Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. Upendo Furaha Peneza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda kwanza kuipongeza Kamati hii ya Huduma na Maendeleo yaa Jamii kwa kuweka pendekezo la Serikali kutoa taulo za kujihifadhi watoto wa kike wakati wa hedhi na Serikali kutoa pads hizo bure mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wenzangu wanafahamu na jamii pia inafahamu, kwamba niliandika hoja binafsi na kuiwakilisha ndani ya Bunge, kwa maana ya kwa Katibu wa Bunge ambayo kwa bahati mbaya haijapata nafasi kwa sababu Ofisi ya Katibu imenijibu kwamba hoja ya kugawa pads bure mashuleni inavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 99(2) ya Ibara hiyo ya Katiba. Hayo ni majibu kutoka Ofisi ya Katibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, bado naipongeza Kamati kwamba wametoa mapendekezo ambayo mimi nimeambiwa navunja Katiba, kwamba sasa Serikali igharamie pads bure mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa hoja yangu ni moja, tuna watoto wa kike wengi mashuleni ambao wanashindwa kukaa vizuri darasani, wanashindwa kuwa na ujasiri wa kujifunza kwa sababu wana hatari ya kujichafua wakiwa katika kipindi cha hedhi.

Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu, amewahi kuliambia Bunge hili kwamba watoto wetu wanatumia vitambaa, wanatumia majani, wanatumia mchanga mpaka wanatumia mavi ya ng’ombe. Hiyo ilikuwa ni kauli ambayo kipindi anatoa kauli hiyo, alikuwa akijibu swali la Mheshimiwa ambaye sasa ni Naibu Waziri wa kupitia Watu wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shida hiyo inayowakuta watoto wetu, bado kuna haja kubwa ya Serikali kuona umuhimu ya kuwapa watoto wetu pads bure mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho ningependa kusema kwamba katika takwimu za Serikali, zilizotolewa na TAMISEMI kwamba wasichana wengi ndio wanaacha shule kuliko..

T A A R I F A . . .

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukaelewa mambo tunayoyajadili, tuache umbea kwenye mambo ya maana yanayogusa maisha ya watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya watoto wanaoacha shule katika kidato cha kwanza, kati ya wanafunzi 9,881 walioacha shule wasichana ni 9,337; kitado cha pili, ni 13,559 wasichana walioacha shule ni 12,617.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu hizi kuanzia form one mpaka form four ni udhibitisho tosha kwamba watoto wetu wanaacha shule kwa sababu ya kukosa vifaa muhimu kama vifaa vya hedhi. Serikali kupitia takwimu za TAMISEMI, imesema wazi kwamba sababu kubwa inayowafanya watoto wa kike kuacha shule ni utoro. Utoro wakiwa kwenye hedhi, siku tano za hedhi wanashindwa kuhudhuria darasani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ifike wakati sasa Bunge ione umuhimu wa kuweza kuwapatia watoto wetu pads bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya mahesabu, kwa bei ya chini kabisa, kama Serikali ingeweza kununua pad ya kila mtoto kwa shilingi 2,500, kwa watoto wa shule wote ambao ni 1,870,889, wanafunzi wa shule ya msingi kuanzia nusu ya darasa la tano, darasa la sita na darasa la saba, Serikali ingegharimia shilingi 46,762,000,000 ndizo ambao Serikali ingegharimia kuwanunulia watoto wetu pads. Kwa sababu ni Serikali, ingeweza kupata pads kwa bei chini kidogo, kwa hiyo, kama Serikali ingenunua pad kwa shilingi 1,500, basi Serikali ingetumia shilingi bilioni 28 tu kuwanunulia watoto wetu pads bure mashuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ikichagua kwamba tutumie re-usable pads suala ambalo mimi mwenyewe siliungi mkono sana kwa sababu vijiji ni asilimia 39 tu ya maji ndiyo yanayopatikana vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ingetumia shilingi 14,963,000,000 kugharimia watoto kama wangeweza kutumia re-usable pads.

T A A R I F A . . .

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, Bunge litakumbuka kwamba nilivyokuwa Mbunge mgeni kabisa kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017 ndiyo hoja iliyolifanya Bunge hili lote mkapiga makofi kwa kuunga mkono hoja hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Maria Kangoye ni Mbunge ambaye amewahi kuchangia hoja hii ya watoto kupata sanitary bure mashuleni. Mbunge ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Walemavu, ni binti ambaye amewahi kuuliza swali ndani ya Bunge hili na ndipo akapata majibu ya kuhusu sanitary pads. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge tulilomaliza Novemba, niliuliza swali na Mheshimiwa Jafo akanijibu kwamba Serikali inajaribu kuweka mikakati ya namna ya kulifanyia ili suala...

T A A R I F A . . .

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Hansard ipo, unaweza ukanipatia muda nikatafuta majibu ya Mheshimiwa Waziri nikakuletea hapa mbele. Nitakushukuru sana kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukiangalia katika takwimu leo na ninatambua michango ya mpaka Waheshimiwa Wabunge wanaume ambao wameweza kuzungumzia hii pads, hata Wabunge wanaume ambao wameunga kampeni ambazo tumezifanya mtaani. Ni ukweli kwamba kadri ya mtoto wa kike anavyopanda kimasomo, akitoka darasa la kwanza kwenda darasa la pili, kwenda darasa la tatu, kwenda darasa la nne, kwenda darasa la tano, ndivyo anavyoongeza uwezekano wa yeye kujipatia kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika takwimu zilizopo, ni kwamba kadiri mtoto anavyosoma, anavyofika Sekondari na kwenda mbele, anaongeza asilimia 15 mpaka 25 ya uwezo wa yeye kuweza kujiingezea kipato. Kwa hiyo, ninaomba watoto wa kike, Serikali tuache kuangalia Upendo unatoka kwa nani, tuangalie suala la msingi linalogusa watoto wetu wa Kitanzania. Ahsante.