Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika hoja ambayo iko mbele ya Bunge lako Tukufu. Nami nianze kuwapongeza kwa kazi nzuri sana ambayo Mawaziri wote wawili pamoja na Naibu Mawaziri wamekuwa wakifanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nitoe salamu za pole kwa mtani wangu Mheshimiwa Kakunda kwa shida aliyoipata ya ajali, lakini Mwenyezi Mungu ameendelea kumsimamia na kumuimarisha; naamini ni kwa sababu ya mambo mema anayowatendea Watanzania, basi hata Mwenyezi Mungu ataendelea kumlinda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa namna ambavyo anatenda kazi na hasa katika Wizara hii ya TAMISEMI. Hivi karibuni alitoa tangazo la kuzuia pesa za Halmashauri ya Bumbuli kutokana na tatizo kidogo la wapi yajengwe Makao Makuu ya Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia fursa hii kutoa shukrani kwa sababu jana yeye mwenyewe amempigia Mbunge wa Bumbuli Mheshimiwa Januari Makamba na kwamba pesa zile zimerudishwa na zitaendeleza ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Bumbuli. Tunamshukuru sana kama Wanatanga, hili ni jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninazo changamoto kadhaa; ya kwanza ni eneo la kiutawala. Lengo la Serikali za Mitaa, madaraka mikoani pamoja na ugatuzi ni kurahisisha shughuli za maendeleo katika maeneo ya Serikali za Mitaa, lakini bado Mkoa wa Tanga unaonekana ndiyo mkoa wenye Halmashauri nyingi nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza, Mkoa wa Tanga una Halmashauri 11, una Majimbo ya Uchaguzi 12. Kwa hiyo, hata kuitendaji, baadhi ya shughuli zinasuasua. Mkoa wa Tanga una Shule za Msingi zaidi ya 1,032. Utaona ni mzigo mkubwa sana kuwa na Afisa Elimu ambaye anasimamia shule hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurudi katika Halmashauri ya Lushoto ina shule 162. Sasa utaona kwamba hii ni idadi kubwa ya shule na tunashindwa kuzisimamia na wakati mwingine hata matokeo yanapotoka mara nyingi unakuta hatufanyi vizuri. Kwa hiyo, inawezekana hatufanyi vizuri siyo kwa sababu watu hawana uwezo ama hatujaandaa mazingira wezeshi ya wanafunzi kupata elimu, lakini tatizo ni kwamba, ni eneo kubwa la kiutawala kiasi kwamba wanashindwa kusimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua liko zuio kwamba sasa hivi hakuna kugawanya mikoa ama Majimbo na kadhalika, lakini ni lazima ukweli tuseme, ieleweke hivyo kwamba Mkoa wa Tanga ndiyo mkoa pekee katika Jamhuri ya Muungano wenye Halmashauri 11 inafuata Morogoro, ina Halmashauri tisa; Mtwara ina Halmashauri tisa; Kagera, Halmashauri nane; na Mara Halmashauri tisa. Kote huko ukiangalia kwenye mikoa ambayo ina Halmashauri nyingi kuna matatizo ya kiutawala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tukae na Serikali iweze kuona. Mathalan kuna mikoa ambayo ina chache. Mkoa wa Rukwa una Halmashauri nne, Mkoa wa Songwe una Halmashauri tano, Mkoa wa Iringa una Halmashauri tano, Mkoa wa Shinyanga, Halmashauri sita; Geita, Halmashauri sita. Kwa hiyo, mkoa wenye Halmashauri 11kulinganisha na mkoa wenye Halmashauri tano au nne, maana yake kwa kweli katika ulinganishi hatuwezi tukatenda sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija katika Shule za Msingi, nimesema Mkoa wa Tanga una shule 1,032; Mkoa wa Kagera 955; Mkoa wa Kilimanjaro 973. Kwa hiyo, Tanga bado inaongoza katika Shule za Msingi. Ukija Iringa kuna Shule za Msingi 499; Katavi kuna shule 177 ambazo ni chache kushinda hata zilizopo Wilaya ya Lushoto. Geita kuna shule 603. Sasa hawa Maafisa Elimu watasimamiaje kwa ulinganifu ambao hauko sawa? Kwa hiyo, tunaomba Wizara hii iweze kuliona hili jambo na kututafutia solution. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye suala la miundombinu ya elimu, tunao uhaba mkubwa wa Walimu katika Halmashauri ya Lushoto. Mahitaji ya Halmashauri ni Walimu 2,408, waliopo ni 1,547. Kuna upungufu wa Walimu 861. Utaona ni gap kubwa sana. Kwa hiyo, tunaomba sana tutoe kipaumbele kwa maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa upande wa Walimu wa Sayansi tunazo sekondari 60 ambazo zina upungufu wa Walimu 123.