Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana wewe na Waheshimiwa Wabunge, kwa heshima mliyotupa Serikali kupitia Wizara yangu kwa michango mizuri sana. Kila mmoja alikuwa anatamani kusikiliza michango kuanzia mtu wa kwanza mpaka wa mwisho, yaani tumefanya kazi ya kibunge vizuri. Hakuna jambo ambalo mimi sikuandika; kila jambo nimeandika. Ingawa sikuandika maneno yote, lakini angalau kila hoja ya mtu naijua. Naweza kusema tulikuwa very serious katika kujadili mjadala huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawapongeza sana nasi kama Wizara tutaendelea kutekeleza mwongozo wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli; yeye kila siku anasema kwamba yeye ni Rais wa CCM, ametokana na CCM ndiyo, lakini amechaguliwa na Watanzania wote na kila mara amekuwa anasisitiza tutoe huduma bila ubaguzi wowote. Kwa hiyo, ndiyo maana spirit ya Wizara yangu ni kutoa huduma kwa wananchi wote na wananchi wote tutaendelea kuwahudumia bila ubaguzi wa aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu nawashukuru sana kwa niaba ya Wizara yangu na wenzangu wote, tuendelee kushirikiana, maana yake hii kama ninyi msingekuwa mnashirikiana nasi pengine tusingejua matatizo yenu. Kwa hiyo, tuendelee kushirikiana na moto ni huo huo. Tuna Ofisi hapa Dodoma, tuna Ofisi sasa kwenye Kanda na hapa nyuma yangu nimeleta viongozi wote wa Kanda nane. Kwa hiyo, kila jambo mlilolisema kama linahusu Mabaraza ya Ardhi, Msajili wa Mabaraza yupo hapa, Amina. Kama linahusu ardhi Kanda ya Magharibi, Kamishna na Msajili wapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lijalo Mungu akipenda, mtazungumza mkiwa na Mthamini wa Kanda, Mpima wa Kanda, Kamishna wa Kanda, Msajili wa Kanda na wote hawa watakuwa wamekamilika na watumishi wao na vitendea kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili alilosema Mheshimiwa Naibu Waziri, tumesema moja ya jambo ambalo mmelizungumza watu wengi humu ndani, kwamba tunakwama kupanga na kupima mashamba na wananchi kupata viwanja vyao kwa sababu hamna vifaa; tumeshaagiza vifaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetangaza kwenye gazeti, tutavisambaza hivi vifaa tena kwa teknolojia mpya, kwa sababu sasa tunatumia satellite na vifaa vya mapokezi ya satellite tumewaonesha jana, tumevinunua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tutakuwa na vifaa ambavyo vinapima kwa upana mkubwa kwa teknolojia mpya na tutawafundisha Maafisa wenu wote. Tutawaita hivi karibuni, Maafisa wenu wote Wapima, hawavijui hivi vitu, tutawafundisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkipata nafasi, kule nyuma tumeweka Maonesho ya Wapima Binafsi, baadhi ya vifaa vya kisasa vya upimaji viko nyuma kule tunakofanyia sherehe. Atakayepata nafasi aende. Tunaposema RTK mtaziona kule, kwa nini kifaa hiki kinaweza kikapima mpaka kilometa 30 kwa wakati mmoja na kikatumia watu wawili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wilaya yako yote inaweza ikapimwa kwa siku tano au sita tukapima mashamba yote. Kwa hiyo, teknolojia hii tumeagiza na tutasambaza kwenye Kanda na awamu ya pili tunakwenda kuandika tunataka tupeleke vifaa hivi kila Wilaya ili hata kama unamwita mpima binafsi, basi uwe una kifaa chako inapunguza gharama. Kwa hiyo, tutatatua kero za ana kwa ana, lakini tunafikiri vilevile twende kwenye mifumo na baadaye tutakuja kwenu kuomba sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachowashukuru ni kwamba mmetusaidia sana kuainisha