hapa duniani na linatufanya tuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira, ukurasa wa 16 walionesha chanzo ambacho tunaweza tukapata fedha kidogo kwa ajili ya Mfuko huu wa Hifadhi wa Mazingira nchini. Pale kwenye bullet ya pili wamesema kwamba tozo zinazotokana na shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira ni nyingi lakini zinakusanywa na taasisi au idara nyingine za Serikali. Kamati inashauri tozo hizo walau kwa asilimia tano ziingie katika Mfuko wa Mazingira mfano tozo za magari chakavu, mkaa, mafuta na magogo.

Mimi nilikuwa na-propose siyo asilimia tano tu bali twende hata asilimia 90 kingine kidogo ndiyo kibaki kwenye sekta nyingine ili ku-make sense. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu la pili nililokuwa nataka niliongelee ni tathmini athari za mazingira ambapo wanasimamiwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC). Hii ni nyenzo ya pili ya kusimamia hali ya mazingira yetu nchini, lakini hawa NEMC ambao ndiyo kitendea kazi chetu na wasimamizi nao wamekatwa mikono. Bajeti hii iliyopita wamepata tu asilimia 36 ya kile walichokiomba ili wafanye kidogo wanachoweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hizi hela zinazotengwa na nyingine za maendeleo hawapati kabisa, tunafanya hivi makusudi kujiharibia wenyewe au hatuna wataalam wa kusisitiza umuhimu wa mazingira nchini na katika uchumi na hali ya wananchi wetu. Tatizo ni nini? Ni Serikali haina macho na masikio, hatujifahamu au tunajifahamu lakini tunafanya makusudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mifano michache, sasa hivi ni nyakati za mvua za masika, Dar es Salaam tunalia mafuriko, Arusha tunalia mafuriko na Morogoro tunalia mafuriko. Ukiangalia kwa upana wake mafuriko ya Dar es Salaam literally hayakutakiwa kuwepo. Mafuriko ya Dar es Salaam yamechangiwa na mito mikuu miwili mmojawapo ni Mto Msimbazi. Kwa mfano tu kwenye Bonde la Mto Msimbazi eneo la Jangwani kuna mradi pale wa Serikali (UDART), sasa unajiuliza NEMC walikuwa wapi, environmental impact assessment (tathmini ya uharibifu wa mazingira) iko wapi kwa sababu hii mito ina overflow kwa sababu mto una njia yake ya asili. Sasa tunapoanza kuingilia njia za asili za mito aidha kwa ujenzi au kutupa taka mle ndani tunaifanya iteme (overflow) kwa sababu tumeingilia lile bonde. Sasa unajiuliza, mkono wa NEMC ulikuwa wapi kwenye mradi wa UDART kwa sababu tayari wananchi wa kawaida waliondolewa. Sasa tunalalamika mafuriko na kuwaletea wananchi hasara na vifo juu yake kwa sababu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nijiulize nikawa nasema okay, NEMC hawana hela, lakini nawafahamu NEMC wana wataalam, ni colleagues wangu, kwa hiyo shida siyo utaalam. Hapa sasa kuna la ziada zaidi ya hela. Tukumbuke kwamba NEMC ni mkono wa Serikali, NEMC huyu ndiye mtathmini wa shughuli za Serikali kwenye masuala ya mazingira, NEMC ana-evaluate vipi mradi wa Serikali ambapo naye ni mpango wa Serikali? Kwa hiyo, decisions tunazifanya politically badala ya kufanya kitaaluma. Kwa hiyo, nafikiri hii NEMC iangaliwe kwa jicho la ziada iwe an independent entity ya kusimamia madhara haya tunayoyaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie haraka haraka, kuna proposal naona inaanza kuzaa matunda ya uzalishaji wa umeme Stieglers Gorge. Mradi huu proposal ya kwanza ilianza 1960 lakini umeenda ukisuasua siyo kwa bahati mbaya lakini ni kwa sababu ya athari za mazingira. Stieglers Gorge iko ndani ya Selous Game Reserve, the largest game reserve, si ndiyo? Ina wanyama na ikolojia ambazo ni unique, ni world heritage site. Mradi huu ambao unaenda kuanzishwa unaenda ku-affect Mto Rufiji na vyote vinavyohusiana na Mto Rufiji. Kwenye mdomo wa Mto Rufiji kuna mangroves/mikoko, ni msitu mkubwa kuliko yote kwa East Africa. Mto Rufiji ndiyo unaoifanya Mafia yako iwepo Mheshimiwa Dau, naomba uniunge mkono kwenye hili. Mradi huu unaenda ku-affect Ramsar Site ya Mafia, Kilwa na Rufiji. Sasa tunaenda kuangalia siyo uhai tu shughuli za uvuvi bali na wananchi wote wanaotegemea pale, maeneo yote ya Kilwa, Rufiji, Mtwara wote mnaenda kupata changamoto za kimazingira na za kusihi. Sasa tunavyoongelea haya mambo ya environmental impact assessment ndugu zangu tusiende politically (kisiasa).

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.