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni suala la mipango pamoja na TARURA. Sasa hivi mpango wa Serikali ni kufikisha umeme vijijini 2020/2021 ndiyo utakuwa mwisho, lakini yapo maeneo ambayo mpaka sasa hivi hayana barabara. Sasa sioni connection kati ya mipango hii ya mwaka mmoja na miaka mitano ya Kitaifa katika Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yangu ni kwamba tunatarajia kwamba TARURA wameanza kuchukua barabara zile ambazo Halmashauri ilikuwa tayari iko nazo, lakini tukumbuke kwamba kuna vijiji vingine viko katika maeneo ya milima kutokana na jiografia, bado havijafikiwa na huduma ya barabara. Ukiwaambia TARURA wanakwambia bado hii hatujaipokea, tumepokea zile ambazo zilikuwa zinahudumiwa na Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe rai kwamba ili mipango ya Serikali isiwe double standard kwamba umeme vijijini mwisho ni 2020/2021, basi iwe sambasamba na utengenezaji wa barabara ili watu wa umeme waweze kufikisha zile nguzo kule. Bila kuwa na barabara, nguzo zitafikaje? Kwa hiyo, nawaomba sana TAMISEMI hili jambo waliangalie kwa kina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo, nataka nizungumze wazi na kwa sababu tunashauri na kuisimamia Serikali, mimi kwenye Halmashauri yangu, sioni umuhimu wa kuwa na Maafisa Ugani kwa sababu hawaongezi chochote katika kilimo. Hapa juzi nimezungumza suala la kilimo cha kahawa, kila Mbunge ananiuliza kwamba Lushoto kuna kahawa? Maana yake ni kwamba hata Serikali inawezekana hawajui kwamba milima ya usambara kuna kilimo cha kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa una Maafisa Ugani ambao hawawezi hata kutoa taarifa kwenye Serikali. Kwa hiyo, hata katika huu uhaba wa Walimu hata mimi nimuunge mkono Mheshimiwa Dkt. Kikwembe kwamba ukiniambia uondoe Maafisa Ugani uniletee Walimu, nitashukuru, kwa sababu sioni kazi wanayofanya kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tumekuwa na idara inayotabiri hali ya hewa, inaeleza kuhusu hali ya hewa kwamba safari hii tutakuwa na mvua chini ya wastani, safari hii tutakuwa na mvua nyingi; unatarajia kwamba Maafisa Kilimo wachukue hizi taarifa za hali ya mvua wazitafsiri kwa wananchi, lakini bado wananchi wanalima kwa mazoea. Hawajui kwamba tukilima mahindi mvua zitakata mapema, hawajui kwamba tukilima labda mahindi sehemu za mabondeni, tumetabiriwa kutakuwa na mvua juu ya wastani, kwa hiyo, kuna mafuriko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika eneo hilo napenda kusema wazi kabisa kwamba Idara ya Kilimo katika Halmashauri yangu ya Lushoto, lakini naamini hili ni katika nchi nzima kwa sababu tumeona hata katika mpango kwamba kilimo kinakua kwa asilimia 3.3, kwa hiyo, hili ni eneo ambalo linatakiwa litizamwe kwa mapana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la utawala bora ambalo tunalizungumza mara kwa mara na kwa bahati Mheshimiwa Mkuchika alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, anafahamu. Tunao Wenyeviti wa Vijiji na kwa mujibu wa kanuni hapa tunaambiwa kwamba sheria asilimia 20 ya mapato ya Halmashauri inatakiwa iende kulipa hawa Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji. Mpaka sasa wana zaidi ya miaka saba wanadai hawajalipwa chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumza hapa asilimia tano na asilimia kumi, tunazungumza tu kwa ajili ya vijana na akinamama, lakini mbona hatuzungumzii hao Wenyeviti wa Serikali za Vijiji ambao mpaka sasa hivi hawapati hizi posho zao, kiasi kwamba hata kwenda kusimamia shughuli za maendeleo wakati mwingine wanafanya kama hisani, kwa sababu hawapi motivation yoyote. Kwa hiyo, nitoe rai kwamba tunapozungumza suala la utawala bora, ni lazima pia tuzingatie maslahi mapana ya hawa watenda kazi katika ngazi za vijiji na ngazi za vitongoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni miradi ya maji. Tunashukuru kwamba miradi ya maji inaendelea kufanyiwa kazi, lakini kwa changamoto hata Kamati ya LAAC ilivyokwenda katika Mkoa wa Tanga kuna matatizo makubwa ya usimamizi wa miradi ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani kwa utafiti wangu, tatizo liko kwa Mhandisi wa Maji wa Mkoa. Anaonekena aidha kama nilivyozungumza awali kwamba ana Halmashauri nyingi za kuhudumia, kwa hiyo, anashindwa kuwa na ufanisi kiasi kwamba hasimamii vizuri maeneo haya ya miradi, inachukua muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninao mradi wa kutoka Gorogoro, Manoro hadi Kijiji cha mwisho ambacho ni Madala, eneo la mradi ni kilometa 54, lakini sasa nazungumza hapa ni mwaka wa tatu, bado kasi ile hairidhishi. Nitoe rai sasa kwamba wasimamie kwa kina kwamba tunapo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzunguzaji)

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.