mambo mbalimbali na haya sasa siyo kujibu tu kwa maandishi lakini tutayapangia na ratiba, tutakuja Mikoani kote huko. Tutakuja Kilimanjaro kufanya audit, tutakwenda Chumbi kwa rafiki yangu Mchegerwa, tutakwenda Mikoa ya Kagera kule Karagwe, tutaenda kila mahali. Tutakuja mikoani. Sasa hatuji mikoani tukisubiri ratiba za mikoa, tutakuja kuthibitisha haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshajua mambo ya kuanza nayo. Tutakuja kila mkoa. Mkoa wa Manyara, Iringa, Ruvuma mpaka Mbinga tutakuja na kila mahali tutakuja, angalau tuna mambo ya kuanzia. Nataka kuwahakikishieni kwamba haya yote tutayaandika, lakini tutawapa majibu ili mjue lakini yatatusaidia sana tukija mkoani kufuatilia haya na kuhakikisha tunayatatua on the spot. Kwa hiyo, tutakuja ndugu zangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepanga Kanda vizuri, sasa tunateua Watendaji wetu wapya kwenye Kanda wafanye hii kazi, mambo yote tutayafanya. Dar es Salaam tutakuja wenyewe nami bado nipo pale, yale yote ya Dar es Salaam tutayamaliza; ya Dodoma hapa tutayamaliza na mikoa yote tutafika na kuyafanyia kazi. Kwa hiyo, nafikiri Waheshimiwa Wabunge hebu msubiri tuje. Tuna ratiba ya miezi 12 kabla hatujakutana hapa, tushirikiane huko huko mikoani kutatua haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mengi yatatatuliwa, tutaulizana tena huko mikoani na wenzangu wanaotoka hapa wanaanza kuyafanyia kazi. Inawezekana baadhi ya mambo mkirudi huko mtakuta yamekwisha kwa sababu viongozi wangu wa kanda wote wapo hapa wamesikiliza. Sasa tumewawezesha na magari mapya, wanakimbia kila mahali, kwa hiyo, hawana shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu nawashukuru sana kwa haya yote mliyoyasema nataka kuwaahidi kwamba tutawajibu kwa maandishi, lakini tutakuja huko mikoani, tutajadiliana sana, tutafanya makongamano, tutaitisha na viongozi wengine wa mikoa tuzungumze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi inayoendelea kubatilisha mashamba ya watu ambao hawayatumii, tutaendelea kuifanya kila mahali; kazi ya kukagua mashamba yasiyotumika, tutafanya; kazi ya kupima kwa kasi ili kila mtu amilikishwe kiwanja, tutafanya. Leo ingawa bado mnazungumza gharama, lakini hizo gharama mnazozijua tumepunguza tozo kwa asilimia 67. Kwa hiyo, Mheshimiwa wa Mbinga hebu angalia taarifa yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama kubwa ambazo hata ninyi Waheshimiwa Wabunge mna offer nilizowapa, angalieni ile kitu inaitwa premium mlicholipa; 67 ya ile mliyolipa imepungua. Kwa hiyo, umilikishaji sasa utakuwa nafuu sana na tungependa kutoka sasa Halmashauri zote zisiruhusu hata kidogo watu kujenga katika maeneo au viwanja ambavyo havijapimwa na kupangwa. Kwa sababu kilio chao cha kupunguza tozo tumefanya, gharama za upimaji zitapungua sana na hivyo hakuna sababu mtu kuendelea kuvamia na kujenga katika maeneo ambayo hayajapimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie ndugu yangu Mheshimiwa Malocha, alizungumza juzi hapa kwa uchungu sana juu ya shamba lake la Malonjo. Watu wako mmelitoa nje ya Mahakama mzungumze. Malizeni mazungumzo, mimi nasubiri. Wakati ule niliwashauri mpeleke notice na mtu wangu alisaidia kuandika notice tuka-serve notice kwa Efatha, lakini akawapeleka Mahakamani. Ninyi mmetoa kesi Mahakamani mzungumze. Zungumzeni, mimi nawasubiri. Kwa hiyo, kabla mambo hayajaja kwangu, msinilaumu. Nilisema miezi sita mkileta kwangu nitakuwa nimeamua, lakini haijaja kwangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri tutashirikiana na nimemwomba Mkuu wa Mkoa wa Rukwa asimamie hayo mazungumzo yenu, Mheshimiwa Malocha na Wabunge mshiriki haya mazungumzo ili yaishe vizuri. Kwa sababu hata yule mwekezaji ajue, lolote atakalofanya,

hataweza kulima lile shamba kwa ustaarabu kwa sababu wale wananchi wamechukia. Kwa hiyo, kwa mwekezaji lazima ajue kwamba lile shamba ni moto na wananchi mtekeleze haya mazungumzo yenu vizuri, win-win situation, mwendelee na hilo shamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani zangu zote nimalizie kwa kusema changamoto zilizoainishwa kwenye mapendekezo yenu na hoja zenu ni nyingi sana, yaani nashindwa hata nianzie wapi; lakini ya Watumishi imezungumzwa sana hapa, Watumishi hatunao. Tutakachokifanya cha dharura kwanza, tutashirikiana na TAMISEMI kuangalia watumishi waliopo tuwapange vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika zunguka yangu nimegundua kuna Wilaya zimependelewa, kuna Watumishi wengi sana. Ilemela na Nyamagana wana Watumishi wasiopungua 100 Wilaya mbili wa Sekta ya Ardhi, tutawaondoa huko. Hii ni kwa sababu kuna Wilaya nyingine haina Mtumishi hata mmoja wa Sekta ya Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutapita, kabla ya kuajiri wapya, tutaangalia uwiano wa jinsi walivyopangwa ili tuwa-switch angalau kazi za dharura ziweze kufanywa kwa watumishi waliopo tugawanye vizuri ili watumishi hawa wasambae maeneo mengine. Watu watapangwa upya halafu baada ya hapo ndiyo tutasimamia vibali kwa Mheshimiwa Angellah Kairuki ili wapya wakipatikana, tuwapange vizuri. Upangaji haukuwa mzuri tutaurekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi mmezungumza habari ya asilimia 30; masuala haya ya upangaji na kodi ya asilimia 30, kinachosisitizwa hapa ni kwamba tungependa miji yetu ipangwe, watu wajenge kwenye viwanja vilivyopangwa, lakini watu wamilikishwe mashamba angalau wapimiwe ili wapate hati. Sasa imekuja tu asilimia 30 lakini faida kubwa zaidi ya watu kujenga kwenye viwanja vilivyopangwa ni kuendeleza miji yetu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, msiangalie tu asilimia 30, mwangalie vilevile kwamba hawa watu kodi tunazokusanya tunazikusanya kwenye viwanja ambavyo vimepangwa na kupimwa, kwa hiyo, Miji yetu imepangika. Kwa hiyo, tuendeleze kasi ya kushirikiana ya kupanga Miji yetu ili iweze kupangika vizuri na kuwawezesha wananchi kupata hati. Kila mwananchi akipata hati, tutaelewana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Mheshimiwa Kiongozi wa Upinzani, lile suala la kutoza kodi kwa viwanja vya mijini na mashamba madogo madogo ya mijini ambayo hayajapimwa, nina maelezo ya ziada. Nitakutafuta wewe na Mheshimiwa Mwassa wenye hoja hii, tuzungumze, tujadiliane. Kinachokufanya wewe useme ni shamba lako mjini ni nini? Hicho hicho tuta-register.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu haiwezekani wewe unapata faida kubwa pale mjini, una ekari 40 Dar es Salaam, una ekari 4,000 Dar es Salaam hutaki kupima, lakini unauza vipande vipande unapata hela; hulipi capital gain. Hivyo hivyo, unavyojifanya wewe vinavyokutambulisha kwamba ni shamba lako, tutavisajili hivyo hivyo na utatulipa pesa, lakini nitawatafuta ninyi wawili, msishike shilingi ili niwafahamishe vizuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, Mwenyezi Mungu awajalie wale wanaoendelea kufunga na sisi wala futari, makobe, tupo, tutawasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.